Huduma ya Roho Mtakatifu: Nyaraka za Petro #7

 

Na Dr. Robert Dean Luginbill

Wa https://ichthys.com

 

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

 

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahsusi na Dr. R. D. Luginbill

Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by

Dr. R. D. Luginbill

 

Ebu tutoke nje ya mada kidogo: Katika kuhitimisha utangulizi wa kanuni za mateso, tuliona kwamba moja kati ya njia kuu ambazo Mungu anazitumia kuwasaidia Wakristo wa leo kustahamili na kuvumilia ni kwa usaidizi usioonekana (kwa macho ya kimwili) wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anakaa ndani ya kila muumini wa Yesu Kristo – Yoh. 14:16-17, na, ni kwa kuwezeshwa Naye ndipo sisi Wakristo tunapokea nguvu/uwezo wa kufanya kila kitu tunachokifanya kwa matakwa au mapenzi ya Mungu, iwe kupevuka kiroho, kuhudumia Kanisa au kuvumilia magumu. Kwa sababu ya mkanganyiko mkubwa katika mafundisho ya Wakristo wa sasa kuhusiana na huduma ya Roho Mtakatifu, itatusaidia sana hapa tukizungumzia kwa undani kazi Anayoifanya kwa niaba yetu. Alipowaandikia Wakorinto ambao walikuwa na tabia ya kupotosha maandiko, Mtume Paulo alizungumzia suala hili katika 2Wakorinto sura ya 3.

 

Kuakisi Utukufu wa Mungu:

 

3.1 Je! Tunaanza tena kujisifu wenyewe [kwenu]? Au tunahitaji, kama wengine, barua zenye sifa kuja kwenu, au kutoka kwenu?

3.2 Ninyi ndinyi barua yetu [ya sifa zetu], iliyoandikwa mioyoni mwenu, inajulikana na kusomwa na watu wote;

3.3 mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo [yenye uzima].

2Wakor. 3:1-3 (SUV)

 

Hapa, Mtume Paulo alianza kwa kukosoa tabia ya Kanisa la Wakorinto wale ya kuiga desturi ya kutumia “barua za utambulisho na pendekezo”, desturi iliyokuwa ya kawaida sana katika utawala wa Roma, na kuileta desturi hiyo katika matumizi ya shughuli za Kanisa. Kama ukitaka kufanya kazi serikalini wakati huo wa Ufalme wa Roma (na nafasi hizo ndizo zilikuwa “nono”), “barua” nzuri za utambulisho zilikuwa ni lazima uwe nazo. Sasa, waumini wa Kanisa la Korinto walikuwa wanadanganywa na “wajanja” fulani walioenda Korinto na barua za namna hiyo (halisia au la) kutoka kwa Makanisa mengine na viongozi wao. Wakorinto wale walianza kuwaheshimu matapeli wale zaidi ya walivyowaheshimu Mitume halisi wa Bwana, kwa sababu tu walikuwa na barua nzuri za utambulisho kutoka kwa wakubwa! Bila shaka hawa jamaa walikuwa wahubiri wazuri sana, wakijenga ‘hoja’ zao kwa ustadi, wakiwafurahisha Wakorinto wale kwa hadithi tamu na ucheshi mwingi! Hili, la watoa hotuba na wahubiri wazuri, halikuwa jambo la kigeni sana kwa wakati ule wa Paulo na Petro. Wahutubi kama Lucian waliishi vizuri sana, wakifundisha falsafa na balagha (elimu ya usemaji: rhetoric); na kwa kweli kuwasikiliza hao jamaa ilikuwa inagharimu fedha nyingi. Sasa, Paulo alichoshwa na tabia ya wana-Kanisa wale wa Korinto ya kuiga desturi hii, na kwa usahihi kabisa, kwani Wakorinto wale waliyapa umuhimu mapendekezo ya watu (barua za utambuisho) zaidi ya mapendekezo ya Mungu (Mitume)!

