Imani na Kukua Kiroho: Nyaraka za Mtume Petro #14
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili Imefanywa na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission For This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

Mapitio: Mchakato wa kukua kiroho, japo ni rahisi katika muundo wake, lakini unahitaji juhudi kubwa. Unahitaji tulitafute na tulisikilize Neno Lake, tuiamini kweli Yake, tuishi maisha yetu kwa kuitumia kweli hiyo, na tuikumbatie kazi ya Kanisa Lake na kuwasaidia wengine kutokana na vipaji tulivyopewa na Roho Mtakatifu.

“Kusikiliza”, kama tulivyoona katika sehemu iliyopita, ni hatua ya kwanza katika mchakato huu. Unaposikiliza Neno la Mungu maana yake unatilia mkazo msingi kwamba sisi waumini tunawajibika kuchukua hatua ya kwanza katika kukua kiroho kwa kujitoa kwa dhati kwa ajili ya Biblia na kwa kukusudia kupata mafundisho sahihi ya Biblia – siyo kusalimisha (na hivyo kuipoteza) ridhaa yetu, siyo kuacha uwezo wetu wa kupambanua na kuhukumu, bali ni kutafuta na kuchagua mazingira ya kujifunza na kuabudu ambamo ndani yake tunapata fursa ya kukua.

Sasa tunaenda kwenye hatua ya pili katika mchakato wa kukua kiroho, “kuamini”. Hii yaweza kuwa awamu muhimu zaidi katika vita yetu ya kumjenga yule “mtu wa [ndani ya] moyoni mwetu”, kwa sababu hii ndiyo hatua ambayo aidha “tunashinda au tunashindwa” katika maendeleo yetu ya kiroho. Tutashughulika na somo hili kwa kuchambua misingi saba inayoelezea mchakato wa kukua kiroho.

II. Kuamini:

(1) Hakuna kukua bila kuwako na imani:

Lakini Neno walilolisikia halikuwafaidia lolote, kwani halikuchanganywa na imani ndani ya mioyo yao, japokuwa walilisikia – Waebr. 4:2.

Kusoma tu Biblia na kusikiliza mafundisho ya Biblia havitoshi kuleta matokeo ya kukua kiroho. Bila ya Neno la Mungu “kuchanganywa na imani” ndani ya mioyo yetu, basi kupata tu elimu “hakutatuadilisha” - Waefe. 4:16. Ili kukua tunahitaji zaidi ya hayo. Tunahitaji imani. Kukua halisi kiroho kunahitaji kupokea mafundisho ya Neno la Mungu, na pia kuamini unachofundishwa.

Kulifanya Neno la Mungu kuwa sehemu ya “mtaji” uliohifadhiwa katika bohari ya mioyo yetu kunatulazimu kuichukua kweli yake yote yenye thamani kuu na kuiweka katika mioyo yetu bila ubishi wala kipingamizi, kwani bila kuyaamini mafundisho ya Biblia, hatutaweza kuiegemean kweli iliyomo ndani yake katika wakati wa magumu na majaribu; tutakuwa tumejenga nyumba yetu ya kiroho “kwenye mchanga” - Mathayo 7:24-27. Ni kwa kuiamini tu ndipo msingi wa kweli ya Biblia unakuwa sehemu ya maisha yetu; ni kwa kuamini tu ndipo chembechembe za elimu itokayo kwa Mungu zinakuwa zenye kueleweka na zinaweza kutumiwa nasi; ni kwa kuamini ujumbe wa Mungu ndipo matofali ya ujumbe huo yanaanza kujenga msingi imara ndani ya roho zetu, msingi utakaoweza kuhimili mashambulizi ya kila siku ya dunia, ya tamaa za miili yetu, na mashambulizi ya Shetani – 1Petro 5:8-9. Ili “kupigana ile vita njema” ya maisha ya Kikristo tunahitaji silaha sahihi ndani ya mioyo yetu: kweli ya Neno la Mungu iliyoshikiliwa imara ndani ya mioyo yetu kwa imani.

(2) Imani maana yake ni kumtumaini Mungu:

Sasa, Abrahamu alimtumainia Mungu, naye Bwana akamhesabia uongofu kwa sababu hiyo – Mwanzo 15:6.

