MAFUNDISHO KUHUSU KARAMA / VIPAJI / ZAWADI ZA ROHO MTAKATIFU

Na Respicius Luciani Kilambo

Mathayo 6:31-33:
6.31 Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?
6.32 Kwa maana hayo yote Mataifa (wasioamini) huyatafuta; na Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
6.33 Bali utafuteni kwanza ufalme Wake, na haki Yake; na hayo mengine yote Atawapa, tena kwa ziada.

Wagalatia 1:6-8 SUV:
1.6  [Mimi Paulo] Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine.
1.7  Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.
1.8  Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiria ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiria, na alaaniwe [na Mungu].

Wagalatia 6:7-8 SUV:
6.7  Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.
6.8  Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

2Tim. 4:2-4:
4.2 Litangaze Neno! Fanya bidii katika hilo, iwe katika mazingira mazuri au magumu! Karipia, kemea [na] utie moyo kwa uvumilivu [wote utakaohitajika] katika mafundisho [yako]!
4.3 Kwani wakati unakuja ambapo hawatapenda [kusikiliza] mafundisho / kanuni sahihi na badala yake, katika kutamani kukunwa masikio yao [yanayowasha], watajikusanyia kwa njia zao wenyewe waalimu watakaoridhisha tamaa [zao].
4.4 Nao watageuza masikio yao kutoka katika ile kweli, na kupenda kusikiliza hadithi za kutunga.

1Yoh. 4:1-6:
4.1  Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, [ili muone] kwamba zimetokana na Mungu [au la]; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.
4.2  Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho inayokiri kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu.
4.3  Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.
4.4  Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.
4.5  Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia.
4.6  Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.

Kumb. 13:1-4:
1 Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,
2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;
3 wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.
4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.

Waebrania 6:7-8:
6.7  Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao yalimwa, hushiriki [hupokea] baraka zitokazo kwa Mungu;
6.8  bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa.

Yaliyomo:

1. Utangulizi …............……………………………………………………….… 5

2. Makundi ya Karama za Kiroho …………………………………………….… 8

2.1 Karama za muda mfupi: Maelezo ………………………………………8

2.2 Karama za Kudumu au za Muda Mrefu: Maelezo.……………………..8

3. Uchambuzi wa Karama za Kiroho ……………………………………………12

3.1 Karama za kiroho za Muda Mfupi ……………………………………..12

3.2 Karama za Kudumu au za Muda Mrefu ……………………………….18

4. Madhara ya kuuchunguza na kujihusisha na “Ulimwengu wa Roho”:
Tathmini ya Tukio Halisi la Kushambuliwa na Kuvurugwa na Pepo ……….. 26

5. Mtazamo Sahihi wa Kibiblia kuhusu Ulimwengu wa Roho …………………33

5.1 Kutoa Pepo (Exorcism) ……………………………………………………….35

5.2 Aya Mojawapo Isiyoeleweka Vyema ………………………………………….36

6. Hitimisho Kama Tahadhari! …………………………………………………..38

1. Utangulizi.

Ndugu yangu katika Kristo, ninakusalimu katika Jina la Bwana wetu, Mkombozi wetu, Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Kwa kumwamini Yeye, sisi tumeokolewa yanasema maandiko:

49.6 … zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru kwa Mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho (kingo za) ya dunia.
Isa. 49:6b SUV

53.5b … Adhabu ya [kufanikisha] amani yetu [na Mungu] ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
Isa. 53.5b SUV

16.31 Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.
Matendo 16:31 SUV

2.8  Kwa maana mmeokolewa kwa neema [ya Mungu], kwa njia ya imani [yenu kwa Kristo]; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa [cha bure] cha Mungu;
2.9  [na] wala si kwa matendo [yenu], mtu awaye yote asije akajisifu.
Waefe. 2:8-9 SUV

Hata hivyo, siku ya leo sitazungumzia namna tunavyookolewa; leo nitazungumzia baadhi ya matokeo ya kuokolewa kwetu. Nitazungumzia jinsi matokeo haya yanavyochukuliwa na makundi mbalimbali ya wanaotumia jina WAKRISTO kama namna wanavyojitambulisha katika ulimwengu kuhusiana na imani yao. Leo nitazungumzia Biblia inatufundisha nini kuhusu vipaji, karama, zawadi ambazo mwanadamu anapewa na Mungu wetu mara baada ya kuamini katika Bwana Yesu Kristo. Leo nitazungumzia jinsi makundi mbalimbali ya WAKRISTO yanavyopotosha mafundisho ya Biblia kuhusu vipaji, karama na zawadi hizi za Roho Mtakatifu, anazozitoa mara mwanadamu anapozaliwa upya, na ambazo [Mungu amekusudia] Mkristo huyu atazitumia katika kulitumikia Kanisa la Bwana Yesu Kristo mara akifikia kiwango au hatua ya kukua kiroho. Ni muhimu kusisitiza hapa, kwamba ni wajibu wa kila Mkristo, mara baada ya kuzaliwa upya, mara baada ya kuamini na kukiri kuwa Kristo ni Bwana na Mwokozi wake, kuanza mchakato huu wa kukua kiroho (Waefe. 4:14-16;2Pet. 3:18). Lakini kukua kiroho maana yake nini?

Kukua kiroho [baada ya kuzaliwa upya, na kuwa kiumbe kipya] ni matokeo ya:

a. kujifunza Neno la Mungu chini ya Mwalimu / Pastor mwenye kipaji/karama/zawadi ya Roho Mtakatifu ya ualimu [ambaye yeye mwenyewe pia amejifunza maandiko ya Biblia] (1Wakor. 2:12),

b. kujisomea wewe mwenyewe Biblia kila siku na kila wakati unapopata fursa hiyo kwa mfumo na ratiba mahususi (1Wakor. 2:12), na

c. kuishi katika namna mafundisho hayo ya Biblia yanavyoelekeza (1Pet. 2:1-3; War. 8: 14, 26-27)

Hatua hizo hapo juu zitapelekea wewe Mkristo kufikia kiwango ambapo Bwana atakuonyesha zawadi / karama / kipaji chako au vipaji vyako na akakuonyesha pia aina ya utumishi anaoutaka wewe uutimize katika Kanisa Lake. Kukua kiroho kunaongeza uwezo wako, kama Mkristo, wa kuisikia ile sauti ya Roho Mtakatifu inayotusaidia kutembea na Bwana Yesu Kristo hapa duniani. Roho Mtakatifu anatumia mafundisho ya Neno la kweli yaliyo ndani ya moyo wa muumini, yaliyoaminiwa kuwa ni kweli ya Mungu mwenyewe. Huu ndio mchakato wa kukua kiroho ambao ni agizo kwa kila Mkristo, yaani mwanadamu aliyezaliwa upya kupitia imani katika Bwana Yesu Kristo.

Hivyo somo letu leo litazungumzia vipaji/karama/zawadi za Roho Mtakatifu. Lakini vipaji hivi ni nini haswa? Katika ujumla wake, vipaji/karama/zawadi hizi ni kama ifuatavyo (War. 12:6-8; 1Wakor. 12:4-12; 12:28-31a):

1. Karama ya UTUME (Apostle-ship)
2. Karama ya UNABII (Prophecy)
3. Karama ya KUTENDA MIUJIZA (Miracles)
4. Karama ya UPONYAJI (Healing)
5. Karama ya KUNENA LUGHA (Tongues)
6. Karama ya KUTAFSIRI LUGHA (Interpretation of Tongues)
7. Karama ya MAARIFA (Knowledge)
8. Karama ya HEKIMA (Wisdom)
9. Karama ya KUSHAWISHI (Exhortation)
10. Karama ya KUPAMBANUA KATI YA ROHO (Discerning Between Spirits)
11. Karama ya IMANI (Faith)
12. Karama ya UCHUNGAJI NA UALIMU (Pastor-Teacher)
13. Karama ya UINJILISTI (Evangelism)
14. Karama ya UONGOZI/UTAWALA (Administration / Governments)
15. Karama ya HUDUMA (Service)
16. Karama ya KUSAIDIA (Helps)
17. Karama ya KUTOA MSAADA (Giving)
18. Karama ya REHEMA (Mercy)

* Tunaona kwamba maandiko hayafundishi “karama ya kutafsiri ndoto” wala “karama ya kutoa pepo”!
** Maelezo ya kina kabisa yatatolewa kuhusu karama hizi jinsi tunavyoendelea na mjadala huu, hapa chini.
Hapa zimetajwa karama 18; lakini kwa uhakika Roho Mtakatifu hutoa karama / vipaji / zawadi nyingi zaidi ya hizo, kulingana na Anavyoona uelekeo na mahitaji ya Kanisa la Bwana Yesu Kristo. Pia hutoa mchanganyiko wa karama hizi kulingana na mahitaji ya Kanisa. Katika somo hili tutazizungumzia na kuzijadili karama hizi zote; tutaona nafasi ya kila Mmoja katika Utatu Mtakatifu kwenye kuzipanga, kuzigawa, kuzisimamia, kuziwezesha, n.k. karama hizi kwa upande wa Mungu wetu (Waefe. 4:7-12); na kwa upande mwingine tutaona nafasi ya muumini/Mkristo katika kuzifanyia kazi karama alizopewa, katika maisha na mwenendo wake ndani na nje ya Kanisa hapa duniani. Katika enzi hii ya Kanisa iliyoanza miaka takriban 2000 iliyopita, Mungu wetu ana-deal na sisi watoto Wake kwa neema, akitupatia Roho Wake akae ndani yetu mara baada ya kuzaliwa upya, kumwamini Kristo, na kubadilisha maisha yetu kabisa kwa nyuzi 180 (Yoh. 14:17; 1Wakor. 6:19-20; 1Wakor 12:13); kwani hapo tunaingia katika familia takatifu ya Mungu, tunakuwa watoto Wake, Naye anakuwa Baba yetu (1Yoh. 3:1-2; Waga. 4:4-7); anatupatia nyenzo za kuishi hapa duniani, uwezo wa kutenda kazi Yake anayotupangia baada ya kupevuka kiroho, karama za kutimiza majukumu yetu yote kama watumishi Wake, ili tuweze kupata na kufaudu thawabu kemkem alizotutayarishia kabla hata ya kuumbwa ulimwengu, kwani Yeye, akiwa ni mwenye kujua vyote alituchagua hata kabla ya kuumbwa ulimwengu, na akatuchagulia na kutupangia nafasi zetu za utumishi katika Kanisa/Mwili/Bi Arusi wa Mwanaye Yesu Kristo (1Pet. 1:1-2; Waefe. 1:3-6; 2Wakor. 11:2; Ufu. 19:7-9).

7. Katika Yeye tunao ukombozi kwa damu Yake, na msamaha wa dhambi zetu, kutokana na utajiri wa Neema za Mungu;
8a. ambazo Alituzidishia [kwa wingi] …
Waefe. 1: 7-8a

Tunasoma hapo juu na kuelewa kwamba kwa sisi tuliojitwalia ukombozi unaotokana na imani katika Kristo, Mungu anatufungulia utajiri wa neema zake ambao Anatupatia, tena kwa ziada. Naomba ieleweke kwamba hili halina maana ya mali [za kukithiri] za ulimwengu huu, bali ni ahadi ya Mungu wetu kwamba atatuvusha salama kwa neema zake kutoka ulimwengu huu hata kuingia katika milele Yake kupitia ufufuo katika ile Siku ya Bwana. Karama/vipaji/zawadi za kiroho ni sehemu ya neema zinazoahidiwa hapa juu katika Neno la Mungu mwenyewe, kwa wale walioweka imani yao kwa wokovu na pia kwa kuishi maisha yao hapa duniani katika Kristo Yesu.

Basi, na tuanze kuzitazama karama/vipaji/zawadi za kiroho moja baada ya nyingine, tukiangalia mahala [katika maandiko] inapofundishwa kila karama, maana ya kila karama, matumizi yake, mafundisho/uelewa sahihi wa karama hiyo, ukomo wake (kama upo), uendelevu wake (kama upo), matumizi yake mabaya, n.k.

Karibu!
2. Makundi ya Karama za Kiroho.

Karama za kiroho hufanya kazi au hutumika tu wakati muumini anapokuwa katika Roho Mtakatifu, yaani amejitakasa kwa kutubu dhambi zake kwa Mungu Baba ndani ya nafsi yake mwenyewe, kufanya sala ya maombi ya kusaidiwa na Roho Mtakatifu katika suala lililo mbele ya muumini huyo, anaituma / anaielekeza sala yake kwa Mungu Baba katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, na hapo anaingia katika ‘fellowship’ na Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ufanisi au kiwango cha ufanyaji kazi wa karama ya/za kiroho ya/za muumini pia hutegemea kiwango cha upevu wa kiroho wa muumini huyu, yaani kiasi cha kanuni sahihi za Biblia ambazo amefanikiwa kujifunza [katika Roho Mtakatifu], kuziamini, na kuzitumia katika maisha yake.

