Kupambana na Mkakati wa Shetani: Nyaraka za Mtume Petro #1
Utangulizi
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo
Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahsusi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili translation has been kindly granted by
Dr. R. D. Luginbill
Utangulizi. Kupambana na Mkakati wa Shetani: Waraka wa Kwanza na ule wa Pili wa Mtume Petro unapaswa kusomwa na/au kufundishwa pamoja, kwani nyaraka/barua zote mbili zinajihusisha na maudhui yaleyale: kupevuka/kukua kiimani/kiroho mbele ya mashambulizi ya Shetani na wafuasi wake – wa kimalaika na wa kibinanadamu. Katika hizi barua mbili, Petro anawakumbusha wasomaji wake juu ya ulazima au umuhimu wa kupevuka kiroho pamoja na mbinu au njia za kufanya hivyo; lakini pia alizungumzia mienendo hatari ya aina mbili ambayo ilikuwa inachelewesha au inapunguza kasi ya kukua kiroho kwa waumini wa wakati ule. Mienendo hii miwili hatari ambayo ni tabia binafsi zilizokuwa zinawaondoa katika msitari wa mpango imara wa Mungu waliokwishafundishwa na kupotoshwa kwa maandiko na mafundisho ya kanuni ambako matokeo yake yalikuwa ni yaleyale ya kuondoka katika msitari imara wa mpango wa Mungu. Mienendo hii miwili bado ni hatari kwa waumini na maendeleo yao ya kiroho hata, na haswa, katika wakati huu tunaoishi. Kuwatoa waumini katika lengo lao ni sehemu muhimu ya mkakati wa Shetani wa kuwapeleka waumini mbali na Mungu. Siyo rahisi kwa muumini aliyepevuka kiroho na ambaye imani yake ni imara na ya uhakika kuasi, kinyume na muumini ambaye imani yake inapungua au inaharibiwa kutokana na mateso ya maishani na/au mafundisho ya uwongo.
-
Katika waraka wake wa kwanza, Mtume Petro anapambanua tatizo kubwa na la kawaida kwa waumini, ambalo linaweza kumvuruga na kumwondoa katika lengo la kutimiza mpango wa Mungu Alioukusudia kwa ajili ya muumini huyo: mateso ya maishani.
-
Katika waraka wake wa pili, Mtume Petro anazungumzia tatizo lingine kubwa ambalo ni tishio kwa muumini na ambalo linaweza kumrubuni na kumpeleka mbali na kweli: mafundisho ya kanuni za uwongo.
Ujumbe wa Petro ni kwamba muumini mwaminifu na imara atastahamili dhidi ya hatari hizi zote mbili. Mtumishi mwaminifu hataruhusu mateso na vishawishi vya maisha kumfanya amtilie mashaka Mungu wake au kumtoa katika msitari wake wa mpango wa Mungu. Vilevile, muumini imara hawezi kukubali kudanganywa na mfumo wa mafundisho ya kanuni za uwongo hata kama unavutia namna gani.
Sasa, Mkristo anawezaje kufanikisha majukumu yake haya mawili magumu? Kwa kujifunza Neno la Mungu – yaani kwa kusikia, kuamini na kutumia misingi na kanuni za kweli za Biblia – Mkristo anakua au anapevuka kiroho, anakomaa katika imani yake, hivyo anaweza kustahamili mitihani na majaribu ya maisha bila kutetereka; na ataweza pia kupambanua kati ya mafundisho ya kweli na yale ya uwongo.
