Wokovu wa Nafsi na Ufunuo Endelevu: Nyaraka za Mtume Petro #28

Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

Tafsiri Sahihi ya 1Petro 1:8-9 SUV:
1.8  Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa ha[mu]mwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye [inayoonyesha] utukufu [mkuu ujao],
1.9  katika [kuipokea kwa ushindi tuzo yenu kuu hapo siku ya mwisho], yaani, wokovu wa roho [uhai wenu/maisha yenu] zenu (yaani wokovu wa nafsi zenu)[ambao ndio lengo/kusudi la imani hii yenu].

Wokovu wa Roho Zenu: Kufuatia desturi ya muda mrefu (ingawa desturi hii si sahihi), tafsiri nyingi za Biblia za Kiingereza (kwa mfano KJV, RSV, NASB, NIV) zinafasili msemo uliotafsiriwa hapo juu kama “wokovu wa uhai/maisha yenu” kuwa ni “salvation of your souls” au kwa kimombo chetu, “wokovu wa roho zenu”. Kosa hili linaonekana pia katika Tafsiri inayotumika hapa, SUV – Swahili Union Version. Tatizo kuu lililoko katika desturi iliyozoeleka ni kwamba inaingia katika mtego wa muda mrefu wa dhana potofu za ki-teolojia na hivyo kumpotosha msomaji kuhusu maana halisi za maneno haya. Kwa kuanza, mwanadamu, kama Mungu alivyomuumba, ni kiumbe mwenye sehemu mbili, ambazo [zinatokana na] mwili (mwili wa mwanadamu) na roho (roho ya mwanadamu).1 Hivi ndivyo kila mmoja wetu alivyo tangu maisha yetu yanapoanza, na hivi ndivyo maisha yetu yatakavyokuwa, kutoka dahari hata dahari. Katika Mwanzo 2:7, Mungu alipompumulia puani pumzi ya uhai (yaani roho), Adamu akawa “nafsi hai” (nephesh kwa Kiebrania, na psyche kwa Kiyunani: cf. 1Wakor. 15:45 ambapo Paulo ananukuu Mwanzo 2:7 na anatumia neno psyche kutafsiri neno nephesh). Lugha hizi mbili ndizo mahususi, lugha asilia za Biblia, ukiacha sehemu ndogo katika kitabu cha Danieli, ambapo lugha ya Kiarami – Aramaic, inatumika. Ndivyo kusema, nephesh au psyche au “nafsi” ndiyo mtu mzima, kamili, muungano wa mwili na roho, sehemu zilizoumbwa na Mungu Mwenyewe na kumfanya mwanadamu (hii ndiyo maana halisi ya nafsi [hai] {“soul” katika Kimombo} katika Biblia, ukiweka pembeni matumizi ya ki-desturi). Nephesh au psyche au nafsi si sehemu mojawapo ya mtu ijapokuwa hivyo ndivyo watu wengi wanavyoichukulia wanaposikia au kutumia neno “nafsi” au “soul”, kwa sababu ya mazoea ya lugha ya Kilatini na matumizi yake katika kanisa la Katoliki la Roma. Katika matumizi ya Kiebrania na Kiyunani mambo hayako hivyo. Na ijapokuwa neno “nafsi” [au “soul”] kama linavyotumika katika maandiko linaweza kutilia mkazo yule ‘mtu wa ndani’ (ambaye kwa kweli ndiye ‘mtu halisi’), Biblia haitumii maneno nephesh au psyche au nafsi/”soul” kuonyesha sehemu tu ya mtu (iwe mwili, roho au mchanganyiko wa sehemu hizo mbili) – hiyo ni dhana inayotokana na nadharia na makisio kutoka NJE ya Biblia na ambayo hayana nafasi yoyote muhimu katika teolojia sahihi ya Kikristo. Kwa lugha nyepesi, nephesh au psyche au nafsi au soul ndiyo “mtu” na hivyo ndiyo “uhai” wa mtu huyo, mke au mume.2 Huyu ndiye anayeokolewa, anayezaliwa upya kupitia imani katika Kristo – siyo sehemu yetu fulani tu, bali mtu wote (na hii ni habari njema kweli!).

Pili, neno la Kiyunani soteria, linalotafsiriwa “wokovu” katika tafsiri mbalimbali zilizotajwa hapo juu, ingawa halijakosewa, [lakini] lina uwezekano wa kupotosha, hasa likitumiwa pamoja na fasili ya nephesh au psyche kwa maana ya nafsi au “soul”. Kwani msemo “wokovu wa nafsi zenu”, kwa mara nyingine tena, unaunda taswira akilini mwa wazungumzaji wa Kiingreza na Kiswahili ambayo si ya Kibiblia kwa 100%. Hili linapaswa kuwa wazi pale msemo “wokovu wa roho zenu” au “wokovu wa nafsi zenu” unapolinganishwa na “wokovu wa maisha/uhai wenu” ambao ndio msemo sahihi. Sisi wanadamu “tunapoteza” au “tunaokoa” maisha yetu kwa msingi wa mtazamo wetu kwa Bwana Yesu Kristo (cf. Matt. 10:39).

