Fundisho-fumbo la Mpanzi: Nyaraka za Petro #12
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com
Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo
Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission For This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill
1Petro 1:1-2: (1) Petro, Mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule ambao japo wametengwa na kutawanywa katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia,
(2) wamechaguliwa na Mungu Baba kwani Aliwajua toka mwanzo kwa utakaso wa Roho Mtakatifu, hata mkapata kutii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani ziongezwe kwenu! (Revised Translation)
Maneno ya mwanzo ya Waraka wa kwanza wa Petro yanakiri kuteseka kwa waumini hawa wa karne ya kwanza, yakitilia mkazo kwamba kama waumini wa Kristo, sisi sote ni watengwa katika huu ulimwengu, na tumetawanywa katika kila nchi ya dunia hii. Lakini, japo sisi ni “wageni katika nchi ya ugenini”, na siku zote tutasumbuliwa na uadui wa dunia hii dhidi yetu, tunapaswa kukumbuka sisi ni wateule wa Mungu, tuliochaguliwa maalum na Yeye kutokana na imani yetu kwa Kristo. Hii hadhi maalum ya “uteule” ambayo Wakristo wote tunayo hatupewi bila malengo na inaambatana na majukumu makubwa: kutimiza malengo ambayo Mungu ametupangia hapa duniani. Lengo la kila mmoja wetu kama Mkristo (yaani lengo la kutumwa kwetu) wakati wote linahusisha kwa namna moja au nyingine, mchango wetu wa hali na mali kwa ajili ya ustawi kiroho wa waumini wenzetu (Kanisa la Bwana wetu Yesu Kristo).
Ili kuwasaidia wenzetu kwa ufanisi, tunapaswa sisi wenyewe kuwa wapevu, na ndiyo maana katika masomo yaliyopita tumetilia mkazo hoja kwamba lengo kuu la maisha ya Mkristo ni kukua kiroho na kuwasaidia Wakristo wengine kufanya hivyo hivyo.
Tunapookolewa, matatizo yetu katika maisha haya hayamaliziki mara moja. Kinyume chake, sasa tunayakabili mateso kama sehemu ya kawaida ya maisha yetu, na kama sehemu ya lazima katika maisha yetu ili kukua kiroho. Tunapojifunza kuyakabili matatizo ya maisha yetu kwa kumwamini Mungu, tunajenga imani yetu, na kukua kwa imani yetu ndiyo kukua kiroho. Ni katika kukiri magumu na mateso waliyokuwa wanayakabili wale walengwa wa barua yake, ndipo Petro alipowapa changamoto ya kupambana kwa moyo mpya na jukumu la kukua kiroho pale anapowaambia katika aya ya 2b, neema na amani viongezeke kwenu!
Maneno haya ya Petro “neema na amani viongezeke kwenu” yanayoonyesha matamanio thabiti, kwa upande wake, juu yao, ni zaidi ya salamu. Petro anavyosema kwamba “matamanio yangu kwenu ni kwa neema na amani viongezeke kwenu”, anawataka wale Wakristo wafanye juhudi za kukua kiroho, kwa sababu kukua kiroho ndiyo njia ya kuongezewa neema na amani. Neema na amani ni pande mbili za sarafu moja. Pande hizi mbili zinahusiana na ongezeko la baraka tunazopokea kutokana na jinsi tunavyozidi kukua kiroho. Neema zinamwonyesha Mungu kuwa ndiye mpaji wa baraka, na amani inatuonyesha baraka halisi tunazopokea kutoka kwa Mungu. Neema ni “Mungu anatoa”, na amani ni “sisi tunapokea”. Petro anasema “nataka Mungu awazidishie”, na pia anasema “nataka ninyi mpokee zaidi kutoka kwa Mungu”.
Tunapaswa kuwa waangalifu sana hapa, tusije kufanya kosa la kuchukulia baraka za Mungu kuwa ni mali. Akiwa ni Baba mwenye upendo, Mungu anataka tupate kile tunachokihitaji, siyo tunachofikiria tunahitaji. Mungu anataka roho zetu zijazwe furaha na kujiamini ambako msingi wake ni upendo tulio nao Kwake na kwa Mwanaye na furaha hii isitegemee mazingira yetu ya hapa duniani. Hii ni sababu mojawapo kwa nini magumu yanayotupata hapa duniani ni muhimu sana katika kukua kwetu kiroho, katika Mpango wa Mungu kwa maisha yetu. Magumu yanatulazimisha tumtegemee Mungu zaidi, na hii inatukomboa kutoka katika utumwa wa kutegemea mali zetu au fedha.
