Mafundisho 3 ya Uwongo Yaliyo Hatari kwa Imani ya Mkristo: Nyaraka za Mtume Petro #27

Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

“Imani ndiyo mapigo ya moyo ya uzima wetu wa milele”

Utangulizi: Kabla ya kumaliza mjadala juu ya 1Petro 1:6-9, tunahitaji kuchambua kanuni 3 zinazofundishwa na makundi mbalimbali kuhusiana na wokovu wa Mkristo. Mafundisho yote matatu yanaweza kuteketeza imani ya Mkristo. Mafundisho hayo ni:

1) Ulinzi/Usalama Ndani ya Dhehebu
2) Ulinzi/Usalama wa Milele
3) Ulinzi/Usalama Katika Dhiki + Dhiki Kuu

Mafundisho haya 3 yameleta madhara katika historia ya Kanisa na yanaendelea kuleta madhara leo hii. Jambo linalotia hofu ni kwamba Wakristo wa siku za usoni watakaokabiliwa na ile Dhiki Kuu (The Great Tribulation) wamo katika hatari kubwa kutokana na fundisho la kanuni hii.

Hatari Zilizofichika Ndani ya Mafundisho ya Uwongo: Mafundisho ya uwongo yamekuwepo tangu mwanzo wa historia ya mwanadamu, tangu ndani ya Bustani ya Edeni, wakati Ibilisi alipopotosha amri ya kisheria ya Mungu dhidi ya kula tunda kutoka katika mti wa ujuzi wa mema na mabaya:

4 Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, 
5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.
Mwa. 3:4-5 SUV

Huu ulikuwa uwongo. Wazazi wetu walikufa [palepale] kifo cha kiroho (utengano na Mungu), kikifuatiwa na kifo cha kimwili baadaye kidogo (ambayo yalikuwa matokeo ya kutotii). Maneno ya Shetani yaliyosemwa kupitia kinywa cha nyoka katika Mwanzo 3:4-5 yanatupatia mfano unaotia hofu ambao waumini wote wanapaswa kujifunza na kuukumbuka, kwani jaribu lile la bustanini ni kielelezo cha uwongo wote uliofuata [baadaye] wa Shetani. Kiini cha uwongo unaofanikisha malengo yake [uwongo huo] ni hiki: una kiasi fulani cha ukweli ndani yake, na unamvuta mtu kuamini, na una taswira ya juu juu ya utakatifu:

1) kiasi fulani cha ukweli: Adamu na Eva hawakuanguka chini mara moja na kufa; na kwa kweli macho yao “yalifunguliwa” - kama watenda dhambi, wakatambua mara moja mema na mabaya, na, matokeo yake ni kutengwa na Yule aliye Mwema, yaani Mungu.

2) mvuto: Unawashawishije watu 2 ambao wana kila kitu? Walikuwa wanaishi paradiso! Shetani, kwa ujanja mkubwa, alipata njia. Adamu na Eva walikuwa na Mwenye Mamlaka juu yao ambaye alikuwa Bwana Mungu waliyekuwa na ushirika Naye kila wakati (Mwa. 3:8; 2:19). Je, hautapenda kuwa “kama Mungu?”, Ibilisi aliuliza. Bila shaka ni ufidhuli wa kiburi cha hali ya juu kwa kiumbe kudhani kwamba anaweza kuwa katika kiwango kimoja sawa na Muumba wake, lakini lugha iliyotumika na Shetani ni ya ujanja sana, kwani masikioni, inasikika kama vile ni “kitu chema”. Mungu ni mwema. Je, kuwa kama Mungu si kitu chema pia? Kwa hakika “kuwa kama Mungu” kwa juhudi zetu wenyewe ni hatua ya kwanza tu katika udanganyifu [wa nafsi] uliojaa kiburi unaopelekea “kutaka kuwa sawa na Mungu”, “kuwa Mungu”, na mwisho wake “kuchukua nafasi na madaraka ya Mungu”. Kwani huu ndio mchakato ule ule ambao Ibilisi mwenyewe aliupitia, yule kerubi aliyependwa na kupendelewa sana, ambaye hata sasa bado yuko katika uasi dhidi ya Mungu, bado akiwa na nia ya kuchukua madaraka ya Mungu. Mvuto wa kuwa “mungu” kwa kiburi tu una nguvu sana, na hii ndiyo motisha (inayofundishwa katika taswira mbalimbali) iliyo nyuma ya makundi (cults) na dini mbalimbali za uwongo zilizoko duniani (hasa zile zinazovaa joho la Ukristo).

3) muonekano wa utakatifu: Kupitia dalali wake, yule nyoka, Ibilisi alitumia maneno machache lakini yaliyopangwa kwa uovu mkubwa, anamzungumzia Mungu, ufahamu [wake wa] Mungu, na maendeleo binafsi ya kiroho. Anamzungumzia Mungu katika namna ya upendeleo, kama vile anamfahamu na kumheshimu. Hamsemei Mungu kwa mabaya moja kwa moja, bali anapenyeza kiasi kidogo cha shaka katika uelewa wa Eva wa maelekezo/amri ya Mungu: ni kama vile anamwambia Eva kwamba yeye [Eva] hajaelewa, na kwa kweli hajapewa dondoo zote za amri ile; lakini sasa ngoja nikwambie kila kitu ambacho unatakiwa kujua, stori halisi; na kama utakula tunda hili linalopendeza, utakuwa umefaidika zaidi; huoni kwamba hata Mungu mwenyewe anataka uwe kiumbe chake bora zaidi, anayejua vyote kuhusu mema na mabaya? Uwongo unaofanikiwa haupingani na ukweli moja kwa moja; badala yake unachukua nafasi ya ukweli. Katika kuuchukua mateka ule ukweli, mwongo atajaribu kuufanya uwongo wake ufanane na ukweli kwa kiasi kikubwa anavyoweza (ndiyo maana “cults” zote ambazo kiuhalisia hazina uhusiano wowote na Ukristo wanasema mambo mazuri kuhusu Bwana Yesu Kristo, haswa mwanzoni). Shetani aliuvalisha uwongo wake katika joho lenye taswira ya utakatifu kufikia kiasi kwamba Eva akaanza kukubali kwamba anachokifanya ni kitu sahihi na cha maendeleo ya kiroho. Hili si jambo la kushangaza tunapotazama ujanja na mafanikio ya shambulio la Shetani, kwani:

a. alitumia sura ya kirafiki ya dalali au wakala wake [aliyezoeleka na Eva]: Katika ujanja wake, Shetani hakumtokea Eva yeye mwenyewe. Badala yake alimtumia nyoka, ambaye tunadhani alikuwa na mazoea na Eva.

b. mazoea na Mungu: Ibilisi anaongea na Eva akitumia lugha/maneno yaleyale ambayo Bwana Mungu aliyatumia (katika Kiebrania ni karibu 100% - isipokuwa kwa neno [hamta]kufa). Anajifanya anafahamiana na Mungu vizuri sana, ingawa anatumia neno-cheo “Mungu” badala ya “Bwana Mungu” (katika Kiebrania) ambayo inaonyesha heshima zaidi (1Petro 3:6).

c. alifanya shauku/tamaa za ndani ya moyo [wa Eva] zionekane kuwa halali: Ahadi ya uwongo ya Shetani ilikuwa na sehemu 2: “kujua mema na maovu” na “kuwa kama Mungu”. Ilikuwa ni ‘dili’ ya Shetani iliyofungwa kama zawadi. Uwongo huu wa kijanja ulimshawishi Eva kwamba gharama (“kujua mema na maovu”) inazidiwa na faida (“kuwa kama Mungu”). Bila shaka yoyote haya yalikuwa makubaliano mabaya sana, kwani ukweli wa jambo hili ni kwamba alikuja kuwa “kama” Mungu tu kwa kutambua kwamba kuanzia hapo [yeye] alikuwa ni mtenda dhambi, wakati “gharama” ya elimu/ufahamu alioshawishika nao ni (kiuhalisia): utengano na Mungu, kupata ghadhabu Yake na hukumu ijayo katika namna ya kifo cha kiroho, cha kimwili na mwisho wa yote kifo cha milele. Tumshukuru Mungu kwa ajili ya Yeye aliyelipia gharama ile kwa ajili ya Eva pamoja nasi kwa kifo Chake kwa ajili yetu, Bwana wetu Yesu Kristo!

Eva [aliyeanza kushawishiwa], na baadaye Adamu, hawakuwa na upungufu wa akili. Hili lilikuwa shambulio lenye ushawishi mkubwa ambalo lililenga mazingira yao, nasi tutafanya vyema kutahadhari na mashambulizi kama hayo leo! Itakuwaje rafiki wa karibu kabisa (au mtu mwenye hadhi, au taasisi inayoheshimiwa), ambaye anaonekana kama [vile] anamjua Mungu, ambaye anakupa zawadi yenye faida za kiroho kwako (kitu cha kuvutia sana kwako!) anakudanganya? Lakini wakati mwingine mtu huyu au taasisi hii inatuambia uwongo, na sisi waumini tunapaswa kujifunza ufahamu ili kupambana na mashambulizi ya uwongo kama haya juu ya imani yetu.

Adamu na Eva walikuwa na chanzo cha uhakika cha kupata taarifa za ukweli na uhakika: Mungu mwenyewe! Nasi pia leo hii tunacho chanzo cha uhakika kabisa, kama wao: Neno halisi la Mungu. Wazazi wetu wa mwanzo hawakulisikiliza Neno lililonenwa na Mungu. Hivyo, si jambo la kushangaza kwamba Wakristo wengi leo wanaweza kudanganywa, kwani wengi wetu hatulifuati Neno lililoandikwa, na hivyo tunaanguka kwa sababu ya uwongo ambao tunapaswa kuuona kwa urahisi unapokuja, na kwa hakika tunajua, lakini tunashindwa kuifuata ile tahadhari kwa imani. Na mara nyingi zaidi, Wakristo wengi wanajiweka hatarini kwa kutochukua muda na fursa ya kujifunza kuhusu matakwa na mawazo ya Mungu wao (kwa kusoma Biblia na kufundishwa Biblia), ili kwamba mitihani na majaribu vitakapokuja, wasidanganyike na waalimu wa uwongo na mafundisho ya uwongo. Hivyo kama ilivyokuwa kwa Adamu na Eva, chanzo cha habari njema kipo, na majibu ya maswali yetu yapo pia, na Mungu ameahidi kutupatia habari tunayotaka kujua ikiwa tu tutamwomba Yeye (Yakobo 1:5). Tukiwa na bidii katika kujifunza Neno lake la kweli, inakuwa vigumu zaidi kwa Ibilisi kupenyeza uwongo wake unaotamanisha, wenye uwezo wa kutia kikwazo kati yetu na kweli, na hivyo kati yetu na Mungu.

Mafundisho/Kanuni 3 za Uwongo Zinazotishia Imani Yetu: Kwetu sisi Wakristo, hakuna suala la muhimu zaidi ya kukuza, kulea na kutunza uhai wa imani yetu katika Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo. Ndiyo maana ninaamini kwamba ni muhimu sana kwa waumini kuwa na ufahamu na tahadhari kuhusu mafundisho haya 3 yaliyoenea sana na yanaheshimiwa sana kwani ni ya uwongo na yanatishia imani yetu (ikiwa tutayaamini na kuyatumainia). Ulinzi/Usalama ndani ya Dhehebu (Institutional Security), Ulinzi/Usalama wa Milele (Positional Security), na Ulinzi/Usalama Katika Dhiki + Dhiki Kuu (Tribulational Security) ni mafundisho ambayo yanaweza kuonekana kuwa hayana madhara yoyote (yakitizamwa juu juu tu), lakini hapo ndipo yanapofanana na uwongo wa Shetani pale bustanini – si shambulizi la moja kwa moja dhidi ya imani yetu, bali ni mashambulizi ya chini kwa chini, ya kijanja, yaliyojificha ambayo yanaweza kuweka imani yetu hatarini katika nyakati za shinikizo.

Ulinzi/Usalama Ndani ya Dhehebu (Institutional Security): Hili ni fundisho kwamba wokovu ni matokeo ya uanachama katika kanisa (dhehebu) au taasisi fulani tu. Kwa hakika kuna aina nyingi na tofauti za fundisho hili. Aina hizi ni kutoka kwa kauli thabiti na za wazi, kama ile ya kanisa/dhehebu la Roma ya non salus extra Ecclesiam (maana yake: “hakuna wokovu nje ya kanisa [Katoliki la Roma]”), mpaka zile kauli zinazopenyezwa kwa ujanja katika mazungumzo kwamba bila “kujiunga” na kanisa letu, uzima wako wa milele uko hatarini; aina hizi za kauli za wokovu-uko-kwetu-tu zinavalisha kiatu cha kulia katika mguu wa kushoto, kwa kufanya ushiriki katika taasisi fulani kuwa ni sharti la wokovu. Hii ni kwa sababu kanuni hii ina lengo la kuwaingiza watu katika taasisi hiyo na wasiondoke mara wakishaingia. Lakini upande wa pili wa fundisho hili ambalo msingi wake ni kutia watu hofu, ni matokeo ya ule uwongo wa upande wa kwanza (unaosisitizwa na makundi mengi yanayofundisha hili) kwamba ukijiunga nao, na ukaendelea kuwa “mwanachama mzuri”, basi utaokolewa kwa sababu ya uanachama wako. Upande wa kwanza wa hoja/fundisho hili, na ule wa pili, hauna msingi wa Kibiblia kabisa!