Ili imani iwe na maana yoyote, inapaswa kuwa na kitu cha maana cha kuaminiwa. Kuanza maisha ya Kikristo, maisha ya imani, Mlengwa wa maana wa imani yetu, wa tumaini letu, ni Bwana Yesu Kristo (Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokolewa – Matendo 16:31). Imani inaanza na tendo hilo dogo la utegemezi kwa Mungu. Mungu anatuahidi uzima wa milele ikiwa tunamkubali na tunampokea Mwana wake, Yesu Kristo. Nasi kwa upande wetu tunamwamini au tunaweka tumaini letu au imani yetu kwa Bwana Yesu. Tumaini letu kwa Mungu na ahadi yake kwetu ndiyo imani inayotuokoa kwa neema ya Mungu (Waefe. 2:8-9).

Kama ilivyokuwa wakati tunaokolewa, ndivyo pia ilivyo katika mchakato wa kukua kiroho, ila kuna tofauti moja tu. Tunaingia katika familia ya Mungu katika namna ya kufumba na kufumbua jicho kupitia tendo moja rahisi la kumtumainia Mwana wa Mungu. Lakini kuendelea kiroho, ile punje ndogo ya haradali, imani yetu ya mwanzo kabisa, inapaswa kuendelea kukua wakati Mungu akiinyweshea na kupogoa matawi yake wakati wote wa maisha ya muumini hapa duniani. Majaribu ya maisha yetu yanapokuja kwa kasi kubwa, tunapaswa kuwa tayari kuitumia imani yetu kuyakabili katika imani ileile kama tuliyokuwa nayo pale tulipomwamini Bwana Yesu kuwa Mwokozi wetu. Tunapaswa kuwa tayari kupambana na mishale hii ya moto kwa kuitumia ngao yetu ya imani -Waefe. 6:16. Kwa ufupi, tunapaswa kuwa tayari kutumainia ahadi za Mungu na hulka ya Mungu ambayo inatupa uhakika wa utimizi wa ahadi hizo.

Kukua kiroho ni, awali ya yote na kimsingi, kukua kwa imani yetu, kujengeka kwa uhusiano wa matumaini kati yetu na [kuelekea kwa] Mungu. Katika mahusiano yetu na watu wengine, tunajifunza kuhusu uaminifu wa wenzetu kutokana na mazoea ya kuishi nao. Tunajifunza kuhusu hulka yao kwa kusikia wanayoyasema na kuona wanayoyafanya. Katika maisha yetu ya Kikristo, tunahusiana na Yeye ambaye hulka Yake timilifu inastahili kutumainiwa. Kulielewa jambo hili kwa uhakika kunahitaji “kumfahamu Mungu” katika namna moja tu aliyoiweka: kulisoma na kujifunza Neno lake takatifu kila siku kwa bidii, na kuitumia kweli iliyomo ndani ya Biblia katika maisha yetu ya kila siku Yohana – 17:17. Ni kutokana na Biblia ndivyo tunajifunza juu Yake siku hadi siku, ndivyo tunauona uaminifu Wake kwa waumini wa kale na kuziona ahadi zake alizozitoa kwetu sisi waumini wa leo. Katika kila sura, katika kila aya, tunaisikia sauti kuu ya neema za Mungu ikizungumza nasi.

Kujifunza kumtumaini Mungu si rahisi wakati wote – hasa tunapokabiliwa na hali ngumu ambapo inaonekana kuwa hakuna matumaini ya kuepuka kuharibikiwa. Lakini tunapaswa kukumbuka mfano wa Abrahamu, muumini ambaye alikuwa na migogoro yake ya kiroho pia – mfano Mwanzo 12:9-20 – lakini licha ya hayo, alikaza moyo katika kukua kiroho akizitumia fursa alizopatiwa kwa faida ya kumfahamu Mungu zaidi na zaidi. Imani yake ilikua kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba hata pale Mungu alipomwambia amtoe sadaka mwanaye wa pekee [wa ahadi], alikuwa na imani, alikuwa na ufahamu wa kutosha wa hulka ya Mungu, akijua kutokana na imani hiyo kwamba aliweza, kwa utulivu kabisa, kumwamini Mungu hata kama atatakiwa kufanya kitu kigumu namna hiyo kukielewa, achilia mbali kukitenda – Waebr. 11:17-19. Imani maana yake ni kumtumainia, kumwamini Mungu, lakini tumaini hilo limejengwa juu ya mwamba imara wa ufahamu (msingi wake ni mafundisho ya Biblia na pia kupitia matukio mengi ya mitihani migumu ambamo Mungu amekuvusha kwa usalama) kiasi kwamba tumaini hilo lina msingi imara, kwamba kwa hakika tunaweza kumtegemea, na kwamba kumtumaini Yeye ndio uamuzi wa maana zaidi, hata kama mazingira yanayozunguka mitihani hiyo ya maisha yanakufanya ufikiri kwamba hakuna matumaini yoyote.

