Ufafanuzi (au Fasiri) wa Biblia sehemu ya III

Ifuatayo ni sehemu ya tatu katika mfululizo wa mafundisho ya ufafanuzi wa aya za Biblia. Mfululizo huu utahusisha maswali na majibu ambayo wasomaji (au wanafunzi wa Biblia) wa tovuti ya https://ichthys.com ya Dr., Professor, Pastor-Teacher Robert D. Luginbill walimwuliza katika nyakati mbalimbali. Nilimwomba Dakta Luginbill ruksa ya kutafsiri maswali & majibu haya kwa faida ya wanafunzi wa Biblia wanaozungumza lugha ya Kiswahili; Dakta alinipatia ruksa hii na haya hapa chini [na sehemu zinazofuata, na iliyotangulia] ndiyo matokeo ya kazi hii.

Ndugu Mkristo, nakukaribisha ili uweze kufaidika [kiroho] na mafundisho ya Neno la Mungu yaliyomo katika mfululizo huu.

Fasiri ya mfululizo mzima na Respicius Luciani Kilambo wa https://sayuni.co.tz

Sehemu ya III: Fasiri (Versions) za Biblia, Wanazuoni wa Biblia, Tafsiri mbalimbali za Biblia, n.k.

Kutoka: Bible Interpretation: Interlinears, Academics, Versions et al.
Na Dr. Robert D. Luginbill wa https://ichthys.com
Of May 17 2008

Swali #3:

Profesa, nina swali moja la haraka-haraka hapa kwa ajili yako. Je, umeshawahi kusikia juu ya waraka unaoitwa "Protoevangelium of James"? Nimesikia kutoka kwa baadhi ya watu kwamba kitabu au waraka huu ulikuwa ukisomwa sana na Wakristo wengi katika Kanisa la mwanzo (karne za mwanzoni za Milenia ya 5) na kwamba ulipewa heshima kuu. Lakini kwa kuwa kitabu hiki kinatoka karne ya 2, kwa jinsi nilivyoweza kuhakiki, Yakobo – yule mdogo wake Bwana Yesu au ndugu yake Yohana [wote waliitwa Yakobo] – asingeweza kuandika kitabu hiki. Je, wewe Profesa una ufahamu wowote kuhusu jambo hili? Je, ni kweli kwamba kitabu / waraka huu ulithaminiwa katika Kanisa lile la mwanzo? Kama ni hivyo, kwa nini kitabu hiki hakikuwekwa katika orodha [rasmi] ya Biblia?

Jibu #3:

Mimi sifahamu mambo mengi tu kuhusu kitabu hiki, isipokuwa nafahamu kwamba [kitabu chenyewe] hakijathibitishwa. Kulingana na waandishi [walioandika historia husika], kitabu hiki kilitajwa kwa mara ya kwanza na Origen wa Alexandria, kwa hivyo [madai kwamba] uandishi wa kitabu hiki ulifanywa katika karne ya 2 au ya 3 ni makisio yanayoweza kuwa sahihi. Kukosekana huku kwa mjadala kuhusu kitabu hiki kabla ya karne ya 2 na ya 3 pia kunaonyesha kwamba kitabu hiki hakikuwa na umuhimu katika Kanisa lile la mwanzo. Lengo mojawapo linaloonekana [katika malengo kadhaa ya kuandikwa kwa waraka huu] ni lile la kutafuta namna ya kuhalalisha kwamba Maria mama wa Yesu Kristo aliendelea kuwa bikira maisha yake yote (katika kitabu hiki, inadaiwa kwamba Yosefu alioa kabla ya kumposa Maria na hivyo alikuwa na watoto kutokana na ndoa hiyo – yaani wale ndugu zake Bwana Yesu wanaotajwa katika Injili rasmi 4 tulizonazo hivi sasa). Hivyo kitabu hiki ni kimojawapo kati ya vitabu vingi vya kughushi vilivyokuwa na malengo ya kuimarisha hoja ambazo Biblia haifundishi na hapa lengo lake lilikuwa ni kutoa "msingi wa ki-biblia" wa kanuni ya uwongo ambayo ilikwishakuwa moja ya mafundisho muhimu ya kanisa Katoliki la Rumi – ile kanuni ya "ubikira daima" wa Maria.

Katika Bwana wetu,

Bob L.

Swali #4:

Profesa, wewe unatumia fasiri (version) gani ya Biblia [kwa ajili yako mwenyewe na kwa ajili ya kufundishia]?

Jibu #4:

Wakati ninafanya utafiti wangu wa Biblia na uandishi wa mafundisho yangu, huwa ninahakikisha kwamba ninasoma vitabu vya Biblia katika Kiebrania, Kiarami na Kuyunani, na pia ninasoma zile nakala za nyaraka asilia za Biblia; pia ninajitahidi sana nisome Biblia kila siku. Mimi huisoma Biblia pia katika lugha ya Kiingereza; husikiliza Biblia ikisomwa kwa sauti katika fasiri (version) ya KJV – King James Bible; huwa naisoma fasiri ya NASB – New American Standard Bible – sambamba na Agano la Kale katika Kiebrania na Kiarami; pia mimi huisoma fasiri ya NIV – New International Version – 1984. Katika mafundisho ninayoyaweka kwenye tovuti yangu ya https://ichthys.com karibu mara zote mimi hutumia tafsiri zangu mwenyewe ninazozifanya kutoka katika nakala za nyaraka asilia za Biblia, lakini wakati mwingine ninatumia NIV, KJV au NASB au RV - Revised Version - au fasiri yoyote ambayo ninaiona imeelezea maana / dhana halisi ya aya husika, kwa mtazamo wangu. Hivyo, kwa kifupi, aghalabu nitatumia tafsiri yangu mwenyewe ya aya husika, lakini ikiwa nitaona siwezi kuiboresha fasiri [rasmi] iliyoko, basi nitaitumia fasiri hiyo. Unaweza kusoma tahakiki (critique) yangu ya baadhi ya fasiri hizi katika linki zifuatazo katika tovuti yangu:

Read your Bible: A Basic Christian Right and Responsibility
FAQ #12. Translations: Where do the translations of scripture that appear at Ichthys come from?
FAQ# 20. Sigla: Would you explain the abbreviations and symbols used in the translations at Ichthys?

Katika Bwana wetu Yesu Kristo,
Bob Luginbill.
Swali #5:
Kwanza ninataka kukushukuru kwa upendo wako wa wazi kabisa kwa Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Wewe una uwezo mkubwa sana wa kufikiri, na umeutumia uwezo huu katika kutimiza jukumu la juu kabisa ambalo Mungu wetu amekusudia sisi viumbe Wake wenye utashi kulitimiza, yaani katika kumtafuta na kumjua Mungu wetu. Kabla sijaendelea na waraka huu, ningependa usome kazi hii hapa chini ambayo ni matokeo ya tafakuri yangu katika Neno. Najua wewe huhitaji rafiki wa kalamu na pia ninajua kwamba muda wako ni muhimu sana kwako, lakini ikiwa utatoa maoni yako hata msitari mmoja tu, nitashukuru sana. Ninaamini kwa moyo wangu wote kwamba ndani ya waraka huu nimeandika sababu ya tatizo kubwa linalosibu madhehebu yote ya Kikristo. Kama mwanazuoni, baadhi ya maoni yangu yaliyomo ndani ya waraka huu yanaweza kukuudhi, lakini mimi nakuomba usikasirike. Kama maoni haya yameelekezwa kwako wewe binafsi, basi ni maoni chanya.
Mungu Akubariki.
Waraka wangu:
NANYI MWANINENA MIMI KUWA NI NANI? - Matt. 16:15 SUV.
Kuna masuala mengi [sana] kama jehannamu na adhabu, ubatizo, utakaso, usalama wa milele [wa muumini] (OSAS), kuishi kitakatifu, uhakika na ukweli wa maandiko /Biblia, nini maana ya wokovu, unyakuo, n.k., ambayo yanaendelea kuwagawanya wateule au watu wa Kanisa la Kristo. Watu wengi wanaokiri kuwa sehemu ya familia ya Mungu wanatofautiana katika [fasiri na] uelewa wao wa maandiko ambayo yanahusiana siyo tu na haya masuala muhimu, lakini pia katika karibu kila mtazamo / msimamo wa kitelojia unaojadiliwa. Kalti / makundi ya uwongo yameasisiwa kutokana na tofauti hizi [kati wa Wakristo], na kukosekana kwa umoja / mshikamano kati ya wateule wa Mungu limekuwa ni jambo la kawaida kutokana na tofauti hizi za mtazamo. Sasa, kwa [Wakristo] wengi, tofauti hizi siyo tu kwamba zinakanganya, bali zina matokeo ya kudhoofisha imani yao binafsi. Inawezekana kabisa wasionyeshe waziwazi mkanganyiko huu, lakini ndani ya mioyo yao watajiuliza, ikiwa hawa wasomi na wasomaji wengine [wa Biblia] wanaweza kusoma maandiko yaleyale na wakakosa maelewano au wakatofautiana namna hii, basi labda hakuna kweli huru, isiyo na masharti wala mipaka, ndani ya Neno la Mungu (God forbid!). Ni mara ngapi tunasikia maoni haya (kwamba Biblia haina ukweli wa Mungu ndani yake yakisemwa na watu wasioamini na pia yakisemwa na wale mbweha ambao lengo la maisha yao ni kuwashambulia wana wa Mungu na Neno Lake? Hili ni shambulizi ambalo limekuwa na mafanikio makubwa katika kuwavuruga Wakristo, lakini je, hili ni jambo muhimu kwa kila mmoja wetu ndani ya nafsi yake? Kwa maneno mengine, je, Mungu wetu Atatupatia thawabu kwa msingi wa umoja au makubaliano ya kanuni za Biblia zinazoaminiwa na Wakristo? Kumbuka kwamba mageuzi ya karne ya 16 (The Reformation) kwa maana fulani yalitokana na kukataa kuliruhusu Kanisa Katoliki la Rumi na viongozi wake kuamuru na kufasili kweli au kanuni za [kiroho] kwa kila mtu. Kimsingi, taasisi hii (nachelea kuliita Kanisa Katoliki la Rumi kama sehemu ya lile Kanisa halisi la Bwana wetu, kwa sababu zilizo wazi – R. K.) ilidai kwamba Mungu Hatomhukumu kila mtu [peke yake], kwa uelewa wao wa maandiko, bali wajibu wa kila mtu ni kuyapokea bila hoja mafundisho ya taasisi hiyo (na huu unaendelea kuwa ndio msimamo wa taasisi hii mpaka leo). Sasa, ni wapi katika maandiko ambapo kanuni au mtazamo au msimamo huu unafundishwa?! Kwa nini Bwana wetu atuambie kwamba tunapaswa tujifunze Neno la kweli ili tujionyeshe kuwa tumekubaliwa na Mungu?
Uwe na ari ya kujionyesha mbele za Mungu kuwa wewe umekubaliwa [katika yale unayoyafanya], mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, [kama seremala stadi] “akilikata sawasawa” (orthotomeo) Neno la kweli.
2Tim. 2:15

