Sababu za Kuteseka kwa Wakristo: Nyaraka za Petro #5

 

Na Dr. Robert Dean Luginbill

Wa https://ichthys.com

 

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

 

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahsusi na Dr. R. D. Luginbill

Permission for This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by

Dr. R. D. Luginbill

 

1Petro 1:1-2: (1) Petro, Mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule ambao japo wametengwa na kutawanywa katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia;

(2) wamechaguliwa na Mungu Baba kwani Aliwajua toka mwanzo kwa utakaso wa Roho Mtakatifu, hata mkapata kutii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani ziongezwe kwenu! (Revised Translation)

 

Mapitio ya Ufafanuzi/Fasili: Kwa wateule ambao japo wametengwa na kutawanywa … lakini wamechaguliwa: Mpaka hapa tumeona kwamba katika kutumia hivi vielelezi viwili ambavyo kwa mtazamo wa juu juu vinapingana, Petro anauleta mtazamo wetu uje kwenye ukweli kwamba ingawa hali yetu halisi ya milele itakuwa yenye furaha isiyokwisha na baraka tele, lakini katika maisha ya dunia hii tutatengwa: tuko ndani ya ulimwengu, lakini sisi si wa ulimwengu. Tumeona pia kwamba haya yote ni sehemu ya Mpango wa Mungu kwa ajili yetu sisi. Katika awamu ya kwanza ya Mpango wa Mungu, tunamwamini Bwana Yesu na tunaokolewa; katika awamu ya tatu ya Mpango wa Mungu, tunapokea mwili mpya ulio mtimilifu pale tunapofufuliwa, na tutaishi milele pamoja na Mungu kwa furaha na amani iliyo timilifu. Lakini katika awamu ya pili (maisha ya muumini hapa duniani), tunaendelea kuwa hapa katika ulimwengu wa Ibilisi, tukipata maumivu, mateso na magumu ya kila namna.

 

Lakini Wakristo wanapoteseka, hayo yanatokea tu kwa ufahamu wa Mungu wa tokea mwanzo (na kwa kweli katika aya ya kwanza ya nukuu ya hapo juu Wakristo wale wanaelezewa kama waliotengwa … kwani aliwajua tokea mwanzo). Mungu anafahamu kila tatizo tutakalokabiliwa nalo. Kwa hakika, Alijua kuhusu mateso tunayoyakabili sasa na tutakayoyakabili katika siku zetu za usoni wakati anaunda Mpango Wake milele iliyopita. Petro anawaambia hawa waumini wa karne ya kwanza kwamba Mungu anayajua mateso yetu yote. Kuna sababu kwa nini tunateseka kama Wakristo, na Mungu anaruhusu mateso hayo yatupate kwa manufaa yetu. Hivyo tusisahau kwamba “kwa sisi tumpendao Mungu, aliotuchagua na kutuita kutokana na Mpango Wake, Yeye ameyapangia mambo yote kuwa na matokeo mema” (War. 8:28). Tunaposhindwa kuzingatia kanuni hizi zinazoelezea sababu za mateso yetu kutokana na mtazamo wa Mungu, sisi, kama wale Wakristo aliokuwa akiwaandikia Petro, tunajiweka katika hatari ya kuchanganyikiwa na mateso na kupoteza mwelekeo. Tunaweza kusahau kwamba Mungu anatupenda, anatulinda, na anahusika katika kila kitengo cha maisha yetu. Ni muhimu pia kutofautisha kati ya mateso tunayopata kwa malengo ya kuturekebisha (Mungu anapotuadabisha), na mateso ya kutupevusha (mateso ya Wakristo au “kushiriki katika mateso ya Kristo”). Kwa kuwa kila upande wa maisha ya Mkristo ni muhimu katika Mpango wa Mungu, mateso yetu yote yanaingia katika makundi haya mawili (kwani, japo ni kweli kama tulivyoona katika somo la nne kwamba mateso ya kawaida ya wanadamu ni matokeo ya kuanguka kwa Adamu, maisha ya Mkristo yanasimamiwa na kuongozwa na Mungu. Kama tunapata mateso tusiyostahili, basi tunafaidika kwa namna nyingi, hata kama kwa wakati ule wa mateso hatulioni hilo kwa wazi. Lakini kama, kwa upande mwingine, tunapata adabisho kutoka kwa Mungu, basi ufumbuzi ni kuungama.

