Maana ya WOKOVU au KUZALIWA UPYA
Original Writing in English by Bartek Sylwestrzak
Tafsiri hii ya Kiswahili imefanywa na Respicius L. Kilambo
3.3 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.
Yohana 3:3 SUV

Yafuatayo ni majibu ya swali alilouliza muumini mmoja wa Dhehebu moja la Kikristo wa huko Poland. Jina lake ni T****. Alimwuliza swali hili rafiki yake B**** ambaye ni muumini wa zamani wa Dhehebu hilo, ila sasa AMEOKOLEWA (amekuwa Born Again – amezaliwa upya katika Kristo). Walikuwa wakifanya mdahalo huu kupitia e-mail.
Katika mazungumzo yao T**** alimwambia B***** kwamba yeye anao WOKOVU kwani amefundishwa na Dhehebu lake huko Poland kwamba anapashwa tu kufuata amri KUMI za Mungu, abatizwe kwa maji (alibatizwa kwa maji akiwa mtoto mchanga, ambayo ni desturi na mapokeo ya dhehebu lake), kusadiki na kufuata mafundisho ya Kanisa, na ataingia Mbinguni! B***** alipinga hilo na kumwambia kwamba Biblia haifundishi hivyo kabisa. Ndipo T**** akamwuliza “basi WOKOVU ni nini?” Naye B***** akamwandikia T**** majibu ya swali kwa kirefu kidogo.
JIBU LA B****:
Kuelewa baadhi ya majibu nitakayokupatia yaweza kuwa vigumu kwako; kuelewa mengine ya hayo majibu yaweza kuwa haiwezekani kabisa kwa mtu ambaye hana ile imani ambayo msingi wake ni kweli [mtu aliyezaliwa upya]. Mfano mzuri hapa unahusiana na mafundisho ya Kanisa lako kwamba mambo muhimu kuliko yote katika kupata WOKOVU ni kufuata amri kumi za Mungu na zile za Kanisa na siyo kuweka IMANI yetu kwa Bwana Yesu Kristo. Jambo la WOKOVU ni muhimu sana, kuliko mambo yote katika maisha yetu. Mimi na wewe tumelelewa katika mazingira ambamo badala ya kufundishwa misingi ya uhakika na kweli ya Biblia, tumepewa TAMADUNI, DESTURI na MAPOKEO yasiyo sahihi, ya kibinadamu. Kwa karne nyingi sasa Makanisa na Madhehebu mengi yamejiweka mbali na ukweli kiasi kwamba kile kinachoitwa “IMANI” inayofundishwa siyo tena ile kweli inayookoa. Ni jambo la kusikitisha sana kwamba ingawa katika macho yao wenyewe Makanisa na Madhehebu haya yanaona kwamba yanafundisha ukweli, lakini hawawaongozi wafuasi wao kuelekea kwenye WOKOVU. Wanafundisha wafuasi wao kufuata SHERIA na DESTURI kama njia ya kuelekea kwenye wokovu, kama vile Wafarisayo wa enzi za Bwana wetu Yesu Kristo walivyofundisha wafuasi wao; na sisi sote tunajua jinsi Bwana Yesu alivyowapinga vikali Wafarisayo wale, mfano:
Luka 11:37-44:- 11.37 Alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. 11.38 Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. 11.39 Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang'anyi na uovu. 11.40 Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia? 11.41 Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu. 11.42 Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. 11.43 Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. 11.44 Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo.

[ NOTE: Kuna Tafsiri kadhaa za Biblia za Kiswahili; unaweza, na inafaa, kutumia ile tafsiri (au zile tafsiri) ambayo WEWE unaendana nayo vizuri. Hapa nimetumia Swahili Union Version]

