Maana halisi ya “Roho aona wivu” katika Yakobo 4:5

Fundisho lifuatalo linatokana na Q & A (Maswali na Majibu) ya Dr. Robert Dean Luginbill inayoitwa ‘The Spirit that dwelleth in us lusteth to envy’: Explaining James 4:5 and other aspects of the Holy Spirit’s Ministries inayopatikana katika: https://ichthys.com/mail-Spirit-that-dwelleth.htm Tafsiri mbalimbali za aya hii (katika lugha mbalimbali hapa duniani) zimeonyesha mapungufu kadhaa ambayo yanapotosha maana halisi kama ilivyokusudiwa na Yakobo aliyeandika chini ya ufunuo wa Roho Mtakatifu.

Tafsiri na maelezo ya ziada na Respicius Luciani Kilambo.

Zifuatazo hapa chini ni tafsiri kadhaa za Kiswahili (na baadaye Kiingereza) za Yakobo 4:5 zinazoonyesha kwa nini msomaji alimwuliza Mwalimu-Mchungaji Luginbill swali hili baada ya yeye mwenyewe kusoma aya hii katika tafsiri kadhaa na kupata mkanganyiko wa kutosha tu. Kama wewe msomaji umesoma Waraka huu wa Yakobo [katika tafsiri mbalimbali], bila shaka umejiuliza maswali kuhusu nini hasa ilikuwa maana ya Yakobo katika kuandika hivi.

Yakobo 4:5 SRUV: Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu?
Hii ni Tafsiri ya Swahili Revised Union Version (SRUV).

Yakobo 4:5 BHN: Msifikiri kwamba Maandiko Matakatifu yamesema maneno ya bure, yanaposema: “Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu ana wivu mkubwa”.
Hii ni Tafsiri ya Biblia Habari Njema (BHN).

Yakobo 4:5 SNT: Au mnafikiri Maandiko matakatifu yanasema bure kuwa, “Anaona wivu juu ya roho (sic!) aliyemweka aishi ndani yetu”?
Hii ni tafsiri ya Swahili New Testament (SNT).

Hizi hapo juu ni namna tafsiri (versions) mbalimbali za Biblia katika lugha ya Kiswahili zinavyoiandika aya hii ya Yakobo 4:5. Nina uhakika kwamba mpaka hapa msomaji makini, hata yule wa kawaida, na pia yule wa kupita [tu] wa Biblia amekwishapata mkanganyiko wa kutosha tu, kutokana na jinsi tafsiri hizi zinavyotofautiana. Ikumbukwe kwamba Agano Jipya liliandikwa na Mitume katika lugha ya Kiyunani. Hata hivyo, ndugu yangu katika Bwana, “tatizo” hili haliko katika lugha ya Kiswahili pekee. Ili kudhihirisha hoja hii, nakusihi utizame aya hii katika tafsiri (Versions) kadhaa za Kiingereza pia. Nanukuu:

KJV: James 4:5:
Do ye think that the scripture saith in vain, The spirit that dwelleth in us lusteth to envy?
Hii ni kutoka King James Version Bible (KJV Bible)

NKJV: James 4:5:
Or do you think that the Scripture says in vain, “The Spirit who dwells in us yearns jealously”?
Hii ni kutoka New King James Version Bible (NKJV Bible)

NIV 1984: James 4:5:
Or do you think Scripture says without reason that the spirit he caused to live in us envies intensely?
Hii ni kutoka New International Version ya 1984 (NIV 1984)

NASB 1977: James 4:5:
Or do you think that the Scripture says to no purpose: “He jealously desires the Spirit, which He has made to dwell in us”?
Hii ni kutoka New American Standard Bible ya 1977 (NASB 1977).

HCSB: James 4:5:
Or do you think it’s without reason the Scripture says that the Spirit who lives in us yearns jealously?
Hii ni kutoka Holman Christian Standard Bible (HCSB).

Ni wazi kwamba katika tafsiri za Kiingereza, mkanganyiko upo kwa kiasi kilekile kama ilivyo katika tafsiri za Kiswahili. Katika NASB 1977 (New American Standard Bible ya 1977) ambayo inajulikana sana na ina sifa za kuwa moja kati ya tafsiri bora za Biblia, maana ya aya hii iko tofauti kabisa na hizo zingine. Mfano huu wa tafsiri ya Kiingereza ya NASB 1977 unadhihirisha jinsi ambavyo maana halisi ya aya hii imepotezwa.

Sasa na turejee katika Q & A yetu ili tuweze kujaza nyama katika mifupa ya hoja hii.