 

Kuungama Dhambi: Tumeona kwamba kwa kutoa sala kwa Mungu ya kukiri dhambi zetu, dhambi hizi husamehewa na Mungu nasi tunatakaswa – 1Yoh. 1:9. Dhambi hutendwa katika mafungu matatu:

 

(1) Dhambi za matendo (dhambi za wazi kama wizi; kwa mf. Kutoka 20:15)

 

(2) Dhambi za maneno/ulimi (kama kusema uwongo; kwa mf. Wakol. 3:8)

 

(3) Dhambi za mawazo/moyoni (kama hasira; kwa mf. Wagal. 5:20)

 

Kama Mtume Paulo anavyotukumbusha, “wote hutenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” - War. 3:23, hivyo hufika wakati waumini wote tunalazimika kutumia ushauri ulioko katika 1Yoh. 1:9 na kutubu dhambi zetu kwa Mungu – 1Yoh. 1:10. Ni muhimu sana kukumbuka kwamba kitu kilicho muhimu sana katika kutubu dhambi siyo hisia zetu katika kutubu dhambi hizo. Kwa hakika hatuwezi kusikia raha wakati tunashindwa katika vita yetu dhidi ya uovu. Tunataka kushinda kama Wakristo na kumfurahisha Bwana wetu. Wakati huo huo, tunapaswa kutambua kwamba tunasamehewa dhambi zetu kutokana na hulka ya Mungu, kwani Kristo alihukumiwa kwa niaba yetu kwa sababu ya dhambi hizo hizo tunazotubu. Kristo ndiye kiini cha msamaha wote wa dhambi, kwa kila mmoja wetu, na haistahili sisi kuwa na hisia zilizokithiri za hatia; hivyo tujiepushe na matendo ya malipizi yetu sisi wenyewe, kwani hayamfurahishi Mungu hata kidogo. Tunahitaji kuwa na unyenyekevu na kutambua kuwa sisi si watimilifu tukingali hapa duniani, japokuwa ni wajibu wetu kujitahidi kuzuia kushindwa na pia tujifunze kutokana na makosa yetu (na tusiitumie hali ya kutokuwa watimilifu kama kisingizio cha kutenda dhambi!). Hivyo tunapaswa kuwa mahiri katika namna tunavyokiri na kutubu dhambi zetu, tukijizuia kuwa na hisia zilizokithiri za hatia nafsini mwetu na katika wajihi wetu. Tunapaswa kuwa na tabia ya kurejea haraka kwa Baba pale tunapopotea njia, tukichunguza matendo yetu wakati wote, kukiri haraka dhambi yote tunayoiona, iwe ya matendo yetu, ya maneno yetu au ya mawazo yetu.

 

Mateso kwa Ajili ya Baraka: Mara tunapokiri dhambi zetu, hata yale mateso yanayotokana na adabisho kutoka kwa Mungu yanabadilishwa na kuwa mateso kwa ajili ya baraka, na hayo ni nafuu/ahueni kwetu, kuliko kupata adhabu kutoka kwa mkono wa Mungu.