Karama za kiroho zimegawanyika katika makundi mawili:

1. Karama za muda mfupi.
2. Karama za kudumu au za muda mrefu.

2.1 Karama za Muda Mfupi: Maelezo.

Karama hizi zilitumika katika Kanisa wakati sehemu ya maandiko au Biblia, ijulikanayo kama Agano Jipya haijakamilika, ijapokuwa Agano la Kale lilikuwa tayari katika ukamilifu wake. Vitabu vya Agano Jipya viliandikwa na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, wakiwa chini ya uvuvio (inspiration) wa Roho Mtakatifu
(kama ilivyokuwa kwa vile vitabu vya Agano la Kale). Hivyo, maandiko ya Agano Jipya yalikuwa bado hayajawekwa katika karatasi (papyrus kwa wakati huo), lakini kile kizazi cha Wakristo cha mitume wa Bwana wetu kilikuwa kinahitaji mafundisho ambayo sasa tunayaita Agano Jipya [kama ambavyo sisi tunavyoyahitaji]. Lakini mafundisho haya yalikuwa bado kuandikwa, hivyo Roho Mtakatifu alitoa vipaji mbalimbali ili kuwawezesha Wakristo wa wakati huo kuzipata kanuni za Agano Jipya kabla hazijakusanywa katika kitabu kimoja na kujumuishwa na yale mafundisho ya Agano la Kale ili nao waweze kukua kiroho kama ambavyo sisi wenye Agano hili tulivyo na fursa hii leo.

Sababu ya pili ya uwepo wa karama za muda mfupi ni katika kushuhudia ukweli wa mafundisho ya mitume wa Mungu. Hivyo mtume halisi wa Bwana (kwa mfano Petro) anaposimama na kufundisha akiwa katika uwezo wa Roho Mtakatifu, alifanya hivyo (kufundisha) na wakati huo huo alipewa karama ya kutenda miujiza ili ujumbe wake uonekane na kushuhudiwa kwamba umetoka kwa Mungu. Wakati ambao alikuwa akifundisha (mwendelezo wa mfano wa Petro) wageni kutoka mataifa mbalimbali waliokuwa na kiu ya Neno la Mungu ambao hawakuifahamu lugha ya Kiebrania au Kiyunani au Kiarami, basi Roho Mtakatifu alimpatia karama ya kunena lugha za hao wageni, na hivyo ujumbe wa Injili uliwafikia wageni hao; wakati huo huo palikuwa na muumini mwingine mwenye karama ya kutafsiri lugha, ambaye aliyatafsiri mafundisho hayo ya mtume Petro. Jisomee mwenyewe masharti ya kunena lugha kama yalivyowekwa katika maandiko na mtume Paulo – 1Wakor. 14:22-23; 27-28 – kunena lugha kulifanyika kwa mpangilio maalum, siyo kila mmoja kwa wakati mmoja!

Sababu ya tatu ya uwepo wa karama za muda mfupi wakati huo ilikuwa ni kusimika na kudhihirisha mamlaka ya mitume na waumini wa wakati huo. Mungu alitaka watumishi Wake wawe na mamlaka mbele za wale waliowafundisha Injili Yake, hivyo aliwapa karama mbalimbali ili kusimika na kudhihirisha mamlaka hayo katika mitume na watumishi Wake wengine.

Kwa njia hizi, zilizoelezwa vyema kabisa katika nyaraka za Paulo na katika kitabu cha Matendo ya Mitume, Wakristo wale wa mwanzo waliweza kupata Neno la Mungu ambalo walihakikishiwa [kwa miujiza, kwa kusikia katika lugha zao wenyewe, kwa kutafsiriwa] kwamba wanalisikia na kufundishwa Neno halisi la Mungu.

Hivyo basi, Mungu wetu aliwapatia karama hizi watumishi Wake, kwa muda tu, mpaka pale Agano Jipya lilipokamilika, mamlaka ya watumishi Wake yalipodhihirika wazi, ukweli wa mafundisho ya mitume Wake ulipoonekana na kushuhudiwa, na akazisitisha. Mfano, mtume Paulo alikuwa na karama ya uponyaji (healing); soma Matendo 14:8-10; Matendo 28:8-9 kuona uponyaji huu. Lakini baadaye Mungu alisitisha karama hii kwa Paulo; hii inaonekana katika Wafilipi 2:25-27 ambapo tunasoma habari za kuugua kwa Epaphroditus, mwenza wake Paulo, na kushindwa kwake kusafiri kwa sababu hiyo; Paulo alikuwa naye, lakini hakuweza kumponya, kwa sababu kufikia wakati huu Mungu alikwisha kuisitisha karama hii ya uponyaji kwa mtumishi Wake Paulo. Mfano mwingine tunauona katika 2Tim. 4:20, ambapo Trophimus alikuwa mgonjwa, na Paulo alilazimika kumwacha pale Miletus akaendelea na safari yake, kwa sababu hapa pia Paulo hakuweza kumponya Trophimus. Pia kuna ule mfano maarufu ambapo Paulo anamshauri Timoteo atumie mvinyo [kwa kuchanganya na maji yake ya kunywa] ili aweze kupata ahueni ya magonjwa yake ya mara kwa mara ya tumbo; hapa pia tunaona kwamba Paulo angemponya Timoteo, lakini hakuweza kufanya hivyo, kwa sababu Mungu alikwishaisitisha karama yake ya uponyaji kutoka kwa Paulo [kwani malengo ya kutolewa karama ile yalikwishatimia].

Hapo tumedhihirisha wazi kabisa kwamba kwa kweli kuna karama ambazo Mungu aliwapatia watumishi Wake wakati ule wa mitume kwa muda tu, na baadaye akazisitisha. Maana yake ni kwamba leo hii ijapokuwa bado tuko katika Enzi ya Kanisa, lakini karama hizi za muda zilikwisha koma pale pale mwanzo wa utumishi wa mitume, malengo ya karama hizo yalipotimizwa.

13.8  Upendo hautasitishwa kamwe; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.
13.9  Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu;
13.10  lakini itakapokuja ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilishwa [itasitishwa].
13.11  Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. 1Wakor. 13:8-11

Hapa chini, nitaweka tafsiri ya 1Wakor. 13:8-11 iliyopanuliwa [katika mabano] ili tuweze kuiona [kwa urahisi] maana halisi ya fundisho la Paulo:

13.8 Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ikiwa [tunajadili karama za] unabii, hizo zitakoma, au [tukijadili] karama za [kunena] lugha, nazo zitakoma, au [karama] ya maarifa, hiyo nayo itasitishwa.
13.9 Kwa maana tunapoitumia karama ya maarifa, matunda/[matokeo] yake ni sehemu [tu ya kile kilicho kamili]. Na pale tunapoitumia karama ya unabii [matunda/matokeo yake ni sehemu tu ya kile kilicho kamili].
13.10 Lakini kile kilicho kamili kitakapokuja (yaani, Biblia/maandiko yatakapokamilika na kupatikana kwa Kanisa), yote yaliyo kwa sehemu tu yatasitishwa.
13.11Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; bali nilipokuwa mtu mzima, nimeyasitisha mambo ya kitoto [yaani, karama za kunena lugha, unabii, uponyaji, n.k.]
1Wakor. 13:8-11

Nanukuu pia maandiko kutoka 2Petro 1:16-19, ambapo anatufundisha kwamba ingawa yeye [pamoja na Yakobo na Yohana] walishuhudia kwa macho na masikio yao wenyewe nguvu, utukufu na ukuu wa Bwana Yesu pale mlimani (Matt. 17:1-8), lakini hata hivyo anayachukulia maandiko kuwa ni “neno la unabii lililo imara zaidi”; 2Pet. 1:16-19:

1.16  Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake [mara ya pili]; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake.
1.17  Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu [kutoka mbinguni], Huyu ni Mwanangu, mpendwa Wangu, ninayependezwa Naye.
1.18  Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu.
1.19  Nasi [hata hivyo] tuna lile neno la unabii (yaani, Biblia) lililo imara zaidi (yaani kuliko yale niliyoyaona na kuyasikia pale mlimani), ambalo, mkiliangalia, kama taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka [siku] kutakapopambazuka, na Nyota ya Asubuhi kutokea (kurudi kwa Bwana katika utukufu).

Biblia, yaani maandiko, haina mgongano wa ndani kamwe! Anayoyasema Petro hapa yanaoana kwa asilimia 100 na yale yaliyonukuliwa kutoka kwa Paulo hapo juu. Maandiko, yaani Biblia iliyo kamili, ni ya kuaminika zaidi ya karama [za muda tu] kama kunena lugha, uponyaji, unabii, n.k. Kwa maneno mengine, Mkristo unaaagizwa kujifunza Neno la Mungu, kwani jukumu hilo ndilo lenye maana zaidi, na kwa kweli ndiyo shughuli kuu ya Mkristo; pata mafundisho ya Neno la Mungu (Biblia) badala ya kutegemea experiences za karama kama kunena lugha, uponyaji, unabii, n.k. ili kuuona na kujifunza utukufu na ukuu wa Mungu. Petro, Yakobo na Yohana waliuona utukufu na ukuu wa Bwana Yesu, lakini Petro huyo huyo anaagiza, katika nafasi yake kama Mtume wa Bwana, ulichukulie Neno lake Mungu kuwa “ni imara zaidi”. Paulo aliponya (Matendo 14:8-10); alinena lugha, tena “zaidi” ya wale Wakorintho (1Wakor. 14:18), lakini anasema katika aya inayofuata, ya 19: “lakini katika kanisa napenda kunena maneno matano kwa akili zangu, nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena maneno kumi elfu kwa lugha”. Ebu yatafakari maneno hayo ya Paulo, yana uzito mkubwa sana.

2.2 Karama za Kudumu au za Muda Mrefu: Maelezo.

Kundi la pili la karama ni lile la karama za kudumu au za muda mrefu. Maana ya usemi huu ni kwamba hizi ni karama ambazo ziko tangu mwanzo wa enzi ya Kanisa (mara baada ya kupaa mbinguni kwa Bwana wetu) mpaka leo na pia karama hizi zitaendelea mpaka kurejea kwa mara ya pili kwa Bwana wetu. Karama za Roho Mtakatifu ni sehemu muhimu sana katika ujenzi na uimarishaji wa Kanisa la Bwana wetu Yesu Kristo. Chukua mifano miwili tu ya karama za Uinjilisti (Evangelism) na nyingine ya Mchungaji-Mwalimu (Pastor-Teacher); wenye karama hii ya Uinjilisti wana uwezo mkubwa wa kuieneza Injili kwa wasioamini; lakini baada ya hapo anaingia Mchungaji-Mwalimu, ambaye atamfundisha maandiko na namna ya kuishi Kikristo muumini huyu mpya aliyeokolewa kupitia kwa kazi ya Mwinjilisti. Hapo tunaona mfano rahisi kabisa wa jinsi vipaji hivi vya Roho Mtakatifu vinavyoshirikiana katika kulijenga na kuliimarisha Kanisa la Bwana Yesu Kristo. Na kwa kweli Mkristo huyu mpya atapitia mikononi mwa Wakristo wenzake wengi tu ndani ya Kanisa ambao watampa ushirikiano wao, kutokana na karama walizopewa, na yeye mwenyewe atawapa ushirikiano wake, jinsi anavyozidi kukua kiroho, na matokeo yake – Kanisa la Kristo linajengwa. Kumbuka maneno ya mtume Paulo katika Waefeso 4:16: “… huukuza mwili [yaani, Kanisa] upate kujijenga wenyewe katika upendo”.

4.11  Naye [Kristo mwenyewe] alitoa [aliwateua] wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;
4.12  kwa kusudi la kuwakamilisha [kuwatayarisha] watakatifu [wote], hata kazi [yao] ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo [Kanisa Lake] ujengwe;
4.13  hata na sisi sote tutakapoufikia [lengo la] umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata [kila mmoja wetu] kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo [kiwango cha kupevuka ambacho kipimo chake ni Kristo];
4.14  ili tusiwe tena watoto wachanga [katika kuelewa kanuni za Biblia], tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.
4.15  Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.
4.16  Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili [yaani, Kanisa] upate kujijenga wenyewe katika upendo.
Waefe. 4:11-16

2.19 Kwani ni kutoka Chanzo hicho (yaani Kristo, aya ya 18) ndiyo mwili mzima [yaani, Kanisa] unapata mahitaji yake na kufundishwa katika viungo na misuli yake [yote], na [hivyo] kuzaa makuzi [ya mwili huo] yatokayo kwa Mungu.
Wakolosai 2:19

3. Uchambuzi wa Karama za Kiroho.

Ufuatao ni uchambuzi wa karama za kiroho, moja baada ya nyingine.

3.1 Karama za Kiroho za Muda Mfupi.

a. Karama ya Kiroho ya Utume (Apostleship):

Hii ni karama ya kwanza na ya juu kabisa. Karama hii inatajwa katika 1Wakor. 12:28, Waefe. 4:11, na mahala pengine.