Hivyo basi, kitu muhimu kwako ni kuelewa Mungu anakutizama vipi kwa IMANI uliyo nayo sasa hivi, na nini hasa maana ya wokovu. Hapa chini nitakueleza kwa kifupi msimamo wa Injili kuhusiana na wokovu.
1. UWEPO WA MUNGU – UFUNUO KATIKA JINSI ULIMWENGU ULIVYO NA KATIKA NAFSI YA BINADAMU
Kwanza, tunajua ya kwamba Mungu yupo, kwani ulimwengu wote – uwepo wake, mpangilio wake, muundo wake – unashuhudia kuwa yuko Muumbaji aliyefanya uwepo.
Zaburi 19:1-7:- 1 Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake. 2 Mchana husemezana na mchana, Usiku hutolea usiku maarifa. 3 Hakuna lugha wala maneno, Sauti yao haisikilikani. 4 Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Katika hizo ameliwekea jua hema, 5 Kama bwana arusi akitoka chumbani mwake, Lafurahi kama mtu aliye hodari Kwenda mbio katika njia yake. 6 Kutoka kwake lautoka mwisho wa mbingu, Na kuzunguka kwake hata miisho yake, Wala kwa hiari yake Hakuna kitu kilichositirika. 7 Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.

Zaburi 97:6:- 6 Mbingu zimetangaza haki yake, Na watu wote wameuona utukufu wake.

Pili, nafsi ya kila mwanadamu/mtu inashuhudia ya kwamba Mungu yupo. Mungu ametuumba katika namna ambayo tunapata ukamilifu katika uhusiano na Yeye tu. Mungu ameumba ndani ya roho zetu SHAUKU au MSUKUMO unaotuelekeza kutaka kujua mambo yalivyo kwa wakati huu, lakini haswa kutaka kujua mambo yatakavyokuwa baada ya kifo. Ni silika yetu kwamba mambo ya mpito hayawezi kutupatia furaha ya kudumu.

Mhubiri 3:11:- 11 Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.

Japokuwa muda tunaoishi hapa duniani ni mfupi sana; tunaishi katika dunia ambamo matukio yanabadilika wakati wote, na hakuna kinachodumu; NAFSI zetu zinatafuta kile kinachodumu MILELE. Mungu ametia muhuri wake katika nafsi ya kila mwanadamu, kiasi kwamba atakuwa anatafuta kile kitu kitakachomfanya aishi milele. Hii ni asili yetu japokuwa hatuwezi kugundua au kujua kila kitu katika ulimwengu tunamoishi; hatuwezi kujua historia yote ya dunia, kwa mfano.

Mhubiri 3:11 ni mmoja kati ya mistari mizuri na yenye maana sana katika Biblia. Keil & Delitzsch (ambao ni wasomi wa Biblia wa Kijerumani wa karne ya 19) waliandika kitabu maarufu kinachofundisha [kinachonyumbulisha] Agano la Kale. Katika kitabu hiki wametoa maoni yao kuhusu msitari huu wa Mhubiri 3:11 (tafsiri yangu):-

“Mwandishi wa msitari huu anamaanisha kwamba Mungu amemwekea kila mwanadamu mahala pake katika historia; ameweka katika ufahamu wa mwanadamu ukweli kwamba AMEUMBWA; ameweka katika nafsi ya mwanadamu shauku au msukumo unaomwelekeza kutaka kujua kuna nini baada ya maisha haya au katika milele. Ni asili ya mwanadamu kutoridhika na mambo ya mpito bali kuvunja kuta za wakati zinazombana ndani ya ngome ya miaka michache anayoishi hapa duniani na kutaka kujua yatakayotokea katika wakati tunaouita MILELE. Na hivyo katika mabadiliko ya matukio yasiyokwisha, mwanadamu anajipa faraja kwa kuelekeza fikra zake katika wakati huo unaoitwa “MILELE.”

“Usemi huu unaohusiana na “desiderium aeternitatis” kwa lugha ya Kilatini (maana yake : hamu/shauku ya kujua mpango wa milele), hamu ambayo imepandikizwa katika roho ya mwanadamu na Mungu ni mmoja kati ya misemo yenye maana kuu katika Biblia, msemo uliomo katika kitabu cha Mhubiri – Mhubiri 3:11. Kwa kweli mwenendo wa mwanadamu unaonyesha kwamba mahitaji yake ya kiroho hayawezi kuridhishwa na vitu/mambo ya mpito. Mwanadamu ni kiumbe anayebanwa na wakati/miaka michache ya kuishi hapa duniani lakini katika asili yake ya kiroho anahusiana na huu wakati tunaouita MILELE. Masuala ya mpito hayampi faraja yeyote; yanamkimbiza kama maji ya mto yanayoelekea bondeni, na yanamlazimisha atafute namna yakujikomboa kwa kujiuliza maswali ili apate majibu ya MILELE. Ama kwa hakika Mhubiri hazungumzii mambo ya kila siku kama shughuli za kutafuta kipato, chakula, nk, bali anazungumzia upande wa kiroho na kiakili wa maisha ya mwanadamu ambao unaonyesha kwamba Mungu amepiga muhuri wake katika roho ya mwanadamu huyu.

