Nyaraka za Petro #23: Kuona Kwa Macho ya Imani
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

1Petro 1:8-9:
[… hapo Bwana Yesu Kristo atakaporudi kwa utukufu.] Iapokuwa hamjamwona, mnampenda tu. Iapokuwa hamwezi kumwona kwa wakati huu, mna imani juu Yake. Kwa sababu hii mna furaha ambayo hamwezi hata kuielezea, ambayo inaonyesha ile milele ijayo yenye utukufu, pale mtakapokabidhiwa ule ushindi mkuu wa siku ya mwisho – wokovu wa maisha yenu – ambao ndiyo lengo na nia ya imani yenu hii.

Utangulizi: Somo letu la mwisho (liliopita) lilizungumzia uwepo usioepukika na ulazima wa majaribu katika maisha ya Mkristo, pamoja na kutiwa moyo na Petro – ili kwamba tuweze kuikabili mitihani migumu inayopima imani yetu (aya za 6-7). Katika aya 2 zinazofuata (nukuu hapo juu), tunaona kwamba Petro ameweka hoja zake mbili zenye ushawishi mkubwa kabisa hapo mwisho. Dondoo hizi mbili zilizo katika mjadala wa utangulizi wa mitihani na majaribu yanayomkabili Mkristo hapa duniani zinatosha kuondoa hisia zote za kujiona kama unaadhibiwa kwa makosa fulani na kujisikitikia ambazo Mkristo anaweza kuwa nazo ikiwa atazielewa aya hizi kwa usahihi, hata kama atahuzunishwa sana na mapigo yasiyokwisha katika maisha yake. Tunaweza kuufafanua ujumbe wa Petro wenye sehemu mbili kama ifuatavyo:

1. “haijalishi ni magumu gani utakayolazimika kuyakabili katika ulimwengu huu wa Shetani wenye uonevu, usio rafiki, kwani maisha yako ni kwa ajili ya Kristo tu”;

2. “kuendeleza imani yako chini ya shinikizo kali la majaribio si kitu rahisi, lakini ni jambo linalohusiana na wokovu wako.”

Kuitumia Vyema Fursa ya “Wakati Huu wa Sasa”: Maisha ni msisimko na shughuli nyingi. Maisha yana mambo mengi. Wakati mwingine unaona kama vile majukumu yetu na shughuli zinazochukua muda na nguvu zetu zinaongezeka kila siku na kuzidi uwezo wetu wa kuzikabili kwa ufanisi. Tunaona kama vile hakuna muda wala nguvu zilizobakia kutimiza shughuli za utumishi wetu! Hata hivyo, ni muhimu kujikumbusha kila wakati kwamba saa, siku, zinaenda, kwamba muda tuluopewa kufanikisha kile Mungu alichokusudia kwa maisha yetu unazidi kupungua siku hadi siku. Kama Paulo anavyosema, “sasa wokovu u karibu nasi kuliko wakati ule tulipoanza kuamini” (War. 13:11). Hulka ya kupungua ya ile rasilimali muhimu sana, yaani wakati, ni kitu ambacho tunapaswa kukitizama kwa makini sana. Hii ni kweli bila kujali kwamba tunajiona tunajua wazi wazi kwamba tunafahamu malengo ya maisha yetu ni nini kuhusiana na utumishi, au kama tunajiona tukipapasa kuelekea uelewa mzuri zaidi wa matakwa ya Mungu kwa maisha yetu. Ama kwa hakika, ni uchache huu wa muda tulio nao ambao unatulazimisha tuweke pembeni mambo yote yanayotukwaza na tuongeze juhudi katika kukua kiroho na uzalishaji wa matunda (kulingana na vipaji vyetu vya kiroho). Pia “wakati wa maisha yetu ambao umepita” ulitosha kwa sisi kumaliza tamaa zetu za kidunia (1Pet. 4:3-4). Huu ndio wakati wetu wa kuutumia ule muda wenye thamani kuu tulio baki nao, kwani kupevuka kiroho na utumishi kwa lengo la faida ya kupevuka kwa wengine ndiyo mambo muhimu na yenye maana ya kufuatilia katika maisha yetu, na ndiyo shughuli za Kikristo pekee zenye kutupatia thawabu katika ufufuo. Sisi ambao tumenunuliwa na Kristo ni lazima tujitahidi “kununua”, kwa upande wetu, muda tuliokabidhiwa, kwa ajili ya Kristo (Waefe. 5:16; cf. Wakol. 4:5). Kama vile ule wimbo maarufu wa kumtukuza Mungu unavyosema: “only one lyfe, twill soon past, only what’s done for Christ will last”, [Maana yake: “twaishi duniani mara moja tuu, na punde twaondoka, kitakachobaki ni kile tulichofanya kwa ajili ya Kristo”]. Tukiwa kama waumini, maisha yetu ni kwa ajili ya Kristo pekee. “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu; Kristo atakapofunuliwa, Yeye aliye uhai wenu, ndipo nanyi mtafunuliwa Naye katika utukufu” (Wakol. 3:3-4; cf. Wagal. 2:20).

