Kuzaliwa Upya Kiroho: Nyaraka za Petro #19
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

Utangulizi: Katika somo hili, tunarudi kwenye fasili/ufafanuzi wa 1Petro. Tulitoka nje ya mada kwa muda mrefu ili kuzungumzia somo la kupevuka kiroho, lililosababishwa na ile salamu ya Petro katika aya ya pili: “neema na amani vizidishwe kwenu”. Kwa maneno haya (kama tulivyoona katika masomo yaliyopita tulipozungumza kwa kirefu kuhusu kupevuka kiroho), Petro anaelezea ombi lake lenye lengo la ongezeko la fadhili za Mungu kwa ajili yetu (neema), na ustawi ndani ya mioyo yetu (amani). Ongezeko la neema katika maisha yetu na amani mioyoni mwetu ni matokeo muhimu ya kupevuka kiroho. Hivyo, pale Petro anapoomba hayo kwa ajili yetu, wazo alilo nalo ni kwamba ombi lake litatimizwa tu ikiwa sisi tutaipokea ile changamoto ya kila mmoja wetu kukua kiroho. Moja kati ya matokeo ya hii salamu ya Petro ni kuweka wazi kwamba aya zinazofuata mara baada ya hizo (aya za kumsifu Mungu za 3-9) zinaunganishwa na ombi hilo. Petro, muumini anayefuata agizo la kukua kiroho, hapo anamsifu Mungu kwa “tumaini hai” alilo nalo katika Bwana Yesu Kristo. Sisi pia twaweza kuyatumia maneno haya, na kuweka mioyo yetu katika tumaini hili hili, ikiwa tunasonga mbele katika kukua kiroho.

Wimbo wa Sifa (aya za 3-9): Katika doxology (neno la Kiyunani ambalo maana yake ni hotuba ya sifa au kutukuza), Petro anamtukuza au kumsifu Mungu katika namna inayotupatia habari/dondoo muhimu kutoka katika maandiko. Mara baada ya kutuombea kupevuka kiroho katika aya ya pili, wimbo huu wa sifa (doxology) wa Petro unaelezea kwa undani uelekeo wa mioyo yetu kupitia zile hatua tatu za fikra adilifu, zinazoelezewa katika mfumo wa wimbo wa sifa kwa Mungu. Petro anayazungumzia maadili haya makuu matatu katika mtiririko wa tumaini, imani na upendo:

Aya za 3-5: Tumaini Lenye Uzima

Aya za 6-7: Mateso Huimarisha Imani

Aya za 8-9: Kristo, Mlengwa wa Upendo wetu

1.3  Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;
1.4  ili tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.
1.5  Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani ili/[hata] mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.
1Petro 1:3-5 SUV

Tumaini Lenye Uzima: Aya hizi tatu zinatupeleka katika fikra adilifu ambayo ni nguzo muhimu katika kupevuka kiroho: tumaini. Kama tulivyoona katika masomo yaliyopita, maadili ni muhimu kwetu na ni lazima tuelekeze fikra zetu kwayo, kwani yanatusaidia kukaa katika mitazamo na mwenendo wa Kikristo unaofaa kwa wito wetu huu mkuu. Tunapoelekeza fikra zetu katika maadili, inatusaidia katika kuweka wazi mafungu na misingi mingi ya kweli, na kutukumbusha umuhimu wa taswira zote ambazo misingi hiyo inagusa. Maadili haya ni muhimu sana katika kuyatafsiri na kuyaelewa matukio yanayofanyika katika maisha yetu ya kila siku, na katika kutumia misingi ya kweli kuhusiana na tunavyoyakabili matukio hayo. Kwa mfano, kwa kuelekeza mawazo yetu kwa makini kabisa katika fikra adilifu ya tumaini, tutakuwa tunaweka fikra zetu (kwa ujumla) katika misingi muhimu inayohusika na uzima wa milele, maisha ya ajabu yajayo ambayo yanayazidi kwa mbali sana maisha haya ya hapa duniani.

