Utakaso: Nyaraka za Mtume Petro #13
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili Imefanywa na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission For This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

Mapitio: Tulipokuwa tunajadili fundisho-fumbo la mpanzi (Mathayo 13:1-9; Marko 4: 1-9; Luka 8:4-8), tulijifunza aina tatu za “udongo mbaya”. Aina hizi, tuliona, ni aina tatu za watu ambao mtazamo wao kwa Mungu na Mpango wake kwao ni hasi kiasi kwamba makuzi yao ya kiroho yanaathirika. Aina hizi tatu za matatizo ya imani ambazo zinazungumzwa katika fundisho-fumbo hili maarifu ni:

(1) Kukosekana kwa imani kabisa: Kristo na Injili yake vinakataliwa moja kwa moja na moyo mgumu ambao hauruhusu Neno la Mungu kuingia kabisa.

(2) Kupotea kwa imani: Gharama inpoonekana kuwa kubwa, Kristo na Injili yake wanatelekezwa na moyo wenye mawe ambao hauruhusu Neno la Mungu kuingia kiasi cha kutosha na kuota mizizi.

(3) Kubanwa kwa imani: Magumu na tamaa za ulimwengu huu vinapewa kipaumbele, Kristo na Injili yake wanawekwa pembeni na moyo wenye miiba ambao hauruhusu Neno la Mungu kustawi na kuzaa.

“Mbegu” inayopandwa mioyoni mwetu ni Neno la Mungu – Luka 8:11, na usikuvu, uwajibikaji, itikio na utiifu kwa Neno hilo ndivyo vinavyosababisha kukua kwa “mmea wa imani”. Imani ya aina hii inastawi tu katika “udongo mzuri”, yaani katika mioyo ya waumini wanaojizatiti kufuata Mpango wa Mungu kwa ajili ya maisha yao – 1Petro 1:7.

Masta Plani ya Mungu: Mungu anatupenda kwa upendo mkuu hata akamtoa Mwanaye mpendwa awe dhabihu kwa ajili yetu, ili kwa kumwamini Mwanaye huyo tusijekufa na kuhukumiwa milele, bali tuweze kuishi milele pamoja Naye – Yoh. 3:16. Ili tuweze kufaidika na ahadi hii ya uzima wa milele wa bure kutoka kwa Mungu, tunapaswa kufuata matakwa yake, ambayo, kimsingi yapo katika hatua tatu:

• (1) Tunapaswa, kwanza na kabla ya yote, kuweka imani na mategemeo yetu kwa mwanaye, na hivyo kuwa waumini wa Bwana Yesu Kristo.

• (2) Mara baada ya kuamini, Mpango wa Mungu unatuamuru tuwe wafuasi wa Kristo katika muda wote uliobakia wa maisha yetu hapa duniani.

• (3) Mwisho wa maisha yetu ya hapa duniani, Mungu ametutayarishia maisha ya shani na furaha milele.

Kwa sisi ambao tumekwishakuwa Wakristo, sehemu ya kwanza (wokovu) imekwisha fanikishwa, na sehemu ya tatu (milele), bado haijafika, ikingojea wakati aliopanga Mungu. Suala lililoko mbele yetu sasa ni namna ya kuwa wafuasi wazuri wa Bwana wetu tukingali hapa duniani, namna mwafaka ya kuelekeza nguvu zetu na akili zetu kwa sehemu ya pili ya mpango mkuu wa Mungu kwa maisha yetu.

Utakaso, lengo la Mpango wa Mungu: Katika kila moja kati ya hatua za mpango wa Mungu, lengo lake ni sisi tuwe “watakatifu” kama Yeye alivyo mtakatifu (1Petro 1:16; Walawi 11:44-45). Mchakato unaotuwezesha “kuwa watakatifu” katika kila awamu ya Mpango wa Mungu unaitwa utakaso - Yohana 17:17,19. “Kutakasa” (kwa Kiyunani hagiazo: άγιάζω) maana yake “kutukuza”, yaani kutoa kitu/mtu (yaani kututoa sisi) katika himaya ya kidunia/kilimwengu na kukihamishia au kumhamishia katika himaya ya Ki-Mungu (kumbuka, Shetani ndiye ‘mfalme’ wa dunia hii). Utakaso ni njia ambayo Mungu anaitumia kutubadilisha ili kuwa watu wanaostahili kuishi Naye na Mwanaye milele. Katika kila hatua ya Mpango wake, Mungu anatusafisha. Katika sehemu ya kwanza (tukio la wokovu), Anaondoa jina la kila mmoja wetu kutoka katika orodha ya mashitaka iliyoko mbinguni – Wakolosai 2:14. Katika awamu ya tatu (milele), Anatupatia mwili mpya (Wakor. 5:1-10) ili tuwe huru kutokana na hulka ya dhambi iliyo katika miili yetu ya sasa (War. 7:17). Katika sehemu ya pili (majira ya wokovu), Mungu Anatupatia fursa na wajibu wa kujibadilisha wenyewe (kwa uweza Wake na neema Zake) kuwa watu wanaoakisi, wanaodhihirisha, utukufu Wake na huruma Yake (War. 12:2; 2Wakor. 3:18; Waefe. 4:22-24).