Swali #1:
Je, unaweza kunieleza maana ya aya hii?
Do you think the scripture saith in vain, The spirit that dwelleth in us lusteth to envy? James 4:5 KJV
AU katika Kiswahili:
Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? Yakobo 4:5 SRUV

Jibu #1:

Yakobo anaposema hapa “maandiko yanasema”, kiuhalisia ananukuu aya ya Wagalatia 5:17. Hii si mara ya pekee ambapo mwandishi wa Agano Jipya anarejea maandiko mengine ya Agano hilo na kuyaita “maandiko matakatifu”; kwa mfano Luka 10:7b; cf Warumi 16:26; 2Petro 3:15. Kwa hivyo utapata uelewa wa ufasaha zaidi kwa kusoma kwanza aya hii ya Wagalatia 5:17 ambayo Yakobo anainukuu katika Yakobo 4:5. Hapa chini nanukuu maelezo yangu ya aya hii ambayo niliyaandika katika sehemu inayoitwa “Genesis Gap” Part 2 ya mfululizo wa “The Satanic Rebellion”:

Maelezo ya Paulo kuhusiana na ukinzani wa Roho Mtakatifu dhidi ya dhambi na uovu katika huduma Yake katika maisha ya kila Mkristo yanajumuisha msingi [wa jinsi Roho Mtakatifu anavyomzuia kila mmoja wetu (sisi Wakristo) kutenda dhambi na uovu katika maisha yetu hapa duniani] (kumbuka kwamba katika Kiyunani – lugha asilia ya Agano Jipya - Yakobo 4:5 kimsingi inafundisha kitu kile kile kinachofundishwa na Wagalatia 5:17):

Waga. 5:17: Hivyo mwili (hulka ya dhambi ya mwanadamu) unaweka nia yake dhidi ya Roho [Mtakatifu], naye Roho Mtakatifu anaweka nia yake dhidi ya mwili. Kwa maana wawili hao wanapingana, na matokeo yake ni kwamba [wewe] hautotenda matakwa yako.

Sehemu ya mwisho ya aya hii ni ya muhimu sana katika kuelewa tofauti kati ya matukio mengi ya huduma ya Roho Mtakatifu ya kumkinga kila Mkristo na dhambi na huduma nyingine zote za Roho Mtakatifu katika ulimwengu huu wa viumbe ambazo tutazizungumzia hapa chini. Kwa maamuzi yetu yanayotokana na utashi wetu huru [kabisa], tunaweza kudhoofisha ufanisi wa huduma Zake [Roho Mtakatifu] zilizo nyingi anazozitoa kwa ajili yetu. Atatuongoza na kutuzuia kufanya makosa – kwa kiasi na mpaka aliojiwekea mwenyewe - lakini mwisho wa yote, Mungu wetu hatatumia uweza Wake mkuu kutulazimisha tuende kinyume na maamuzi ya utashi wetu huru pale yanapopelekea kwenye uovu ikiwa tumeamua kutenda uovu huo. Hii ndiyo maana ya “msimzimishe Roho” katika 1Wathess. 5:19 (SUV) na “msimhuzunishe Yule Roho Mtakatifu wa Mungu” katika Waefe. 4:30 (SUV), yaani pale tunapokamia kwa kiburi kuendelea na matendo maovu bila kusikia wala kujali sauti ya wazi ya Roho Mtakatifu inayoongea katika dhamira yetu. Hali hii ya kuweka vipingamizi dhidi ya huduma ya Roho Mtakatifu ya kutuzuia kutenda dhambi inapoendelea na kuzidi sana, inafikia katika matendo mabaya zaidi ya “kusema uwongo kwa Roho Mtakatifu” (Matendo 5:1-11) na “kumkufuru Roho” (Matt. 12:31). Mifano hii yote iliyotajwa hapo juu inadhihirisha ubishi wa mwanadamu (japo ni yule aliyezaliwa upya!) dhidi ya ukinzani wa Roho Mtakatifu [ambaye yu ndani ya kila mtu aliyezaliwa upya – Mkristo] dhidi ya dhambi na uovu, lakini, katika mifano hii yote, tunaona matendo yanayofanyika katika utashi huru kabisa ambayo Roho Mtakatifu mwenyewe anafikia mahala ambapo anaacha kutuzuia na kutukinga tusitende dhambi na uovu huo.

