KIONGOZI WA TAIFA AMBAYE NI CHAGUO LA MUNGU TUNAMTAMBUAJE? ANAPATIKANA VIPI?
Nawasalimu katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo!
Suala hili hujitokeza katika kila kipindi cha uchaguzi. Na kwa hakika mwaka huu wa 2020 hapa Tanzania suala hili limejitokeza tena na tena katika mijadala mbalimbali baina ya raia wa nchi hii na hata baina ya raia wa nchi za jirani. Hata hivyo ni watu wachache sana wanaolijadili suala hili kwa mtazamo wa Mungu; je, Mungu wetu, katika Neno lake, amelizungumzia suala la namna wanadamu, walio viumbe wake wenye utashi, wanavyoweza kumtambua kiongozi bora kwa ajili ya nchi yao na namna wanavyoweza kumpata kiongozi wa aina hiyo?
Kila kiongozi wa kila taifa hapa duniani ni chaguo la Mungu kwa taifa hilo kwani kila watu wa taifa moja wanampata kiongozi wanayemstahili kutokana na kiwango chao cha tabia njema, kiwango chao cha kufuata sheria zilizopo na kiwango chao cha kuwatii viongozi waliopo na juu ya yote ni kutokana na wale watakatifu waliomo ndani ya nchi hiyo, ubora wa watakatifu hao kama “chumvi” kwa taifa hilo, na jinsi wanavyotendewa na wananchi wenzao na uongozi uliopo.
Nukuu zifuatazo zinathibitisha hili:
2.13 Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.
2.14 Maana ninyi, ndugu, mlikuwa wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyo katika Uyahudi, katika Kristo Yesu; kwa kuwa mlipata mateso yale yale kwa watu wa taifa lenu wenyewe, waliyoyapata na hao kwa Wayahudi;
2.15 ambao walimwua Bwana Yesu, na hao manabii, na kutuudhi sisi; wala hawampendezi Mungu, wala hawapatani na watu wo wote;
2.16 huku wakituzuia tusiseme na Mataifa wapate kuokolewa; ili watimize dhambi zao siku zote. Lakini hasira imewafikia hata mwisho.
1Wathess. 2:13-16 SUV
23.34 Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji;
23.35 hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu.
23.36 Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki.
23.37 Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!
23.38 Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa.
Matt. 23:34-38 SUV
11.50 ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu;
11.51 tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki.
Luka 11:50-51 SUV
Yaani je, watakatifu hawa wa Mungu wanathaminiwa na kuheshimiwa na viongozi na raia wenzao au wanadharauliwa na kuteswa? Ninaposema Watakatifu waliopo ninamaanisha wale raia wa nchi hiyo waliozaliwa upya, wanaojifunza Neno la Mungu, wanaoishi kwa Neno hilo, wanawafundisha wenzao Neno na kulitumikia, na wao wenyewe wanaishi, kukua kiroho kwa Neno hilo. Katika Israeli ile ya kale, matokeo ya kutowathamini, kuwatesa na hata kuwaua watakatifu wa Bwana yalikuwa kwamba Israeli iliendelea kupata viongozi / watawala wabovu na hatimaye ikaingia chini ya ghadhabu kali kutoka kwa Mungu.
Katika Warumi 13: 2 – 5 tunasoma hivi:
13.2 Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao na hao watajipatia hukumu.
13.3 Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;
13.4 kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana [yeye] hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.
13.5 Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri.
War. 13:2-5
Tunafundishwa “kutowaasi wenye mamlaka” maana yake tusiwafanyie jeuri viongozi wetu na tukifanya hivyo basi tunashindana na tunaenda kinyume na agizo la Mungu. Na hili lina matokeo mabaya. Ule msitari wa 4 unasema “yeye (mwenye mamlaka) ni mtumishi wa Mungu kwako” Tunapaswa kumtii kiongozi wa nchi na kufuata sheria za nchi tunamoishi.
2.13 Tiini kila kiamriwacho na watu [wanaotawala nchini mwenu], kwa ajili ya Bwana; ikiwa ni mfalme, ama [mtu] mwenye cheo kikubwa;
2.14 ikiwa ni wakubwa, [basi muwatii] kama wanaotumwa naye [Bwana] ili kuwalipiza kisasi watenda mabaya na kuwasifu watenda mema.