“Haitoshelezi kwa mwanadamu kujua kwamba kila jambo linalotokea limepangwa na Mungu ili litokee kwa wakati wake. Mwanadamu ana silika ya kipekee katika viumbe* inayomsukuma kuvuka hii elimu ya wakati hadi wakati na kutaka kujifunza elimu ya MILELE; lakini jaribio lake hili halifanikiwi, kwani kama Mhubiri anavyosema “……jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya …..” Matendo ya Mungu yanaonekana yakiendelea katika historia ya dunia ambamo maisha ya mwanadamu mmoja ni sehemu tu….. hivyo basi ile shauku ya kujua masuala ya milele iliyomo ndani ya nafsi yake haiwezi kupata majibu katika kipindi kifupi cha maisha yake. Mwanadamu hutaka kuiona ile taswira ya uumbaji/kazi ya Mungu katika kipindi chake cha maisha ya hapa duniani lakini hili haliwezekani kwake.”

Kutoka “Commentary on the Old Testament: explanation of Eccl. 3:11”

*Sambamba na Malaika.

Maisha bila Mungu hayana maana yeyote, japokuwa ukiwatizama na ukawahoji watu wanaoipenda dunia hii watakupa jibu tofauti. Watu wanaoipenda dunia hii na starehe zake huanza kwa kutafuta raha fulani, kitu fulani, mafanikio fulani ambayo wanaamini wakipata basi watakuwa na ile furaha timilifu; lakini wakipata raha, kitu au mafanikio hayo, macho yao huona kingine ambacho ni kizuri zaidi, kikubwa zaidi au kinavutia zaidi ya kile walichopata. Mali, starehe, mafanikio ya maisha hayaleti furaha halisi ya rohoni. Kama huna furaha rohoni mwako wakati ukiishi ndani ya nyumba ya vyumba vitatu, ukipata nyumba ya vyumba sita haitoongeza furaha katika roho yako. Utafika katika kilele cha Mlima Meru lakini utaona kwamba haitoshi; utataka kufika katika kilele cha Kilimanjaro, na ukimaliza hilo utaambiwa: “kuna Himalaya bwana!” Amani ndani ya roho zetu haipatikani kwa mafanikio ya kidunia. Kama Mwalimu kutoka katika kitabu cha Muhubiri anavyosema: Kila kitu cha kidunia ni bure – ubatili – na kukimbiza upepo. Nakushauri usome kitabu hiki kwani kinadhihirisha ubatili wa maisha ya kidunia kwa mwanadamu anayeishi bila Mungu.
Mhubiri 1:1-11:- 1 Maneno ya Mhubiri mwana wa Daudi, mfalme katika Yerusalemu. 2 Mhubiri asema, Ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. 3 Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua? 4 Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima. 5 Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa maawio yake. 6 Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake. 7 Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena. 8 Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia. 9 Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua. 10 Je! Kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, Tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi. 11 Hakuna kumbukumbu lo lote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lo lote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.

Ulimwengu huu na roho zetu sisi wanadamu zinashuhudia kwamba Mungu yupo! Tunapokubali ukweli huu (kwamba Mungu YUPO) tunapaswa kufanya maamuzi – je, tunataka kumfahamu Mungu? Tunaweza kuufuatilia wito huu wa kumfahamu Mungu au la; tunaweza kuupuuza wito uliomo rohoni mwetu. Watu wengi walioishi na wanaoishi sasa hapa duniani wameamua kuupuuza wito huu.

Kwa upande mwingine kuna watu wengi wanakataa wito huu; wanaamini dhana ya uwongo kwamba hakuna Mungu na wanakumbatia mambo ya dunia ambayo hayadumu. Baadhi yao hujitupa moja kwa moja katika maisha ya kujiridhisha kimwili au kustarehe kupita kiasi na kumwacha Mungu.

