Kuendeleza Mashambulizi Sahihi ya Kikristo Katika Vita Yetu ya Kiroho: Nyaraka za Mtume Petro #29

1Petro 1:13

Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

1Petro 1:13:
Hivyo basi, vifungeni imara viuno vya nia zenu, na muwe macho kiroho; mkiweka tumaini lenu katika ile neema mtakayoletewa wakati wa ufunuo wake Yesu Kristo.

Kwa Hiyo: Tuzungumzie kidogo aya hii kwa mtazamo wa lugha ya Kiyunani ambayo ndiyo lugha yake asilia. Matumizi ya neno dio (διό) hapa badala ya maneno mengine ya viunganishi, yana matokeo ya kuhusisha aya ya 13 kwa ukaribu sana na kilichoandikwa mara tu kabla: sababu ya sisi kuhitaji “kufunga mshipi” viuno vya nia (mind) zetu katika kuwa watulivu kiroho, tukielekeza fikra zetu katika “matukio yajayo”, ni kwamba msimamo huu wa kufikiri kwa usahihi na kwa kutazama mbele ni matokeo sahihi ya kutambua neema tulizo nazo kama waumini katika Bwana Yesu Kristo. Kwa hakika sisi ni waumini katika Bwana Yesu Kristo. Kwa ukweli na uhalisia, hivyo ndivyo tulivyo. Lakini duniani ni mahala penye “kelele”, na pamejaa mambo mengi yanayoweza kutuondoa kwenye msitari tunamotembea, mengi kati ya hayo mambo ni sehemu ya kawaida kabisa ya kuishi hapa duniani, mengi kati ya hayo yameundwa mahususi na yule mwovu kama sehemu ya mfumo wake ili kuwapoteza njia waumini, au angalau kuhujumu mwendo wao na kumaliza nguvu ya ufanisi wao. Tunaye Bwana huko mbinguni ambaye alikufa kwa ajili yetu, Yesu Kristo, ambaye tunadai kumpenda kwa moyo wote. Wakati huo huo, malaika wanatutizama ili waone jinsi KWELI hizi zinavyoathiri mwenendo wetu – *Je, ni kweli kwamba tunaishi kama vile tunatambua wokovu huu mkuu, kama vile tunampenda Bwana Yesu Kristo zaidi ya tunavyoupenda ulimwengu huu? Kujifunza nini Biblia inafundisha kuhusu [dhana ya milele], kuwa mahodari katika kuitumia kweli hii na nyingine tunazojifunza katika mateso na mitihani tunayopitia maishani, na kuendelea kuwa macho katika hayo yote ni sehemu kuu ya maisha ya mafanikio ya kiroho ambapo tunaweza kujibu kwa ari “Ndiyo!” kwa swali lililoulizwa hapo *juu.

Fungeni imara viuno vya nia zenu kwa kuwa macho [kiroho]: Kitu cha kwanza cha kuona katika amri hii inayotokana na ufunuo wa Roho Mtakatifu kwa mtume Petro ni kwamba inahusisha kuchukua hatua chanya kutoka ndani ya mioyo yetu na kuelekea nje (yaani katika wajihi na mwenendo wetu). Baada ya kutukumbusha kuhusu maajabu ya wokovu ambayo sisi kama Wakristo, tuliozaliwa upya tunayo (na tutayafaidi hapo baadaye), Petro sasa anaendelea na kutuambia jinsi tunavyopaswa kuenenda. Lakini haanzi kwa kutupatia orodha ya “fanya hili, usifanye lile!”. Badala yake, Petro anatuelekeza “tupange” jinsi tunavyofikiri kama msingi wa mwendo wetu na Bwana Yesu Kristo. Wazi kabisa, kuyatawala na kuyaelekeza mawazo yetu ya ndani kabisa katika namna ya Kikristo isiyotetereka ambayo inaupa kipaumbele UKWELI katika yote tunayofanya si mambo ya uchanga (utoto) wa kiroho. Hivyo kuzingatia amri hii kwa ufanisi kunamlazimu muumini kukua kiroho na kuendelea kusoma na kusikiliza Neno la Mungu hata baada ya kupevuka kiroho. Moyo ambao haujazaliwa upya una ukinzani mkubwa kwa mtazamo wa Kimungu; ni kwa kujifunza na kujikumbusha KWELI katika namna endelevu na kuutisha mwili na nia yetu kwa kutumia KWELI hiyo ndipo muumini anaweza kikweli-kweli kuwa “tayari kwa vita” kiroho. Ushindi wa kiroho wa waumini wote tunaowatazama kwa staha kuu katika Biblia kama Abrahamu, Daudi na Danieli ni matokeo, siyo tu ya imani wakati ule wa ushindi wao bali ni wa uaminifu katika kuamini KWELI tena na tena mpaka ikawa sehemu ya nafsi zao, na pia ni matokeo ya kuitumia KWELI hiyo katika fikra zao zote za ndani ya nafsi zao na katika tafakuri zao, hasa wakati magumu yalipojitokeza (Zab. 1:2).

6.14  Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii [deraya] ya haki kifuani,
Waefe. 6:14