 

Sababu kuu ya Wakristo kubakizwa hapa duniani baada ya wokovu ni kumtukuza Mungu. Sasa, tunafanikisha vipi jukumu hili kuu? Wakorinto wale walifikiri kwamba “watu mashuhuri, watu maarufu” wakisema kwamba wewe Mkristo, unamtukuza Mungu, basi ni lazima iwe kweli! Kwa mtazamo wao potofu, katika kumtukuza Mungu tusiogope kutumia mbinu zozote za “kibinadamu” tunazoweza kupata. Kwa hivyo, tunaweza kutumia “barua za utambulisho” zilizoandikwa na “wakubwa”, tujitangaze wenyewe, na tutumie mbinu ambazo ulimwengu unazitumia, bila kujali utakaso/usafi wake katika kueneza Neno la Mungu. Paulo, kwa upande mwingine, anawaambia bila ya kumumunya maneno, kwamba wanakosea. Anasema kwamba yeye, Paulo hahitaji alama za kibinadamu za mafanikio kama hizo “barua zao za utambulisho”. Yeye, Paulo, anazo alama za Ki-Mungu za mafanikio, zilizo dhahiri kwa Wakorinto wenyewe, kwani wao Wakorinto, ndio barua zake, uhakiki wa huduma zake kwa Kanisa. “Barua” za Paulo haziandikwi kwa wino na karatasi zinazochakaa, bali zimeandikwa na Roho Mtakatifu ndani ya mioyo ya Wakorinto wale. Unaiona hoja ya Mtume Paulo? Nguvu halisi inayotuwezesha tuishi maisha ya Kikristo inatoka kwa Mungu (kupitia kwa Roho Mtakatifu) siyo kutoka katika juhudi za wanadamu, na alama halisi ya mafanikio ya Mkristo inapatikana katika matokeo halisi ya kiroho, siyo sifa za wanadamu.

 

Paulo angeweza kuwashawishi Wakorinto wale ili wamwandikie “barua nzuri za utambulisho na pendekezo”. Paulo angeweza kuitangaza huduma yake mwenyewe kwa shamrashamra, kujipa sifa na vyeo, kutafuta ‘promota’, n.k.Lakini Paulo alijua ya kwamba kujitangaza Ki-Mungu ni kupitia katika maisha ya Wakorinto wenyewe. Maisha yao pekee ndiyo “barua za utambulisho” halisi, maisha hayo yakidhihirisha matokeo ya huduma ya Mitume. Watu wanaotizama kundi hili la wafuasi wa Bwana Yesu, wanaona kiwango chao cha juu cha kupevuka kiroho na utumishi wao, na kusema “ama kweli, hii tunayoiona ndiyo kazi ya Mungu”. Tunamtukaza Mungu wetu kwa namna gani? Tunamwacha apate utukufu kupitia sisi, maisha yetu, mazao yetu. Kama tunaendelea kumfuata, tunaendelea kupevuka kiroho, tunaendelea kuyakabili na kuvumilia magumu na mitihani Anayotuletea, na kukabili changamoto za kuhudumia Kanisa Lake Krsisto, basi Nguvu Zake, Upendo Wake, Utukufu Wake utaonekana katika maisha yetu. Maneno ya Paulo hapa hayana maana ya kwamba tuutangaze Ukristo wetu kwa kelele nyingi. Paulo hawaambii Wakristo wale wapige chapa kwenye T-shirt zao kwa maandishi yanayosema “mimi naenda mbinguni”, la hasha! Utukufu wa Mungu hauonekani/haudhihiriki kwa kusema “mimi ni Mkristo”. Tunaweza tu kuudhihirisha utukufu wa Mungu kwa kuishi kama Wakristo ili wengine wanaotuona waseme “hii ni nguvu ya Mungu tunayoiona hapa”.

Faida ya Roho Mtakatifu:

 

(4) Hii ndiyo inaonyesha tunamwamini Mungu kiasi gani kupitia kwa Bwana Yesu Kristo.