12.28  Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina [mbalimbali] za lugha.
1Wakor. 12:28 SUV

4.11  Naye [Kristo mwenyewe] alitoa [aliwateua] wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;
4.12  kwa kusudi la kuwakamilisha [kuwatayarisha] watakatifu [wote], hata kazi [yao] ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo [Kanisa Lake] ujengwe;
Waefe. 4:11 SUV

Mifano ya Mitume ni Paulo, Petro, Yohana, n.k. Hao ndio wanaotajwa katika nukuu hizi mbili hapo juu. Kuna kundi lingine la mitume linalotajwa katika maandiko, mfano Barnabas, Yakobo, Apollo, Sylvanus, Timoteo, Tito, Apophroditus, n.k. ambao ni mitume katika maana ya wamisionari waasisi / chipukizi; hawa hawakuwa mitume waliopewa karama ya utume. Hawa walitumwa na mitume wa Bwana Yesu kama Wainjilisti wa mwanzo kabisa, wakienda katika maeneo mbalimbali ya misioni za Kikristo, na hivyo waliitwa mitume kwa maana hii.

Karama maalum ya utume ilitolewa kwa wanaume 12 pekee katika historia yote ya Kanisa: idadi hii ikijumuisha wanafunzi wa Bwana wetu 11 (Yuda Iskaryote hayumo katika hao 12) pamoja na Paulo, ambaye aliteuliwa na Bwana wetu mwenyewe, akiwa njiani kwenda Damascus. Hii ilikuwa karama ya muda mfupi, na ilisitishwa mara Mtume wa mwisho, Yohana, kufa baada ya kuandika kitabu cha Ufunuo.

15.7  baadaye [Kristo, ref. Aya ya 3] akamtokea Yakobo; tena na mitume wote;
15.8  na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi [Paulo], kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.
1Wakor. 15:7-10

Katika Matendo ya Mitume 1:23-27, chini ya uongozi wa Petro, ambaye kwa wakati huu alikuwa bado katika mchakato wa kukua kiroho (yaani alikuwa bado Mkristo mchanga), wale mitume 11 walifanya mkutano na kumchagua mtume wa 12. Maandiko yanaweka wazi kwamba karama zote za kiroho zinatolewa na Roho Mtakatifu. Mtume hachaguliwi na watu kamwe! Mitume wote, pamoja na Paulo, waliteuliwa na Bwana Yesu Mwenyewe. Na tunaona wazi kabisa hapo kwamba Mathias alichaguliwa na waumini wenzake, na baada ya hapo hakusikika tena! Katika enzi ya Kanisa, karama ya kiroho ya UTUME inabeba mamlaka makuu kuliko yote yaliyotolewa na Mungu. Mtume alikuwa na mamlaka juu ya makanisa yote yaliyokuwa ndani ya eneo lake. Ukilinganisha na leo, mchungaji/pastor ana mamlaka juu ya kanisa moja tu la eneo lake. Kitabu cha Matendo ya Mitume ni cha kihistoria, kinaorodhesha historia ya mwanzo ya Kanisa.

Karama ya utume ilikuwa na mamlaka na nguvu kubwa sana kwa wale waliokabidhiwa karama hii. Mifano: Petro katika kisa cha Ananias na mkewe Sapphira (Matendo 5:1-11) ambapo kwa sababu ya dhambi kadhaa walizozitenda dhidi ya Mungu (udanganyifu, tamaa, ufisadi, n.k.) katika tukio lile, Petro aliwaanzishia mchakato wa “dhambi ya kifo” dhidi yao na wote walikufa kifo cha maumivu na aibu, japokuwa waliokolewa (1Yoh. 5:16). Soma pia kisa cha yule mzinzi wa Korintho (1Wakor. 5:1-5) aliyekuwa akitenda dhambi na mke wa baba yake. Mtume Paulo alimwanzishia mchakato wa “dhambi ya kifo” (1Yoh. 5:16), tena kutoka mbali kabisa, na mtu huyo aliteseka kweli kweli. Katika kisa hiki tunaona kuwa mtu yule alitubu, akajirudi, ref. 2Wakor. 5-8.

b. Karama ya Kiroho ya Unabii (Prophecy).

Rejea 1Wakor. 12:28 na Waefe. 4:11 hapo juu. Cheo cha unabii kinatajwa katika Agano la Kale pia; katika Agano la Kale, wengi kati ya manabii walikuwa viongozi wa kitaifa pia, kama Eliyah, Isaya, n.k. Karama ya unabii inayozungumziwa hapa haihusiani na uongozi (cheo cha) wa kitaifa wa Israeli. Manabii wa Agano Jipya walifanya kazi na walikuwa na mamlaka ndani ya Kanisa pekee. Kimsingi, karama ya unabii ilimwezesha mwenye nayo kupata maono kutoka kwa Mungu yaliyoliongoza Kanisa, wakitoa tahadhari dhidi ya maamuzi yasiyo sahihi ya watu mbalimbali ndani ya Kanisa. Mfano wa kwanza, nabii aliyeitwa Agabus alitabiri (kwa uwezo wa Roho Mtakatifu) tukio la ukame na njaa katika ufalme wa Rumi, na kwa njia hiyo Wakristo waliweza kuwasaidia wenzao wa Yuda kwa kujitayarisha na chakula kabla ya njaa hiyo (Matendo 11:27-30). Mfano wa pili, nabii huyo huyo Agabus alimpa tahadhari/onyo Paulo asiende Yerusalemu (Matendo 21:10-14); [na hata Bwana wetu mwenyewe akampa onyo la kuondoka Yerusalemu (Matendo 22:17-18)]. Hata hivyo, Paulo alikaidi na kuenda Yerusalemu; kwa uamuzi huu Paulo aliteseka sana pale Yerusalemu; onyo hili lilitolewa na Mungu mwenyewe, kupitia Nabii Agabus, kwa makusudi na malengo Yake. Manabii walikuwa wanafunuliwa na Roho Mtakatifu maono ya matukio ya muda mfupi ujao yaliyowahusu Wakristo, kama tunavyoona hapa. Mifano ya Manabii katika kitabu cha Matendo ya Mitume ni Barnabas, Simeone, Lucius, Judas, Menaen, na watoto 4 wa kike wa Philip. Karama ya Unabii nayo ilikuwa karama ya muda mfupi, na ilisitishwa na Mungu katika kile kipindi cha mwanzoni cha Kanisa la Bwana wetu.

c. Karama ya Kiroho ya Kutenda Miujiza (Miracles).

Rejea nukuu ya 1Wakor. 12:28 na ya Waefe. 4:11 hapo juu. Karama ya kutenda miujiza ilitolewa kwa Mitume wa Bwana Yesu kwa malengo ya kuthibitisha na kuhakiki kuwa ujumbe wao wa Injili na mafundisho ya Neno la Mungu wakiwa kama Mitume Wake ulikuwa ni wa kweli na halisi. Yaani, waumini na watu wengine wangewezaje kujua kwamba mtu anayeitwa Paulo / Petro / Yohana / n.k. aliyekuja kuwapa mafundisho ya Injili na kanuni nyingine za Biblia kabla Agano Jipya halijaandikwa, kweli ni Mtume wa Mungu? Hakukuwa bado na Injili iliyoandikwa ili kuhakiki, kuthibitisha na kupima mafundisho ya Mitume na Wainjilisti wa mwanzo, kama sasa tulivyo na Biblia iliyo kamili. Hivyo Mitume na Manabii walipewa pia karama ya kutenda miujiza ili iweze kuthibitisha na kuhakiki kwamba kweli wao walikuwa Mitume na Manabii wa Bwana wetu. Hakuna muumini yeyote leo hii mwenye karama ya Roho Mtakatifu ya kutenda miujiza kwa sababu maandiko yamekamilika na yamefungwa. Hata hivyo, hii haina maana ya kwamba miujiza ya Mungu haifanyiki tena, kwani Mungu mwenyewe bado anafanya miujiza Yake katika maisha yetu moja kwa moja kutoka mbinguni, pale Anapoona mwujiza unahitajika, bali si kwa kupitia kwa Mitume na Manabii, kwani hao hawako tena.

d. Karama ya Kiroho ya Uponyaji (Healing).

Karama hii inatajwa katika 1Wakor. 12:9,28,30. Lengo la karama hii ya uponyaji lilikuwa ni kuelekeza fikra za waumini na watu wengine katika ujumbe wa Mitume na Manabii wa Mungu. Itakumbukwa kwamba lengo la karama ya miujiza lilikuwa kuelekeza fikra za waumini na watu wengine katika nafsi ya Mtume au Nabii wa Mungu. Hizi zilikuwa ni karama za kiroho zilizoonyesha nguvu na uwezo mkuu wa Mungu wetu; waliozishuhudia walishikwa na bumbuwazi, mshangao na tishio juu ya Mungu wetu. Watu waliokuwa na magonjwa walimgusa tu Mtume mmojawapo na papo hapo wakapona – bila kuchelewa hata sekunde moja. Wakati mwingine Mtume muhusika hakuwa hata na habari juu ya kiasi cha matumaini ambacho watu walikuwa nayo juu yake; mfano, katika Matendo 5:15-16 tunasoma kwamba watu wagonjwa walijipanga tu barabarani katika matumaini kwamba hata kivuli cha Mtume Petro kikiwapitia basi nao watapona pale pale! Aya ile ya 16 [nafikiri] inathibitisha tumaini lao hili. Soma pia taarifa za miujiza aliyotenda Mtume Paulo katika Matendo 19:11-12. Kama kuna shaka yoyote kuhusu hulka ya muda tu ya karama hii, basi tazama wale wanaodai kuwa na karama hii leo wanavyohangaika kwa masaa mengi kwa kelele na fujo na mgonjwa mmoja tu na mgonjwa huyo asipone kama wanavyodai!! Tuendelee. Mara baada ya hadhi yao kama Mitume, Manabii, n.k. ilipothibitishwa, Mungu alisitisha / akaiondoa karama hii kutoka kwa akina Paulo, Petro, na wengine. Tunawezaje kufahamu hili? Kwa sababu wawili kati ya wenza wa karibu kabisa wa Paulo walikuwa na matatizo ya kiafya na hakuweza kuwaponya; hili tunaliona baadaye kabisa katika maisha na utumishi wa Mtume Paulo na wenzake. Nanukuu kutoka katika “1. Karama za Muda Mfupi” hapo juu:

Lakini baadaye Mungu alisitisha karama hii kwa Paulo; hii inaonekana katika Wafilipi 2:25-27 ambapo tunasoma habari za kuugua kwa Epaphroditus, mwenza wake Paulo, na kushindwa kwake kusafiri kwa sababu hiyo; Paulo alikuwa naye, lakini hakuweza kumponya, kwa sababu kufikia wakati huu Mungu alikwisha kuisitisha karama hii ya uponyaji kwa mtumishi Wake Paulo. Mfano mwingine tunauona katika 2Tim. 4:20, ambapo Trophimus alikuwa mgonjwa, na Paulo alilazimika kumwacha pale Miletus akaendelea na safari yake, kwa sababu hapa pia Paulo hakuweza kumponya Trophimus. Pia kuna ule mfano maarufu ambapo Paulo anamshauri Timoteo atumie mvinyo [kwa kuchanganya na maji yake ya kunywa] ili aweze kupata ahueni ya magonjwa yake ya mara kwa mara ya tumbo; hapa pia tunaona kwamba Paulo angemponya Timoteo, lakini hakuweza kufanya hivyo, kwa sababu Mungu alikwishaisitisha karama yake ya uponyaji kutoka kwa Paulo [kwani malengo ya karama ile yalikwishatimia].
e. Karama ya Kiroho ya Kunena Lugha (Tongues).

Karama hii inatajwa katika 1Wakor. 12:10,28. Karama hii imeleta mgogoro na mabishano mengi katika historia ya hivi karibuni ya Kanisa, hata sasa. Karama hii nayo ilikuwa ni ya muda tu, katika kipindi cha mitume pekee. Baadaye ikasitishwa, hata kabla mitume wote hawajalala [kaburini]. Karama hii ilitabiriwa na Nabii Isaya katika Isaya 28:11 (jitahidi usome sura yote ya 28):

11 La, bali kwa midomo ya watu wageni, na kwa lugha nyingine atasema na watu hawa [Wayahudi];
Isaya 28:11 SUV

Katika kipindi hiki Israeli ilikuwa katika uasi kwa sehemu kubwa dhidi ya Mungu. Na Mungu aliwatabiria uharibifu mkuu utakaokuja dhidi yao na hatimaye kusambaratika kwa nchi yote, ambako kulikuja kutokea mwaka 70AD. Utabiri wa Isaya katika Isa. 28:11 ulitimia siku ya Pentecoste pale Roho Mtakatifu alipowapatia mitume uwezo wa kunena lugha za kigeni na Wayahudi waliokuja kuhiji katika nchi yao ya asili wakaisikia Injili katika lugha za kule nchi walikotoka! Hivyo karama hii iliwawezesha wenye nayo kusema lugha halisi za hapa duniani. Karama hii ilikuwa ya muda mfupi tu, nayo ikasitishwa. Hakuna mtu aliyeweza [kwa uhalali] kunena lugha tangu wakati karama hii ilipositishwa mpaka leo.