Katika nukuu hii, Paulo anatumia kitenzi (verb) kile kile, katika Kiyunani, kwa ajili ya neno ambalo maana yake ni “kujifunga [mkanda] kiunoni” (kiambishi-awali, yaani prefix, tu ndiyo tofauti), ili kuelezea dhana ya kawaida ya Kiyunani kwamba “kuvaa mavazi” kunahusisha kuweka mkanda kuzunguka kiuno ili kupanga, kukaza nguo zilizovaliwa. Hivyo, katika kueleza dhana hii kiroho, “kujifunga mkanda” maana yake ni kujiweka tayari kwa ajili ya vita, kinyume na kuwa “si tayari” - kama vile ambavyo mtu ambaye hajatoka kitandani hayuko tayari kushughulika na matukio ya siku. Hivyo basi, isitushangaze kabisa kwamba “kuwa macho” na “kuamka” ni amri zinazofanana katika maandiko, zikitumika kuelezea dhana hii hii ya kuwa tayari kiroho ndani ya moyo wa muumini kupitia kukua kunakotokana na kusikia, kujifunza, kuamini na kutafakari juu ya UKWELI wa Neno la Mungu (Matt. 24:42-43; 25:1-13; 26:41; Mrk. 13:33-37; 14:38; Lk. 12:35-37; 21:36; 22:40; 22:46; Matendo 20:31; 1Wakor. 16:13; Waefe. 5:14; 6:18; Wakol. 4:2; 1Wathess. 5:6; 1Pet. 4:7; 5:8; Ufu. 3:2; 16:15). Kushindwa kutii amri hii, amri ambayo inaweza kutimizwa tu na wale ambao kwa moyo mmoja wamekuwa wakiitafuta KWELI na kuitunza katika mioyo yao [wanapoipata], kunamaanisha kwamba hatutakuwa tayari kukabiliana na kile Bwana atakachokileta tukabiliane nacho, tukaonekana “uchi” na “waliolala” badala yake, pale wakati wa kujaribiwa utakapofika.

16.15  Tazama, naja kama mwivi [bila taarifa!]. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.
Ufu. 16:15

Hivyo basi, “viuno vya nia zenu” ni namna mioyo yetu inavyowaza, mahala ambapo nia, fikra za kimwili na roho ya kibinadamu vinakutana, mahala ambapo panahusika na fikra, hisia na tafakuri, mahala “sisi ndio tunakuwa sisi”, ndani kabisa. Hivyo, kumtayarisha yule mtu wetu wa ndani kunahitaji mabadiliko ya kimsingi ya njia za fikra tulizokuwa nazo kabla ya kuzaliwa upya. Hata kama tumeokolewa kwa muda mrefu sana, mchakato huu wa kubadilisha na kujenga upya namna tunavyofikiria kila kitu katika hii dunia hautaisha mpaka ufalme wa Mungu utakapokuja. Ulimwengu, mtazamo wake na [ma]shinikizo yake, viko wakati wote, hivyo wakati wote kutakuwa na nafasi ya kuboreshwa kwa hali yetu, jinsi “mtazamo wetu wa Kimungu” unavyozidi kutahiniwa. Kwa masikitiko makubwa, kwa sehemu kubwa ya Wakristo wanaoishi katika hii enzi tulimo ya Laodikia, hii “nafasi ya kuboreshwa” ni kubwa mno kwa sababu kukua kiroho halisi kunakofanyika ni kidogo sana – kwa sababu KWELI inayofundishwa kwa kina ni kidogo mno.

11 Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.
12 Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.
Amos 8:11-12

Tunapookolewa, tunapewa moyo mpya, uliosafishwa (Ezek. 36:26; 10:22), “fikra mpya” au “namna mpya ya kufikiri”, kama Yohana anavyoelezea hali hii (1Yoh. 5:20), na pamoja na huduma/utumishi wa Roho Mtakatifu, kila muumini anapozaliwa upya anapata hisia ya furaha ya huu mtazamo mpya pale macho yetu yanapofunguliwa kwa mara ya kwanza katika kweli na ulimwengu unapoonekana katika uhalisia wake. Hapo kabla tulikuwa vipofu, na sasa tunaona (Yoh. 9:25; 9:39).1 Lakini, hii epifania (ufunuo/ufahamu) ya mwanzoni haitoshelezi kumbeba muumini mpaka mwisho. Moyo wetu uliozaliwa upya una ulazima wa kulishwa wakati wote na KWELI hii – ili mtazamo huu mpya wa wokovu uweze kukua, na bila kusinyaa.

5.20  Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli [tuijue ile kweli]; nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele. 1Yoh. 5:20 SUV
Tulijifunza “fikra adilifu”hapo nyuma,2 na mbinu za kubadilisha mwelekeo wa fikra zetu baada ya kuzaliwa upya kupitia mchakato wa kukua kiroho na kuendelea katika kuitumia KWELI.3 Pointi muhimu ya kujifunza hapa ni kwamba mara baada ya kujifunza kanuni za kutosha za KWELI na kuzifanya sehemu ya fikra zetu na zinazowezekana kutumika na Roho Mtakatifu kwa kuziamini kanuni hizi, tunapaswa kuchukua hatua nyingine ya “kuvaa mkanda wa viuno vya [fikra zetu]”. Mchakato huu wa kuikumbuka na kuitumia KWELI, kanuni zile moja-moja na misingi ya kweli kwa ujumla, utakuwa, katika harakati za kukua/kupevuka, ukijiendesha wenyewe kiasi fulani, lakini tutahitaji wakati wote kuwa tayari “kujipa moyo katika Bwana”, kama Daudi alivyofanya (kwa mfano 1Sam. 30:6), pale nyakati ngumu zinapotuangukia bila kutegemea (Mhubiri 9:12):

4.6  Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.
4.7  Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
4.8  Hatimaye, ndugu zangu, [mnavyoendelea katika imani], mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi [matakatifu], yo yote yenye kupendeza [kwa Mungu , siku ya hukumu], yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.
4.9  Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.
Wafi. 4:6-9 SUV