(3) Imani inatataka tuelekeze macho yetu kwa Mlengwa wetu bila kutetereka:

… ebu na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu, tukielekeza macho yetu kwa Bwana Yesu, mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu - Waebr. 12:1b-2.

Wakati tunaokolewa, tulimwamini Bwana Yesu Kristo kwa ahadi ya uzima wa milele. Kwa kuwa sasa sisi ni Wakristo, tunapaswa kuendelea na zoezi la imani hii kila siku – kwa hakika kukua kwetu kiroho kunategemea jambo hili. Tunavyosonga mbele katika maisha yetu ya Kikristo, lengo letu siyo tu kuendelea na imani yetu katika Kristo, bali ni kuipa nguvu imani yetu hii kulingana na jinsi tunavyojifunza kuwa wanafunzi Wake siku hadi siku kila wakati tunapomtumaini, kila wakati tunapoamini aliyoyasema, imani yetu inakuwa na nguvu zaidi. Hii ndiyo maana vipindi vigumu vya maisha yetu vinaweza kuwa ndivyo vyenye thamani na faida kubwa kiroho. Hali ngumu ya maisha angalau ina faida ya kutufanya tuelekeze macho yetu kwa Mungu na msaada Wake ambao upo wakati wote.

Ikiwa tunamtumainia wakati tunamhitaji sana, yaani wakati tukiwa na magumu, na tunapoona msaada Wake na huruma Yake, ni dhahiri pia kwamba baada ya mtihani huo kupita tunapaswa kuendelea na tumaini hilo na imani hiyo pia. Lakini katika maisha, mara nyingi kinyume chake ndiyo hutokea. Inaonekana kuwa ni silika ya wanadamu kwamba katika nyakati za neema tuna tabia ya kusahau ule ushupavu wa tabia na imani tuliouonyesha wakati tulipokuwa na magumu – Waebrania 10:32-29. Kwa kweli kuweka tumaini letu kwake Bwana Yesu Kristo wakati wote ni ufunguo wa kukua kiroho, kwani kufahamu hilo kunatusaidia kuwa na mtazamo sahihi kuhusu vivutio/vishawishi na hatari za ulimwengu huu – Waebr. 11:26-27.

Ili “tupige mbio kwa saburi katika mashindano yaliyoko mbele yetu” tunahitaji kila siku “kugeuza macho yetu yamwelekee Bwana Yesu, “mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu” (Waebr. 12:1b-2). Neno “geuza” hapa ni Kiyunani aphorao, neno-tenzi au kitenzi ambacho maana yake ni kuondoa mwelekeo wa mawazo kutoka mambo mengine yote na kuelekeza mawazo hayo kwa kitu kimoja tu. Ii imani yetu ikue na kufanikisha suala hili muhimu la kuelekeza fikra zetu zote kwa Bwana Yesu, Mungu anailea imani hii, anaipalilia na kuinyweshea, anaipogolea ili kuifanya ikue na izae – Yoh. 15:2. Imani inahitaji misingi yote hii miwili ili ikue. “Kulishwa” na Neno la Mungu kunaipa imani yetu uelewa wa wazi zaidi wa Mungu wetu aliyetuahidi mengi, na “kupogolewa” kwa kupitia majaribu na mitihani ya maisha kwa kila wakati kunasaidia kuyabadilisha mafunzo tunayopata kutoka kwenye Neno la Mungu na yanakuwa busara yenye [kutuwezesha] kustahamili. Hivyo imani yetu inajenga “misuli” ambayo tunaweza kuitumia wakati wa shida.