1. Utakaso [wa Mwanzo] Katika Kristo: Tulipoamini katika Kristo, “tulitakaswa” (1Wakor. 6:11). Hii ina maana, tunaweza kusema, kwamba katika kitabu cha Mungu majina yetu yalihamishwa kutoka katika orodha ya “kidunia” na kuwekwa katika orodha ya “utakatifu”. Kuanzia dakika ile tulipokuwa Wa-Kristo, Mungu hatutizami tena kama wenye dhambi, walengwa wa ghadhabu Yake (War. 1:18), bali walengwa wa upendo Wake (War. 8:39). Hapo Mungu anatutangaza rasmi kuwa “watakatifu”. Kitendo hiki cha utakaso wetu hata kidogo hakihatarishi hulka yake ya Uungu: Bwana Yesu Kristo amelipia gharama yote ya utakaso wetu kwa kifo chake msalabani. Kumbuka pia kwamba fadhila hii mpya tunayopewa hatuipati kutokana na juhudi yoyote kwa upande wetu, la hasha. Tabia tuliyokuwa nayo kabla hatujaokolewa haina athari kabisa kwa hadhi yetu mpya ya “utakatifu” ya sasa, kwa sababu tunaupata huu utakaso wa mwanzo, tunaweza kuuita utakaso “shirikishi”, kwa msingi wa kazi aliyoifanya Bwana Yesu pekee. Tunashirikishwa Naye katika hadhi yake ya utakatifu. Kwa kujiweka katika kundi la Kristo na kujitambulisha Naye, kwa kuipokea na kuikubali kazi aliyoifanya kwa niaba yetu, tunapokea mafao ya “kufanywa watakatifu” mbele za Mungu bila kufanya kazi yoyote au kustahili kwa namna yoyote.

2. Utakaso [katika] Milele: Hii awamu ya mwisho ya utakaso nayo pia ni kazi ya Mungu pekee. Tunapoondoka katika maisha ya hapa duniani, tunaingia katika milele “isiyo na huzuni, machozi au suluba” - Ufu. 21:4. Tutakapofufuliwa, miili yetu itabadilishwa na kuwa miili mipya, inayoishi milele, bila uharibifu, na hivyo tutakuwa watakatifu kweli kweli, na tutaitwa watakatifu – Wafilipi 3:21. Kuanzia hapo hatutaweza kutenda dhambi tena na hatutotenda tena tendo la kutotii ambalo litachafua utakatifu wetu na kututenga na Mungu (Ufu. 21:27; 1Wakor. 15:35-57). Hivyo hapo mwanzoni tunapookolewa na hatimaye tunapofufuliwa, badiliko hili la kwenda kwenye hadhi mpya, takatifu (utakaso), hutokea kufumba-na-kufumbua na halihitaji kazi yoyote kwa upande wetu, kwani hii ni kazi ya Mungu pekee.

3. Utakaso Katika Majira ya Wokovu Duniani: Tumefanywa “watakatifu” (kwa tamko la haki, lisilo na upendeleo, la Mungu ambalo msingi wake ni kazi ya Kristo), na tutafanywa “watakatifu” (kwa kupewa mwili usio na dhambi katika ufufuo), na hivyo ni mapenzi ya Mungu kwamba sasa tuwe watakatifu katika maisha yetu ya hapa duniani (War. 6:19-22; Waefe. 5:26; 1Wathess. 4:3; Waebr. 12:14; 1Petro 1:15-16; 1Yoh. 3:3; Ufu. 22:11). Tulipookolewa na kuwa Wakristo, hatukubadilika mara moja na kuwa watimilifu. Tumekuja na hulka yetu ya dhambi na kasoro zake zote kwenye maisha yetu na Kristo – War. 7:17. Changamoto yetu kwa sasa kama Wakristo ni kubadilika. Tunaendelea kuishi hapa duniani baada ya kuokolewa ili tumtukuze Mungu kwa kufanikisha mabadiliko haya, mageuzi ya kushangaza kiasi cha kuufanya ulimwengu ushindwe kujizuia kuona utukufu wa Mungu ukidhihirika ndani yetu – 2Wakor. 3:18; Wafi. 2:15. Tuko hapa ili “kutimilisha utukufu” ambao Mungu aliuanzisha ndani yetu wakati wa wokovu wetu na ataukamilisha katika ‘wakati’ tunaouita milele:

7.1  Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza [tukitimilisha - perfecting] utakatifu katika kumcha Mungu - 2Wakor. 7:1 SUV