Kwa kiasi fulani, kujaa, hata kufurika kwa imani, tumaini na upendo wetu katika uweza wa Roho Mtakatifu kutatokea, kutakua na kuendelea kwenyewe kwa jinsi tunavyoendelea kiroho, “tukikua kwa neema na ufahamu wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo” (2Pet. 3:18). Lakini hata katika aya iliyonukuliwa hapo juu, ingawa dalili zote zinaonyesha kwamba Paulo anawaandikia waumini ambao wamepevuka kiroho na wa kipekee katika ubora, bado anaona uhitaji wa kutumia shuruti mbalimbali hapa: “furahini!” (aya ya 4, mara mbili); “upole wenu ujulikane … katika kutafakari kurudi kwa Bwana” (aya ya 5); “endeleeni kusali … ili muwe na amani ndani yenu!” (aya ya 6); “muyatafakari mambo haya mema” (aya ya 8); “na muyatende” (aya ya 9). Kama mchakato wa kuuweka moyoni ule mtazamo sahihi wa kiroho ungekuwa unajiendesha wenyewe au ungekuwa [sehemu ya] hulka yetu ya asili, yaani “second nature”, bila shaka amri nyingi namna hii zisingekuwa na ulazima. Kwa hali ilivyo, kutimiza amri inayofanana ya “kufunga mkanda wa viuno vya nia zetu” kunalazimu kukua kiroho, mazoezi/mazoea (mpaka inakuwa desturi nzuri ya kawaida kwetu), na kukazania katika kuitimiza amri hii tena na tena kila inapolazimu – na hayo yote ni lazima yafanyike angalau kila siku. Ni kwa sababu hii Petro anasisitiza juu ya ulazima wa kujielekeza hata kufikia na kudumu katika kuwa macho kiroho na kiakili, kwani yaweza kuwa jambo gumu kidogo – kwa sababu mwili katika hulka yake unapinga mtazamo wa kiroho kuutawala, wakati huo huo ulimwengu na mtawala wake mwovu wana shauku kubwa ya kuturudisha katika fikra za kimwili kwa kutumia vishawishi vyao vingi. Kwa neema kuu za Mungu, hata hivyo, sisi waumini sote tunaye Roho Mtakatifu kama Mshirika wetu katika vita hii, akitusaidia kufanya fikra adilifu zitawale miili yetu:

8.5  Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao [wanaomfuata] Roho huyafikiri mambo ya Roho.
8.6  Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya Roho ni uzima na amani.
8.7  Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.
8.8  Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu (yaani wasioamini, walio watumwa wa miili yao).
8.9  Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwai[m]fuata r[R]oho [Mtakatifu] [- kama kwa kweli Roho wa Mungu anakaa ndani yenu]. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.
War. 8:5-9

5.16  Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.
5.17  Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.
5.18  Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria [ya Musa].
5.19  Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu [mwenendo wa aibu], ufisadi,
5.20  ibada ya sanamu [madawa ya kulevya, kutegemea watu, malaika], uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
5.21  husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia [nawapa onyo] mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia [kuwapa onyo], ya kwamba watu watendao [wenye desturi ya] mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.
5.22  Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
5.23  upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.
5.24  Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
5.25  Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.
Wagal. 5:16-25

“Kufunga mkanda” moyo na nia yetu maana yake ni kuwa tayari kwa njia ya kujifunza na kujitayarisha kwa lolote linaloweza kuja [katika maisha yetu]. Kama vile tunavyojitayarisha [kimwili] kuikabili siku kimwili, vivyo hivyo, Petro anatuambia, tujitayarishe kiroho. Matayarisho hayo ni lazima yafanyike wakati wote [unaofuata] baada ya kuokolewa. Kama ambavyo hatuwezi kuvaa mavazi asubuhi bila kufanya kwanza matayarisho fulani (kununua nguo, kuzifua, kuzafisha na kung’arisha viatu, kwenda bafuni, n.k.), vivyo hivyo tusitegemee kutimiza amri hii ya kiroho ya kujifunza misingi wakati ule mitihani na majaribu yanapokuja kutukabili isipokuwa kwa kujifunza kweli za Mungu kabla, na hivyo kukua na kuendeleza nguvu muhimu za ndani za kiroho zinazotokana na kuamini kweli hizo ili kutuwezesha kukabili mitihani na majaribu hayo. Na kama vile kabati lililojaa nguo nzuri na safi bado linahitaji mtu azitoe nguo hizo na kuzivaa siku yake ikifika, vivyo hivyo kutimiza kwetu kwa amri hii kunahitaji matumizi ya hii kweli siku hadi siku, saa hadi saa, kutoka mioyoni mwetu: kama Wakristo, tunapaswa kuwa tayari “kuvaa mkanda” wakati wote, kwa sababu adui wetu Ibilisi anazunguka-zunguka wakati wote, akiwa mawindoni kutafuta wale ambao hawako tayari ili awashambulie, ikiwa kukosekana kwa utayari huo ni kwa siku zote au ni kwa muda tu pale tunapojisahau na kushusha chini ngao na silaha zetu. Vita hii ya kiroho tunayopigana - na ambayo tutapigana katika kila saa ya uhai wetu mpaka Bwana wetu atakaporudi – inahitaji tuwe tayari wakati wote “kuvaa mikanda” haraka sana, wakati wowote yule mwovu na watumishi wake watakapotushambulia, wakati mwingine kwa ghafla sana. Kutimiza agizo hili ni jukumu la muhimu sana. Tunatazamwa kwa karibu sana, kama Waebrania sura ya 11 inavyofundisha, na “wingu” kubwa la mashahidi, na tunachunguzwa na malaika (kama tulivyoona katika aya ilyopita: 1Pet. 1:12), pia na Bwana wetu mpendwa Yesu Kristo! Kama ilivyo katika vita yoyote, katika uwanja wowote wa vita, ushindi katika mapambano ni muhimu sana kwa motisha, lakini kushindwa pia kunaweza kumtia huzuni hata mpiganaji shujaa wa muda mrefu na aliyepata mafunzo ya kiwango cha juu. Lakini, “tunafungaje mikanda” kwa ajili ya vita hii?

Jibu la swali hili linaweza kupatikana kwa namna mbili. Kwanza, kama vile jeshi lolote vitani linalazimika kuongeza mahitaji ya vita (yaani chakula, maji, silaha, n.k.) wakati wowote muda unaporuhusu, vivyo hivyo ili kuwa tayari asilimia 100 kwa taabu za maisha haya, waumini wanapaswa kuchukua/kutumia kila nafasi wanayopata kwa ajili ya kujifunza, kuamini na kulitumia Neno la Mungu, kwani KWELI ya maandiko ndiyo mabomu, risasi, baruti, n.k. zinazotumika katika *silaha za vita hii. Hivyo jibu la kwanza kwa swali: “tunafungaje mikanda?” ni kuendelea kuisikiliza, kujifunza na kuiamini KWELI ya Neno la Mungu kutoka kwa Mwalimu aliye bora, imara, wa kuaminika, sahihi, kila tunapopata nafasi ya kufanya hivyo. Pili, mara muumini atakapokuwa amejifunza kiasi cha kutosha kumwezesha kuvuka kiwango cha “mafunzo ya msingi”, Bwana wetu atampa muumini huyu fursa za kuyatumia aliyojifunza na aliyoyaamini. Yumkini ni salama kusema kwamba haitapita siku katika maisha ya Kikristo ambamo hatutapata fursa ya kutumia ile kweli ya Neno la Mungu kwa yanayotukabili katika mpito wetu katika dunia hii (hata kama majaribu makubwa hayatokei kila siku, kwa neema za Mungu). Mitihani hii,