Kwa nini Bwana Yesu atasema ondokeni mbele ya uso wangu, kwani “Mimi sikuwajua”, kwa wale ambao watamwita “Bwana, Bwana” - Matt. 25:11-12?

25.11 Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.
25.12 Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.
Matt. 25:11-12 SUV

Hata kama viongozi wetu wa kiroho [wa sasa] wangekuwa Mitume halisi, jambo ambalo si kweli, je, wangeweza kutulazimisha tuwe wafuasi wao bila ya kujali usahihi (au la) wa kanuni wanazotufundisha? Je, Mtume Paulo hakulitumia neno “sisi” katika tahadhari yake juu ya wale watakaoihubiri Injili tofauti (Waga. 1:8)?

1.8  Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiria ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiria, na alaaniwe.
Waga. 1:8 SUV

Ni haki na wajibu wa kila mtu aliyeokolewa (aliyezaliwa upya) kulichambua kwa usahihi (kama seremala stadi anavyonyoosha msumeno) Neno la kweli yeye mwenyewe. (Tazama pia mfano wa waumini / Wakristo wa Berea: Matendo 17:11). Kanisa la Kiinjilisti la sasa na jumuia ya sasa ya Kiinjilisti wako karibu sana na kuunda Uprotestanti wa Kirumi (unaofanana sana na Ukatoliki wa Kirumi!). Aghalabu wanawawekea vikwazo au kuwapachika chapa ya “ukosefu wa imani ya kweli” wale wote wanaotaka kutafiti ukweli (au la) wa masuala ya kanuni za kiteolojia yanayoainishwa na kundi lao, na ambayo yanaweza kutofautiana. Watausema mdomoni tu na kujidai wanauheshimu sana msingi wa Kibiblia wa utakaso endelevu (soma Nyaraka za Petro #13, na #30), lakini kiuhalisia hawataki kuutumia msingi huu wao wenyewe. Viongozi wa makundi haya watawadhalilisha hadharani wale wote watakaowauliza maswali [magumu] kuhusu mahubiri na mafundisho yao ya kanuni mbalimbali, na kuwapachika chapa ya “ukorofi” na kuwaambia kwamba basi ni afadhali wakaenda kuabudu mahala pengine. Hawaoni kwamba Mungu wetu anaweza kufurahishwa tu pale watoto Wake wanapouamini, ndani ya mioyo, yao ukweli mahususi uliomo ndani ya Neno Lake?

Kitu kibaya zaidi ni pale watoto [hawa] wa Mungu wanapokuwa au wanaposhikwa na shauku ya kukubalika na ulimwengu au kanisa / kusanyiko / kikundi chao bila kujali na pia huku wakiyazima yale mashaka mioyoni mwao wenyewe yanayohusiana na kanuni fulani ambayo wameigundua kuwa ni ya uwongo. Ni jambo la kusikitisha sana kwamba [sasa] ulimwengu ndio unaofasili au kufafanua imani ya Kikristo [badala ya Wakristo na Biblia yenyewe]; mifano kadhaa ni: Mungu wetu ni upendo halisi na Anawapenda wote [na matendo, fikra, kauli zao]; Mungu katu hatompeleka yeyote jehannamu; Mungu hajali wala hajisumbui na mambo yatakayotokea baadaye (siku za usoni katika historia ya wanadamu na malaika) na kudura (kliki hiyo linki upate fundisho hili) ni kanuni isiyo sahihi; mwanadamu atatathminiwa na kuhukumiwa (au la) kwa matendo yake pekee; miungu yote ni sawa; Bwana Yesu siyo Mungu bali Alikuwa tu ni mwanadamu mwenye uelewa na weledi wa hali ya juu; uwe mkweli moyoni mwako na uwaonyeshe upendo wengine na mambo yako yote yatakuwa ok na Mungu; n.k. Mawazo na ‘mafundisho’ haya na ya aina yake yanazidi kuimarisha mizizi yake katika kanisa la Kiinjilisti leo hii, ingawa siyo ya Kibiblia kabisa. Bwana Yesu alisema kwamba wapo na watakuwepo waalimu wa uwongo ambao kiuhalisia ni mbweha waliovaa ngozi ya kondoo tu. Alitufundisha na kutuonyesha namna ya kuwagundua na Akatuelekeza kwamba tunapaswa kuwa na akili na roho ya kupambanua.

7.15 Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
7.16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?
7.17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.
7.18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.
7.19 Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.
7.20 Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.
Matt. 7:15-20 SUV

Alitupatia tahadhari kwamba Shetani kamwe hawezi kujiondoa mwenyewe wala kujifichua mwenyewe. (Hii imelengwa kwa wale wanaoamini kwamba kuna ‘wachungaji’ leo hii wenye uwezo wa kutoa pepo, n.k.; kama unataka kujua ukweli wa Kibiblia kuhusu uwongo huu, kliki linki hii: Karama za Roho Mtakatifu | Sayuni ).

11.17 Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka.
11.18 Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli.
11.19 Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu.
11.20 Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.
11.21 Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama;
11.22 lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.
Luka 11:17-22 SUV

Shetani ni mwongo na mdanganyifu, na shauku yake ni kuwaangamiza watoto wa Mungu. Ebu litazame suala hili kwa namna hii: kila mwalimu wa Biblia anawajibika (na atawajibika, hapa duniani na pia katika siku ya hukumu / thawabu) kwa ukweli na usahihi (au la) wa mafundisho yake. Lakini kustahili kwake adhabu ikiwa mafundisho yake ni ya uwongo hakuna maana ya kwamba na mimi nitapata adhabu hiyo ikiwa mimi ni mwanafunzi wake. “Mwalimu” atawajibika kwa mafundisho yake, bali mimi (msikilizaji wake) nitawajibika kwa kile nitakachokiamini katika mafundisho hayo, kilicho cha kweli au la. Hivyo msomaji unaweza kuona hapa kwamba ni wazi kuwa sisi Wakristo, kila mmoja wetu, tuna wajibu wa kuitafuta kweli, na tutawajibishwa kwa kuutambua ukweli au la. Kama baadhi ya viongozi wa kanisa lako ni mbweha, hawatajifichua wenyewe, sivyo? Italazimu wafichuliwe!

Wapo watu wengi sana, wakati wakiwa mbele za wenzao wanaendelea kusimama “imara” katika “misingi ya imani” ya kanisa au kundi lao, lakini katika faragha za mioyo yao wana imani nyingine kabisa ambayo msingi wake ni maandiko matakatifu. Kura nyingi sana za maoni zinazofanyika [hapa USA] zinaonyesha kwamba ingawa sehemu kubwa ya wale wanaojiita Wakristo “wanathibitisha” kwamba wanaifahamu kweli ya maandiko wanapohojiwa katika mazingira ya kanisa au kundi lao, wanapohojiwa katika faragha wanaukana kabisa msimamo huo. Wanaikubali dhana ya kuishi maisha safi ya Kikristo, lakini kiuhalisia wanaishi kama walimwengu, na katika faragha za mioyo yao wanaikana misingi ya imani [ya Biblia] ambayo ni muhimu hata kwa wokovu wao wenyewe. Je, Mungu anaweza kufurahishwa na mwenendo huu, au katika siku ile watakapomwita “Bwana, Bwana” watayasikia tu maneno Yake: “Sikuwajua ninyi!”. Ni muhimu, tena muhimu sana, kwamba tunajitahidi kumjua Mungu, kila mmoja peke yake, kwa juhudi zake, ingawa kwa wakati huo huo tunapaswa kufundishwa na mwalimu wa Biblia aliye mahiri. Bwana ametuelekeza tufanye hili na inatupasa tusiukimbie wajibu huu.

