Kukua Kiroho, Somo la Awali: Nyaraka za Mtume Petro #10
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo
Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission For This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted By
Dr. R. D. Luginbill
Mapitio: Katika masomo ya nyuma, tumeona jinsi Petro alivyoanza barua yake ya kwanza kwa kuwakumbusha wasomaji wake kuhusika kwa karibu kabisa kwa Nafsi zote tatu za Utatu Mtakatifu katika maisha ya kila Mkristo. Japokuwa ugumu wa maisha ya hawa Wakristo wa mwanzoni ulikuwa unawasababishia simanzi kubwa, Petro aliwaambia kwamba badala ya kufa moyo, wanapaswa kuichukulia hali yao katika “mtazamo wa imani”.
Mtazamo wa Imani: Katika macho ya ulimwengu, hawa waumini masikini wa karne ya kwanza walikuwa ni watu waliotengwa, walikuwa ni watu walioshindwa maisha, lakini “kwa macho ya imani” tunaona taswira tofauti kabisa. Mbele za macho ya Mungu, waumini wale walikuwa “washindi”, baada ya kuchaguliwa na Mungu mwenyewe kwa ajili ya neema tele katika maisha yao ya hapa duniani na neema zisizo mfano katika maisha ya milele. Kwa kumwamini Kristo, wamekuwa sehemu muhimu ya Mpango wa Mungu, ambao kwa kila mmoja wao ulikuwa unawapeleka mbele, unawalinda na unawaongoza katika namna ambayo macho ya wanadamu hayawezi kuona. Ni nani anayeweza kuona usimamizi wa Mungu Baba, wenye uangalifu mkuu, wa mazingira ya kila mmoja wetu ambao umetufikisha katika wokovu, kila mmoja wetu katika namna na wakati wake? Ni nani anayeweza kuona na kuelewa jinsi walivyoongozwa (walivyohawiliwa) na Roho Mtakatifu mpaka wakaingia katika familia ya Mungu, au kusamehewa dhambi zao kwa msingi wa kazi ya Bwana Yesu waliyoiamini? Japokuwa ulimwengu haukuuona mchakato huu ukifanyika, waumini hawa walikuja kuwa wana wa Mungu, na warithi wa ahadi Zake zote. Hata hivyo, mpango wa Mungu kwa ajili ya maisha yao haukumalizika baada tu ya wao kuwa Wakristo. Walitakiwa kuendelea kubaki hapa duniani ili wafanikishe wito na lengo ambalo Mungu aliwaamrisha kwa kila mmoja wao. Wakati Mpango wa Mungu kwa kila mmoja wetu ni tofauti, misingi yake ni ile ile: kukua kiroho, na kuwasaidia wengine katika kukua kiroho.
Kuwasaidia wengine kukua kiroho inaitwa “huduma” au “utumishi”. Kama waumini wa Bwana Yesu Kristo, sisi sote, kwa namna moja ama nyingine, ni watumishi wa Bwana, na kwa kiasi kile tulichoendelea katika kukua kiroho, Mungu anatupa fursa ya kuwasaidia wengine kukua pia. Kwa mfano, sote tuna rafiki na jirani Wakristo ambao wanahitaji kutiwa moyo na pia kupewa msaada wa aina nyingine kwa nyakati tofauti. Kwa kuwapa msaada wa hali na mali, tunawapa mkono katika njia inayoelekea kwenye lile lengo letu ambalo ni moja, la kupevuka kiroho. Kwa ujumla, tunavyozidi kupevuka kiroho, utumishi wetu au huduma yetu kwa Kanisa la Bwana inazidi kuwekwa na kuonekana wazi katika akili na nia zetu, na inazidi kuwa na “kishindo” zaidi katika matokeo yake.