Matokeo mengine yanayotokana na kanuni hii ya uwongo yanahusika na utoaji wa ibada (kama ubatizo); utoaji wa baraka (kama “second blessing” ya Wa-karismatiki ambamo wanadai utanena lugha, utatoa unabii, utaponya, n.k.); ufahamu maalum (special knowledge) au desturi yoyote ile ndani ya dhehebu, iwe halali au siyo halali, pale unapolazimishwa ushiriki katika desturi hiyo ili upate wokovu. Imani kwamba kiongozi wa kanisa, kanisa lenyewe, au kundi fulani lina ufahamu fulani wa muhimu sana, tena ni wa lazima ili upate wokovu, ambao hauwezi kupatikana mahali pengine, hupelekea watu kufikiria kwamba utii na wajibu wao kwa mtu huyu au kundi hili ndio unamhakikishia wokovu, na sio utii na wajibu wao kwa Kristo na Kanisa Lake.

Hakuna kielelezo kizuri cha fundisho hili la uwongo na matatizo yake, zaidi ya hali au mazingira aliyokabiliana nayo Bwana wetu. Katika wakati wa Bwana Yesu Kristo hapa duniani, ibada ya Mungu ilikwishafanywa kuwa ni “taasisi” nje ya Sheria ya Musa, na kupungua katika uhalisia na ufahamu wa kiini cha kweli iliyomo ndani ya Sheria hiyo, kiasi kwamba ingawa mfumo wa Mafarisayo, Masadukayo na Waeseni ulikuwa na njia nyingi za kumtafuta Mungu, haukuwapatia njia yoyote ya kumwona [Mungu]. Wakati fulani, Bwana wetu aliwaambia baadhi ya wawakilishi wa jamii hizo za kidini wazi wazi kwamba ijapokuwa wao walidhani kuwa wana uzima wa milele ndani ya maandiko waliyoyaazimia na kuyatamka, kiuhalisia walikosa kukiona kiini halisi cha maandiko hayo: maandiko yanamhusu Yeye (Yoh. 5:39; tizama pia Matt. 23:13-28). Ama kwa hakika, hiki ndicho kiini cha maandiko. Tunatakiwa kumwamini na kuwa wafuasi wa Bwana Yesu Kristo. Watumishi wa Mungu, taasisi zinazoundwa kumtumikia Yeye, lengo lake ni kuwasaidia waumini kufanikisha jukumu lao la kuishi kama Wakristo. Matatizo hutokea pale watu na taasisi zinazotakiwa na zilizokusudiwa kufanya hivyo, zinaanza kuwa na lengo tofauti na hilo.

Kutoka kwa mtazamo wa muumini, hatari iliyoko inahusiana na wokovu. Kwani mtu hawezi kuweka utiifu wake katika nafsi asiye Kristo, au katika taasisi badala ya Kristo, na wakati huo huo akawa muumini katika Kristo. Na pale taswira ya imani inapoanza kuchafuliwa kwa utiifu kwa mtu au utiifu kwa taasisi kwa kufundisha kwamba wokovu unapatikana kwa msingi wa utiifu huo, hatari nyingine (nayo si ndogo!) ni kuridhika na hali hiyo. Mara mtu huyu au taasisi hii inapokuwa ndiyo mlengwa wa imani, basi ile haja, ule msukumo wa kukua kiroho, kumfuata Mungu na kusogea karibu Naye, kama jambo lisiloepukika, kunapungua. Na kuridhika na hii hali nako kunaongeza hatari dhidi ya usalama wetu wa kiroho, kama tutakavyojadili hapa chini.

Katika historia ndefu ya Kanisa, kanuni hii ya uwongo ya kwamba wokovu u katika dhehebu fulani imekuwa na madhara makubwa zaidi ya zile kanuni nyingine 2 tutakazojadili hapa. Kama ilivyokuwa katika udanganyifu wa Shetani kwa Eva, uwongo huu una ushawishi mkubwa:

1) una kiasi kidogo cha ukweli ndani yake: Umuhimu wa kuwa sehemu nyeti ya Kanisa la Kristo hauna mjadala, lakini ni kosa kuilinganisha hadhi hii ya kiroho ya Wakristo wote wa kweli, na mtu yeyote au kikundi/taasisi yoyote. Kwa Wakristo, sisi sote ni sehemu ya Mwili mmoja, sote tuna karama maalum na tumekabidhiwa majukumu ya kitumishi yenye lengo la kujenga imani ya Wakristo wenzetu (Waefe. 4:11-16). Mwili huu ni “Mwili wa Kristo” na Bwana wetu anamjua kila aliye wa Kwake (2Tim. 2:19; cf. Yoh. 10:14; 1Wakor. 8:3). Hakuna mtu mwenye kibali rasmi [binafsi] cha imani ya kweli katika Kristo. Hakuna taasisi yenye ufunguo wa wokovu wetu. Kama kweli tunaamini katika Bwana Yesu Kristo, basi sisi ni sehemu ya Kanisa Lake, na katika mabadiliko na maendeleo mengi ya mifumo ya ibada, ya huduma na ya taasisi kwa mileniamu zote hizi mbili za historia ya Ukristo, ukweli huu haujabadilika. Utiifu na uaminifu wa Mkristo ni lazima uelekezwe kwa Kristo, si kwa mazoea, utamaduni, mila na desturi, si kwa taasisi, si kwa mtu. Kwani ni uaminifu wetu usiotetereka kwa Kristo, imani yetu endelevu Kwake, ndiyo inayopelekea kwenye wokovu, na si uaminifu kwa mtu, kikundi au taasisi yoyote hapa duniani.

2) una ushawishi mkubwa: Kuna taswira kadhaa za kanuni hii ambazo wengi wamevutiwa nazo. Ya kwanza (na iliyo wazi) ni kwamba yule mfuasi wa taasisi hana ulazima wa kufanya mabadiliko ya kiroho ambayo kwa muumini wa kweli wa Kristo ni mchakato muhimu unaoendelea katika maisha yake yote hapa duniani (War. 12:1-2; Waefe. 4:23-24). Hata makundi ya Ukristo wa uwongo yanadai mabadiliko ya kuonekana nje/usoni kutoka kwa wanachama wao, lakini kujitoa kwelikweli kwa Mungu kutoka rohoni, ufuasi wa kweli wa Ki-biblia kwa Kristo, kubeba msalaba wako kila siku na kumfuata – kujisabilia (kuwa ‘devoted’) kwa namna hii kwa kawaida si lazima kwao ili uendelee kuwa mwanachama mzuri. Kwani kwa kufuata na kutimiza sheria za taasisi, basi “bima” ya mwanachama au mfuasi inaendelea kuwa “hai”. Sehemu au taswira ya pili ya mvuto wake [kanuni hii ya uwongo] imefichwa kwa werevu zaidi. Anachokitaka Mungu kutoka kwetu ni mabadiliko ya rohoni na ufuasi wa kweli wa rohoni kupitia kwa Mwanaye, lakini watu wengi wanataka kupita njia yao wenyewe, yaani kuwa wafuasi kwa juhudi zao wenyewe na kupata thawabu kwa kustahili wao wenyewe. Sasa, njia ya Mungu wetu ni neema, nacho ni kitu chema kwetu, kwani kwa vile hulka yetu ni ya dhambi, chochote tunachokifanya bila Yeye (yaani nje ya Mungu) maana yake ni machukizo kwa hulka Yake iliyo timilifu, takatifu na safi. Hii ndiyo sababu Bwana Yesu Kristo alilazimika kufa kwa ajili yetu (mahala petu) ili tuweze kumsogelea Mungu aliye Mwongofu kwelikweli kwa msingi wa kazi ya Kristo na siyo kazi yetu sisi wenyewe. Lakini tangu pale Kaini, ambaye aliamua kumpa Mungu matunda ya kazi yake mwenyewe (badala ya sadaka ya damu ambayo inaashiria ulazima wa mbadala kufa kwa ajili yetu), wamekuwepo wale ambao wanavutiwa na kile wanachoweza ‘kumfanyia’ Mungu badala ya kile Mungu alichokifanya kwa ajili yao (tizama mfano wa Namani Msiria: 1Wafa. 5). Kazi za “kiwango cha juu kabisa” cha namna hii zina nafasi kubwa sana katika taasisi zinazofundisha kanuni hii ya udanganyifu: siyo tu kwamba uko salama mbele za Mungu kwa sababu umejiunga na ‘kundi Lake’, lakini [pia] tizama yale uliyoyafanya ‘kwa ajili ya Mungu!’ Mafundisho na mitazamo yote ya namna hii ni [upumbavu] (folly) wa hatari kabisa.

3) una mwonekano/taswira ya utakatifu:

a) taswira ya kirafiki: Likiwa na historia ya miaka mingi, mila na desturi zilizoota mizizi, kanisa la wakati wa Martin Luther (hakukuwa na taasisi nyingine ‘ya Kikristo’) lilikuwa na wadhifa mkubwa na wa kutisha, na mamlaka ya pekee. Je, mtu alikuwa na wapi pengine pa kugeukia? Na tumshukuru Mungu kwamba Martin Luther na wenzake ambao walimtafuta Mungu kikwelikweli, waligeuka kwa Mungu na Neno Lake badala ya kutegemea mazoea, usalama wa taasisi na mila na desturi. Hata hivyo, tahadhari! Tusisahau mvuto wa mazoea, mila na desturi. Walengwa wa ule waraka kwa Waebrania walishamtambua Kristo, lakini wakati huohuo ibada za hekalu la Yerusalemu zilikuwa na kishawishi kikubwa kwao, na, ijapokuwa walikwishafundishwa kwamba ishara zile za ibada za Agano la Kale ziliishatimizwa kwa kifo cha Bwana Yesu, kwa sababu ya mazoea na kuogopa kusemwa na Wayahudi wenzao, wakavutwa nyuma na kufanya tena ibada za kuchinjwa hekaluni, tendo ambalo ni sawa na kuazimia kwamba sadaka ya Kristo haikufaa kitu katika maondoleo ya dhambi (Waebr. 6:4-6).

b) mazoea na Mungu: Dini maarufu duniani ambazo zimefanywa taasisi, hata zile ambazo ni za Ukristo wa uwongo, mara nyingi husema mambo mazuri kuhusu Mungu na wameweka nafasi ya pekee kwa ajili ya Kristo. Lakini tunajua ya kwamba kuna njia moja tu ya kwenda kwa Mungu Baba, nayo ni kupitia Mwana wake pekee. Hakuna ibada ya kuchanganya “miungu” wengine wadogo au watakatifu au malaika au watu, waume kwa wake – wanaoishi au waliokufa, inayokubalika na Mungu (Yoh. 14:6).

c) kuhalalisha shauku/tamaa za siri za ndani ya moyo: Ni hulka ya wanadamu kwamba tuna uhitaji wa kuwa sehemu ya makundi makubwa yanayotuondolea mashaka na kutojiamini kwetu tunapokuwa peke yetu. Hii ni shauku halali kabisa, na inaridhishwa kwa 100% na uhusiano wetu na Mungu wetu mwenye upendo mkuu, kwa njia ya Bwana Yesu Kristo. Lakini kutafuta ridhaa ya shauku hii kwa watu au taasisi za kibinadamu ni [upumbavu] (folly), na kusalimisha utashi na uwezo wetu wa kuamua kwa mtu au taasisi ni kutafuta janga la kiroho, kwani mwisho wa yote, tunawajibika na maamuzi yetu, hata kama tulisalimisha jukumu hilo kwa taasisi iliyo “kubwa” kuliko sisi wenyewe. Hatari iliyoko ni halisi na kubwa, kwani wanadamu hupata faraja wanapokuwa sehemu ya kundi kubwa na wenzao: “Watu wengi namna hiyo haiwezekani wakakosea!” na “Kuna usalama katika idadi kubwa ya watu!” Labda kama Mungu wetu angekuwa hajatupatia mahala pa kwenda kuipata kweli, yaani maandiko, na mafundisho ya Neno Lake, mtazamo huu ungekuwa na uzito kidogo. Lakini tunayo Biblia tunayoweza kuisoma na kuitafakari kwa wakati wetu, na ni lazima tuwe wafuasi wa Bwana wetu, kokote Atakakoongoza, hata kama kuna kundi kubwa la wengine wanaoenda upande mwingine (Ufu. 14:4).