24 bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema Bwana,
Yer. 9:24 SUV

Sisi sote [tuliozaliwa upya, tulio sehemu ya Kanisa la Bwana wetu Yesu Kristo] tunawajibishwa, na tutawajibishwa kila mmoja kwa nafsi yake, na Mungu wetu. Kama tunaisikia au tunaiona kweli, halafu hatuiamini kweli hii, hili linakuwa jambo lisilo na maana kabisa mbele za Mungu. Kama Mungu anatufahamu, kama tutamwamini, basi Atajifunua kwetu. Sasa, tuseme nini basi kuhusu yale maeneo yote ambamo sisi Wakristo tunatofautiana? Ili kumwelewa na kumjua Mungu, [tunapaswa kulisikia / kulisoma, tunapaswa kufundishwa], tunapaswa kulitafakari Neno Lake, na kisha tunapaswa kulinganisha yale tunayojifunza na maandiko yote mengine tunayoyasoma. Kamwe tusiutelekeze uchunguzi na utafiti wetu wa ile kweli kwa kutegemea mawazo ya wengi au mafundisho ya viongozi wetu wa makanisa [pekee], hata kama tunafikiri [viongozi hao] wana vipawa kiasi gani. Mungu wetu hatotuondolea hatia na hatotupatia zile kweli za kiroho na umaizi wa kiroho ikiwa tutamtegemea mtu au ikiwa tutaacha kitu fulani kichukue nafasi ya Roho Mtakatifu kama kiongozi wetu pekee [katika mchakato wa kujifunza Neno la Mungu]. Kumtelekeza Roho Mtakatifu na kuyaacha maandiko na badala yake kufuata mafundisho fulani [kwa sababu tu] yanapendwa na watu wengi, na pia kufuata mamlaka ya kanisa au kundi letu kunafanana sana na hali iliyoko katika Kanisa Katoliki la Rumi, na inampasa kila mteule wa Bwana kuikataa hali hii. Kila mmoja wetu, kila nafsi peke yake, atatoa maelezo ya maisha yake na fikra zake [hapa duniani] katika ile siku ya tathmini na hukumu, na Mungu wetu hatotuondolea hatia au lawama kama tukisema “lakini kanisa langu lilifundisha [hivi]” au “mchungaji wangu alifundisha [hivi]”. Pale Pilato alipomwuliza Bwana Yesu kama Yeye alikuwa mfalme wa Wayahudi, jibu la Bwana Yesu lilikuwa “je, wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikwambia habari zangu?”

18.33 Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia, Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?
18.34 Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?
Yohana 18:33-34 SUV

Alichokuwa anakiuliza Bwana Yesu hapa ni: Je, wewe [Pilato] ulilisikia hili na ukaamini ndani ya moyo wako kwa utashi wako mwenyewe, au unarudia kusema kitu ulichosikia watu wengine wakisema? Utashi wetu wenyewe na juhudi za kutaka kuelewa ndivyo vitakavyosababisha ni kiasi gani cha ile kweli ya Biblia kitafunuliwa mioyoni mwetu [na Roho Mtakatifu]. Hakuna hata mmoja atakayeweza kusimama mbele ya Bwana katika siku ile kwa msingi wa yale aliyoyasikia lakini hakuyaamini ndani ya moyo wake. Kumwita tu “Bwana”, bila ya Yeye kutukubali [kutokana na viwango Vyake alivyoviweka ndani ya Neno lake], hakutatusaidia kitu. Hatuwezi kudai kwamba tunamjua, ikiwa Yeye hatujui sisi. Bwana Yesu anatuuliza sisi sote, “nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?”. Msijidanganye na msidanganyike, Mungu anaijua mioyo yetu, na atatuhukumu / atatutathmini sisi sote siku ile tutakaposimama mbele Yake. Viongozi wetu wa kiroho wana jukumu na wajibu mkubwa waliopewa na Mungu. Wanapaswa kuwa waaminifu kwa Neno lake, wawafundishe kondoo wa Bwana kama Roho Mtakatifu anavyowapa ile kweli, na kuwachunga watoto wa Mungu. Lakini pia hawa ni wanadamu ambao wakati mwingine wanatofautiana na wenzao juu ya zile kanuni kuu za Biblia na wakati mwingine juu ya kanuni ndogo. Viongozi wa watu wa Mungu wanatakiwa kufundisha na kutia mwanga katika kanuni za kweli (Neno) za Mungu. Tizama vizuri, kweli zimo ndani ya Biblia. Hii ina maana kwamba hata bila ya [kufundishwa] na mwalimu, kanuni za kweli bado zipo na bado zinapatikana, sivyo? Siku zote linganisha mafundisho ya mwalimu wako na Biblia / maandiko na umwombe Mungu akupatie uelewa (Matendo 17:11). Kumbuka tu kwamba maandiko ni pumzi ya Mungu (2Wakor. 3:16-17) na kwamba ni maneno ya Bwana Yesu ambayo hayatapita [kamwe] (soma Matt.24:35).

3.15  na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.
3.16  Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;
3.17  ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.
2Tim. 3:15-17 SUV

4.12  Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo (mifupa) na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li (Neno lililo ndani ya dhamiri zetu) jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
4.13  Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu [vi uchi] na kufunuliwa machoni pake Yeye tunayepaswa kujihusisha naye.
Waebr. 4:12-13

Ukiweka pembeni ulazima wa kutafsiri Biblia ambao unayawezesha maandiko kuwasilishwa kwa watu wote ili watu hao waweze kuukubali au kuukataa ufunuo wa Mungu kwao, ufunuo ambao unahusisha mipango Yake ya kale, ya sasa, na ya baadaye, ya uumbaji Wake huu, taarifa zote ambazo ziko nje ya maandiko kwa maana fulani hayana ulazima / umuhimu na kwa kiasi kikubwa (na mara nyingi) taarifa hizi zina madhara kwa afya yetu ya kiroho. Kwa maneno mengine, hakuna elimu au ufahamu wa kale, wa sasa na hata wa siku za usoni ulioko nje ya Biblia, ambao unaweza kuwa bora zaidi ya elimu au ufahamu uliomo ndani ya Biblia. Kufundisha maandiko na maana yake ni jambo lenye kufaa sana kwa sababu shughuli hii inawakusanya na kuwakutanisha pamoja watoto wa Mungu na wale wanadamu ambao hawajazaliwa upya, na hili hufanikisha uinjilisti, ushirika / uanazuoni (fellowship), ibada, ushuhuda wa hadhara / wazi wa Kristo, kushiriki katika sakramenti, kushiriki katika sala ya pamoja, umoja, kutiana nguvu, na mengi mengine ambayo maandiko yameamuru yafanyike katika kusanyiko, lakini kwa hakika amri ya kuifundisha Biblia imo katika Biblia yenyewe, kwa mfano 2Pet. 3:18. Bila ya kulitamka na kulifundisha Neno la Mungu, wale wasiojua kusoma na / au wale wasiokuwa na kitabu cha Biblia watazikosa neema, tahadhari, na amri zilizomo ndani ya Biblia.
Hata hivyo, kudai kwamba kulitamka na kulifundisha Neno la Mungu kunalazimu elimu ya juu ya anthropolojia, falsafa, isimu, desturi, sayansi, saikolojia, matukio ya ulimwengu, methodolojia za kutafsiri maandiko, au mfumo wowote wa habari (mfumo wa habari – information system) ulio nje ya maandiko ni kuyakataa mamlaka ya Mungu. Wale wanaoamini kwamba mafunzo ya ziada ni ya lazima kwa ajili ya kufundisha na kuhubiri Neno la Mungu wanapaswa kuchukua tahadhari; wale wanaowaamini watu wenye imani hii wanapaswa kuchukua tahadhari mara dufu.
Kimantiki, kama jambo fulani ni la ulazima katika kufundisha na kuhubiri Biblia, basi jambo hilo ni la ulazima pia katika uelewa wa Biblia hiyo hiyo.

