Nyaraka za Mtume Petro #22: Mitihani ya Imani Yetu
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

1Petro 1:6-7:
Katika kutazamia kwa hamu wokovu wa siku ile ya mwisho, furaha yenu inazidi sana, japokuwa kwa sasa yaweza kuwa mnateseka kwa muda mkipitia mitihani ambayo malengo yake ni kwamba imani yenu idhihirike kuwa ni halisi. Uthibitisho huu wa imani yenu una thamani kuu zaidi ya dhahabu, kwani dhahabu, japo nayo hupimwa ubora wake kwa moto, mwisho wake huharibika. Bali imani yetu, inapohakikishwa kuwa ni halisi katika majaribio makali ya maisha, itawasababishia sifa, utukufu na heshima kwenu pale Bwana Yesu Kristo atakaporudi katika utukufu wake.

Utangulizi: Somo letu lililopita lilijihusisha na umuhimu wa kuendelea na imani yetu licha ya [ma]shinikizo na majaribu mbalimbali yaliyoenea katika ulimwengu wa Ibilisi. Hili si jambo rahisi, ukichukulia ukweli kwamba lengo kuu la mfumo wa [ki]dunia wa Shetani ni kuwaweka wanadamu katika hali ya kutoamini (au, kwa waumini, kuwarudisha katika hali ya kutoamini). Hii ndiyo sababu katika somo lilopita, hatari zilizomo katika matendo yanayolegeza nguvu za imani yetu katika Kristo zilitiliwa mkazo, kwani, kama aya ya 5 inavyosema, “wokovu wetu siku ile ya mwisho” kutoka mauti [na kuwa na uzima wa milele] unategemea moja kwa moja katika uendelevu wa imani yetu. Katika aya za 6 na 7, Petro anahamisha msisitizo wa mjadala wake kuhusu imani na anatupatia msukumo chanya na motisha ya kustahamili katika imani yetu kwa Bwana Yesu Kristo. [Kumbe] shinikizo ambalo ulimwengu unaweka katika imani yetu linaonekana kuwa ni muhimu sana na lenye faida kwetu! Kwani bila mitihani, hakungekuwa na namna ya kuboresha imani yetu, kuitia nguvu, kuidhihirisha kuwa ni halisi. Ni mpango wa Mungu, Petro anatuambia, kuipima imani yetu mbele ya baraza la mbinguni, na kwa haki kutupatia thawabu kwa kuendelea na uaminifu licha ya [ma]shinikizo, majaribu na vishawishi tunavyokabiliana navyo katika ulimwengu wa Ibilisi.

Tanuru la Moto: Pale mfalme Nebukadnezza alipoamuru marafiki wa Danieli (Shadraki, Meshaki na Abednego) kutupwa katika tanuru lenye moto mkali kwa sababu ya kukataa kuisujudia sanamu aliyoisimamisha, hakuna aliyefikiria (katika umati uliokuwako) kwamba waumini wale wangeweza kupona (Danieli 3:1-30). Lakini Mungu aliwaokoa, tena kwa muujiza mkuu, akiwafanya waweze kuvumilia joto lile kali katika namna ambayo hata “harufu ya moto hawakuisikia”. Kujaribiwa kwa imani yetu katika tanuru la ulimwengu wa Shetani kunafanana na mtihani wa moto wa marafiki wa Danieli, kwani, katika namna ile ile, Mungu [wakati mwingine] huruhusu tupitie majaribu ambayo katika macho ya dunia “lazima yataunguza” imani yetu. Hata hivyo, tunapostahamili mitihani hiyo migumu, inakuwa ni ushuhuda kwa ulimwengu – na uhalisia wa imani yetu na uwezo wa kimiujiza wa Mungu wa kuwaokoa wale wanaomwamini Yeye na Mwanaye.