Kutakasa Mioyo Yetu: Ni nini basi maana ya “kuwa mtakatifu”, na tunafanikiwa vipi, tukingali wanadamu wenye dhambi, “kufanywa watakatifu?” Tutaanza zoezi hili kwanza kwa kutambua hali ya kutokuwa na utakatifu. Kwa mfano, kuonekana tu kwa watu wengine kama vile u mtakatifu hakumaanishi utakatifu wa kweli. Bwana Yesu aliwafananisha Wafarisayo na “makaburi yaliyopakwa chokaa”, kwa sababu walionekana wasafi na watakatifu kwa sura na matendo yao ya ibada, lakini ndani ya mioyo yao walikuwa wachafu na waliojaa uharibifu – Mathayo 23:27; cf 2Tim. 3:5. Kubadilisha tu namna tunavyovaa mavazi, namna tunavyozungumza, na namna tunavyoshirikiana na watu wengine haitoshi kututakasa mbele za macho ya Mungu (cf Wakolosai 2:23). Kwani mwonekano tu waweza kudanganya! “Tapeli”, hata mwenye uwezo mdogo tu, anaweza kujiunga na makanisa mengi na ndani ya wiki kadhaa akaonekana kuwa ni kondoo wa kiroho kwelikweli, wakati kiuhalisia amekuja kuwaibia mali zao. Mtume Paulo alitoa tahadhari kwetu dhidi ya wale wanaoonekana kuwa ni viongozi wa kiroho, lakini kiuhalisia ni watumishi wa Shetani. Si jambo la kustaajabu, alisema, kwamba watu wa namna hiyo wanaweza kujifanya kuwa ni “watumishi wenye uadilifu”, kwani hata Ibilisi anajionyesha kuwa ni “malaika wa nuru” - 2Wakor. 11:13-15.

Hivyo, japokuwa utakaso wa muumini utaongezeka kutokana na muda anaoishi hapa duniani kuongezeka, na hii kwa uhakika itabadilisha tabia na mwenendo wake sambamba na anavyojifunza Neno na kufaulu mitihani anayopewa na Mungu, kubadilisha tabia na mwenendo kwa nje tu, hata kama malengo yake ni mema, hakutafanikisha utakaso [halisi] – kwani hiyo ni kugeuza mchakato wa utakaso kuwa kichwa chini miguu juu! Utakaso halisi hufanyika tu kutoka ndani (moyoni) kwenda nje (katika mwenendo wa muumini). Ni kwa kubadilisha kiuhalisia mawazo yetu na nia zetu, matamanio mbalimbali ya mioyoni mwetu (siyo kwa kuonyesha ‘taswira’ ya utakatifu kwa faida ya watazamaji) ndio utakaso halisi unafanikishwa (2Wakor. 4:16; War. 6:4-11; 12:2). “Hulka ya mtu huonekana kwa kujua nia na fikra za moyoni mwake” - Mithali 23:7. Uwanja wa vita ya maisha ya Mkristo uko katika moyo wake – 2Wakor. 10:4-5. Ni kwa kusafisha mawazo na nia za mioyo yetu ndipo “sisi-wa-zamani” tutatoa nafasi ambayo itachukuliwa na “sisi-wapya” (Waefe. 4:22-24). Huyu “mtu mpya” anatokea kwa kuzifanya upya akili zetu kwa kutumia ufahamu wa kweli wa Mungu – Wakolosai 3:10-11, yaani kwa mchakato wa kukua kiroho.

Njia ya Utakaso: Njia pekee ya kufikia utakatifu katika maisha ya hapa duniani ni kukua kiroho. Mabadiliko halisi ya ndani tunayoyatafuta yanaweza tu kupatikana kwa kuunganisha imani yetu na Neno la Mungu – 2Petro 3:18. Kama ilivyo kweli kwamba sisi kama Wakristo tuko duniani lakini siyo wa dunia hii, vivyo hivyo tunapaswa kutumia njia za Mungu za kufanikisha utakaso, na siyo njia za ki-dunia. Bwana wetu hakuacha shaka yoyote kuhusu njia ya kweli ya kupata utakaso katika sala Yake ya usiku ule kabla hajasulibiwa ambapo alituombea sisi tupate utakaso: “Uwatakase kwa ile kweli. Neno lako ni kweli” - Yoh. 17:17-19. Hatuwezi kuwa watakatifu mbali na kweli yake iliyomo ndani ya Neno lake (Waefe. 5:26-27). Hatuwezi kuitumia kweli hiyo bila kuiamini na bila kuishi kutokana na misingi yake (Waebr. 4:2). Katika fundisho-fumbo la mpanzi, mahala pekee ambapo “mmea wa imani” uliweza kukua ni katika udongo wenye mbolea wa moyo uliokuwa tayari kuitikia wito wa Neno la Mungu. Mungu amekwishatupatia Neno lake. Njia ya utakaso kupitia kukua kiroho inapatikana kwa kila mmoja wetu kama tuko tayari kulisikia na kuishi kwa Neno lake.

Mchakato wa Kukua Kiroho: Kimsingi, mchakato wa kukua kiroho unaweza kuelezwa katika hatua nne. Ili muumini akue kiroho, anapaswa:

1. Kulisikia Neno la Mungu.
2. Kuliamini.
3. Kuishi kwa misingi ya Neno hilo.
4. Kuwasaidia wengine kufanya hivyo hivyo.

Japokuwa ni rahisi katika nadharia, mchakato wa kukua waweza kuwa mgumu katika utekelezaji wake, kwa sababu haujiwezeshi wenyewe. Kukua kunahitaji kwanza ridhaa ya nafsi zetu. Utashi wetu ni lazima uhusishwe katika mchakato huo. Hata kama nia yetu ni njema, hiyo haitoshi katika kutimiza hatua zote nne kikamilifu na kwa makini. Udhaifu wetu wa kibinadamu (Mathayo 26:11), misongo ya duniani (1Yoh. 2:15-17;Luka 8:4), na ukinzani wa kila wakati wa Shetani (Waefe. 6:11-12; Ayubu 1:6-11) hushirikiana pamoja kupinga hatua zozote chanya tunazofanikisha. Hata hivyo, maandiko yanatuhakikishia kwamba tunapofanya juhudi za kwenda mbele katika Mpango ambao Mungu ametupangia, Yeye anatusaidia kwa kila namna, kutoka katika “nia” yetu ya kufanya hivyo mpaka katika utekelezaji wake (Wafi. 2:13).