*Silaha ni “medium” inayotumika katika kulitumia Neno la Mungu, kama kanisa au darasa la kufundishia Neno, website, unaposhinda mtihani, n.k.
hata ile midogo-midogo, inafanya tofauti kati ya “kuwa na mkanda” (yaani kujifunza na kuamini sehemu kubwa ya KWELI), na “kuuvaa mkanda huo kiunoni” (yaani kuwa tayari kuitumia KWELI hii na kuitumia kwa ufanisi) wazi kabisa. Ikiwa mtihani utakuja ghafla wakati ambao ulinzi wetu uko chini au tutashambuliwa wakati ambao tuko tayari, vyovyote vile waumini wanapaswa kuwa weledi katika kuikumbuka na kuitumia KWELI ya Biblia waliyojifunza na kuiamini katika kulinda usalama wao wa kiroho wakati wowote ule [ma]shinikizo yanapotokea.

3.1  Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
3.2  Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.
Wakol. 3:1-2 SUV

Inapaswa kuwa wazi katika kutafakari nukuu hiyo hapo juu, kwamba kuendeleza mtazamo wa Kimungu kunahitaji juhudi kiasi fulani. Kama suala la “kuendeleza kutafakari” maajabu ya mbinguni, utukufu wa Bwana wetu, mambo adhimu ambayo Mungu ametufanyia, anatufanyia na atatufanyia – katika upendo Wake kwetu usio na mfano – lingekuwa ‘automatic’, yaani hali hii ‘ingekuwa inajipa yenyewe’ tu mioyoni mwetu, basi kusingekuwa na haja ya Paulo kutupatia amri ya kufanya hivyo. Kwa lugha nyepesi, kuweka moyoni kanuni na kweli njema tunazojifunza kutoka katika Neno kutokana na sisi wenyewe kusoma Biblia na pia kufundishwa na waalimu kunahitaji kitu kingine zaidi kutoka kwetu, zaidi ya kujifunza misingi ya mwanzo na kuiamini: inahitaji uangalifu na uthabiti katika kujikumbusha kanuni hizi na kuzitafakari tunavyotembea katika ulimwengu huu kila siku na katika kila hatua tunayopiga njiani, ii kwamba tuweze kuwa tayari kuukabili kila mtihani kwa “upanga wa Roho” (Waefe. 6:17).

4.8  Hatimaye, ndugu zangu, [mnavyoendelea katika imani], mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi [matakatifu], yo yote yenye kupendeza [kwa Mungu , siku ya hukumu], yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.
Wafi. 4:8 SUV

Hivyo, zaidi ya kutuamuru tufanye hivyo, maandiko hayatupatii maelekezo ya namna haswa ya kufanya hivyo. Maamuzi hayo (kwa usahihi na kwa neema kwetu) yanaachwa kwa kila mmoja wetu afanye katika utekelezaji wa kweli ya maandiko. Kitu tunachoweza kusema kwa uhakika ni kwamba Bwana Yesu Kristo ndiye taswira halisi ya ile kweli na upendo, na Yeye anapaswa kuwa ndiye mlengwa wa juhudi zetu zote kuhusiana na suala hili.

3.14  Kwa [sababu] hiyo nampigia Baba magoti,
3.15  ambaye kwa jina lake familia yote ya mbinguni na ya duniani inaitwa,
3.16  awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kuimarishwa katika mioyo yenu (yule mtu wenu wa ndani) kwa njia ya Roho Wake;
3.17  Ili kwamba, shina na msingi wenu vikiwa katika upendo, Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani;
3.18  ili mpate kufahamu, pamoja na watakatifu wote, jinsi ulivyo na upana, na urefu, na kimo, na kina [upendo Wake kwenu];
3.19  na [ili mweze] kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu [wa mwanadamu] kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kujazwa na utimilifu wote wa Mungu.
Waefe. 3:14-19

1.21  Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida [katika milele].
Wafi. 1:21 SUV

1.24  Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;
11.25  akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;
11.26  akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake [kwa ajili ya] Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo [yake ya milele].
11.27  Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye Yeye asiyeonekana.
Waebr. 11:24-27 SUV

Kukumbuka aya muhimu na Zaburi na kuziweka wakati wote katika akili zetu, kusoma Biblia zetu tena na tena kila tunapopata fursa, kumtafakari Bwana wetu na KWELI mbayo Yeye ni mfano wake halisi kama Neno wa Mungu aliyetwaa mwili, na kuendelea na mazungumzo na Yeye tumpendaye sana kupitia fursa kuu tuliyopewa ya sala, zote hizi ni njia nzuri za kutumia kanuni zinazofundishwa hapo juu, kujiweka katika nafasi ya kutimiza agizo la “kuvaa mkanda kiunoni” mwa fikra na hisia zetu katika kumtumikia Bwana wetu. Zaidi ya hapo, ni kweli kabisa kwamba kuna faida katika kuandaa orodha endelevu ya binafsi ya mambo mema ya kukumbuka ambayo yanahusiana mahususi na amri ya “kufunga mkanda” katika viuno vya fikra zetu na hisia zetu kwa ajili ya vita za kiroho ambazo nyingi hututokea kwa ghafla. Orodha hii inaweza kuwa na vipengele kama kukumbuka alichokifanya Bwana kwa ajili ya wengine (kwa mfano kuwaokoa wana wa Israeli katika Bahari ya Shamu; cf. Yoshua 24:6; Neh. 9:9; Zab. 106:9; 136:13; Mat. 7:36; Waebr. 11:29), na kujumlisha kumbukumbu hizi na nyingine ambapo Alituokoa sisi wenyewe katika maisha yetu na katika maisha ya wale tuwapendao. Tunapotiwa moyo na Roho Mtakatifu katika nyakati za magumu (2Wakor. 1:3-7), sura, aya, mifano na kweli Anazozitumia kututia moyo ni muhimu sana kuzikumbuka, ili kuzitumia katika kupunguza makali kwa hisia zetu wakati wowote hapo baadaye tutakapopata mshituko au shambulizi la ghafla kutoka kwa yule mwovu (na mashambulizi haya ni lazima tutayapitia). Orodha ifuatayo isichukuliwe kuwa haiwezi kuboreshwa au kuwa ni kamili, lakini dondoo zilizomo zinaweza kumsaidia msomaji katika nyakati za [ma]shinikizo – na kwa kweli zimemsaidia sana mwandishi (wa mafundisho haya) katika nyakati zake za magumu:

