Ufafanuzi (au Fasiri) wa Biblia sehemu ya II

Ifuatayo ni sehemu ya pili katika mfululizo wa mafundisho ya ufafanuzi wa aya za Biblia. Mfululizo huu utahusisha maswali na majibu ambayo wasomaji (au wanafunzi wa Biblia) wa tovuti ya https://ichthys.com ya Dr., Professor, Pastor-Teacher Robert D. Luginbill walimwuliza katika nyakati mbalimbali. Nilimwomba Dakta Luginbill ruksa ya kutafsiri maswali & majibu haya kwa faida ya wanafunzi wa Biblia wanaozungumza lugha ya Kiswahili; Dakta alinipatia ruksa hii na haya hapa chini [na sehemu zinazofuata, na iliyotangulia] ndiyo matokeo ya kazi hii.

Ndugu Mkristo, nakukaribisha ili uweze kufaidika [kiroho] na mafundisho ya Neno la Mungu yaliyomo katika mfululizo huu.

Fasiri ya mfululizo mzima na Respicius Luciani Kilambo wa https://sayuni.co.tz

Sehemu ya II: Je, tunawezaje kujua ni TAFSIRI / FASIRI (Version) ipi ya Biblia ndiyo sahihi (Part 2)?

Kutoka: Mail-Bible_Interpretation_2: How Can we Know Whose Interpretation of the Bible is Right (Part 2)?

Na Dr. Robert D. Luginbill wa https://ichthys.com
Septemba 18, 2004.

Swali:

Nashukuru sana kwa kunijibu. Mimi ni mtu ninayependa kujadili masuala ya dini na siasa (siyo kwa malengo ya mabishano tu, bali kuongeza ufahamu, n.k.), na kwa kweli nimekwishawahi kuandika maswali mbalimbali na kuyatuma kwa tovuti kadhaa, ikiwa ni pamoja na tovuti za jamii za Waisilamu (ingawa hakuna hata mmoja wao aliyejisumbua kunijibu). Ninataka kusema kwanza [kwamba] ninao marafiki kadhaa ambao ni Wakristo wenye msimamo wa “imani pekee [ndiyo inayookoa – Waefeso 2:8-9]” au katika Kilatini, “sola fide”; wawili kati yao ni wahudhuriaji wa Kanisa la Anglikana, mmoja wao ni Msabato, na mwingine ni Mpentekoste (Karismatiki). Wote hao wanasema kwamba msingi wa imani yao siyo ‘mamlaka ya Kanisa [lao]’ bali ni mamlaka ya Biblia, lakini namna zao za kuabudu ni tofauti kabisa! Hata sisi Waothodoksi pamoja na Wakatoliki [wa Roma], msingi wa imani yetu ni Biblia … ndiyo maana tunanukuu maandiko kama kitabu cha Yakobo (“imani bila matendo ni bure … n.k.”). Na kumtukuza Maria – veneration of Mary - (jambo ambalo rafiki zangu hawa niliowataja hapo juu wanalipinga kabisa na ndicho kikwazo chao kikubwa dhidi ya dini ya Othodoksi – tazama katika Luka pale malaika Gabrieli anaposema “umebarikiwa wewe katika wanawake” na pia pale Maria anaposema atabarikiwa katika enzi zote). Hivyo basi hapo hakuna anayekubali kushindwa! Watu wote hao wameweka Biblia kuwa ni msingi wa imani yao, wote wanasali kwa Mungu, lakini wote wako tofauti kabisa. Wewe umesema kwamba “unaposoma zaidi na unapokuwa na mazoea zaidi na maandiko basi matokeo yake ni mfumuko wa tafsiri”. Mimi sijaona ushahidi wa jambo hili katika mitazamo ya wale rafiki zangu [niliowataja hapo juu] ingawa wote hao ni wenye msimamo wa ‘sola fide’, na wote wanajifunza Biblia wakati wote. Mmoja kati ya wale marafiki Waanglikana alikuwa kiongozi wa Chama cha Wanafunzi Wainjilisti wakati tulipokuwa chuoni. Yule rafiki yangu mwingine Muanglikana siku zote anamwuliza maswali [Muanglikana mwenzake] ambaye amesoma katika chuo cha teolojia ili kuhakiki masomo yake ya Biblia, na pia wakati wa mijadala, lakini hata hawa wawili wanatofautiana (haswa katika mitazamo yao kuhusu suala la ushoga). Wakristo wengine wanashiriki katika ‘matamko ya kiimani’ kama ile “nasadiki” au “credo” ya Wakatoliki (the Nicene creed) – ambayo mimi nafahamu kuwa ilikuwako hata kabla ya Biblia kuandikwa. Wengine wameandika “credo” zao wenyewe. Hivyo basi, hata hao Wakristo wenye msimamo wa “Biblia pekee” wana mitizamo mingine ambayo siyo ya Kibiblia (Nafikiri msemo wa kiteolojia katika Kilatini ni “sola scriptura”, nimesahau kidogo). Nafikiri kwamba Kristo aliunda Kanisa. Halafu Kanisa likaiunda Biblia. Hivyo mimi namheshimu kwanza Kristo, halafu pili ni Kanisa. Mimi ninaridhika kabisa katika ufuasi wangu wa itikadi / kanuni za kanisa [langu], kwa sababu lilisimikwa na Kristo. Wale ambao walimjua Kristo waliandika vitabu kama Didache ambacho kinaizungumzia Ekaristi. Watu wengine pia waliandika kabla ya Biblia, watu kama Klementi wa Rumi ambaye kama sikosei alifariki mwaka 115 A.D. Klementi aliandika kuhusu kufanya “matendo mema”. Kuwadharau waandishi hawa ni sawa na kuidharau historia ya Kanisa. Na, waandishi hawa siku zote wamekuwa wakiheshimiwa sana (ingawa kuna kiasi fulani cha mashaka kuhusiana na Didache ambayo kwa muda mrefu ilikuwa imepotea), lakini waandishi wengine kama Athanasius, Ignatius wa Antiokia, Klementi wa Alekzandria, Diognetusi, Justin the Martyr, wamekuwa wakiheshimiwa kwa muda mrefu sana sana. Mimi naamini kwamba Martin Luther alijaribu kufuta miaka 1500 ya mwanzo ya historia ya Ukristo kwa kusema “sikilizeni nyie marafiki – mmekuwa mkikosea miaka hii yote!” Yeye alikuwa mwanadamu tu na hivyo Kanisa lake liliundwa na wanadamu. Kama vile kanisa la Waanglikana, kanisa la Methodisti, na lile la Presibiteri. Jirani na mahala ninapoishi pana kanisa linalojiita ‘Four Square Gospel Church’ (sijui hata hii ina maana gani)! Halafu kuna makanisa yenye majina mazuri kabisa, kama ‘Church of God’, ‘Assemblies of God’, n.k. Ninavyoona mimi ni kwamba ikiwa hawa watu wote wanaisoma na kujifunza Biblia, basi wanapaswa kuwa wamoja. Rafiki yangu aliyeko Ulaya (mimi niko US) ananiambia kwamba hao wote ni wamoja kwa sababu wote wanamwabudu Kristo. Lakini kama hii ni kweli, kwamba wote wanamwabudu Kristo, basi kungekuwa na Kanisa moja tu. Sisi Waothodoksi wote tuna Liturujia moja tu, ingawa kuna Othodoksi ya Ugiriki, Urusi, Siria, n.k.; huu ni mgawanyiko wa kiutawala tu, wakati ndani ya Kanisa la Anglikana, Liturujia inatofautiana baina ya makundi ya maeneo mbalimbali ya Kanisa hilo – wengine wakivunja mkate halisi, wengine Ekaristi, wengine wakiawapangia Walei (waumini wasio na daraja la ukasisi) kutoa sakramenti, wengine hapana. Mimi nakushukuru sana kwa kuniandikia na kunijibu swali langu. *Dh’eirich Criosda (maana yake Christo amefufuka)!

*Hii ni lugha ya Gaelic inayozungumzwa huko Scotland, UK.

Jibu:

Kama umeridhika na msimamo wako, basi kiuhalisia hakuna mambo mengi ninayoweza kuyasema kwako. Katika utumishi wangu huu wa hapa https://ichthys.com nimejitolea kwa dhati katika kuwasaidia wale wanaotaka kukua kiroho kwa njia ya Biblia waweze kufanya hivyo. Kwa mtazamo wangu, ambao nimeufikiria na kuutafakari kwa muda mrefu, hii ndiyo njia pekee ya kusogea karibu ya Bwana wetu Yesu Kristo, yaani kwa “kula” chakula cha Neno la Mungu, kumwacha Mungu atubadilishe kutoka ndani ya mioyo yetu, na kuyaishi yale tunayojifunza na kuyaamini kutoka katika Biblia kwa kuwa wanafunzi na wafuasi waaminifu wa Bwana wetu.

