Mwalimu, Utahukumiwa kwa Ukali Zaidi! Yakobo 3:1
Ndugu zangu, ninawasalimu katika Jina Takatifu la Bwana Yesu Kristo!
Baada ya kuokolewa (Yoh. 3:16), tunaamriwa kukua kiroho katika Neno (kusoma Biblia na kupata mafundisho ya Biblia), kuamini Neno hilo na kuishi kwa kulitumia na mwisho kulihudumia Kanisa la Kristo, yaani Mwili Wake, kulingana na vipaji tulivyopewa wakati tunazaliwa upya. Katika wakati ule tunapookolewa tunapewa vipaji au vipawa na Roho Mtakatifu ili tupevuke navyo kiroho, na kisha tuvitumie vipawa hivyo katika huduma yetu kwa Kanisa tunapofikia kiwango stahiki cha kupevuka kiroho kwa misingi ya Neno tunalofundishwa.
Leo nitazungumzia kipaji cha Mkristo cha Ualimu. Mchungaji, Mwalimu, Mzee wa Kanisa, hao wote HUFUNDISHA. Lakini Yakobo anasema, anapowazungumzia WAALIMU wa Neno la Mungu katika Yakobo 3:1: “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua yakuwa mtapata hukumu kubwa zaidi (SUV). Katika tafsiri ya NENO BIBLIA aya hii imeandikwa hivi: Ndugu zangu, msiwe walimu wengi, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi.
Ebu tutizame kwa kifupi fundisho la vipaji unavyopewa wewe MKRISTO mara tu unapozaliwa upya; unapewa vipaji hivi kupitia uwakala wa Roho Mtakatifu. Tunaona orodha ya vipaji vya Roho Mtakatifu katika 1Wakorintho12, Isaya 11:2-3, na pia Warumi 12.
Kipaji cha BUSARA: Mfalme Solomoni aliomba kipaji hiki na alipewa. Ikumbukwe yeye alikuwa mtoto wa Mfalme Daudi ambaye alikuwa mpendwa wa Mungu. Mara nyingi Mungu alimwelezea Daudi kama “mtumishi wangu”. Solomoni alijua kwamba viatu vya mfalme Daudi ni “vikubwa” kweli; hivyo aliomba busara ili aweze kuvivaa na vimwenee!
Kipaji cha ELIMU: Kipaji hiki hupewa wale ambao hufundisha. Mchungaji, Mwalimu, Mzee wa Kanisa, n.k., wote hao HUFUNDISHA.
Kipaji cha IMANI: Abrahamu na Musa ni mifano mizuri.
Kipaji cha UPONYAJI: Tahadhari! Hapa kuna utata mwingi tu katika Kanisa. Kwa kweli kumekuwa na mifano mingi ya udanganyifu katika Kanisa la LEO kuhusiana na UPONYAJI. Pia kwa uhakika Kanisa la wakati ule wa Mitume lilikuwa na kipaji cha uponyaji. Wakati ule mtu aliweza kupitiwa na kivuli tu cha Mtume wa Bwana Yesu na akaponywa ugonjwa wake (Matendo 5:15). Kwa upande mwingine, LEO HII, nguvu ya sala huponya – Yakobo 5:16. Mungu anapojibu sala yako, basi Atakuponya kama inaendana na MPANGO WAKE KWAKO na kwa Kanisa lake!
Kipaji cha MIUJIZA: Mfano mzuri wa mwujiza ni kumwombea mtu asiyeamini, kumtangazia Injili, naye anakuja kwa Bwana Yesu.
Kipaji cha UNABII: Kwa lugha ya Kiingereza tutasema “PROPHECY” – maana yake SIYO kujua yatakayotokea baadaye (!) bali kuutangaza Ufalme wa Mungu. Ina maana kufundisha Neno kwa watu, au mbele ya watu; kuutangaza Ufalme. Kipaji hiki kinaendana na kile cha ELIMU hapo juu.
