Ifuatayo ni sehemu ya kwanza katika mfululizo wa mafundisho ya ufafanuzi wa aya za Biblia. Mfululizo huu utahusisha maswali na majibu ambayo wasomaji (au wanafunzi wa Biblia) wa tovuti ya https://ichthys.com ya Dr., Professor, Pastor-Teacher Robert D. Luginbill walimwuliza katika nyakati mbalimbali. Nilimwomba Dakta Luginbill ruksa ya kutafsiri maswali & majibu haya kwa faida ya wanafunzi wa Biblia wanaozungumza lugha ya Kiswahili; Dakta Luginbill anilipatia ruksa hii na haya hapa chini [na sehemu zinazofuata] ndiyo matokeo ya kazi hii.

Ndugu Mkristo, nakukaribisha ili uweze kufaidika [kiroho] na mafundisho ya Neno la Mungu yaliyomo katika mfululizo huu.

Fasiri ya mfululizo mzima na Respicius Luciani Kilambo wa https://sayuni.co.tz

Sehemu ya I: Je, tunawezaje kujua ni TAFSIRI / FASIRI (Version) ipi ya Biblia ndiyo sahihi (Part 1)?

From: Mail-Bible_Interpretation: How Can we Know Whose Interpretation is Right?

Na Dr. Robert D. Luginbill wa https://ichthys.com
September 11, 2004.

 

Swali:

Mwalimu, nilisoma kwa shauku kubwa kilio / [wito wako] dhidi ya kalti (cults) au makundi kama yale yanayofundisha / yanayohubiri “injili ya mafanikio”. Ingawa ninakubaliana na wewe kwamba wanainukuu Biblia isivyo sahihi, bado [mimi] ninashangazwa na fikra zako wewe mwenyewe.

Kwa kuwa wewe ni Mprotestanti, ninahisi kwamba unahubiri kwamba Biblia inatakiwa kusomwa na kueleweka na kila Mkristo katika namna yake. Na hivyo watu wengi wataifasiri Biblia katika namna nyingi; Msabato (anayedai kuifuata Biblia) hatakula nyama ya nguruwe, wakati Mlutheri anaweza kula nyama hiyo.

Muanglikana atashiriki katika ekaristi, lakini Mpresibiteri atashiriki katika kula mkate [na kunywa divai]. Ninyi nyote [Waprotestanti] mnadai kwamba mnaiamini Biblia. Sasa yupi kati yenu yuko sahihi? Wewe unajuaje kwamba fasiri / tafsiri yako ya Biblia ndiyo sahihi, na ile ya mwenzako siyo sahihi?

Ni nani aliyevikusanya vitabu vya Biblia hata vikawa kitabu kimoja? Ninauliza hivi kwa sababu kuna swali jingine ambalo linafuata [swali hili], nalo ni kwamba: kwa nini Biblia yako ndiyo iko sahihi na Biblia nyingine, inayojumuisha [kitabu cha] “injili ya Petro” [kwa mfano], isiwe sahihi?

 

Jibu:

 

Hoja muhimu ni, je, mhusika ana ile imani inayookoa katika Bwana Yesu Kristo, au la? Je, mhusika kikwelikweli ameweka imani yake katika Yesu Kristo ambaye ni Mungu, Mwana wa Mungu, aliyekuja duniani kama mtu ili afe kwa ajili ya dhambi zetu, au la? Na je, mhusika huyu ameweka imani yake katika Yesu Kristo pekee kwa ajili ya wokovu wake, au la? Tunaokolewa kwa neema [ya Mungu] kwa njia ya imani [yetu] (Waefeso 2:8-9), na kwa wale wote ambao ni wanafunzi halisi wa Bwana Yesu Kristo, kuwa wafuasi wake waaminifu katika maisha yao yote hapa duniani, kukua kiroho kwa kunywa maziwa halisi ya Neno, kukua katika upendo, na kuakisi / kuonyesha upendo wake kwa ulimwengu katika yale wanayoyawaza, wanayoyasema na wanayoyatenda (na kuwasaidia Wakristo wenzao kufanya hivyo hivyo); kwa wale ambao kuishi ni Kristo, na kufa ni faida (Wafilipi 1:21), uhusiano wetu na Bwana Yesu Kristo, sasa na milele yote, ndilo suala lenye umuhimu.

 

Bila Biblia, hatuwezi kumjua Kristo. Hatungeweza kujua Yeye ni nani, wala kile Alichokifanya kwa ajili yetu, wala kile Anachotaka sisi tufanye. Biblia inamsimulia Yeye kuanzia Mwanzo 1:1 mpaka Ufunuo 22:21, na ni kwa njia ya kujifunza Biblia [pekee] kwa bidii ndiyo tunasogea karibu Naye. Kwani bila ya ile kweli, na katika Biblia pekee ndimo tunaipata kweli ya Mungu, hakuna njia yoyote nyingine ya kumwabudu Mungu katika Roho na katika kweli (Yohana 4:21-24).