Zaidi ya msaada wa kawaida na fadhila kwa Wakristo wenzetu, kila mmoja wetu alipewa kipaji au vipaji vya kiroho na Roho Mtakatifu wakati ule tulipomkubali na kumpokea Kristo kama Mwokozi wetu – Wakor. 12:11. Tunaweza kusema kipaji hiki au vipaji hivi vya kiroho vina lengo la kumwezesha Mkristo katika maeneo fulani ya kazi ya Kanisa ili kuwawezesha Wakristo wengine kukua katika imani yao. Kwa mfano, si kila mmoja wetu ana kipaji cha kuwa mmsionari, yaani kutumika katika nchi na/au mazingira ya kigeni. Lakini Mungu amenyunyiza kipaji hiki cha umisionari kati yetu, na waumini wenye kipaji hiki wanavyokua kiroho na wanavyoanza kujiuliza kuhusu uelekeo wa kipaji chao na eneo wanaloweza kutumika katika Kanisa la Bwana, wanajikuta wanaanza kuvutika na eneo fulani la utumishi: katika mfano wetu ni kazi ya umisionari. Ninataka kutilia mkazo hapa kwamba mafanikio ya kipaji cha kiroho yanategemea kukua kiroho kwanza, na hata kutambua tu kipaji chako cha kiroho kunahitaji muda pia, na maendeleo ya kutosha ya kiroho.
Vipaji vingine vinahitaji mafunzo ya kipekee na matayarisho kabla havijatumiwa ipasavyo, lakini ni muhimu sana kukumbuka kwamba Mwili wa Kristo, yaani Kanisa Lake, linahitaji waumini wake wote, na vipaji vyao vyote, ili kufanya kazi sawasawa. Paulo anatilia hili mkazo katika 1Wakor. 12:12-31, anaposema kwamba Kanisa linahitaji sehemu au idara zake zote ili kufanya kazi kwa ufanisi kama vile mwili wa mwanadamu hauwezi kufanya kazi kabisa ikiwa kila kiungo kitakuwa jicho na/au sikio tu.
Kitu kingine cha kukumbuka kuhusu utumishi ni kwamba mafanikio yake hayawezi kupimwa kwa viwango vya dunia. Tutakapofika mbinguni bila shaka tutashangaa sana kuona kwamba baadhi ya watumishi waliosifika sana (na kujisifia wenyewe pia!) hapa duniani, kwa kweli walifanikisha malengo machache ambayo Bwana aliwawekea. Paulo anatukumbusha kwamba kuna “aina mbalimbali za karama (vipaji) … kuna huduma za aina mbalimbali … kuna tofauti za kutenda kazi, lakini Bwana ni yuleyule atendaye kazi zote kwa wote” - 1Wakor. 12:5-7. Hii ina maana, pamoja na mambo mengine, kwamba hatuchagui vipaji vyetu vya kiroho, wala hatuchagui aina ya utumishi ambao Mungu ametupangia kutokana na vipaji hivyo, na pia wala hatuna uwezo juu ya matokeo ya utumishi wetu. Sisi sote tunatumika katika shamba la mizabibu la Bwana, na Yeye ndiye anayeongeza matunda ya mazao ya mizabibu hiyo. Juhudi zetu zinaweza kuoneka finyu sana mbele za macho ya dunia, lakini kama zinamfurahisha Mungu, basi zina umuhimu mkubwa zaidi Kwake na kwa Mpango wake kuliko huduma inayojitangaza kwa sauti kubwa na kelele nyingi, lakini ambapo Mungu mwenyewe anahusishwa kwa kiasi kidogo sana. Tunavyozidi kupevuka kiroho, na mafanikio ya utumishi wetu yanakuwa makubwa zaidi. Hivyo basi, ufunguo wa mafanikio ya utumishi wa kila mmoja wetu ni kupevuka kiroho. Sasa je, tunawezaje kupevuka kiroho?