Ulazima wa Kukua Kiroho: Hakuna mbadala wa kukua kiroho. Katika maisha ya Kikristo haiwezekani kusimama, ni lazima usonge mbele, kwani ni hatari kwako kusimama. Mwandishi wa Barua kwa Waebrania anatupa tahadhari kwa jambo hili pale anapotuambia kuhusu hatari ya “kuacha [kuupoteza] wokovu wetu” - Waebr. 2:1-4. Kwa Mkristo kuna njia mbili tu: kukua na kupevuka au kuporomoka na [yawezekana] kuanguka. Ule “mmea” wetu wa imani” utatunzwa na kustawi tu kwa kuutafuta utakaso kwa bidii yote – Wakol. 1:22-23; Waebr. 12:14. Ni Neno la Mungu pekee “linapopandwa” katika mioyo yetu ndipo mioyo hiyo inakuwa salama. Hivyo basi …

• Tunapaswa kuwa na tahadhari tukingali katika himaya hii ya Ibilisi (Mathayo 24:42; 1Wathes. 5:6).
• Tunapaswa kuujenga wokovu wetu (Filemoni 2:12; 2Petro 1:10).
• Tunapaswa kulisukuma mbele gurudumu la kukua kiroho (Waebr. 10:39).

Kiini cha Kukua Kiroho: Njia pekee ya kukamilisha Mpango wa Mungu wa utakaso ni kwa kukua kiroho. Kukua kiroho, ambayo ni mabadiliko ya moyoni ya Mkristo yanayotokea kwa kujifunza na kuishi kwa misingi ya Neno la Mungu, kunaelezwa katika namna kadhaa katika Biblia, lakini wakati wote maelezo hayo yanalenga kwenye utashi wetu. Tunapaswa kuwa tayari kubadilika katika njia au namna aliyoipanga Mungu. Biblia inatumia analojia (mifananisho) kadhaa katika kuieleza na kuifundisha kanuni ya kukua kiroho, ikifananisha mchakato wa kukua kiroho na, pamoja na vitu vingine:

a. MTU ANAYEKUA: “2.2  Kama watoto wachanga [waliozaliwa sasa] yatamanini maziwa yasiyoghoshiwa [ya kiroho], ili kwa hayo mpate kukua katika wokovu [wenu]” - 1Peter 2:2 SUV
b. MMEA UNAOKUA: “3.6  Mimi nilipanda, Apolo akamwagilia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu.” - 1Wakor. 3:6 SUV
c. RIADHA: “9.24  Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate [tuzo].
9.25  Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote [anayoyatamani]; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo [hatimaye]; bali sisi [twashindana ili] tupokee taji isiyoharibika. - Wakor. 9:24-25 SUV
d. KUVAA VAZI LA KUJIHAMI WAKATI WA VITA: 6.11  Vaeni [kinga zote dhidi ya] silaha [za Shetani], mlizopewa na Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. - Waefe. 6:11SUV
e. KUJENGA JENGO: 20.32 Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. - Matendo 20:32 SUV
f. KUTIMILISHA MWENDO WETU WA KIKRISTO: 1.10  mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu [mafundisho ya Biblia]; - Wakol. 1:10 SUV
g. KUONGEZA UTHABITI (UIMARA) WETU: 3.13  apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote. - Wathes. 3:13 SUV
h. KUELEKEA KWENYE UTIMILIFU AU KUPEVUKA: 6.1  Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza [ya awali] ya Kristo, tukaze mwendo [tuendelee na mafundisho ya kanuni za juu zaidi] ili tuufikilie utimilifu [kupevuka kiroho]; - Waebr. 6:1 SUV
i. KUONGEZEKA NGUVU: 6.10  Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake – Waefe. 6:10 SUV
j. KUWA WATU WA KIROHO ZAIDI: 5.18  Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi [ambao unafuja tabia njema uliyokuwa nayo awali]; bali mjazwe Roho (na muendelee katika Yeye ambaye ndiyo njia ya kelekea kukua kiroho) - Waefe. 5:18 SUV
k. KUWA KARIBU ZAIDI NA MUNGU: 4.8  Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. - Yakobo 4:8a SUV
l. KUFANYA MABADILIKO YA KIROHO: 12.2  Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. - War. 12:2 SUV

Aya hizi na nyinginezo zinatilia mkazo sura au pande tofauti za mchakato wa kukua kiroho zikitumia mifano mbalimbali. Hata hivyo, kuna dhana moja ambayo inaonekana katika kila mfano, nayo ni kwamba mifano yote hapo juu inatia mkazo kwamba waumini wanapaswa kubadilika kwa uwezo wa Mungu ulio dhahiri katika Neno Lake. Tukiwa Wakristo tunaoishi katika himaya ya Ibilisi, “ajira yetu ya wakati wote” ni kukua kiroho, kubadilika kiroho, utakaso wa kila taswira ya maisha yetu.