Walio wengi kati ya wahubiri na waalimu wa Neno la Mungu wanajifunganisha na makundi mbalimbali yanayotofautiana kiteolojia kwa kiasi kidogo au kikubwa. Wana-teolojia au wanazuoni hawa huchukua misimamo yao [hii ya kiteolojia] mapema tu katika maisha yao ya kiimani, na ni nadra sana kuwaona wakibadilisha misimamo yao hii. Kubadilisha misimamo hii kutaionyesha kadamnasi kwamba walikosea, jambo ambalo [wao wanafikiri] linawafanya wasiaminike [sana] kama waalimu na wahubiri! Kama mtu mmoja atasema “baada ya kujifunza upya na kuichunguza kwa uangalifu [kanuni fulani] nikiomba uongozi wa Roho Mtakatifu wakati wote, sasa nina uhakika maandiko yana msimamo huu [mwingine] kuhusu kanuni hii”, basi matokeo ya wao kubadilisha msimamo wao kuhusiana na kanuni hii yatakuwa yapi? Sasa, msingi wa Kikristo wa utakaso-unaoendelea-kujengeka unalazimu mabadiliko hayo ya msimamo katika maisha ya mwalimu au mhubiri huyu wa Biblia, lakini matokeo ya mabadiliko ya msimamo wake yatakuwa yapi miongoni mwa wanateolojia au wanazuoni wenzake? Fikiria hili kwa undani. Orodha ya makundi tofauti ya kiteolojia ni ndefu sana: Kalvinisti, utashi huru, ubatizo wa Roho Mtakatifu, neno / imani, open theism, covenant theology / teolojia ya agano, n.k., n.k. Je , hawa watu wana tabia ya kukubali kwamba wamekosea na kuendelea kuitafuta kweli kwa moyo wao wote(?), sidhani. Hata John MacArthur alisema kwamba alianza na kanuni fulani mahususi na mtazamo wake kuhusiana na kujifunza na kufundisha Biblia ni [kuendelea] kukaa ndani ya mipaka ya hizo kanuni zake [kiitikadi]. Sasa, huu unaweza kuwa ni mtazamo wa kawaida na unaofaa, lakini pia wengine wengi miongoni mwa wenza wa bwana John MacArthur wameonyesha kwamba wana mtazamo kama wa kwake. Suala muhimu siyo kwamba hawa ndugu wako sahihi au la, bali ni kwamba, je, sisi tunaofundishwa na walimu hawa tuko tayari kuuweka uhakika wetu wa uzima wa milele katika mikono ya watu ambao kwa kauli zao wenyewe kamwe hawatakubali kwamba [wao] hukosea? Wanaweza kukubali kwamba wao hufanya makosa madogo-madogo, ambayo “hayatawachafua” mbele za macho ya wanazuoni wenzao, lakini hawatokubali kufanya makosa yatakayolazimu kufanya mabadiliko ya kikanuni ya nyuzi 180! Makosa madogo-madogo yanawafanya waonekane kuwa wacha Mungu, lakini makosa makubwa yanawafanya waonekane kuwa ni wenye mapungufu makubwa ya kiroho! John Stott, mwana-teolojia maarufu Mwingereza, Muanglikana aliyeishi karne iliyopita, alibadilisha mtazamo wake kuhusu ‘kanuni’ ya “God’s wrath” au “the punishment of the lost” - adhabu ya wale waliopotea. Mara baada ya kutangaza mabadiliko haya, John Stott alipachikwa chapa ya uasi wa imani sahihi (heresy) na mliberali, na kuitwa majina mengine mengi yenye sifa mbaya. Wafuasi wake wengi walishindwa kukubali mabadiliko ya msimamo na mtazamo wake kwa sababu bwana Stott alikiri kwamba alikosea, na hii ilimaanisha kwamba na wao walikosea pia. Tatizo halikuwa mtazamo wao, bali ni kiburi na majivuno yao. Yawezekana wenyewe hawakujiona kwamba walikuwa na kiburi na majivuno, lakini huo ndio ukweli wenyewe!
Robert van Kampen, ambaye aliandika kwa kirefu juu ya dhana inayoitwa “pre-wrath / tribulation rapture”, yaani “unyakuo utakaotukia kabla ya Dhiki Tuu”, alizungumzia mambo aliyoyaona kwa wasomaji wake katika kimoja kati ya vitabu vyake. Yeye aliweka namba ya simu ambayo wasomaji wake waliweza kupiga bila malipo kwa wale waliotaka kujadili kitabu chake. Katika kitabu hiki, van Kampen anasema kwamba alipokea mamia ya simu alizopigiwa na watu ambao, baada ya kusoma kitabu chake walibadili msimamo / mtazamo wao na kuacha kuamini juu ya fundisho la “pre-wrath / tribulation rapture” au “unyakuo kabla ya Dhiki Kuu”. Lakini, watu hawa walimwambia pia kwamba mbele ya kadamnasi (ikiwa ni pamoja na mbele ya waumini wa makanisa / madehehebu yao) hawatatamka juu ya mabadiliko ya msimamo wao huu, kwa sababu kufanya hivyo kutahatarisha kazi au ajira zao kama wachungaji na / au waalimu wa makanisa yao. Ebu tafakari juu ya jambo hili kwa dakika tano tu! Hata hivyo, jambo muhimu ni kwamba Mungu wetu hatotuchukulia kwamba tunawajibika kwa mafundisho ya mwana-teolojia au mwanazuoni yeyote, bali Atatuwajibisha kwa kile tulichokiamini [juu ya Neno lake] hapa duniani. Kumbuka, kama Mungu anataka kujifunua Mwenyewe, atafanya hivyo kwa watoto Wake waliojitoa kwa kusudi la kumfahamu na kumwelewa ili wawe watumishi bora na wafuasi bora wa Kristo. Kama Ametupatia kweli iliyofunuliwa, ambayo ndiyo kweli Atakayotuwajibisha nayo, basi Yeye mwenyewe ataifanya iwe wazi na rahisi kueleweka kiasi kwamba hata mtoto mdogo ataweza kuielewa. Yeye anayajua na kuyaelewa mawazo yetu yote na anaifahamu nia yetu na kila jambo tunalokusudia.

Mungu ametupatia maelekezo Yake yanayohusiana na wokovu, utakaso na kuishi kimungu. Roho Mtakatifu atamulika njia ya wale wote wanaolisoma au kulisikiliza Neno Lake na wana shauku ya kumwelewa na kumfahamu Mungu. Hata hivyo, ikiwa sisi wenyewe tunasisitiza kuendelea kufundishwa na waalimu waongo, basi Yeye hatofanya mashindano na waalimu hao.
1.12  Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu anasema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo.
1.13  Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?
1Wakor. 1:12-13 SUV

3.4  Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu [tu]?
3.5  Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa.
3.6  Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu.
1Wakor. 3:4-6 SUV

Kama tunafikiri kwamba “kujifunza ili kujionyesha mbele za Mungu kwamba sisi tumekubaliwa” ina maana ya kujifunza mambo yaliyo nje ya Neno la Mungu, yanayohusisha mafundisho ambayo watu fulani wanadai wamefunuliwa au yanatuonyesha / kuashiria kitu fulani katika wakati na mahala tunamoishi, basi mkanganyiko na mfarakano vitakuwa ndiyo matokeo ya “mafundisho” hayo [kama ambavyo tunaona leo katika makundi / madhehebu mengi ya Kikristo]. Je, Mungu wetu ni mwenye upendeleo kiasi kwamba [ati] sisi tunaoishi katika hii “enzi ya habari” tumebarikiwa zaidi ya wale ambao waliishi katika enzi za kale? Kwa kuwa jibu sahihi na la wazi kabisa katika swali hili ni “hapana”, basi ni kwa nini tunakiri kwamba maandiko yanajitosheleza, halafu tunashangilia kwa kiasi hiki mafanikio yetu katika elimu ya kidunia, elimu ya dini – zinayofundisha hadithi za kutungwa na wanadamu - na shahada – za elimu ya kidunia - tunazozipata? Leo hii tunawaona “wavuvi wa watu” wachache sana wakisimama katika mimbari (pulpits) za makanisa yetu. Labda tuwatunze wale Mitume 12 wa Bwana wetu shahada za heshima za udakitari ili tuweze kuwaheshimu zaidi. Kwa nini tunadai kwamba maandiko yanatosha kwa mahitaji yetu yote ya kisaikolojia, halafu tunasomea shahada ya masomo ya kidunia ili tuweze kufundishana yale ambayo tulikwishasema kwamba Mungu amefanya (yaani Amekwishafundisha) katika maandiko? Je, huu sio unafiki? Makanisa yanaamua nani watakuwa viongozi wao wa kiroho kwa kutumia vigezo vya kidunia; huo sio unafiki? Waumini wanathamini mafundisho ya wanadamu na mafanikio katika vyuo vya kidunia badala ya kuongozwa na Roho Mtakatifu; huo sio unafiki? Halafu tunashangaa na kujiuliza kwa nini hakuna umoja kati ya watoto wa Mungu? Tunatoa kauli kwamba kumfuata Mungu na kuamini Neno Lake kunatosha, halafu kiuhalisia tunamfuata na kumtegemea mwanadamu na mafundisho yake.

22Acheni kumtumainia mwanadamu, ambaye hana kitu ila pumzi katika pua zake. Yeye ana thamani gani?
Isa. 2:22

Paulo alituonya kuhusiana na mtazamo huu na mara kadhaa alitukumbusha tusijiunge na kufuata mafundisho ya mtu fulani anayejiita ‘kiongozi wa kiroho’ ikiwa kumfuata mtu huyu kutamaanisha kutomsikiliza Roho Mtakatifu. Musa alipoandika kitabu cha Mwanzo, hakuandika kuhusu utangamano (complexity) wa ulimwengu / uumbaji, DNA, n.k. Watu wa Mungu waliamini masimulizi ya uumbaji yaliyomo katika kitabu cha Mwanzo bila ya kuwa na elimu ya sasa ya sayansi. Mimi nafikiri tunaweza kuwa na uhakika kabisa kwamba Mungu wetu alijua kuhusu misingi yote ya sayansi lakini akaamua tu kusema kwamba Yeye ndiye aliyefanya uumbaji wote, na kwamba sisi tunapaswa kuamini kwamba hii ni kweli na kumtegemea Yeye, ingawa hatukuwapo wakati huo! Unafikiri wale watakatifu wa yale Maagano mawili, la Kale na Jipya, watakuwa na shauku kiasi gani ya kujua na kufuatilia mijadala ya leo ya jinsi sayansi inavyokubaliana au inavyopingana na masimulizi ya uumbaji yaliyomo katika kitabu cha Mwanzo [na vitabu vingine]? Mimi nafikiri watatabasamu tu na kutuuliza kwa nini tulitumia nguvu na wakati wetu kwa kiasi kikubwa namna hii katika shughuli isiyokuwa na faida kama hii. Kama tunahitaji mtu au kitu chochote kututhibitishia kwamba Neno la Mungu ni la kweli, basi hatutatembea kwa imani, na bila imani haiwezekani kumfurahisha Mungu – Waebr. 11:6. Sayansi inaweza (au la) kulithibitisha Neno la Mungu, lakini Neno la Mungu kamwe halina sharti la kuthibitishwa kwa namna yoyote ile na sayansi au maarifa yoyote yale ya kidunia. Ebu watizame tu hawa Mafarisayo wa sasa, yaani Wakatoliki wa Rumi na wale wa Othodoksi, na utaona pale mwanadamu anapotegemewa matokeo yake ni nini.