Matumaini yanaondoa uelekeo wa macho yetu kutoka kwenye udanganyifu wa ulimwengu unaotuzunguka na yanatukumbusha kwamba tunayo maisha mengine, mema, ya milele, yanayotungojea mbinguni. Biblia ina habari nyingi zinazohusiana na suala la uzima wa milele, lakini, katika aya za 3-5, Petro anatizama kwa undani taswira tatu muhimu za matumaini. Taswira hizi zote tatu zinaelezewa katika mfumo sambamba, kwa namna ambayo ni rahisi sana kueleweka katika maandiko ya lugha ya Kiyunani, na ambayo yametajwa katika vifungu vitatu hapo juu. Petro anaunganisha hizi taswira tatu za maisha yetu mapya tunayoyatarajia (na, katika Kristo tunayo tayari), na anaanzisha/anatanguliza kila taswira kwa kihusishi eis (Kiyunani, inatafsiriwa hapa kama “ili”). Kwa huruma ya Mungu tumezaliwa upya:

1) ili tupate tumaini lenye uzima (aya ya tatu)

2) ili tupate na urithi usioharibika (aya ya nne)

3) ili mpate wokovu (aya ya tano)

Tumaini lenye uzima la aya ya tatu linaelekeza macho yetu kwenye mwili mpya wa ufufuo ambamo ndani yake [mwili huo] tutafaidi uzima wa milele; urithi usioharibika wa aya ya nne unatukumbusha juu ya thawabu za milele ambazo hazitaharibika milele; wokovu wa aya ya tano unatutia moyo kwamba “tutasimama” katika hukumu ya mwisho, ikiwa katika maisha yetu ya hapa duniani tumeishi kwa imani isiyotetereka (cf. Zab. 1:5).

Zaidi ya hapo, kila moja kati ya taswira hizi tatu za matumaini zinaenda sambamba na yale mabadiliko ya aina tatu ya maisha ya Kikristo (cf. Wakol. 1:13). Kama tulivyoona katika somo #13, mabadiliko haya (au mchakato wa utakaso au kufanywa watakatifu) ni namna maandiko yanavyoelezea maendeleo ya Mkristo katika “utakatifu”, yaani mabadiliko yetu kutoka katika himaya ya ulimwengu na kwenda katika himaya ya kiroho [ya Mungu]. Tunaanza kama “watakatifu” kwa sababu ya nafasi tuliyo nayo katika Bwana Yesu Kristo, Yeye “aliye Mtakatifu” (utakaso wa mwanzo) na tunaishia kuwa “watakatifu halisi” katika ufufuo ambapo hatutakuwa hata na chembe ya hali yetu ya dhambi ya mwanzo katika miili yetu mipya tutakayopata (utakaso wa mwisho); hapa katikati, katika kipindi cha maisha ya hapa duniani, tunapaswa kuwa tunaondoa taratibu ushawishi wote wa dhambi na uchafu ili tuweze kuishi maisha “matakatifu” (utakaso maishani). Huu utakaso katika maisha, ambao ni mabadiliko ya kiroho yanayotokea kati ya utakaso wa mwanzo na utakaso wa mwisho, unategemea maamuzi ya saa hadi saa na siku hadi siku; hivyo basi mchakato wa utakaso maishani ni sawasawa na mchakato wa kukua kiroho.

Hivyo, wokovu wa aya ya tano unazungumzia ule usalama tulio nao sasa (na tunaoutarajia milele) kwa sababu ya nafasi tuliyo nayo katika Bwana Yesu Kristo (utakaso wa mwanzo); tumaini lenye uzima la aya ya tatu na mwelekeo wake makini katika ufufuo unaonyesha jinsi tunavyojiamini katika mabadiliko matakatifu ya miili yetu (utakaso wa mwisho); urithi usioharibika wa aya ya nne ni tumaini letu la thawabu linalotegemea kukua kwetu kiroho na uzalishaji wa matunda unaotokana na kukua huko (utakaso maishani). Kila taswira ya tumaini inaonyesha uhakika wa mazuri yanayokuja kwa wale wanaompenda Bwana Yesu Kristo na kumfuata kwa uaminifu katika maisha yao ya hapa duniani (War. 8:28), kwani hawafuatishi mfano wa ulimwengu huu, bali wanageuzwa kwa kufanywa wapya kulingana na mpango wa Mungu kwa kila mmoja wao (War. 12:2).