Kwa mara nyingine tena, hatua nne zitakazotuwezesha kukua kiroho ni (1) kulisikiliza na kujifunza Neno la Mungu (2) kuliamini (3) kuishi kulingana na unavyojifunza, na (4) kuwasaidia wengine kufanya vivyo hivyo. Ili kupevuka tunapaswa kuutafuta ukweli wa Biblia, kuuingiza ndani ya mioyo yetu kikamilifu, tuutumie katika maisha yetu, na kutoa mchango wetu kulingana na vipaji alivyotupatia Mungu kulisaidia Kanisa la Kristo katika mchakato huu muhimu.

I. Kusikia: Tunapoanza kujifunza njia/mbinu za kukua, tusisahau pia umuhimu wa jukumu hilo. Kupevuka ndiyo njia pekee ya kuilinda, kuitunza na kuijenga imani yetu, njia pekee ya kuwa wazalishaji wa matunda na watumishi halisi wa Mungu, na njia pekee ya kuhakikisha tunapata thawabu tele za milele. Ni muhimu sana, basi, kwetu sisi, kutafuta chakula muhimu kinachowezesha kukua huko, yaani ile kweli iliyomo ndani ya Neno la Mungu!

Jikoni: “Jiko” la Mungu ni Biblia, ikiwa imesheheni kila aina ya chakula cha msingi ambacho ni muhimu kwa ajili ya makuzi ya kiroho. Kweli yote tunayoihitaji ili kukua hata tufikie kupevuka iko ndani ya Biblia. Ugumu uko katika kuitoa ile kweli na kuiweka katika mfumo unaoeleweka. Kwa kweli tunaweza kupata faraja tele kwa kusoma Biblia zetu sisi wenyewe, na kila Mkristo ana wajibu wa kusoma Biblia yeye mwenyewe kila wakati. Kama sala, kuisoma Biblia na kutafakari mafundisho yake ni sehemu ya lazima katika kupevuka kiroho kwa Mkristo. Lakini Mkristo huyu asifanye kosa la kufikiria kwamba kusoma Biblia kwa namna hii kunatosheleza. Kusoma Biblia ni muhimu katika kukua kiroho, lakini siyo mbadala wa mafundisho. Tukiendeleza mfano wetu wa JIKONI, ebu fikiria umeenda jikoni ili kupata mkate halafu unakuta hakuna mkate bali kuna unga wa ngano tu! Katika namna hiyo hiyo, Biblia imesheheni kiasi kikubwa cha ukweli, lakini sehemu kubwa ya kweli hii iko katika mfumo wa “unga”, siyo katika mfumo wa “mkate” uliopikwa tayari kwa kuliwa mara moja. Roho Mtakatifu amewapatia baadhi ya watu katika Mwili wa Kristo na vipaji vya kufundisha kwa malengo ya kuutoa katika maandiko ukweli ulio katika mfumo wa “chakula kilicho tayari kuliwa” (ukipenda chakula cha kiroho; cf. Waefe. 4:11-16). Ili kukua kiroho kwa kiwango cha juu, na pia kujilinda dhidi ya tabia ya kufikia hitimisho zenye makosa na kanuni hatari za uwongo (kutokana na kusoma kwao Biblia), waalimu kama hao, wenye vipaji walivyopewa na Roho Mtakatifu, ni muhimu sana kuwa wametayarishwa na kufundishwa ipasavyo (katika lugha za Kiyunani cha kale, Kiebrania cha kale, teolojia, historia ya kale, historia ya Kanisa, n.k.), na ikiwa wanamfuata Bwana Yesu Kristo kikwelikweli. Hizi sifa za mwalimu nilizozitaja hapa ni muhimu sana, na zinampa muumini mtihani wa mtanziko (dilemma) wa kuchagua! Kwani sitakuwa mbali na ukweli nikisema kwamba kwa wakati huu, sehemu kubwa ya watu wanaojiita Wakristo wanafundishwa na walimu au madhehebu/makundi ambayo hayajapata matayarisho yanayostahiki, wenye malengo ya ki-binafsi au wanaofundisha uwongo mtupu. Lakini muumini halisi wa Bwana Yesu Kristo, kama kweli kweli ana kiu ya kutembea hatua kwa hatua na Mungu kupitia kukua kiroho, atastahamili (atang’ang’ana) katika kuitafuta ile kweli, na kwa neema ya Mungu, atampata mwalimu wa kweli ambaye hatapotea katika lile “jiko” wakati anaitafuta ile kweli ya kufundisha.