Kipaji cha UFAHAMU: Kwa lugha ya Kiingereza “discernment”. Hii ni kujua nia au malengo ya watu hata bila kuambiwa. Mfano ni Petro katika Matendo 5:1-10, alipoijua dhamira mbaya ya Ananias na mkewe Sapphira kuhusiana na pesa.
Kipaji cha LUGHA: Tahadhari ingine HAPA. Kipaji hiki hukuwezesha kunena lugha ya/za kigeni ambayo/zo hujafundishwa, na MKALIMANI akatafsiri. Ieleweke kwamba katika 1Wakorinto 12-14, Paulo anazungumzia LUGHA kwa maana ya ONYO kwa sababu Wakorinto wale walitumia vibaya kipaji hiki. Hivyo kunena kwa lugha kama kipaji cha Roho Mtakatifu ni LUGHA inayoeleweka, siyo kubwabwaja sauti zisizoeleweka (ecstatic gibberish)! Katika Matendo 2, baada ya kujazwa na Roho Mtakatifu, walinena lugha za kigeni wakitangaza Neno ili wageni waweze kuielewa Injili na kuiona nguvu ya Bwana, halafu waokoke.
Kipaji cha KUTAFSIRI LUGHA: Paulo alionya kuwa ni lazima kuwe na MKALIMANI mahala inaposemwa lugha ya kigeni, kwa kipaji au la, katika mafundisho ya Neno. Kama hakuna mkalimani basi nyamaza, kwani hakuna atakayeelewa kinachosemwa, na lengo ni kuelewa. Pili, lugha ya kigeni isemwe na mtu mmoja baada ya mwingine; vinginevyo, wakisema wote kwa pamoja inakuwa fujo na asiyeamini akiwaona hataamini na atadhani ninyi ni wendawazimu! Au walevi. Kipaji hiki kinalengwa kama ushuhuda kwa wasiomamini, siyo kwa Kanisa.
Katika Warumi 12: 7-8 tunasoma kuhusu vipaji vya ziada: kufanya kazi mbalimbali katika Kanisa Lake, kutiana moyo, kusaidiana, kuongoza, kusameheana/huruma.
Katika Waefeso 4:11 tunakutana na vipaji vya Uinjilisti, Unabii, UTUME (kwa Kimombo “Apostleship”). Tahadhari kubwa hapa: Hakuwezi kuwa na MITUME tena LEO. Hao walichaguliwa na Bwana Yesu Mwenyewe. Kuna mfano wa Matias na Paulo, Matendo 1:15 – 26: Matias alipigiwa kura na Mitume na wanafunzi wengine, lakini Paulo alitokewa na kuchaguliwa na Bwana Yesu Mwenyewe na kuchaguliwa kuwa Mtume Wake kwa Mataifa, Matendo 9:15. Hivyo Paulo ndiye mbadala wa Yuda Iskariote. Hawa mitume Wake ni LAZIMA WAWE 12, idadi yao, kutokana na Mpango wa Mungu, Ufunuo 21:14. Hivyo hao wanaojiita MITUME (APOSTLES) LEO HII wanafanya hivyo kwa mamlaka yao wenyewe!
Kuna vipaji vingine lukuki ambavyo Mungu havigawa kwa watakatifu Wake.
Sasa turudi kwenye mada. Tuanze na tafsiri ndefu ya Yakobo 3:1:
Ndugu zangu, kaka na dada, kabla ya kuamua kuwa waalimu wa Neno, tujichunguze kama kweli tunacho hicho kipaji au kipawa (cha ualimu), kwani sisi tutahukumiwa (tutapimwa, tutatathminiwa) kwa kiwango cha juu zaidi.