Je, itamfaidia nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akaipoteza nafsi (psyche) yake? Luka 9:25

[Tafsiri hii ni kutoka: What good is it for a man to gain the whole world, and yet lose or forfeit his very self (psyche)? Luke 9:25 NIV]

self = nafsi = psyche = nephesh = soul

Mafundisho ya Petro hapa kuhusiana na wokovu yanaendana kwa usahihi na maandiko mengine yanayohusiana na somo hili. Kupitia imani yetu kwa Bwana Yesu Kristo, uhai wetu “unaokolewa” kutoka katika matazamio ya kutisha ya kuishi milele mbali na Mungu. Kutokana na sadaka ya Bwana Yesu ambayo ndiyo tunaitegemea, maisha haya mafupi ya duniani yatafuatiwa na maisha yaliyobarikiwa ya milele kuanzia saa ile Mwokozi wetu anatuita nyumbani tukakae Naye. Huu “ndio ushindi” wa aya ya 9 (dhidi ya kifo; cf. 1Wakor. 15:54-57), hii ndiyo “tuzo kuu” ambayo Petro anaizungumzia hapa, ambayo sote tunaitamani, uzima au uhai wa milele katika Bwana Yesu Kristo pamoja na Baba yetu wa mbinguni milele daima (cf. War. 2:7), na wokovu kutoka kifo cha pili kinachowangojea wale waliomkataa Bwana wetu (Ufu. 2:11; 20:6). Hivyo kwa aya hizi Petro anahitimisha mjadala wake uliouanza katika aya ya 3 pale mwanzo wa ibara (paragraph) ambapo kuzaliwa kwetu upya, kupewa uzima huu wa milele katika dunia hii kwa wote wanaojisalimisha kwa Bwana Yesu Kristo, kunatazamiwa kama tendo halisi litakalotimizwa wakati wa ufufuo wa waongofu, pale atakaporudi Bwana wetu.3 Kupitia imani yetu katika Bwana Yesu Kristo, sote tutapata hii “tuzo kuu ya siku ya mwisho”, “wokovu wa maisha/uhai wetu”, yaani kufika kwetu salama huko mbinguni kuanza maisha ya milele na Kristo, tofauti na wale wanaomkataa Kristo na “kupoteza maisha yao” (i.e. hawaokolewi kutoka kifo bali badala yake “wanakufa mara ya pili”: Ufu. 2:11; 20:6; 20:14; 21:8). Kwa hakika hilo ndilo “lengo na nia ya imani yetu”, uzima wa milele katika Kristo Yesu na wokovu kutoka hukumu ya kifo cha milele.

Ikumbukwe kwamba uzima huu wa milele tutakaoufaudu pamoja na Bwana wetu mpendwa Yesu Kristo milele (somo #20) utakuwa uwepo halisi, katika mwili halisi wa ufufuo utakaoishi milele. Hata hivyo, katika umati wa watakaofufuliwa, kiwango cha thawabu kutokana na utumishi wetu hapa duniani kitakuwa tofauti kwa kiasi kikubwa.4 Hivyo, siyo tu kwamba matazamio yetu ya kurudi kwa Bwana wetu na sisi kukusanywa pamoja na kuwa Naye katika ufufuo kwa uzima wa milele ni faraja kuu kwetu tukingali katika dunia hii ya taabu na machozi, bali pia matazamio yetu, kwa kujiamini, ya thawabu adhimu tutakazopokea kwa utumishi wa uaminifu Kwake licha ya upinzani kutoka kwa Ibilisi pia ni sehemu muhimu na halali ya “tumaini letu lenye uzima” (Waebr. 11:6; cf. 1Pet. 1:3). Ni katika kusimama imara katika kukua kiroho, imani katika kweli ya Neno na kulitumia Neno katika maisha yetu, na kutumikia kweli hiyo kwa wengine kwa kutumia vipaji vya kiroho na huduma tulizokabidhiwa kila mmoja wetu ndipo tunaweza kuongeza thawabu zetu [za milele] na kukwepa mtego wa kanuni za uwongo ambazo zinaathiri thawabu hizo na kuhatarisha wokovu wetu huo.

Mwisho, wokovu huu adhimu na yote yanayoambatana nao, mwili mtimilifu wa milele, ushirikiano ulio timilifu kati yetu na kaka na dada zetu, na ile baraka kuu kuliko zote: kufaidika na uwepo wa Bwana wetu mpendwa Yesu Kristo pamoja na Mungu Baba milele yote, ni jambo linalostahili kupiganiwa – na ni tuzo ambayo kimsingi tumekwishaishinda, hivyo inastahili kutunzwa. Hii inataka ustahamilivu katika imani yetu, kwa sababu ni wale tu wanaoamini, wale wanaovumilia na imani yao imara mpaka mwisho, ndio wanaookolewa (Matt. 10:22; 24:13; Mrk. 13:13). Kwa wale wanaosonga mbele katika barabara iendayo Sayuni vile Bwana Yesu anavyotaka tutembee, majaribu, shida, mateso, mitihani na dhiki tunazokutana nazo hapa duniani zinaituliza na kuiimarisha imani yetu. Ijapokuwa shida hizi zote hazituletei furaha wakati zinatukuta, tunapokabiliana nazo kwa mtazamo wa Kikristo na kufanikiwa kushinda, hii itasababisha furaha kuu mbele ya Bwana wetu katika siku ile tutakapotathminiwa Naye (1Pet. 4:13; Ufu. 7:17; 21:4). Lakini kwa wale wanaorudi nyuma au kwa namna yoyote wanaruhusu magumu ambayo ni lazima yawakute Wakristo hapa duniani yawakatishe tamaa na kuwaweka mbali na Bwana wetu, kuna hatari kwamba imani inayodhoofishwa taratibu inaweza isidumu. Hivyo basi tufanye juhudi zote ili tuyatizame mambo hayo kwa kutumia macho ya Bwana wetu, tukielewa kwamba yuko upande wetu na atatuvusha katika shida yoyote itakayotokea, tukimtegemea yeye bila kujalai macho yetu yanaona nini, masikio yetu yanasikia nini au moyo wetu una hisia gani (War. 8:31). Kwani kwa njia hii imani yetu inasitawi na kuwa wokovu wa maisha yetu, nao unasitawi na kuwa uzima wa milele tulioahidiwa hapa duniani, lakini kwa wale wanaokata tamaa, wajue kwamba wamo katika hatari ya kupoteza imani yao kutokana na kusogea mbali na Mungu (1Tim. 1:19).