2.6 Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
2.7 Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?
2.8 Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?
2.9 Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia,
2.10 Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,
2.11 Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.
2.12 Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?
Matendo 2:6-12

Ndugu yangu, soma mwenyewe! Zilikuwa lugha halisi!

f. Karama ya Kiroho ya Kutafsiri Lugha (Interpretation of Tongues).

Hii ilikuwa karama ya muda tu. Inatajwa katika 1Wakor. 12:10,30. Karama hii iliambatana na karama ya kunena lugha. Karama hii ilifanya kazi wakati Wayahudi wasioamini wakiwamo katikati ya kundi la waumini; muumini / Mkristo mmoja atasimama na kuanza kunena Injili katika lugha tofauti na Kiebrania; hapo muumini mwingine mwenye karama ya kutafsiri lugha atasimama na kutoa tafsiri ya maneno hayo ya kigeni kwa Kiebrania, akieleza ujumbe wa Injili uliosemwa. Karama hii ilitumika na Roho Mtakatifu wakati wenye nayo wakiwa katikati ya kadamnasi, na wasioamini wakiwepo, na si vinginevyo. Kwani lengo lilikuwa ni kuonyesha ukuu, utakatifu na uweza wa Mungu.

g. Karama ya Kiroho ya Maarifa (Knowledge).

Karama hii inatajwa katika 1Wakor, 12:8 na 1Wakor. 13:8. Wakati ule ambapo vitabu vya Agano Jipya havijaandikwa na kukusanywa (yaani, Biblia haijakamailika), muumini mwenye karama hii alizijua kanuni zilizomo sasa katika Agano Jipya kupitia karama ya maarifa. Roho Mtakatifu alitoa (kupitia karama hii) elimu maalum na mahususi ambayo hapo baadaye ilikuja kuandikwa katika Agano Jipya. Karama hii ilifanya kazi bila ya mwenye nayo kujifunza maarifa aliyoyasema kutoka katika maandiko yaliyokuwako, yaani Agano la Kale; alishushiwa na Mungu moja kwa moja, kwa faida ya Wakristo wa wakati huo.

h. Karama ya Kiroho ya Hekima (Wisdom).

Karama hii inatajwa katika 1Wakor. 12:8. Karama hii ilimpatia mwenye nayo uwezo wa kueleza na kufundisha matumizi ya kanuni za Agano Jipya katika maisha ya Mkristo, kuiona nguvu ya kanuni hizi katika maisha ya Mkristo, kabla vitabu vya Agano Jipya lenyewe havijaandikwa. Hii ndiyo namna matumizi ya kanuni za Mungu kuhusiana na namna Mkristo alivyotakiwa kuishi ilivyofundishwa wakati huo.

i. Karama ya Kiroho ya Kushawishi (Exhortation).

Karama hii inatajwa katika War. 12:8. Hii nayo ilikuwa karama ya muda mfupi. Kabla ya Agano Jipya kuandikwa na kukamilika, katika siku za mwanzoni za Ukristo, kulikuwa na umuhimu wa karama hii ya kushawishi. Lakini, karama hii ni nini? Mwenye hii karama alishauri, alitia moyo, alifariji na alisihi Wakristo katika masuala na matatizo mbalimbali ya maisha ya Wakristo.

j. Karama ya Kiroho ya Kupambanua Kati ya Roho (Discerning Between Spirits).

Karama hii inatajwa katika 1Wakor. 12:10. Karama hii nayo ilikuwa ya muda tu. Kusudi lake lilikuwa ni kumwezesha mwenye nayo kupambanua kati ya mafundisho mbalimbali na kuwaelekeza Wakristo katika mafundisho na kanuni zilizokuwa sahihi, zilizotoka kwa Mungu. Hii ilikuwa muhimu sana katika wakati ambao Agano Jipya lilikuwa halijaandikwa na kukamilishwa, ijapokuwa Wakristo walikuwepo, hapo mwanzo kabisa wakati wa kipindi cha Mitume. Mitume walikuwa 12 tu, na hawakuweza kuwepo kimwili kila mahala walipokuwapo Wakristo. Baada ya Agano Jipya nalo kukamilika, karama hii haikuwa na uhitaji tena kwani neno la Biblia lilikuwako na lilitumika katika kulinganisha kati ya mafundisho ya kanuni za Biblia ya mwalimu / pastor na Neno lenyewe la Mungu.

k. Karama ya Imani (Faith).

Karama hii inatajwa katika 1Wakor. 12:9. Nayo ilikuwa ni karama ya muda tu, kabla ya kukamilika kwa maandiko. Karama hii ilifanya kazi namna gani? Manyanyaso dhidi ya Wakristo yalikuwa mengi na yalienea sana. Wakati waumini walipokuwa wanavunjwa moyo na shida za maisha yao, morale imeshuka katika kikundi chao mtu mwenye karama hii atainuka, atasimama na kuwaonyesha wenzake imani kuu, msimamo imara katika imani. Huyu atawatia moyo wenzake na kuwakumbusha kuwa na imani katika wokovu wa Bwana, kwamba utakuja. Bwana hakawii katika ahadi Zake, ijapokuwa sisi wanadamu tunaweza kuona hivyo; lakini wakati Wake wa wokovu ukifika ni lazima atafanya hivyo, nasi tunapaswa kujua kwamba wakati Wake ndio mwafaka kwetu.

Hapa ndiyo mwisho wa orodha hii ya Karama za muda mfupi za Roho Mtakatifu kama zilivyotajwa katika sehemu mbalimbali za Agano Jipya. Karama zote hizi 11 ziligawiwa na zilifanya kazi mara baada ya Pentekoste na zilisitishwa na Mungu baada ya kipindi cha uhai wa Mitume wa Bwana wetu na nyingine hata kabla ya Mitume wale 12 kufariki. Hii ilitokana na jinsi Mungu mwenyewe alivyoendelea kuzisimamia na kuona / kuamua wakati mwafaka wa kuzisitisha. Sasa na tuitizame tena nukuu ya 1Wakorintho 13:8-10, lakini safari hii ikiwa na mabano ya mraba yanayoeleza maana halisi ya aya hizo na misemo iliyo ndani yake:

13.8  Upendo hautasitishwa kamwe; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.
13.9  Kwa maana tunafahamu kwa sehemu [karama ya muda mfupi ya MAARIFA]; na tunafanya unabii kwa sehemu [karama ya muda mfupi ya UNABII];
13.10  lakini itakapokuja ile iliyo kamili [maandiko/Biblia itakapokamilika], iliyo kwa sehemu [karama za kiroho za muda mfupi] itabatilishwa [itasitishwa].
1Wakor. 13:8-10

3.2 Karama za Kudumu au za Muda Mrefu.

Karama hizi zinafanya kazi ndani ya Kanisa katika kipindi / enzi yote ya Kanisa. Je, unamwamini Bwana Yesu Kristo kuwa ni Mwokozi wako? Kama jibu lako la dhati kwa swali hili ni “ndiyo”, basi wewe unayo karama ya kiroho inayowezeshwa na Roho Mtakatifu. Swala linalobakia baada ya hapo ni: Ni karama gani uliyopewa? Waumini wote wako sawa katika jambo hili, kila muumini wa Bwana Yesu Kristo anayo angalau moja kati ya hizi karama za kiroho. Karama hizi zilikuwa zikifanya kazi / zikitumika kabla maandiko / Biblia haijakamilika na zinafanya kazi / zinatumika wakati wa kipindi / enzi ya Kanisa. Karama za kiroho za kudumu au za muda mrefu zitaendelea kutumika mpaka mwisho wa enzi ya Kanisa [kwani Kanisa litanyakuliwa wakati huo].

12.7  Lakini kila mmoja hupewa ufunuo (karama) wa Roho [Mtakatifu] kwa faida ya wote.
1Wakor. 12:7

12.11  lakini kazi hizi zote [zilizotajwa katika aya za 8-10] huzitenda Roho huyo huyo akimgawia kila mtu [muumini] peke yake kama aonavyo Yeye [kuwa ni sahihi].
1Wakor. 12:11

12.18  Bali Mungu ameviweka viungo kila kimoja katika Mwili (Kanisa) kama Alivyotaka [Mwenyewe].
1Wakor. 12:18

12.28  Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano [gift of HELPS], na uongozi [gift of ADMINISTRATION], na aina za lugha.
1Wakor. 12:28

Pale unapozaliwa upya (unapookolewa), Mungu Roho Mtakatifu anafanya uamuzi wa kukupatia angalau karama moja ya kiroho ambayo utaitumia katika utumishi wako ndani ya Kanisa. Kwa hakika, katika enzi ya Kanisa kuna mchanganyiko wa karama mbalimbali ndani ya muumini mmoja. Katika nukuu ya Waefeso 4:7-12, tunaona kwamba Bwana wetu Yesu Kristo ndiye anayegawa karama za kiroho, ambapo Mungu Roho Mtakatifu ndiye anayeziwezesha:

4.7  Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha [karama]/kipawa chake (anachokitoa) Kristo.
4.8  Hivyo husema, “Alipopaa juu Aliteka mateka (yaani, wale waumini waliookolewa kabla ya msalaba), Akawapa wanadamu vipawa”.
4.9  Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi?
4.10  Naye aliyeshuka ndiye Yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote (mpaka mbingu ya tatu, makazi ya sasa ya Baba), ili atimize mambo yote.
4.11  Naye [Kristo mwenyewe] alitoa [aliwateua] wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;
4.12  kwa kusudi la kuwakamilisha [kuwatayarisha] watakatifu [wote], hata kazi [yao] ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo [Kanisa Lake] ujengwe;
Waefe. 4:7-12

12.6 Sote tuna karama tofauti, kwa kadiri ya neema tulizopewa. Kama karama yako ni unabii, basi fanya unabii kulingana na imani yako;
12.7 kama karama yako ni kuhudumia, basi hudumu; ikiwa ni kufundisha, basi fundisha;
12.8 kama ni kutia moyo, basi tia watu moyo; kama ni kusaidia, basi toa msaada kwa moyo mweupe; mwenye karama ya uongozi / utawala, basi fanya hivyo kwa bidii; mwenye karama ya rehema, kwa tabasamu pana!
Warumi 12:6-8

Sasa na tujadili karama za kudumu katika enzi ya Kanisa. Ikumbukwe, kwa sasa tumo katika enzi hii ya Kanisa, iliyoanza Pentekoste na itaisha katika Ujio wa Pili wa Bwana wetu, ambapo tutaingia katika mileniamu.

a. Karama ya Kudumu ya Mchungaji-Mwalimu:

Ya kwanza katika orodha yetu ya karama za kudumu ni ile ya Mchungaji-Mwalimu. Karama hii, na kusudi lake, inatajwa katika Waefe. 4:11-12; 1Wakor. 12:28; . Karama hii imepangwa na Mungu itumike katika kikundi cha Wakristo nitakachokiita kanisa la msingi (tafsiri ya LOCAL CHURCH).

Kanisa la Msingi ni sehemu ya Mwili au Kanisa la Bwana Yesu Kristo ambalo ni jumuiya ya Wakristo [yaani, watu waliozaliwa upya] wote walio hai katika wakati wowote duniani kote. Kanisa la Msingi ni dogo, likijishughulisha katika mtaa, kijiji, sanasana kata, basi. Kanisa la Msingi hukutana kwa ratiba iliyopangwa mara kadhaa kwa wiki. Kanisa la Msingi halina madhehebu, wala siyo sehemu ya dhehebu lolote. Kazi zake kuu ni kufundisha Neno la Mungu (Biblia), kutoa fursa ya fellowship, kutoa fursa kwa karama ya kiroho ya kila Mkristo kufanya kazi, kwa kusudi la kumwezesha kila Mkristo kukua kiroho na kulijenga Kanisa/Mwili wa Kristo hapa duniani.