(5) Siyo kwamba tuna uwezo mkubwa sana kwa kupitia nguvu zetu wenyewe, kwamba tumeyafanikisha haya yote kwa uwezo wetu, la hasha; bali uwezo wetu unatoka kwa Mungu;

(6) ambaye ametufanya wachungaji mahiri wa Agano Jipya - siyo la Sheria, bali lile la Roho. Hii ni kwa sababu Sheria inatufanya tuwe wafu, bali Roho Anatuhuisha (anatufanya tuwe hai).

2Wakor. 3:4-6 (Revised translation)

 

Katika msitari wa 4 mpaka wa 6, Paulo anaongeza hoja na kusema kwamba kujiamini kwake hakutokani na nguvu zake mwenyewe, bali kunatoka kwa Mungu. Paulo anatuambia kwamba yeye hawezi kujitosheleza mwenyewe, bali Mungu awatosheleza wote, na ndiye anayeiwezesha huduma/utumishi wake katika Kanisa. Hii ni kweli kwa kila upande wa maisha ya kila Mkristo. Kama vile Mungu alivyomwezesha Paulo kumtumikia, vivyo hivyo anatuwezesha sisi kufanya yote anayotuamuru kufanya katika maisha yetu. Nguvu iliyo mbele yetu sasa hivi ni ile ya Roho Mtakatifu, na iko tayari wakati wowote tunapoihitaji. Katika utumishi au huduma inayoongozwa na Roho Mtakatifu, sisi Wakristo tuna karama ya pekee ambayo Waumini wa Agano la Kale hawakuwa nayo. Paulo anatilia mkazo jambo hili kwa kusema katika aya ya 6 kwamba sisi ni wahudumu/wachungaji wa Agano Jipya ambao “tabia yao kuu siyo andiko, yaani Sheria, bali ni Roho” kwani Roho anatia uzima/uhai. Katika kusema hili Paulo anamaanisha kwamba chini ya sheria ya Musa (kama ilivyoandikwa katika Pentateuch – vitabu 5 vya kwanza vya Biblia), Neno la Mungu lilitizama mbele (siku za usoni kwa wakati ule) – kwa Kristo ambaye alikuwa bado hajakufa kwa ajili yetu, likitilia mkazo hali yetu ya dhambi nauhitaji wetu wa Mwokozi; bali katika Agano Jipya (ambapo Bwana Yesu alikuwako tayari na alishafanya kazi ya wokovu wetu), Neno la Mungu linatilia mkazo wokovu wetu katika Yeye (Kristo), *unaofanyiwa kazi na Roho Mtakatifu, na maisha yetu mapya katika Kristo yakitiwa nguvu na Huyo Huyo Roho Mtakatifu – Yoh. 7:39. Katika kujazwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu, sisi Wakristo tuna faida kuu kabisa. Paulo anatueleza hapa kwamba bila ya Roho Mtakatifu, asingekuwa na uwezo wa kutumikia kama ambavyo alikuwa anatumikia, kwani akiwa na Roho Mtakatifu, yeye anawezeshwa kufanikisha hayo yote.

 

Utukufu Usio na Kifani wa Usaidizi wa Roho Mtakatifu:

 

3.7 Basi, ikiwa huduma [ya Sheria ya Musa] ya mauti, iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika [ukipungua];

 

*wrought by – mfano wa chuma kinachoundwa upya kwa moto

3.8 je! Huduma ya Roho [Mtakatifu] haitazidi kuwa katika utukufu?

3.9 Kwa maana ikiwa huduma [ya Sheria] ya adhabu ina utukufu, siuze [kwa hakika] huduma ya haki ina utukufu unaozidi.

3.10 Maana hata ile iliyotukuzwa [mwanzo] haikuwa na utukufu hivi, kwa sababu [hii ya sasa ina] utukufu uzidio sana.

3.11 Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika (inayopungua) ilikuwa na utukufu, [basi] zaidi sana ile ikaayo [ya Roho Mtakatifu kwa Waumini] ina utukufu.