Warumi 1:16-32:- 1.16  Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia (maana yake mtu asiye Myahudi, mfano Mgiriki, Muhindi, Mwafrika, nk). 1.17  Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani. 1.18  Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. 1.19  Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. 1.20  Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru (kisingizio); 1.21  kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. 1.22  Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; 1.23  wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo. 1.24  Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. 1.25  Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina. 1.26  Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; 1.27  wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. 1.28  Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. 1.29  Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, 1.30  wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari (proud/wanaojiona bora kuliko wenzao), wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, 1.31  wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; 1.32  ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendayo hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.

Wengine (soma hili kwa makini!) hawakatai uwepo wa Mungu, lakini hawataki kumtafuta, hivyo hugeukia DINI mbalimbali zilizoko duniani, ambamo hukumbatia mafundisho mbalimbali yasiyo na ukweli wowote (au ukweli kidogo sana!) kulingana na ule uwongo wanaoupenda, au kwa sababu ya familia walimozaliwa au kulelewa nayo. [ kumbuka ukishakubali kwamba Mungu yupo, kinachofuata ni kuitikia huo wito na kumtafuta kwa roho yako yote! ] Hivyo wanaoamua kufuata DINI fulani kati ya DINI nyingi zilizoko (au madhehebu yake) huamini mfumo fulani wa WOKOVU kupitia MATENDO fulani (siyo imani!) na huridhika na “KAZI” wanayomtendea Mungu (kwa mfano “Mungu yupo na mimi huenda kanisani kila Jumapili, hivyo natenda au natimiza wajibu wangu kwa Mungu, na hiyo yatosha!)
Wengine huamini kwamba wakifunga/wakijinyima kula au/na kunywa kwa saa kadhaa kila siku kwa kipindi cha siku kadhaa, wakitoa “sadaka” kusaidia masikini, wakienda kwenye hekalu kila siku mara kadhaa, wakivaa nguo za aina fulani, basi wanakuwa wametimiza wajibu wao kwa Mungu. Watu wa namna hii wanaweka muonekano wa nje tu; hakuna nia halisi ya kuutafuta ukweli wala shauku ya rohoni ya kumtafuta Mungu bali dhamira zao huridhishwa na kile kitendo cha kwenda hekaluni, nk au ibada yeyote ile aliyoichagua au aliyochaguliwa na wazazi au walezi wake.
Wengine pia wanakubali kwamba Mungu yupo lakini hawashughuliki naye; hao hujikita katika shughuli za kila siku na kila saa za kimaisha – kazi, shule, familia, burudani, sherehe, nk kwa asilimia mia moja. Sote tunajua, katika dunia tunamoishi sasa, mambo hayo yanaweza kuchukua asilimia 100 ya muda wao wote!
2. UFUNUO WA MUNGU KATIKA NENO LAKE NA KATIKA YESU KRISTO
Mwanadamu anaposikia ile sauti iliyo ndani ya roho yake, inayomtuma kumtafuta Mungu, na akatii wito huo, basi Mungu atamwongoza kwake kwani Yeye hutaka wanadamu wote waje kwake.
Kumbukumbu la Torati 4:29:- 29 Lakini huko, kama mkimtafuta Bwana, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote.
Isaya 45:22:- 22 Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine.
Isaya 55:6-7:- 6 Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; 7 Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.

Yeremia 29:13-14a:- 13 Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. 14 Nami nitaonekana kwenu, asema Bwana

Siku utakayoamua kwamba unataka kumtafuta na kumjua Mungu, basi Yeye mwenyewe ataiona hiyo nia au shauku ndani ya roho yako na atakuongoza kwake; atafungua ule mlango na atakukaribisha ili uone ule Ufunuo wake maalum – Neno lake Takatifu na Yesu Kristo.

Matayo 7:7-8:- 7.7 Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni (hodi), nanyi mtafunguliwa; 7.8 kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.

Haya ni maneno ya Bwana yesu mwenyewe akikuhakikishia kwamba ukimtafuta Mungu, basi Mungu anajua hilo na anajibu shauku yako hiyo na atakuonyesha njia. Mungu anataka sisi sote tuje kuufahamu ule ukweli.

1Timoteo 2:3-4:- 2.3  Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu;
2.4  ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.

Na ukweli uko wapi? Ukweli umo katika Biblia.

Yohana 17:17:- Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.