Historia: Mtume Petro aliandika nyaraka hizi mbili akiwa Roma alikokuwa akiishi miaka ya 62 – 63 A.D. mpaka alipouawa pale kati ya mwaka 66 – 67 A.D. Hatujui kwa uhakika ni lini Petro aliondoka Roma. Kuna taarifa nyingi zisizo za uhakika kuhusiana na hilo. Ila inafahamika kwamba Petro alikuwa Roma wakati wa utawala wa Nero ambaye alitawala tangu 54 hadi 68 A.D. Kitabu cha Tacitus kinachoitwa Annales 15.44 kinatoa taarifa chache zinazojulikana kuhusu mateso yaliyoamriwa na mfalme Nero dhidi ya Wakristo. Mfalme Nero alitajwa kwamba yeye ndiye aliyeamrisha mji wa Roma uunguzwe kwa moto mwaka 64; hivyo katika kujitetea akawasingizia Wakristo mashitaka hayo, na akaamrisha wateswe kikatili, kwa mfano kwa kuwasulibisha (kuteswa msalabani), kuwachoma moto hadharani, kuwavalisha ngozi mbichi za wanyama halafu kuwafungulia mbwa mwitu ili wawakamate, kuwaua na kuwala. Petro mwenyewe inaelekea aliuawa kwa sababu ya imani yake mwishoni mwa kipindi hiki cha mateso haya dhidi ya Wakristo, mwishoni mwa utawala wa Nero. Hakuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha kwamba mateso haya dhidi ya Wakristo yalivuka mipaka ya mji wa Roma, lakini mashambulizi haya bila shaka yaliwatia hofu waumini waliokuwa wakiishi katika majimbo ya utawala wa Roma; kwa uhakika mwandishi Tacitus alivyoielezea imani ya Kikristo kwamba ni “potofu, isiyistahili heshima, na ya aibu” inaonyesha kwamba watu wengi wa wakati ule waliwaogopa, hawakuwaelewa na waliwachukia Wakristo wenzetu wa miaka hiyo. Katika karne ile ya Kwanza kuwa Mkristo ilikuletea hatari katika maisha yako.
Mwandishi Pliny katika andiko lake namba 10.96–97 akiandika miaka 50 baada ya kipindi hiki kwa mfalme Trajan akiomba maelekezo ya namna ya “kupambana” na Wakristo, anatufichulia mazingira magumu ambamo Wakristo wenzetu hawa walilazimika kuishi. Mwandishi Pliny anamwuliza mfalme ikiwa kuwa na jina “Mkristo” ni sababu ya kutosha kushitakiwa: sasa, mfalme Trojan alimjibu Pliny kwamba asipoteze muda sana kuwasaka Wakristo, bali mtu yeyote akikamatwa akaletwa kwake, na ikathibitishwa wazi kwamba mtu huyo ni Mkristo, na kama hataukana Ukristo wake na kumtolea mfalme ‘sadaka’, basi mtu huyo auawe (maana katika ufalme wa Roma ya kale, mfalme alikuwa “mungu” na raia wote walilazimika kuchinja mnyama au ndege kama kuku, n.k., kama “sadaka/kafara” kwa ajili yake ili apate “baraka/neema”). Barua zote za Pliny zinaonyesha kwamba haki za Wakristo kisheria zilikuwa finyu kabisa, na walikuwa hatarini kufichuliwa na kushitakiwa wakati wowote na kwa sababu zozote, nyingi zikiwa za uonevu. Kwa mfano katika Matendo17:5: ambapo baadhi ya Wayahudi walikusanya vijana wahuni na kuwalipa ili wafanye fujo kwa sababu waliona wivu walipoona watu wa mataifa wakipokea Neno. Matendo 16:19 ambapo watu waliokuwa wakimtumia binti mwenye pepo pale Filipi aliyekuwa akitabiri na tajiri zake kupata pesa nyingi kwa namna hiyo; Paulo na Sila walisumbuliwa na binti huyo hata Paulo akamtoa pepo huyo hivyo kuwaudhi matajiri zake binti huyo hata wakashitakiwa na kufungwa jela. Pia katika Matendo 19:23-41 ambapo huko Efeso wafuasi wa “mungu wa kike” Artemis walifanya fujo kwani watu wengi walimgeukia Bwana na wao hawakuwa wanauza sanamu za kutosha za “mungu” huyo kama hapo mwanzo. Wakristo wa karne ya kwanza A.D. walikabiliwa na vishawishi na majaribu ya jamii iliyopoteza maadili kama hii tuliyo nayo sisi katika karne hii ya 21; juu ya hayo, walilazimika kuwa macho wakati wote kwa sababu walikuwa wanawindwa na vyombo vya serikali na raia wenzao ili wakamatwe. Katika mazingira yale, simanzi na majonzi zilikuwa hisia za wakati wote: ni imani chanya, yenye nguvu pekee iliwayowawezesha kustahamili na kuweza kuendelea kukua kiroho.