Kipindi cha Mitume (Apostles) kilipofika mwisho wake, yaani baada ya Mtume wa mwisho, Yohana, kuuawa, mfumo wa “kulisha kondoo” (Yohana 21:17) ukaanza kuendeshwa vile Biblia inavyofundisha kwamba unapaswa kuwa, yaani mfumo wa Kanisa la Msingi ulioelezwa katika ibara (paragraph) iliyopita. Neno la Mungu katika Kanisa la Msingi linafundishwa na Mchungaji-Mwalimu. Huyu ni mwanaume (1Tim. 3:1-7) mwenye karama ya kufundisha, aliyetayarishwa kwa kufundishwa Biblia ili naye aje kuwafundisha Wakristo hawa Neno la Mungu, akisaidiwa katika kazi hii na mfumo fulani rahisi wa uongozi / utawala utakaopangwa na wote, mfumo huu ukimsaidia katika kazi yake kwa kusimamia uendeshaji wa Kanisa zima la Msingi. Lengo pekee la mfumo huu rahisi wa kanisa kwa Mchungaji-Mwalimu ni kufundisha Neno la Mungu bila usumbufu / vikwazo vya kuhangaika na mambo kama fedha, n.k., ili kila Mkristo ndani ya Kanisa la Msingi aweze kufanikisha kusudi la kukua kiroho. Karama ya Mchungaji-Mwalimu itafanikisha kusudi lake la kuwawezesha Wakristo kukua kiroho ikiwa itapewa mazingira ya Kanisa la Msingi ili karama hii ifanye kazi. Hakuna ushahidi wowote katika Biblia unaoonyesha kwamba kuna mfumo wa kanisa juu na zaidi ya ule wa Kanisa la Msingi baada ya utumishi (wa muda) wa Mitume wale 12 wa Bwana wetu kufikia mwisho wake. Mfumo huu rahisi unaweza kuwa: Mchungaji-Mwalimu (wanaweza kuwa zaidi ya mmoja) + Kamati/Bodi ya Wazee + Wahudumu / mashemasi + Waumini Wote.

21.17 Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.
Yoh. 21:17 SUV

4.15  Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.
Waefe. 4:15 SUV

4.2  lihubiri Neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote katika mafundisho yako!
2Tim. 4:2

10.14  Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri [kufundisha ile kweli]?
War. 10:14 SUV

4.13  Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha.
4.14  Usiache kuitumia karama ile [ya kiroho ya Mchungaji-Mwalimu] iliyomo ndani yako, uliyopewa [na Roho Mtakatifu, ikatamkwa na ikathibitishwa] kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee.
1Tim. 4:13-14

b. Karama ya Kudumu ya Uinjilisti.

Ya pili katika orodha yetu ya karama za kudumu ni ile ya Mwinjilisti. Karama hii inatajwa katika Waefe. 4:11. Ufanyaji kazi wa karama hii ni kwamba watu watakutana au watakusanyika kupitia njia mbalimbali zilizoko za mawasiliano (uso kwa uso, radio, runinga, tovuti, machapisho, n.k.), na kusikiliza INJILI inayookoa ya Bwana wetu Yesu Kristo ikiwasilishwa kwao na mwenye karama hii; karama hii ina malengo ya kuwahudumia watu wasioamini. Karama hii inatumika haswa nje ya Kanisa la Msingi. Wakati karama hii inapotumika, watu hupata mvuto wa kumsikiliza mwenye nayo, nje (au wakati mwingine ndani) ya Kanisa la Msingi. Wasioamini watausikia ujumbe wa Injili na watauelewa, utaleta maana ndani ya mioyo yao [ikiwa kiu ya kuijua kweli imeiva]. Mungu wetu amepanga maisha ya kila mwanadamu katika namna ambayo imehakikisha kila mmoja wetu anafika katika njia panda mara kadhaa katika maisha yake, ambapo anakutana na fursa ya kuamua kumchagua Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya wokovu wa maisha yake, au la. Karama hii inampa mwenye nayo uwezo wa kuwafanya wasioamini kuyaelewa kwa ufasaha masuala yanayohusika katika wokovu wao, na hivyo kuwawezesha kufanya uamuzi sahihi katika suala hili muhimu kuliko yote katika maisha ya mwanadamu. Mfano kutoka katika Biblia:

21.8 Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili [yaani, Mwinjilisti], aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake.
Matendo 21:8

4.5  Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili [yaani, Mwinjilisti], timiliza huduma yako.
2Tim. 4:5 SUV

Wainjilisti wanapewa msukumo na Roho Mtakatifu wa ku-share / kuitangaza Injili bila hofu ya kukataliwa na kutengwa na watu wasioamini. Karama / kipawa hiki kinawawezesha kufanya mawasiliano na aina zote za watu na kwa njia mbalimbali zinazopatikana katika maisha yao.

7 Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu …!
Isaya 52:7 SUV

c. Karama ya Kudumu ya Utawala / Uongozi (Gift of Governments / Administration).

Karama hii inatajwa katika Warumi 12:8. Mwenye karama hii huratibu, hupanga, hutekeleza, hufuatilia shughuli mbalimbali za kimasijala, katibu-muhtasi, usafi, matumizi-fedha, misaada, usafiri, chakula, n.k. Katika Kanisa la Msingi, Wakristo wote wanaofanya shughuli za kiutawala [ambazo kwa hulka ya Kanisa la Msingi ni za kujitolea], wanayo karama hii. Mashemasi wanapaswa kuwa na karama hii; wasimamizi wa shughuli mbalimbali nao wanayo karama hii; Mchungaji-Mwalimu hana karama ya utawala / uongozi, wala hapaswi kujishughulisha na kazi hizi. Mtu aliye katika ajira rasmi ya uongozi katika idara za serikali, mashirika au sekta binafsi anaweza asiwe pia na karama hii [katika Kanisa la Msingi]; yaani mtu anaweza akawa na ufanisi mkubwa katika shughuli za utawala jeshini, serikalini, kampuni binafsi, na bado asiwe na karama ya utawala / uongozi, kwani karama hii ina kusudi la kuhudumia kwa ufanisi mkubwa katika Kanisa la Msingi na mahitaji yake.

Soma mfano mzuri wa jinsi karama hii inavyofanya kazi katika Matendo ya Mitume 6:1-4, ambapo ilitokea dharura ya mapungufu katika kugawa chakula kwa wajane wa Kiyunani, na jinsi kanisa zima walivyolitatua; waliteua Wakristo wenye karama ya uongozi / utawala kusimamia suala hilo:

6.1 Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Wayahudi wa Kiebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku [ya kutoa / kugawa chakula].
6.2 Wale Thenashara (yaani Mitume) wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuacha [kulifundisha] neno la Mungu na kuhudumu mezani!
6.3 Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili;
6.4 na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.
Matendo 6:1-4

d. Karama ya Kudumu ya Huduma (Spiritual Gift of Service).

Karama hii inatajwa katika Warumi 12:7. Mwenye karama hii aghalabu hutumika akiwa chini ya mwenye karama ya uongozi / utawala, hivyo Kanisa la Msingi ni muhimu liwe na Kamati ya Kudumu ya Utawala ambayo mwenyekiti wake ni Shemasi (Deacon). Wakristo walio katika kamati hii ni wale wenye karama ya kudumu ya huduma. NB.: Mchungaji hana karama ya utawala / uongozi. Kanisa la Msingi litashindwa kuendelea na kudumu bila ya kuwa na Wakristo wenye karama sahihi katika nafasi hizi muhimu. Mchungaji huunda na kutayarisha sera za Kanisa la Msingi; sera hizi zinapaswa kuoana na kuendana na Neno la Mungu. Mchungaji hapaswi kujishughulisha na mambo ya fedha za Kanisa la Msingi wala namna kanisa linavyoendeshwa. Katika makanisa ambapo Wachungaji wanajihusisha na fedha hapa Tanzania migogoro mingi na mikubwa imetokea na kusababisha Neno la Mungu na ufundishaji wake kuchukua kiti cha nyuma.

Karama hii ndipo wanawake wanaanza katika kupewa karama za kudumu za kiroho (1Tim. 2:12; 1Tim. 3:1-13; Tito 1:5-9); karama za (a), (b) na (c) hupewa wanaume tu. MUHIMU: Hili haliwazuii wanawake kuwafundisha wanawake wenzao, kufundisha watoto - wa kiume na wa kike, vijana, au kushiriki katika uinjilisti na utawala. Wanawake wana hulka wanazozaliwa nazo za ualimu, uinjilisti na utawala/uongozi na wanapaswa kuzitumia hizi katika kulijenga Kanisa.

e. Karama ya Kudumu ya Kusaidia (Helps).

Karama hii inatajwa katika 1Wakor. 12:28. Maelfu ya Wakristo wanayo karama hii. Kuwahudumia wagonjwa, wenye shida, walemavu, wasio na uwezo, wazee, yatima, n.k. Si wajibu wa Mchungaji-Mwalimu kutembelea wagonjwa, na wengine wenye shida; agizo hili halimo katika Biblia! Wala hana wajibu wa kuwatembelea watu. Lakini wale wenye karama ya kusaidia, hili ndilo jukumu lao kuu, na wanalifanya kwa furaha na ucheshi kabisa. Katika Warumi 12:8 karama hii inatajwa kama “wenye kukirimu” - SUV.

f. Karama ya Kudumu ya Kutoa Msaada (Giving).

Hii ni karama ya kutumia mali za dunia hii kwa faida ya kuridhisha mahitaji ya Wakristo wenzetu. Kila muumini ana wajibu wa kutoa msaada kulingana na mahitaji ya mwenzake/wenzake na kwa jinsi mahitaji hayo yanavyojitokeza katika maisha. Kutoa msaada siyo zaka/sadaka [kwa kimombo tithe]. TITHE ilikuwa kodi ya mapato katika taifa la Israeli la wakati ule, ambayo ilikuwa ni lazima kwa waumini na wasio waumini. Mwandishi atalijadili suala la zaka/sadaka/tithe katika somo maalumu kama hili katika siku za usoni. Suala la sadaka / zaka / tithe limekuwa chanzo cha vurugu katika makanisa/madhehebu hapa Tanzania. Karama hii inafaa kuonyeshwa au kutumiwa katika mazingira ya faragha (Soma Matt. 6:3-4).

g. Karama ya Kudumu ya Rehema (Mercy).

Karama hii inatajwa katika Warumi 12:8. Karama hii inahusiana na kuwaonyesha upendo watu, waumini na wasio waumini, wanaoonewa na kuteswa katika maeneo mbalimbali. Karama hii pia inafaa kutumiwa katika mazingira ya faragha (Matt. 6:3-4).

NB. Kuna karama nyingi, nyingi zaidi ya hizi zilizotajwa hapa juu, kutokana na Bwana anavyoona uhitaji wake katika Kanisa Lake. Mara nyingi wewe muumini hutajua ni karama gani uliyo nayo. Isipokuwa katika karama ya Mchungaji-Mwalimu na Uinjilisti, si jambo la lazima Mkristo kujua karama yako ni ipi. Kuhusiana na karama hizo mbili, ni lazima kuifahamu karama yako, na hili linatokea kwa jinsi unavyozidi kukua kiroho, kwa sababu karama hizi zinahitaji matayarisho makubwa na ya muda mrefu ya kujifunza kabla ya kuanza kutumika.

Katika 1Wakor. 12:15-21, Mtume Paulo anazungumzia desturi mbaya na matumizi mabaya ya karama za kiroho. Mojawapo kati ya desturi mbaya katika matumizi ya karama za kiroho ni kujaribu kuendeleza karama za muda mfupi za kiroho kama uponyaji, miujiza, kunena lugha, kutafsiri lugha, n.k. Karama za muda mfupi zilisitishwa katika kipindi kilekile cha Mitume, na kwa sasa hazitolewi na hazitumiki tena.
Pia kuwa na karama ya aina yoyote, kwa mfano karama ya Mchungaji-Mwalimu hakumfanyi muumini mmoja kujiona yeye ni bora zaidi au amependelewa na Mungu zaidi ya wengine. Wakristo wote ni sawa mbele za Bwana, hakuna aliye zaidi na hakuna aliye chini ya mwenzake. Kila mmoja wetu atatathminiwa na Bwana wetu kwa usawa, bila upendeleo, na atathawabiwa kutokana na jinsi alivyotumia fursa alizopewa na Bwana za kutumia karama aliyopewa katika maisha yake hapa duniani.

12.15  Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo?
12.16  Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo?
12.17  Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa?
12.18  Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka.
12.19  Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?
12.20  Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja.
12.21  Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi.
1Wakor. 12:15-21 SUV

3.10  Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake.
3.11  Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo.
3.12  Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri [itakapopimwa ubora wake].
3.13  Maana siku ile [ya hukumu] itaidhihirisha [jinsi ilivyo kiuhalisia], kwa kuwa [kazi hiyo] yafunuliwa [ubora wake] katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu [utaipima] kazi ya kila mtu, [ina ubora wa] namna gani.
3.14  Kazi ya mtu aliyoijenga juu [ya imani] yake [katika Kristo ikipona tathmini ya moto], atapata thawabu [kwa kazi hiyo].
3.15  Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara [ya kutothawabiwa]; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa [kupitia katikati ya] moto [ambao ulitathmini kazi yake na kuiona haina thamani na kuiunguza].
1Wakor. 3:10-15 SUV

Mungu anagawa karama za kiroho kwa utashi na uamuzi Wake mwenyewe, hakuna mwanadamu ‘anayestahili’ kupewa karama fulani ya kiroho. Hakuna muumini yeyote anayeweza kusema kwa wenzake kwamba ‘mimi sikuhitaji wewe’ kwa sababu ya karama yake. Karama zote zinategemeana kwa faida ya kulijenga Kanisa la Kristo.