Tanuru Linaloboresha Imani: “Majaribio makali ya maisha”, kama Petro anavyoyaita (1Petro 4:12), pia yanatumika kuboresha imani yetu. Kama vile dhahabu inavyotathminiwa katika moto na kutenganishwa na chembechembe za uchafu, na kama chuma kinavyoimarishwa katika tanuri, vivyo hivyo imani yetu inaweza tu kuboreshwa kwa ustahamilivu chini ya shinikizo [kali], na itaimarishwa tu tunapojifunza kumtegemea Mungu katika nyakati za hatari. Mungu anaruhusu tukabiliwe na mitihani kwa faida yetu na faida ya ndugu zetu katika Kristo hapa duniani. Tunaposhinda kwa imani magumu yanayoletwa katika mapito yetu, mazoea tunayopata yanajenga imani yetu kwa Mungu, kwani tunajifunza kwamba Yeye atosha kutuokoa, si kwa nadharia tu, bali katika vitendo halisi. Majaribu yetu ya hapa duniani yanampa Mungu fursa ya kutuonyesha kuwa anaweza na atatuokoa kutoka katika mitihani yetu ya maisha; kwa upande mwingine sisi tunapata fursa ya kumwonyesha Mungu kwamba tunamwamini Yeye na Mwanaye, na tuko tayari kumtegemea Yeye hata wakati hali inaonekana kuwa ni ngumu sana. Tunapofanya hivyo, tunakuwa mashahidi kwa Wakristo wenzetu kwa kushuhudia juu ya uwezo na wema wa Mungu, na uwezo na thamani ya imani. Tunapoitumia imani yetu kwa ufanisi, mara nyingi tunajenga imani ya wenzetu hata zaidi ya imani yetu wenyewe. Katika mchakato huo, pia tunajifunza juu ya taswira mbali mbali za mateso kwa undani zaidi, na hii inatusaidia katika wakati tunapolazimika kuwatia moyo wengine katika majaribu yao yanayofanana na yetu (1Wakor. 1:3-4).

Kupogolea (Pruning) Imani Yetu: Majaribu yanaweza kuchukuliwa kwa mtazamo wa mafunzo, yaani matumizi kwa vitendo ya “mafundisho ya uongofu” tunayojifunza kwa nadharia (2Tim. 3:16). Kama tulivyoona hapo kabla (cf. Yoh. 15:2), Mungu anaupogolea mmea wa imani yetu (kupitia mitihani na majaribu) ili tuweze kuongeza uzalishaji wetu wa matunda kwa ajili Yake. Mchakato huu wa kupogolewa, japo mara nyingi una maumivu kwa wakati huo, una malengo ya kuleta matokeo chanya. Majaribu huzaa baraka, kwani ni kwa njia ya mitihani tu ndipo imani yetu inaimarika, na hivyo kuendeleza kupevuka kwetu kiroho na kuongezeka kwa baraka zinazotokana na kukua huko.

Msamiati wa Kiyunani unaotumika katika Yohana sura ya 15 unatupa mwanga katika mchakato wa kupogolewa kwa “mmea wetu wa imani” kutokana na mitihani tunayopitia. Katika aya ya pili, neno ambalo kwa kawaida linatafsiriwa kama “kupogoa” (pruning) ni neno la Kiyunani kathairo, na kwa kweli neno la Kiingereza “catharsis” linatokana na neno hili, maana yake kusafisha hisia [moyoni]. Waandishi “wamepanua” maana ya neno hili hapa, kwani hawakutaka kusema kwamba Mungu “anasafisha” matawi au mmea, bali aya ya 3 inaonyesha kwamba uamuzi wa Yohana wa kutumia msamiati huu ni wa makusudi, kwani Kristo anasema pale kuwa “ninyi mmekwishakuwa safi” (aya ya 3) [kitenzi cha Kiyunani kathairos, pia kutoka neno kathairo].

Maana ya analojia inayotumika katika Yoh. 15 ni hii: Kama Wakristo, tayari tumesafishwa na dhambi, kwani Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu na Mungu ametusamehe kwa msingi wa imani yetu katika Kristo na kazi Yake. Lakini japokuwa sisi ni wasafi kabisa kutokana na “nafasi” tuliyo nayo katika Kristo kwa sasa, bado tunaishi hapa duniani na tunaendelea kuishi hapa duniani na haiwezekani kuwa wakamilifu katika maisha yetu ya siku hadi siku. Kwa maneno mengine, utakaso tulio nao kwa nafasi hii (mara baada ya kuokolewa) hauwezi kuzaa utakaso wa papo kwa papo na endelevu uliotimilika (tizama somo #13): mara tunapokuwa Wakristo, bado tunahitaji kujifunza kuishi kama Wakristo. Kwa hiyo, mitihani ya imani yetu, kusafishwa au “kupogolewa” kwa namna tunavyoishi, ni sehemu muhimu katika mwendo wetu kuelekea kwenye kupevuka kiroho. Mitihani inapepeta, inapembua mapungufu yetu mengi na dosari zetu nyingi kwa jinsi tunavyojifunza kuanza kumwamini na kumtegemea Mungu zaidi na zaidi, na kupunguza kutegemea amana zetu wenyewe zaidi na zaidi.