Ulinzi/Usalama wa Milele (Positional Security): Haya ni mafundisho kwamba wokovu hauna masharti yoyote na hauwezi kupotea mara mtu anapoweka imani yake katika Kristo. Tumekwishalizungumzia fundisho hili na kuona kwamba ni la uwongo katika sehemu kubwa ya masomo haya ya Nyaraka za Petro, haswa katika somo #12, (ijapokuwa si moja kwa moja). Kwani ingawa dhana ya “ukishaokolewa, basi umeokolewa daima” (OSAS – Once Saved Always Saved) ni ya kutia moyo sana, fundisho hilo halimo katika maandiko. Kwa kweli mwelekeo na tabia ya mafundisho ya Bwana wetu inazungumzia uhitaji wa uaminifu katika ufuasi wetu Kwake, na tumeona (na tutatizama tena hapa chini) aya nyingi za Biblia ambazo kwa wazi kabisa zinaonyesha mtazamo ulio kinyume na fundisho hili la uwongo, mfano: “Mwenye kuvumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka” (Matt. 10:22). Kama vile katika fundisho-fumbo la mpanzi wa mbegu, maandiko yanafundisha kwamba kuna kundi la watu ambao wanaamini Neno (kama vile kiuhalisia), lakini baadaye wanaanguka kutoka katika imani yao wakati wa taabu na mateso (Matt. 13:20-21); kuna wengine wanamea na kuota mizizi mirefu kuliko hawa (waliotajwa kwenye mfano uliopita), lakini wanashindwa kuzaa matunda kwa ajili ya Kristo kwa sababu ya kutafuta mali na anasa za dunia (Matt. 13:22). Ndugu yangu, kuwa makini katika hili – Mungu anataka na anatarajia tuwe, na tuendelee kuwa waaminifu. Kwa hakika, mapenzi Yake ni kwamba tuokolewe (1Tim. 2:4; 2Pet. 3:9). Wale wasiomtafuta kabisa, wale wanaomtafuta na kumwona na baadaye wanamgeuka na kumwacha, [yaani] wale wanaoenda kuonana Naye [wanapokufa] mikono mitupu – wote hawa wanafanya hayo kwa uamuzi huru na mapenzi yao wenyewe.

Ikiitwa pia kwa jina lingine la “Positional Security”, kanuni hii ikitazamwa katika maendeleo yake kihistoria, inaweza kueleweka kwa nini waanzilishi na watetezi wake wamekuwa na mtazamo huo, ijapokuwa si wa Kibiblia. Katika mapambano yao na kanisa la kitaasisi la miaka ya 1100 – 1500 AD ambalo liliwafundisha waumini wake kanuni zake ambazo hazikuwa za Kibiblia na zisizowezekana za kufika mbinguni kwa “matendo mema”, si jambo la kushangaza kwamba wana-teolojia wachanga wa kiinjilisti wa wakati huo wakatilia mkazo kwamba wokovu wa Mungu unapatikana bila masharti yoyote. Na pia si jambo la kushangaza kwamba wainjilisti wa miaka ya sasa wametafuta namna ya kuweka bayana teolojia ya wokovu na kuipambanua katika namna inayoeleweka kwa urahisi ya “OSAS” yaani “Once Saved Always Saved” au kwa kimombo chetu: ukishaokolewa, huwezi kupoteza wokovu wako. Lakini ukweli ni kwamba Mungu anawachagua wale wote wanaomtafuta Yeye (tazama somo #3 na somo #4), na anawafikisha salama Kwake wale wote wanaomfuata kwa uaminifu – na si waumini watimilifu wasiotenda dhambi (kwani watu wa aina hii hawako duniani; tazama somo #15), bali watu ambao wana imani inayostahamili katika milima na mabonde ya maisha yao, katika shida na raha, furaha na huzuni, wakimchagua Yeye na Mwanaye na si ulimwengu, katika hayo magumu yote. Kanuni ya uwongo ya “Ulinzi/Usalama wa Milele” inawapa faraja kubwa Wakristo, na kwa uhakika inasaidia sana katika kuondoa ukakasi na ukungu wa wokovu kwa matendo mema. Kwa waumini ambao kwa kawaida wanafuatilia kwa makini uhusiano wao na Mungu, wanamfuata Mwokozi wao, wanatumia kwa uaminifu vipaji walivyopewa na Roho Mtakatifu na utumishi waliokabidhiwa, kanuni ya OSAS si shida kwao – angalau katika nyakati za neema. Tatizo kubwa linalotokana na kuamini kwamba mara unapojitoa kwa Kristo basi umeokolewa maisha yako yote – hata iweje – ni kuridhika na kujisahau. OSAS inapelekea kujisahau katika imani yako na kujisahau katika dhambi (ambazo, zikifikia kiasi kikubwa bila kitubio, huwa ni tishio/hatari kubwa kwa imani na wokovu).

Tatizo hili limekwishajitokeza katika historia ya mwanzo ya Kanisa – si jambo la sasa pekee. Mwandishi wa waraka kwa Waebrania alifanya haraka kuwaonyesha wasomaji wake walioonyesha dalili za kuridhika na kujisahau kwamba walikuwa katika hatari ya “kupotea [pole pole] bila kujitambua” (Waebr. 2:1). Kumwasi Mungu na kuruhusu dhambi kuifanya mioyo yetu kuwa migumu, anawaambia, husababisha kutoamini (kwa Kiyunani apistia – hali ya kutokuwa na imani):

3.12  Angalieni [tahadharini], ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu [mwovu] wa kutokuamini, kwa kujitenga [kuasi kutoka kwa] na Mungu aliye hai.
3.13  Lakini mwonyane [na kutiana moyo] kila siku, maadamu iitwapo leo [tunapoendelea kuwa duniani]; ili mmoja wenu asifanywe mgumu [moyoni] kwa udanganyifu wa dhambi.
3.14  Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu [wa imani] kwa nguvu mpaka mwisho;
Waebr. 3:12-14 SUV

Jambo la kusikitisha ni kwamba, huu ulikuwa ni mwenendo kama ule wa kutoonyesha imani wa kizazi cha kutoka Misri uliosababisha karibu wote waanguke kutoka kwa Mungu, hata baada ya kuona miujiza ya kustaajabisha ya mkono wa Bwana (Waebr. 3:15-19; 12:25). Hivyo fundisho la uwongo la “Ulinzi/Usalama wa Milele wa Muumini” si tatizo kubwa kwa wale Wakristo wanaomfuata Kristo kwa bidii. Tatizo la fundisho hili ni kwamba likiaminiwa na Mkristo linaweza kuzaa tabia hatari ya kuridhika na hali iliyoko na kujisahau kwa sisi ambao si “wapiganaji” au si “wakereketwa” sana katika mwenendo wetu wa Kikristo. OSAS (Ulinzi/Usalama wa Milele wa Muumini) inapunguza kwa kiasi kikubwa mfumo wetu wa tahadhari wa kiroho, inapelekea tuanze kusinzia wakati dhambi inapoanza kuhatarisha maendeleo yetu ya kiroho, na inaweza kutia ganzi na kufifisha motisha yetu ya kuendelea kumtii Bwana kwa ari siku hadi siku. Katika hali ngumu, chini ya shinikizo kali na mateso, nyakati ambazo zinaweza kuipima imani yetu kwa Mungu mpaka ukingoni mwake, ni hatari mara dufu kuamini kwamba kila kitu kitakuwa murua hata iweje (hata nikivunja sheria za Mungu kiasi gani). Hii ni kweli … kwa wanaoamini, ikiwa tu tunakuwa waangalifu kutoihatarisha na kutoitelekeza imani yetu.

Kwa Wakristo wa sasa, Kanuni ya Usalama/Ulinzi wa Milele wa Muumini imekuwa ni fundisho lenye madhara makubwa zaidi kwa imani kuliko kanuni zile nyingine 2. Kama ilivyokuwa katika udanganyifu wa Eva na Shetani, nayo pia imekuwa uwongo wenye ushawishi mkubwa:

1) ina kiini cha ukweli: Ni kweli Mungu anatupenda, na Bwana Yesu alikufa kwa ajili yetu. Kwa sasa, sisi ni sehemu ya familia ya Mungu. Tumelipiwa, tumetakaswa, tumechaguliwa – na tuna uzima wa milele (na tuna Roho Mtakatifu kama dhamana ya uzima huu wa milele). Kanuni zote hizi 4 na nyingine zinatufundisha juu ya umuhimu wa milele, na mwisho wake usalama usiovunjika wa uhusiano wetu na Mungu kupitia imani yetu katika Kristo, Mwana Wake. Bali kwa sasa hatuwezi bado kuuishi kiuhalisia uzima huu wa milele. Kwani bado hatujawekwa katika ule mwili wetu mpya wa milele. Bado hatujaondolewa katika hii dunia, hatujapelekwa mbinguni, hatujatathminiwa, hatujathawabiwa na hatujakaa na Kristo milele. Bado tupo hapa – katika ulimwengu huu wa Shetani. Na kwa vile tupo hapa, mapambano bado yanaendelea; tunapoendelea kuwa katika maisha haya, ni lazima tuwe waaminifu, na juu ya yote, tuitunze na tuiendeleze imani yetu. Baraka zote za milele tulizoahidiwa zinapatikana kwa, na msingi wake ni, imani hii tuliyo nayo kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini tukiitelekeza imani hii, tunatelekeza faida zote zinazotokana nayo (tizama hapa chini kwa maelezo ya sharti hili muhimu).

2) ina ushawishi/mvuto mkubwa: Ushawishi mkubwa wa fundisho hili lisilo sahihi ni uhakika wa uwongo linalompa Mkristo kwamba mwenendo wake hauna athari, [haswa] ile athari nzito zaidi – upotevu wa wokovu wake. Je, dhambi binafsi zinakushinda nguvu? Hujisumbui kufuatilia uhusiano wa karibu zaidi na Mwokozi wako? Huna shauku ya kumtumikia Mungu kwa kutumia karama na utumishi uliopewa? Haya yote hayawezi kuhatarisha wokovu wako! Tulia na uwe na amani – unaweza kupata shida katika maisha yako, lakini hata ukiwa mvivu, hata ukiwa safihi (irreverent) kwa Mungu, hata ukiwa mwovu katika maisha yako, ukweli kwamba wakati fulani katika siku za nyuma ulikiri imani kwa Baba na Bwana Yesu Kristo unatosha kukuhakikishia uzima wa milele pamoja Naye na Mwana Wake – hata kama ulifikia hatua ya kumkataa Mwana Wake! Lakini kama tutakavyoona hapa chini, kuupuuza na kutoutunza uhusiano wetu na Mungu na kusalimu amri kwa dhambi kutatufanya, muda unavyozidi kwenda, tuwe wagumu katika mioyo yetu kiasi kwamba tunaweza kufanya mambo ambayo hatungefikiri kuyafanya – hata kumkataa Bwana aliyetugharamia na ambaye wakati fulani tulimwamini:

2.1  Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia.
2.2  Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa.
2.3  Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.
2Pet. 2:1-3

3) ina mwonekano (taswira) wa utakatifu:

a) wakala wa kirafiki: Baadhi ya wahubiri na walimu wazuri wa kiinjilisti wenye kuheshimika wanafundisha kanuni hii.

b) mazoea na Mungu: Fundisho la Usalama wa Milele, kwa usahihi kabisa linatilia mkazo upendo wa Mungu kwetu, lakini linaweka pembeni haki Yake na uongofu Wake.

c) kuhalalisha hamu/shauku/tamaa za siri za ndani ya moyo: Katika nyakati mbalimbali, sote tungependa kuamini kwamba Mungu mwenye upendo hawezi kututupa mkono, hata tukifanya nini. Na kwa kweli Mungu anatusamehe dhambi zetu kwa msingi wa kazi ya Mwana Wake msalabani kwa ajili yetu. Lakini tukimkataa Mwana Wake na kuikana kazi Yake, naye hawezi kujikana mwenyewe (2Tim. 11-13).

Ulinzi/Usalama Katika Dhiki na Dhiki Kuu Ijayo (Tribulational Security): Hili ni fundisho linalosema kwamba waumini wa zama za mwisho (dahari hii), hawatalazimika kupitia kipindi cha Dhiki + Dhiki Kuu, kwani watakusanywa katika ufufuo hai mara tu kabla ya kuanza kwa kipindi hicho kigumu. Kwa lugha nyingine ikiitwa The Pre-Tribulational Rapture Doctrine (au kwa kifupi “the rapture” yaani “unyakuo”: itazungumzwa hapa chini), kanuni hii si ya zamani sana. Ilianza kufundishwa mnamo karne ya 19, wakati wa majadiliano na shauku kubwa kuhusu unabii wa Biblia na mafunzo yake kuhusiana na matukio yaliyotabiriwa. Kiini cha fundisho hili kina msingi wake haswa katika 1Wathessalonike 4:13-18 [pekee], ambapo Paulo alikuwa akitafuta namna ya kuwaondolea Wathessalonike wale hofu kubwa waliyokuwa nayo kuhusu taarifa za uwongo zilizoingizwa katika mafundisho ya kanisa lao. Uvumi na minong’ono ilikuwa ikienezwa, kwamba ufufuo utawahusu wale tu ambao watakuwa hai wakati Kristo atakaporudi – hii ikiwa inamaanisha kwamba wale ambao walishakufa walikuwa wamepoteza nafasi yao ya kupata mwili mpya wa milele na uzima wa milele. Paulo anawahakikishia kwamba hiyo si kweli, na kwamba, waliokufa katika Kristo ndio watakaofufuliwa kwanza:

4.15  Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja [parousia] kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti.
4.16  Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni na sauti ya [amri itasikika], malaika mkuu [atapiga] parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.
4.17  Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa [harpazo, raptured] pamoja nao katika mawingu (umati), ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 1Wathess. 4:15-17 SUV

Kwa sababu kanuni hii inaambatana na ubishani na mgogoro mkubwa [ilipoanza kufundishwa, hata sasa], kuna ulazima hapa wa kuipinga kwa kifupi kanuni ya unyakuo wa kabla ya Dhiki Kuu, kabla ya Mileniamu:

1. Neno parousia: Katika aya hii hapo juu, neno linalotafsiriwa “ujio” ni neno la Kiyunani parousia, neno ambalo hutumika karibu kipekee katika muktadha wa ki-teolojia katika Agano Jipya kuelezea kurudi kwake Kristo, yaani pale atakaporudi Bwana wetu hapa duniani kuusimika ufalme wa mbinguni (cf. Matt. 24:3; 24:27; 24:37-39; 1Wakor. 15:23; Yak. 5:7; 2Pet. 1:16, 3:4 & 12; 1Yoh. 2:28). Hata katika muktadha wa hii barua ya 1Wathessalonike pekee, kigezo hiki kinabaki kuwa kweli (cf. 1Wathess. 2:19; 5:23), na kinapelekea tuhitimishe kwamba kukusanywa kwa waumini na Bwana wetu (katika aya hii) kutafanyika pale atakaporudi mara ya pili, na siyo (kama hoja ya kabla-ya-dhiki inavyodai) kabla ya Dhiki Kuu.