Kumbuka: Bwana Yesu anatushikilia kwa mkono (Yoh. 10:28-29; cf. Kumb. 33:27).

23 Walakini mimi ni pamoja nawe daima, Umenishika [kwa] mkono [wangu] wa kuume.
24 Utaniongoza kwa [u]shauri [w]ako, Na baadaye utanikaribisha [katika] utukufu [milele].
Zab. 73:23-24 SUV

Kumbuka: Bwana Yesu yuko nasi katikati ya tufani (Zab. 107:29; Mithali 10:25).

8.24 Kukawa msukosuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi.
8.25 Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia.
8.26 Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu.
Matt. 8:24-26 SUV

Kumbuka: Bwana Yesu anatuongoza katikati ya mawimbi makubwa (Zab. 66:12).

14.26 Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu.
14.27 Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope.
14.28 Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.
14.29 Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu.
14.30 Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.
14.31 Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?
Matt. 14:26-31 SUV

Kumbuka: Mungu amepangilia na Bwana wetu Yesu Kristo anafanya kila jambo linalotutokea kwa ajili ya mema yetu (War. 8:29-31; Waefe. 1:7-14).

8.28  Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
War. 8:28 SUV
Kumbuka: Bwana Yesu anafurahishwa nasi tunapoamini kweli na siyo vile tunavyoviona [kwa macho yetu] (2Wakor. 4:18; 5:7).

11.1  Basi imani [katika Neno lililoandikwa na lenye uhai] ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, [imani] ni bayana [proof] ya mambo yasiyoonekana.
11.2  Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa [walimpendeza Mungu].
Waebr. 11:1-2 SUV

Kumbuka: Bwana Yesu anatimiza mapenzi ya Mungu kwa ajili yetu kwa mema kwa kila namna ili tuweze kuwa na furaha hata pale tunapositushwa na matukio au tunaposhinikizwa na mateso.

5.16  Furahini siku zote;
5.17  ombeni bila kukoma;
5.18  shukuruni kwa [katika mazingira yote] kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.
1Wathess. 5:16-18 SUV

4.4  Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.
Wafi. 4:4 SUV

1.2  Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;
1.3  mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.
1.4  [Basi acheni] Saburi na [ifanye] kazi [yake kwa] ukamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno [kitu].
Yak. 1:2-4 SUV

Kumbuka: Mioyo yetu ni hekalu ambamo tunashirikiana na Bwana Yesu Kristo, na kwa sababu hiyo inastahili kutakaswa na kulindwa dhidi ya kuingiliwa na mambo ya kidunia (cf. Yer. 17:9).

14.23 Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.
Yoh. 14:23 SUV

Kumbuka: Bwana Yesu hufurahishwa hata na kiasi kidogo sana cha imani kutoka kwetu, kwani [hata] mbegu ndogo sana yaweza kukua na kuwa mti mkubwa sana wa imani, na imani kidogo tu yaweza kuhamisha milima (Matt. 13:31-32).

17.20 Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.
Matt. 17:20 SUV

Kumbuka: Sisi ni dhaifu, lakini Bwana Yesu ni mwenye nguvu tele, na Yeye huufanya udhaifu wetu uwe ni nguvu kuu tunapomuegemea Yeye na siyo sisi wenyewe (2Wakor. 11:30; Waebr. 11:34).

12.9  Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu [wako]. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.
2Wakor. 12:9 SUV

Kumbuka: Hata tukipita katika bonde la giza nene, Bwana Yesu yuko nasi, na muda si mrefu atageuza giza hilo kuwa mwanga tunaousubiri kwa hamu.

4 Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
Zab.23:4 SUV

2.8  Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu; kwa kuwa giza linapita na ile nuru ya kweli imekwisha kung'aa.
1Yoh. 2:8 SUV

Kumbuka: Bwana Yesu yuko upande wetu, na si dhidi yetu, hivyo vita inayotukabili inatoka kwa yule mwovu, na Bwana atatulinda.

Tazama, ikiwa yeyote atawashambulia, Mimi sitakuwa chanzo cha hilo; yeyote atakayewashambulia, atakuja kusalimu amri mbele yenu.
Isa. 54:15

6.13 Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu.
Matt. 6:13 SUV
au:
Na usitueleke katika mitihani [inayoweza kutuzidi nguvu], bali utuepushe na yule mwovu.
Matt. 6:13

6.12  Kwa maana mapambano yetu sisi si dhidi ya viumbe wenye damu na nyama; bali ni dhidi ya falme na mamlaka ya ki-malaika, dhidi ya wakuu wa giza hili la sasa, dhidi ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
Waefe. 6:12

Kumbuka: Bwana Yesu ndiye Mchungaji wetu, hata tukilazimika kupita katika bonde la kivuli cha kifo, na Atatupatia mahitaji yetu katika shida zote (Yoh. 10:11-16).

Bwana ndiye Mchungaji wangu. Hivyo, sitapungukiwa na chochote [nitakachokihitaji].
Zab. 23:1

Kumbuka: Bwana Yesu ndiye anayeendesha vita hii; yote yanamhusu Yeye, na siyo sisi, hivyo tunaweza kutegemea wokovu Wake, kwa lolote litakalotokea.