Hivyo, kuanzia dakika ile ya wokovu, maisha yetu katika hii dunia yanahusisha matukio na matendo endelevu [zaidi na zaidi] ya Mungu “akitupogoa” na “kutusafisha”. Kwa hakika, mchakato huu haumaliziki hapa duniani mpaka kifo: Mtume Paulo, mmoja kati ya waumini wakuu kabisa katika historia ya Kanisa, alijaribiwa tena na tena kwa kiasi ambacho sisi wengine tusingeweza kustahamili. Akafikia hitimisho (conclusion) kwamba katika wakati na hali ngumu ya majaribu, alilazimika kuweka moyo wake kwa, na kutegemea uwezo wa Mungu zaidi ya wakati mwingine wowote; katika namna ambayo ulimwengu hauwezi kuelewa, udhaifu wake ndio uliomfanya awe na nguvu, kwa sababu ulimlazimisha kumtegemea Mungu na siyo nguvu zake mwenyewe (2Wakor. 12:9-10).

Kwa hivyo, maisha ya Kikristo yanahusisha kwa kiasi kikubwa sisi kukabiliana na mitihani mingi ambayo inatoa changamoto, inaimarisha, inaboresha na kuhalalisha imani yetu. Hivyo kwa maana hii, dhambi ni kinyume kabisa cha imani, kwani imani inamtegemea Mungu na kufanya mambo yote kwa maelekezo ya Mungu bila kujali maoni ya ulimwengu, wakati dhambi inamshakia Mungu na kusema, “nitalishughulikia hitaji hili mimi mwenyewe!”. Hivyo mbinu anayoitumia Mungu ya kutahini imani yetu ni kufanyia kazi mapungufu yetu kwa kutuweka katika mazingira ambamo tutayaona mapungufu yetu hayo na kuyafanyia kazi (kuyarekebisha) kwa kumwamini na kumtegemea Yeye na Mwanaye kutuvusha katika hali hiyo ya hatari. Hivyo tutaendelea kukua kiroho kwa kiasi chetu cha utayari wa kupata chakula cha kiroho kutoka katika Neno lake, na kutumia tulichojifunza kutoka katika Neno hilo pale tunapopata shinikizo, na tutaendelea kukua kwa kiasi hicho hicho, vile Mungu anavyotaka.

Mitihani ina viwango: Si wengi wetu tulio na kudura/majaliwa ya kujaribiwa kufikia kiwango walichojaribiwa Paulo au Ayubu, lakini licha ya mitihani migumu sana waliyopitia Paulo na Ayubu, waumini ambao ni mifano ya imani kuu, Paulo alisema kwa kujiamini kabisa, “hata hivyo, kutoka katika magumu yote haya, Mungu aliniokoa” (2Tim. 3:10-11), na Ayubu aliona mali zake zote zikirejeshwa na alipata familia nyingine pia (Ayubu 42:7-17). Sisi tunaokiri kuamini ahadi za Mungu na kumtegemea Yeye kwa wokovu wetu, wa hapa duniani na hata wa milele, tunapaswa kukumbuka kwamba mitihani ya duniani si ya milele, bali ni vikwazo vya muda tu katika safari ya kuelekea kwenye utukufu wa milele. Mitihani itaisha. Maisha yetu na Mungu hayataisha. Hivyo tunapokuwa hapa duniani, “tukitazamwa kwa makini na watu na malaika” kama Paulo anavyosema, tunalazimika kutizama kwa undani misingi fulani ambayo itatupa mtazamo chanya kuhusiana na magumu tunayoyakabili:

1. Majaribu/Mitihani Inavumilika: Msingi mmojawapo wa viwango/kiasi/mipaka ya majaribu/mitihani ambao tunapaswa kuukumbuka wakati wote ni ule anaotukumbusha mtume Paulo:

Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida [katika maisha] ya wanadamu; ila [zaidi ya hapo] Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo [kustahamili]; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea [namna ya kutatua tatizo], ili mweze kustahimili [shinikizo]. 1Wakor. 10:13 SUV.

