Maria “Mama wa Mungu”!?
Biblia inasema nini kuhusu Maria, mama wa Bwana wetu, na jinsi ya kumwonyesha heshima kuu anayostahili?
Dibaji.
Maneno ya Kiingereza: venerate, worship; maana yake ni moja: abudu, sujudia, tukuza, -cha, penda mno, heshimu sana, sifu, jali sana. Baadhi ya maneno haya yametumika na Kanisa Katoliki – lile la Orthodox la Mashariki na lile la Roma, pamoja na makanisa mengine katika kumfanyia wasifu na ibada “Bikira Maria”.
Mathayo 4:9-10:
4.8 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno [vantage point], akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,
4.9 akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.
4.10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake (Kumb. 6:13).
Warumi 1:25:
1.25 Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayepaswa kuhimidiwa milele. Amina.
Wakolosai 2:18:
2.18 Usiache mtu yeyote amiliki maisha yako, katika kusudi lake la [kukufanya uwe mtumwa wake], akikuonyesha unyenyekevu wa kinafiki na ibada zake za malaika, akikusimulia ‘maono’ yake, wakati ni majivuno tu yanayotokana na fikra zake za kimwili, na wala hakishiki Kichwa [ambacho ni Kristo].
Ufunuo 22:8-9:
22.8 Nami Yohana ndimi niliyeyasikia na kuyaona mambo hayo. Na hapo nilipoyasikia na kuyaona nalianguka, ili nisujudu mbele ya miguu ya malaika yule mwenye kunionyesha hayo.
22.9 Naye akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako (mtumishi kama wewe!), na wa ndugu zako manabii, na wa wale wayashikao maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu!
=0=
Maria, aliyekuwa mnyenyekevu sana, “alionyeshwa fadhila, neema” na Mungu (Luka 1:28) na ndugu yake Elizabeti alimwita “mama wa Bwana wangu” (Luka 1:43). Zaidi ya hapo, wimbo wa Maria mwenyewe, ambao ulitokana na kujazwa na Roho Mtakatifu, ulisema kwamba vizazi vijavyo vitamwita “mbarikiwa” (Luka 1:48).
Hii inaonyesha kwamba waumini wanapaswa kuwa na heshima kuu kwa Maria. Lakini heshima ambayo baadhi ya Wakatoliki wanamwonyesha Maria inavuka mipaka ya neno “heshima” na hii ndiyo sababu wakati mwingine wanashambuliwa na Waprotestanti kwa kusema kwamba wanamwabudu.
Hapa ndipo suala hili linakuwa changamano na lenye utata. Tafadhali rejea dibaji hapo juu. Tofauti kubwa hapa ni kwamba kuabudu/ibada/uchaji huelekezwa kwa Mungu. Hata hivyo neno “worship” wakati mwingine hutumika kwa watu kama walengwa. Kwa mfano, nikisema katika Kiingereza “I worship my wife” nitakuwa ninamaanisha kwamba ninampenda na kumheshimu sana. Lakini pia nikisema “Our culture worships youth”, hii itakuwa na maana kwamba katika utamaduni wetu, vijana na ujana uanaabudiwa katika namna ya kidini.
Katika maana yake sisisi (literal meaning), maneno ya Kiebrania na Kiyunani yanayomaanisha “kusujudia” ambayo ni shachah na proskuneό yanaashiria ‘kulala kifudifudi’ au ‘kuinama mpaka chini mbele ya’ mlengwa wa matendo hayo kwa makusudi ya kuonyesha heshima kuu, ibada.
Yote haya yanatupeleka kwenye swali: Je, Wakatoliki na watu wengine wanaomwabudu “Bikira” Maria wanaonyesha heshima kuu kwake au wanamsujudia kama mungu? Kama wanaonyesha heshima kuu kwa mama wa Bwana Yesu Kristo katika ubinadamu wake, basi hakuna tatizo lolote, kwani Luka 1:48 inatuambia kwamba vizazi vijavyo (ambavyo sisi ni wamoja wapo) vitamwita “mbarikiwa”. Lakini ikiwa wanamwabudu “Bikira” Maria kama mungu au katika namna au staili ya ‘kuabudu sanamu’, basi ni dhahiri kabisa hapa kuna mushkeli, kwani hii ni kuvunja amri zile kuu za mwanzo kati ya zile amri kumi za Mungu:
1. Usiwe na miungu mingine ila Mimi.
2. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu kingine kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvionyesha heshima kwa kuviinamia; kwa kuwa Mimi Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.