Hivyo kwanza tunapaswa kuwa na hicho kipaji cha kufundisha, lakini hiyo pekee haitoshi; tunapaswa kuwa tumejielimisha pia, katika Neno la Mungu (Biblia), kwa muda wa kutosha, na kupimwa na Mungu Mwenyewe katika elimu hiyo kwa kupitia mitihani mbalimbali. Tunapaswa kuwa na uhakika kuwa Roho Mtakatifu ametuongoza katika uamuzi wetu wa kuwa waalimu wa Neno, 1Wakorintho 12:11. Yakobo anasema kuwa MWALIMU atatathminiwa (na Bwana Yesu Mwenyewe, baada ya ufufuo) kwa kiwango cha juu zaidi, kwani yeye, mwalimu, anahusika na maendeleo ya kiroho ya watu wengine – Kanisa Lake. Na tusisahau, Bwana Yesu hafanyi mchezo na Kanisa Lake, alilinunua kwa Damu Yake, kwa mateso makuu ya moto kwa masaa matatu katika lile giza la Golgotha, na hata kabla ya hapo, katika maisha Yake. Hivyo Mwalimu akifundisha uwongo au kanuni isiyo ya kweli, atakuwa amempotosha mtu au watu wengine wanaomtegemea yeye kwa makuzi yao ya kiroho.
Sasa, ebu tutizame mfano kutoka katika maandiko. 1Timoteo 2:11-12 tunasoma hivi: “Simpi mwanamke ruksa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kuwa kimya”. Katika 1Timoteo 2:13-14, Paulo anaelezea SABABU za fundisho/elekezo hilo. Na katika 1Timoteo 2:16, anaelezea mojawapo ya THAWABU atakazopata mwanamke mwadilifu hapa duniani kuhusiana na uzazi. Tukienda katika 1Timothy 3:1-15 tunapata maelekezo zaidi kutoka kwa Mtume Paulo kuhusiana na UONGOZI wa juu wa kanisa la msingi (local church). Soma pia Tito 1:6-9. Ni wazi kabisa Paulo anatufundisha kwamba uongozi wa juu wa kanisa ni mwendelezo wa uongozi wa FAMILIA, ambao ni jukumu la mwanaume, mahala popote pale litakapokuwa. Sasa, tukirudi kwenye fundisho la VIPAJI, haijaandikwa pale kwamba ni wanaume TU waliopewa vipaji vya kufundisha, au vipaji vya uongozi! Kwenye FUNDISHO LA VIPAJI, HAKUNA MGAWANYIKO WA JINSIA, ni wazi kwamba vipaji vimegawanywa kwa jinsia zote (Miriam – Exodus 15:20; Deborah – Waamuzi 4:4; Huldah - 2Wafalme 22:14; mke wa Isaya - Isa. 8:3, wote hawa walikuwa manabii). Na pia tunajua kwamba Maandiko hayana mgongano wa ndani kwa ndani. Hivyo mwanamke naye hupata vipaji vya ualimu, elimu, uongozi, nk., na kwa uhakika ukitizama katika Kanisa wapo wanawake wenye vipaji hivi. Sasa, akitokea Mwalimu ambaye hajalielewa hili katika mapana na marefu yake akamfundisha mwanamke (mwenye vipaji hivi) kwamba asivitumie atakuwa amempotosha Mkristo mwenzake. Rudia tena kusoma Yakobo 3:1. Swali, Mungu kampa dada huyu vipaji hivi ili afanye navyo nini? Ili Dada yetu awe Askofu? HAPANA, Paulo amelikataza hilo. Awe Mchungaji? HAPANA. Awe Mzee wa Kanisa? HAPANA, Mtume Paulo amelikataza hilo pia! Ama kwa hakika Kanisa linazo nafasi nyingi ambazo zinahitaji vipaji vya ualimu, uongozi, elimu, nk. Huyu Dada mpendwa wa Mungu aliyepewa vipaji hivi anaweza KUFUNDISHA WANAWAKE WENZAKE, WATOTO, VIJANA WADOGO, anaweza kushirikiana na wanaume katika uinjilisti, kwaya, nk. Anaweza kushika nafasi mbalimbali (tofauti na hizi) za uongozi katika Kanisa; na tusisahau, Kanisa la leo lina Idara, sekta, shughuli nyingi ambamo mwanamke hakatazwi kushika nafasi za ufundishaji, uongozi, nk.