Ugumu wa kuelewa kila kitu katika Biblia pale unapoisoma kwa mara ya kwanza unapaswa kuiweka wazi haja/ulazima wa kuwa na walimu waliohitimu. Kwa mfano, nyaraka za Agano Jipya zilitumwa kwa Wakristo ambao walikwishapokea mafundisho ya uso kwa uso kutoka kwa mitume wa Bwana Yesu – 2Tim. 2:2; Matendo 20:7-12. Sababu inayozifanya barua/nyaraka hizi kuwa ngumu kuelewa (mara nyingi) ni kwamba ziliandikwa kwa watu ambao tayari walikuwa wamekwisha pata misingi ya Biblia, hivyo walikuwa wanakumbushwa tu. Sisi watu wa sasa, wa leo, ambao hatujapata mafundisho kama hayo kutoka kwa Mitume, na ambao tunaishi katika wakati tofauti, tuna utamaduni tofauti, lugha tofauti, si jambo rahisi kuelewa kanuni zote zinazofundishwa na nyaraka hizi. Kuna kiasi kikubwa cha fununu au dondoo kuhusu historia ya wakati wa uandishi wa nyaraka hizi ambacho ni muhimu na lazima kieleweke kabla. Tunapaswa kuelewa mazingira ambamo nyaraka hizi ziliandikwa (utamaduni wao, lugha walizoongea na elimu waliyokuwa wanafundishwa). Zaidi ya hapo, hatuwezi kutafuta maana ya maandiko kwa kutazama kitabu kimoja cha Biblia peke yake. Ukiwa ni ujumbe wa Mungu kwetu sisi (2Petro 1:20-21), kila kitabu cha Biblia ni sehemu muhimu ya Biblia nzima, na mafundisho yake yanaweza tu kueleweka kwa kuzisoma sehemu zake mbalimbali kama sehemu ya/za kitu kimoja kikuu katika ujumla wake (jukumu ambalo si dogo kufanikishwa na mtu mmoja, hata kama akifanya hivyo maisha yake yote).

Tukiwa kama waumini wenye njaa ya chalula cha kiroho, kufungua tu kurasa za “jiko” laMungu tukitafuta ka-ugali, itakuwa sahihi kama tutashikwa na uwoga kidogo tukikabiliwa na jukumu la kuielewa Biblia na mafundisho yake, na kama tutalazimika kufanya huo “upishi” wa ka-ugali hako sisi wenyewe. Mungu wetu amelitafutia ufumbuzi tatizo hili. Katika Kanisa la Bwana Yesu Kristo kuna mgawanyo timilifu wa kazi. Tunapookolewa, Roho Mtakatifu anampa kila mmoja wetu anayemwamini Bwana Yesu wakati huo kazi ya kiroho atakayoifanya na kipaji cha kuifanya na kuifanikisha kazi hiyo (1Wakor. 12:3-11). Pamoja na shughuli zote muhimu za kulijenga Kanisa lake, Mungu ametupatia “wapishi” katika “jiko” lake pia (Waefe. 4:11-13).

Mpishi: Katika 1Wakor. 12:12-31, Paulo Mtume analinganisha Kanisa na mwili wa mwanadamu. Anaeleza kwamba kama vile viungo vyote vya mwanadamu ni muhimu kwa uhai na afya yake, vivyo hivyo Kanisa la Kristo linamhitaji kila muumini wake, kwa sababu waumini hawa ndio “viungo”muhimu vya “mwili” wake. Katika “mwili” wa Kristo kila “kiungo” kinapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano na “viungo” vingine kama timu moja ili Kanisa lifanye kazi sawasawa kwa kila “kiungo” kutoa huduma ya utumishi ambao Mungu amekipangia – 1Wakor. 12:11. Kazi mojawapo muhimu ya mwili wa Kristo ni kuwasaidia waumini wake katika mchakato wa kukua kiroho. Sehemu mojawapo ya mchakato huu ni “kupika” chakula cha kiroho kifikie kiwango cha “kuweza kuliwa” kutokana na chakula ghafi kilichomo ndani ya Biblia. Kwa kuwa uandishi wa Biblia umekamilika, nyadhifa za mwanzoni ndani ya Kanisa za MITUME na MANABII hazijawezeshwa tena, hivyo wajibu wa kutayarisha “chakula” cha kiroho sasa kimekuja haswa kwa Mchungaji-Mwalimu – Waefe. 4:11. Hivyo wakati wanatafuta chakula chao cha kiroho, waumini wanapaswa kuzingatia jambo hili na kutafuta huduma zenye kufundisha Neno ambazo zimetoka kweli kweli kwa Mungu.

Hii haina maana kwamba Wakristo wenyewe hawana wajibu wa kusoma na kujifunza Biblia zao wenyewe. Kwa kweli ni lazima wafanye hivyo, (vinginevyo itakuwa rahisi kwao kupotea na kuingia katika mafundisho potofu); mfano, Matendo 17:11:

11 Sasa, Wayahudi wa Berea walikuwa na tabia ya kiungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwani walilipokea lile Neno kwa shauku kubwa mioyoni mwao, wakiyachunguza maandiko kila siku, ili waone kama aliyowafundisha Paulo ni kweli. - Tafsiri yangu kutoka NIV.