Kutoka 20:3-5 SUV
Hii yote inaonyesha kwamba kinachofanyika ndani ya moyo wa mtu ndicho kilicho muhimu katika suala hili. Kwa maneno mengine, Mungu na mtu anayemheshimu Maria ndio wanaojua kwamba heshima hiyo ni heshima tu na si zaidi, au ni kuabudu kwa maana iliyo sawa na ibada ya sanamu au mungu wa kuchonga. Ni dhahiri, hata hivyo, kwamba mwenendo wowote ambao unatoa hata ‘harufu’ tu ya ibada ya sanamu au mwenendo huo huo ukionyesha kwamba Maria anachukuliwa kuwa ni zaidi ya mwanadamu aliyepewa fadhili na neema kuu na Mungu, basi unapaswa kuachwa mara moja.
Je, Maria ni “Mama wa Mungu”?
Jibu ni hapana. Kama vile Elizabeti alivyoonyesha katika Luka 1:43, Maria ni mama wa Bwana wetu Yesu Kristo aliyekuwako hapa duniani kimwili miaka takriban 2000 iliyopita, lakini siyo “mama wa Mungu”, huyu Mungu aliye hai, Yahweh. Aya ifuatayo inasaidia kueleza hili:
6 Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani [ustawi].
Isaya 9:6
Wakati mtoto mchanga alizaliwa hapa duniani kupitia Maria kwa uweza wa Roho Mtakatifu, tulipewa Mwana wa Mungu, kwa sababu Mungu Mwana amekuwepo tangu milele yote. [Tofautisha hapa kati ya hulka Yake ya kibinadamu na ile ya Kimungu!] Aya hii hapa chini inatupatia mwanga zaidi. Usisahau kwamba “Neno” inamaanisha Kristo.
1.1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno [Yesu Kristo], naye Neno alikuwako kwa Mungu [Baba], naye Neno alikuwa Mungu.
1.2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
1.3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.
1.4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.
1.5 Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza.
1.6 Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.
1.7 Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye.
1.8 Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru.
1.9 Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu.
1.10 Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua.
1.11 Alikuja kwake [ulimwenguni], wala walio wake hawakumpokea.
1.12 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;
1.13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.
1.14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Yohana 1:1-14
Kama unavyoona, yule Kristo mkuu ni Mungu, na dunia pamoja na ulimwengu viliumbwa kupitia kwa Yeye. Kwa hiyo Maria siyo mama wa yule anayeitwa Neno, kwani Neno alikuwako tangu milele iliyopita na Ndiye aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo; Maria alikuwa [tu] ni chombo kilichobarikiwa, kilichopewa fadhila kuu ya kutumika katika kumleta yule Neno kama mwanadamu hapa duniani.
Mtazamo wa Bwana Yesu mwenyewe kwa Maria.
Kristo alikuwa na mtazamo gani kwa mama yake? Ebu tafakari mazungumzo haya kati ya Bwana Yesu na mwanamke fulani aliyeshuhudia Bwana Yesu akitoa pepo kutoka kwa bubu mmoja:
11.27 Ikawa alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya.
11.28 Lakini yeye alisema, Afadhali [ungesema], heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.
Luka 11:27-28
Kristo hakubisha kwamba Maria alikuwa amebarikiwa, lakini kwa uwazi kabisa hakukubaliana na wazo la kumfanya mlengwa wa ibada, sujudu, kwani mama yake hakuwa mungu na haikuwa sahihi kumchukulia hivyo. Nafasi ya heshima aliyokuwa nayo Maria kama mama wa [ki]mwili wa Kristo haikumpa heshima kubwa zaidi ya kubarikiwa kwa watu wengine waliolipokea Neno la Mungu, kuliweka moyoni na kulifanyia kazi.