Sifa (aya ya tatu): Petro anaposema katika aya ya 3 “Ahimidiwe (apewe sifa) Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo!”, anatutia moyo tuelekeze furaha na shukrani zetu kwa Yeye anayetupatia baraka zinazotajwa katika wimbo/hotuba ya sifa (doxology) inayofuata. Neno linalotafsiriwa kama “ahimidiwe/apewe sifa” katika aya ya 3 ni neno la Kiyunani eulogetos, ambalo (pamoja na kitenzi chake eulogeo hutumika wakati wote katika Agano Jipya kama lenye maana sawa na neno la Kiebrania barach (“ku-bariki”). Neno hili la Kiyahudi/Kiebrania hapo mwanzo lilimaanisha “kupiga magoti” na uwezekano mkubwa ni kwamba limetokana na neno berech, yaani goti. Na mara nyingi katika Kiebrania, mkao (pozi) wa aina fulani unakuja kuhusishwa na kitendo kinachoambatana nao (kwa mfano neno todah, au “shukrani” hapo mwanzo inawezekana lilimaanisha “kunyoosha mkono juu” kama ishara ya kushukuru). Hivyo, mtu alivyopiga magoti mbele ya mkubwa au yeyote ambaye alistahili heshima, maneno atakayosema wakati huo yatakuwa pia ya upole na ya kuheshimu. Hivyo, maneno-tenzi yote haya ya Kiebrania na Kiyunani yakaja kumaanisha “kusema mema juu ya, kutoa sifa juu ya, kubariki”. Yanaweza pia kutumika katika kuomba baraka kutoka kwa Mungu, na Mungu “anaposema mazuri na kwa upendo” juu ya mtu fulani, kwa kawaida kuna faida, “baraka” inayotokea. Baadhi ya “baraka” za Agano la Kale (Yakobo na Yosefu/Yusufu ni mifano mizuri) zilikuwa zaidi ya maombi, kwani aliyeomba au aliyesihi kwa malengo ya baraka hizo pia alikuwa na kipaji cha unabii kutoka kwa Mungu. Leo, “tunapombariki” mtu tunaomba baraka za Mungu juu yake mtu huyo.

Matakwa ya Petro kwamba “tumsifu Mungu” yana hisia [kali], na itakuwa vyema tusitenganishe furaha na hisia kutoka katika maana anayokusudia [hapa], lakini pia ni muhimu sana kwetu kuyaona mambo mawili mengine hapa:

1) Sifa zinazotakiwa kuelekezwa kwa Mungu siyo tu tupu na zisizo na maana; bali ni furaha na shukrani zilizo na msingi wake katika kweli ya maandiko. Tunajua kwa nini tunamsifu Mungu, na tunaelekeza fikra zetu kwenye jambo la maana sana, hivyo tunaoanisha hisia za shukrani na fikra sahihi za kimaandiko (cf. 1Wakor. 14:18-19).

2) Sifa tunazoamriwa kuzionyesha hapa zina lengo la kutufanya turejeshe macho yetu kwa Mungu, na hivyo ni hisia za makusudi na zenye lengo maalum. Msingi wa sifa tunazotoa ni shukrani zetu Kwake kama Chanzo cha kupevuka kiroho (kama inavyosemwa kabla ya sifa kutolewa) na chanzo cha “tumaini lenye uzima” (kama inavyojadiliwa baada ya sifa hizo). Kwa kuelekeza shukrani zetu kwa Mungu, Petro anaondoa hisia zozote za kujiona tumefanikisha kitu chochote (kwa juhudi zetu wenyewe). Tunapaswa kuchunguza maendeleo yetu ya kiroho na kutarajia utimizo wa tumaini letu, lakini tunapaswa kukumbuka pia kwamba huu ni mpango wa Mungu, na kwamba sisi ni washirika kwa neema zake na kwa ajili ya utukufu wake.

Huruma (aya ya 3): Katika 1Timothy 1:2 (linganisha na 2Tim. 1:2 na 2Yoh. 1:3), katika salamu za utangulizi zinazofanana sana na zile Petro anazozitoa katika waraka wake, Paulo anamwombea neema, huruma na amani Timoteo, hivyo anaongeza “huruma” katika maneno mawili ya baraka yanayotumiwa na Petro. “Huruma” pia ni neno linalotumiwa na Petro katika barua hii, ambalo limeongezwa hapa katika aya ya tatu kuelezea mtazamo wa Mungu katika kutupatia uhai mpya. Huruma inaelezea taswira ya msamaha ya hulka ya Mungu katika baraka zake kwetu, wakati huo huo ikielezea utoaji wa Mungu na upokeaji wetu na shukrani zetu. Kumtakia mtu neema, huruma na amani ni kumwombea mzunguko/mpango mzima wa baraka za Mungu: fadhili [za bure] kutoka kwa Mungu (neema), kwa wote wanaostahili kuzipata kupitia/kutokana na msamaha wa Mungu katika Bwana Yesu Kristo (huruma), na matokeo yake ni faida za kiroho kwao wote wanaoipokea kupitia kukua kiroho (amani).