10.35  Basi msiutupe ujasiri [wa imani] yenu, kwa maana una thawabu kuu.
10.36  Maana mnahitaji [kuendelea kwa] saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate [kutimiziwa] ile ahadi.
10.37  Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.
10.38  Lakini mwenye haki [mwongofu] wangu ataishi kwa imani; [Lakini] Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.
10.39  Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao [katika imani yao] na kupotea [kwa woga], bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu [milele].
Waebr. 10:35-39 SUV

Tafsiri Sahihi ya 1Petro 1:10-12:
1.10 Hata wakati walipokuwa wakitabiri huu wokovu uliopangwa kuja kwenu, manabii wa kale walichunguza kwa bidii na kuulizia [kwa uangalifu] kuhusu hii zawadi kuu ya neema,
1.11 Wakiwa na shauku ya kugundua (kutambua) ni wakati upi [haswa] Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alikuwa akionyesha alipokuwa akitabiri mateso ya Kristo na utukufu [wa wokovu, pamoja na mambo mengine] utakaofuata baada ya [msalaba].
1.12 Kwani ilifunuliwa kwao kwamba katika kutabiri mambo haya, hawakuwa wanajitumikia wao wenyewe, bali walikuwa wanawatumikia ninyi – na mambo haya haya kwa sasa yametangazwa kwenu kupitia wale waliowapatia Injili kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetoka mbinguni – kwani hata malaika wanatamani kuyachunguza hayo.

Ufunuo wa Maandiko Unaoendelea: Aya hizi zinaweza kuwa udhihirisho wa wazi kabisa katika Biblia wa kanuni inayojulikana kama “Ufunuo Unaoendelea au Endelevu”* (Progressive Revelation). Ufunuo Unaoendelea ni kanuni inayofundisha ukweli kwamba si kweli yote inayofahamika na waumini wa leo/sasa, ilikuwa ikifahamika na waumini hapo kale/mwanzo, na pia si kwamba iliweza kufahamika katika maandiko yaliyokuwako, ijapokuwa ilikuwepo katika maandiko hayo (yaani haikuwa bayana). Walichokifahamu Adamu na Eva juu ya kweli ya Mungu, yaweza kujengwa hoja, kilikuwa kidogo zaidi ya kinachoweza kufahamika na waumini wa leo/sasa – ikiwa watajibidiisha katika mchakato wa kukua kiroho, kusoma Biblia zao, kutafuta mahala ambapo kweli ya Biblia inafundishwa kwa usahihi na kuendelea napo kila wakati, kuamini kweli wanayoisoma na kufundishwa, kuitumia kweli hiyo

* Tafsiri yangu – R. Kilambo.
katika maisha yao ya kila siku, na kuwasaidia wengine wafanye hivyo hivyo kwa kutumia vipaji vyao mara wakifikia kiwango cha kupevuka kiroho. Tunachoweza kusema kutokana na tendo la Adamu na Eva kupokea mavazi ya ngozi waliyopewa na Mungu katika Mwanzo 3:21 ni kwamba hata pale mwanzo, wanadamu wale wawili walipoondolewa kutoka paradiso, Injili ilifundishwa: sadaka ya kuchinjwa wanyama ambayo ilitakikana ili kutengeneza mavazi yale ya ngozi kwa ajili yao iliwakilisha kifo cha Bwana wetu kwa ajili ya dhambi zote, na ndiyo njia sanifu (standard) ya kuonyesha ufumbuzi wa Mungu wa kutatua tatizo la dhambi kabla na baada ya kutolewa kwa Sheria [ya Musa] hadi uhalisia wa msalaba (kwa sababu hii Mwanzo 3:21 mara nyingi huitwa protoevangelium au “kutolewa kwa mara ya kwanza kwa Injili). Tofauti ya msingi kati ya Injili kama ilivyofundishwa wakati ule na sasa ni kwamba kabla ya msalaba wanadamu walitazamia ufumbuzi wa Mungu [kwa tatizo la dhambi] bila kujua kikamilifu kuhusu “mateso ya Kristo na utukufu utakaofuatia” (1Pet. 1:11), bali zaidi zaidi kama “taswira hafifu kwenye kioo” (1Wakor. 13:12), lakini sasa, baada ya msalaba tunamwona “Bwana Yesu Kristo … akionyeshwa wazi, amesulibiwa” (Wagal. 3:1). Katika wokovu kutoka kwa Mungu, kumtegemea Yeye kwamba atatuokoa kutoka dhambi zote ikiwa tunajiweka katika mikono Yake, ndiyo kiini cha kuitikia wito wa Injili ili tuokolewe.