Mateso: Maneno machache yanapaswa kusemwa hapa kuhusu mashambulio ya Shetani dhidi ya imani ya Wakristo katika kipindi hiki. Mateso na shida za maisha ni changamoto kwa imani inayokua na kuimarika. Mkristo anashawishika “kuzimia” na kushakia uwezo wa Mungu wa kumkomboa na kumtoa katika shida zake. Lakini zaidi ya hili, mafundisho ya uwongo ni tishio lililojificha kwa Mkristo, likihujumu misingi ya imani, na kuozesha nguzo za imani hiyo. Katika masomo haya, tutachambua mafundisho ya uwongo ya karne ile ya kwanza, na pia tutaangalia mafundisho ya uwongo ya wakati huu wetu; lakini tunapaswa kukumbuka kwamba wenzetu wa karne ile walikosa baadhi ya vinufaishi ambavyo sisi tunavyo kwa wingi; kwa mfano, Biblia ilikuwa haijakamilika. Viongozi wa Kanisa walikuwa wapya kabisa, walikuwa hawajasomea utumishi, hakukuwa na vyuo/shule (seminaries), hakukuwa na vitabu vya kikristo, mitume waliweza kutembelea maeneo machache tu yaliyokuwa na Wakristo wengi. Lakini licha ya mapungufu haya yote, Wakristo wenzetu wale waliweza kustawisha imani yao. Katika barua hizi mbili, Mtume Petro alilenga kuwatahadharisha Wakristo wa wakati ule dhidi ya matishio hayo mawili (matokeo ya mateso na mafundisho ya uwongo), kuwakumbusha na kuwafundisha mbinu sahihi za kuilinda na kuiimarisha imani yao, kuwapa changamoto ili wafikie hatua za juu kabisa za upevu wa kiroho, na maisha yao yabarikiwe, na waweze kupata mavuno makuu baada ya ufufuo, katika milele ijayo.
Muhtasari Hitimisho:
Wakati wa uandishi wa Nyaraka: 62-67 A.D.
Walengwa wa Nyaraka: Wakristo wote wa Asia Ndogo
Mwandishi na Mahali pa Uandishi: Mtume Petro, kutoka Roma
Mada ya Barua ya Kwanza: Mkristo, usiruhusu mateso ya maisha yavuruge/yadumaze maendeleo yako ya kiroho!
Mada ya Barua ya Pili: Usiruhusu mafundisho ya uwongo yadumaze maendeleo yako ya kiroho!
Kupevuka Kiroho: Mungu anatupa mahitaji yetu yote ili tujifunze Neno Lake: Biblia, utashi au hiari (ya moyo), mahitaji ya maisha, fursa za kulisikia Neno likifundishwa na kunyumbulishwa. Tunapolisikia Neno Lake, tunapolikubali (kulielewa, kuliamini, kulitenda) basi “tunajengwa” na kukua katika roho zetu, taratiibu tunaongezeka katika mapana na kina cha imani yetu ili tuweze kustahamili vurugu na matatizo ya maisha yetu na kuimarisha upendo kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na pia imani ya kutosha kufanikisha kazi zozote ambazo Mungu atatutuma kuzifanya katika Kanisa Lake.
2Petro 3:18: Na sasa kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi, Yesu Kristo.
=0=
Translated from: Counteracting the Devil’s Strategy: Peter’s Epistles #1; Introduction
=0=
Basi, na tuonane katika somo #2 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!