Maneno haya matatu yanatangamana na yale maadili 3 ya imani, tumaini na upendo. Imani inaamini/inaweka tegemeo lake katika neema za Mungu. Tumaini linaelekeza uso wake katika huruma za Mungu. Upendo unaenda hatua kwa hatua na amani ya Mungu. Imani inanyoosha mkono kuipokea neema [ya bure] ya Mungu ambayo ni zawadi ya Mwanaye wa pekee, Bwana wetu Yesu Kristo (1Wakor. 9:15; Waefe. 2:5-9), hivyo kujitwalia neema za ahadi za Mungu (kama vile Abrahamu alivyoamini ahadi ya Mungu ya kumbariki kwa kumpatia mrithi: Mwa. 15:6). Tumaini ni kujiamini kwetu katika milele ijayo, ukombozi wetu kutoka katika mikono ya hukumu na kuwepo kwetu katika ufufuo unaotegemea huruma na msamaha wa Mungu kupitia dhabihu ya Bwana Yesu Kristo (Waefe. 2:4-5; Yuda 21). Upendo wetu kuelekea kwa Mungu na kutoka kwa Mungu ndiyo sifa bainifu (hallmark) ya kupevuka kiroho na inazaa amani ya ndani ya moyo ambayo ulimwengu huu hauwezi kuizaa wala kuielewa.

Unyenyekevu huchukua nafasi kubwa katika kutuelewesha (kutupa ufahamu) juu ya hulka ya kutoa (neema, n.k.) ya Mungu na ndiyo daraja linalounganisha fikra adilifu za imani, tumaini na upendo pamoja na neema, huruma na amani. Kwa kuwa imani haiwezi kutenganishwa na unyenyekevu (1Pet. 5:5-6), tunapomwamini Mungu kutatua shida zetu, tunapaswa kutambua kwamba sisi wenyewe hatuwezi kuzitatua, na inabidi tutegemee hulka ya neema na ya kutoa ya Mungu (Waefe. 2:8-9). Vivyo hivyo, tumaini letu, kwa unyenyekevu na kwa kujiamini, linazingatia msingi kwamba msamaha wa Mungu (na hivyo wokovu wetu) hautegemei tendo au kazi yoyote tuliyofanya, bali Yeye ametuokoa kwa huruma yake (Tito 3:5), na huruma hii huwaendea wale wanaompa heshima stahiki kwa unyenyekevu (Lk. 1:50). Mwisho, Yakobo anaielezea amani ya kweli ya Kikristo katika misingi inayofanana sana na kanuni ya upendo katika Roho Mtakatifu inayofundishwa na Paulo (linganisha Yakobo 3:17-18 na Wagalatia 5:14-26). Tunavyopata amani kwa kuendelea kukua kiroho (1Pet. 3:10-12), na katika unyenyekevu tunajifunza kumwachia Mungu matatizo yetu (Matt. 6:25-34), tunawekwa huru mioyoni mwetu na mambo ya ulimwengu huu, na tunakuwa huru kuakisi upendo wa Mungu kwa wengine.

Kuzaliwa Upya Kiroho (aya ya 3):

Yesu akamjibu, akamwambia, “Amin, amin nakwambia, mtu hawezi kuuona ufalme wa Mungu asipozaliwa mara ya pili” Yohana 3:3