Kukua kwetu, kufanikiwa kwetu katika maisha ya Kikristo, kunategemea jinsi tunavyoelekeza akili yetu yote kwa Mwana wa Mungu, Bwana Yesu Kristo, na kwa ujumbe anaotupatia. Kama tunavyoambiwa katika Waebr. 1:2, Mungu “katika siku hizi za mwisho amesema nasi kwa njia ya Mwanaye”. Kupitia kutwaa kwake mwili na kazi yake msalabani, kwa mkono wa manabii na mitume wake, Kristo ametupatia sisi, Kanisa lake, “njia ya kumwona japo Yeye haonekani” - Waebr. 11:27, na njia ya “kumpenda japo hatumwoni” - Petro 1:8. Ametupatia Neno lake takatifu.

(4) Ni mafundisho yaliyopokelewa kwa imani tu ndiyo yanayoweza kutumiwa kwa imani:

Kwa yeyote mwenye nia ya kumkaribia Mungu, yampasa kuamini kwamba Yuko, na kwamba atawapa thawabu wale wanaomtafuta kwa bidii – Waebr. 11:6.

Kukua kiroho kunawezekana tu ikiwa tunapata “chakula cha kiroho”, na ni kwa msingi huu ndio Petro anatuasa “tuyatamani maziwa ya kiroho yasiyoghoshiwa (kweli isiyo na hila) ili kwa hayo tupate kukua kuelekea wokovu” - 1Petro 2:2. Lakini haitoshi kusoma tu Neno la Mungu. Ili ile kweli tunayoipata kutokana na kusoma Biblia na kufundishwa Biblia iwe na faida kwetu, tunapaswa kuiamini. Vinginevyo, tunakuwa kama yule mtu katika Waraka wa Yakobo ambaye alitazama kioo, akaondoka, na mara akasahau taswira yake mwenyewe – Yak. 1:22-25. Kitu kama hicho kiliwatokea waumini wa Korinto ambao walifundishwa na mtume Paulo mwenyewe kuhusu kanuni ya ufufuko wa wafu, lakini walitilia shaka kile walichofundishwa. Matokeo yake, hawakuwa tayari kwa mitihani na mafundisho ya uwongo yaliyokuja baadaye (kwa mfano wangeiweka imani yao mashakani katika tukio la kifo cha mtu aliyependwa katika jamii yao) na kwa kweli mtume Paulo alisema nao kwa ukali – 1Wakor. 15:12-19.

Vivyo hivyo, tunaposikia kanuni ya kweli, lakini tukawa na mashaka nayo na hivyo hatuiamini, kanuni hiyo haitakuwa na faida kwetu wakati wa shida hata kama tutaikumbuka wakati huo. Kanuni ambayo hatuiamini haiwezi kuwa chanzo cha faraja kwetu. Imani yetu ni lazima iwe na kitu fulani cha kutegemea wakati wa magumu. Imani yetu inapaswa kuimarishwa na kanuni za kweli katika mioyo yetu. Imani ya kweli inapaswa kuelekezwa kwa Kristo, lakini pia inapaswa kuwa imeimarika katika kweli ambayo Yeye ametupatia kama “petroli” ndani ya tanki la gari letu la imani, gari ambalo linatuwezesha kusafiri kwa usalama katika safari yetu ya maisha. Kutoamini misingi ya kweli iliyomo ndani ya Biblia ni sawa tu na hatari ya kushindwa kuitafuta misingi [ya kweli] hiyo, na kwa mtaji huu, haraka sana tutaona tanki letu la “petroli” ya imani limeisha na safari yetu kusimama ghafla!

(5) Imani ya kweli chanzo chake ni Biblia tu (Eclectism SI sahihi):

Na kwa sababu hiyo tunamshukuru Mungu wakati wote, kwani mlipolipokea Neno kutoka kwetu, mlilipokea si kama maneno ya watu, bali kama lilivyo – Neno la Mungu – 1Wathess. 2:13.