Mimi sina nia ya kulichambua na kulishambulia kanisa lako, lakini ni jambo jema ikiwa utaona kwamba baadhi ya hoja zako dhidi ya Biblia zinafaa kutumiwa dhidi ya kanisa lako wewe mwenyewe na mamlaka ya kanisa hilo unayoyategemea. Umesema kwamba Bwana Yesu aliunda na kulisimika Kanisa; hii ni kweli kabisa, lakini tatizo ninaloliona hapa mimi ni kwamba wewe unafikiri Kanisa alilosimika Bwana Yesu ni sawasawa (au ni lilelile) na taasisi ya kibinadamu ambayo wewe ni mwanachama na mfuasi wake! Kwa hakika Kanisa la kweli linajumuisha wale wote waliomwamini na wanaomwamini Bwana Yesu Kristo na kumfuata, siyo dhehebu fulani (Yoh. 3:16). Adamu na Eva, ambao walikuwa wanadamu wa kwanza kuamini, wengine wote waliofuata hadi mtu wa mwisho kuamini kabla ya ujio wa pili wa Bwana wetu, wote hao ndio sehemu ya “kusanyiko” la Bwana wetu (“kusanyiko” ndiyo tafsiri na maana ya neno la Kiyunani ekklesia ambalo kwa kawaida hutafsiriwa kama “kanisa” katika Kiswahili).

Ni kanisa gani (la kidunia) ambalo Bwana Yesu aliliunda na kulisimika? Makanisa ya Othodoksi na Katoliki la Roma (na Koptiki na lile la Siria na la Nestori) hayafanani na yale [Makanisa ya Msingi – Local Churches] tunayoyaona katika kitabu cha Matendo ya Mitume, wala yale tunayoyaona katika karne ya pili hadi ya nne. Hata kama unataka kusema hii si kweli, basi niambie ipi kati ya taasisi hizi “ndilo Kanisa” alilolisimika Bwana Yesu, kwani yote hayo yanatofautiana katika dondoo nyingi kama wewe mwenyewe ulivyosimulia kuhusiana na madhehebu yaliyoundwa baadaye [na wanadamu].

Pia unasema kwamba Bwana Yesu aliunda “kanisa”, na kanisa hilo likaiandika Biblia. Kwa hakika, ni vigumu sana kuipata sura ambamo Bwana Yesu anafundisha bila kunukuu Biblia. Vilevile ni vigumu sana kuyaona mafundisho yoyote katika Agano la Kale ambayo hayarudiwi katika Agano Jipya (hata kama ni katika msemo -phraseology – tofauti), kwanza katika zile Injili nne, na pili katika zile Barua za Mitume. Pale Bwana Yesu anapoona umuhimu wa kurejea (anapofanya “reference”) mamlaka fulani, basi anaitumia Biblia. Kwa hiyo maandiko (Biblia) yalikuwako zaidi ya miaka 1,000 kabla ya madhehebu yote yanayotajwa hapa.

Ni kuidanganya nafsi [yako mwenyewe] unaposema kwamba kwa sababu taasisi na makundi mbalimbali yanadai kuwa msingi wa ‘kanuni’ zao ni Biblia na wakati huo huo kila kundi linafundisha kanuni zinazotofautiana basi [eti] Biblia ina mapungufu fulani. Nilikwishakukueleza katika sehemu ya I kwamba Biblia ndiyo yenye mamlaka, na siyo taasisi wala kundi – dhehebu – fulani, iwe ‘kanisa’ au kundi lolote lile.