12.4  Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja;
12.5  Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, na kila [kiungo kinasaidiana na kingine] mmoja kwa mwenzake.
12.6 Sote tuna karama tofauti, kwa kadiri ya neema tulizopewa. Kama karama yako ni unabii, basi fanya unabii kulingana na imani yako;
12.7 kama karama yako ni kuhudumia, basi hudumu; ikiwa ni kufundisha, basi fundisha;
12.8 kama ni kutia moyo, basi tia watu moyo; kama ni kusaidia, basi toa msaada kwa moyo mweupe; mwenye karama ya uongozi / utawala, basi fanya hivyo kwa bidii; mwenye karama ya rehema, kwa tabasamu pana!
War. 12:12:4-8

4 Madhara ya kuuchunguza, kujihusisha na kujiingiza katika “Ulimwengu wa Roho” : Tathmini ya Tukio Halisi la Kushambuliwa na Kuvurugwa na Pepo

Uchambuzi wa kisa kilichotokea huko Kijiji cha Ndama, Karagwe, Mkoa wa Kagera, katika kanisa la Pentekoste la “Huruma Katika Kristo”, ambapo waumini wa kanisa hilo waliocheza na “Ulimwengu wa Roho” [na matokeo yake] walivurugiwa maisha yao kwa kiasi kikubwa sana na malaika waasi au pepo, kwa kimombo “demons”.

Vyanzo vya habari.

Kuna vyanzo 3 vya habari vilivyoweza kupatika na mwandishi:

1. Link hii: https://www.youtube.com/watch?v=XNg-pPKPSPY ya MillardAyo Tv kupitia YouTube, ya tarehe 8 May 2017, yenye kichwa cha habari: “HII KALI: Mchungaji aliyeoa mke wa muumini wake Kagera”.

2. Ripoti ya www.eatv.tv ya 9 May 2017, yenye kichwa cha habari: “Mchungaji anaishi na wake za watu Kagera”.

3. Kutoka Global Publishers: “Ripoti Kamili Ya Mchungaji Aliyeoa Mke wa Muumini, Aongea na Risasi”, May 14, 2017.

Ndugu msomaji, unaweza uka-Google na kupata taarifa kamili ambazo zinafanana sana, kutoka katika vyanzo vyote hivyo 3 vya habari hii ya kushtua na kusikitisha.
Wahusika Wakuu.
Wahusika wakuu ni 1. J. J ambaye ndiye Mchungaji wa kanisa la Pentekoste la “Huruma Katika Kristo”.
2. D. D. ambaye ni Shemasi wa kanisa hilo, mke wa D.A.
3. D. A. ambaye ni mume wa Shemasi huyo.
4. Mke wa Mchungaji.
5. Waumini wa kanisa hilo.
Onyo kutoka kwa Mungu:
1.8  Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiria ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiria, na alaaniwe [na Mungu].
Wagalatia 1:8
18 Wala usizini.
Kumb. 5:18 SUV

21 Wala usimtamani mke wa jirani yako;
Kumb. 5:21a

Taarifa ya tukio kwa ufupi:
Waumini wa kanisa hili walikuwa na desturi ya “kuingia katika Ulimwengu wa Roho” kwa njia ambazo hazitajwi bayana katika vyanzo hivi vyote 3. Katika muda mrefu wa kufanya hivyo, wahusika wetu wakuu, kwa nyakati tofauti walimwona “malaika” ambaye wote walisadiki kwamba “alitoka kwa Mungu” kwa jinsi alivyokuwa wa ajabu na mwenye mvuto, na waliamini kwamba aliyoyasema yalikuwa ujumbe kutoka kwa Mungu mwenyewe. Malaika huyo, ambaye waumini hao hawapambanui kuwa ni “pepo” - kutoka kwa jeshi la Shetani au “malaika mwema” - kutoka katika jeshi la Mungu, aliwapa ujumbe unaofanana katika nyakati tofauti ambao uliwaagiza waumini hao hivi: “Mungu” amesema kwamba mke wa Mchungaji, D. D., hafai kuwa katika nafasi hiyo, na aondoke; Shemasi, ambaye ni mke wa muumini D. A. aachane / atalikiane na mume wake huyo na aolewe na Mchungaji J.J; mume wa Shemasi, D. A., hafai kuwa katika nafasi hiyo, naye “aondoke”. Waumini hawa waliuamini ujumbe wa malaika huyu kuwa ni maagizo ya Mungu, na wakafuata maagizo hayo kama yalivyotolewa kwao na malaika huyo. Baadhi ya wanakanisa walipinga na wengine waliafiki mambo hayo. Hata hivyo wanakijiji wengi walipinga kile walichokiona kuwa ni “uchafu” na wakatoa ripoti polisi. Fujo zilianza kunukia kijijini hapo. Ndipo Mkuu wa wilaya hiyo alipoingilia kati …

Uchambuzi wa tukio.
Wana-kanisa hili, wakiongozwa na Mchungaji wao, walikuwa na desturi ya “kuingia katika ulimwengu wa roho”. Hili linasemwa wazi katika clip ya Youtube ya MillardAyo na D.D. ambaye ni Shemasi wa kanisa hili na mke wa muumini mmojawapo, D.A. Suala hili la “kuingia katika ulimwengu wa roho” linaleta maswali kadhaa:
Swali 1: Walikuwa “wanaingia katika ulimwengu wa roho” kufanya na/au kutafuta nini?
Swali hili ni vigumu kulijibu kwa mtu ambaye anafuata mafundisho sahihi ya Biblia ambayo kwa kweli hayatoi ruksa kwa Mkristo “kuingia katika ulimwengu wa roho” yeye mwenyewe. Na katika maelezo yao, Mchungaji, Shemasi, mume wa Shemasi, wote hawakulisema lengo lao la “kuingia katika ulimwengu wa roho”. Ninaweza kusema kwamba kwa dalili nilizoziona kwa watu wenye tabia au desturi hii ni kwamba ukiisha fanya jambo hili mara moja, inakuwa kama vile “umeonja unga” na ukauona “utamu wake”, ijapokuwa ni tabia / desturi hatari kwako – kama ambavyo tumeona matatizo yaliyowakuta wana-kanisa hawa wa Karagwe. Watu wengine hufikiri kwamba watapata uwezo wa kuwatambua wachawi, watapata utajiri, watakuwa na nguvu za kiroho zitakazowafanikisha kushinda adui zao wa hapa duniani, watapata fursa ya “kuongea” na Mungu, sala zao zitasikilizwa haraka na Mungu, n.k. Lakini kwa kweli “faida” hizi zote ni kinyume na matakwa ya Mungu. Uhusiano wa Mkristo na Mungu wake ni wa neema, na hii inapelekea kwenye sala, maombi kwa Mungu Baba, katika Jina la Bwana Yesu Kristo, kila tunapokuwa na uhitaji wa kitu chochote. Na si kuingia sisi wenyewe katika ulimwengu wa roho na kujitwalia huko “uwezo” tunaofikiri tunauhitaji.
Matt. 18:19-20:
18.19 Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.
18.20 Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.

Yoh. 14:13 SUV:
14.13 Nanyi mkiomba lo lote [kwa Baba] kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
14.14 Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.

Nukuu hizi mbili hapo juu za maneno ya Bwana wetu zinaainisha fundisho hili kwamba Mkristo hajitwalii yeye mwenyewe anachokihitaji kwa “kuingia katika ulimwengu wa roho”, bali anaomba kwa Mungu. Narudia, uhusiano wetu na Mungu wetu ni wa neema!

Swali 2: Je kuna agizo katika Biblia kutoka kwa Mungu linaloamuru / linaloruhusu wanadamu “waumini” na “wasiokuwa waumini” kuingia katika “ulimwengu wa roho”?
Ebu soma hii nukuu:
5.4 Hivyo, mtakapokusanyika, nami nikiwa pamoja nanyi katika roho, na uweza wa Bwana wetu Yesu Kristo ukiwapo [kati yetu];
5.5 mtamkabidhi mtu huyo kwa Shetani, ili mwili wake uharibiwe, bali roho yake iweze kuokolewa katika ile siku ya Bwana wetu. 1Wakor. 5:4-5 SUV

Maandishi katika italiki/mlazo hapo juu yanatoa jibu zuri na sahihi kabisa kwa swali hili. Bwana wetu Yesu Kristo ni Mungu. Tunaweza kuingia katika ulimwengu wa roho ikiwa tuko na Bwana Mwenyewe! Mungu anajua hatari zilizoko katika ulimwengu wa roho, kwamba huko kuna uwepo wa Shetani na malaika wake waasi. Sisi hatuwaoni, lakini viumbe wenzetu hawa wanatutizama wakati wote (Waebr. 12:1-2a), wale wema wanatutizama kwa shauku ya kuuona mpango wa Mungu [yaani historia] ukifunuliwa na kuendelea mbele za macho yao, na Mungu mwenyewe akiwatuma [hao malaika wema] kuja kutusaidia ikiwa tunaomba msaada Kwake katika kipindi cha magumu (soma Danieli 10:2-3; 5-12); lakini wale wabaya wanatutizama ili watusome na kuona mbinu za namna ya kutukwaza na kutuangusha ili tushindwe katika mwendo wetu wa imani na kukua kiroho, soma Danieli 10:13-14; Ayubu 1 na 2). Mkristo, kama una shida, omba, sali kwa Mungu Baba katika imani kwamba Yeye anajua namna ya kukusaidia, na atakusaidia. Mungu hujibu kila sala [kuna kanuni za kusali pia!), ijapokuwa wakati mwingine sisi wanadamu huona kama vile anachelewa, lakini sala ikijibiwa papo hapo, imani yako itadhihirika vipi? Kwa Mkristo halisi, fursa yako ya kuingia katika ulimwengu wa roho ni katika sala na maombi pekee, ukitubu dhambi zako kwanza na kisha ukimshukuru Mungu kwa neema zake na hapo ndipo utampelekea maombi yako, katika Jina la Bwana Yesu Kristo. Usipofuata kanuni hii utaingia katika ulimwengu wa roho, lakini, utajikuta katikati ya pepo (malaika wabaya) ambao sisi wanadamu, hasa Wakristo, ni adui zao na watafanya kila wanaloweza kutukwaza – na hawa wenzetu wana nguvu kuliko sisi! Kuna ushahidi tosha katika kisa hiki kuona kwamba haya ndiyo yaliyowasibu hawa ndugu zetu wa Karagwe – tunapoona matokeo ya mazoezi yao ya kuingia katika ulimwengu wa roho.

Swali 3: Je, kuna mifano ya watu fulani katika Biblia ambao waliingia katika ulimwengu wa roho?
Nitatoa mifano kadhaa hapa, kutoka katika Biblia, ya waumini ambao kwa wazi kabisa waliingia katika ulimwengu wa roho. Petro, Paulo, Danieli, Yohana, Ezekieli, Isaya, n.k. waliingia katika ulimwengu wa roho.
- Petro: Soma Matendo 5:1-11; Matendo 10:9-17; soma pia 2Pet. 3:10-12
- Paulo: Soma 2Wakor. 12: 1-4, 6-7
- Yohana: Soma kitabu chote cha Ufunuo
- Danieli: Soma Danieli 7-8; 10-12
- Ezekieli: Soma sura za mwanzo
- Isaya: Soma kitabu cha Isaya
Ukisoma sehemu hizi chache za Biblia utaona mwenyewe kwamba kwanza, hao ni mitume na manabii waliopendwa na Mungu kwani walitimiza matakwa Yake; pili, Mungu Mwenyewe aliwaingiza katika ulimwengu wa roho, na siyo wao wenyewe kwa kutaka; tatu, Mungu aliwaingiza humo kwa malengo Yake maalum, ambayo yanaonekana na yanaelezwa wazi ukisoma sehemu hizo za Biblia; nne, wakiwa ndani ya ulimwengu wa roho, malaika wema waliotumwa na Mungu Mwenyewe kwa kazi hiyo walimlinda Danieli, Yohana aliongozwa sehemu mbali mbali na Bwana Yesu na malaika wema, Petro aliongozwa na Roho Mtakatifu Mwenyewe. Paulo hakusimulia tukio lake kwa utondoti (in detail). Ezekieli alitokewa na Bwana Yesu Mwenyewe (Christophany). Sasa hawa ndugu zetu wa Karagwe waliingia katika ulimwengu wa roho kwa uongozi na ulinzi wa nani!? Kwa kutizama yale madhara makubwa yaliyowakuta, ni wazi hawakuwa na ulinzi wa Mungu katika safari zao hizo za hatari ndani ya ulimwengu wa roho.
Ebu tukichunguze kwa ufupi kisa kinachosimuliwa katika 1Samweli 28, ambapo mfalme Sauli anapofungiwa mlango wa mawasiliano na Mungu Mwenyewe, anaamua kuvunja amri ya Mungu (Kutoka 22:18; Walawi 19:26b) na kutafuta kuingia katika ulimwengu wa roho kwa njia ya “mwanamke mwenye pepo wa utambuzi” au ‘medium’ kwa kimombo. Tizama mshangao na woga wa mwanamke yule anapomwona Samweli [ambaye alikwishakufa] akiwa katika mwili wa mpito ambao nao una utukufu mkuu anatokea; mwanamke yule anamwelezea Samweli kuwa ni mungu (tizama ile ‘m’ ndogo!) kwa maana ya mfano wa malaika. Ni wazi hili halijawahi kumtokea hata mara moja, kwa kuangalia mshangao na woga wake. Mwanamke huyu alikuwa akidanganywa tu na pepo katika kazi yake hii. Mungu aliingilia kati hapa ili Sauli apate ujumbe licha ya kwamba Alishakataza wana wa Israeli kujihusisha na pepo kwa njia ya waganga wa kienyeji. Kuingilia kati kwa Mungu katika suala hili kulimwezesha Sauli kujua majaliwa yake na ya baadhi wa watoto wake ambayo yalitimia siku ya pili yake katika vita na Wafilisti.
18 Usimwache mwanamke mchawi kuishi.
Kutoka 22:18 NB: Hatuko katika taifa la Israeli, nimenukuu aya hii kukuonyesha msomaji jinsi Mungu anavyolichukulia suala hili. Hapendi kabisa ujishirikishe na pepo! Hapo katika enzi ya Wayahudi, watu hao waliuawa mara wakibainika!