47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.
1Sam. 17:47 SUV

6 Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakutelekeza wala hatakuacha ushindwe.
Kumb. 31:6

Kuna mengi sana yanayoweza kusemwa – labda kunukuu Biblia yote, ikiwa na maelezo kamili na yaliyoeleweka kwa usahihi. Kitu muhimu cha kukumbuka ni kwamba kila kitu kiko chini ya mamlaka na uweza wa Mungu, na kwamba sisi, kama wale ambao tuko upande wa Bwana Yesu Kristo hatuna cha kuogopa: mambo yote yanamhusu Bwana Yesu Kristo, “ambaye ndani Yake imefichwa hazina yote ya busara na ufahamu” (Wakol. 2:3).

Kuwa Macho Kiroho: Msemo unaotafsiriwa “katika kuwa macho [kiroho]” ni hali ya tendo linaloendelea (participle; tafsiri kutoka kiyunani, kutoka kitenzi nepho) inayotumika katika mazingira ya msemo huu. Hii ni kusema, “kufunga mkanda viuno vya fikra zetu” kunafanyika katika mazingira ya “kuwa macho [kiroho]” kama Petro anavyoeleza katika sura ya kwanza, aya ya 13. Petro anaunganisha dhana hizi mbili ili kuweka wazi kwamba “kufunga mkanda” au kujitayarisha kwa ajili ya vita ya kiroho ni jukumu la sasa na la wakati wote – yaani tunapaswa tayari kuwa na mtazamo wa kiroho kuhusiana na kila jambo wakati wowote lakini pia ni lazima tuwe tumejitayarisha kabla kwa kujifunza kila siku [mara baada ya kuokolewa] ili kupambana na changamoto zitakazokuja katika maisha yetu ya Kikristo. Baadhi ya tafsiri za Kiingereza zimetumia neno “sober” katika aya hii; neno hili, linalomaanisha “akili iliyotulia” au “akili isiyovurugwa na kilevi”, linaweka wazi kwamba tunapaswa kuwa macho kiroho wakati wote. Kama tuko macho – na kama tumekuwa tukijitayarisha kwa ajili ya vita ya kiroho kwa kukua kiroho katika Bwana – basi tutakuwa na nafasi nzuri zaidi ya “kuvalisha mkanda mioyo yetu” kwa ajili ya vita vya kiroho pale [ma]shinikizo yanapotukabili ghafla. Hivyo “sobriety” au “hali ya akili iliyotulia na/au isiyokuwa na vurugu zinazosababishwa na kilevi” si tafsiri mbaya kwa neno nepho, lakini pamoja na maana halisi ya “kutokuwa na ulevi wa pombe”, kitenzi hiki pia kinamaanisha “kuwa macho – bila chembe ya usingizi” na “kuona kila kinachoendelea” kwa ujumla, na ni jambo la wazi kwamba ingawa pombe ni tatizo kwa Wakristo wengi, kwa hakika si tatizo pekee, na kwa kawaida si tatizo kubwa au kikwazo kikubwa cha kumfanya mtu ashindwe kujilinda dhidi ya mbinu na mitego ya yule mwovu. Kwa hakika ni vigumu sana kuwa 100% macho wakati wote, katika nyanja yoyote ile ya maisha. Hata kama askari akiwa macho lindoni pake, hakuna dhamana kwamba ataendelea na kiwango kile kile cha kuwa macho ili kumwona adui akimnyemelea katika lindo lake hilo. Kwa Wakristo, hali hii ni ngumu zaidi – na ni muhimu zaidi. Hutokea wakati fulani utamwona Mkristo akitembea karibu sana na Mungu katika amani na furaha kubwa kwa sababu ya ushindi fulani wa kiroho alioupata katika mpambano fulani na/au kujifunza na kuelewa ukweli fulani wa kiroho … halafu anarudi nyuma na kukumbatia tena fikra za kidunia. Si lazima jambo hili liwe dhambi, lakini kutokana na ukweli kwamba tunayo hulka ya dhambi, tumezungukwa na fujo na vishawishi vya ulimwengu, tuna shughuli na majukumu mengi yanayohitaji na yanayogombania muda wetu, si jambo geni sana kujikuta, hata kama tumepevuka kiroho na mwendo wetu na Bwana ni mzuri sana, tunapoteza dira katika mioyo yetu – hata kwa muda mfupi tu – kutoka kwenye zile kweli ambazo tunajua ndani ya mioyo yetu kuwa ni muhimu sana. Tatizo ni kwamba hata katika kujisahau kwa muda mfupi tu tunapokuwa “lindoni” kunaweza kusababisha tushambuliwe ghafla – na yule mwovu ni nguli katika mashambulizi ya ghafla:

Muwe watulivu (sober/nepho) na mkeshe, kwani adui yenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka akimtafuta wa kummeza.
1Pet. 5:8

Waumini waliopevuka ambao wamefanya desturi ya kujitayarisha kwa vita kwa kujifunza kweli ya Mungu, kuiamini na kuitumia wakati wote, wanakuwa wagumu kuathirika kwa kiasi kikubwa hata kama “wanajisahau” kwa muda mfupi na kushambuiwa ghafla. Hakuna aliye mkamilifu, hata yule aliyeendelea sana kiroho, hivyo basi mbinu tulizojadili hapo mapema katika somo hili – pamoja na harakati ambazo kila mmoja wetu ameziendeleza binafsi katika kujirejesha kwenye msitari na kurekebisha hisia zetu mara matatizo yanapotokea – huhitajika kila wakati tunaposhambuliwa ghafla. Lakini wale wote wanaotembea karibu na Bwana wanapata urahisi katika kurejea kwenye msitari na inakuwa kama ‘hulka yao ya pili’ (second nature) kufanya hivyo, wakati wale ambao hujihusisha na kweli mara moja-moja tu, katika kuisoma/kuisikiliza na kuitafakari, wataona [ma]shinikizo ya maisha yakiwatingisha kiroho – wakati wale wanaolegalega kiroho watamwona yule “simba angurumaye” akiwa nyuma yao wakati wote.