2Timoteo 3:16:- Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki

Ukweli ni Neno la Mungu – Yesu Kristo.

Yohana 1:1-2:- 1.1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 1.2 Huyo Neno tangu mwanzo alikuwako kwa Mungu.

Yohana 1:14:- Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.

Yohana 14:6:- Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi[kupitia kwangu].

Hivyo ni dhahiri, kama tutakuwa na KIU ya kuujua ukweli, Mungu atatuongoza mpaka tufike kwenye ukweli, kwa njia moja ama nyingine. Atamtuma mmisionari, mwinjilisti au rafiki yako anayeamini; unaweza ukijikuta ukifungua Biblia iliyoko katika chumba cha kulala wageni; au intaneti, e-mail, radio, runinga, kipeperushi, gazeti, nk.
Matayo 7:7-8:- Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni (hodi), nanyi mtafunguliwa!

3. TATIZO LA DHAMBI YA MWANADAMU

3a. Utakatifu wa Mungu na kiwango alichoweka cha Uongofu au Haki.

Hata kabla hujachukua Biblia kwa mara ya kwanza na kuanza kuisoma, ulimwengu na jinsi ulivoumbwa unaonyesha au unashujudia baadhi ya sifa zake – Uwezo wake, Busara zake, Nguvu zake, Upendo wake, Utukufu wake, nk. Kwa hivyo wale wanaomkataa hawana kisingizio chochote:

Warumi 1:18-21:- 1.18  Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. 1.19  Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. 1.20  Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru (kisingizio); 1.21  kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.

Bali tunapoanza kusoma Neno lake utakatifu wake unaanza kudhihirika:

Walawi 11:45:- 45 Kwa kuwa mimi ni Bwana niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu.

Matayo 5.48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Zaburi 99:9:- 9 Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu; Sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu; Maana Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.

Isaya 6:1-3:- 1 Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. 2 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. 3 Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.

Ufunuo 4.8  Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja.

Kutokana na utukufu wake huu, anatupa kiwango chake cha Uongofu au Haki:
Kumbukumbu 32:4:- 4 Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili.
Zaburi 11:7:- Kwa kuwa Bwana ndiye mwenye haki, Apenda matendo ya haki, Wanyofu wa moyo watamwona uso wake.

Zaburi 33:5:- Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za Bwana.

Zaburi 50:6:- Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu

Zaburi 89:14:- Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako, Fadhili na kweli zahudhuria mbele za uso wako.

Zaburi 119:142:- Haki yako ni haki ya milele, Na sheria yako ni kweli.

Isaya 61:8:- Maana mimi, Bwana, naipenda hukumu ya haki, nauchukia wivi na uovu; nami nitawalipa malipo katika kweli, nitaagana nao agano la milele.

Ufunuo 16:5:-  Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi.

Hivyo kulingana na kiwango chake hiki cha Uongofu au Haki, Mungu atatuhukumu sisi sote:

Zaburi 7:11:- Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.

Zaburi 9:7-8:- 7 Bali Bwana atakaa milele, Ameweka kiti chake tayari kwa hukumu.
8 Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki; Atawaamua watu kwa adili.

Zaburi 96:11-13:- 11 Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie, Bahari na ivume na vyote viijazavyo, 12 Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo, Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha; 13 Mbele za Bwana, kwa maana anakuja, Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa uaminifu wake.

Zaburi 98:7-9:- 7 Bahari na ivume na vyote viijazavyo, Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
8 Mito na ipige makofi, Milima na iimbe pamoja kwa furaha. 9 Mbele za Bwana; Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa adili.

Yeremia 11:20 Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki, ujaribuye akili na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu. 

Matendo 17:31:- Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.

2Timoteo 4:8:-  Baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.

1Petro 1:14-17:- 1.14  Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; 1.15  bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; 1.16  kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. 1.17  Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni.

Kila upande wa maisha yetu unatufundisha kwamba hukumu inayotokana na matendo yetu haizuiliki, kwani tunaona dhahiri matokeo ya matendo katika dunia tunamoishi. Na Biblia ambayo ni Neno la Mungu inatuhakikishia:

Waebrania 9:27:-  Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa, hukumu.