26 ... wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi (mediums).
Walawi 19:26b

Swali 4: Wana-kanisa hawa walikuwa wanaingia katika “ulimwengu wa roho” kwa njia au mbinu gani?
Katika clip ya video, na pia hata makala zile mbili nyingine, hakuna taarifa zinazoonyesha namna au mbinu walizozitumia au waliyoitumia katika kufanikisha mazoezi yao ya kuingia katika ulimwengu wa roho. Lakini katika uzoefu wa mwandishi wa kuyachunguza madhehebu ya namna hii (mitandao imejaa habari za madhehebu ya namna hii), watu hawa huingia katika ulimwengu wa roho kwa “kunena lugha” huku wakipandisha hisia kali. Sasa, ikumbukwe kwamba katika uchambuzi hapo juu, tumeona kwamba kunena lugha ni karama ya Roho Mtakatifu iliyositishwa tangu wakati ule ule wa Mitume. Sasa, hawa ndugu zetu wananena lugha gani!? Na pia tumeona hapo juu kwamba Mungu Mwenyewe aliwaingiza katika ulimwengu wa roho (kwa malengo Yake) watu aliowachagua. Na hili lilitokea mara chache sana katika Biblia, jambo ambalo linaonyesha wazi Mungu analipa uzito zoezi hili. Kwamba si la kufanyika kiholela, kwani madhara yake ni mazito ikiwa hakuna uongozi na ulinzi Wake.
Swali 5: Je, ile tahadhari ya 1Yoh. 4:1-6 ya … “zijaribuni hizo roho, [ili muone] kama zimetoka kwa Mungu [au la]” … ilifuatwa na wana-kanisa hawa?
Ebu tuone nukuu hii inasemaje:
1Yoh. 4:1-6:
4.1  Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, [ili muone] kwamba zimetokana na Mungu [au la]; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.
4.2  Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho inayokiri kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili [yaani ujumbe wa Injili] yatokana na Mungu.
4.3  Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.
4.4  Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia [i.e. Shetani na pepo].
4.5  Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia.
4.6  Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.

Je, nia na kusudi la Mungu haliko wazi kabisa katika nukuu hii hapa? Wakristo tunapaswa “kuzijaribu roho”, maana yake, tunapaswa kuyaweka kwenye mzani mafundisho na maagizo yoyote ya mchungaji-mwalimu, malaika, shemasi, n.k. anayetuambia kwamba yeye ana maagizo kutoka kwa Mungu, na kuyapima na Neno halisi la Mungu, yaani Biblia, ili tuone kwamba yanaendana au la! Ikiwa kuna mgongano wowote kati ya sehemu hizo mbili, basi mafundisho ya mchungaji-mwalimu huyo, malaika huyo, shemasi huyo, n.k. yanapaswa kutupwa nje! Sasa, tutawezaje kuyapima mafundisho hayo dhidi ya Biblia kama hatuijui Biblia? Hapo ndipo agizo la kujifunza Neno la Mungu linapoingia; hili ni agizo kwa kila Mkristo: soma Biblia wewe mwenyewe, pata mafunzo ya Biblia kutoka kwa mchungaji-mwalimu aliyejitayarisha na anayeonekana kuwa yu sahihi katika mafundisho yake, sali / omba kwa Mungu akuongoze, na utaanza kukua kiroho, hali ambayo itakuwezesha kupambanua ukweli na uwongo pindi mtu yoyote atakapojaribu kukuingiza katika desturi hatari namna hii.

Mathayo 5:32:
5.32 lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati (ngono nje ya ndoa), amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, [naye] azini.

Tizama vizuri nukuu hapo juu. Sababu pekee halali ya kuvunjika kwa ndoa ni uzinzi. Lakini ndugu zetu hawa wa kanisa la Pentecoste la “Huruma Katika Kristo” waliambiwa na malaika yule kwamba Shemasi amwache mume wake, Mchungaji amwache mke wake, halafu Shemasi aolewe na Mchungaji, bila ya kuwako kosa lolote kwa pande zote hizi mbili. Na ndugu zetu hawa walitii agizo la malaika huyo!! “Hawakuujaribu” ujumbe huu kwa kuulinganisha na kanuni za Biblia. Je, ujumbe huu, kwa kiwango halali cha Biblia, ulitoka kwa Mungu? Jibu ni hapana. Yule alikuwa pepo, malaika mbaya. Lakini ujumbe huu ulitoka ulimwengu wa roho! Msomaji wangu, unaiona hatari iliyoko ya kubarizi katika ulimwengu wa roho bila ulinzi wala agizo la Mungu? Mungu hawezi kukuagiza uvunje sheria Yake Mwenyewe, kamwe.

Mume wa Shemasi, bwana D. A. alichukulia tukio la ‘jogoo wake kutowika’ kuwa ni uhakiki kwamba hiyo ni sms kutoka kwa Mungu inayomwagiza amtaliki / amwache mke wake, Shemasi D.D. Kwa kweli alishangaa, nami nina uhakika kwamba wewe msomaji utasumbuliwa na tukio hili. Ili kuona nguvu ya pepo, ebu soma nukuu hii:

Marko 5:1-13:
5.1 Wakafika ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi.
5.2 Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;
5.3 makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;
5.4 kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda.
5.5 Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe.
5.6 Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia;
5.7 akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese.
5.8 Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.
5.9 Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi.
5.10 Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile.
5.11 Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha.
5.12 Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao.
5.13 Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini.

Hiyo ndiyo nguvu ya pepo. Hawa viumbe wenzetu wana uwezo kuliko sisi (miili yao haifi, wanasafiri haraka sana, hawaonekani kwa macho yetu japo wao wanatuona, n.k.). Na pia ni wajanja sana, na ni maadui kabisa wa wanadamu. Pepo hawakufurahia kitendo cha Mungu kuumba Binadamu. Bila ya ulinzi wa Mungu, hatuwawezi kamwe. Sasa, kama waliweza kumfanya huyu mtu aliyeishi makaburini awe na nguvu namna ile asiweze kushikika, watashindwa kumzuia “jogoo wa mume wa Shemasi asiwike!?” Kwa hakika hili ni suala dogo sana kwa viumbe hawa wa kiroho. Nami nina uhakika karibu asilimia 100 kwamba mume wa Shemasi alikuwa chini ya ushawishi wa kiroho wa pepo ili yule “jogoo wake ashindwe kuwika” na hivyo pepo wale wafanikishe kusudi lao la kulipoteza kundi hili la “Kanisa la Pentekoste la Huruma Katika Kristo”. Unauona udanganyifu wa pepo hapo? Hakika ni muhimu sana “kuzijaribu roho, ili kuona kama zinatoka kwa Mungu au la!”

Kinyume na pepo, malaika wa mbinguni wako upande wetu:

15.7 Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.
Luka 15:7 SUV

1.14  Je! Hao wote (malaika, aya 13) si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?
Waebr. 1:14 SUV

5. Mtazamo Sahihi wa Kibiblia Kuhusu Karama za Kiroho.

3 Usiwe na miungu mingine ila Mimi.
Exodus 20: 3 SUV

Ulimwengu wa roho [unaweza kuuita ‘the super-natural world’] una:
1. Mungu Mwenyewe katika Utatu Wake: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
2. Malaika wema ambao hawakushiriki katika uasi wa Shetani na malaika wenzake. Hawa ni watumishi wa Mungu na hufanya yale yote wanayoagizwa na Mungu. Mwanadamu hana agizo wala fundisho la kujihusisha na hao moja kwa moja kama ambavyo madhehebu fulani yanafundisha [mfano “Sala kwa malaika mlinzi” ya Kanisa Katoliki]. Muumini utasali na kuomba kwa Mungu, utamwachia Yeye maombi yako, na Yeye anajua namna atakavyojibu sala na maombi yako; ikiwa Atamtuma malaika, kama alivyojibiwa Danieli katika mifano ya hapo juu, au Atakusaidia kwa kuwatumia wanadamu wengine, au Atakusaidia moja kwa moja Yeye Mwenyewe, hayo ni maamuzi Yake Mungu.
3. Malaika wabaya au pepo ambao, wakiongozwa na Shetani, waliasi dhidi ya Mungu dahari nyingi zilizopita. Hawa wanatuchukulia sisi wanadamu kuwa ni adui zao; wao hufanya yote wanayoweza [chini ya uongozi wa Shetani] ili kutukwaza, kutuangusha, kutuharibia mwendo wetu, kutudanganya, kututesa, n.k. Hata hivyo hawawezi kufanya hayo bila uangalizi wa karibu kabisa wa Mungu Mwenyewe, ambaye amewawekea mipaka ya majaribu yao; na katika hili Mungu anawatumia katika kuwakomaza na kuwaimarisha waumini Wake katika imani yao kwa kuruhusu magumu hayo mbalimbali yawapitie (1Pet. 1:3-9). Kitabu cha Ayubu kinafundisha wazi somo hili (Ayubu 1, 2). Pia majaribu aliyopitia Bwana wetu Yesu yanafundisha na kutoa mifano ya jambo hili (Matt. 4:1-11). Kitabu cha Matendo ya Mitume pia nacho kina mafundisho haya (kupitia mateso makuu waliyopitia Mitume wote na waumini wengine).
4. Wanadamu wenzetu waliokufa ambao wako katika makundi mawili:
a) Wale walio mbinguni kutokana na kufanya uamuzi sahihi wakati walipokuwa hapa duniani.
b) Wale walioachwa/waliotengwa na Mungu kwa sababu hawakumchagua Bwana wetu wakati wakiwa hapa duniani.

Sasa, sisi wanadamu tulio hai hapa duniani kwa wakati huu hatuwezi kamwe kuwa na mahusiano yoyote na kundi namba 4 hapo juu (Luke 16:27-31). Hata hivyo pepo hudanganya watu kwamba wanaweza kuongea na ndugu zao waliokufa. Hili halifanyiki kamwe. Kisa cha Sauli na yule mama mchawi wa Endori kiliwezeshwa na Mungu Mwenyewe, ili kumpa mfalme Sauli ujumbe wa matukio ya kesho yake vitani (1Samweli 28). Hii inathibitishwa na ukweli kwamba pepo ni viumbe, hawana uwezo wa kujua nini kitatokea kesho, kama ambavyo sisi wanadamu hatuna uwezo huo.

Rejea namba 1, 2 na 3 hapo juu. Sisi wanadamu tunaweza kuwasiliana na:

1. Mungu Mwenyewe, kupitia sala, maombi na Neno Lake,
2. Malaika wema ikiwa TU Mungu amewatuma, kuna mifano mingi katika Biblia, na
3. Malaika wabaya (pepo) ikiwa sisi tutalazimisha mawasiliano hayo, kwa kupiga ramli, kuwaruhusu wamiliki utashi wetu (demon posession), n.k. (lakini tuelewe kwamba hili limekatazwa kabisa na Mungu na lina matokeo mabaya kwetu, kama mfano halisi wa yaliyowakuta hawa ndugu zetu za Karagwe unavyodhihirisha).