15.51  Angalieni, nawaambia ninyi siri [fumbo]; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,
15.52  kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe [pasipo] na uharibifu, nasi tutabadilika.
1Wakor. 15:51-52 SUV

Jambo hili ni siri/fumbo kwa sababu kabla ya Paulo kupewa ufunuo huu (cf. 1Wathess. 4:13-18), maandiko hayakupambanua kati ya awamu na mazingira ya ufufuo kama ilivyo sasa. Hapo zamani ilikuwa imefunuliwa tu kwamba wafu watafufuliwa, wengine wataingia katika uzima na wengine wataingia katika hatia au hukumu:

Kwani wengi wanaolala wataamka, wengine kuingia katika uzima wa milele, lakini wengine kuingia katika aibu na utengano [na Mungu] wa milele.
Dan. 12:2

Bali sasa tunafahamu zaidi, kwani Mungu amesababisha ufunuo wake wa mambo haya “uendelee”, kiasi kwamba sasa tunafahamu yote kuhusu awamu za ufufuo wa waongofu: 1) Kristo; 2) Kanisa (ukihusisha waliokwishalala na walio hai anaporudi Kristo; na 3) waumini watakaopatikana katika mileniamu, ama “Marafiki wa Bi Harusi”:

15.23  Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko [zao la mwanzo] ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja [katika Ujio wa Pili].
15.24  Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme Wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu [zote].
15.25  Maana sharti amiliki Yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake.
15.26  Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.
1Wakor. 15:23-26 SUV

Tafadhali kuwa makini na angalizo kwamba KWELI ni ile ile siku zote. Kweli haijabadilika. Kilichobadilika ni kwamba Mungu, katika neema Yake ameruhusu tupate fununu zaidi kuhusu maajabu yajayo kwa jinsi ufunuo wa kweli Yake kwa watu wa Mungu kupitia Roho Mtakatifu tunaopewa sasa umeendelea kutoka katika vile vivuli vya Sheria na kufika katika uhalisia wa neema Yake inayofunuliwa katika uso wa Bwana Yesu Kristo: “hata malaika wana shauku ya kutazama mambo haya” (Yoh. 16:12-13; 1Wakor. 2:12-16).

3.4  Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuuelewa ufahamu [utambuzi/umaizi] wangu [wa kiroho] katika siri/fumbo lake Kristo.
3.5  Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine [vilivyopita]; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;
3.6  ya kwamba Mataifa [sasa] ni warithi pamoja nasi [Wayahudi] wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili [tangazo la ushindi Wake];
3.7  Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake.
3.8  Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri [kuwatangazia] Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika;
3.9  na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka [uenezi wa habari hiyo - dispensation of the mystery] ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote;
3.10  ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho (yaani malaika);
3.11  kwa kadiri ya kusudi la [mpango wa enzi hata enzi, yaani historia] alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Waefe. 3:4-11 SUV (with some corrections)

Shauku ya Malaika:

15.7 Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.
Luka 15:7 SUV

15.10 Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.
Luka 15:10 SUV

Maneno ya Bwana wetu hapa yanaweka wazi kwamba uwanja wa vita tunamotembea na kuishi hapa duniani unachunguzwa kwa ukaribu sana huko mbinguni, kwani malaika wana shauku kuu na kila ushindi. Kwa hakika ni zaidi ya hapo. Tunafundishwa ya kwamba malaika wanatusaidia sisi waumini katika vita yetu ya kiroho:

1.14  Je! Hao wote (yaani malaika, soma muktadha wa sura ya 1) si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?
Waebr. 1:14 SUV