Zaidi ya hayo, katika matumizi ya neno parousia katika aya hiyo hapo juu, Paulo alikusudia Wathessalonike wale waelewe kwamba ni ujio wa pili wa Bwana Yesu na hili linawekwa wazi katika barua yake ya pili kwa hao hao Wathessalonike. Kwani katika 2Wathess. 2:1-3 na 2:8 Paulo anasema bila kumumunya maneno kwamba parousia ya Bwana ni lazima ifuate Uasi Mkuu na utawala wa mpinga Kristo (matukio ambayo bila shaka ni ya Dhiki Kuu), kiasi kwamba neno parousia katika aya hizo litakuwa linazungumzia Ujio wa Pili (kurudi), ambao ni ujio wa mwisho wa Bwana Yesu Kristo baada ya Dhiki Kuu, na siyo kwa ujio wa kinadharia wa muda mfupi kabla ya Dhiki Kuu kwa malengo ya “kulinyakua Kanisa”.

Muktadha wa aya hiyo hapo juu unathibitisha mtazamo huu. Wakati Wathessalonike wamechanganyikiwa kiasi kile kuhusu wakati wa ufufuo, bila shaka kulikuwa na umuhimu mkubwa wa kuwaelimisha kama Paulo alitumia neno parousia kumaanisha ujio wa muda tu ambapo Kristo anaishia hewani ili awanyakue Wakristo haraka-haraka, halafu kungekuwa na parousia nyingine kwa ajili ya kupambana na mpinga Kristo, kuwaokoa Wayahudi kutoka kwa wauaji wa mpinga Kristo, kunyakua Wakristo wengine (na hasa kwa vile tukio kama hilo halipo mahala pengine katika maandiko). Lugha inayotumiwa na Paulo katika aya hii pia kwa uwazi kabisa ingechukuliwa na wasomaji wake kumaanisha Ujio wa Pili wa Bwana wetu – bila ya maelezo mengine kinyume chake. Sauti kuu yenye mamlaka (Yoh. 5:28; na cf. Yoh. 11:43), malaika mkuu na mlio wa parapanda (Matt. 24:31; 1Wakor. 15:52; Ufu. 11:15; na cf. Yoh. 19:1-6) ni dalili za kukusanywa pamoja kwa wanaoamini, wafu na wazima, kulikotabiriwa kufanyika pale atakaporudi Mfalme (Matt. 24:31; Mk. 13:27; cf. Karamu ya Matarumbeta/Parapanda, ambayo inasherehekea kukusanywa kulikotabiriwa kwa Wayahudi wote wakati wa ujio wa pili wa Bwana: Walawi 23:23-25; & Hesabu 29:1-6. Hata kutajwa kwa “mawingu” (majeshi ya waumini waliofufuliwa wanaorudi: Ufu. 19:14) ni kuhusishwa kwa wazi kwa tukio hili na Ujio wa Pili (Dan. 7:13-14; Matt. 24:30; 26:64; Mk. 13:26; 14:62; Lk. 21:27; Ufu. 1:7).

2. Kutokuwapo kwa ushahidi wowote wa waumini walionyakuliwa: Licha ya umuhimu ambao kanuni hii ya unyakuo unapaswa kuwa nao kwa muumini wa wakati huu, hatuoni utajwa wa unabii wa waumini waliofufuliwa na kunyakuliwa wakingoja huko mbinguni mpaka wakati wa ujio wa pili. Hoja hii inayotokana na kimya hiki ina uzito mkubwa, kwani Ufunuo 6:9-11 inawataja wazi waumini ambao hawajafufuliwa ambao waliuawa (watauawa) wakati wa Dhiki Kuu na ambao wako mbinguni wakingojea ufufuo wakati wa ujio wa pili (hawa pia wanatajwa katika Ufu. 7:9-16 & 15:2-4).

3. Daraja/ngazi 3 za ufufuo: Wasifu aliouandika Paulo wa awamu au ngazi za ufufuo katika 1Wakor. 15:20-28 unatoa taswira ya wazi ya jinsi ufufuo wa waongofu utakavyofanyika katika historia (somo #20). Ufufuo utatokea katika ngazi 3, kama ifuatavyo:

a. “Kristo, zao la mwanzo” (aya ya 23). Kwa hakika Bwana wetu ameishafufuliwa, tukio kuu la asubuhi ya siku ile ya Pasaka!

b. “Baadaye, walio wake Kristo, atakapokuja” (aya ya 23). Neno “atakapokuja” ni lile lile “parousia” tena (tizama dondoo #1 hapo juu), hivyo awamu hii ya pili, kwa uhakika inahusisha waumini wote walioko mbinguni na walioko duniani wakati wa ujio wa pili. Hawa ni yale “mawingu” ya waumini watakaorudi na Mfalme wa Utukufu (cf. Dondoo #1 hapo juu, na Ufu. 19:14, ambapo panasimuliwa ‘kurudi kwao Naye’).

c. “Halafu mwishoni, atakapomkabidhi Baba ufalme Wake” (aya ya 24). Katika hitimisho la utawala wa mileniamu wa Kristo, historia ya wanadamu itafika mwisho wake, na mbingu na nchi kama tunavyozifahamu sisi zitabadilishwa na mahala pake “Yerusalemu Mpya, mbingu mpya na nchi mpya vitasimikwa” (Zab. 102:25-27; Isa. 34:4; 51:6; 65:17ff; 66:22; Matt. 24:35; Waebr. 1:10-12; 12:22-27; 2Pet. 3:10-13; Ufu. 20:11; 21:1-4). Wakati huu, “Ufalme wa Mbinguni” (enzi ya milele, ikitawaliwa na Baba na Mwana Kutoka Yerusalemu Mpya: tizama haswa Ufu. 21:22; 22:2-3), na awamu ya mwisho ya ufufuo wa waumini wa mileniamu (ambao bado wamo katika “miili hii ya nyama”, mwishoni mwa mileniamu), itafanyika. Kwani “mwili na damu haviwezi kupokea urithi katika ufalme wa Mungu (1Wakor. 15:50), “ili kwamba vitu visivyoweza kutetemeshwa vibakie” (Waebr. 12:27). Hii ndiyo maana ya Paulo katika 1Wakor. 15:25-26 anaposema kwamba Kristo anapaswa kutawala mpaka adui Zake watakapowekwa chini ya miguu yake, adui wa mwisho akiwa kifo. Awamu ya mwisho ya ufufuo itakapokwisha na enzi ya milele kuanza, kifo hakitakuwa tena suala la kuhangaika nalo, na haitawezekana tena kufa – hakutakuwa tena na kifo kwa wanadamu. Ikifika hapo, wote watakuwa wamepokea ufufuo wao, wengine kwenye uzima wa milele, yaani waumini, na wengine kwenye hatia/hukumu ya milele, yaani wasioamini (Dan. 12:2; Matt. 25:46; Yoh. 5:28-29; Ufu. 20:11-14).

Kama mjadala hapo juu unavyoonyesha, awamu 3 za ufufuo anazozielezea Paulo zinaoana kwa utimilifu kabisa na aya nyingine za maandiko zinazohusiana na ufufuo. Dhana ya awamu nyingine ya ufufuo (ambayo unyakuo-wa-kabla-ya-Dhiki-Kuu utailazimisha iwepo), haionekani mahala popote katika maandiko.

4. Aya nyingine za ujio wa pili: Ni vigumu pia kuhakiki kutokana na maandiko mengine yanayozungumzia Ujio wa Pili wa Bwana wetu, mtazamo/msimamo huu wa unyakuo wa waumini wa kabla-ya-mileniamu, kabla-ya-Dhiki-Kuu (pre-tribulation, pre-millenial rapture doctrine). Aya hizi nyingine zote za ujio wa pili wa Bwana wetu zinatazamia ujio wa mwisho (yaani wa pili) kama lengo kuu la tumaini letu, na siyo tukio linalotangulia tukio hili kwa miaka 7.

a. 1Wathess. 1:3-12: Katika aya hizi ambamo ni sehemu ambayo Paulo amejadili kwa kirefu sana ule ujio wa pili kuliko sehemu nyingine yoyote, waumini hawa wa Thessalonike wangekuwa na wakati mgumu sana kutokana na maelezo ya matukio ambayo yangetokea punde, ikiwa tutachukulia kwamba 1Wathess. 4:14-18 inafundisha unyakuo-wa-kabla-ya-Dhiki-Kuu. Kwani taswira inayojitokeza katika muktadha wa 2Wathess. 1:3-12 ni ya waumini waliopata shida kwa muda mrefu na mwishowe wakipata ahueni “katika ufunuo wa Bwana Yesu Kristo” (1Wathess. 1:7, aya ambayo ni wazi kabisa inazungumzia Ujio wa Pili wa Bwana wetu; cf. Ufu. 1:1-3), wakati wale watesi wao wakipokea hukumu ya haki kutoka mikononi mwa Mfalme anayerejea “katika ile siku anayokuja ili kutukuzwa katikati ya watakatifu Wake na kustaajabiwa katika wote waliosadiki” (aya ya 10). Kama Paulo angefundisha katika 1Wathess. 4:14-18 kwamba wangenyakuliwa miaka 7 kabla ya hapa (wakati huu) na kwamba wangekuwa wanangojea Dhiki Kuu iishe wakiwa salama mbinguni, basi tunaweza kufikiria (na kuuona) mshangao wao mkubwa na kuchanganyikiwa wanapoona katika aya hii kwamba badala yake wangekuwa bado wanahitaji kupata ahueni kutoka mateso katika siku ya kurejea Kristo kwa utukufu (aya ya 7).

b. 1Wathess. 5:1-11: Katika sura inayofundisha yale yanayodaiwa kuwa ni mafundisho ya Paulo ya unyakuo-kabla-ya-Dhiki-Kuu, waumini wa Thessalonike wanaambiwa wasiwe na wasi wasi juu ya tarehe ya matukio yajayo (aya ya kwanza), kwani “siku ya Bwana” (yaani Ujio wa Pili) utakuja “kama mwivi usiku” (yaani bila ilani). Kwa wasioamini, hii inamaanisha “kuangamizwa ghafla” na “bila nafasi ya kuponyoka” (aya ya 3). Waumini wanatakiwa “wakeshe, wawe macho na wenye kiasi” (aya ya 6), wakijivika “kifuani deraya na imani na upendo” na “helmet – chapeo – ya tumaini la wokovu” (aya ya 8). Na, ni kwa ajili ya “kupata wokovu huu” (aya ya 9), ndiyo tumechaguliwa. Kama tulivyoona katika 2Wathess. 1:3-12, kwa wazi kabisa huu ni muktadha wa hukumu ya wasioamini ukitofautishwa na wokovu wa waumini pale anaporudi Bwana wetu. Maana ya aya hii iko wazi: kama wangeishi mpaka kufikia kipindi hiki, Wathessalonike wale wangelazimika kuitunza imani yao na kuwa macho katika siku zote za Dhiki Kuu mpaka itakapofika ile “siku ya Bwana”, bila kupata “ahueni” kupitia unyakuo kabla ya Dhiki Kuu.