Neno la Mungu ni kamilifu na yakini, na mahitimisho (yaani mafundisho) yote yanayotokana na maandiko ni lazima yawe makamilifu na kwa namna yoyote ile yasiwe na mgongano na maandiko. Mambo, matukio na mafumbo yatokayo kwa Mungu, mara yakishaeleweka kutokana na uongozi wa Roho Mtakatifu, yanatufunulia zile sifa za Mungu, yanampa Mungu utukufu, na yanalazimu uwepo wa imani kwa upande wetu, lakini migongano haitokuwako. Kwa kuongezea, kama Mungu ameongea na mwanadamu katika Neno Lake, na kwa hakika hili ni kweli, basi [kwa hakika pia] Neno Lake hili litakuwa na maelekezo ya wazi na yasiyo na utata ya elimu inayohusiana na wokovu na kuishi kitakatifu. Yawezekanaje Mungu akawa na matakwa fulani juu yetu ikiwa [Yeye] hatuambii matakwa hayo ni yapi na jinsi ya kutambua njia inayoelekea kwenye matakwa hayo ni ipi? Bwana Yesu alisema kwamba Yeye aliongea na wale wasioamini kwa mafumbo, lakini kwa wateule wake hakufanya hivyo.

4.12 ili wakitazama watazame, wasione; Na wakisikia wasikie, wasielewe; Wasije wakaongoka, na kusamehewa.
Marko 4:12 SUV

Rejea pia Isaya 6:9 - Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione.

Kwa kuwa Yeye ndiye aliyetuumba na Yeye anatujua na kuifahamu mioyo yetu (1Sam. 16:7) na mipaka (upeo) ya uwezo wetu, tunaweza kuwa na uhakika kwamba anajua namna ya kuwasiliana na sisi watoto Wake. Kama Mungu ametupatia Neno Lake lililoandikwa kuhusiana, kwa mfano, na somo au kanuni fulani, basi atakuwa anatuita tulikubali somo au kanuni hiyo kwa imani kama fumbo la Mungu ambalo ufahamu wa maana yake umefungwa katika Mungu mwenyewe mwenye nafsi tatu, au anatuita ili “tuelewe” somo au kanuni hiyo kwa uweza wetu sisi wenyewe. [Kwa] vyoyote vile Mungu anapata utukufu. Kubishana na hili kutakuwa ni sawasawa na kudai kwamba hakuna jambo lolote [linalotokatoka kwa Mungu] ambalo tunapaswa kulipokea kwa imani, yaani bila kutumia mantiki ya kibinadamu, au kudai kwamba mambo yote [yanayotoka kwa Mungu] yako wazi kwa, au yanaweza kueleweka na, mantiki yetu ya kibinadamu.Vyovyote vile itakavyokuwa, Mungu hatapata utukufu anaostahili kama sisi tunasalimu amri tunapokabiliwa na msimamo na mtazamo wa ulimwengu huu [ambao tunajua unaongozwa na yule mwovu]. Mambo ya Mungu ni upumbavu kwa wale wanaoangamia, na si wale walio njiani kuelekea kwenye wokovu.

1.18  Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.
1Wakor. 1:18 SUV

Ujio wa pili wa Bwana wetu utakuwa kama [ujio wa] mwizi usiku kwa wale wasioamini, lakini [haitakuwa hivyo] kwetu sisi tulio katika mwanga.

5.2  Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku…
5.4  Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.
1Wathess. 5:2,4 SUV

Bali ni kubwa kiasi gani, lile fumbo la Mungu la amri na uchaguzi [wa wateule Wake], amri na uchaguzi unaotokana na ufalme / mamlaka Yake juu ya kila kitu na kila kiumbe. Mungu, akiwa na uhakika wa 100% aliamuru Bwana Yesu auwawe msalabani katika wakati (karne ya 1 A.D.) na mahala (Golgotha) palipopangwa Naye katika historia. Wayahidi na Warumi walimsulubu. Je, walikuwa na uamuzi (utashi) wowote katika jambo hili (tukio la kifo cha Bwana wetu)? Hapana, ilikwishaamriwa na Mungu kwamba tukio hili litatokea vile lilivyotokea. Je, Wayahudi na Warumi wale watawajibishwa kwa kitendo chao kile? Ndiyo, Mungu atawawajibisha wale wote waliohusika na ule uhalifu mkubwa kuliko uhalifu wowote ule katika historia.

2:23 Huyu mtu, akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu [kabla ya kuumbwa ulimwengu], ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimwua kwa kumgongomea msalabani.
Matendo 2:23 Biblia NEN (Kiswahili Contemporary Version)

Ni jambo lisilofaa kabisa kwa sisi kujaribu kutenganisha kudura ya Mungu (predestination) kutoka katika chanzo / sababu na matokeo (cause and effect). Kama Mungu aliamuru jambo fulani lifanyike hapa duniani mahala fulani na wakati fulani, basi Yeye ndiye chanzo / sababu ya tukio hilo. Kudura ya Mungu ni mchakato ambamo Mungu anaamuru yote yatakayotokea hapa duniani kabla hayajatokea, na siyo kwamba Mungu anangojea viumbe Wake, n.k., wafanye kitu fulani halafu Yeye ndiyo aamue “kujibu” matokeo ya matendo hayo ya viumbe Wake; wala siyo mchakato ambamo Mungu anategemea aina fulani ya “ufahamu” wa matukio kabla
hayajatokea ndipo Naye aamue kutoa “majibu” Yake. Vinginevyo, kanuni ya kudura inapoteza maana na umuhimu wake. Tunaweza kuikubali kanuni hii na maana yake katika maisha yetu kikamilifu kwa imani, lakini kamwe hatuwezi kuielewa kanuni hii kwa kuitumia mantiki ya akili zetu.

NB. Ndugu msomaji, chukua tahadhari hapa ili usijikanganye na aya kama Matendo 2:23! - R. K.

Robert van Kampen alipendekeza kwamba tunapojaribu kutatua tatizo la mwonekano wa mgongano katika Biblia (nasisitiza neno mwonekano hapa, kwani Biblia haina mgongano wowote) tunapaswa kufikiria na kuzingatia kila njia iliyo na maana ya wazi halafu tujaribu kutafuta maana inayofanana (common denominator) na hiyo katika hizo njia zote ambayo inaonekana au inaweza kuleta suluhu katika aya zote zinazohusu kanuni au somo fulani lenye huo mwonekano wa mgongano. Kama ile “maana inayofanana” itakuwa ndiyo sahihi, basi hii itakuwa na matokeo ya kutuweka katika njia iliyo sahihi katika kutafuta suluhu ya “mgongano” husika. Maandiko yanapaswa kueleweka katika “tafsiri yake sisisi” pale inapoonekana wazi kuwa hivyo, na aya zote “zinazotofautiana” ambazo zinalihusu suala moja zinapaswa kutazamwa. Kama aya fulani (z)inazungumzia jambo muhimu, “usi(z)ifunike chini ya zulia” hata kama ni aya pekee inayoonekana kugongana na uelewa wako. Soma na uone ni nani Mungu alikuwa anaongea naye na pia muktadha wa mazungumzo hayo. Wakati wote iache Biblia yenyewe iitafsiri Biblia kila inapowezekana. Kamwe isitokee tukaruhusu mawazo yetu binafsi au “masikio yetu yanayowasha” (2Tim. 4:3) yakaongoza tafsiri zetu za aya za Biblia. Kusiwe na kitu katika mioyo yetu au mtazamo wetu ambacho motisha / nia yake ni kumweka Mungu katika kizimba cha mshitakiwa mahakamani! Tukifanya hivyo, Yeye atatuacha aonekane “mwenye hatia” na huo ndio utakuwa mwisho wa utafiti wetu wa ile kweli! Mungu anaijua mioyo yetu na motisha za mioyo hiyo. Kama nia Yake ni sisi kuwa na busara ya kuyaelewa mafumbo Yake, atafanya hivyo, tena kwa furaha kuu atatuonyesha kweli zake.

Sasa, itakuwaje ikiwa baada ya utafiti, mafunzo, tafakuri na sala, mahitimisho yako yanakuwa kinyume na mafundisho ya kanisani kwako? Kama suala lolote lile linatokea na linahusu wokovu wako, basi suala hilo ni muhimu kuliko yote katika maisha yako, na unapaswa kuomba mwongozo kutoka kwa wale unaowaamini. Wako viongozi ambao wameitwa na wamewezeshwa na Mungu ili kulichunga kundi la kondoo Wake. Wape fursa ya kuondoa mkanganyiko wowote ambao unaweza kuwa nao. Lakini, kumbuka kwamba Mungu atakuwajibisha kwa yale uliyoyaamini kutokana na utashi wa moyo wako mwenyewe, siyo yale ambayo watu wengine wanayaona kuwa ni kweli. Kwa hakika ni jambo la busara kulinganisha matokeo ya mafundisho unayopata pamoja na utafiti wako mwenyewe, na yale ya wengine ambao umeona na kuamini kwamba Mungu amewapa karama ya kufundisha, lakini Mitume hawako tena na hakuna mtu au kikundi cha watu waliochukua nafasi ya Roho Mtakatifu kama kiongozi wetu katika kweli na kuishi kitakatifu. Ebu lifikirie hili kwa dakika moja: hivi ni jambo linalowezekana hata kwa mbaaali … kwamba Bwana wetu atafumbua mafumbo Yake kuhusiana na upendo Wake kwa watoto Wake kwa wana-teolojia, viongozi wa kanisa, makasisi au ma-papa wa Rumi pekee? Kwa hakika mtu mmoja inabidi ampe taarifa papa [wa Wakatoliki] kuwa Petro amekufa na kwamba Kanisa la Kristo halihusiani kwa vyovyote na sheria za urithi za ufalme wa Rumi! Kama tunayasikiliza tu yale tunayofundishwa bila kuyaamini, basi tunamwabudu mwanadamu na siyo Yule Mungu aliye katika Nafsi Tatu. Bwana anataka kujua sisi tunafikiri Yeye ni nani. Hatupati tija yoyote, na Yeye hajali kitu, kuhusi kile tulichokisikia au kile tunachokikariri na si tunachokiamini.