Lakini kama ilivyo katika maeneo mengi muhimu ya maisha yasiyo ya kiroho ya wanadamu (afya, sheria, fedha), vivyo hivyo katika eneo hili muhimu la maisha ya kiroho, “kujifundisha mwenyewe” kunaweza tu kuwa shughuli ya ziada ya kiroho, na siyo mbadala wa mfumo maalum wa utumishi (yaani mfumo wa Waalimu na Wachungaji) ambao Mungu ameuamuru (1Tim. 5:17; Waebr. 13:17). Watu wengi tu hawataki kupokea msaada kuhusiana na mafundisho ya Neno la Mungu (Mathayo 13:54-56; Yoh. 6:60). Lakini kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu si tu ni muhimu kwa ajili ya kupevuka kiroho, bali pia ni muhimu sana katika kuzuia “kurudi nyuma kiroho”, jambo lililowakuta waumini wa Yerusalemu walioandikiwa waraka na mwandishi wa kitabu cha Waebrania. Mwandishi huyu asiyejulikana, lengo la somo lake ni kuwarudisha katika msitari wana-kikundi Wakristo walioacha kujikusanya pamoja na kusikiliza Neno – Waebrania 10:25. Matokeo ya kulichukulia Neno katika namna vuguvugu kama hivi ambayo ilipelekea kushuka kasi ya kukua kiroho, ni kwamba walikuja kuwa “wagumu katika kusikia” na wakajikuta tena katika hali ya kuhitaji mafunzo ya msingi ya Kikristo, kama mwandishi anavyowaambia, “baada ya muda huu (katika Ukristo), wote mlipaswa kuwa waalimu wa wengine” (Waebr. 5:11 – 6:2). Zaidi ya hapo, kutokukijali kwao chakula kuliwaweka katika hatari ya kudhoofisha imani yao kwa Mungu - Waebr. 10:35-39. Kukua kiroho, na hata usalama wa kiroho, unataka tuwe na unyenyekevu wa kukubali msaada kutoka kwa wengine ili kupata “chakula” hiki muhimu sana – Zab. 25:9; Matendo 18:24-26.

Kuchagua Mpishi: Wakristo walioko Marekani leo hii yumkini wana uwanda mpana sana wa kuchagua waalimu wa kuwafundisha Neno zaidi ya Wakristo wote katika historia. Madhehebu, makanisa, taasisi za ki-dini na watumishi huru (wote wakijiita “Wakristo”), wamejaa katika taifa hili. Bila shaka hali si tofauti sana katika nchi nyingine zilizotembelewa na wamisionari. Fursa nyingi namna hiyo za kuchagua zinaweza kuufanya mchakato wa kuchagua mafundisho ya Biblia yanayofaa kuwa mgumu kidogo. Zaidi ya hayo, ukweli kwamba kuna “mbweha” wengi walio katikati ya “kondoo” unamaanisha kwamba mchakato huu una hatari zake pia – Mathayo 7:15-20. Kutokana na maandiko mengi yanayotoa tahadhari dhidi ya mafundisho ya uwongo (Mathayo 24:24; War. 16:17-18; Waebr. 13:9; 2Petro 2:1-22; Yuda 4:13), ushauri mwema unahitajika sana hapa:

• Awali ya yote, tafuta huduma (kanisa) ambamo kufundisha Neno la Mungu ndiyo shughuli iliyopewa kipaumbele, kwani ni katika kuunganishwa na Neno ndipo imani yako itakua – War. 10:17. Kuna taasisi nyingi zinazofaa sana kwa ajili ya fellowship, kwa mfano, lakini ambazo ni dhaifu katika kutoa chakula cha kiroho ambacho sote tunahitaji ili imani yetu iwe na nguvu zaidi.
• Pili, ukiishapata huduma inayoridhisha mahitaji haya mawili ya fellowship na mafundisho sahihi, kaa nao, usiwatelekeze. Inachukua muda kidogo kuzowea huduma mpya au mfumo mpya wa mafundisho, na pia haiwezekani (na haifai) kukua kiroho kwa kuchanganya mifumo mingi ya kufundisha Biblia. Tunapaswa kuwa na kiasi fuani cha msimamo katika mafundisho tunayopokea (consistency); kuruka-ruka kutoka kwa mwalimu mmoja na kwenda kwa mwalimu mwingine kila wakati si jambo jema. Kujihusisha na migogoro ya kanuni za mafundisho ni jambo lisilofaa – 2Tim. 2:14. Hivyo unapoona Mungu amekuongoza kwenye mafundisho sahihi na mema, usiyaache.
• Tatu, usijihusishe na huduma ambayo akili yako ya kuzaliwa inakunong’oneza kwamba kuna shaka. Aina tatu za “huduma” ambazo unapaswa kuziweka mbali, ambazo ziko katika mazingira ya Ukristo wa udanganyifu katika miaka hii ni:

a. Huduma au makundi yanayotilia mkazo na kuyapa kipaumbele maandiko mengine zaidi ya Biblia: Kuna mvuto mkubwa katika dhana ya “mafunzo ya kanuni za siri” zilizo katika vitabu fulani au kanuni fulani nje ya Biblia (mvuto huu unaonekana tangu wakati ule wa mafundisho ya kupotosha [heresies] ya Unostiki [Gnosticism] ya wakati wa Kanisa la Mitume); lakini ikiwa mafundisho haya yanatoka katika vitabu vya ziada (mfano, The Book of Mormons), vitabu vilivyoongezwa katika Biblia (The Apocripha au deutero-canonicals), au uandishi au mafundisho ya mwalimu yeyote au mhariri/mtoa-maoni, halafu hayo yanaanza kuwa na uzito unaofanana na au unaozidi ule uzito wa Biblia, haya unapaswa kuyaweka mbali, pamoja na makundi yanayofanya hayo na kuyasambaza. Biblia pekee ndiyo inapaswa kuwa kiwango na kipimo halisi cha imani yetu – 2Tim. 3:16.