2.15 Kwa sababu ndiyo mapenzi ya Mungu, kwamba kwa kutenda mema mzibe vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu;
2.16 kama walio huru, ila wasioutumia uhuru huo kwa kusitiri ubaya, bali kama watumwa (watumishi) wa Mungu.
2.17 Waheshimuni watu wote. Wapendeni ndugu (Wakristo wenzenu). Mcheni Mungu. Mpeni heshima mfalme (mtawala wa nchi mnamoishi).
1Pet. 2:13-17
Hapa tunaona jinsi mtume Petro anavyotoa maagizo yanayofanana na yale ya mtume Paulo. Viongozi pamoja na sheria ya nchi unamoishi Mkristo vinapaswa kuonyeshwa utii na uaminifu. Mkristo, onyesha jinsi ambavyo wewe ni “chumvi” yenye ubora wa hali ya juu katika mazingira unamoishi.
Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu.
Matt. 22:21b SUV
Hata kama nchi siyo ya Kikristo [haina Wakristo ndani yake], kama raia ni watulivu, wanaoepuka shari na uhalifu, wanaofuata sheria za nchi yao, wana maadili ya kuheshimiana, basi nchi hiyo itapata kiongozi mwema kutoka kwa Mungu ambaye ndiye anajua ndani ya moyo wa kila mtu.
Tunasoma katika Mithali 14:34: Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu na huleta hukumu kwa watu wo wote.
Hapa tunaona kuwa Mungu anasema kwamba haki ikitendeka ndani ya taifa italiinua taifa hilo, na kwamba taifa lenye dhambi ni aibu na huleta hukumu kwa taifa hilo; maana yake ni kwamba kumbe Mungu anatizama mwenendo wa mataifa yote! Na pia Mungu hutoa hukumu inayolingana na mwenendo wa mataifa hayo – hukumu njema kwa mwenendo mwema na hukumu mbaya kwa mwenendo mbaya. Mfano mzuri tunaupata kutoka taifa la Mungu mwenyewe, Israel. Taifa hili lilimwasi Mungu mara nyingi na wakati wa mwanzoni walikuwa wakitubu na kurudi kwake baada ya maasi ya muda. Sambamba na maasi yao walikuwa wakipata wafalme wanaoendana na tabia zao. Mpaka mwisho wa yote walipoteza kila kitu wakasambaratika mpaka enzi za sasa.
Mfano wa kisasa ni nchi ya USA. Kabla ya miaka ya 1960 yaani kabla ya rais J. F. Kennedy nchi hiyo ilijitambulisha duniani kote kama ya Kikristo, ijapokuwa kikatiba USA haina dini; ilikuwa na sheria murua na za haki, upendo, maadili, raia wema na ilipata viongozi ambao wanajulikana kihistoria kuwa ni waadilifu. USA ilistawi, ilinawiri, ilikuwa na amani, upendo na kwa kweli ilikuwa kimbilio la wengi waliokuwa wakionewa nchini mwao. Lakini maadili yao yalipoanza kumong’onyoka ndio ukaanza mtiririko wa maraisi ambao historia imeonyesha kuwa hawakufaa kimaadili. Mmoja wao alilazimika kujiuzulu baada ya kashfa ya aibu - Watergate. JFK mwenyewe aliondolewa ulinzi na Mungu na akauawa kwa risasi ya mwuaji – assassin. Miaka hii wamepata rais ambaye amekuwa kinara wa kutunga sheria za kuhalalisha “ndoa za mashoga” - ndugu yetu Obama. Leo hii huko USA, kama wewe umezaliwa upya katika Kristo na unafanya biashara ya kuoka keki za harusi, wakija wanaume wawili wakakwambia uwatengenezee keki ya “ndoa” kwani wao wanaoana na ukikataa kwa misingi ya imani yako basi utashitakiwa mahakamani! Maadili yao yameporomoka, na ubora wa marais wao umeporomoka vile vile! Na angalia mwenyewe jinsi CV-19 inavyong’ang’ania nchi ile kama ruba, ijapokuwa kwa kweli CV-19 ni tahadhari kwa dunia nzima.