Mambo haya tumekwishayazungumza kabla ya hapa.5 Kinachotuhusu hapa siyo shauku ya malaika katika utondoti (details) wa mkakati wa vita isiyoonekana inayopiganwa vikali katika mazingira yanayotuzunguka na wala si ushiriki wao katika vita hiyo, bali ni shani inayowatia bumbuwazi na/au mshangao ambao wanahisi wanavyoushuhudia Mpango mzima wa Mungu unaoleta ushindi mkuu na kamili [kwa Mungu] kwa kuja na kufanywa sadaka kwa Bwana Yesu Kristo. Zaidi ya hayo, kitu cha msingi ambacho malaika hawa wanakiona cha kuvutia sana ni kile kinachosemwa kuwa ni “mateso ya Kristo na utukufu mkuu utakaofuata”. Sasa, kifo cha kiroho* cha Bwana wetu Yesu Kristo pale msalabani kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote ni jambo lenye mvuto mkubwa zaidi ya yote katika historia ya wanadamu na malaika. Msalaba, kwa hakika, ndio msingi wa mpango mzima wa Mungu, na hata sehemu ndogo tu ya kile alichokifanya Kristo pale Kalvari kwa ajili ya yule mtu, [kwa mfano], mwenye kiasi kidogo zaidi cha dhambi, kinazidi kwa umuhimu, shani na ajabu, mambo yote na matendo yote katika ujumla wake, katika historia yote ya mtu huyu – kwa kiasi kikubwa zaidi na zaidi. Hivyo basi, juhudi zote za Shetani kabla ya tukio la msalaba, ziliekezwa katika kulizuia tukio hilo lisifanyike au lisitokee – na juhudi zote baada ya msalaba, zinaelekezwa katika kushusha umuhimu wa msalaba. Na kama vile malaika walivyokuwa na shauku kubwa ya kuona jinsi tatizo la dhambi linavyoweza kutatuliwa na linavyotatuliwa [katika historia] na kwa mateso ya Kristo, vivyo hivyo kwa sasa wana shauku ya kuona matokeo ya sadaka ile ya pekee, “utukufu utakaofuata”, “utukufu” ambao sote tunaingia[mo] (tunaingia ndani yake) tunapokuwa wafuasi wa Bwana wetu kama Alivyonuia tufanye, tukibeba msalaba wetu. “Tunaposhiriki katika mateso Yake” (War. 8:17; 2Wakor. 1:5; Wafi. 1:29-30; Wakol. 1:24; 1Pet. 4:12-13; cf. Matt. 10:38; 10:24; Mark. 8:34; Lk. 9:23; 14:27; Matendo 5:41; 2Wakor. 4:10-11; Wagal. 6:17; 1Wathess. 1:6; 2Wathess. 1:4-5; 2Tim. 3:12), tunaingia katika kilele cha Mpango wa Mungu ambao msingi wake ni Mwamba wa Mwokozi na kifo Chake kwa ajili yetu.
*Tafsiri yangu ya msemo “spiritual death”
Ama kwa hakika hili linawatia shauku malaika, walioanguka na wateule:
Walioanguka wana shauku ya kutufanya tushindwe kumfuata Kristo na hivyo wanafanya yote wanayoweza kutupa mateso; na wateule wana shauku ya kuuona uweza wa sadaka ya Kristo na katika maendeleo makubwa katika Kristo yanayofanywa na waumini kwa uweza wa Roho Mtakatifu, wakitusaidia sisi kwa njia zozote halali wanazoruhusiwa na Mungu. Tunachotakiwa kujifunza kutokana na fundisho hili kutoka katika Neno la Mungu ni kwamba sisi siyo waumini walio kila mmoja peke yake akipambana hapa duniani, la hasha; sisi waumini, kila mmoja wetu ni sehemu ya Mwili wa Kristo ambao unapingwa na yule mwovu na majeshi yake katika kila hatua tunayopiga [kuelekea mbele], lakini tunasaidiwa katika vita hii na malaika wateule au watakatifu katika namna stahiki: sisi siyo tu sehemu ya vita ya malaika inayoendelea (ambayo kwa macho yetu hatuioni) – sisi ndiyo kitovu tukiwa kama wawakilishi wa Yeye ambaye ndiye Bwana wetu na Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

4.9  Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume [tuonekane kuwa watu wa] mwisho, [chini kabisa], kama watu waliohukumiwa wauawe; kwani tumekuwa tamasha kwa dunia [nzima]; kwa malaika na wanadamu.
1Wakor. 4:9 SUV

12.1  Basi na sisi pia [kama waumini wanaotajwa katika sura ya 11], kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii [watu na malaika], na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi [yaani maeneo ya tabia zetu ambamo tuna udhaifu mkubwa zaidi]; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,
12.2  tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
12.3  Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao [waliotenda] dhambi [dhidi ya nafsi yake], msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu [na kukata tamaa].
Waebr. 12:1-3 SUV

Jinsi Mungu anavyoendesha Mpango wake wa wokovu ni dondoo ya msingi inayowatia shauku malaika, wateule na walioanguka, kwa sababu wokovu wa wanadamu katika mapana yake (kazi ya Kristo) na mafupi yake (wokovu wa mtu mmoja mmoja) ni ushuhuda wa huruma, neema, wema na upendo wa Mungu, na hivyo ni ushuhuda kwamba hakuna uonevu katika kuwatia Kwake hatiani Shetani na malaika wake walioasi naye.

Wokovu Endelevu: Wanaoamini wanaokolewa. Sasa, Petro anawezaje kusema katika aya ya 9 kwamba kwa sasa tunangojea Ujio wa Pili wa Bwana ili tuweze kupata wokovu? Na Paulo anawezaje kusema “utimizeni [yaani ufanyieni kazi] wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka” (Wafi. 2:12)? Jibu ni kwamba ijapokuwa tumeokolewa (tumechukua nafasi yetu ya wokovu katika Kristo), na tunaendelea kuokolewa (tunapitishwa salama hapa duniani ambapo imani yetu inakabiliwa na mashambulizi daima), matunda ya yote tunayotumainia hayajafika bado. Kila kisichoonekana kinapaswa kutumainiwa (kama Paulo anavyosema katika War. 8:23-25). Lakini tumaini letu halipo kwenye aina fulani ya kitu kilicho kigumu kushikika au kupatikana. Badala yake, tumaini letu ni imani kamili katika yale ambayo Bwana atafanya kwa ajili yetu katika siku ile tukufu ya kurudi Kwake. Kwa waumini ni uhakika wa uhalisia wa yale yasiyoonekana (Waebr. 11:1); imani inayotazama mbele kwa kujiamini ni tumaini la Kikristo, na tumaini hilo limewekwa kwanza kabisa katika ufufuo:

8.23  Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya (tuliompokea) Roho [Mtakatifu], sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu [yaani ufufuo].
8.24  Kwa maana tuliokolewa kwa taraja [tumaini] hii;
War. 8:23-24a SUV