Mwisho wa waraka wangu.

Jibu #5:

Ni jambo jema kufahamiana na wewe. Kwa shauku kubwa ninakubaliana na karibu kila dondoo uliyoijadili hapa. Kwa hakika, sababu kuu ya kwa nini Ichthys iko katika internet na siyo “kanisa” lililojengwa kwa matofali na simenti mahala fulani ni kwamba aina hii ya utumishi (inayotaka kufundisha KWELI ya Biblia pekee) inaweza tu kufanyika kwa ufanisi ikiwa itafanyika “nje ya malango”. Ningependa kukueleza, na pia wewe mwenyewe unaweza kutaka kujua, kwamba kwa wakati huu kuna idadi kubwa tu ya wanaume ambao wamejitayarisha kwa bidii kwa ajili ya kutoa huduma ya kulifundisha Kanisa la Kristo hapa duniani lakini wanaume hao hawatumikii katika makanisa yaliyoko kwa sababu wamekuwa wakikutana na matatizo yanayofanana ambayo ni matokeo ya makanisa ya Kiinjilisti yaliyokuwa yakifuata utamaduni sahihi [sasa] kupoteza shauku waliyokuwa nayo ya kupenda kulifundisha na kulisikiliza Neno la Mungu – kwa sasa Neno la Mungu linatajwa-tajwa kwa mdomo tu, lakini halitiliwi mkazo, halipewi uangalifu linaostahili, halisikilizwi kwa makini, kwa heshima na kupewa nafasi ya juu kabisa katika Kanisa, mambo ambayo ni ya lazima ili kusanyiko la watakatifu wa Mungu liweze kukua kiroho.

Sehemu ndogo ambayo mimi ninatofautiana [kidogo] na wewe ni katika dondoo [yako] kuhusu elimu, na tofauti hii inaweza kuwa ni ya msisitizo zaidi kuliko ya msimamo wako halisi. Uko sahihi kabisa unaposema kwamba kuwa na shahada, stashahada, n.k., pamoja na aina mbalimbali za “elimu ya juu” hakuna maana ya kwamba Mungu anakupa “heshima” ya juu, na, kwa kweli kihistoria ni nadra kuwakuta wasomi wa aina hii wakiwa na imani sahihi katika Bwana Yesu Kristo na wanaoongozwa na Roho Mtakatifu; badala yake wengi wa watu hawa utawakuta katika makundi yanayotilia shaka uwepo wa Mungu, ingawa kwa ujumla wana upendo na wanadamu wenzao. Lakini kuna baadhi ya maeneo au nyanja za elimu ya juu ambazo zina faida kubwa tu katika kanisa la Kristo. Nimeona katika waraka wako huu, kwa mfano, kwamba unao msingi mahususi kabisa katika kuitafsiri na kuielewa Biblia, wa uwepo wa “migongano” katika maana za aya kadhaaa ndani ya Biblia, “migongano” ambayo kiuhalisia ni ya mwonekano wa nje tu, na inatokana na uelewa wa “juu-juu” wa mafundisho ya maandiko. Na pia umemnukuu msomi fulani (Robert van Kampen – R. K.) ambaye amefanya utafiti na uandishi katika somo hili. Siyo kwamba ninakukosoa, bali ninapenda tu kusisitiza kwamba hili ni jambo ambalo linapaswa kufundishwa kwa Wakristo, kwani “Mkristo wa kawaida” ni vigumu kuigundua kanuni hii (ya uwepo wa mwonekano wa “migongano” katika baadhi ya aya na maana zake katika Biblia) yeye mwenyewe katika kusoma kwake Biblia.
Tatizo lenyewe haliko katika matayarisho [ya utumishi katika Kanisa la Kristo], bali yako katika matumizi ya matayarisho hayo. Kama ambavyo ni kweli kwamba “bunduki haziui watu bali watu ndio wanaoua wenzao”, vivyo hivyo ni kweli kwamba shahada za Ph.D na Th.D hazipandikizi mbegu za mashaka kuhusu nguvu ya kweli ambayo ni Neno la Mungu, Biblia, ambayo ni dhahiri kwa yeyote aliye tayari kufungua macho yake na kuiona, lakini watu wenye shahada hizi ambao wanazitumia katika kulitafiti Neno la Mungu wanaweza kuigundua nguvu yake - au la (kama katika analojia ya bunduki, hapo juu).

Kwa maneno mengine, Biblia, kama ambavyo umeeleza kwa ufasaha, ina nguvu na ushawishi mkubwa, inatuwajibisha kulitafuta Neno la Mungu na kuliamini, tukimaizi kwa uangalifu yaliyo, na yasiyo kweli (katika yale tuliyofundishwa makanisani mwetu na walimu mbalimbali) chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Lakini ni wazi pia kwamba jukumu hili linahusisha Mkristo kujitafutia walimu wa Biblia wenye weledi, na pia kujisomea Biblia sisi wenyewe. Hakuna mashaka yoyote kwamba Biblia inafundisha kuwa pana ulazima wa kujisomea maandiko sisi wenyewe (tafadhali soma: Read your Bible: A Basic Christian Right and Responsibility). Lakini pia kuhusiana na ulazima wa kuwa na walimu wenye weledi katika kuifundisha Biblia pia hakuna shaka, kama ambavyo aya mahususi na pia historia yote ya watu wa Mungu inayosimuliwa katika Biblia hiyo hiyo inavyoweka wazi (kw. mf. 1Wakor. 12:28; Waefe. 4:11; 1Tim. 5:17).

Sasa, ikiwa mtu ana karama ya Roho Mtakatifu, kwa hakika hilo ndilo suala muhimu. Lakini je, mtu / mwalimu huyu hatafaidika kwa kujifunza, kwa mfano, Kiyunani, Kiebrania na Kiarami, na kujifunza lugha hizo kwa bidii ili awe na weledi, ili asitegemee kwa 100% watu ambao hawajui, waliotafsiri zile nakala lukuki za Biblia zilizoko mezani kwake? Nitakupa mfano; kila mara ninaposoma nakala yangu ya Kiyunani ya Agano Jipya, huwa nagundua taswira fulani [mpya] katika aya ninayosoma, hata kama taswira hiyo imejificha sana, ikiangazwa na maana ya aya hiyo kuonekana kwa udhahiri zaidi kwa sababu wakati huo ninaisoma Biblia katika moja kati ya lugha zake asilia. Na kwa upande wa pili wa “sarafu” hiyo, kila mara ninapoona au kusikia aya fulani ya Biblia ikitafsiriwa kimakosa na “walimu” fulani wenye nia njema tu, aghalabu hii inatokana na kutoelewa, au kuelewa kimakosa, kile maandiko yanachokisema kiuhalisia. Sasa, wakati mwingine hili ni suala la kutafsiri [tu], wakati mwingine ni suala la “teolojia pangilifu” yaani kwa kimombo “systematic theology” (Teolojia Pangilifu ni kutafsiri na kuona kile ambacho Biblia inakifundisha kuhusiana na somo / kanuni fulani, na baada ya hapo kutumia yale unayojifunza ili kufafanua au kufasili aya ambazo zina ugumu katika kuzielewa, zilizo katika sehemu nyingine za Biblia), wakati mwingine ni suala linalotokana na kutoyajua mazingira ya kihistoria ya wakati ule [wa kale] wa Agano la Kale na Jipya, na wakati mwingine ni – siku hizi ni mara nyingi (!) - ni pale mtu anapotafuta aya ambazo ‘zitaunga mkono’ mahubiri ya mchungaji ya Jumapili. Hili la mwisho, kwa mtazamo wangu, ndio mfano mzuri wa tatizo unalojaribu kulieleza hapa. Karne takriban mbili tu baada ya Mitume wa Kristo kuondoka – wa mwisho akiwa ni Yohana – ulianza mtindo wa wachungaji na waalimu wa Kanisa kutoa mahubiri, na hiki ndicho chanzo cha kupungua kwa ubora wa mafundisho ya Neno la Mungu kutoka kwa wachungaji na waalimu wa Biblia katika madhehebu. Kilichofuata hapo ni kwamba mahubiri hayo yalianza kuchukuliwa na madhehebu yaliyojitokeza kuwa ni mbadala wa mafundisho halisi ya Neno la Mungu, kwani mahubiri haya yalikuwa na maudhui finyu sana kutoka katika Biblia yenyewe na badala yake yakawa na wingi wa burudani, mbinu za kuchangisha fedha, n.k., hadi sasa tunaiona hali ya kusikitisha kabisa ambapo “wachungaji” na “walimu” wetu wanafundisha mbinu za “kufanikiwa kimaisha”, “kutajirika”, “kunena lugha”, “kutafsiri ndoto”, “uponyaji”, n.k., huku wakidai, bila aibu nyusoni mwao, kwamba hayo yote yanatoka katika Biblia, na yamekusudiwa kwa enzi hii ya sasa ya Kanisa! Sasa hivi, wanaohudhuria katika makanisa haya wanatarajia kupata mbinu za “kufanikiwa” katika ndoa, biashara, afya, siasa, ajira, burudani, n.k., badala ya kufundishwa Neno la Mungu (na hii ni sababu nyingine huduma hii yangu – Ichthys.com – inapatikana katika tovuti ya internet badala ya mjengoni, kwani watafutaji wa mafundisho halisi ya Neno kwa sasa ni wachache sana). “Ugonjwa” huu umeenea mpaka katika kile kinachoitwa “nyimbo za Injili” ambamo maudhui yake yamekuwa na uhaba mkubwa wa Injili yenyewe!