3b. Sote tu wenye dhambi

Kama vile tunavyotambua kwamba Mungu yupo na kujua baadhi ya Tabia zake hata kabla ya kusoma Biblia, vile vile DHAMIRA zetu zinatuambia au zinatushitaki (hata kabla ya kusoma Biblia) kwamba sisi hutenda dhambi au hufanya matendo yasiyostahili.

Warumi 2:14-15:- 2.14  Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. 2.15  Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea.

Lakini tunapoanza kusoma Biblia na tunapoanza kuuona Utukufu wa Mungu katika Neno lake; anapotuamrisha tuwe watakatifu kama Yeye alivyo mtakatifu; tunapojifunza kiwango chake cha juu kabisa cha Uongofu au Haki, inakuwa dhahiri kabisa kwamba sisi wanadamu ni wenye DHAMBI.

Walawi 11:44-45:- 44 Kwa kuwa mimi ni Bwana, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yo yote, kiendacho juu ya nchi. 45 Kwa kuwa mimi ni Bwana niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu.

Walawi 19:2:- 2 Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.

Walawi 20:7:- 7 Jitakaseni basi, iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu

1Petro 1:14-16:- 4.14  Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia. 4.15  Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine. 4.16  Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.

Wafalme 8:46a:- Ikiwa wamekutenda dhambi, (maana hakuna mtu asiyetenda dhambi), hata ukawaghadhibikia, ………

Ayubu 14:4:- Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana awezaye. [maana yake: mwanadamu katika hali yake ya dhambi hawezi kuzaa mema]
Ayubu 15:14:- Je! Mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi? Huyo aliyezaliwa na mwanamke, hata awe na haki

Zaburi 130:3:- Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?

Zaburi 143:2:- Wala usimhukumu mtumishi wako, Maana kwako hakuna aliye hai mwenye haki.

Muhubiri 7:20:- Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.
Mithali 20:9:- Nani awezaye kusema, Nimesafisha moyo wangu; Nimetakasika dhambi yangu?

Warumi 5:12:-  Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi;

1Yohana 1:8:-  Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
Tunaposoma hii mistari ya Neno la Mungu na kuelewa nini maana yake tunatambua ugumu au utata unaomkabili mwanadamu. Mungu ni mtakatifu na anatuamuru sisi tuwe watakatifu. Kiwango chake cha uongofu au haki ni TIMILIFU au KAMILI na anatuhukumu sisi kwa sasa na baadaye kwa kutumia kiwango hiki (japo kwa HURUMA nyingi pia). Sisi wanadamu kwa upande mwingine, ni wenye DHAMBI na kama tutajitizama nafsini mwetu kwa ukweli tutakiri kuwa hatuwezi kufikia kiwango hiki cha uongofu au haki, ambacho Mungu anacho, kwa juhudi zetu wenyewe. Dhambi inatutenganisha na Mungu; inaweka ufa mkuu kati yetu sisi na Mungu; na kwa juhudi zetu sisi wenyewe hatuwezi kujenga daraja la kuvuka ufa huu na kumfikia Mungu. Tunapojaribu kujenga daraja hili tunaanguka kabla ya kupata mafanikio yeyote.
Warumi 3:23:-  kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;

3c. Hatuwezi kutatua tatizo la dhambi zetu sisi wenyewe na kufikia kile kiwango timilifu cha Mungu

Hatuwezi kuishi bila kutenda dhambi na hatuwezi kuzisafisha dhambi zetu sisi wenyewe kwa juhudi zetu. Ninapofundisha watu juu ya tatizo hili la mwanadamu, mimi hutumia mfano wa chombo chenye maji yaliyo masafi kwa asilimia mia moja (100%). Tunaweza kusema haya maji yaliyo katika hiki chombo ni masafi kwa kiwango timilifu. Sasa, ukiyachafua haya maji, hata kwa kiasi kidogo tu (na sisi sote huchafuka kwa dhambi, kubwa au ndogo) maji hayatokuwa masafi kamwe, kwa kiwango kile cha asilimia mia moja (100% au timilifu). Hata ukiweza kumimina kiasi kikubwa namna gani cha maji mengine yaliyo masafi kwa kiwango timilifu (100%), ule uchafu utakuwepo tu kwa kiasi fulani – hata kama ni kidogo sana. Wale wanaofundisha kwamba Wokovu unaweza kupataikana na mwanadamu kwa kutenda matendo fulani ambayo yatakuwa adhabu ya kulipia dhambi, au kutenda mema fulani mfano kutembelea wagonjwa, wanapuuza ukweli huu (kama vile kusema kiasi fulani cha matendo mema yanaweza kuuondoa “uchafu” huu wa dhambi).