Si lazima kwamba kundi (au taasisi) fulani (iwe Othodoksi, n.k.) linaposema kwamba aya fulani inamaanisha a, b, c, basi ni hivyo – kwa sababu mtazamo huu utakuwa unalipa mamlaka kundi hilo, na siyo Biblia. Biblia ina maana yake katika yote inayoyatamka. Ukweli kwamba ni watu wachache sana katika historia ya enzi hii katika mpango wa Mungu waliojisumbua kufanya kazi ngumu ya kujifunza lugha za [kale] za Biblia, teolojia ya Biblia, historia ya Biblia, wakifanya utafiti wa ndani kabisa na kupekua uhusiano wa kanuni zote zinazofundishwa [kila kanuni moja na mwenzake], wakiutumia muda wao katika kutafuta maana halisi ya mafundisho yake, haumaanishi kwamba Biblia ina makosa, kwamba Biblia haina usahihi, kwamba mamlaka ya Biblia yamepungua. Watu wote ambao wewe unadai wameiunda Biblia wamekwishakufa; hivyo basi katika kanisa lako au katika kanisa lolote lile hakuna kitu chenye mamlaka kilichobakia isipokuwa 1) Biblia (ambayo mamlaka yake madhehebu karibu yote ya kale yanayakataa), au 2) taasisi au dhehebu hilo la kale ambalo sheria na tafsiri zake [za Biblia] zimetungwa tu na viongozi wake – wa kale na wa sasa – kwa sababu zao wenyewe (katika karne hizi zote tangu madhehebu hayo yaasisiwe).

Hoja unayoitoa hapa ni ya kawaida sana, na inaonekana kuwafariji wale wote ambao hawataki kujisumbua kutimiza majukumu magumu yanayotokana na imani halisi [kwa Kristo] inayookoa. Liturujia inatia faraja na ni rahisi sana kwani ni marudio-rudio tu ya maneno na matendo yaliyokaririwa. Kusoma Biblia na kujifunza Biblia kwa usahihi kunalazimu mtu ajitoe kikwelikweli, autumie muda wake vizuri akiacha mambo mengi mengine [ya kujistarehesha], na pia kuna gharama za hisia zetu za moyoni – kwa sababu tunapaswa kuwa tayari kubadilisha mawazo na imani zetu za miaka mingi pale kweli ya Biblia inapoelekeza wazi kwamba tunapaswa kufanya hivyo. Laki Mungu atakuongoza na kukupeleka – kwa njia ya Neno Lake na kwa Roho Wake Mtakatifu – mahala pema anapotaka Yeye kukupeleka, ikiwa tu uko tayari kuongozwa Naye.

Mimi siyo Mkarismatiki, siyo Msabato, siyo Mkatoliki. Ukweli ni kwamba madhehebu yote [makubwa na ya kale] yamekwishaweka misimamo yao kuhusiana na kanuni zao, na hawana mpango wa kubadilika. Katika madhehebu fulani ya kale ya Kiprotestanti, kwa mfano, tunaona kwamba walianza vizuri, lakini hawakuendeleza juhudi njema za waasisi wao – cf. Kalvini, Luther, n.k. Katika madhehebu mengine yaliyoanzishwa kabla ya yale ya Kiprotestanti, tunaona uharibifu na upotevu wa ile kweli unaotokana na kufuata mapokeo kufikia kiasi kwamba mamlaka ya Biblia yanapingwa kabisa, tena bila soni wala aibu yoyote, kama tunavyoona kwako wewe (na hili ni jambo la kusikitisha sana).

Nina uhakika kwa kiasi kikubwa tu kwamba wewe hujaonana uso kwa uso na Bwana wetu. Pia nina uhakika kwa kiasi kikubwa tu kwamba hakuna hata mtu mmoja katika dhehebu au kanisa lako ambaye ameonana uso kwa uso na Bwana wetu [na kuongea naye]. Ni kwa namna gani basi unaweza kujua jambo lolote kumhusu Bwana wetu, kuhusu yale Anayoyataka wewe uyafanye, kama siyo kwa kutumia chanzo cha kweli pekee ambacho Bwana wetu ametupatia, yaani Biblia? Hakuna hata mtu mmoja katika Israeli ile ya kale, karne nyingi kabla ya Masihi kuja, ambaye alikuwa na shaka yoyote kwamba vile vitabu vitano vya Musa (Pentateuch) vilikuwa ni Neno la Mungu (kati ya wale waliokuwa wafuasi Wake na waliomcha Mungu). Mpito wa karne 25 au 30 haujabadilisha ukweli huu. Badala yake, tumepata neema ya Biblia iliyo kamili, Neno la Mungu lililo katika ukamilifu na utimilifu wake. Ni jambo la kusikitisha (na lenye kinaya – irony – ya kutosha tu) kwamba katika wakati huu ambapo tuna fursa na rasilimali za wakati, nyenzo, masomo ya lugha za kale zilizotumika katika kuandika Biblia, na fursa za kuisoma na kujifunza Biblia zaidi ya wakati wowote mwingine katika historia wa wanadamu, ni “Wakristo” wachache zaidi na zaidi walio na shauku ya kumjua Kristo – kando ya yale ambayo viongozi wao wanaamua kuwafundisha (ambayo yanaweza kuwa ya kweli au la) na hakuna namna ya kupambanua hili bila ya wewe mwenyewe kuisoma Biblia.