 

Kitu cha kwanza tunachokiona kuhusiana na mateso ambayo Mungu katika upendo Wake anayaruhusu yaje kwetu ili tupambane nayo (pale ambapo hakuna dhambi isiyofanyiwa toba katika maisha yetu), ni kwamba mateso ya Wakristo yanavumilika. 1Wakor. 10:13 inayaelezea mateso kuwa ni “mitihani” (kwa Kiyunani peirasmos maana yake “mtihani” au “tathmini”). Kama ambavyo tulikuwa na mitihani shuleni ambayo ilikuwa na lengo la kupima maendeleo yetu, kama tumesoma na kuelewa masomo tuliyopewa katika mtaala fulani, vivyo hivyo Mungu anatupatia mitihani katika awamu ya pili ya Mpango Wake. Anaruhusu magumu yaje katika maisha yetu ili kuona namna tunavyoyakabili. Je, tumekuwa na jitihada katika kujifunza ukweli wa Neno Lake? Je, tutamkumbuka Yeye na kumwamini katika ile saa ya shinikizo na msongo wa mawazo? Au tumekuwa wavivu katika kuitikia wito wa kujifunza Neno na kulitumia Neno katika maisha yetu, tumesahau kwamba Yeye anaweza kutuokoa katika magumu yoyote yatakayotukabili? Tunafundishwa katika 1Wakor. 10:13 kwamba “ … Yeye hataruhusu mjaribiwe kupita uwezo wenu wa kuhimili ...”

 

Wakati fulani huonekana kama kwamba baadhi ya Wakristo hupata magumu kuzidi wengine. Kumbuka tu kwamba wewe na mimi tunapata shida kubwa katika kutathmini maisha yetu wenyewe, hivyo kwa hakika hatuwezi kujua kama shida za mtu mwingine zinavumilika au la. Mungu anajua kiasi gani cha shinikizo anachoweza kuhimili kiumbe Wake, na kiasi gani kitamvunja nguvu. Mara nyingi tu Mungu atatupa zoezi litakalotuchosha kwelikweli, lakini kamwe hatutovunjika nguvu au moyo. Kama tukiasi dhidi ya Mungu (na kuanguka katika hali ya kurudia dhambi tena na tena, bila kuifanyia toba), hapo mateso yetu yatakuwa hayavumiliki; bali kama tunasonga mbele katika Mpango wa Mungu kwa maisha yetu, tukitubu dhambi tunazotenda, na kujitahidi katika mafunzo ya Neno la Mungu, basi tunayo ahadi ya Mungu kwamba hatutakabiliwa na chochote kitakachotuzidi nguvu.

 

Kingine tunachoambiwa katika 1Wakor. 10:13 ni kwamba Mungu “… atawapa njia ya kutokea ...” kutoka katika mateso au magumu. Neno la Kiyunani ekbasis, maana yake ni “njia ya kutokea”. Msemo unaofuata katika aya ile, “ili muweze kustahamili” inatufundisha kwamba ile “njia ya kutokea” yaweza kukupitisha katikati ya hayo magumu, utapewa uwezo wa kustahamili, lakini magumu hayataepukika na hutayaepa – vinginevyo utashindwa mtihani huo; pia msemo huu “njia ya kutokea” una maana ingine ya wewe “kuepa” magumu kabisa, amabapo mtihani wako utakuwa ni katika kuliona tu tatizo, na si kulipitia (kuli-experience). Hii ina maana ya kwamba tunapomwomba Mungu atupe ahueni katika mateso yetu, ahueni hiyo itakuja, lakini kuna uwezekana isije mara moja au papo hapo! Mateso, na mitihani ya imani yetu inayohusiana na mateso hayo, ni nguzo muhimu katika Mpango wa Mungu kwa maisha yetu katika awamu ya pili (maisha hapa duniani). Kwa kweli bila magumu hakuna kupevuka kiroho, na pia hakuna namna nyingine ya kudhihirisha maendeleo yetu ya kiroho.

 

Katika somo la sita tutajifunza umuhimu wa magumu katika maendeleo ya kiroho ya Mkristo.

=0=

 

Imetafsiriwa kutoka: Reasons for Suffering: Peter’s Epistles #5

 

=0=

 

Basi na tuonane katika somo #6 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!