c. Fundisho-fumbo la mabikira (Matt. 25:1-13), na lile la talanta (Matt.25:14-30), yote mawili yanafundishwa na Bwana wetu katika muktadha wa kurudi Kwake (mara baada ya sura ya 25), yanazungumzia ukaribu wa kurudi Kristo kwa mtazamo wa Ujio wa Pili, na si kwa mtazamo wa unyakuo wa kabla ya Dhiki Kuu. Tunapaswa kuwa waangalifu katika matumizi ya rasilimali (za kimwili na za kiroho) ambazo Mungu ametupatia, kama wale watumishi waaminifu, kwani ujio wa Bwana wetu u karibu na waweza kutukia bila ilani yoyote. Baada ya kurudi Kwake, atagawa thawabu zake kwa waaminifu, na adhabu kwa wasiokuwa waaminifu (katika Ujio wa Pili; cf. Ufu. 11:18; tizama somo #18 kwa fununu zaidi). Na kama wale bikira wenye busara, tunapaswa kuhakikisha mwanga wa taa yetu ya imani unaendelea kuwaka vizuri mpaka pale Bwana wetu atakaporudi. Kwani pale atakaporudi, wale ambao waliacha taa ya imani yao “izimike”, hawataingia katika Ufalme pamoja na Bwana Harusi (cf. Ufu. 19:5-10), bali wataachwa nje. Mafundisho-fumbo yote mawili yanaweka wazi kabisa kwamba Ujio wa Pili, ambao ni ujio wa mwisho wa Kristo mara baada ya Dhiki Kuu, ni tukio la kutazamiwa, kutumainiwa na kukaliwa macho (kungojewa kwa kukesha), na si unyakuo unaotangulia Dhiki Kuu na ujio wa mwisho wa utukufu wa Bwana wetu.

d. Aya nyingine zinazoweka tumaini letu katika Ujio wa Pili:

i. Tito 2:13: … tunapongojea tumaini lililotukuka, yaani ufunuo adhimu (majestic) na uliotukuka wa Mungu na Mwokozi wetu, Yesu Kristo …

[NB: Ufunuo ni tafsiri ya neno la Kiyunani epiphaneia, neno ambalo (pamoja na kivumishi/ki-sifa {adjective} chake) katika Agano Jipya linamaanisha Ujio wa Pili wa Kristo likisisitizia mng’ao wa mwonekano Wake: Matendo 2:20; 2Wathess. 2:8; 1Tim. 6:14; 2Tim. 4:1&8; isipokuwa katika 2Tim. 1:10 ambapo unazungumziwa ujio Wake wa kwanza]

ii. 2Pet. 1:19-20 SUV: 1.19  Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka [siku] kutakapopambazuka, na Nyota ya Asubuhi kutokea (kurudi kwa Bwana katika utukufu).
1.20  Mkijua [mkitafakari neno hili mioyoni mwenu] ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani [kwa fikra zake] tu.

iii. 1Wakor. 1:7: Hata hamkupungukiwa na karama zozote za kiroho, mkitazamia sana ufunuo wa Bwana Yesu Kristo.

[NB: Ufunuo ni neno la Kiyunani apokalypsis ambalo (pamoja na kivumishi/ki-sifa chake) katika Agano Jipya mara nyingi linamaanisha Ujio wa Pili wa Kristo, likisisitizia ufunuo wa utukufu Wake: Lk. 17:30; War. 2:5; 8:18; 8:19; 2Wathess. 1:7; 1Pet. 1:5; 1:7; 1:13; 5:1; Ufu. 1:1]

iv. Lk. 21:25-28: Basi mambo hayo yatakapoanza kutokea (matukio ya aya ya 25-27) simameni na mnyanyue vichwa vyenu, kwani ukombozi wenu umekaribia.

[NB: ukombozi (kwa Kiingereza redemtion) ni neno la Kiyunani apolutrosis ambalo, pamoja na kivumishi/ki-sifa {adjective} chake linamaanisha kuokolewa kutoka utumwa[ni]. Katika Agano Jipya, maneno haya kwa kawaida humaanisha kuokolewa kwetu kutoka dhambini kwa kazi inayookoa ya Kristo, lakini wakati mwingine humaanisha ule wokovu wa mwishoni wa miili yetu kupitia ufufuo (War. 8:23; Waefe. 1:14). Dondoo muhimu ni kwamba wokovu, siku zote ni kutoka hali fulani kwenda hali ingine. Hapa, wokovu ni kutoka dhiki, kwa maana ya hali ya kutisha ya Dhiki Kuu (cf. Waefe. 4:30 – wokovu kupitia ufufuo mwishoni mwa Dhiki Kuu; na Waebr. 11:35 – wokovu wa milele ambao ni bora zaidi kuliko ule wa hapa duniani)]

v. Wafi. 1:6: Nami nina imani katika suala hili, ya kwamba Yeye aliyeianza kazi hii njema mioyoni mwenu ataendelea kuiboresha hata siku ya Kristo Yesu.

[NB: “Siku ya Kristo” ni kisawe (synonym – neno lenye maana karibu sana au ile ile) cha “Siku ya Bwana [Kristo]”, yote ikimaanisha Ujio wa Pili. Tizama 3.b. hapo juu, na 1Wakor. 1:8; 5:5; 2Wakor. 1:14; Wafi. 1:10; 2:16]

Pamoja na ushahidi wa aya mbalimbali hapo juu, tunaweza kusema kwamba mwelekeo/hali ya ujio ambao uko karibu sana unaoonekana katika unabii wa Agano Jipya ni vigumu sana kuupuuza. Ebu tuone mifano miwili tu ambapo Bwana wetu anazungumzia Ujio Wake wa Pili; anasema katika Mathayo 16:27 kwamba “Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake watakatifu, na ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake”, na katika Ufunuo 2:25 kwamba “mlichofanikiwa kukipata mkishike imara, hata nitakapokuja”. Kwa kutumia mtazamo/mwanga wa mjadala wa hapo juu, itakuwa vyema kuyachukulia maneno haya ya Kristo – neno moja kutoka katika Injili na lingine kutoka katika kitabu cha mwisho cha Agano Jipya – kuwa yanatuhusu sisi, wanafunzi Wake, hivyo kwamba ile siku ya ufunuo Wake ni wazi kabisa kwamba ni siku ya Ujio wake wa Pili.

Suala hili lina umuhimu mkubwa. Hata katika nyakati za shinikizo hafifu la kiroho, kuwa macho kwa sababu ya ufahamu wa matukio haya ya siku za mwisho kunasaidia kuendeleza mtazamo zaidi wa kimbinguni na pungufu wa kidunia. Kwani mtazamo wetu ni kwamba sisi tumo katika dunia, lakini sisi si wa dunia hii (Yoh. 17:11-16). Kuamini kanuni au fundisho la Unyakuo wa Muumini Kabla ya Dhiki Kuu (Tribulational Security) kunatoa mwanya wa kutenganisha (badala ya kuunganisha) dondoo na mafundisho yote ya siku za mwisho Kibiblia (eschatology),(1) kunaweka gizani sehemu muhimu sana na yenye thamani kuu ya Biblia, na kuuondoa mtazamo wetu kutoka mbinguni na kuuleta duniani (1Wakor. 7:29-31). Badala yake, tunapaswa kutazamia ile siku ya Bwana, tukifanya juhudi kwa ajili ya thawabu ya mbinguni na si vitu vya kupita vya dunia hii:

6.19 Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba;
6.20 bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi;
6.21 kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.
Matt. 6:19-21

Kwa kuwa mafundisho ya Unyakuo [wa Muumini Kabla ya Dhiki Kuu] yana athari ya kupeleka mwelekeo wa mtazamo wa Mkristo nje ya mafundisho ya siku za mwisho (kwani siku za mwisho zitaonekana kutokuwa na umuhimu kwa Mkristo huyu), mtazamo huu utaelekezwa, si kwenye masuala ya [ki]mbinguni, bali kwenye kupanda na kushuka kwa masuala ya kidunia (cf. Wakol. 3:1-4). Tunapozidi kufikiria kuwa unabii wa maandiko ya Biblia hautatuhusu, ndipo tunazidi kupoteza mtazamo wetu wa uraia wetu wa mbinguni (cf. Wafi. 3:20), na kufikiria mambo ya duniani badala yake (Yoh. 2:15-17). Mtazamo wa namna hii utakuwa na athari hasi katika maisha yetu ya Kikristo.

Athari nyingine hasi inayotokana na kuamini kanuni ya Unyakuo ni kwamba inapelekea kwa Wakristo kulegeza kamba kuhusiana na dhiki binafsi (tizama masomo #25 na #26). Kujiridhisha pamoja na kulegeza kamba/mkanda kunamfanya muumini awe rahisi kushindwa kustahamili punde majaribu makali yanapokuja. Sababu yake ni rahisi sana: ukiamini kwamba wewe mwenyewe hautapitia ile Dhiki Kuu, kipindi cha majaribu na mateso makali ambacho maandiko yamekizungumzia sana, basi pia utapuuzia kujiimarisha kiroho kwa ajili ya mitihani binafsi ambayo humtokea kila Mkristo kwa nyakati mbalimbali za maisha yake. Kwa uhakika tutakabiliwa na mateso mengi binafsi katika safari yetu ya Ukristo, na ni lazima tuyakabili kwa namna ile ile ambayo waumini wa siku za usoni watayakabili mateso ya wakati wa Dhiki Kuu yenyewe (Matendo 14:22b). Katika siku za mwanzoni za Kanisa, au katika kipindi cha Reformation (miaka ya akina Luther, Calvin na wengineo), ambapo waumini halisi wa Kristo waliuawa kwa wingi, mtazamo huu wa kulegeza kamba ulikuwa vigumu kuwa nao. Lakini katika dunia tunamoishi leo katika nchi zenye demokrasia ya ki-liberali, mateso ya namna hii ni nadra sana. Lakini, kama tulivyojifunza hapo nyuma, mateso binafsi ni kitu kinachomkabili kila Mkristo, kila wakati. Kwa neema ya Mungu, tunajua kwamba tunaweza kukabili na kuvumilia mitihani yoyote Anayoruhusu ije kwetu (1Wakor. 10:13). Lakini hatari inakuja pale inapokuwa hatuko imara kwa sababu hatujajitayarisha [kiroho] na hivyo tunashindwa kuitumia neema hiyo ya Mungu pale mitihani inapokuja, iwe ya binafsi au ya siku za mwishoni za Dhiki Kuu. Inapofikia hapo, misingi ya imani ya Mkristo husika inaweza kutingishwa kweli kweli. Kwa kuutoa mtazamo wetu kutoka mbinguni na kuupeleka hapa duniani, na hivyo kutufanya tuwe hatuko tayari kukabiliana na mitihani mikali, fundisho la uwongo la ‘Ulinzi/Usalama katika Dhiki na Dhiki Kuu’ au ‘Unyakuo kabla ya Dhiki Kuu’ linadhoofisha imani na hivyo kuhatarisha uzima wetu wa milele.

Fundisho hili la ‘Ulinzi/Usalama katika Dhiki na Dhiki Kuu’ lina uwezekano wa kuleta madhara hapo baadaye, haswa kwa kile kizazi cha Wakristo ambao ghafla watajikuta wamo katikati ya Dhiki Kuu ambayo hawakutegemea kukabiliana nayo. Kwa mara nyingine tena, kama ilivyokuwa kwa mafundisho yote mengine ya uwongo, kanuni hii ya uwongo nayo inafuata taswira ile ile ya udanganyifu wa mwanzo wa Shetani:

1) Ina kiini (kiasi fulani) cha ukweli: 1Wathess. sura ya 4 kwa hakika inafundisha kwamba sisi waumini tutakaokuwa hai wakati anaporudi Bwana wetu tutakusanywa na malaika na kupaa na tutakuwa na Bwana milele. Na ukitizama juu juu tu utaona kama vile muda halisi wa tukio hili hauna umuhimu sana au una umuhimu kidogo tu. Lakini kama tulivyoona pale Ibilisi alivyopindisha ukweli kidogo tu kwa ujanja wake, tofauti hizi “ndogo ndogo” zina matokeo mazito sana. Mungu anawalinda na kuwatunza wale wanaomtumaini Yeye na Mwanaye. Hata hivyo, wakati mwingine Yeye hutuokoa kwa kutulinda katika safari yetu ya imani wakati tukipita katikati ya mateso, badala ya kutuokoa kwa kutuepusha na mateso hayo. Hili ni somo muhimu, tofauti muhimu ambayo waumini wote tunapaswa kuwa macho nayo na pia kuwa makini nayo sana, isijetokea “siku ile ikafika ghafla kama mwivi” (1Wathess. 5:4).

2) Ina mvuto mkubwa: Mvuto wa kuamini ‘Unyakuo kabla ya Dhiki Kuu’ uko, na unapaswa kuwa, wazi. Haswa kwa waumini wenye shauku, au vinginevyo wamejifunza juu ya matukio ya siku za mwisho (eschatology) na wameona tishio la siku hizo za mwisho za Dhiki Kuu. Inatia faraja ukiweza kujipa moyo kuwa hautalazimika kuyakabili matukio hayo ya kutisha, kwamba utaepuka tishio hilo kwa kukusanywa na kuwa na Mungu, bila tanuru la mateso ambalo waumini wa wakati huo watalazimika kupitia. Tatizo kubwa la mtazamo huu kama tulivyoona, ni kwamba mtazamo potofu unampa muumini hisia ya usalama na kumpeleka katika shimo la kuipenda dunia na kuridhika, ikimwacha akiwa hana utayari si tu wa kuikabili Dhiki Kuu, tukio ambalo linaweza kumkuta angali hai (kwani li karibu sana!), lakini labda hata katika mateso binafsi ambayo Mkristo yeyote ni lazima ayapitie (1Pet. 1:7; 4:12; 5:9).