Uzito wa hoja hii unaongezwa na tukio lingine lililofanyika baadaye:
8.19 Wakamwendea mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano.
8.20 Akaletewa habari akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe.
8.21 Akawajibu akasema, Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya.
Luka 8:19-21
Kristo alimpenda, alimjali (Yoh. 19:25-27) na kumheshimu sana mama Yake, hata hivyo aliwapa heshima sawa sawa (kama aliyompa mama Yake) wale waliokuwa wakiitafuta kweli na walioishi maisha yao kutokana na kweli hiyo – vigezo hivi ndivyo alivyovitumia katika uhusiano wake na ndugu zake, yaani utayari wao wa kuipokea na kuishi kutokana na kweli.
Ebu jipe dakika kadhaa, uliache hili liingie moyoni mwako na ulitafakari.
Neno la tamati.
Maria anapaswa kuheshimiwa kama mwanamke aliyetunukiwa na Mungu kumzaa na kumlea mtoto Yesu, kutoka utotoni mpaka ukubwani. Anapaswa kupendwa sana – kuheshimiwa sana – kwa jambo na jukumu hili alilolifanikisha kwa weledi mkuu. Lakini, kama Kristo mwenyewe alivyoainisha hapo juu, mtu yeyote anayelitafuta Neno la Mungu na anayeweka juhudi katika kuishi kwa mafundisho ya Neno hilo, anapaswa kupewa heshima sawa sawa na mama Yake (na hili linatujumuisha wewe na mimi, ikiwa tunatimiza hili kwa dhati).
Nukuu katika maandiko (katika vitabu vya Injili na Matendo ya Mitume) zinazomzungumzia Maria zinamdhihirisha kuwa ni mwanamke wa kawaida, ingawa alipewa na Mungu jukumu lisilo la kawaida:
• Baada ya Bwana Yesu kuzaliwa, Maria na Yosefu walikuwa na mahusiano ya kawaida ya kimwili kama mke na mume yeyote wa kawaida, ambapo walizaliwa watoto kadhaa (Matt. 13:54-56; Marko 6:3). [“Bikira daima?!”].
• Bwana Yesu alimlaumu kwa upole mama Yake pale aliposhindwa kuiona shauku Yake kuu kuhusu masuala ya Mungu (Luka 2:43-50).
• Miaka 18 baadaye Bwana Yesu alitenda mwujiza pale Kana kwa ombi la mama Yake, lakini pia hapa alimwonya tena kwa upole (Yoh. 2:1-11).
• Kristo alipokuwa msalabani, alikabidhi matunzo ya mama Yake kwa Yohana (Yoh. 19:26-27) na, baada ya kupaa mbinguni, Maria na wanawe wa kiume walikuwa pamoja na waumini wengine Yerusalemu wakimngojea Roho Mtakatifu waliyeahidiwa (Matendo 1:14).
Kama unavyoona, hakuna sababu yoyote ya uwepo wa “kanuni” za Kikatoliki zilizobuniwa mamia ya miaka baada ya matukio yaliyoorodheshwa hapa juu ambazo ziliongeza sifa zisizostahili katika kuonyesha heshima kwa mama wa Kristo. Tazama yafuatayo:
• “Kukingiwa dhambi ya asili” - kanuni hii inapendekeza kwamba Maria hakuwa na dhambi, yaani alizaliwa “bila dhambi ya asili”. Kwanza, fundisho au kanuni yenyewe ya “dhambi ya asili” siyo sahihi. Kanuni sahihi ya Kibiblia inaitwa “hulka ya dhambi” iliyo katika miili yetu, ambayo tumerithi kutoka kwa Adamu baada ya yeye kuanguka. Imani ya “kukingiwa dhambi ya asili” ambayo si kanuni sahihi ilifanywa dogma ya kanisa Katoliki mwaka 1854 (mara nyingi inachanganywa na kanuni sahihi ya Kibiblia ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu na Maria wakati angali bikira – the Incarnation, yaani umwilisho).