Paulo hakuwa na uwezo wa kutuandikia kinaga-ubaga utatuzi wa mitihani yetu utakavyokuwa. Katika baadhi ya mifano ya mitihani, kama kugawanywa kwa Bahari ya Shamu, Mungu aliokoa watu wake kwa mwujiza wa wazi kabisa. Wakati mwingine, hata hivyo, wokovu Wake hauonekani kwa wazi namna ile, na pia hauna kishindo kama kile. Pia ni kweli ya Mungu kwamba wakati mwingine (na hii hutokea mara nyingi zaidi) Mungu anatuokoa na majaribu/majanga wakati tunapita katikati ya majanga/majaribu hayo, badala ya kutuepusha nayo kabisa yasituguse, ili kwamba tuweze kudhihirisha imani na subira tuliyo nayo mpaka mwisho wa jaribu, badala ya kuokolewa kimwujiza [kutoka] katikati yake. Kitu ambacho aya hiyo hapo juu inaonyesha wazi kabisa, ni kwamba Mungu ameahidi kwamba atatusaidia katika kila mtihani tutakaopitia katika maisha yetu. Ni wajibu wetu kuwa na subira na imani ya kulikubali zoezi la “kupogolewa” analotupatia ambalo amaelitayarisha ili litufikishe katika kiwango cha juu kabisa cha kupevuka kiroho. Kama tutayakabili majaribu ya maisha ya Kikristo kwa moyo na mtazamo huu, basi tutaongezeka katika kukua kiroho na pia katika baraka/neema tutakazopokea kutoka kwa Mungu, kwa faida yetu na faida ya wanaotuzunguka.
2. Kila Mtihani/Jaribu Lina Mwisho Wake: Msingi wa pili wa viwango au kiasi au mipaka ya majaribu/mitihani na ambao tunapaswa kuukumbuka ni kwamba japokuwa mtihani fulani unaweza kuonekana kama vile hauna mwisho, inabidi tuwe na subira inayotokana na mtazamo wa Mungu. Katika kuwajibu wanaodhihaki kwamba ulimwengu uko vile vile kama ulivyokuwa siku zote, mtume Petro anatuambia kwamba kwa Mungu “siku moja ni sawa na miaka 1,000”, na kwamba Mungu “hakawii” kutimiza ahadi zake licha ya madai yao wasioamini. Wakati ukifika, wakati wake Mwenyewe ukifika, wakati mwafaka aliopanga Yeye Mwenyewe, Mungu anatuokoa na jaribu, kama ambavyo siku ya hukumu atakavyokuja “kama mwivi usiku” wakati watu wasiokuwa na imani wamejisahau kabisa (2Pet. 3:8-10). Katika historia ya ulimwengu, waumini wengi wamekabiliwa na mtihani wa kungojea majibu kutoka kwa Mungu (Ayubu 35:14; Dan. 10:1-13). Kwa zaidi ya miaka mitatu, Eliya alilazimika kungojea wokovu wa Mungu kutokana na mateso aliyoyapata kutoka kwa Ahab na Jezebeli, mwanzoni akijikimu kwa chakula kilicholetwa na kunguru na maji yaliyotiririka kutoka mto Kerithi, na baadaye kwa mwujiza wa Mungu wa ngano na mafuta yasiyoisha pale kwa mjane wa Zarepa (1Wafa. 17). Lakini licha ya [muda mrefu] wa mtihani ule, Mungu alimweka Eliya salama na alimpatia mahitaji yake wakati wote, mpaka mwisho wake alipoonyesha ushindi mkuu kwa mkono wake dhidi ya manabii wa uwongo wa Baali (1Wafa. 18). Neno la Kiebrania lenye maana ya kumngojea Mungu (yachal, ambalo mara nyingi hutafsiriwa kama tumaini), linachukuliwa na baadhi ya wataalamu wa maandiko [ya Biblia] kumaanisha “kugeuka huku na kule kwa mahangaiko” kwa sababu ya mateso na maumivu makali. Kumngojea Mungu katika wakati wa shinikizo kunaweza kutupa taswira au hisia ya kufurukuta na kujinyonga-nyonga mwili kwa maumivu, lakini ni aina hii ya mitihani inayotakiwa kujenga imani yetu kwake Mungu na kuendeleza kwa haraka kukua kwa imani yetu.