 

Biblia inapumua kwetu Nafsi na hulka ya Mungu Mwenyewe katika kila ukurasa wake. Injili ya Petro!? Sidhani kwamba unaweza kunionyesha waumini halisi wa Bwana Yesu Kristo hata watano tu hapa duniani watakaokubali kwamba kitabu hicho ni sehemu ya maandiko matakatifu. Kama utawapata waumini hao watano, tutawaweka meza moja, wataisoma “injili” hiyo, na watamaizi mara moja kwamba kitabu hicho siyo kabisa sehemu ya maandiko matakatifu. Kwa sababu maandiko matakatifu [yenyewe] yana ujazo wa uweza na nguvu ya Roho Mtakatifu [wa Mungu], na unapoyalinganisha na maandiko mbadala kutoka katika kalamu za wanadamu tu basi yale maandiko ya wanadamu yanasambaratishwa na kuwa mavumbi tu – yanaposomwa na wale ambao ndani yao Roho Mtakatifu wa Mungu aliye hai anakaa, wale ambao ni waumini halisi wa Bwana Yesu Kristo, wale ambao wamekuwa wakiisoma Biblia.

 

Si kweli kabisa (kama ambavyo walio wengi ambao hawajajitoa kwa dhati katika kujifunza Biblia wanavyofikiria) kwamba unavyozidi kujifunza na unavyozidi kuyazoea maandiko, basi matokeo yake ni kuwa na mkanganyiko na uelewa mbovu wa maandiko – hii ni dhana yenye makosa, ambayo makundi mengi yaliyoweka mamlaka ya kufundisha [Biblia] mikononi mwa watu wachache kwa malengo ya kuamuru kwa wafuasi wao jambo lipi ni la kweli na lipi si la kweli bila kuifuata Biblia yanavyopenda kusema. Kinyume chake, kinachotokea pale mtu anapoweka nia ya kweli ya kumfuata Mungu kwa njia ya Neno Lake ni ongezeko la mwanga wa ile kweli ya Mungu ndani ya moyo wa Mkristo huyu, kanuni moja baada ya nyingine ya kweli ya Mungu ikiangaza na kuimarisha kanuni nyingine za kweli zilizoaminiwa, mpaka migongano yote inatoweka, na inakuwa wazi kwamba ujumbe wa Biblia ni mmoja – wokovu kwa njia ya imani kwa Bwana Yesu Kristo (Yoh. 3:16), ujumbe huu ukiandikwa katika mfumo wenye nguvu, mfumo wa ki-nelibini (kaleidoscopic) unaopanga kanuni moja ya kweli ndani ya kanuni ingine ya kweli katika uweza mkuu wa Roho Mtakatifu.

 

Hakuna mtu yeyote anayeweza kukuthibitishia jambo hili kimantiki, yaani katika namna ya kisayansi, kwa sababu hili ni jambo la kiroho (super-natural), siyo la kidunia / kimwili. Na hakuna mtu mwingine anayeweza kuuwasha moto wa kumpenda Mungu ndani ya moyo wako – ni wewe unayepaswa kulifanya hili, kufanya uchaguzi kwa kuutumia utashi huru uliopewa na Mungu (Mwa. 1:26a; Yoh. 3:16-18). Lakini, ikiwa una nia na unafanya jitihada ya kumtafuta Mungu [bila kujali] Yeye Mwenyewe atakuongoza na kukupeleka wapi (hii ndiyo maana mojawapo ya imani kwa Mungu!), basi mimi napendekeza [kwako] usome Biblia. Biblia itakupeleka mahala pamoja tu – katika mikono salama ya Bwana wetu. Badala ya mkanganyiko wa “njia” lukuki za dini lukuki zinazotofautiana, maandiko yatakupeleka kwenye njia moja tu, Njia Pekee, Yesu Kristo (Yohana 14:5-7). Kama utastahamili katika njia hii, utapata wokovu, amani moyoni mwako, nguvu, utukufu, na furaha isiyoelezeka – na Biblia yenyewe itakusaidia katika kukuonyesha mahala sahihi utakapopata mafundisho stahiki, itakunyooshea njia yako na kukuonyesha mahala palipo na mafundisho mabovu (ambapo utapaswa kupaepuka), kwa mfano kanuni isiyo sahihi ya “injili ya mafanikio”. Kwanza, uwe na imani isiyotetereka kwamba Mungu amekupatia ile kweli katika Neno Lake na ujiwekee lengo la kulisoma na kujifunza Neno hilo – na kwa hakika Mungu hatashindwa kukupatia Mwalimu wa Biblia na mafundisho yatakayokuwezesha kukua [kiroho] kutokana na Neno Lake.

 

Kwa habari zaidi, tafadhali tazama link: Read your Bible: Protection against cults.

 

Uamuzi na uchaguzi ni wako – mimi ninaomba Mungu akujalie neema ya kumpenda Yeye kama ambavyo Yeye anakupenda wewe.

 

Katika Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo,

 

Bob L., wa https://ichthys.com

 

Basi tuonane katika Sehemu ya II ya mfululizo huu, kwa utukufu wa Bwana wetu, amen!

 

R. Kilambo, wa https://sayuni.co.tz