• “Bikira daima”, kanuni inayodai kwamba Maria alikuwa bikira wakati wote – kabla, wakati na baada ya uzazi wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kanuni hii bandia ina mwanzo wake katika miaka ya 350 – 400 AD.
• “Kupalizwa mbinguni”, dhana potofu kwamba Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho baada ya uhai wake wa hapa duniani. Hii ilichukuliwa kama dogma rasmi ya kanisa Katoliki mnamo mwaka 1950.
• “Mpatanishi” (Mediatrix), dhana kwamba Maria anaweza kutumika kama mpatanishi wetu huko mbinguni, yaani mpatanishi katika kuokolewa kupitia Kristo na kwamba Kristo anatupatia neema kupitia yeye. Dhana hii potofu ya Maria kuwa ni mpatanishi wa dunia nzima ilianza kuenea hapo karne ya 4 kwa njia ya ‘sala ya Efraim Msiria’. Viongozi kadhaa wa kanisa Katoliki wametumia dhana hii katika mafundisho yao tangu karne ya 5, kwa mfano waandishi Louis de Montfort na Alphonsus Ligioni katika karne ya 18.
Imani hizi zote zilianza baada ya Biblia kukamilika na kufungwa, na hivyo zimetoka nje ya Biblia; tusisahau kwamba dhana/mafundisho haya ni ya kutungwa na watu, ni ya kubuni, na hivyo yanapaswa kukataliwa.
Somo hili limetoka katika tovuti ya https://fountainoflifetm.com “What’s the Bible say about Mary and Mary veneration?”, kwa ruksa mahususi ya mwenye tovuti. Kama kuna makosa yoyote, basi ni yangu mimi niliyetafsiri.
This article has been translated from the website https://fountainoflifetm.com by specific permission from the owners of that website. If there be any errors in translation causing any changes in meaning, I bear all responsibility.
Respicius Luciani Kilambo.
Mafundisho ya ziada:
Maria alihusika tu katika kuhakikisha Yesu Kristo anapata mwili na hulka ya kibinadamu – alipata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu na hivyo yeye ndiye mama wa Kristo katika upande wake wa kibinadamu. Ni wazi kwamba katika Uungu Wake alikuwako tangu milele iliyopita, muda mwingi kabla ya Maria kuzaliwa hapa duniani, na kama Mungu, hawezi kuwa na mama! Kwa kuwa Bwana Yesu Kristo amepokea mwili wake kutoka kwa Maria kwa njia ya Roho Mtakatifu, maandiko hayamwiti Maria “mama wa Mungu”.
Ni muhimu sana kuelewa kwamba title aliyopewa Maria na Elizabeti katika Luka 1:43 – “mama wa Bwana wangu” - haimaanishi/haiko sawa sawa na kusema “mama wa Mungu”. Title ya “Bwana” inamzungumzia Kristo kuwa na hulka mbili – uanadamu na uungu. Kristo wakati wote amekuwa Mungu na hivyo kwa wazi kabisa hawezi kuwa na mama, lakini kwa ajili yetu amekuwa pia mtu (Isa. 9:6; Yoh. 1:14; Waga. 4:4; Wafi. 2:6-7; 1Tim. 3:16; Waebr. 2:14; 1Yoh. 1:1, 4:2; 2Yoh. 7), na Maria ndiye mama wa hulka Yake ya ki-utu.
Akiwa chini ya ufunuo wa Roho Mtakatifu (Luka 1:41), Elizabeti asingeweza kusema Maria ni “mama wa Mungu wangu”, kwa sababu Kristo mwenyewe ni Mungu wa milele yote, aliyeumba na hakuumbwa (Yoh. 1:3, 10; Wakolosai 1:16-17), Yeye si muumbwa anayehitaji mama. Lakini aliweza kuitumia title ya “mama wa Bwana wangu”, kwa sababu hii title “Bwana” inajumuisha hulka mbili za Kristo, ile hulka ya kibinadamu ambayo wakati huo ikikaribia kudhihirika kwani Maria alikuwa tayari na mimba wakati Elizabeti na Maria wanakutana.
Mwisho.
Respicius Luciani Kilambo
https://sayuni.co.tz