3. Hatari ya Kuzimia: Kama vile mwanadamu anavyopoteza fahamu pale anapozimia, kuzimia kiroho ni kupoteza mtazamo wa maadili ya Kikristo kwa muda mfupi – kupoteza mtazamo wa ki-imani kwa Mungu kwa muda mfupi, tumaini la uhakika kabisa la thawabu ya milele na upendo wa kudumu kwa Mungu na watoto wake. Kuzimia kiroho ni matokeo ya kuogopa kwa muda [ukiwa] chini ya shinikizo kali la mtihani (na pia ipo mifano ya hili katika maandiko), kama vile Eliya alivyokimbia, Petro alivyokataa kumfahamu Kristo, na pale Ayubu alivyopoteza subira na Mungu. Watu wote hawa watatu walikuwa waumini wa kiwango cha juu sana, na wote walijirudi kutoka katika makosa yao [karibia] mara moja. Hata hivyo ni muhimu kukumbuka kwamba chini ya shinikizo kali la mazingira walimojikuta, wote walipoteza imani kwa muda, au wote walizimia kiroho kwa muda. Ikiwa jambo kama hili linaweza kuwasibu waumini wa kiwango cha juu kama hao, sisi pia tunapaswa kukubali uwezekano kwamba tunaweza kuwa hatarini kama ilivyokuwa kwao, haswa ikizingatiwa kwamba mateso na mitihani ni sehemu ya kawaida ya maisha ya Mkristo. Kama mtume Yohana anavyogusia, sisi sote tunashiriki katika “dhiki na taabu” zinazowasibu waumini wote, “ufalme” ambao waumini wote wanatazamia ujio wake, na “ustahamilivu katika Yesu Kristo” ambao waumini wote wanapaswa kuudhihirisha katika kuendeleza imani yao (Ufu. 1:9). Tunapojikuta tuko chini ya shinikizo kubwa, shinikizo ambalo pengine tunahisi hatustahili (au tunaonewa), au shinikizo linaloonekana kuwa ni kubwa kupita kiasi, basi tukumbuke kwamba sisi sio wa kwanza kubeba mzigo huu, na hatutakuwa wa mwisho (1Pet. 5:8-9). Waumini wa siku za usoni ambao watalazimika kustahamili shida za Dhika Kuu watajikuta wakikabiliana na [ma]shinikizo na mitihani mikubwa ambayo sisi wengine [labda] hatutakutana nayo (cf. Ufu. 8).

4. Kristo Aliweka Mfano Kwa Ajili Yetu: Kabla hatujadhani kuwa tumechaguliwa ili tupewe mateso makali kupita kiasi, tunapaswa kuukumbuka mfano wa Bwana wetu “ambaye alistahamili [ma]pingamizi makuu (upinzani mkubwa) dhidi yake kutoka kwa watenda dhambi, msije mkachoka mkazimia mioyoni mwenu” (Waebr. 12:3). Maisha ya Bwana wetu yalikuwa magumu kuliko maisha ya mwanadamu yeyote yule katika dunia hii, ukweli ambao unapaswa kututia heshima kuu juu Yake, haswa ikikumbukwa kwamba alijishusha hadhi Yake kwa kuamua mwenyewe ili sisi tuweze kuokolewa (Wafi. 2:6-8). Aliishi maisha ya utumishi mkamilifu kwa ajili ya wale aliowapenda, nao wakampa [thawabu] ya upinzani , kutomwamini, kumdharau, usaliti, mateso, na mwisho wake wakamwua katika namna katili kama vile alikuwa mhalifu. Hata hivyo anatufundisha kwamba ikiwa tunataka kikwelikweli kuwa wanafunzi wake (wafuasi wake) katika maisha yetu, basi nasi tunapaswa “kuubeba msalaba wetu na kumfuata Yeye” (Matt. 16:24). Kwa sisi kama Wakristo, hii ina maana kwamba maisha siyo kusukuma wakati huku tukifurahisha nafsi, bali ni jukumu tulilopewa na Mungu, na kumaliza jukumu hilo kwa mafanikio kunahusisha magumu, kuumia moyoni na mateso. Tumeambiwa na mtu mwenye mamlaka kutoka kwa Mungu mwenyewe kwamba yeyote anayetaka kuishi maisha ya kuwa mfuasi wa Bwana wetu atapitia mateso na shida (2Tim. 3:12). Lakini bila ya ustahamilivu mbele ya uso wa Ibilisi, bila “kushiriki katika mateso ya Kristo”, hatuwezi kufanikisha majukumu ambayo Mungu ametuwekea katika muda huu mfupi wa maisha yetu hapa duniani (2Wakor. 1:3-7; Wafi. 3:7-11; 1Pet. 4:13).