Tuchukue mifano ya mataifa 3 ya Denmark, Sweden na Switzerland, ambayo yako Ulaya. Mataifa haya yanaongoza duniani kwa uongozi bora, amani, uchumi bora, raia wenye afya, nk. Hii ni kwa sababu wanaongozwa kwa sheria za haki, ni watiifu kwa viongozi wao, wanayazungumza matatizo yao kwa usawa, nk. Na matokeo yake wanapata viongozi wema. Japokuwa hawana idadi kubwa ya wanaomfuata Bwana Yesu, Mungu anawapa uongozi bora kwa sababu ya tabia yao njema tu!
Matendo 17.24 Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono;
17.25 wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote.
17.26 Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika (kwa mwanadamu) mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao;
17.27 ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.
Mistari hii kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume inatufundisha kwamba vitu vyote tunavipata kutoka kwa Mungu; hii ni pamoja na nyakati tunamoishi na mipaka ya nchi zetu! Lengo lake ni nini? ILI TUMTAFUTE MUNGU! Kila mwanadamu anawekwa katika mazingira ambayo yanamfaa ili afanye yale maamuzi ya muhimu kuliko yote katika maisha yake: KUMFUATA MUNGU, KUMCHAGUA BWANA YESU KRISTO. Nchi ile ambayo inao watu wengi waliomchagua Bwana Yesu itapata viongozi bora pia.
Lakini kwa upande mwingine, katika kitabu cha Danieli sura ya tatu, tunawaona Shadrak, Meshak na Abednego wakikataa kutii amri ya mfalme Nebukadneza ya kuisujudia sanamu aliyoichonga mfalme huyo. Wayahudi wale waliokuwa utumwani Babeli walikuwa wanatii amri ya Mungu iliyotolewa kwa Musa katika Kutoka 20:2-5a; Kumbukumbu la Torati 5:6-9a; yaani zile amri kumi za Mungu, “The Decalogue”. Hapa tunapata fundisho kuu linalosema kwamba ikiwa amri ya serikali yoyote ya nchi ambamo tunaishi inapelekea kutufanya au kutulazimisha kuabudu kiumbe au sanamu yoyote, basi inatupasa, kama Wakristo, kuipuuza amri hiyo ya serikali, kwani inaenda kinyume na agizo mahususi la Mungu wetu. Suala hili litajitokeza tena katika kipindi ambacho Biblia inakiita “ile miaka mitatu na miezi sita (miaka 3.5) ya Dhiki Kuu” - Ufunuo 13:11-17.
Wakristo hawatakiwi kuhangaika kuhusu namna ya kumpata kiongozi kupitia kura, ijapokuwa hatukatazwi kupiga kura. Wanatakiwa kuwaombea viongozi wao, hata kama ni viongozi “wabaya”. Zaliwa upya, jifunze Neno la Mungu, enenda kwa Neno la Mungu, fundisha au uhudumie wengine ili nao wafanye vivyo hivyo na ulijenge Kanisa la Bwana Yesu na utaona matokeo ya kazi ya Mungu: atakupa mazingira bora ya kuishi, atakupa viongozi bora wa kuiongoza nchi yako na atakupa neema nyingine. Mfalme Daudi alikuwa mtawala bora kuliko wote katika historia ya Israeli; katika utawala wa Bwana wetu wa Mileniamu, Daudi ndiye atakayekuwa Regent (yaani kaimu) wa Bwana wetu katika Israeli, soma Yeremia 30:8-9; Hosea 3:5. Sasa, taifa linalotaka mtawala / kiongozi kama mfalme Daudi linapaswa kuwa na sifa hizo za kuwa na wacha Mungu wa kutosha ndani yake, na ikumbukwe Mungu ndiye anayewachagulia kiongozi wenu. Katika demokrasia kama ya kwetu yenye wagombea wengi wa urais, “Daudi” hatakuwepo kati ya wagombea wote, hata wakiwa elfu[!], ikiwa raia husika hawana sifa ambazo Mungu mwenyewe anataka kuziona katika raia wa nchi hiyo!
Ee Mkristo, Bwana Yesu ndiye Mfalme wako, Rais wako, Waziri wako, Diwani wako, nk. Mtizame Yeye kwa kila kitu, timiza wajibu wako Kwake na mengine YOTE yatajipanga kwenye msitari!
Mathayo 6:31-33:
6.31 Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?
6.32 Kwa maana hayo yote Mataifa (wasioamini) huyatafuta; na Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
6.33 Bali utafuteni kwanza ufalme Wake, na haki Yake; na hayo mengine yote Atawapa, tena kwa ziada.
Imeandikwa na Respicius Luciani Kilambo