 

2Wakor. 3:7-11 (SUV)

 

Ukilinganishwa na utukufu wa huduma mpya (katika Agano Jipya) ya Roho Mtakatifu kwa waumini wote, ule utukufu uliodhihirishwa chini ya Agano la Kale ni pungufu sana – aya ya 10. Hii ina maana gani? “Utukufu” kwa lugha ya Kiingereza ni “glory”, ni tafsiri ya neno la Kiyunani doxa ambalo maana yake ni “mng’ao, kumeremeta”, lakini pia ni “sifa, fahari”. Kwa hiyo kumtukuza Mungu ni kudhihirisha ung’aavu, sifa, ufahari mkuu wa Nafsi Yake na Kazi Yake. Katika mfano wa Agano la Kale alioutumia Paulo, Mungu aliuonyesha ulimwengu sehemu ndogo tu ya ung’aavu ule alipoufanya uso wa Musa kung’aa. Musa alikaa siku 40 na Mungu akipokea Sheria, na kiasi kidogo cha utukufu Wake kikamgusa Musa katika uso wake. Utukufu ue ulianza kufifia, na Musa akafunika uso wake ili wana wa Israeli wasione mwisho wake. Utukufu wa Mungu unaoletwa na Roho Mtakatifu haufifii na unadumu. Ni mwanga mng’aavu unaowaka ndani ya kila Mkristo, na unadhihirika mbele ya watu kutokana na maisha ya Mkristo huyu. Paulo anasema utukufu huu unazidi miujiza ya Agano la Kale kwa ukuu wake. Imani, tumaini na upendo unaomiminika kutoka kwetu sisi Wakristo kutokana na Roho Mtakatifu ni nyota ing’aayo zaidi ya miujiza yoyote ile.

 

Vioo vya Mungu:

 

2Wakor. 3:12-18: (12) Kwa kuwa tuna tarajio la uhakika wa mafanikio [kwa msingi wa usaidizi wa huduma ya Roho Mtakatifu], tunaisema ile kweli kwa uwazi kabisa;

(13) na siyo kama pale Musa alipolazimika kufunika utaji usoni mwake ili wana wa Israeli wasione utukufu ule wa mng’ao wa sura yake ukififia.

(14) Sasa, mioyo yao ilikuwa migumu, na hata sasa wanaposoma Agano lile la Kale bado kuna utaji unaofanana na ule wa Musa, unaoficha utukufu halisi; na utaji huu hauondolewi mioyoni mwao kwani ni katika Kristo tu ndipo mwanga wa ile kweli unaangaza.

(15) Hivyo, mpaka sasa, wakati wowote Sheria inaposomwa [nao], utaji huu unazingira mioyo yao;

(16) bali wakati wowote mmoja wao anapomkimbilia Kristo, utaji huondolewa.

(17) Sasa, Bwana ndiye Roho na palipo na Roho [Mtakatifu], hapo pana uhuru.

(18) Na kila mmoja wetu, iwapo tutaakisi utukufu wa Bwana bila “utaji kufunika sura zetu” [yaani katika ushuhuda wa Kikristo usio na doa], tunabadilishwa na kuwa mfano ule ule [wa Mungu] (yaani tunazidi kufanana na Kristo tunapoitumia nia yetu kumwitikia Yeye), hivyo tunaakisi utukufu Wake zaidi na zaidi (kutoka utukufu hata utukufu) – kitu ambacho ndilo tunda la Roho wa Bwana pale anapokuwa Wakala wa kuzaliwa kwetu upya. (Revised translation)

 