Ijapokuwa hauelezwi kwa dhahiri kila mara katika maandiko, ufufuo ndio unaotimiza ukamilifu wa “tumaini letu la Kikristo”, siku ile kuu kutoka kifo na kuingia katika uzima, siyo tu kwa nafasi tukufu tuliyo nayo leo kama waumini wa Bwana Yesu Kristo, bali katika mafanikio yote ya ahadi zote za Mungu kwetu: kuwa na mwili wa milele pamoja na thawabu zinazoambatana nao, na urithi utakaodumu milele katika Yerusalemu Mpya tukiwa pamoja na kaka na dada zetu katika uwepo wa Bwana tunayempenda sana:

5.8  Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo [helmet] yetu iwe tumaini la wokovu.
5.9  Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake [hakututeua tupitie ghadhabu yake], bali tupate wokovu, kwa [njia ya] Bwana wetu Yesu Kristo;
1Wathess. 5:8-9 SUV

Kama vile tulivyoona katika hali ya utakaso (mwanzo wa mfululizo wa masomo haya; tizama masomo #8, #13, #19), ambamo tunatakaswa mara tu tunapomwamini Bwana Yesu Kristo (kwani Mungu Baba anatuchukulia kuwa ni “watakatifu pale tunapoungana na Mwana Wake, Bwana wetu), tutatakaswa milele wakati wa ufufuo (ambapo tutakuwa ndani ya miili yetu mipya [mi]timilifu, hatuwezi kamwe kutenda dhambi tena, milele) hata hivyo tumeitwa tuishi maisha matakatifu hapa duniani, tukiurekebisha mwenendo wetu ili tutembee katika utakatifu pamoja na Bwana katika kuendana na nafasi yetu ya utakatifu na katika matazamio ya ule utakaso wetu wa mwisho katika siku ile ya ufufuo, na hivyo hivyo kwa wokovu wetu. Tumeokolewa kama waumini katika Bwana Yesu Kristo, lakini hatutau-ishi wokovu huu na hatutapokea wokovu huu kikamilifu mpaka siku ile tutakapokamilisha ufufuo wa miili na mwanzo wa maisha yetu ya milele. Kwa kuwa hivyo ndivyo hali ilivyo, tunapaswa kuweka tumaini letu siyo tu kwa wokovu ujao (wakati huo huo tukifurahia na kutegemea wokovu tulio nao tayari na tunaou-ishi kwani tu wamoja na Kristo), bali pia tujibidiishe/tujitahidi kuhakikisha kwamba hakuna kinachoingilia muunganiko ulio muhimu sana kati ya pointi ‘A’na pointi ‘C’. Kwani pointi ‘B’, yaani maisha yetu hapa duniani, katika mwili huu tulio nao sasa, inaweza kudumu au kuchukua muda mrefu kidogo baada ya kujitoa kwa Kristo (ingawa katika Mpango wa Mungu ni sawa na kufumba na kufumbua tu ukilinganisha na milele), na ule ‘wokovu wa mwisho’ unakuja tu kwa wale waliookolewa, yaani waumini katika Kristo.

2.12  Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyo[i]tii [ile kweli] sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu [pamoja nanyi], bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.
Wafi. 2:12 SUV

Akiwa kama mwalimu mzuri wa Biblia aliyewajali ‘kondoo wake’ sana, Paulo anawaambia Wafilipi wale “ukweli wote”. Kama waumini, wokovu wetu ni salama kabisa … kama waumini. Hata hivyo, kuna kundi la mbegu katika fundisho-fumbo la mpanzi, ambalo linaanguka juu ya mwamba. Mbegu hii huota haraka na kwa furaha kutokana na wokovu iliyopata … kwa muda tu. Lakini kukatishwa tamaa na [ma]shinikizo ya maisha kunasababisha kundi hili la watu kufifia katika imani mpaka mwisho wake imani inapotea kabisa:

8.13 Na wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi [imara], huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga (huasi).
Lk. 8:13 SUV

Aina hii si waumini tena baada ya kuanguka kwani wanakoma kuamini. Wokovu ni matokeo ya kuweka imani yetu katika Kristo; lakini ikiwa imani inapotea, na wokovu hupotea. Ukweli huu unapaswa kutupa motisha, kama waumini wa Filipi walivyopokea ilani ya kutoka moyoni ya Paulo, ya “kufanyia kazi” wokovu wetu, kwani hilo ndilo jambo muhimu kuliko yote katika maisha yetu. Kwani ikiwa tunasonga mbele kiroho, tukipevuka katika Neno na hivyo katika imani, tukifaulu badala ya kushindwa mitihani inayokuja kwa wale wanaompenda Mungu, na tukivitumia vipaji tulivyopewa katika kulitumikia Kanisa (Mwili) wa Bwana wetu Yesu Kristo, hatutakuwa na la kuogopa: ni wale tu wasiojali ndio walio hatarini, kutokana na kutojali [kwao] kiroho, ya kuanguka. Mungu hatuzuii kuokolewa. Na Apishe mbali wazo hilo! Alimtuma Mwanaye aje kufa ili sisi tuweze kuishi kwa sadaka Yake kwa ajili yetu (Yoh. 3:16); Alimtuma Bwana Yesu Kristo kuukomboa ulimwengu, na si kuuhukumu; matokeo yake, wote walio na imani katika Bwana Yesu Kristo wanaokolewa – na wataokolewa katika siku ile kuu ya mwisho, ikiwa tu imani, ambayo ndiyo chanzo muhimu cha wokovu huu, inaishi.