5. Mungu Ndiye Anayetupa Nguvu za Kusimama: Katika shida zote na mitihani yote, Mungu yuko pamoja nasi (Zab. 3:3). Alimtuma Mwanaye aje kufa kwa ajili yetu, ili nasi tuwe watoto wake, na ametupatia Roho Wake Mtakatifu akae ndani yetu na kutupatia faraja. Baba yetu anayajua mahitaji yetu yote. Yeye huvisha na kunyweshea [maua ya] yungiyungi ya porini na ndege wa angani, na anafanya hivyo hivyo kwa ajili yetu (Matt. 6:25-34). Mungu anayajua mahitaji yetu ya kimwili, na mahitaji yetu yote mengine pia. Alifanya mpango wa kuyatimiza mahitaji yetu yote hata kabla historia ya ulimwengu kuanza. Mungu pia hungojea kujibu sala na maombi yetu wakati wa uhitaji. Baba yetu hatotunyima kitu chochote chema tunachokihitaji (Matt. 7:7-12). Maandiko yamesheheni ushuhuda wa waumini waliouona uaminifu wa Mungu wa namna hii. Kama Daudi anavyoshuhudia, kupitia yote aliyoyaona katika maisha yake, hakuona Mungu akiwatelekeza wenye uongofu (haki), wala watoto wao wakiomba-omba chakula (Zab. 37:25). Ikiwa tutaendelea kuwa waaminifu na kumfuata Bwana wetu kwa uaminifu, tunaweza kuthibitisha kwa uhakika kauli/tamko la mtume Paulo: “Mungu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri Wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu” (Wafi. 4:19).

6. Jua Kwamba Mungu Anakutumia Wewe kwa Malengo Yake Mapana Zaidi: Tumeona kwamba majaribu ni suala binafsi na linalomhusu kila mmoja wetu peke yake, na lengo lake limepangwa kuwa ni kimarisha imani yetu na kuionyesha kuwa ni halali. Lakini mchakato wa kuipima imani ni zaidi ya hili. Majaribu (na kuyashinda pia) ni huduma ya ushuhuda, ni ishara, na inawatia moyo wale wanaotazama na kuona thamani na nguvu ya imani kwa jinsi imani ile inavyothawabiwa na kusimamiwa/kusaidiwa na Mungu. Katika nyakati za mitihani au majaribu, unaweza kuhisi kwamba hakuna mtu mwingine anayeona au kuelewa maumivu na/au magumu yetu, lakini tunapaswa kukumbuka kwamba ni Mungu tu anayejua ni nani wanaguswa na mwenendo wetu adilifu chini ya shinikizo. Hivyo tunapaswa kuiweka akilini huduma hii yetu [ya ushuhuda kwa wengine] wakati wowote mambo yetu yanapoonekana kama vile yanasambaratika, tusisahau kwamba tumaini letu la kwanza ni katika ufufuo kupitia imani yetu kwa Kristo na utukufu mkuu ujao, maisha ya baadaye ya mastaajabu kiasi kwamba shida zetu za sasa hazifai kulinganishwa nayo (War. 8:18).