3) Ina mwonekano (taswira) ya utakatifu:

a) sura ya kirafiki: Sifa za Ukristo za watu na makundi mengi yanayofundisha Unyakuo-kabla-ya-Dhiki-Kuu ni za kiwango cha juu sana. Hii ni sababu mojawapo ya kwa nini kanuni hii, japokuwa haina miaka mingi tangu ianzishwe – kama tulivyoona - imefikia mahala pa kupewa hadhi kubwa namna hii. Fundisho hili la Unyakuo linatokana na shauku halali kabisa katika eneo la maandiko ambalo kwa kiasi kikubwa sana halikushughulikiwa au lilipuuzwa wakati ule wa Mageuzi (Reformation) ya akina Luther, Calvin na wengineo (kwani Wakristo wa wakati huo walikuwa na mateso mengi sana binafsi yaliyowakabili). Hata hivyo, watu na makundi ya waumini ambao wana desturi na falsafa ya kuutafuta ukweli wa maandiko licha ya msongo wa utamaduni na desturi iliyozoeleka wanapaswa kujiweka mbali na tabia ya kutopima kanuni zote kwa kipimo cha maandiko.

b) mazoea na Mungu: Kuna ubaya gani ikiwa tutatazamia ujio wa pili wa Bwana wetu kukusanya watu Wake ili wawe pamoja Naye? Sisi sote tunatizamia kutimia kwa tumaini hili takatifu la kuwa na Kristo na Mungu Baba milele, lakini imani kuwa tukio hili litakuwa kabla na siyo baada ya kipindi cha Dhiki Kuu itakayoikumba dunia yote inapunguza thamani ya tumaini hili. Unyakuo unakuwa sasa kisingizio cha kutojisumbua kabisa na matukio ya unabii yaliyotabiriwa, badala ya kuwa matazamio na mategemeo ya ukombozi mkuu wa Mungu kwa wale wote “watakaovumilia mpaka mwisho” (Matt. 24:13). Kuamini kwamba utaokolewa kabla ya wakati wake kunavuruga mtazamo wetu. Badala ya kujipa mazoezi, kujiimarisha kwa ajili ya changamoto nyingi za maisha zitakazoikabili imani yetu, kanuni ya uwongo ya Unyakuo-kabla-ya-Dhiki-na-Dhiki-Kuu inatushawishi tutafute-tafute njia rahisi za kuepuka majaribu na mitihani na hivyo tunakuwa hatuko tayari kukabiliana na uhalisia wa mitihani.

c) kuhalalisha shauku/tamaa za siri za ndani ya moyo: Ukweli ni kwamba hakuna atakayechagua kwa makusudi, maumivu au mateso au majaribu makali. Tunaelewa kutokana na maandiko kwamba mitihani ni zoezi zuri na linalofaa kwa ajili yetu, ni mchakato unaoboresha na kuimarisha imani yetu (kama tulivyoona katika mfululizo wote wa masomo haya), lakini hatuyatafuti kwa makusudi mateso haya. Ni kiasi gani, basi, tungependa kuepuka kile kipindi chote cha Dhiki kinachokuja! Ndani kabisa ya mioyo yetu, hatutaki kupoteza vyote tulivyo navyo – mali zetu, uhuru wetu, hata uhai wetu. Hatutaki hata kuwazia matokeo ya matukio ya kutisha yanayosimuliwa katika Danieli, Ufunuo na sehemu nyingine za maandiko, achilia mbali kuteseka kiuhalisia katika matukio hayo yanayokuja. Ukweli wa mambo ni kwamba Ufalme wa mbinguni na ufalme [wa sasa] wa Shetani wa dunia hii wamo katika vita. Kwa kumchagua Kristo, tumejiweka upande mmojawapo, na tangu wakati wa kifo cha Bwana wetu msalabani kwa ajili yetu, wengi kati ya Wakristo wenzetu wamelazimika kuweka msimamo ambao maana na matokeo yake ni kupoteza maisha kwa ajili ya Jina Lake takatifu. Sisi wenyewe binafsi yawezekana tusilazimike kufanya kafara hii ya mwisho, lakini tumeitwa tuwe tayari kufanya hivyo:

16.24 Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.
16.25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona [ataitunza].
16.26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?
16.27 Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
Matt. 16:24-27 SUV

Katika neema Yake kuu, isiyo na mfano, Mungu ametupatia Mwana wake – afe ili sisi tupate kuishi. Je, hawezi kuwa mwaminifu kutuvusha salama katika tukio lolote ambalo mapenzi Yake yamepanga tupitie? Majaribu yoyote, tanuu lolote [la moto wa] mitihani tulilopangiwa [Naye] kulivumilia, ikiwa tu tutatembea Naye, atatuongoza kwa upole akitushika mkono mpaka atakapotufikisha nyumbani ili tuwe Naye pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo milele (War. 8:31-39).

Maelezo Mafupi Kuhusu Fundisho la Unyakuo-Baada-ya-Dhiki-Kuu: Kama tulivyodhihirisha hapo juu, Unyakuo unafanyika baada ya kipindi cha mateso cha Dhiki Kuu kinachotabiriwa katika maandiko, na si kabla, yaani Unyakuo utatokea katika Ujio wa Pili. Bwana wetu alisema wazi kabisa kuhusu “kukusanywa kwetu pamoja” baada ya matukio ya siku hizo, Atakaporudi kuwaokoa walio Wake kutoka ule moto wa mitihani na majaribu:

24.31 Naye atawatuma malaika zake pamoja na [mlio wa] sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.
Matt. 24:31 SUV

Neno “unyakuo” lina kusudi la kuonyesha kuchukuliwa kwa sisi Wakristo ghafla kutoka hapa duniani na kuenda kuwa na Bwana (cf. Matt. 24:36-44; Luka 17:34-37). Wazo la neno hili linatokana na neno la Kiyunani harpazo, ambalo linatafsiriwa kama “kunyakuliwa na kwenda juu” katika nukuu ya 1Wathess. 4:15-18 (hapo juu), na, ni aya hii ndiyo inayohusika na ukweli kwamba tunauita ufufuo wa waumini walio hai katika Ujio wa Pili, “Unyakuo” au kwa kimombo, “rapture”. Istilahi au jina hili lilianza katika tafsiri ya Kilatini inayoitwa “Latin Vulgate” ambamo neno harpazo au “Unyakuo” linatafsiriwa na neno la Kilatini rapio. Neno rapio likichukuliwa katika wakati uliopita unaoendelea – yaani past participle – linakuwa rapt, likiunganishwa na kiambishi tamati (suffix) tura, tunapata neno la Kilatini raptura – ambalo ndilo neno la Kiingereza “rapture” au kwa Kiswahili “Unyakuo” - maana yake ikiwa ni “hali ya kunyakuliwa [ghafla] kwenda juu”. Kuna matukio mengine mawili katika Agano Jipya ambapo waumini “wananyakuliwa” na Mungu, ingawa hayahusishi ufufuo hai wa siku za mwisho. Tukio la kwanza la Unyakuo linasimuliwa katika Matendo 8:39, ambapo Filipo “ananyakuliwa” (neno linalotumika ni harpazo katika Kiyunani) na Roho Mtakatifu na kupelekwa Azoto (Ashdod), ambapo ni umbali wa safari ya siku nzima kutoka pale alipokuwa akiongea na yule towashi wa Kiethiopia. Filipo alisafirishwa kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine, lakini yeye mwenyewe anabaki katika mwili wake ule ule. Vilevile maelezo ya Paulo ya “mtu mmoja … katika mwili au nje ya mwili, sijui … alinyakuliwa mpaka mbingu ya tatu” yanaonyesha mtu aliyekuwa katika hali [ya muda] ya kiroho, lakini alibaki katika jamii yake ya Wakristo na kusimulia aliyoyasikia huko mbingu ya tatu (2Wakor. 12:2-4). Hivyo ni katika aya ya 1Wathess. 4:15-18 ndipo neno harpazo (Kilatini raptura) linazungumzia “Unyakuo” wenyewe, yaani ufufuo wa Wakristo wakiwa hai katika Ujio wa Pili wa Bwana wetu Yesu Kristo.(2)

Aya Zinazofundisha Unyakuo-Baada-ya-Dhiki-Kuu: Kuna aya kadhaa muhimu katika Agano Jipya ambazo zinaweka na kuthibitisha “tumaini letu tukufu” la ufufuo katika Ujio wa Pili wa Bwana wetu:

1. 1Wakor. 15:51-52 SUV: 15.51  Angalieni, nawaambia ninyi siri [fumbo]; hatutalala sote (yaani baadhi yetu tutafufuliwa tukiwa hai atakaporudi Kristo), lakini sote tutabadilika,
15.52  kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho (itakayotangaza mwisho wa Dhiki Kuu, na Ujio wa Pili wa Bwana wetu); maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe (pasipo) na uharibifu, nasi [pia] (yaani waumini walio hai) tutabadilika [wakati huo (yaani katika Ujio wa Pili wa Bwana wetu).

[NB: Aya hii, kwa wazi kabisa inaunganisha Unyakuo na ufufuo katika Ujio wa Pili. Katika tukio hili la awamu ya pili ya ufufuo (ya kwanza ni ile ya Kristo – tizama pia hapo juu, na somo #20), yaani waumini “walio wa Kristo katika ujio Wake”, siyo tu kwamba waliokufa katika Kristo watafufuliwa, bali na walio hai katika Kristo “wanabadilika”, yaani wanafufuliwa wakiwa hai. Mabadiliko haya ni siri au fumbo, kwa sababu mpaka Paulo alipopokea ufunuo mahususi wa ukweli huu, haikuwa inajulikana bayana kwamba hata walio hai na ambao watakusanywa katika Ujio wa Pili wa Kristo pia watabadilishwa na kuingia katika uzima wao wa milele, wakipokea miili yao ya ufufuo kama wale waliokwisha lala (waliotangulia ‘kufa’) na kuwa pamoja na Bwana]

2. Wakol. 3:1-4 SUV: 3.1  Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo [kwa sababu ya nafasi mliyo nayo Kwake(3)], yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
3.2  Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.
3.3  Kwa maana mlikufa [kwayo yaliyo chini], na uhai wenu [halisi] umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.
3.4  Kristo atakapofunuliwa [katika Ujio wa Pili], aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu [wa ufufuo].(4)

3. 1Yoh. 3:2 SUV: 3.2  Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado [jinsi] tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa [revealed] [Kristo], tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.

4. Wafilipi 3:20-21 SUV: 3.20  Kwa maana sisi, [u]wenyeji [uraia] wetu uko mbinguni; kutoka huko tena [kwa shauku] tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;
3.21  atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.

5. Warumi 8:18-24 SUV: 8.18  Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu [katika Ujio wa Pili].
8.19  Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.
8.20  Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili [kwa sababu ya dhambi ya Adam]; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake Yeye aliyevitiisha [-lakini si bila] tumaini;
8.21  kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu (yaani ufufuo), hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu [siku ya Ujio wa Pili].
8.22  Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa.
8.23  Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu [ufufuo].
8.24  Kwa maana tuliokolewa kwa taraja [tumaini] hii; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho?

Hatari Ratika Siku za Usoni: Sasa tuko tayari kufanya muhtasari wa hatari za zile kanuni tatu za uwongo zinazotishia imani ya Mkristo. “Siku za mwisho” (2Tim. 3:1; 2Pet. 3:3), kile kipindi kilichotabiriwa kinachoishia kwenye Ujio wa Pili wa Bwana wetu (yaani Dhiki Kuu ikimalizwa na Ujio wa Pili), kitatuletea changamoto kali na za kipekee kwa imani yetu. Kipindi cha Dhiki kimekuwa kikielezewa na maandiko kuwa ki karibu tangu siku za mwanzoni za Kanisa, lakini tusifikiri kwamba hakitatugusa, na tutahadhari tusijekuwa kama wale wadhihaki/wasutaji wa 2Petro 3:4 wanaouliza kwa kejeli, “Iko wapi ahadi ile ya kurudi Kwake? Kwa maana tangu hapo siku za babu zetu ambao wamelala siku nyingi, ulimwengu umekuwa ukiendelea kwa namna ile ile – tangu mwanzo wa uumbaji”. Jibu la Petro kwao ni wazi kabisa, akiwaeleza kwamba ulimwengu huu ambao wanatarajia utadumu milele, utachomwa moto na kuteketea, na mahala pake itaumbwa Dunia Mpya na Mbingu Mpya (2Pet. 3:5-13). Yaweza kuwa kizazi chetu hiki sicho kilichopangiwa kupitia kipindi cha Dhiki Kuu, lakini vyovyote itakavyokuwa, si busara kudhani hivyo, na mwisho wake si vyema kwa imani yetu, kama tulivyoona hapo juu. Kutegemea mojawapo au zote katika hizo kanuni na mafundisho haya matatu ya kutegemea dhehebu/taasisi (Institutional Security), kutegemea kutopoteza wokovu (Positional Security/OSAS) na kutegemea Unyakuo na kuepushwa na Dhiki na Dhiki Kuu (Tribulational Security), ni hatari kwa sababu imani yetu kwa Kristo ndicho kitu pekee kilicho muhimu kuliko vyote. Hatari hii ni halisi, kwa sasa, lakini pia kuamini mafundisho haya ya uwongo ni hatari kubwa katika siku za usoni ambao ndio wakati wa Dhiki Kuu yenyewe.