Kumwona Kristo kwa Kutumia Macho ya Imani: Ukristo ni uhusiano – uhusiano wetu na Mungu ambao msingi wake ni imani ya kila nafsi ya mmoja wetu na Mwana wake, Bwana wetu Yesu Kristo. Katika aya za 8-9 sura ya 1, Petro anathibitisha upendo wetu kwa mwokozi wetu ambaye ametukomboa kutoka mauti na kutubariki na uzima wa milele kupitia sadaka yake: tunampenda, tunampenda kwa moyo wote (cf. Matt. 22:37; War. 5:8; 1Yoh. 4:19), ingawa hatujamwona uso kwa uso; na ndiyo maana tunatarajia kwa shauku kuungana Naye katika milele iliyotukuka, tukio tunalolitafuta kwa nguvu zote.

Mbinguni, uhusiano yetu na Mungu utakuwa mtimilifu, lakini hapa duniani mahusiano yote, hata yale ya kiroho, yanataka juhudi na kujitoa ili kuyajenga na kuyaimarisha. Hii ni wazi kuona katika kila uhusiano tulio nao na kila mtu yeyote: kuna juu na chini, milima na mabonde. Kitu kimoja tunachoweza kuwa na uhakika nacho, hata hivyo, ni kwamba bila shaka matatizo yoyote tuliyo nayo katika uhusiano wetu na Mungu kwa uhakika ni kosa letu, kwani katika hili tunahusiana na Yeye ambaye ni mkamilifu, mtimilifu, ambaye ametupatia mahitaji yetu kwa ukamilifu. Ili kuimarisha uhusiano wetu na Mungu, tunachohitaji kufanya ni kuacha kutilia shaka uwezo na utashi wa Yeye kutimiza jukumu la kutimiza upande wake, na badala yake tuelekeze juhudi zetu katika jinsi tunavyoweza kumwitikia. Tunahitaji kujifunza kufuata uongozi Wake, na kuacha kusisitiza kutengeneza njia yetu wenyewe. Hii inataka maono, kuona kisichoonekana, uwezo wa kuona ambacho hakionekani.

Lakini hili lawezekana vipi? Macho yetu hayana uwezo wa kumwona Mungu ili tuweze kuhusiana naye kama tunavyohusiana na mwanadamu. Hivyo inabidi tujifunze kuwona kwa macho ya mioyo yetu, kwa macho ya imani. Tukishajifunza hili, tutaweza kutembea kwa kujiamini katika njia isiyoonekana kama ambavyo Mungu ametuchagulia kila mmoja wetu.

Kuendeleza uwezo wa kiroho wa kuelekeza imani yetu kwa Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo ufunguo wa maendeleo endelevu katika njia ya uongofu (Mithali 12:28; 15:19 & 24; 16:9). Katika Zaburi 16:8, Daudi anasema “Nimemtanguliza Bwana siku zote mbele yangu kwa kuwa Yeye yuko kuume kwangu, sitatetereka. Sasa, Bwana hakumtokea Daudi, lakini Daudi alikuwa mtu mwenye hisia kali katika imani yake. Katika maisha yake yote yaliyojaa mapambano mengi (alipitia maanguko mengi ya kiroho, kujikwaa), Daudi alistahamili katika mahusiano yake na Mungu, akiwekeza muda wake, juhudi na unyenyekevu uliotakikana kwa uhusiano huo kukua. Alikuwa mng’amuzi kweli katika hilo kiasi kwamba hakuwa na ugumu katika kuuona uwepo wa Bwana - “wakati wote”, anatuambia – halafu kumtegemea pia, waweza hata kusema kumwegemea, Bwana katika magumu yote ya maisha. Hatuzungumzii msingi wa kinadharia hapa. Daudi anamzungumzia Bwana kuwa ni Nafsi halisi ambaye yuko naye pale “wakati wote” - uwepo wa kutiisha na wenye nguvu wa Mwana wa Mungu Mwenyewe! “Bwana ndiye anayenichunga” anasema katika Zaburi 23:1, na kwa hakika ni uwezo huu wa kumwona Bwana wake, kumwita katika jicho lake la kiroho Bwana wake na mwokozi wake ndio umesababisha sehemu kubwa ya mafanikio ya kiroho ya Daudi.