Kauli ya Bwana Yesu kwa Nikodemo ni dhahiri na hairuhusu shaka, kama inavyoonyeshwa na kurudia kwake neno la dhati la Kiebrania amen (maana yake “kwa kweli” i.e. “hili linapaswa kuaminiwa”): bila ya kuzaliwa upya, hatuwezi kuingia katika uzima wa milele, ufalme wa Mungu. Kuingia katika uzima wa milele kunalazimu mabadiliko makubwa ndani yetu. Uhai tuluozaliwa nao mara ya kwanza hautoshi. Tunapaswa “kuzaliwa upya” ili kupata uhai mpya, uzima wa milele ambao unatokana tu na imani katika Bwana Yesu Kristo. Sasa, miili tuliyo nayo sasa, ambayo ni damu, mifupa na nyama haina uwezo wa kuishi mpaka, wala katika, ufalme wa milele (1Wakor. 15:50). Ni lazima tuwe na mwili mpya, tofauti na huu, ili tuweze kuishi katika huu uzima mpya wa milele. Kwa kuunganisha dhana ya kuwa “wazaliwa wapya” katika namna ya moja kwa moja namna hii na kuingia katika ufalme wa milele wa Mungu, Bwana wetu anatuelekeza kwenye hii kweli. Tunapozaliwa upya, yaani kuzaliwa mara ya pili kwa Roho na wala si kwa mwili, (Yoh. 3:6), tunamiliki uzima huu kutokana na nafasi tuliyo nayo (yaani, tuna stahiki kamili na ya nguvu juu ya uzima huu kutokana na nafasi yetu iliyo imara na salama katika Bwana Yesu Kristo) lakini hatuwezi kuutumia uzima huu kikamilifu kwa sababu miili yetu bado haijafufuliwa/haijabadilishwa. Kufaidika kwetu kikamilifu na uzima wa milele ambao tunapewa pale tunapozaliwa upya kutapatikana tu pale miili yetu mipya ya baadaye itakapooana na hii kweli mpya (uhai mpya) tuliyo nayo sasa. Tutafaudu uhalisia wa uzima wetu mpya katika siku ya ufufuo na kuendelea. Mwili wa ufufo ni mwili mpya ambao “utavaliwa” na uzima wetu mpya (tunaoupata pale tunapozaliwa upya). Kwa kuokolewa, kuzaliwa upya, tunakuwa na uzima mpya na tunapata uhakika wa mwili mpya ambao utaendana na kutangamana na uzima huo kukamilifu. Kwa kuzaliwa upya, tunakuwa na uhakika wa kuingia katika ufalme wa Mungu.

“Kuzaliwa upya”, kulingana na kauli za Kristo katika muktadha huu (pamoja na aya nyingine katika maandiko ambapo kanuni hii inafundishwa), ni fundisho linalorejea katika maisha mapya tuliyo nayo katika Kristo, maisha ya milele ambayo [kwa sasa] tunajitwalia kwa sababu ya imani tuliyo nayo katika Yeye na kwa sababu tunajitambulisha kwa Jina na Nafsi yake, ni yetu kuyafurahia kikamilifu pale miili yetu isiyo na ukamilifu itakapobadilishwa na kuwa yenye uwezo wa kuishi milele katika tukio la ufufuo. Hivyo sisi, japokuwa tulifaa tu kwa kifo kutokana na kuzaliwa kwetu kimwili ile mara ya kwanza (War. 5:12-14; 1Wakor. 15:22; Waebr. 9:27; Zab. 51:5), kwa imani yetu katika Bwana Yesu Kristo tumezaliwa “tena”, na tumetoka katika kifo (hukumu ijayo na kifo/mauti ya pili) tunaenda katika uzima (uzima wa milele, tulio nao kwa sasa na utakaotimizwa katika siku ya ufufuo: Yoh. 5:24; 1Yoh. 3:14). Hivyo, “kuzaliwa upya” maana yake ni kuwa na uhai mpya, wa pili; yaani uzima wa milele unaotolewa na Mungu kwa wote wanaomwamini Mwanaye (Yoh. 3:15-16). Kama waumini, tunao huu uzima wa milele kutokana na nafasi yetu katika Kristo kwa wakati huu (1Yoh. 5:13) kama dhamana ya kupatiwa uzima wa milele hapo baadaye pale miili yetu ya uharibifu itakapofufuliwa bila uharibifu (1Wakor. 15:53-55). Hivyo sisi “tuliozaliwa upya” ni “viumbe wapya” (2Wakor. 5:17; Waga. 6:15; Waefe. 2:15; 4:24). Tumezaliwa upya kwa sasa kupitia imani yetu kwa Neno la Mungu (Yoh. 3:36), na pia tunatazama siku za usoni pale tutakapoona matunda ya uzima wetu wa milele katika miili yetu mipya ambayo Mungu ametuahidi tutakuwa nayo:

3.1  Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
3.2  Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.
3.3  Kwa maana mlikufa [kwayo yaliyo chini], na uhai wenu [halisi] umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.
3.4  Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu [wa ufufuo].
Wagalatia 3:1-4 SUV

Uzima wa milele tulio nao “umefichwa kwa usalama” na Mungu. Pale Yeye aliye tumaini letu, Bwana Yesu Kristo, atakaporudi katika utukufu hapa duniani, nasi pia tutavikwa utukufu, utakatifu halisi wa miili yetu mipya, ya milele, ambayo ni “nyumba” mpya za uzima wetu wa milele. Hivyo katika aya hizo hapo juu, misingi yote miwili ya kuzaliwa upya, “nafasi” yetu ya sasa katika Kristo, na kutimizwa kwake hapo baadaye kupitia ufufuo, vinaelezwa waziwazi.