7. Malaika Wanatutazama: Kwa dahari (aeons, eons) nyingi tusizozijua, ulimwengu ulikuwepo bila ya uwepo wa wanadamu ndani yake. Usaliti wa Shetani na hukumu kali ya Mungu iliyofuata juu ya dunia vikahitimisha nafasi ya upekee ya malaika kama viumbe wenye utashi, kwani mwanadamu aliumbwa ili kudhihirisha kwa malaika wote juu ya uwezo wa huruma ya Mungu. Hivyo kuumbwa kwa mwanadamu ilikuwa ni matokeo ya uasi wa malaika dhidi ya Mungu; basi hapa tutatazama kwa kifupi matokeo ya uhusiano wetu na hawa viumbe wenzetu wa mbinguni ili tuweze kuielewa vita yetu ya hapa duniani katika mwanga mpana zaidi. Kwani tukitumia mtazamo mwembamba, wa kidunia, sisi wanadamu tunakuwa na mayopia (kutoweza kuona mbali) pale tunapokabiliwa na changamoto, vurugu na mitihani ya maisha. Ama kwa hakika, uwepo wetu na maendeleo yetu ya kiroho vinatazamwa na kufuatiliwa kwa makini sana na malaika.

Malaika wamekuwepo [hata] kabla Mungu hajampa Adamu pumzi ya kwanza, na bila ya shaka yoyote ikiwa tungali [bado] katika miili hii ya nyama, tunapaswa kukaa mbali sana na hawa viumbe wenzetu [kwetu sisi, wao ni ‘moto wa kuotea mbali’] (2Pet. 2:10-11). Hata hivyo, japo wanadamu wanaanza maisha yao wakiwa “chini kidogo ya malaika”, (Zab. 8:5), katika ufufuo sisi tutahukumu malaika (1Wakor. 6:3). Tunaweza kuona kutokana na swali la Bwana wetu kwa Shetani, “Je, umemwangalia mtumishi wangu Ayubu?” (Ayubu 1:8), kwamba uwepo wetu una lengo la kuwa mfano endelevu na majibu ya Mungu kwa uasi wa malaika ulioongozwa na Ibilisi. Mungu anawatumia wanadamu, japo kwa kiasi tu, kuwaonyesha wale viumbe wake wengine kwamba kwa upande mmoja (upande wetu) yawezekana kuwa na imani kuu licha ya udhaifu na kwa upande mwingine (upande wa Mungu kwa njia ya Bwana Yesu Kristo) kuwa na huruma licha ya dhambi.

Hivyo tusisahau kamwe kwamba tunatizamwa – na siyo na Mungu pekee: “kuna furaha kuu katika umati wa malaika wa Mungu” pale mwenye dhambi mmoja tu anapotubu kuliko [pale] wengi wa wale waliookolewa tayari wanapoendelea kuamini (Lk. 15:10); wanawake wanashauriwa kuenenda kwa hekima “kwa sababu ya malaika [ambao wanatizama]” (1Wakor. 11:10; msingi huu unawahusisha wanaume pia); malaika wana shauku kubwa ya kujua maendeleo ya Mpango wa Mungu katika historia ya wanadamu (1Pet. 1:12); na Paulo alilalamika kwa Wakorintho kwamba amefanywa aonekane “kioja mbele za watu na malaika” (1Wakor. 4:9).