Tatizo la kutoamini linafanana sana na lile tatizo jingine la “kuchagua” kanuni za kuziamini kutoka katika Biblia na kuziacha zingine. Tofauti ndogo iliyoko katika hali hizi mbili “gonjwa” za kiroho ni kwamba kutoamini kabisa ni tendo la wazi la uasi ambapo mtu anaamua kuikataa kweli ya Mungu kwa sababu mbalimbali binafsi zisizokuwa za kweli. Kuchagua kuamini kanuni fulani za Biblia na kuacha zingine kwa upande mwingine, ni kujidanganya mwenyewe, na siyo uasi. Tunaweza kutumia mfano wa jinsi Paulo alivyowasifia Watesalonike kwa kuyapokea mafundisho yake ya Biblia kwa imani, na vile alivyowahukumu Wakorinto kwa kuyaacha kwa urahisi sana mafundisho yake baada ya kupata mafundisho mapya ya uwongo – 2Wakor. 11:4. Tukiwa kama waumini, pamoja na mashaka ya dunia ya sasa tunayopaswa kuyakabili, ukichanganya na Ukristo wa sasa wenye sura na taswira nyingi unazoweza kuchagua, kuna hatari kwamba tunaweza kuamua “kubadilisha”, japo kidogo, kutoaminika kwa ujumbe wa Biblia wa aina nyingi [za Ukristo wa sasa] unaotuzunguka, (hivyo nasi kujiingiza kwenye “mchezo” uleule wa hatari). Lakini tukijifanya sisi wenyewe kuwa ndio waamuzi/wasimamizi (ma-refarii) wa mwisho wa mafundisho tunayopokea, kuna hatari ya kuyakuza mashaka madogo madogo tuliyo nayo mpaka yakawa makubwa nasi kubaki kutokuwa na uhakika na kitu chochote. Akili ya kawaida tu inapaswa kutuonyesha hatari ya kujiona sisi wenyewe kuwa tuna mamlaka ya pekee na ya mwisho katika kupambanua na kuamua ukweli wa fundisho/kanuni fulani.

Kwanza, ni kwa makusudi ya kuasisi na kuimarisha imani yetu ndiyo Mungu wetu amegawa vipaji kati yetu ambavyo vinatuwezesha kutoa huduma ya Neno – Waefe. 4:11-16. Kwa uhakika, jinsi kulivyo na makundi (kalti/cults) na waalimu wengi wa uwongo, tunahitaji kuwa na tahadhari kubwa kuhusu nani na ni nini cha kuamini, kabla ya kuwa na ushirika na kikundi chochote au kuingia katika kanisa fulani, na kufuata mafundisho yake. Maandiko yanatuasa waziwazi kufanya hivyo – 1Yoh. 4:1. Lakini kama tuna uhakika na kanisa au utumishi/mtumishi fulani kutokana na mtazamo wa kukua kiroho, ni vizuri zaidi tukishiriki kwa imani mara baada ya kujihakikishia ukweli wa mafundisho yake. Licha ya kuiweka imani yetu matatani, kuchagua kanuni za kuamini na kuacha zingine kuna hasara ya ziada ya kuhujumu “nyumba ya kiroho” ya mafundisho ya Biblia tunayoendelea kuijenga siku hadi siku – Waefe. 2:19-22. Biblia imesheheni kanuni, misingi, mafundisho tele – yote yakiwa, kila moja kipekee, muhimu kujifunza. Matumizi ya kila “tofali” moja (yaani kanuni) katika mjengo wa nyumba ya kiroho tunayoendelea kuijenga ndani yetu yanaweza kuwa si wazi kwetu hapo tunapoanza “ujenzi” wa mjengo huu wa kiroho. Hatuwezi kujua kipande fulani cha msingi tunaouweka kitakuwa na “faida” gani wakati ule tunapokiweka lakini tunapaswa kufahamu kwamba ni msingi imara, uliokamilika ndio inaoweza kuhimili mtihani wa tufani za maisha ya hapa duniani.