3.18 Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina [yaani Nafsi] la Mwana pekee wa Mungu.
Yoh. 3:18 SUV

5.4  Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu [katika Kristo].
1Yoh. 5:4 SUV (cf. Aya ya 1)

Wakikutumikia Wewe na si Wenyewe: Kuna mengi yanayotia shani na ya kustaajabisha kuhusiana na Mpango wa Mungu wa jinsi Bwana alivyoambatanisha kila kitu kinachotokea katika maisha yetu na katika historia ya dunia, lakini kimoja kati ya yale yanayostaajabisha zaidi ni ile namna timilifu ambayo maandiko yanawapa waumini ukweli wote unaohitajika kwa ajili ya kukua kiroho na kuishi hapa, katika dunia au ulimwengu wa Shetani.

2 Katika malisho ya majani mabichi hunilaza [mahitaji ya kimwili], Kando ya maji ya utulivu huniongoza (maji ya ile Kweli; Isa. 55:1; Yoh. 3:5; Ufu. 22:17).
3 Hunihuisha nafsi yangu [ie. maisha ya kimwili na kiroho]; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Zab. 23:2-3 SUV

Upaji mtimilifu wa Mungu wa ile kweli ni pamoja na kiasi cha kutosha cha katika maandiko cha habari zinazoonyesha, baada ya kutwaa mwili, kifo cha [ki]roho na ufufuo wa Kristo, kwamba msalaba na Yeye aliyebeba dhambi zetu akiwa juu yake (msalaba) ni sehemu ya mpango wa Mungu tangu Mwanzo – kwa hakika Bwana Yesu Mwenyewe ndiye mpango wa Mungu. Kitu ambacho manabii wa kale hawakukiona na ambacho sisi tumekiona ni Kristo Yeye Mwenyewe, na tunamwona kwa dhahiri zaidi kwa sababu ya maneno waliyopewa kuandika karne nyingi kabla Bwana wetu hajaja katika dunia hii.

15.4  Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini.
War. 15:4 SUV

Kusudi kamili la Sheria ni kuongoza watu waelekee kwenye wokovu (kwa kudhihirisha dhambi ya wanadamu na kutojitosheleza kwetu: War. 3:20; 7:7; Waga. 3:24), lakini ndani yake kuna vivuli ambavyo bila ubishi vinatuelekeza katika ujio wa Kristo na kutolewa Kwake sadaka kwa ajili yetu.

1.29 Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!
Yoh. 1:29 SUV

Injili: Sehemu mojawapo muhimu ya ufunuo endelevu na ambayo Petro anaitilia mkazo katika muktadha wetu wa 1Pet. 1:10-12 ni ile ya namna Injili ilivyoletwa kwa wanadamu. Siku zote Injili ni ile ile: kumtegemea Mungu kwa ajili ya wokovu kutoka dhambi, kifo na hukumu/hatia kwa kuweka imani yetu katika Mbadala Wake kwa ajili ya dhambi zetu, Bwana na Mwokozi wetu mpendwa Yesu Kristo. Walengwa wa barua hii wanakumbushwa na Petro juu ya ukweli kwamba wokovu wao uliasisiwa kupitia kupewa kwao kwa ile kweli na wainjilisti waliopita katika jamii za Asia Ndogo wanaozungumzwa hapa. Kwa kuwa fahirisi (contents) ya waraka huu ina ukweli wa Biblia wenye kina na neema nyingi, tunaweza kuwa na uhakika kwamba Petro, wakati akizungumzia zaidi kuhusu “ile saa walipoamini kwa mara ya kwanza”, analitumia pia neno “Injili” kama linavyotumiwa mara nyingi katika maandiko, yaani kweli yote iliyomo katika maandiko ambayo ndiyo inafanya “habari njema” kuhusu Bwana Yesu Kristo, na ambayo si yote inahitajika ili mtu aokolewe, lakini yote “yanafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kuwaongoza katika uongofu na kuwasahihisha/kuwaadibisha” (2Tim. 3:16). Kuieleza kwa urahisi zaidi, ingawa tunaokolewa kama [watoto] wachanga wa kiroho, tunazaliwa upya kupitia mbegu ya Neno la Mungu, kukua kwetu kusiishie katika utoto huo wa kiroho bali kuendelee kupitia malisho ya maziwa ya Neno Mpaka sote “tufikie kiwango cha kupevuka ambacho kipimo chake ni Kristo” (Waefe. 4:13).