Ulinzi/Usalama Ndani ya Dhehebu/Taasisi (Institutional Security);

Hatari ya Sasa: Kutegemea kanisa (kundi) fulani au mtu fulani kwa wokovu wako kuna hatari ya kupotea kutoka wokovu wa kweli ambao hupatikana kupitia imani katika Kristo (Waebr. 2:1-4).

Hatari ya Siku za Usoni: Wale wenye mtazamo huu watakuwa hatarini kuvutwa na kushawishiwa na ile DINI KUU itakayoenea dunia nzima katika kipindi cha miaka saba ya Dhiki na Dhiki Kuu, na wanaweza kujikuta wakimwabudu yule mnyama badala ya Mwanakondoo wa Mungu (Matt. 24:24; 2Wathess. 2:1-12; Ufu. 13:1-18).(5)

Ufumbuzi wa Tatizo Hili: Ikiwa, badala ya uaminifu kwa dhehebu au mtu fulani katika taasisi, tunategemea uanachama wetu katika Mwili wa Kristo kupitia imani ya kwelikweli kwa ajili ya wokovu wetu, basi imani hii haitaharibika, hata kama taasisi yetu au viongozi wetu wanatetereka.

Ulinzi/Usalama wa Milele au OSAS (Positional Security):

Hatari ya Sasa: Imani katika wokovu ambao ni salama kabisa bila kujali mwenendo wetu inadhoofisha azimio letu la kupambana na dhambi na yaweza kupelekea kwenye kuifanya mioyo yetu kuwa migumu, uasi na upotevu wa uzima wetu wa milele (Wagal. 6:7-8; Yak. 1:14-16).

Hatari Katika Siku za Usoni: Hatari hii itaongezeka sana pale Uasi Mkuu katika kipindi cha Dhiki Kuu utakapoanza, na mashinikizo makali ya wakati huo yatasababisha watu wengi kuanguka kutoka katika imani (Matt. 24:9-13; 2Wathess. 2:3ff; tizama somo #26).

Ufumbuzi wa Tatizo Hili: Kama tunaendelea katika kukua kiroho, imani yetu itaongezeka sambamba na hakutakuwa na haja ya kuogopa kuangukia katika mtego huu (1Tim. 4:16; Yoak. 1:21; tizama mjadala hapa chini).

Ulinzi/Usalama Katika Dhiki na Dhiki Kuu (Tribulational Security):

Hatari ya Sasa: Kujiaminisha kwamba hautalazimika kuikabili Dhiki pamoja na Dhiki Kuu inayofuata (jumla miaka 7), kipindi ambacho ni tishio kubwa kwa imani yetu, kunasababisha athari hasi katika umakini wetu wa sasa. Kunatufanya tusiwe tayari kuyakabili mateso na dhiki za maisha yetu ya kawaida ya Kikristo, kunaondoa mtazamo wetu kutoka Ujio wa Pili wa Kristo na kuupeleka kwenye “mambo ya dunia hii” na hivyo kupunguza sehemu kubwa ya motisha yetu ya kuzaa matunda kwa ajili ya Bwana wetu wakati tukitizamia thawabu yetu ya siku ya ufufuo (Wakol. 3:1-4; Wafi. 3:19).

Hatari Katika Siku za Usoni: Kama tumepangiwa na Mungu kukabiliana na kipindi hiki cha mwisho cha utawala wa Shetani, kuwa macho itakuwa ni muhimu sana kama tunakusudia kupona kwa imani yetu. Kuamini kuwa hatutakabiliwa na hatari za aina mbalimbali kutatuweka wazi kwa mashambulio ya kipekee ya kipindi cha Dhiki na Dhiki Kuu (kwa mfano kushawishiwa na dini ya Kishetani itakayoenea dunia nzima). Mtazamo wa namna hiyo utawafanya wahusika wasiwe tayari kuukabili mgogoro huo na pia kutokuwa macho na hatari zake (Luka 12:37 & 40; 18:8).

Ufumbuzi wa Tatizo Hilo: Kungojea na kutazamia Ujio wa Pili wa Bwana wetu ambao u karibu, kunatusaidia kuweka tumaini letu kwake Yeye [pekee], kwenye uzima wetu wa milele, thawabu ya milele na ufufuo. Kutazamia kusimikwa kwa Ufalme Wake kama lengo letu litakalotimizwa mudu mfupi ujao (kama ambavyo tunaomba kila siku katika sala ya Bwana) kunaweka tumaini letu mbinguni, kama tegemeo ambalo linaweka fikra zetu na malengo yetu yakielekea katika Milele, likitulinda kutoka yote ambayo ni ya bandia hapa duniani (Waebr. 6:18-20).

“Mlango ni mwembamba, na njia imesonga, iendayo kwenye uzima, nao waionayo ni wachache” (Mathayo 7:14). Sisi Wakristo tunamjua Yeye tunayepaswa kumwamini: Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo – na hakuna mtu wala taasisi (Institutional Security) inayoweza kuwa mbadala wake. Tunajua ni nini tunachopaswa kukifanya katika maisha yetu: kumfuata Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo – na hakuna azimio la imani Kwake ambalo lilifanyika zamani na ambalo sasa limefifia na kukosa nguvu linaloweza kumfanya Yeye sasa awakubali wale ambao sasa wanamkataa (Ulinzi/Usalama wa milele). Mwisho, tunajua ni vipi tunapaswa kumfuata: tunabeba msalaba wetu – na hakuna ndoto za mchana kuhusu wokovu rahisi kutoka kwenye mitihani yetu (Ulinzi/Usalama Kutoka Dhiki na Dhiki Kuu) zitakazotuepusha na majaribu, ya binafsi na yale ya unabii (yaani ya siku za usoni), ambayo ni lazima yavumiliwe ili imani iweze kuimarika.

Katika maisha yetu ya Kikristo, kweli ndilo jambo muhimu. Bwana wetu ndiye “njia, na kweli na uzima” (Yoh. 14:6), na wale wote wanaotaka kumwabudu Yeye na Baba ni lazima wafanye hivyo katika “roho na kweli” (Yoh. 4:24). Chanzo chetu cha kweli ni Neno la Mungu (Yoh. 17:17a), na hivyo ni kwa kuitumia ile kweli ndipo tunatakaswa, tunawekwa mbali na ulimwengu ulioharibika wa Shetani (Yoh. 17:17b). Kwa kuwa mafundisho ya uwongo na kanuni za uwongo vinaharibu ukweli huu na hivyo kushambulia msingi wa imani yetu (Matt. 7:15; Yoh. 10:1-8; Matendo 20:29), tunapaswa kuheshimu maandiko kama vile Bwana wetu alivyodhihirisha (Matt. 5:17-20; Yoh. 10:34-35; Yoh. 17:12), na kuitumia fursa ya kusoma, kujifunza na kufundishwa Biblia kila siku. Kwa kufanya hivyo, na kuendelea katika kupevuka kiroho, tutajilinda siyo tu kutokana na mafundisho na waalimu wa uwongo yaliyozungumzwa katika somo hili, bali dhidi ya mafundisho ya kutunga ambayo tunaweza kukutana nayo hapo baadaye.

Muhtasari:

Fundisho la uwepo wa ulinzi/usalama ndani ya dhehebu au taasisi fulani pekee (Institutional Security) siyo sahihi: Kuupata wokovu wetu, ni lazima tuweke imani yetu katika Kristo kwa ajili ya wokovu huo, na siyo kuweka tumaini (la wokovu huo) katika taasisi fulani au ufuasi kwa mtu fulani anayegusa au kukonga nyoyo zetu kwa umahiri wa mazungumzo yake au mvuto wa wajihi wake au cheo chake cha kidini. Isije kuwa, kama ile mbegu iliyoanguka kando ya barabara, imani yetu ikakosa mizizi thabiti (Matt. 13:4, 19; Mrk. 4:4, 15; Lk. 8:5, 12):

4.12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo
Matendo 4:12 SUV

14.6 Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Yoh. 14:6 SUV

2. Fundisho la usalama wa milele wa imani yetu (OSAS, Positional Security) siyo sahihi: Kuutunza/kuulinda wokovu wetu, ni lazima tuendelee kumfuata Kristo kwa imani yetu, na si kudhani kwamba kwa kuwa tuliamini wakati fulani, basi mwenendo wetu si suala muhimu (kwani mwenendo wetu unaathiri imani yetu – kwa mema au kwa mabaya). Isije kuwa, kama ile mbegu iliyoanguka kwenye udongo wenye mwamba, tukatelekeza imani yetu kwa sababu ya vishawishi na mitihani (Matt. 13:5-6, 20:21; Mrk. 4:5-6, 16-17; Lk. 8:6, 13).
11.22  Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali.
11.23  Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa [upya]; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena.
War. 11:22-23 SUV

3. Fundisho la ulinzi/usalama katika dhiki katika maisha ya Mkristo na katika Dhiki Kuu (Tribulational Security) siyo sahihi: Ili tuwe salama katika wokovu wetu, ni lazima tuendelee kupevuka katika Kristo na kuwasaidia wengine wafanye vivyo hivyo kwa kutumia vipaji vyetu vya kiroho, na tusiwe na malengo ya kidunia bali tuwe na yale malengo ya thawabu ya milele. Isije kuwa, kama ile mbegu iliyoanguka katikati ya magugu na miiba, imani yetu ikapoteza mtazamo wake wa milele, na kusongwa na tamaa na dhiki za maisha, kiasi kwamba kukua kwetu na uzalishaji wetu unadumaa (Matt. 13:7, 22; Mrk. 4:7, 18-19; Lk. 8:7, 14;):

1.8  Maana mambo [maadili] hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
1.9  Maana yeye asiyekuwa na hayo [maadili ya aya za 5 - 7] ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani.
1.10  Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo [maadili, kukua kiroho na kuzaa matunda] hamtajikwaa kamwe.
1.11  Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo.
2Pet. 1:8-11 SUV

Hatari ya Kurudi Nyuma: Si mafundisho hayo 3 yaliyotajwa hapo juu pekee ndiyo yanayotishia imani ya Mkristo. Kwa hakika, mafundisho yote yanayompa muumini hisia bandia ya usalama/ulinzi wakati mwisho wake yanamwacha na hisia za kungakanyikiwa, kusalitiwa na kutelekezwa, yanaweza kusimamisha makuzi ya kiroho, na hata kurudisha nyuma kasi na maendeleo [chanya] aliyokuwa nayo Mkristo. Neno ambalo mara nyingi hutumika kuelezea kugeuka kwa namna hii kwa uelekeo wa kiroho ni “kukengeuka” au kwa kimombo, “backsliding”, na mchakato wa kupotoka kiroho namna hii hutokea kwa urahisi sana na unahujumu uaminifu wa moyo mmoja kwa Kristo ambao tunauita imani kwa Kristo:

1) uzembe: Mungu anataka nini kutoka kwetu kama siyo kutenda kwa haki, kupenda huruma na kutembea kwa unyenyekevu mbele Yake (Mika 6:8)? Hatuwezi kutembea Naye bila kumsikiliza, kujifunza kutoka kwake na kumtafuta [wakati wote] kwa moyo mmoja, na hii haiwezekani bila kujizatiti kwa Neno Lake (Yoh. 4:24). Kuzembea katika makuzi yetu ya kiroho, kunaathiri vibaya kila kitu katika maisha yetu, kwani ni kupitia kweli ya Neno ndio tunabadilika, ndio tunatakasika (Yoh. 17:17-19). Kunapozidi kiasi, kutojali Neno la Mungu kunatengeneza utupu/shimo katika mioyo yetu ambapo [sasa] uwongo ndio unajaza utupu/shimo hilo (Waefe. 4:17-19).

2) urahisi wa kusikiliza uwongo: Kama tulivyoona hapo juu wakati tunajifunza juu ya uwongo mwerevu wa Ibilisi katika ile bustani, kila uwongo huanza kwa kuishambulia kweli. Muumini anayeshindwa kumfuata Bwana Yesu hawezi akabaki amesimama mahala pamoja. Katika maisha ya Kikristo, haiwezekani “kuchukua msimamo katikati ya maoni mawili tofauti yaliyo kulia na kushoto kwako” kwa muda mrefu (1Wafa. 18:21), kwani kutokuwa na upendo na njia ya Mungu kutatoa nafasi ya kufuata njia zingine. Kutelekeza jukumu letu la kuitafuta kweli ya Mungu ni hatua ya kwanza katika kubadilisha kweli ya Mungu iliyoko mioyoni mwetu na kuweka furushi la uwongo mahala pake (War. 1:25). Kutojali ukweli kunatuweka katika hatari ya kuvurugwa na uwongo.