Kwa hali yoyote ile, makosa yote yaliyotajwa hapo juu yanahusiana kwa namna fulani na kile kinachoitwa “utovu wa elimu”. Hii inatoka, kwanza kabisa, katika ujinga juu ya kile ambacho Bwana wetu anakitaka kutoka kwetu ambacho ni kumjua vema zaidi na zaidi kwa njia ya kujifunza Neno lake na kisha kuitumia elimu hiyo, baada ya kuielewa na kuiamini, katika maisha yetu [ya Kikristo], na kuwasaidia wengine kufanya vivyo hivyo.

Hivyo basi, “uhaba huu wa elimu” unaweza kuwa au usiwe sawa na “uhaba wa shahada, stashahada, n.k.”. Ukweli ni kwamba, kwa upande mmoja kujielimisha wewe mwenyewe katika suala la nini Bwana anakitaka kutoka kwetu kunahitaji, kwanza kabisa, moyo unaoitikia [wito wa Bwana] zaidi ya mafunzo ya kitaaluma, na kwa upande mwingine, inawezekana kujifundisha wewe mwenyewe katika maeneo yote yaliyojadiliwa hapo juu bila ya kupitia mafunzo rasmi (ingawa hili ni gumu sana, haswa katika eneo la mafunzo ya lugha [za kale zilizotumika katika kuandika Biblia], na mimi mwenyewe ninaweza kukuhakikishia hili). Zaidi ya hapo, inawezekana kabisa kufanikiwa kupata “shahada”, “stashahada”, n.k., za idadi yoyote ile siku hizi bila ya kupata elimu halisi yenye faida yoyote ile, na, wakati mwingine badala yake ukajazwa kasumba ya mambo ambayo yana madhara (ikiwa ‘mwanafunzi’ husika anayaamini mambo anayofundishwa). Hata hivyo, kwa mara nyingine tena, kama ilivyokuwa katika mfano wa bunduki na mwuaji, kosa litakuwa kwa mtumiaji wa bunduki na siyo bunduki yenyewe. Kwa sababu tu baadhi, au wengi kati ya, au hata karibu wote, ambao siku hizi wanapita barabara ndefu na ngumu ya kusoma ili wapate utambuzi rasmi kutoka vyuo mbalimbali wanaweza kufanya hivyo kutokana na motisha zisizo sahihi au safi, na, licha ya juhudi yote hiyo, wakapata matokeo yasiyoridhisha, haimaanishi kwamba kila mtu ambaye kwa moyo wake wote amejitoa katika kujitayarisha ili amtumikie Bwana Yesu Kristo atakuwa na matokeo hayo hayo.

Kwa kumalizia, siyo kiasi cha matayarisho au aina ya masomo ambayo mtu anajitayarisha nayo ambayo ndiyo tatizo hapa, bali ni moyo wa mtu anayetamka kwamba yeye ni mwalimu wa Neno la Mungu wakati malengo yake ni mengine kabisa. Hivyo, ingawa ninakubaliana na wewe kwamba “mfumo wa elimu” umeharibu mambo mpaka kufikia mahala ambapo kiasi cha masomo na aina ya masomo havina tofauti au maana yoyote, mimi nafikiri kwamba huduma yangu hii (https://ichthys.com) na huduma nyingine ninazozifahamu na ninazoweza kushuhudia ubora wake zinathibitisha kwamba si sahihi kutamka bila kuchunguza kwa undani kabisa kwamba matayarisho [ya kutosha] kwa njia ya masomo / mafundisho rasmi (yaani katika chuo fulani) yanamaanisha kwamba mhusika hana motisha ya kutosha [ya utumishi], ana imani potofu, ana uvuguvugu wa imani, au ana woga wa kiroho. Kwa mfano, nina uhakika na ninafahamu kwamba hakuna hata dhehebu moja hapa duniani ambalo linakubaliana 100% na mafundisho yote yanayopatikana katika ichthys.com. Kuna sababu mahususi nimeifanya https://ichthys.com kuwa huduma huru kabisa. Mafundisho yake hayafungamani na upande wowote. Mitazamo na misimamo yake yote kuhusu Biblia inafundisha nini na kanuni zote zinazofundishwa katika tovuti hii, inatokana na uelewa wangu wa kile kinachofundishwa na Biblia kiuhalisia, na hii imetokana na kujifunza Biblia kwa muda mrefu na kuitafakari kwa uangalifu katika sala. Kwa mfano, kuhusiana na kanuni au fundisho lisilo sahihi la “unyakuo kabla ya Dhiki Kuu” au “pre-Tribulation Rapture”, hata mimi nilijazwa ‘kasumba’ ya kuliamini fundisho hili hapo zamani, na wakati huo nilikuwa nalitetea kwa nguvu zangu zote mpaka pale maandiko yaliponionyesha bila mgongano kwamba fundisho lenyewe ni la kutunga tu na linatokana na uelewa wa Biblia usio sahihi. Mara baada ya kujihakikishia mwenyewe juu ya ukweli unaofundishwa na aya husika, sikusita kubadilisha mafundisho yangu kuhusiana na ni wakati gani unyakuo utatukia. Hii imekuwa ni kawaida kwangu, na nina matumaini kwamba itaendelea kuwa hivyo siku za usoni. Ninachokitaka ni ukweli, siyo mapokeo wala makubaliano yanyouweka ukweli kikapuni na kuufunika – na huduma yangu hii nimeiweka wakfu kwa ajili ya Wakristo wote wenye mawazo na msimamo kama huu. Msimamo na mtazamo huu umenigharimu mimi binafsi; katika mahusiano yangu na watu wa karibu kumetokea mvutano na shinikizo, na kama nilivyosema, umekuwa na matokeo ya kunifanya nitengwe na wale niliokuwa na maelewano mazuri nao kabla, haswa wale ambao ni wafuasi wa madhehebu na taasisi za Kikristo. Siweki kinyongo dhidi ya mtu yeyote, lakini nimedhamiria kuufuata ukweli popote pale utakaponiongoza, kumfuata Bwana Yesu Kristo popote pale Atakaponipeleka, kwa gharama yoyote ile.

Ninaamini kwamba unauona msingi huu ukidhihirika katika kila kitu unachokisoma hapa Ichthys.com.

Katika Yeye ambaye ni Neno la Mungu aliyekuwa mwili, mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo,

Bob L.

Swali #6:

Ndugu yangu Robert,

Nataka nikushukuru sana kwa majibu yako ya upole, wema na yaliyofikiriwa kwa undani kabisa. Siku zote mimi nimekuwa nikisema kwamba Mkristo mwenye umuhimu na maana kubwa ambaye tutakutana naye katika maisha yetu ni yule aliye mbele yetu, uso kwa uso na sisi. Baada ya kusema hayo, nina shaka kama majibu yako yangekuwa ya kufikiriwa kwa kina namna ile kama ungekuwa unamjibu MacArthur na siyo mimi, mtu asiye na umaarufu wowote. Nakushukuru sana kwa kunipa sifa hii, kwamba unakubaliana na sehemu kubwa ya yale niliyojifunza katika Biblia na ninayoyaamini mimi. Pia nimefurahia [sana] na nitaiweka moyoni mwangu ile sehemu ya barua-pepe yako ambapo umetofautiana na mimi kidogo kuhusu elimu. Huwa nina katabia ka kuusema mtazamo wangu kwa nguvu kidogo, na hili huenda linasababisha ‘kupindisha’ kidogo mawazo na nia yangu, pale ninapoandika au kuongea. Kwa kweli ninajua kwamba elimu, ya kidunia na ya kiteolojia haina madhara yoyote, na kwa kweli ina faida kubwa kwa Mkristo. Kitu ninachokiona kuwa siyo sahihi ni pale watu wenye elimu ya juu wanapojiona kuwa elimu yao inawafanya wao kuwa ni vyombo bora zaidi [katika] kujifunza Neno la Mungu na katika kumtumikia, kwamba elimu tu inatosha. Kwa maneno mengine, ikiwa unayo shahada ya udakitari (wa falsafa kwa mfano), hautakuwa sahihi ukidhani kwamba shahada hiyo (yaani elimu iliyomo ndani yako) pekee, inakufanya uwe mtu wa kiroho zaidi ya wengine, au mtu mwenye uwezo wa kuendelea kiroho zaidi ya wengine. Ile karatasi ya shahada haina maana yoyote, bali mtu mwenye hiyo karatasi ndiye muhimu kabisa. Kushindwa kulielewa hili ndiko kumesababisha uwepo wa Ukatoliki wa Rumi ambao unampa umuhimu mtu badala Mungu, na sasa wengi kati ya “ndugu” zetu Waprotestanti nao wamejiundia “Uprotestanti wa Kirumi” wa kwao wenyewe! Ni uwongo ule ule, kama lile “fundisho” linaloitwa “Mtazamo Mpya juu ya Paulo” - “The New Perspective on Paul” - lakini wenyewe umejificha zaidi, hivyo inahitajika tahadhari. Mimi ninajua kwamba wewe unakubaliana nami katika hili, hivyo hakuna haja ya kulijadili upya hapa. Kinachoamua kiasi cha kweli ya kiroho ambacho mtu anafunuliwa ni namna Mungu anavyoutazama moyo wake na dhamiri yake [mtu huyo]. Nilifikiri nimeliweka hili wazi nilipoandika kuhusu jinsi kulivyo na wanaume waliochaguliwa na Mungu kwa ajili ya kufundisha na kuhubiri. Hoja yangu haikueekezwa kwa wanazuoni peke yao, bali haswa kwa wale wanaoweka hatma yao ya kiroho katika mikono ya wanazuoni hao kwa sababu tu wao ni wanazuoni. Mimi ninawashutumu tu wale wanazuoni ambao wanapofikia mahala fulani katika utumishi wao, wanaamua na kuanza kumtumikia mtu badala ya kumtumikia Mungu. Kiukweli, van Kampen hakuwa mwanazuoni. Yeye alikuwa mfanyabiashara tajiri na mwenye mafanikio makubwa katika biashara zake na ambaye aliamua, kama nilivyoamua mimi, kwamba Neno la Mungu ndilo linalozifungua kweli za Mungu, na Neno Lake linapatikana kwa kila mtu.