Tukirudi kwa aya yetu ya Yakobo 4:5 na hasa katika muktadha wake, aya hizi pia zinafundisha kuhusu huduma ya Roho Mtakatifu ya kutuzuia kutenda dhambi ambayo ni sehemu muhimu sana ya zile neema za kiroho anazopewa kila Mkristo, na, kama ilivyo katika aya ile katika Wagalatia, nayo inatuonyesha ukinzani wa moja kwa moja katika unyenyekevu na busara ya kumsikiliza na kumfuata Roho Mtakatifu dhidi ya mwenendo wa kiburi na upumbavu wa kuifuata tamaa ya mwili, pale unapofanywa kuwa ni mwenendo wa kawaida wa maisha (ambalo ndilo jambo Yakobo anatutahadharisha nalo, akihusisha matendo mabaya yanayotajwa katika aya ya 5 kuwa msingi wake ni “wivu”). Hivyo basi, mimi (Dr. Luginbill), ninazitafsiri aya hizi (Yakobo 4:4-6 na nukuu inayorejewa humo ya Wagalatia 5:17) kama ifuatavyo:

4.4 Enyi wazinzi (yaani walio na maadili mabovu)! Hamjui kwamba urafiki wenu na dunia unamaanisha uadui dhidi ya Mungu? Kwa hivyo yeyote anayetaka kuwa rafiki wa ulimwengu anajiweka kuwa ni adui wa Mungu.
4.5 Au mnafikiri kwamba maandiko (i.e. Waga. 5:17) yanasema bure tu kwamba “Roho akaaye ndani yenu “ameweka nia yake dhidi ya” wivu wa aina hii [ambao umeenea miongoni mwenu (kama inavyodhihirishwa katika mifano iliyotolewa katika aya za 1-4)]?
4.6 Lakini Mungu “anatoa neema zilizo kuu” [kuliko vishawishi vyote hivi] (anapotupatia Roho Wake ambaye anapingana na nia ovu za mwili). Hii ndiyo sababu imeandikwa, “Mungu huwapinga wenye kiburi, bali huwapa neema Yake wenye unyenyekevu”.
Yakobo 4:4-6

5.17 Hivyo mwili (yaani hulka ya dhambi ya mwanadamu) unaweka nia yake dhidi ya Roho [Mtakatifu], naye Roho Mtakatifu anaweka nia Yake dhidi ya mwili. Kwa maana wawili hao wanapingana, na matokeo yake ni kwamba hautotenda matakwa yako.
Wagalatia 5:17

Tafadhali tazama pale kirai / msemo ulio katika italiki / mlazo: “-weka nia yake dhidi ya”. Hii inatokana na misemo inayofanana sana katika Kiyunani kilichotumika katika Wagalatia na Yakobo (epithumei kata na epipothei pros). Vitenzi (verbs) hivyo viwili ni visawe (synonyms) vinavyokaribiana sana hivyo kufanya fasili / ufafanuzi / maelezo ya Yakobo ya ule msemo anaounukuu kutoka katika Waraka wa Paulo kwa Wagalatia (Waga. 5:17) kuwa na maana ya karibu kabisa. Yawezekana jambo ambalo limewasababishia watoa maoni na wafasiri wengi wa Yakobo 4:5 kushindwa kuona kwamba chanzo cha nukuu hiyo ni Wagalatia 5:17 (na hii kupelekea kushindwa kuelezea maana yake) ni matumizi ya Yakobo ya neno “wivu” katika kuelezea mwenendo wa dhambi wa aya za 1-4. Kwa uwazi kabisa, hata hivyo, “ameweka nia yake dhidi ya wivu [wa aina hii]” ni namna bora zaidi ya kutafsiri Kiyunani kilichotumika. Tafsiri ya King James inavyosema “to envy” inapindisha ukweli; tafsiri ya New International inaposema “envies intensely” inageuza misingi yote ya elimu ya kutafsiri lugha kuwa juu chini, [chini juu], kwani imetafsiri nomino kuwa kitenzi, na kitenzi kikuu kimekuwa kielezi (adverb), na imetelekeza kabisa kihusishi (preposition) [cha Kiyunani] pros ambacho maana yake ni “dhidi ya”, “against” katika muktadha huu! Fundisho la Yakobo hapa ni kwamba Roho Mtakatifu ni Msaidizi wetu katika kupambana na tamaa / uchu unaotokana na hulka ya dhambi tuliyozaliwa nayo, ambayo hapa [Yakobo] anaielezea kuwa “inakionea wivu” kile kizuizi cha Roho Mtakatifu kinachotusaidia sisi. Ama kwa hakika, hiki ndicho kitu ambacho Paulo alikifundisha katika Wagalatia 5:17, ijapokuwa amekisema katika namna tofauti kidogo: Roho anapingana na mwili; mwili unapingana na Roho; sisi tunaamua kama tutamfuata Roho Mtakatifu au tutazifuata tama zetu wenyewe.

Katika Yeye aliyetupatia Roho Wake mwema ili atuongoze katika mitihani na vishawishi tunavyopitia, Mwokozi na mpendwa wetu Yesu Kristo,

Robert Luginbill, https://ichthys.com