b. Huduma au makundi yanayomsikiliza na kumkweza kiongozi mmoja mwenye kipawa badala ya mamlaka ya Biblia: Sisi sote tuna silika ya kumsikiliza na kumfuata kiongozi “mteule” anayejua vyote. Lakini kama Wakristo, tunapaswa kuelekeza macho yetu kwa, na kumfuata, Bwana wetu Yesu Kristo, na tusiwafanye watu kuwa “miungu ya sanamu” - 1Wakor. 3:21; Wagal. 4:17.

c. “Huduma” au makundi yanayotilia mkazo na kutoa kipaumbele kwenye “miujiza” na “maono” kuliko mafundisho ya Biblia: Sote tungependa kuona nguvu na uwezo wa Mungu ukidhihirika kimaajabu katika maisha yetu na mbele za macho yetu. Je, si tumesoma katika Injili juu ya wale watu waliokuwako wakati wa Bwana Yesu wakidai kuona “ishara”? Itakuwa “vyema” sana kuona ikitendeka (au sisi wenyewe tukitenda) miujiza ya aina ile ambayo Biblia inasimulia. Hata hivyo, katika kipindi hiki cha historia ya mwanadamu, Mungu ameamua kutilia mkazo Neno lake lililokamilika – Biblia Takatifu. Tunapotafakari kwamba Bwana Yesu Kristo ndiye Neno Lenye Uhai, inaleta maana vichwani mwetu kwamba katika wakati huu ambapo Biblia imekamilika na inapatikana kwa urahisi sana, Mungu ameelekeza macho yetu katika maneno yenye uhai ya Neno Lake badala na matendo na ishara za kumiujiza (hata kama ishara hizo zinasisimua kiasi gani!). Dhana muhimu hapa ni kwamba Mungu, kwa wakati huu, inaelekea hajatoa na hatoi vipaji vya kutenda miujiza kama ile iliyoonekana wakati wa Bwana wetu Yesu Kristo na Mitume wake. Miujiza ya namna hii ilielekezwa kwenye, na ilikuwa na lengo la, kuonyesha mamlaka waliyopewa na Mungu wale waliyoitenda. Muujiza mkuu wa kushangaza ambao Mungu anautenda wakati huu ni ule wa kutubadilisha sisi kwa kuzaliwa upya kutoka kuwa watu wenye dhambi, wanaoelekea kwenye kifo, na kuwa wana wa Mungu aliye hai kupitia kwa imani katika Yesu Kristo. Kuzaliwa upya - huo ndio mwujiza! Japokuwa, kama ulivyo upepo, uzazi wetu huu mpya hauonekani kwa macho, nguvu yake ni kuu na ni ya ki-nyuklia kweli kweli – Yoh. 3:8. Hivyo hatupaswi kuelekeza macho yetu kwenye ishara, unabii/utabiri, maono, miujiza, kunena lugha au mengine kama hayo, wakati huu tunapongojea kurudi kwake Mwokozi wetu katika utukufu mkuu, bali tuelekeze macho yetu Kwake, kupitia Neno Lake. Maandiko yanatufundisha kwamba tuko mahala pazuri zaidi kwa Neno lake, kwani hili ni la uhakika zaidi kuliko kitu chochote tunachokiona kwa macho yetu – 2Petro 1:16-21. Kung’ang’ana juu ya kunena lugha, uponyaji na matendo mengine ya Ki-karismatiki kama hayo ni hatari, na yanakutoa katika mstari wa kukua kiroho – Mathayo 16:4. Ni hatari kweli kweli! Tunapolazimisha mambo hayo kutokea, tunadhoofisha dhamiri zetu, na mwenendo ambao ulionekana kuwa si sahihi hapo mwanzoni, unaanza kuonekana kuwa ni wa kawaida na unakubalika, licha ya kwamba sio sahihi – Waefe. 4:17-18. Matokeo ya kuyafanya hayo ni kututenga na marafiki, familia na Wakristo wengine wa kawaida, na haya yote ni matokeo ya kujiunga na vikundi vya namna hii.

Muhtasari: Kutafuta na kuupata mfumo unaokufaa wa mafundisho ya kiroho (yaani ya Biblia) inaweza kuonekana kuwa ni shughuli ngumu. Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba kama Mungu ameamuru mafundisho ya namna hiyo, basi pia ameamuru uwepo wa waalimu, watumishi na taasisi zenye uwezo wa kutimiza mahitaji yetu yote ya kukua kiroho, ikiwa tu tuko tayari kufanya utafiti wa kuzipata huduma hizo na kuomba au kupokea msaada pale unapotolewa. Baba mwenye upendo ambaye anawapatia chakula hata ndege wa angani na anayavisha vizuri hata maua ya porini, kwa hakika atatupatia mahitaji yetu yote katika Yesu Kristo Bwana wetu – Mathayo 6:25-34; Yakobo 1:5.

Katika sehemu ifuatayo tutajifunza kuhusu: Awamu zilizobakia za kukua kiroho (kuliamini Neno, ku-liishi Neno na kuwasaidia wengine, katika Neno).

=0=

Translated from: Sanctification: Peter’s Epistles #13

=0=

Basi, na tuonane katika sehemu ya 14 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!