Tunaingia katika familia ya Mungu kwa imani ndogo kama mbegu ya haradali, na ni mpango wa Mungu kwetu sisi kwamba imani hii ndogo ikue mpaka iwe mti mkubwa unaotoa kivuli na makazi kwa ndege wa kila aina wa angani – Mathayo 13:31-32. Kukua kiroho kwa namna hiyo kunataka imani yetu inyooshe “mikono” yake na kuikumbatia misingi yote ya kweli iliyomo ndani ya Biblia mpaka inatengeneza [kitambaa imara cha] hulka imara ya kiroho, kama misuli na mifupa ya mwili wa mwanadamu inavyoshonana pamoja. Yote tunayojifunza kuhusu mpango wa Mungu, hata yale yatakayoonekana kuwa ni ya kawaida na yasiyo na umuhimu kwa wakati huo, yote haya yanachangia kujenga msingi ambao juu yake kukua kwetu kiroho kwa baadaye kunategemea. Kweli zilizomo ndani ya Biblia zinaungana na imani yetu, na kuunda “uti wa mgongo” wenye nguvu unaoweza kubeba mzigo wa mitihani inayotukabili katika maisha yetu kama Wakristo.

Zaidi ya hapo, mchakato huu unajirudia-rudia na kila mzunguko wa marudio unatia nguvu katika mzunguko uliopita mwanzo. Kila fundisho unalolielewa na kuliamini linaingia katika jedwali lililo kamili, linakuwa tofali katika ule msingi imara wa imani yako. Kukubali mafundisho ya Biblia kwa unyenyekevu ndiyo njia pekee ya kujenga “nyumba yako ya kiroho” unayoijenga juu ya MWAMBA ambapo itahimili tufani, mafuriko na upepo mkali wa maisha – Mathayo 7:24-29.

Roho Mtakatifu ndiye mwenzi wetu katika kujenga imani yetu:

2.12  Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. SUV

Kujifunza misingi ya kweli iliyo muhimu kwa makuzi yetu ya kiroho hakutegemei akili yetu au uwezo wetu wa kufikiri. Mungu amewapa Wakristo wote Roho wake Mtakatifu ili awasaidie katika shughuli muhimu ya kuweka/kujenga msingi wa kweli katika mioyo yetu ili tuweze kutambua na kuthamini yale mambo makuu ambayo Mungu amefanya kwa ajili yetu – 1Wakor. 2:12. Bila ya msaada wa Mungu katika jambo hili (likihudumiwa na Roho Mtakatifu ndani yetu), haitawezekana kujifunza kweli Yake kabisa, hata kama tuna I.Q. kubwa kiasi gani, kwani kweli ile itakuwa ni upuuzi kwetu – 1Wakor. 1:18. Siyo kwamba habari iliyomo ndani ya Biblia na misingi ya kweli iliyomo haiwezi kusomwa na kueleweka kwa maana ya kinadharia, lakini bila imani, na bila kufundishwa na Roho Mtakatifu, mafundisho ya Neno la Mungu hayaleti maana kwani hayatii mwanga ndani ya moyo na hayamletei msomaji wake kukua kiroho. Bila ya Roho Mtakatifu kufanya kazi pamoja na imani yetu, mafundisho ya Biblia yanaishia kwenye akili zetu tu, na siyo mioyo yetu, na tunakuwa kama mtu anayemsikia mwenzake “akinena lugha”: anayoyasema yanaweza kuwa mema na kweli, lakini hayana maana kwake na ‘hayamsaidii chochote’ - 1Wakor. 14:4.

Bila ya Roho Mtakatifu, “mtu hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanatathminiwa tu kwa jinsi ya rohoni” - 1Wakor. 2:14. Neno la Kiyunani lililotumika hapa na linalotafsiriwa kama “yanayotathminiwa” ni anakrino, maana yake “kuchunguza kwa makini”. Mtu anaweza kuyafahamu maandiko kwa undani, lakini bila ya kumulikiwa mwanga na Roho Mtakatifu, hataweza kupata uelewa wa kweli wa maana halisi na uelekezi wa maandiko hayo.

Sisi waumini kwa upande mwingine, “tuna akili ya Kristo”, Roho Mtakatifu, anayetusaidia – 1Wakor. 2:16. Kwa hivyo hatutegemei akili ya kibinadamu au waalimu wa kibinadamu katika kiu yetu ya kujua matakwa kamili ya Mungu - War. 12:2. Hakuna nafasi kwa majivuno wala kuvunjika moyo katika kutafuta kwetu kuijenga imani yetu kwa kujifunza Neno la Mungu kwani hatujifundishi sisi wenyewe, na hatumtegemei mwanadamu anayeweza kufanya makosa, bali tunaye Mwalimu wetu, ambaye ni Roho Mtakatifu – Yoh. 14:17,26; 1Wathess. 4:9; 1Yoh. 2:27.