Kama Daudi, nasi pia tunaamini kwamba Yuko hapa nasi – na hata ndani yetu (Yoh. 17:23; War. 8:10; Wagal. 2:20; Waefe. 3:17; Wakol. 1:27). Lakini kukumbuka hili katika mshike-mshike ya maisha, kujizoeza nalo, kufika mahala pa kuitumia kweli hii kama ngao dhidi ya mikuki ya Ibilisi, na pia kama egemeo la imani yetu si jambo rahisi tu. Mtume Tomasi hakuridhika mpaka alipomwona Bwana Yesu Kristo uso kwa uso katika ufufuko Wake, lakini ebu tukumbuke maneno ya Bwana Yesu kwake: “wamebarikiwa wale ambao hawaja[ni]ona lakini wameamini” (Yoh. 20:29).

Inataka imani ili kuona uwezo halisi na utukufu wa Mungu. Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anatuambia kwamba Musa “alistahamili, kama yeye aliyeendelea kumwona Yeye asiyeonekana” (Waebr. 11:27). Ijapokuwa Mungu alikuwa haonekani machoni mwake, Musa hakutetereka. Nia yake ya kuendelea kumwona Bwana kupitia macho ya imani [yake] ilikuwa ndiyo msingi wa kukua kwake kiroho, na ndio msingi wa nguvu zake kuu za kiroho. Katika namna hiyo hiyo, mwandishi kwa Waebrania anaendelea kutuambia, nasi pia tuwe na desturi ya “kumtazama Bwana Yesu, Yeye ambaye ni mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu” (Waebr. 12:2). Akiwa ndiye kiongozi na mwenye kuhitimisha yote tunayoamini, Kristo anapaswa kuwa ndiye mnara wetu wa taa gizani, ile Nyota ya Alfajiri ambayo siku moja itachomoza katika ulimwengu huu wa giza inapaswa/ni lazima hata sasa iangaze mioyo yetu na iwe ndiyo nyota inayoongoza safari yetu katika maisha yetu (2Peter 1:19-20).

Ingawa hatumwoni Bwana na Mwokozi wetu kwa sasa, Petro anatuambia katika aya hii, bado tunampenda tu, na kitenzi-neno ambacho Petro anakitumia kuelezea upendo huu ni kile cha matumizi ya kawaida katika uandishi wa Agano Jipya, agapao (cf agape). Ingawa wino mwingi umemwagika katika fasili ya neno hili, [hata hivyo] yaweza kuwa na faida kidogo kuona kuwa mwana-historia wa Kiebrania wa karne ya kwanza Josephus analitumia neno hili katika kuelezea dhana ya kurudia kufanya kitu fulani tena na tena, au kupenda kufanya kitu fulani (akitumia tenzi-neno hili katika sehemu ya 1.64 ya kitabu chake Antiquities kueleza kwamba Jobel, mtoto wa kiume wa Ada “alijitoa au alijisabilia” katika maisha ya kichungaji). Analojia hii ni nzuri, kwani inatusaidia kulielezea neno-amri la maandiko la “kumpenda Mungu wako kwa nguvu zako zote” (Marko 12:30). Japo hatujamwona kwa macho yetu, tunapaswa kujisabilia Kwake, yaani tufanye uhusiano wetu na Bwana Yesu kuwa ni kitu tunachopendezwa nacho, kitu ambacho tunakistahi, tunakistawisha, kitu ambacho tunakifanyia kazi siku hadi siku. Ikiwa tuna uhusiano wa kidunia ambao ni muhimu, tutafanya hivyo hivyo; ni kwa kiasi gani basi tunapaswa kufanya juhudi za makusudi za kujitolea sehemu ya fikra zetu na nguvu zetu kwa Kristo – kumtafakari Yeye na sadaka aliyoitoa kwa ajili yetu, pamoja na kujitoa kwa namna tunavyoishi, iliyopangwa kumfurahisha Yeye.

Hitimisho: Maisha yetu ni kwa ajili ya Kristo tu. Kama, hata kwa mara moja tu, tutayaona haya yote kwa macho ya kiroho kwa wazi kabisa kama mtume Paulo alivyoyaona, basi hapo tunaweza kusema kwa kujiamini kabisa, “kwangu mimi, kuishi ni Kristo, na kufa ni mafao makuu” (Wafi. 1:21). Tukiwa na mtazamo na msimamo huu, ambao ndio utaimarisha imani yetu, basi ile “tuzo ya wokovu” ya aya ya 9 hapo juu (nukuu ya 1Pet. 1:8-9) itakuwa ni kitu cha uhakika kupata. Jambo hili - kuendelea na imani katikati ya mitihani ya maisha – ndilo litakuwa somo letu katika sehemu ijayo.

=0=

Imetafsiriwa kutoka: Seeing With the Eyes of Faith: Peter’s Epistles #23

=0=

Basi, na tuendelee na mfululizo huu katika somo #24, kwa neema za Mungu, Amina!