  1. matokeo ya huduma ya Roho Mtakatifu kwake, Paulo ana “kujiamini” (neno la Kiyunani elpis, maana yake “tumaini chanya”) na hivyo anatiwa moyo kuendelea mbele na utumishi wake mwenyewe – aya ya 12. Wakati wa Agano la Kale, Musa alifunika uso wake kwa utaji (aya ya 13), lakini sisi waumini wa sasa tuna agizo tofauti (aya ya 18: kwa Kiyunani ni apodosis au hitimisho la aya ya 13). Tunaamrishwa kuakisi utukufu wa Bwana (“kuakisi utukufu wa Bwana”; note: tafsiri nyingi za maandiko za Kiingereza zimetafsiri kitenzi cha Kiyunani cha wakati unaoendelea katoptrizomenoi kuwa ni “kutazama”, lakini maana yake halisi ni “kuakisi”, ikitamkwa katika “middle voice” au mesaίa fonί katika Kiyunani, kama ilivyotafsiriwa hapa). Sasa, ule mwanga mng’aavu kutoka katika uso wa Musa ulikuwa mwanga halisi (mng’ao - maana ya kwanza ya neno la Kiyunani doxa), lakini utukufu tunaoelekezwa tuuakisi ni ile Nafsi Yake Mungu mwenyewe (yaani ile maana ya pili ya neno doxa hapo juu, yaani sifa na fahari ya Mungu Mwenyewe). Tunawezaje kuakisi nafsi heshimika ya Mungu, upendo Wake usiomithilika na ukweli Wake uliotukuka? Paulo anasema kwamba tunaweza kufanikisha jambo hili kwa “kubadilishwa tufanane na taswira hiyo hiyo, kutoka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Roho wa Bwana”. “Taswira hiyo hiyo” ni mfano wa Bwana Yesu Kristo. Katika hulka yetu hatufanani na Kristo kabisa, lakini kama “jina” letu “Wakristo” (maana yake [wa]-Kristo wadogo-wadogo) linavyoashiria, tunapaswa kufanya bidii siku hadi siku katika kukua kiroho ili tuwe kama Bwana wetu. tukifanya jitihada hii, matokeo yake ni “kuakisi utukufu kunakoongezeka siku hata siku” (ambayo ndiyo maana ya msemo “toka utukufu hata utukufu”), na wale wanaotuona tukikua katika neema watakubali (kama ilivyo mwisho wa aya ya 18) kwamba sababu ya haya mabadiliko ya kimwujiza yanayoonekana katika mwenendo wetu ni kutoka “katika Roho wa Bwana”. Ili tuakisi utukufu wa Mungu kikwelikweli, tunapaswa kufanya hivyo kwa kutumia njia Yake. Chanzo cha nguvu ya kweli ya mabadiliko hayo inapaswa kuwa Roho Mtakatifu, siyo juhudi zetu wenyewe za kibinadamu. Tunapolazimisha kutukuka kwa juhudi zetu wenyewe, watu wanaotutazama wataziona sura zetu wenyewe wanapoangalia “vioo” vya maisha yetu, badala ya kuiona taswira ya Bwana na Mungu wetu, Yesu Kristo.

 

Tamati:

 

Tunatimizaje matendo na mwenendo wetu katika namna ambayo Mungu ametupangia? Kwa maneno mengine, tunatembeaje katika njia Yake? Kwanza kabisa, tunapaswa kuhakikisha hatutendi matendo yetu kwa namna ya wanadamu; watu wanaona matendo au mwenendo wa udanganyifu kwa urahisi sana, kama vile kuigiza au ‘kujifanya’ kwamba una furaha [katika Bwana Yesu]. Kutumia ‘misemo’ na nahau zinazo-sound Kikristo katika kila kauli tunazotoa, au kuonyesha watu kwamba sisi ni ‘Wakristo sana’ bila ya kuwa na nuru ya ile kweli ndani yetu ni kupoteza muda tu. Katika mapana yake, maisha ya Kikristo ni rahisi tu. Mwamini Kristo na unaokolewa. Lakini kinachofuata hapo ni shughuli ya maisha yako yote: kuutafuta na kuufuatilia utakatifu. Kupevuka kiroho kunataka kujifunza Neno la Mungu, kuliamini na kuitumia kweli ya Mungu unayojifunza katika maisha yako. Halafu tunavyopevuka kiroho, Mungu anatupa fursa za kukabili magumu, majaribu, mitihani na pia kuwatumikia Wakristo wengine kulingana na karama au vipaji tulivyopewa wakati tunaokolewa. Kama tutatembea katika njia hii, kwa hakika tutaakisi neema na upendo wa Mungu kwa kiasi kinachoongezeka, na hapo tutatimiza yale maagizo tuliyopewa katika 2Wakorinto sura ya 2.