3) urahisi wa kuingia katika dhambi: Dhambi ni hatari iliyoko siku zote, wakati wote – mpaka saa tutakapoondoka kutoka katika hii miili ya mauti. Mara tunapoanza kusogea mbali na ukweli wa Neno la Mungu kama kiwango cha kipimo cha mwenendo wetu na badala yake kuenenda kwa kutumia kanuni zisizo sahihi, ile ruwaza (pattern) ya kuporomoka katika dhambi inayoelezwa katika kitabu cha Yakobo inakuwa rahisi kwetu kuingia[mo] (Yak. 1:14-15). Nje ya Neno la Mungu, shauku na hamu za kidunia za aina mbalimbali mara nyingi zinakubalika na hata kuhalalishwa, hivyo kwamba mchakato wa shauku au hamu, kupelekea kwenye tendo la dhambi, na baada ya hapo kupelekea kwenye ku[li]rudia tena na tena bila kujizuia, huenda kwa kasi (1Pet. 2:11; Yak. 4:1b) [mfano mzuri wa mchakato huu ni 1Wakor. 5:1-2].

4) mioyo kuwa migumu:(6) Kuongezeka kwa dhambi katika maisha yetu, dhambi hiyo iwe ya mafichoni au iwe ya wazi kwa kadamnasi, ya kawaida katika jamii au inayopingwa vikali, kunaimarisha utengano wetu na Mungu. Tunapoanza kulegeza msimamo wetu kwa dhambi, roho zetu zinaingia sugu kuhusiana na mapenzi ya Mungu, Naye anaanza kufifia na kutoweka polepole kutoka katika fikra zetu (Yoh. 12:40; 2Wakor. 3:14). Inapofikia hapo, tunakuwa hatuna mvuto wa kuja Kwake tena, kwani matendo yetu ni maovu, na hatuna shauku ya Yeye kumulika mwanga Wake katika matendo hayo [maovu] (Yoh. 3:19-21; Waefe. 4:17-24; 5:8-14). Njia ya dhambi imetutenga Naye (Isa. 59:2). Hatua kali za kinidhamu kutoka kwa Mungu zinakuwa lazima zichukuliwe wakati huu ili kuupenya ukuta mnene ambao muumini huyu msaliti ameuweka kati yake na Mungu (1Wakor. 5:5; Ufu. 3:19-20).

5) kifo cha kiroho: Hatimaye, kama Yakobo anavyotusimulia/tufundisha, dhambi hii isiyodhibitiwa huzaa kifo, yaani kifo cha [ki]roho, ambayo ndiyo hali yetu wakati tunazaliwa, ndiyo hatma ya mchakato wa kukengeuka (kurudi nyuma). Kwani kuendelea kufuata njia ya dhambi, bila kitubio, bila kujirudi, kunataka wakati wote, kwa makusudi kabisa, tumkatae Bwana wetu Yesu Kristo, mpaka anafifia kutoka katika fikra zetu, na taratibu anapotea kutoka katika mioyo yetu na hatimaye tunampoteza, pale imani yetu inapokufa kabisa (Matt, 7:21-23). Hii ndiyo maana thawabu ya dhambi siku zote ni mauti (War. 6:23). Kufikia hapo, utengano na Mungu unakamilika, na huyu muumini wa kale wa Kristo amekuwa sasa adui wa msalaba Wake (Wafi. 3:18), na anarudia katika utumwa wa dhambi (Yoh. 8:34-35). Na hali yake ya mwisho ni mbaya kuliko ile ya mwanzo (2Pet. 2:20-23), kwani mwisho wake njia hii inaelekea kwenye kumkataa Kristo (1Yoh. 5:16-17; cf. Matt. 12:31; Waebr. 6:4-6).

Si jambo la kustaajabu, basi, kwamba maandiko yamesheheni aya zinazotupa tahadhari ya kuwa macho na kutathmini mwenendo wetu wa maisha kwa uangalifu. Tusizichukulie aya hizi kirahisi-rahisi tu, kwani zinahusisha imani yetu na uzima wetu wa milele.

1. Aya zinazodhihirisha kwamba wokovu wetu unategemea kuendelea kwa imani [yetu katika Kristo]:

Wakolosai 1:21-23 SUV:
1.21  Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa [na Mungu], tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa;
1.22  katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama [hatia];
1.23  mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake …

2Timoteo 2:11-13 SUV:
2.11  Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia;
2.12  Kama tukistahimili, tutamiliki [tutatawala] pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi;
2.13  Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.

1Wakorintho 15:2 SUV:
15.2  na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana [imara] maneno niliyowahubiri isipokuwa [vinginevyo] mliamini bure.

Waebrania 3:6 SUV:
3.6  ... ambaye nyumba yake [Kristo] ni sisi, (sisi ni wa familia ya Kristo) kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya taraja [tarajio] letu mpaka mwisho.

Waebrania 3:14 SUV:
3.14  Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu [wa imani] kwa nguvu mpaka mwisho;

2. Aya zinazotutahadharisha tulinde imani yetu:

2Wakor. 13:5:
Jipimeni wenyewe kama mmesimama katika imani; jithibitisheni wenyewe kama kweli mu wa Kristo. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu?(7) Kama hayumo, basi mmekataliwa.

1Wakor. 10:6-12 SUV:
10.6  Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani.
10.7  Wala msiwe waabudu [miungu]-sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.
10.8  Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu.
10.9  Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu (yaani kizazi cha Kutoka Misri), wakaharibiwa [wakauwawa] na nyoka.
10.10  Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa [wakauwawa] na mharabu [Destroying Angel].
10.11  Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani [tunaoishi enzi za mwisho].
10.12  Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke!

2Yohana 8-9 SUV:
1.8  Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatend[e]a [kazi ngumu kufanikisha], bali mpokee thawabu timilifu [kwayo].
1.9  Kila apitaye cheo [aondokaye katika msitari], wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana [hayuko na] Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.

Yoh. 15:5-6 SUV:
15.5 Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.
15.6 Mtu asipokaa ndani yangu, [ni kama tawi linalokatwa na kutupwa] nje na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.

3. Aya zinazofundisha kwamba mwenendo wa dhambi ni kinyume na imani:

Wagalatia 5:19-21 SUV:
5.19  Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu [mwenendo wa aibu], ufisadi,
5.20  ibada ya sanamu [madawa ya kulevya, kutegemea watu, malaika], uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
5.21  husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.

1Wakorintho 6:9-10
6.9  Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, malaya wa kiume [kwa wanaume wenzao], mashoga,
6.10  wala wevi, wala watamanio [wasioridhika na walicho nacho], wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi [matapeli]

Waefeso 5:3-7 SUV:
5.3  Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;
5.4  wala aibu [matusi] wala maneno [utani] ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali [ni muhimu] kushukuru.
5.5  Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, [kwani mwenye tamaa] ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.
5.6  Mtu asiwadanganye kwa maneno [matupu] yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi [na wasioamini].
5.7  Basi msishirikiane nao.

1Timoteo 6:9 SUV:
6.9  Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.

Kuutunza Uzima Wako wa Milele: Tukiwa waumini katika Kristo, tuna uzima wa milele. Kama yule mtu aliyegundua hazina iliyofichwa katika shamba na akauza vyote alivyokuwa navyo na kununua shamba hilo (Matt. 13:44), uzima wa milele ni furaha isiyo na mfano wa aina yake hapa duniani. Pia kama hazina iliyofichwa, uzima wetu wa milele haujapatikana. Uzima wetu wa milele umefichwa katika/pamoja na Kristo, tayari kufunuliwa wakati wa ufufuo (Wakol. 3:1-4). Wakati huo huo, tunao uzima huu wa milele, hapa na sasa hivi, na hakuna kilicho muhimu zaidi ya kuulinda, kwani ndicho kitu muhimu kuliko vyote. Ikiwa imani inaishi, uzima wetu wa milele unaendelea kuwepo, kwani imani yetu ndiyo mapigo ya moyo ya uzima wetu wa milele (Yoh. 5:24). Kwa kuilinda na kuiimarisha imani yetu, tunauweka salama uzima wetu wa milele (2Pet. 1:10). Hakuna taasisi – dhehebu, dini – inayotoa uzima huu. Azimio la imani la mara moja tu haliwezi kutuhakikishia uzima huu. Imani hii haiwezi kulindwa dhidi ya mashaka na mitihani tunayopaswa kuikabili, sasa na baadaye, kwa kukataa uwepo wa [ma]shinikizo ya maisha [ambayo ni lazima tuyakabili kama Wakristo]. Ulinzi/usalama wetu hauwezi kupatikana kwa kugeuka na kurudi Misri ya ulimwengu huu, bali katika kuendelea na safari yetu kuelekea kwenye nchi ya ahadi ya milele. Katika kumtafuta Mungu kupitia Neno Lake (1Pet. 2:2), na katika kumtumikia Mungu kwa kutumia vipawa alivyotupatia (1Tim. 3:13; 4:15-16), tutaendelea kupanda mlima wa njia hii ya kuelekea milele bila kujali gharama yake, tukijua kwamba mwisho wa njia hii kuna maajabu yote ya milele [yakitungojea], baraka na thawabu za ushindi, mbingu mpya, nchi mpya, Yerusalemu Mpya, ufufuo na uzima wa milele pamoja na Bwana wetu Yesu Kristo, milele.

Tukijenga maisha yetu juu ya Mwamba huu, Mwokozi wetu Yesu Kristo, msingi wetu utakuwa salama katika hali yoyote, mazingira yoyote. Kwani Yeye ndiye usalama wetu wa kweli, imara kuyakabili mateso yoyote tunayopangiwa kuyakabili. Kama tunaendelea kumwamini na kumtegemea Yeye, kama tunaendelea kuunyanyua msalaba wetu, kuubeba na kumfuata kila siku, hapo hatutakuwa na chochote cha kuogopa, na imani yetu itakuwa kama punje ya haradali, pale tutakapoona kwamba kilichoanza kama mche mdogo kimekua mbele ya macho yetu hadi kuwa mti mnene, mkubwa ambao hauwezi kutikiswa na mateso ya dhoruba za maisha, hata zikiwa kali namna gani.

Notes:

1. Neno “eschatology”, mambo/matukio ya siku za mwisho [mwisho wa dahari], linatokana na neno la Kiyunani eschaton, maana yake “jambo la mwisho”, hivyo kwamba somo la Kibiblia la Eschatology ni somo la matukio ya siku za usoni kutokana na unabii na kama yalivyofunuliwa katika Biblia.

2. Katika Ufunuo 12:5, neno harpazo, Unyakuo, linatumika katika istiari (allegory – taswira au hadithi inayomaanisha au inayowakilisha dhana maalum) ya Mwanamke na Joka Kuu kuelezea “kunyakuliwa na kupelekwa mbinguni” kwa Mwana wa Kiume wa Mwanamke. Matukio yanayomaanishwa/yanayosimuliwa katika muhtasari huu ni ufufuo, kupaa na kukaa katika mkono wa kuume [wa Baba] kwa Kristo.

3. i.e. kwa sababu sisi ni Wake, tunashiriki katika kila kitu Alicho nacho, na tumefufuliwa “kwa dhamana”, yaani kwa sababu Yeye amefufuliwa, nasi tunashiriki katika ufufuo huo. Ufufuo [wetu] haujatokea bado, lakini tuna ahadi yake ya uhakika na ya kweli. Hivyo Paulo anaelezea tukio hilo la baadaye kama tendo kamili, kwa sababu ni tendo la uhakika kutokana na ukweli kwamba Mungu ndiye Aliyeliahidi. Hivyo, ufufuo wetu umekwishawekwa kwenye akaunti yetu”, ijapokuwa tarehe halisi ya “kuutoa [kutoka] kwenye akaunti hiyo” bado haijafika. Linganisha na ‘utakaso wa nafsi yetu Kwake (somo #13).

4. Neno “mtafunuliwa” au kwa kimombo “revealed” ni neno la Kiyunani phaneroo, kutoka katika neno-asili phan-, (kama vile epiphaneia), maelezo yake yanapatikana katika 4.d (katika Note) chini ya Ulinzi na Usalama Katika Dhiki na Dhiki Kuu Ijayo, hapo juu (cf. 1Pet. 5:4). Katika Agano Jipya, maneno haya mara nyingi hutumika kumaanisha ufunuo wa Kristo katika Ujio Wake wa Pili. Pamoja na kuzungumzia mng’ao mkuu na usio na mfano na sifa za Mungu, “utukufu” ni neno ambalo mara nyingi hutumika kuzungumzia ufahari wa ufufuo wetu na uzima wa milele baada ya hapo: cf. War. 2:7; 8:17; 8:18; 1Wakor. 15:43; 2Wakor. 3:18; 4:17; Wakol. 1:27; 1Wathess. 2:12; Waebr. 2:10; 1Pet. 5:1; 5:10.

5. Kuhusu desturi za waalimu wa uwongo wa dini hii, tizama pia 1Tim. 4:1-5; 2Tim. 2:16-3:9; 2Pet. 2:1-3; Yuda 3:19.

6. Tizama mfululizo wa Mafundisho: Exodus 14: Hardening Pharaoh’s Heart, inayopatikana kutoka https://ichthys.com

7. Yoh. 14:23.

NB: Dhiki Kuu: The Great Tribulation
Dhiki Binafsi: Personal Tribulation
The Tribulation: Kipindi/wakati wa Dhiki na Dhiki Kuu

=0=

Translated from: Three False Doctrines that Threaten Faith: Peter’s Epistles #27

=0=

Basi, na tuonane katika somo #28 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amen!