Na Paulo anaposema “… inampasa kukaa kimya” maana yake nini? Asiseme lolote? HAPANA! Asitoe dukuduku lake kwa hali yoyote? Hapana kabisa! Katika Darasa la Neno la Mungu, mwanamke atafuata taratibu zote zilizowekwa, ikiwa ni pamoja na kutomvuruga mwalimu, kutopiga kelele, kutoingilia mtiririko wa somo bila mpango, n.k., kama ilivyo kwa wanaume. Kanuni hii haina maana kwamba mwanamke asiongee kabisa katika Kanisa; lakini ikiwa Kanisa fulani limeiweka kanuni hii kwa maana hiyo, basi Dada yetu anaweza kuuliza swali au kutoa hoja kupitia mume wake, kaka yake, baba yake, nk. Kitu muhimu ni kwamba Kanisa hili liwe na taratibu za kuendesha mambo yake bila kukandamiza daraja fulani la waumini wake mpaka wakajiona wao ni watu wa chini. Na haiyumkini wako wanawake ambao katika UFUFUO watakuwa na MATAJI YOTE MATATU wakati waume zao wa hapa duniani hawana hata moja! Haya niambiye, Mr mimi-ni-mwanaume, nani atakuwa “bosi” wa nani hapo?!
Tuchukue mfano mwingine. Fundisho la UNYAKUO. Kuna Pre-Tribbers – wanaoamini kuwa Maandiko yanafundisha kwamba Wakristo watanyakuliwa KABLA ya dhiki – pre-tribulation rapture (mfano ni vitabu na filamu za Left Behind); Mid-Tribbers – wanaoamini kuwa Maandiko yanafundisha Wakristo watanyakauliwa KATIKATI ya kipindi cha dhiki – mid-tribulation rapture; na Post-Tribbers – wanaoamini kuwa Maandiko yanafundisha Wakristo watanyakuliwa BAADA ya dhiki – Post-Tribulation rapture. Sasa, WEWE Mwalimu, Askofu, Mchungaji, nk, unayefundisha kuwa Unyakuo-Kabla-ya-Dhiki ndiyo sahihi (kama Left Behind series wanavyotuambia); ikitokea kwamba siyo sahihi, kwamba Wakristo imewapasa kupitia Dhiki – iwe Dhiki ndogo ya miaka 3.5 au baada ya hapo NA Dhiki Kuu pia, nayo ya miaka mingine 3.5 (jumla 7!), ndipo Bwana Yesu atakuja kunyakua Kanisa Lake kutoka mikononi mwa Mpinga-Kristo, si utawaacha Wakristo wenzako wakiwa hawana utayari wa kiroho na kisaikolojia wa kupambana na dhiki ile (Ufu. 14:12), kama kukosa uwezo wa kufanya biashara, nk, na wanaweza kupoteza imani yao?
Nafikiri mpaka hapo tunaweza kuona umuhimu wa mwalimu wa Biblia kuwa amejitayarisha kiasi cha kutosha, siyo tu darasani/chuoni, bali yeye mwenyewe kujisomea kwa bidii kweli kweli na kuielewa misingi yote mikuu kwa kiasi cha kutosha (kwa uwezo wake wote; haiwezekani kwa mtu mmoja kuelewa vyote kwa asilimia 100!); lakini ile misingi, kanuni, unapaswa kuwa umeipatia sawasawa, usijekutana na lile panga la HAKI la Bwana Yesu linalokata sawasawa na ukaonekana na mapungufu ya kufundisha kanuni zisizo za kweli. Lakini, hayo yote hapo juu yaongozwe kwa SALA zisizokoma kila siku, usijepoteza mataji yako matatu bure.
Ndugu zangu, kaka na dada, ninawaombea upendo; lakini pia ninawaombea masomo mema ya Biblia. Natumaini mumeona umuhimu wa kujifunza kila siku.
Imeandikwa na Respicius Kilambo Luciani
rk@sayuni.co.tz 0737-050950.