5.18  Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi [ambao unafuja tabia njema uliyokuwa nayo awali]; bali mjazwe Roho (mwendelee kukua kiroho);

5.19  mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu;
5.20  na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo;
Waefe. 5:18-20 SUV

3.15 Na amani itokayo kwa Kristo iwe mwamuzi katika mioyo yenu [katika nini na namna ya kufikiri]: hii ndiyo amani ambayo kwayo wote mumeitwa katika Mwili mmoja; na muwe na shukrani!
3.16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkijifunza na kujipatia maonyo [ndani ya mioyo yenu] kwa busara, na kwa zaburi, kwa nyimbo na tenzi za kiroho mkiimba ndani ya mioyo yenu kwa Mungu.
3.17 Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa Jina lake [Kristo].
Wakol. 3:15-17

Hivyo basi, ili kuweza “kuvalisha mkanda viuno vya fikra/nia zetu katika kuwa macho kiroho”, kunatakikana mafunzo ya awali (ya kujitayarisha) ya kiroho, kuwa tayari kujiweka katika msitari wa kiroho wakati wa shinikizo, na kutimiza tendo halisi la kuvaa “deraya (armour) yote ya Mungu” tunavyopambana huku tukipanda mlima kuelekea Sayuni kwa ajili ya Kamanda wetu, Bwana Yesu Kristo.

2.3  Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu.
2.4  Hakuna apigaye [mpiganaji wa] vita ajitiaye katika shughuli za dunia, [hujizuia na mambo kama hayo] ili ampendeze Yeye aliyemwandika awe askari.
2Tim. 2:3-4 SUV

6.11  Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
6.12  Kwa maana mapambano yetu sisi si dhidi ya viumbe wenye damu na nyama; bali dhidi ya falme na mamlaka ya ki-malaika, dhidi ya wakuu wa giza hili [la sasa], dhidi ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
6.13  Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
6.14  Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii [deraya] ya haki (uongofu) kifuani,
6.15  na miguu yenu ikiwa imevalishwa utayari unaotokana na Injili ya amani;
6.16  zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
6.17  Tena [katika vita hii ya kiroho] ipokeeni chapeo [helmet] ya wokovu, na [mvae kiunoni] upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
Waefe. 6:11-17

6.12  Pigana vita vile vizuri vya imani;
1Tim. 6:12a SUV

1.18  Mwanangu Timotheo, nakukabidhi agizo hilo liwe akiba, kwa ajili ya maneno ya unabii yaliyotangulia juu yako, ili katika hayo uvipige vile vita [vya kiroho] vizuri, [kulingana na maneno yale ya unabii];
1Tim. 1:18 SUV

4.7  Nimepigana ile vita njema vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda;
2Tim. 4:7

Weka Tumaini Lako Katika Neema Zijazo:

“Ufunuo wa [Bwana] Yesu Kristo” unamaanisha ujio Wake kwa mara ya pili katika utukufu akiwa amevaa taji Lake la Ufalme na atasimika Ufalme Wake wakati huo. Katika siku hiyo tukufu, sisi waumini, ikiwa tungali wazima hapa duniani au tukisubiri siku hiyo kuu tukiwa katika uwepo Wake huko huko mbinguni, sote tutafufuliwa, “waliokufa katika Kristo” wakianza, halafu “sisi tulio hai” tukibadilishwa bila kifo cha mwili na kupaa katika ufufuo ili “kukutana na Bwana angani” (1Wathess. 4:15-17). Hilo ni lile “tumaini lililotukuka” ambalo Wakristo wote tumeliweka kama lengo kuu na ambalo tunapaswa kulitazama wakati wote.

2.13  Tukilitazamia tumaini lenye baraka na epifania ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; (nasi pia tutafufuliwa katika utukufu pale Atakapokuja).
Tito 2:13

Kama waumini wa Bwana Yesu Kristo waliozaliwa upya, sisi sote ni wapokeaji wa “ile neema ya Mungu yenye taswira nyingi mbalimbali” (1Pet. 4:10). Kwani katika “utimilifu” wa Kristo, sote tumepokea “neema juu ya neema” (Yoh. 1:16). Neema ni fadhila njema ya Mungu, na je, tunaweza kufikiria kuwa Mungu huyu huyu anaweza kutufanyia fadhila kubwa zaidi ya ile ya kufanya mauti kugeuzwa na kuwa uzima kwa njia ya dhabihu ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo kwa maondoleo ya dhambi zetu? Msalaba ni “neema”, na ndio mwanzo wa fadhila zote tunazopokea kutoka kwa Mungu baada ya kuamini. Katika dunia hii ya sasa, tutaendelea kuwa na “dhiki” (Yoh. 16:33), lakini katika uzima ujao, hakutakuwa na dhambi, hakutakuwa na kifo, hakutakuwa na uovu wa kuzuia ule mmwagiko/mtiririko usiokuwa na mfano wa neema zitakazokuwa za kwetu katika siku ile ijayo tukiwa kama memba wa Kanisa la Kristo.

2.9  lakini, kama ilivyoandikwa, “Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu); haya ndiyo yale ambayo Mungu aliwaandalia wampendao”. 1Wakor. 2:9
Ni kwa namna ipi basi, “tunaweka tumaini letu” katika neema zijazo? Kwa maelezo rahisi, tunapaswa kwanza kujifunza yote tunayoweza – mafundisho yote katika Biblia – kuhusu utukufu ujao. Hii inahusisha mafundisho yote yanayohusiana na ufufuo na mengine yote yanayohusiana na thawabu zetu za milele na urithi wetu katika Yerusalemu Mpya.4 Lakini pamoja na kujifunza na kuamini misingi hii ya kweli, tunapaswa kuwa tayari kutumia kanuni hizi katika maisha yetu ya kila siku. Na kwa hakika, kukumbuka kwamba tunao mwili usioweza kuharibika ukitungojea “milele [huko] mbinguni” (2Wakor. 5:1), na thawabu za milele, zinazohifadhiwa kwa ajili yetu mbinguni “ambapo hapaharibiki kitu kwa nondo wala kutu, na wevi hawawezi kuvunja na kuiba” (Matt. 6:20) ni jambo la kutia moyo sana, hasa tunapokuwa na maumivu ya mwili au uhaba wa mahitaji yetu katika muda huu mfupi wa uhai wetu hapa duniani, kwani tumaini hili la thawabu na ufufuo ni lengo halali na la lazima kwa imani yote ya Wakristo kama inavyotumiwa katika “mtazamo wa uwanja wa vita”, mtazamo ambao ni lazima tuwe nao ili tufanikiwe katika vita ya kiroho ambayo tunapambana:

11.6  Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba Yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.
Waebr. 11:6 SUV

1.3  Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;
1.4  tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.
1Pet. 1-4 SUV

Kwa maneno mengine, “kuweka tumaini letu” katika utukufu ujao wakati Bwana wetu atakaporudi ni mfano wa “kuvisha mikanda viuno vya nia zetu” katika kuwa macho (na “sober”) kiroho. Kuelekeza fikra zetu katika neema za milele ijayo ni sehemu muhimu ya namna ya “kupita salama na kuimaliza kila siku” kwa Mkristo anayeendelea kukua, maadamu inaitwa “leo” (Waebr. 3:13; cf. Zab. 118:24), kwa sababu ijapokuwa yule mwovu hajisumbui sana na waumini wanaorudi nyuma au waliosimama, tuwe na uhakika kabisa kwamba kwa muumini anayefanya maendeleo halisi ya kiroho, jambo hili huleta upinzani na uadui halisi wa yule mwovu na wakala wake. Mungu ametupatia KWELI yote tunayohitaji (Biblia yote), uwezo tunaouhitaji (Roho Mtakatifu ndani yetu), na mbinu tunazohitaji (“kuvaa mkanda” kifikra ili kutumia kweli hizi kupitia uwezo wa Roho Mtakatifu). Kinachohitajika hapa ni sisi kutumia rasilimali hizi katika kumtumikia Bwana Yesu Kristo.

10.4 Kwani silaha za vita tunayopigana si za kimwili, bali zina uwezo katika Mungu, wa kuangusha ngome,
10.5 kubomoa hoja za ghiliba, za uwongo; na kila kiburi au ufidhuli unaojipandisha dhidi ya ufahamu wa Mungu, na kuiteka nyara kila fikra ili ipate kumtii Kristo;
10.6 tukiwa tayari kutoa onyo kwa kila wazo lenye ukaidi mara tunapofikia kiwango cha kutii katika upevu wetu wa fikra adilifu.
2Wakor. 10:4-6

Tumo katika vita halisi na ya kufa na kupona, “vita ya kiroho” ambamo silaha zetu si za dunia hii, bali ni silaha za kanuni za KWELI, za Roho Mtakatifu, na medani za kukusanya silaha hizi pamoja, na kupambana na uwongo wowote, [ma]shinikizo yoyote, majanga yoyote, mashaka yoyote, zitapatikana katika maisha ya hapa hapa duniani (kwa hakika tutapata mbinu hizi). Hii ni kusema, yote yanahusiana na ile kweli, kujifunza (kwa kujituma sisi wenyewe kusikiliza, kusoma mafundisho ya Biblia kutoka kwa mwalimu mahiri), kuamini mafundisho hayo (ambapo Roho Mtakatifu Anatufanya tuweze kuitumia kweli hiyo), nasi kuweza kuitumia kweli hii katika mazingira yoyote yatakayotukabili katika maisha yetu, kweli hii ni upanga mkali wa vita, ikiwa imefunuliwa kwetu, imefanywa halisi, na imetiwa nguvu na Roho Mtakatifu:

6.17  Tena [katika vita hii ya kiroho] ipokeeni chapeo [helmet] ya wokovu, na [mvae kiunoni] upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
Waefe. 6:17 (cf. Waebr. 4:12)

Sasa, “kuvaa mkanda” na “kuwa macho” na “kuweka tumaini letu”, kiuhalisia ndiyo njia pekee ya kuimarisha mwendo wetu kwa ajili ya Bwana Yesu Kristo katika maisha yetu, njia pekee halali ya kushinda, kwa ajili Yake, mateso, mitihani, majaribu na dhiki ambazo waumini wote wanaoendelea [kiroho] ni lazima wapitie. Vita hii yaweza kuogofya, kukatisha tamaa wakati fulani, lakini tunapaswa kukumbuka kwamba Bwana wetu amekwishashinda kwa kishindo, na sisi tunatumia tu nyara alizoshinda Yeye ili tupate mgawo wa hizo nyara kama thawabu yetu ijayo – ikiwa tutaingia katika vita hiyo kwa kupigana vita njema ya imani kwa ushujaa.

16.33 Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo [mtapitia] dhiki [tribulation]; lakini jipeni moyo (muwe na ushujaa); [kwani] mimi nimeushinda ulimwengu!
Yoh. 16:33 SUV

5.4  Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu [katika Kristo].
1Yoh. 5:4 SUV (cf. aya ya 1)

2.26  Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu [moyoni mwake] hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,
2.27  naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, [na atawaponda] kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea [mamlaka kutoka] kwa Baba yangu.
Ufu. 2:26-27 SUV

Notes:

1. Ili kuona sehemu muhimu sana ya Roho Mtakatifu katika medani/mbinu za vita ya kiroho inayojadiliwa katika somo hili, tafadhali tazama: Bible Basics Part 5: “Pneumatology”, Section II.B.3.b, Empowering the Believer”.

2. Katika masomo #16 na #17 ya mfululizo huu.

3. Katika Bible Basics Part 4B: “Soteriology”, Section II.7.c, “Our New Orientation as Reborn Believers”.

4. Pamoja na sehemu zingine ambapo mambo haya yanajadiliwa na Ichthys.com, tafadhali tazama mahususi: Coming Tribulation: Part 6: The Millenium and New Jerusalem.

=0=
Imetafsiriwa kutoka: Maintaining a Sound Christian Offense in our Spiritual Warfare: Peter’s Epistles #29

=0=

Basi, na tuonane katika sehemu #30 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!