5.1 Kutoa Pepo (Exorcism).

Pepo huingia na kumiliki mwili wa mwanadamu kwa ruksa ya huyo mwanadamu mwenyewe; baadhi yetu husalimu utashi wao, kwa sababu yoyote ile, kwa pepo, na hivyo pepo huyo anamiliki sehemu kubwa ya utashi, akili, mwili na dhamiri ya mtu huyu. Hili linapotokea, mwanadamu mwingine hawezi kumtoa pepo huyu (exorcism); ni Mungu ndiye anaweza kulifanya jambo hili. Hata hivyo kuna baadhi ya watumishi wa Mungu waliopewa, kwa nyakati fulani, karama na Mungu mwenyewe ya kuiita nguvu hii ya Mungu ili kuweza kutoa pepo. Hii ilikuwa sehemu ya karama za Mitume wale 12, mara walipowezeshwa (Matt. 10:1,8; Marko 6:7; Luka 9:1); Bwana Yesu alitoa pepo [hili halina haja ya maelezo]. Mitume wake 12 walitoa pepo, wale wanafunzi 72 walitoa pepo (Luka 10:1). Maandiko yanaonyesha kwamba wakati wa maisha ya Bwana wetu hapa duniani, kulikuwa na waumini wengine waliotoa pepo (Marko 9:38) na walifanya hivyo kwa uhalali kabisa kama ambavyo majibu ya Bwana wetu kwa swali la Yohana katika Marko 9:37 yanavyoonyesha. Katika kitabu cha Matendo ya Mitume tunamwona Mtume Petro na Mitume wengine wakitoa pepo (Matendo 5:14-16); Mtume Paulo baada ya kuokolewa (Matendo 16:16-18; 19:12); tunamwona Filipo Mwinjilisti / Shemasi akitoa pepo (Matendo 8:7); yawezekana pia viongozi wengine katika Kanisa la wakati ule walipewa uwezo wa kutoa pepo pia. Kama ilivyokuwa kwa Bwana wetu, vivyo hivyo ilivyokuwa kwa Mitume na viongozi wengine wa Kanisa katika siku zile za mwanzo za Enzi ya Kanisa, kwamba kazi za kimiujiza kama hii ya kutoa pepo iliwezeshwa na Mungu kwa malengo ya kusimika na kuonyesha mamlaka ya wale waliotenda miujiza hiyo ili kudhihirisha kwamba ujumbe wao ulitoka kwa Mungu kweli. Matukio yanayotafsiriwa kuwa ni kutoa pepo leo hii ni sehemu ya udanganyifu wa Shetani na pepo wake katika enzi ya Kanisa. Hakuna mtu yeyote katika Agano la Kale anayetoa pepo. Masimulizi ya jinsi Mitume wa Bwana wetu walivyoshindwa kutoa pepo katika Mathayo 17:14-18 yanaonyesha jinsi jambo hili lilivyokuwa gumu hata wakati huo. Hili linaonekana pia katika tukio linalosimuliwa katika Matendo 19:13-16, ambapo Wayahudi fulani (watoto wa kuhani Skeva) walishindwa kumtoa pepo mmoja, na walipata kipigo kutoka kwa mwenye pepo mara waliposhindwa katika jaribio lao hilo! Wayahudi wale walijaribu kutumia Jina la Bwana wetu na pia kumtaja Paulo lakini pepo yule hakuwezekana, ijapokuwa alikubali mamlaka ya Bwana wetu na yale ya Paulo. Ni wazi utashi wa mwenye pepo ulikuwa na sehemu / umuhimu fulani katika shughuli hii [hili ni wazo na tafsiri yangu ya haya matukio]. Dondoo muhimu sana ya kukumbuka ni kwamba kitabu cha Matendo ya Mitume ni cha kihistoria zaidi kuliko cha mafundisho ya kanuni; hivyo ni muhimu kuona kwamba siyo kila kitu kinachosimuliwa humo ni cha kufuata. Mfano mzuri ni jinsi Mtume Petro alivyokuwa akikataa kabisa kuhusiana na watu wa mataifa, mpaka Bwana wetu alivyompa maelekezo ya nguvu sana ndipo alipoanza kuona umuhimu wa kuwapatia Injili watu wa mataifa (Matendo 10:9-48).

Tunaelekezwa katika nyaraka: Waefeso 6:12, “tupigane vita ya kiroho”; 1Pet. 5:8, “tuwe waangalifu na mbinu za Shetani”; Waefe. 4:27, “tusimpe Ibilisi nafasi yoyote”; Yakobo 4:7, “tumpinge Shetani”, lakini hatuambiwi “tutoe pepo”. Kama tungekuwa na maagizo ya “kutoa pepo”, kungekuwa na maelekezo ya kufanya hivyo. Tizama tu mwenyewe vurugu zilizomo katika makundi yanayofanya majaribu ya “kutoa pepo” na utakubaliana na mimi kwamba hili si jambo la kujihusisha nalo kabisa. Udanganyifu iliomo katika makundi haya ni mkubwa sana. Lakini je, ikiwa leo hii tunakutana na mtu aliye na dalili za wazi za kuwa anakaliwa na pepo, tufanyeje?

Tukumbuke ukweli mmoja. Ndani ya mwili wa mwanadamu mmoja haiwezekani kuwemo Mungu na pepo; Mkristo hawezi kamwe kukaliwa na pepo, kwani yeye ni hekalu la Roho Mtakatifu na Bwana Yesu Kristo yu ndani yake. Hivyo mtu mwenye pepo akipewa Injili na akaipokea, pepo atatoka. Mifano mingi iliyomo ndani ya vitabu vya Injili inaonyesha wale waliokaliwa na pepo wakimwita Bwana wetu na kumwomba msaada wa kutolewa pepo wale. Hivyo basi, ngojea wakati ambapo mtu mwenye pepo ana kipindi kama hiki cha utulivu na akili yake mwenyewe (na ikiwa kuna nia ya wokovu basi Mungu atahakikisha muda huo unapatikana) na umpatie Injili mtu huyu; mara Injili ikipokelewa na kukubaliwa moyoni mwake, pepo atatoka.

5.2 Aya Mojawapo Isiyoeleweka Vyema.

Yohana 14:12:
14.12 Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi,
yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, …..

Hayo ni maneno anayoyasema Bwana Yesu, akizungumza na wanafunzi wake, wakati akimjibu Filipo ombi lake la “… Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha”. Itakuwa vyema kabisa ukisoma muktadha wote wa Yohana 14:1-14. Bwana Yesu anamwambia Filipo kuwa yeyote aliyemwona Yeye, kamwona Baba; Yeye yu ndani ya Baba, na Baba yu ndani Yake; maneno [yaani mafundisho ya ile kweli] ayasemayo Bwana Yesu hayasemi kwa mamlaka yake mwenyewe, bali Baba aliye ndani Yake anazifanya kazi zake; hivyo kazi anazomaanisha Bwana wetu ni mafundisho Yake. Neno kazi hapa limepelekea Wakristo wengi kukimbilia kufikiri “miujiza”[!!] Bwana wetu alitenda mwujiza wa kumpa uwezo wa kuona mtu aliyezaliwa kipofu; sasa, ni nani anayeweza kunionyesha mahala, katika Agano Jipya, ambapo Mtume fulani anampatia uwezo wa kuona mtu yeyote. Au, tuchukue miujiza kwa ujumla, kusanya miujiza yote iliyotendwa na Mitume wa Bwana baada ya Yeye kupaa mbinguni, uiorodheshe, uone kama inazidi, kwa kishindo chake, ile miujiza aliyoitenda Bwana wetu! Utaona hakuna, na hii ni kwa sababu Bwana wetu katika aya hii hakuwa anazungumzia miujiza, bali mafundisho ya Neno la Mungu; alikuwa anasema kwamba ukiamini kwa uthabiti ndani ya moyo wako utawezeshwa kufundisha Neno la Mungu kwa ufanisi mkuu. Alikuwa anasema kwamba kufanya kazi ya kutumikia katika kueneza kweli yote ya Neno la Mungu na kushiriki katika kupanua shughuli za uenezi huu ili kuwafikia watu wengi zaidi walio tayari kuipokea kweli hii itakuwa ni “kazi kuu” zaidi ya kutenda miujiza ambayo kusudi lake lilikuwa ni kuwafanya waipokee kweli hii. Dunia inaona miujiza kuwa ni jambo “kuu”; lakini sisi tuliookolewa tunajua, au tunapaswa kujua, kwamba Yeye tuliyemchagua ni mkuu zaidi, na kweli anayotufundisha ni yenye umuhimu zaidi ya kishindo chochote tutakachokipata kutokana na mwujiza wowote tutakaoushuhudia mbele za macho yetu. Hili fundisho la Biblia linathibitishwa na Mtume Petro katika 2Pet. 1:16-19 ambapo anatufundisha kwamba ingawa yeye (Petro) alishuhudia utukufu wa Bwana wetu pale katika mlima mtakatifu na kuisikia sauti kutoka mbinguni (Matt. 17:1-8), lakini ni vyema kwa kila mmoja wetu kulichukulia Neno lilioandikwa la unabii kuwa ni la uhakika zaidi ya [kitu kama] maono ya ujio wa pili wa Bwana wetu alioushuhudia yeye pale mlimani. Kusudi la kutenda miujiza katika huduma ya Bwana wetu na katika huduma za Mitume Wake [baadaye] wakati wote lilikuwa ni kuishuhudia kweli ya Neno la Mungu waliyoifundisha na siyo kutafuta sifa, kukusanya pesa, mali, utajiri, n.k. Hakuna kisichowezekana kwa Mungu. Na pia ni sahihi na halali kuomba msaada Wake [ambao Yeye ataamua atupatie] “kimiujiza” au kupitia waumini (na wasio waumini) wenzetu ambao tunawaona kwa macho yetu. Ukweli ni kwamba miujiza haifanyiki tena na wale wanaofanya kazi Yake kwa sababu rahisi sana ambayo ni kwamba sasa tunatakiwa tuelekeze macho, mioyo na imani yetu katika Neno Lake na Yeye mwenyewe ili tuweze kuamini ile kweli anayotufundisha. Kweli ya Mungu ni kwa ajili ya walio na imani yenye nguvu katika Mungu wao, bali miujiza ni kwa ajili ya walio na imani dhaifu na ya “kitoto” (soma 1Wakor. 13:11-12). Watoto huhitaji msaada mpaka wanapokua watu wazima. Lakini wanapokuwa watu wazima, hapo wanaweza kuacha, “kubatilisha”, mambo ya kitoto (aya ya 11). Mara baada ya Kanisa kukua kiasi cha kutosha, likiwa limejengeka katika idadi ya Wakristo; makanisa yaliyoimarika; wazee, walimu, watumishi wanaotumikia Kanisa; na [muhimu kabisa] Agano Jipya lilipokamilika kuandikwa, basi “mambo ya utotoni” yaliweza kuachwa. Jambo la kusikitisha ni kwamba Wakristo wengi sana leo hii, ambao wamekuwa Wakristo kwa muda mrefu, bado wanahitaji (kama Paulo anavyosema katika waraka huo huo) “kunywa maziwa, na si chakula [kigumu cha kiutu uzima]”, na hii ni kwa nini? Kwa sababu “mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi” (1Wakor. 3:2). Hivyo, tuwe makini katika kuielewa aya hii ya Yohana 14:12.

6. Hitimisho Kama Tahadhari!

Ndugu zangu mnaopenda kushuhudia miujiza, nawasihi muisome tahadhari [hapa chini] kutoka kwa Mtume Paulo, ambayo anaitoa kwa kizazi hiki ambacho kitashuhudia ujio wa yule ambaye Biblia inamwita mnyama / mpinga Kristo / pembe [ndogo] ambaye kwa kuwa Shetani mwenyewe atampa nguvu zake, ataonekana akitenda miujiza mikuu mbele za wanadamu, lakini miujiza hii yote itakuwa na makusudi ya kuwadanganya watu na kuwapeleka katika maangamizi. Watu watakaodanganyika si wale tu wasiomwamini Kristo, bali pia wale Wakristo wanaotia umuhimu mkubwa katika miujiza, badala ya Neno la uzima ambalo linaleta upevu wa kiroho unaoimarisha imani ya muumini katika mazingira magumu ya hapa duniani.

Ndugu yangu, ukishazaliwa upya, soma Biblia, jifunze Biblia, ishi kulingana na mafundisho ya Biblia, saidia wengine kufanya vivyo hivyo! Hayo ndiyo majukumu ya Mkristo.

2Wathess. 2:8-12:
2.8 Hapo ndipo atakapofunuliwa yule mwasi [mvunja sheria, mhalifu] (yaani mpinga Kristo), ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza pale Atakaporudi [mara ya pili] katika utukufu
2.9 [yule yule mhalifu] ambaye ujio wake utatiwa nguvu na Shetani na utaambatana na kila aina ya miujiza ya uongo (inayopelekea katika udanganyifu), ishara na ubashiri wa ajabu na kutisha;
2.10 na kila aina ya udanganyifu usio na haki unaolengwa kwa wale wanaoangamia [yaani, wale watakaoamini uongo huo] kwa sababu hawakuzifungua nyoyo zao kwa ile kweli ili waokolewe.
2.11 Kwa sababu hii Mungu anawaletea ghiliba yenye nguvu ili wauamini uongo;
2.12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakifurahia udhalimu.

Imeandikwa na Respicius L. Kilambo.
+255 754 37 5474

Strongly Recommended Bible-teaching websites:
https://ichthys.com
https://bibleacademyonline.com