Wakala wa Injili: Kama ambavyo wakala halisi wa wokovu wetu ni Roho Mtakatifu, Yeye ambaye anaufanya ukweli wa Biblia uwe dhahiri kwetu na ueleweke na roho zetu pale tunapoamini kwa mara ya kwanza katika Bwana Yesu Kristo, vivyo hivyo [ni] Roho Mtakatifu ndiye aliyefunua (inspired) maandiko yote matakatifu. Zaidi ya hapo, Yeye ndiye anayefanya iwezekane sisi kuelewa kanuni zote nyingine za Biblia tunapozisikia na tunapokuwa tayari kuziamini – kitu ambacho asiyekuwa Mkristo au asiyeamini hawezi kufanya (1Wakor. 2:13-14). Kukua huku kwa Kanisa mmoja mmoja pekee na kwa ujumla, kutoka uchanga mpaka kupevuka, katikati ya ulimwengu wa Shetani na licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa yule mwovu, ni mwujiza halisi ambao tunapaswa kuupa thamani kuu katika mioyo yetu – na ni kitu ambacho malaika wana shauku kubwa ya kukitazama (1Pet. 1:12).6

Mateso ya Kristo: Utukufu wote ujao una msingi wake katika Bwana Yesu Kristo, katika utimilifu wa Nafsi Yake na kazi Yake katika mateso kwa ajili yetu (1Wakor. 3:11). Bwana Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu na kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote. Kweli hii ndiyo msingi ulio imara wa kila tunachokiamini, matumaini yetu yote na matarajio yetu yote. Alichokifanya katika kujitoa kwa ajili yetu ni vigumu [kwetu] sisi kutambua vyema kwa sasa, lakini tunajua kwamba lilikuwa tukio kuu [lililotokea] katika historia yote, ya wanadamu na malaika. Zaidi ya hayo, kuingia Kwake katika miali ya moto [msalabani] ili abebe dhambi zetu zote ni jambo ambalo ni vigumu kwa sisi kujenga taswira yake mioyoni mwetu. Sehemu ndogo kabisa ya sadaka Yake iko nje kabisa ya uwezo wetu kuelewa, na thamani yake haina kipimo. Bila ya Bwana Yesu kusingekuwa na historia [ya wanadamu] – kusingekuwa na sababu ya kuwa na historia. Bila ya utayari Wake wa kuteswa kwa ajili yetu, tungekuwa tumepotea, na kina cha kupotea huko ni vigumu kukitafakari, kwani kinatisha. Kutwaa hulka ya uwanadamu ijapokuwa Yeye ni Mungu, akatembea hapa duniani kwa utimilifu, alishambuliwa kwa nguvu zote na ukali sana na wajumbe wa Shetani – wa kibinadamu na malaika (waasi), alipata maumivu makali na ufidhuli wa kusulibiwa na matukio yote yaliyotangulia msalaba – ingawa hata sehemu moja tu ya mateso haya yanapaswa kutufanya tutetemeke kwa heshima na woga – hakuna hata moja kati ya hayo inayofikia Yeye kuingia katika lile giza kwa ajili yetu, kupaa katika mwali wa moto (Waamuzi 13:20), kuungua bila kuteketea (Kutoka 3:2) mpaka Aliporidhisha kiwango cha msamaha kwa ajili ya dhambi zetu zote. Hatukuwa laiki (fit), hatukuwa na uwezo, hatukuwa na nia (tuseme ukweli!) wa kubeba adhabu hata ile ndogo kabisa iliyostahili adhabu – lakini Bwana yesu alifanya yote hayo kwa ajili yetu, kutuokoa, kufanikisha ushindi Wake ili aweze kutupata sisi, Bibi Harusi Wake, Kanisa la Kristo.7

19.7  Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.
Ufu. 19:7 SUV

Hitimisho: Maajabu ya ile KWELI ambayo sasa inapatikana ni faraja kwetu katika mateso yoyote ambayo Bwana anaweza kuruhusu tukabiliane nayo, na KWELI hizi zinapaswa, kwa kujifunza, kuziamini na kuzitumia katika maisha yetu, kutusaidia kisaikolojia na kiroho kwa kuweka tumaini letu si katika mambo ya kidunia, bali katika thawabu za milele na tarajio la ripoti nzuri kutoka kwa Mwokozi wetu Yeye aliyeteseka kwa ajili yetu ili tuweze kuwa na uzima wa milele pamoja Naye – tutakapokutana Naye uso kwa uso hatimaye.

Notes:

1. Tazama haswa L. S. Schafer, Systematic Theology, v2, ukurasa 162-199.

2. Kwa mjadala wa kina wa msingi huu na nyaraka zenye utondoti (deatails) mwingi, tizama The Satanic Rebelion, Part 3: “The Purpose, Creation and Fall of Man”, na Bible Basics, Part 3A: “Anthropology”.

3. Juu ua somo la kuzaliwa upya kiroho na uzima wa milele, tizama somo #19 la mfululizo huu, “Spiritual Rebirth”, [#19 “Kuzaliwa Upya Kiroho”: tafsiri ya Kiswahili], pamoja na “Bible Basics, Part 4B: “Soteriology”.

4. Tizama “The Judgment of the Church”, section I.7 ya Coming Tribulation part 6, “Last Things”.

5. Katika somo #22 la mfululizo huu, na pia sehemu ya 1 ya Satanic Rebellion, sehemu ya I.2.d, “Angels are similar to mankind in several important ways”. Ili kuona uwezekana kwamba matukio ya hapa duniani yanatizamwa kwa makini na waumini walioondoka duniani, tazama sehemu ya 2B ya Coming Tribulation series, chini ya “The Heavenly Sea”.

6. Tazama Bible Basics Part 5: “Pneumatology: The Study of the Holy Spirit”.

7. Tazama Bible Basics, Part 4A: “Christology”, sehemu II.5: “The Spiritual Death of Christ”.

=0=

Translated from: Personal Salvation and Spiritual Progress: Peter’s Epistles #28

=0=

Basi, na tuonane katika somo #29 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!