Kitu kingine, malaika hawa siyo kwamba wanatutazama bila kujali, bila “ushabiki” (for want of a better term/sina neno linalofaa zaidi). Kama vile Ibilisi na watumishi wake wanavyojaribu wakati wote kuharibu imani yetu na kutufanya tuangukie katika kutoamini na uasi kwa Mungu kama ilivyokuwa kwao (1Pet. 5:8), vivyo hivyo malaika wateule ni ndugu zetu: ni kwa lengo la kutusaidia sisi ndio maana “Mungu aliwafanya malaika zake kama upepo, na watumishi wake kama miali ya moto” (Waebr. 1:7 {Zab. 104:4} na 1:14; cf. Dan. 10:12-13); [Kristo anatuambia kuhusiana na watoto wadogo kwamba “malaika wao huko mbinguni” wakati wote wanautizama uso wa Mungu (Matt. 18:10); na malaika wamewekwa kulinda kila kanisa kati ya yale makanisa 7 ya Ufunuo (Ufu. 1:20). “Tukiwa na wingu hili kubwa la mashahidi [wanaotutizama]” na kuona mwenendo wetu wa kila siku tukiwa hapa duniani, tunawezaje kutetereka katika imani yetu? (Waebr. 12:1)? Tunapokumbuka kwamba viti vya mbinguni vimejaa malaika, wakishangilia maendeleo na mafanikio yetu ya kiroho, wakisikitika pale tunapoanguka au kujikwaa, hii inapaswa kutupa moyo na kututia nguvu. Moyo wa mtumishi wa Elisha uliyeyuka kwa hofu pale alipoyaona majeshi ya Aramu, lakini Elisha alimwomba Mungu afungue macho yake naye Mungu alifanya hivyo, akaona wazi kabisa “mlima wote umejaa farasi na magari ya vita kumzunguka Elisha” (2Wafalme 6:17). katika namna hiyo hiyo, tunapaswa kufungua macho ya mioyo yetu na kuuona uhalisia kwamba hatuko wakiwa. Mungu yu pamoja nasi, na watumishi Wake wanatutizama. Hakuna mtihani, hakuna jaribu, hakuna vita isiyokuwa na mashahidi wa mbinguni. Hivyo basi, “na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu” (Waebr. 12:1), tukifahamu fika kwamba ndugu zetu malaika wanatushangilia kule mbinguni.

Hitimisho: Tumaini letu ni la milele: Na hivyo tunastahamili katika imani, tukivumilia kwa saburi majaribu ambayo ni heshima kwetu kuyapokea tukiwa ni wale “wanaoshiriki mateso ya Kristo” (1Pet. 4:13), tukingojea kwa matarajio ule wakati ambapo imani yetu “itahakikishwa kuwa ni halisi katika majaribio makali ya maisha” (1Pet. 1:7a), na mwisho wake “tupate ile sifa, na utukufu na heshima pale atakapofunuliwa Bwana Yesu Kristo” (1Pet. 1:7b). Imani yetu ni yenye nguvu kwani tunajiamini katika tumaini letu, yaani katika matarajio ya wokovu wa siku ya maisho, ya ushindi wa siku hiyo, ya kuhalalishwa siku hiyo, na thawabu kuu kuzidi kitu/shida yoyote tuliyolazimika kustahamili katika maisha haya mafupi ya duniani. Wana wa Israeli walifikishwa, katika namna hiyo hiyo, kutoka Misri na hadi kufika katika nchi inayomiminika “maziwa na asali”, na vivyo hivyo, bila kukosa mitihani na majaribu makuu. Basi na tuone hapa na sasa, kwa kutumia macho ya imani, uhakika wa kuokolewa na kuthawabiwa, ili tuweze kuuona wokovu huo hata kabla ya wakati wake. Na tufurahie kule kugawanyika kwa bahari yetu binafsi ya Shamu hata kabla yale maji ya kutisha hayajatingishwa, na tujue kwa uhakika usiotingishika kwamba Mungu atatuvusha bila ya sisi kulowana katika wakati wake Yeye mwenyewe alioupanga. Ni kwa mtazamo na mwenendo huo tu ndipo ile “sifa, utukufu na heshima” inayosemwa katika aya ya 7 itakuwa yetu: pongezi kutoka kwa Mungu (ule mkono wa “umefanya vyema” kutoka kwa Bwana wetu), utukufu kutoka kwa Mungu (atakapodhihirisha kwa wote mafanikio yetu), na heshima kutoka kwa Mungu (tutakapopewa thawabu halisi zitakazodumu milele). Ama kwa hakika baraka hizi si za kulinganisha na shida na masikitiko ya wakati huu. Milele iko mbele yetu, imesambaa hadi na kupita upeo wa macho yetu. Basi na “tukimbie kwa uvumilivu” mashindano haya mafupi yaliyo mbele yetu tukijua kikamilifu kwamba Mungu yuko nasi katika mbio hizo, na amesimama pale sisi tutakapopiga ile hatua ya mwisho, akiwa tayari na thawabu yetu kwa “kazi” tuliyoifanya ya kuijenga, na kwa ajili ya uvumilivu, wa imani yetu.

=0=

Imetafsiriwa kutoka: The Testing of Faith: Peter’s Epistles #22

=0=

Basi, na tuonane katika sehemu #23 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!