Nina matumaini kwamba wewe utaupokea ujumbe wangu huu katika moyo ule ule ambao mimi nimeuandika [ujumbe wenyewe] – sala na maombi yangu [kwa Mungu] kwa ajili yako ni kwamba [wewe] uweze kukua katika Bwana Yesu Kristo. Lakini ili uweze kukua [kiroho], ni lazima uwe na fikra Zake zikipita na kumiminika ndani ya moyo wako – na hili linalazimu wewe mwenyewe uingie ndani zaidi na zaidi katika maandiko kila siku inayopita. Kwa hakika mimi siwezi kudai kwamba mimi pekee ndiye mwenye haki ya kuhodhi mafundisho sahihi ya Neno la Mungu – na huwa nasisitiza kwa wote wanaotumia mafundisho yangu katika kujifunza Neno la Mungu wajisomee pia Neno hilo wao wenyewe na kuhakiki nukuu za Biblia ninazozitoa, wakati mwingine kwa wingi sana (Matendo 17:11-12)! Tazama pia linki hii katika tovuti ya https://ichthys.com – (Read your Bible) na linki hii katika tovuti ya https://sayuni.co.tz – Fasiri ya Biblia I: Je, tunawezaje kujua ni TAFSIRI / FASIRI (Version) ipi ya Biblia ndiyo sahihi (Part 1)? Mimi mwenyewe ninajua fika kwamba, kulingana na mfumo na mtindo wangu wa ufundishaji, si watu wote watakaopenda kujifunza Biblia kupitia tovuti hii; wakati huo huo, sina nia ya kudokeza kwamba chaguo lako la dhehebu au kanisa linafanya mafanikio ya mpango wa Mungu kwa maisha yako yasiwezekane. Hapa ninakueleza suala ambalo mimi mwenyewe ninalifahamu kuwa ni la msingi kuliko masuala yote katika maisha ya Mkristo – kukua kiroho kunalazimu kupitia mchakato wa kula chakula cha kiroho. Bila ya kusoma Biblia, bila ya kufundishwa na kujifunza Biblia, bila ya kuamini yale unayojifunza na kuyatumia hayo yote katika maisha yako na halafu kuwasaidia wengine wapitie mchakato huo huo kama wewe mwenyewe ulivyosaidiwa kwa kutumia kipaji au vipaji ulivyotunukiwa na Mungu, basi haitowezekana kwako kufanikisha ule mpango wa Mungu kwa maisha yako hapa duniani kama mfuasi wa Bwana Yesu Kristo. Bila ya kulielewa na kulikubali hili moyoni mwako, dondoo zote nzuri za liturujia unazoweza kukariri na kunukuu hapa zitakuwa na mafao kidogo sana.

Sasa, ni tafsiri ipi ya Biblia ndiyo sahihi? Kama unasoma tafsiri (versions) zote unazojisikia unaridhika nazo (katika lugha unazozijua) na kuamini unachosoma (licha ya kwamba baadhi ya yale unayoyasoma yatakuwa magumu kuelewa mwanzoni), kama unayapenda yale unayoyasoma moyoni mwako na una shauku ya kuyaelewa na pia una shauku ya kuyaishi katika maisha yako, basi Mungu wetu hatashindwa, kwanza kukuongoza katika suala la masomo yako, na pili katika kukupatia mwalimu stahiki na/au kundi la Wakristo wenzako ambapo utapata chakula chote cha kiroho unachohitaji hata kuzidi matarajio yako yote.

Wako katika Yeye ambaye ndiye Neno halisi la Mungu, Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo,

Bob L.
Wa https://ichthys.com

Basi tuonane katika sehemu ya III ya mfululizo huu, kwa utukufu wa Bwana wetu!

R. Kilambo
Wa https://sayuni.co.tz

NB: Mwulizaji wa maswali mawili yaliyopita hakuendelea na maswali mengine kwa wakati huu. Hivyo sehemu ya III haitokuwa na mjadala au uzi huu.
R. Kilambo.