“Uchafu” wa dhambi hauwezi kuondolewa kwa matendo mema; na wale wanaofuata “njia” hii hawauoni ukweli mwingine wa ziada – kwamba yale maji wanayoongeza kwenye maji yaliyochafuka nayo pia hayawezi kuwa masafi kwa 100% kwa sababu maji ya hapa duniani hayawezi kusafishwa yakawa masafi kwa 100% (tukirudia mfano wetu wa maji wa hapo juu). Hata uyasafishe namna gani! Vivyo hivyo kwa mwanadamu: hata atende mema kiasi gani, bila imani inayokubalika mbele za Mungu hawezi akawa “msafi”. Matendo ya mwanadamu, kwa sababu yanatendwa na mwanadamu MWENYE DHAMBI, hayawezi kusafisha dhambi yake kamwe. Maji machafu yatazaa …… maji machafu ….. Hivyo mtu yeyote anayefikiri kwamba anaweza “kusafisha” tendo baya kwa kutenda tendo jema anafanya kosa kubwa sana. Siyo tu kwamba tendo baya litabaki kuwa baya (dhambi) bali tatizo lililokusudiwa kuondolewa na tendo lile “jema” linaendelea kuwepo; kwani lile tendo “jema” siyo jema kwa kiwango kinachokubaliwa na Mungu kwa sababu limechafuliwa na hali ya dhambi ya mtendaji wa hilo “jema”. Kama mtu anaamini kwamba anaikomboa (anaisafisha) dhambi aliyotenda kwa kutoa fedha kusaidia walio masikini wenye shida, basi anapuuza ukweli kwamba tendo hili la msaada “linachafuliwa” na dhambi iliyo ndani yake (dhambi iliyo ndani yetu sisi sote), mfano majivuno yanayotokana na imani kwamba unakuwa “mwema” kwa sababu ya tendo “jema” ulilotenda (hili huonekana sana kwa wanaoamini kuwa WOKOVU huweza kupatikana kupitia matendo mema). Pia tendo jema huchafuliwa na hisia kwamba aliyetendewa naye anajiona ana “deni” la kurudisha wema ule. Hivyo basi kuna TATIZO: kuna dhambi ndani yetu (na yeyote mwenye dhamira yenye “afya” analiona hili) na pia hatuwezi kuiondoa dhambi hii.

4. WOKOVU AU KUZALIWA UPYA – UFUMBUZI WA TATIZO LA DHAMBI KWA NJIA YA BWANA YESU KRISTO

Tunajua kwamba Mungu yupo, Yeye ni muumbaji ambaye kiwango chake cha uongofu ni timilifu. Tunajua pia kwamba sisi wanadamu ni wenye dhambi na kwamba hatuwezi kutatua tatizo la dhambi kwa juhudi zetu wenyewe ili kufikia kile kiwango timilifu cha uongofu cha Mungu. Na ni kwa kufikia kiwango hiki timilifu cha uongofu ndipo tunaweza kuishi MILELE na Mungu, kwani Yeye hatokubali hata kiasi kidogo cha uchafu – kufanya hivyo itakuwa ni kinyume na tabia yake. Kwa kujitegemea sisi wenyewe tutaelekea kwenye hukumu isiyoepukika na tunayostahili – kama Mungu asingetupa mkono wa msaada.

Basi Mungu, katika upendo wake usiopimika, ametupa mkono sisi wanadamu na ametatua tatizo hili la dhambi kwa niaba yetu. Uongofu wake uliotimilika unamaanisha kwamba kila dhambi inayotendwa inapaswa kuadhibiwa. Kwa upande mwingine, Upendo wake usiomithilika unatuonyesha na unatufanyia huruma na msamaha. Sura/tabia hizi mbili za Mungu ambazo ukizitama kwa juu-juu zinaonekana kupingana – HAKI inayodai adhabu kwa upande mmoja na UPENDO unaodai msamaha pamoja na huruma kwa upande mwingine – zinapata suluhisho katika Yule Mwana wa Mungu, Yesu Kristo.