Kwa hakika ziko aya nyingine za maandiko zinazozungumzia somo hili pia, zikiongeza mwanga katika taswira nyingine za maisha yetu mapya katika Kristo. Neno la Mungu linashika usukani katika huku kuzaliwa kwetu upya. Katika Yakobo 1:18, imeandikwa kwamba Mungu “ametuzaa kwa Neno la kweli” ili tuweze kuwa kama “mazao ya kwanza” katika viumbe vyake (kauli inayorejea ufufuo unaokuja; cf. 1Wakor. 15:23). Huko mbele katika barua yake, Petro (katika 1Pet. 1:23) anatuambia kitu kinachofanana na hicho anachosema Yakobo, anapotamka ya kwamba “tumezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile mbegu isiyoharibika, kwa Neno la Mungu lililo hai na linalodumu milele”. Jinsi Neno la Mungu linavyodumu milele, nasi pia tulio na ile mbegu ya kweli ya milele ndani yetu tutaiona ikichipua na kusitawi na kuwa ule mwili wa ajabu utakaoishi milele (1Wakor. 15:35-41). Usalama kamili wa anayeamini “ambaye mbegu [ya Mungu] yakaa ndani yake” unathibitishwa na Yohana, na unamaanisha hii mbegu ya kweli ya Injili ya Kristo inayotia uzima na kujenga dhamana ya uzima wa milele ndani yetu (1Yoh. 3:9): tunapoendelea kumwamini Yeye, ile kweli iliyo ndani yetu ni mbegu inayotupa dhamana ya uwepo wa uzima wa milele wakati wa ufufuo (tizama pia 1Yoh. 4:7; 5:1; 5:4; 5:18).

Kama aya yetu katika 1Pet. Inavyosema, Mungu, katika huruma zake nyingi “ametufanya tuzaliwe upya ili tupate tumaini lenye uzima”. Tumaini letu ni kulishinda kaburi kwa ufufuo na uzima wa milele. Kwa imani yetu katika Bwana Yesu Kristo ambaye kazi yake katika kulipia dhambi zetu imeweka njia safi kwa ajili ya msamaha wetu, hata sasa tunao uzima wa milele ambao ni dhamana ya ule ufufuo. Kwa huduma ya wokovu ya Roho Mtakatifu “tumefanywa wapya” na “tumezaliwa upya” (Tito 3:5). Hatujazaliwa mara moja tu (ambayo mwisho wake ni mauti), bali “tumezaliwa mara ya pili” (ambayo mwisho wake ni uzima wa milele), tulio nao sasa, bali utatimizwa katika ufufuo unaokuja (Matt. 19:28).

“Tumezaliwa upya” katika tumaini hili la ufufuo na thawabu (1Pet. 1:3); ni tumaini hili ambalo linashusha nanga ya mashua yake huko mbinguni (Waebr. 6:19) na kuelekeza macho yetu kwa mambo yaliyo mbinguni (Wakol. 3:1-4); ni tumaini hili linalotupa changamoto ya kuyafanya maisha yetu hapa duniani kuwa “mapya” kama tunavyotarajia maisha mapya ya mbinguni ambayo siku moja tutaishi (Waefe. 4:22-24).

Petro anaposema “tumezaliwa upya”, anamaanisha tumepata/tumepewa uzima wa milele, na tumaini ambalo kwalo tumezaliwa mara ya pili ni tumaini la kuona uzima huu wa milele tulio nao sasa (kwa kuzaliwa upya kwa imani yetu katika Kristo) likitimizwa katika ufufuo wa mwili huu wa duniani ambao utabadilishwa na kuwa mpya, wa milele ambamo tutaishi milele, na Mungu. Kwa namna hii, “mauti imemezwa na ushindi” (1Wakor. 15:55), ushindi dhidi ya kaburi ukifanikishwa na ufufuo wa mwili kupitia imani yetu katika Kristo. Katika kuzaliwa upya, (na katika dhamana ya Roho Mtakatifu, Waefe. 1:13-14) tuna uhakika wa tukio hili la baadaye. Katika somo linalofuata, tutazungumzia kile Biblia inachosema juu ya ufufuo huu.

=0=

Imetafsiriwa kutoka: Spiritual Rebirth (Being Born Again): Peter’s Epistles #19

=0=

Basi, na tuonane katika sehemu #20 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!