(7) Imani ya kweli ni lazima izae matunda:

Kwani kama vile ambavyo mwili pasipo roho hufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa. - Yak. 2:26.

Aya hii kutoka katika kitabu cha Yakobo, kwa kiasi kikubwa haieleweki na wengi. Mara nyingi inaeleweka kama vile “tunapaswa kutenda matendo mema ili tufike mbinguni”. Kauli hiyo iko mbali kabisa na ukweli na maana halisi ya aya hii. Kanuni ya wokovu kwa neema pekee imeelezwa wazi kabisa katika Waefeso 2:8-10. Zaidi ya hapo, Paulo anasisitiza kwa uwazi kabisa katika muktadha (context) ule kwamba “wokovu [haupatikani] kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu” - aya ya 9. Sasa, “matendo” anayozungumzia Yakobo (ambayo bila hayo imani imekufa), ni yale yale yanayosemwa na Paulo katika Waefe. 2:10 ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa [ili] tupate kuishi katika hayo”.

Hivyo basi, hatupaswi kufikiria kwamba matendo mema ni kitu kinachopangwa na kufanywa nasi, bali tunajua katika uhalisia wake: matendo mema ni fursa zilizotayarishwa na Mungu kwa ajili yetu ili tuweze kuzitumia na kudhihirisha imani yetu. Na pia, hatupaswi kufanya kazi katika upweke katika jukumu hili la kuitumia imani yetu katika mazingira tunamoishi. Ili kusaidia katika kulifundisha kanisa la Kristo, Mungu ametupatia vipaji (kwa ajili ya kila mmoja wetu) ambavyo vinagawanywa na Roho Mtakatifu na kutiwa nguvu Naye – 1Wakor. 12:1-11. Hatuchagui uelekeo wa utumishi wetu kwa ajili ya Mungu katika maisha yetu. Hilo linafanywa na Mungu mwenyewe. Ni wajibu wetu kukua kiroho mpaka tunafikia kiwango ambapo vipaji tulivyopewa vinakuwa wazi na dhahiri na ambapo tunakuwa tumepevuka kwa kiasi ambacho tunaweza kutumia vipaji hivyo kwa ufanisi. Kanuni hii ya vipaji vya kiroho tunavyopewa na Mungu ili viwe ndio msingi wa utumishi wetu wa Kikristo, siyo tu kwamba inaondoa sababu zote za kujisifu na majivuno kutokana na kazi njema tutakazofanya, lakini pia inatuhakikishia kwamba Mungu ndiye anayedhibiti asili/hulka, uwezo na uelekeo wa utumishi wetu Kwake katika maisha yetu hapa duniani – 1Wakor. 12:4,11.

“Tendo jema” lililofanywa na Abrahamu ambalo linathibitisha kwamba imani yake ilikuwa hai halikuwa tendo la msaada (charity) kwa mtu yeyote, bali lilikuwa tendo la imani kuu na utiifu kwa Mungu – Yako. 2:21-22. Abrahamu alimtukuza Mungu kwa kazi/tendo lake la imani, na kutukuza huku ndilo lengo kuu la vipaji vya kiroho, utumishi wa Mkristo na matendo yote mema ambayo sisi kama Wakristo tunapaswa kuyakamilisha ili kuhalalisha imani yetu – Isa. 43:7; 1Pet. 4:10-11. Ni kwa kupitia imani yetu iliyo hai na yenye nguvu ndipo mwanga ulio ndani yetu unang’ara katikati ya ulimwengu wenye giza, ukimtukuza Mungu, ukiwavutia watu waje kwenye upendo Wake, na kuwathibitishia watu wote waone kwamba tunaposema kwamba tunamwamini Bwana Yesu Kristo na Neno Lake, tunamaanisha hivyo kikwelikweli – Mathayo 5:15-16.

=0=

Translated From: Faith and Spiritual Growth: Peter’s Epistles #14

=0=

Basi, na tuonane katika sehemu #15 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!