Yesu Kristo alikomboa (alilipia, alipata adhabu kwa ajili ya) kila dhambi iliyotendwa na kila mwanadamu katika historia yote ya wanadamu.

Matayo 27.45 Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa.

Marko 15.33 Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa.

Luka 23.44 Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda (tisa),

Katika yale masaa matatu ya giza pale Kalvari ile haki ya Mungu (uongofu wake) iliridhishwa kwa Bwana Yesu Kristo kulipia dhambi zote za wanadamu.

Warumi 5.8  Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. 9  Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.

2 Wakorinto 5.21  Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.

1Yohana 2.2  naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.

Kile kiwango timilifu cha uongofu cha Mungu – ambacho hakiwezi kufikiwa kwa matendo mema ya wanadamu – kimefikiwa kwa njia hiyo kwa wanadamu kuwezeshwa na Mungu mwenyewe, kwa kulipiwa dhambi zao na Bwana Yesu Kristo. Uongofu huu wa Mungu sasa unaweza kupatikana na wanadamu pale wanapoweka IMANI yao ya WOKOVU kwa Bwana Yesu Kristo.

Warumi 5.8  Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. 9  Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.

Tunaokolewa kwa NEEMA ya Mungu kupitia IMANI yetu kwa Yesu Kristo.

Waefeso 2.8  Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; 9  wala si kwa matendo yenu, ili mtu awaye yote asije akajisifu.

“Kwa Neema” kwani hii ni zawadi kutoka kwa Mungu kwamba alimtuma Yesu Kristo aje kulipia dhambi zetu na hakuhitaji malipo ya dhambi zetu kutoka kwetu. Ni malipo ambayo hatuwezi kuyafanya sisi wenyewe, kwani adhabu stahiki ya dhambi ni mauti.

Warumi 6.23  Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.
Kristo alilipa ile bei ya wokovu alipokufa msalabani kwa niaba yetu (kwa ajili yetu).

Warumi 3.21  Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; 3.22  ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; 3.23  kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; 3.24  wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; 3.25  ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa.

Warumi 4.25  ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.

Warumi 5.10  Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake.

Waefeso 1.7  Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.

4.32  tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

Wafilipi 3.8  Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; 3.9  tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani;

Timoteo 2.5  Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; 2.6  ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.

Tito 3.4  Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; 3.5  si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; 3.6  ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; 3.7  ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.

1Petro 2.24  Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.

1Petro 3.18  Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,

“Kupitia Imani yetu” au “kwa Imani” kwa sababu ni kwa kuweka IMANI yetu kwa Kristo, kwamba tunayapokea malipo aliyoyafanya Yeye kwa ajili ya dhambi zetu, na tunajitwalia ule UONGOFU ambao sasa unaweza kupatikana kwetu. Tuko huru kumwamini Yesu Kristo au la.

Yohana 3.16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Yohana 3.36 Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.

Yohana 14.1 Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. 14.2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. 14.3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo.

Matendo 4.12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.

Matendo 10.43 Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.

Matendo 16.31 Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.

1Yohana 5.11  Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. 5.12  Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. 5.13  Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.

Kwa njia hii Mungu anabaki Mwongofu, mwenye Haki iliyo timilifu – kwa sababu kila dhambi imepata adhabu inayostahili; wakati huo huo anabaki kuwa mwenye Huruma na mwenye Upendo – kwa sababu amebeba mzigo wa adhabu hii Yeye mwenyewe katika Nafsi ya Mwanaye Yesu Kristo – Mungu-Mtu; ametupatia nafasi ya kupokea msamaha wa dhambi kupitia imani yetu kwake. Hivyo Mungu ameadhibu na pia Mungu amebeba adhabu hiyo, akikomboa kila dhambi ya mwanadamu katika Kristo.

Kwa wakati huu swali muhimu sana kuliko yote ni: Je, unaamini kwamba Yesu Kristo ni mwokozi wako ambaye amegomboa kila dhambi uliyotenda, kitu ambacho huwezi kufanya wewe mwenyewe?

=0=

Maelezo/Tafsiri/Ufafanuzi wa baadhi ya maneno:

Uongofu Righteousness
Timilifu Perfect
Haki Justice
Silika Instict, character, disposition
Adili just, righteous (enye haki)
Karama blessing/kipaji (Baraka)