 

(2) Uchungaji au huduma ya Roho Mtakatifu inafanya kazi kwa namna gani? Kwanza kabisa, tusiyasahau maneno ya Bwana kwa Zerubabeli katika Zakaria 4:6: “Si kwa nguvu, wala kwa uwezo, bali ni kwa Roho Yangu”. Sisi ni vyombo tu, vifaa tu, watumishi tu. Mungu amekwishatupatia maelekezo kamili ya namna ya kwenda mbele. Tunatakiwa kutii tu na kutekeleza, kama watumishi wema wanavyotii na kufuata maelekezo, na pamoja na utiifu wetu, Roho Mtakatifu anaongezea uwezo, usitawi na matokeo/matunda mema. Nabii Eliya alipokimbilia Mlima Horebu kwa hofu, Mungu aliona njia ya kumfundisha somo hili hili kwa kumletea, upesi upesi, kando ya pango alimojificha, upepo mkali, tetemeko na mwisho moto. Lakini Mungu hakuwemo katika matukio yote hayo matatu, licha ya nguvu zake za kutisha. Hatimaye Mungu akatuma “sauti tulivu ya kunong’oneza”, na hii sauti ndiyo iliyokuwa na uwezo na uwepo wa Mungu – 1Wafalme 19:1-18. Sauti ya chini, tulivu ya Roho Mtakatifu ambayo huelekezwa kwa mioyo yetu, ikitutia moyo, ikituonyesha njia, ikitufariji, ina uwezo mkuu zaidi ya miujiza yoyote inayoonekana mbele za macho ya watu. Kama kwa ukweli tutatembea na Mungu, tukitubu dhambi zetu na kwenda mbele kiroho, basi Roho Mtakatifu wa Mungu atatusaidia. Uchungaji au huduma ya Roho Mtakatifu haionekani kwa macho yetu, lakini matunda yake yako wazi. Kwa kifupi, kama tunasukuma gurudumu la kukua kiroho mbele, tunapata msaada wa Roho Mtakatifu. Ukweli kwamba hatuwezi kupima upeo wa huduma Yake, au kuiona kwa macho, au kupata hisia Yake kama tunavyohisi joto na baridi, haina maana kwamba huduma hii siyo halisi au muhimu. Hili ni jambo muhimu sana kwa sababu Wakristo wengi sana leo hii wanajihusisha na ibada zenye utata katika uhalali wake kimaandiko, na pia ibada potofu, kwa sababu ya nia na shauku yao ya kupata “hisia halisi” ya Mungu. Tunahitaji kuonyesha nia na kuanza tu, na Roho Mtakatifu atatonyesha njia.

 

  1. Hayo yote hapo juu yanahusiana vipi na mada yetu ya mateso katika maisha ya Mkristo? Kama tukielekeza mikono yetu kwa Bwana kwa imani, Roho Wake Mtakatifu (ambaye ametupatia kama Msaidizi na Mfariji) atatusaidia kuhimili magumu yoyote ambayo tutalazimika kuyakabili. Kama tunaamini kwamba Bwana ndiye mchungaji wetu, kwamba anatulinda na kutujali sana, kwa nini tunalalamika, kwa nini tunazimia katika imani yetu? Tunalalamika kwa sababu tuna maumivu na kwa sababu sisi ni wanadamu. Maandiko ya Zaburi ya Daudi yanaonyesha kilio chake cha uchungu kwa Mungu, lakini Daudi hakuzimia katika imani yake. Katika maumivu yake makali alimtegemea Mungu tu. Alitoa machozi yake kwa Mungu akiamini kwamba Mungu atamwokoa kwa neema na huruma Yake kuu. Faida yetu kubwa kama Wakristo ni kuwa na imani kama hiyo, kujiamini katika imani yetu namna hiyo, kuamini kwamba yuko Mungu mwenye upendo mkuu atakayetusaidia. Kama tutachukua hii hatua ya kwanza wakati wa magumu, Roho wake Mtakatifu atatufariji na kutusaidia pia.

 

=0=

 

Translated from: Peter’s Epistles #7: The Ministry of the Holy Spirit

 

=0=

 

Basi na tuonane katika somo #8 kwa neema ya Mungu, Amen!