“Nanyi mtanitafuta na mtaniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote”
Yer. 29:13.

Pia aliamini, kama ninavyoamini mimi, kwamba kanuni nyingi zenye kina kutoka katika Neno la Mungu zinaweza kufundishwa na kueleweka ikiwa shauku yetu ni kupata busara kwa “lengo pekee la kumfahamu na kumjua Mungu”. Van Kampen aliunga mkono msimamo wangu, na mimi nilivyomnukuu inaonyesha kwamba hakuna mgongano kati yetu. Yeye alitafiti mawazo na mitazamo ya wanazuoni kuhusiana na kila taswira ya mtazamo wake [juu ya kanuni fulani], kisha akalinganisha mitazamo ya wanazuoni hao na maandiko. Hitimisho la mchakato wake huu ziku zote lilitoka katika maandiko, na kama mtazamo wake uliungwa mkono na wanazuoni hao aliokuwa akiwatafiti, hili lilitia nguvu tu, na sio kuamua msimamo wake. Yeye hakuwa na tabia ya kusema kwamba mtu analazimika kukubaliana naye kwa sababu tu bwana MacArthur anakubaliana naye. Nina matumaini kwamba haya niliyoyasema hapa yanaleta maana.

Ninamshukuru sana Mungu kwa sababu Amenikutanisha na wewe; nitakuweka katika sala zangu. Kuna tofauti kati ya kweli zilizofunuliwa na Mungu [kwetu] ambazo sote tutawajibishwa kwa kujifunza na kuzifahamu, na yale mambo ya siri ya Mungu ambayo mimi na wewe tunapenda kuyajadili. Mimi ninaamini kwamba Mungu wetu anafurahi sana pale watoto Wake wanapojipa jukumu la kuyajua na kuyaelewa hata haya mambo ya siri Zake, ambayo kwa kiasi fulani yataendelea kuwa siri. – Kumb. 29:29.

Mimi ndugu yako katika Kristo.

Jibu #6:

Asante sana kwa barua pepe yako yenye maneno yenye ukarimu. Naomba radhi kama nili-’overreact’katika majibu yangu kutokana na maelezo yako [ya nguvu] ya mtazamo wako. Kwa mara nyingine tena, ninakubaliana na mengi kati ya yale unayoyasema hapa. Hapo awali nilifikiria na nilitaka kuachana kabisa na matayarisho rasmi [kwa ajili ya utumishi wangu] katika chuo fulani, yaani nilitaka kujifunza mwenyewe ili baadaye nifundishe Neno la Mungu. Pamoja na hoja zinazotajwa katika barua pepe iliyopita (swali na jibu #5) na ushauri mzuri sana nilioupokea (kwa mfano, maoni ya L. S. Chafer kwamba miaka 10 ya kujitayarisha [kwa jili ya utumishi] ikifuatiwa na mwaka mmoja tu wa utumishi wenyewe si kitu kibaya ikiwa mhusika ana nia ya dhati ya kufanya kazi nzuri kwa ajili ya Kanisa), moja kati ya vipengele vilivyonisukuma kuelekea katika kuamua nifuate njia rasmi ya matayarisho yangu ya utumishi ilikuwa ni utambuzi wangu wa upande wa pili wa kile unachokisema hapa, yaani, kwa watu wengi [nitakaowafundisha baadaye] upungufu wa shahada katika masomo husika ungekuwa kikwazo. Na wakati ninayaona mapungufu katika hoja inayodai kwamba mtu mwenye shahada na vyeti vingine ni chombo bora zaidi (au chombo sahihi kwa sababu ya kuwa na vyeti hivyo), kwa upande wangu niliona si vibaya kuuliza kwa nini mtu ambaye anafikiri na anaamini kwamba kujifunza na kufundisha Neno la Mungu ni jambo muhimu kuliko mambo yote ulimwenguni hataenda kujifunza katika seminari au atashindwa kujitafutia shahada ya juu katika masomo yatakayomsaidia / yatakayomwezesha katika kufundisha. Kuna majibu mengi kwa suala / swali hili, lakini kwa kuwa mimi binafsi sikuwa na jibu hata moja, nilihisi, na niliamua kufanya matayarisho rasmi ya kiroho vyuoni.

Mtazamo na uamuzi wangu huu umeniletea faida kubwa sana katika miaka hii yote iliyofuata, na mojawapo kati ya faida hizi ni ile ya kunipa nafasi ya kutathmini, kukataa na kutupilia mbali, bila ya kuwa na hisia za hatia (guilt), kazi zozote za wanazuoni wenzangu ambao wamekosea na kupoteza maana halisi ya kile kilichosemwa ndani ya Neno la Mungu. Kwa kweli kuna kazi chache sana sana za wanazuoni katika teolojia na chache zaidi ya hizo katika kazi zinazofanana, zinazofasili Biblia ambazo zimekuwa na faida yoyote kwangu baada ya uanzilishi wa utumishi wangu katika tovuti hii yangu. Sababu moja kubwa ya hali hii, ninavyoona mimi, ni kwamba katika mijadala na jumuiya ya wanazuoni na wachapishaji, ukiwa na mtazamo na msimamo wa kuupenda na kuutamka ukweli halisi wa Neno la Mungu, basi utapingwa na watajaribu kukuzuia kufanya hivyo. Mimi sijali kilichosemwa na wafasili wengine 100 au 1,000 kuhusu sura fulani ya Biblia, bali ninajali kile kinachosemwa na sura yenyewe. Siyo kwamba ninawapuuza hao 100 au 1,000. Ni kwamba jinsi miaka inavyopita, msaada wa mafundisho wanaoutoa (mafundisho ambayo naweza kusema yametiwa maji!) umekuwa hauna faida (ingawa kuna baadhi ya mafundisho mazuri sana: “Commentary on the old Testament” ya Unger ni kazi yenye umaizi mkubwa, kwa mfano). Hii ni sababu mojawapo katika kazi zangu kuna nukuu chache sana za kazi za watu wengine. Kwa ujumla, kuna fursa chache sana za kuweka nukuu za watu wengine katika mafundisho yangu (ingawa na mimi nina mizizi na asili yangu ambayo huwa naitaja kwa wazi kabisa, pia mimi hunukuu majina ya walimu walionifundisha katika miaka ile ya kuanza kukua kiroho na baadaye, ambao nilifaidika na mafundisho yao – mimea yote inatokana na mbegu zilizopandwa). Nakubaliana na wewe kabisa kwamba mamlaka ya kufundisha yamo katika Biblia yenyewe, na inampasa mwalimu wa Biblia kufundisha kile kinachosemwa na Biblia yenyewe na si vinginevyo. Siku zote mipango yangu mimi ni kujaribu kudhihirisha kutoka katika fasiri mbalimbali za Biblia, aya zinazofanana, teolojia pangilifu, na kwa kutoa hoja za kweli, kwa nini ninakiamini kile ninachokifundisha kuhusiana na aya na dondoo / dhana fulani – yaani mimi nafundisha kanuni fulani kwa sababu ninaamini Biblia inaifundisha kanuni hiyo, nami nitajaribu, kwa uwazi kabisa kufafanua ni sehemu gani ya Biblia na kwa nini na kwa namna gani Biblia inafundisha kanuni hiyo.

Kwa hakika mimi nataka kujua kila kitu kilimo katika Biblia, kukiamini kwamba ni kweli na kukifundisha kwa wote walio tayari kufundishwa [na mimi], kwani kila sehemu ya ile kweli ni muhimu, ikiunganisha, ikifanya kama mhimili, ikitia uhai, kwa Neno zima/lote. Niwie radhi kwa sababu wakati mwingine maelezo yangu na istilahi ninayotumia ni “ya kitaaluma” zaidi. Kama ningelikuwa mwandishi mzuri zaidi [kuliko nilivyo], ningeweza kuyafanya mafundisho yangu haya yasiwe “mazito” sana lakini yenye ufanisi ule ule katika kueleweka. Lakini Mungu mwenyewe aliamua kutupatia sisi Wakristo wote karama tofauti, na hatuwezi kubishana Naye kwani Yeye ana busara isiyo kifani.

Mwisho, wewe na mimi sote ni watu tusiojulikana wala kuwa na umaarufu wowote, na hili si jambo baya kwa sisi Wakristo, tukifanya kazi katika shamba la mizabibu katika nafasi tuliyopangiwa na Bwana. Kwa hakika ni pale tunapokuwa na umaarufu fulani katika macho ya ulimwengu ndipo mambo ya hatari yanaanza kutokea.

Nakushukuru kwa yote, haswa kwa sala zako!

Katika Bwana Yesu,

Bob L.

https://ichthys.com

Basi na Tuonane katika Sehemu ya IV ya Mfululizo Huu, kwa Utukufu wa Bwana Wetu!

R. Kilambo
Wa https://sayuni.co.tz