Mwanzo kabisa mwa waraka wake, Petro anawapa wasomaji wake maelezo ya hatua tatu za kuchaguliwa kwetu ili kuingia katika familia ya Mungu (tizama somo #3 kwa mjadala kamili wa awamu za Mpango wa Mungu: awamu ya kwanza: wokovu/imani kwa Kristo; awamu ya pili: historia/mchakato wa kupevuka kiroho; awamu ya tatu: milele/ufufuo na thawabu):
-
Baba alipanga wokovu wetu (alijua yote kabla hatujazaliwa)
-
Roho Mtakatifu alitekeleza mchakato wote wa wokovu wetu (utakaso)
-
Mwana akalipia wokovu huo (alitugomboa) na ndiye mlengwa wa imani yetu kwa wokovu huo (imani kwa Kristo)
Hatua hizi tatu za “mgawanyiko wa kazi” zinaenda sambamba na kazi ya Utatu Mtakatifu kwa niaba yetu katika awamu ya pili ya Mpango wa Mungu (muumini katika historia). Kila Nafsi katika Utatu anatusaidia kufanikisha ile kazi yetu mahususi ambayo Mungu ametupangia: Baba, kupitia Mpango wake anatupatia mahitaji yetu ya kimwili na kiroho hapa katika himaya ya Shetani; Bwana Yesu Kristo ni kiongozi wetu na ndiye tunayemtazama hapa duniani, na kazi Yake msalabani inaendelea kusafisha dhambi zetu kila tunapotubu; Roho Mtakatifu anatuwezesha kujifunza Neno la kweli la Mungu na namna ya kulitumia katika maisha yetu (ambacho ndicho kiini cha kupevuka kiroho). Kwa kuwa sehemu kubwa ya 1Petro na 2Petro inajihusisha na kupevuka kiroho (na tukichukulia kwamba misingi muhimu ya kanuni hii inaeleweka), huu ni wakati mwafaka wa kulizungumzia hili. Katika masomo yanayofuata, tutazichambua hizi “neema na fadhila [kutoka kwa Mungu] zinazotuwezesha” kukua kiroho, kwa undani, lakini hapa tuone muhtasari wake:
Baba: Utaratibu wa Mgao wa Neema au/na Mahitaji Yetu
a. Mahitaji ya kimwili: kila kitu tunachokihitaji ili tuweze kuishi kila siku tunapokuwa duniani (kwa mfano chakula, malazi, mavazi na kazi ya kufanya ili kupata hayo mahitaji; ulinzi dhidi ya hatari kwa maisha yetu).
b. Mahitaji ya kiroho: kila kitu tunachokihitaji ili kutimiza malengo yetu ya kiroho, na kufanikisha kukua kiroho na utumishi ambao Mungu ametupangia (kwa mfano Biblia, mafundisho ya Injili, kanisa, waalimu, vipaji, nafasi/fursa za kujifunza, kutumia neno, kutumikia Kanisa).
Mwana: Uongozi
a. kazi Yake: (kwa kuwa mbadala wetu msalabani, Yesu Kristo ametuokoa kutoka ghadhabu ya Mungu na kufanya wokovu wetu uwezekane; msamaha wa dhambi baada ya kuokolewa umewekewa msingi wake na msalaba na pia ni msingi wa kukua kiroho)
b. nafsi Yake: (Bwana Yesu Kristo ndiye mlengwa wa upendo wetu; maisha yake ni mfano wetu wa kuigwa; Yeye ndiye “Neno” tunayemtukuza na kumpenda; kwa kifupi, kujifunza juu Yake, kujifunza kuishi kama Yeye, kuishi kwa ajili Yake ndiyo kukua kiroho).
Roho Mtakatifu: Mafunzo
a. huduma Yake ya Neno: (ni kupitia huduma ya Roho Mtakatifu pekee ndipo tunapojifunza na kuelewa kweli ya Mungu).
b. huduma Yake katika maisha yetu: (Roho Mtakatifu anatusaidia kuitumia kweli tunayojifunza na kuielewa, katika mazingira ya maisha yetu: ambayo ni sehemu muhimu ya maisha yetu ya kila siku, na ya utumishi wetu)
=0=
Imetafsiriwa kutoka: An Introduction to Spiritual Growth: Peter’s Epistles # 10
=0=
Basi, na tuonane katika somo #11 katika mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!