Neno neema kama lilivyotumika hapa na Petro limetokana na neno la Kiyunani “charis”, (Kiebrania chen), na maana yake ni “fadhila” au “nia njema”. Katika Agano Jipya, neno “grace” limetumika katika maana maalum ya ki-istilahi. Hivyo katika Agano Jipya, tunaposoma neno neema tunapaswa kuelewa kwamba Mungu ana uelekeo wa “nia njema” kwetu, “upanaji” au “wema” kwetu, kwani sisi ni watoto Wake. Sisi ni walengwa wa neema ya Mungu, ikiwa pamoja na baraka zote zinazoambatana, si kwa sababu tumestahili kwa lolote tulilofanya, bali ni kwa sababu kama waumini, Mungu anatuona tu mwili mmoja na Mwanaye, Bwana wetu Yesu Kristo, Yeye ambaye wakati wote amekuwa akifurahishwa naye Mathayo 3:17; 17:5.
Kama Wa-Kristo, sote tunapata fadhila za Mungu kwa sababu ya uhusiano wetu na Mwanaye Yesu Kristo. Kabla ya kumwamini Yesu Kristo, haki timilifu inayotokana na hulka ya Mungu ilimaanisha hukumu juu ya wanadamu – War. 1:18-23, lakini baada ya wokovu, dhambi zetu zinafunikwa na damu ya Yesu Kristo, “tunafanywa kuwa ni wenye haki” mbele za macho ya Mungu kupitia kazi iliyofanywa na Mwana – War. 5:1. Mwenendo wa Mungu kwetu unakuwa si wa hukumu kwa dhambi zetu tena, bali ni wa fadhila na baraka, yaani neema. “Neema” inamaanisha Mungu anataka kutubariki (Isa. 30:18: “Awangojea kule juu aliko ili awabariki – chanan kwa Kiebrania), na yuko huru kufanya hivyo kwa sababu Kristo amelipia dhambi zetu zote.
Kama wapokeaji wa neema za Mungu, tunapata amani ya Mungu. Amani ni neno la Kiswahili linalotokana na neno la Kiyunani eirene (ambako tunapata jina Irene), maana yake ni kuwa huru kutokana na migongano na kuwa huru kutoka kuhangaikia mambo yasiyo na umuhimu. Lakini waandishi wa Agano Jipya hawakuifkiria amani nje ya neno la Kiebrania shalom. Shalom ni neno linalomaanisha zaidi ya kukosekana shida; linamaanisha kuridhika, furaha, pumziko na utulivu. Shalom, kama linavyotumika Israeli leo hii, linamaanisha ukamilifu, kutopungukiwa na kitu.
Kama waumini, hakika hatupungukiwi na kitu. Sisi ni watoto wa Mungu, warithi wa ahadi zake, tumehakikishiwa ahadi zake, tumehakikishiwa maskani ya milele, na uzima wa milele, tukiwa na Mungu na Mwanawe, milele. Tunapookolewa, tunapewa Roho Mtakatifu kama alama na ahadi ya maisha yetu yajayo yaliyo na furaha tele, na kama Msaidizi wa maisha yetu ya hapa duniani pia.
Petro anapowatakia amani hii (na neema zinazoileta) iongezeke, kwa kweli anatuambia tuone kitu kile ambacho tunacho tayari, tupate faraja kutokana nacho, na tukitumie kwa ari yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Petro anatutaka tupevuke. Petro anataka imani yetu (ambayo ndiyo muhimu katika kukua kiroho), iwe imara na iongezeke. Kwani kukua kiroho ni kukua kwa imani yetu. Kwa hakika imani yetu itazaa matunda yake (upendo, utumishi, n.k.), lakini kazi zote njema za Mkristo msingi wake ni imani. Tunaokolewa kwa kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo, tunapevuka kwa kuamini mafundisho Yake na kuyatumia katika maisha yetu.
Mapitio ya Kukua Kiroho: Fumbo la Mpanzi
Fundisho-fumbo la mpanzi wa mbegu linatokea katika Injili zote tatu ambazo zinafanana sana (synoptic gospels) katika Mathayo 13:1-9; Marko 4:1-9; Luka 8:4-8, na Bwana Yesu anaeleza maana yake katika Mathayo 13:18-23; Marko 4:13-20; Luka 8:11-15. Japokuwa kimsingi fundisho hili linahusu wokovu, lina umuhimu hapa kwa sababu linafundisha pia mchakato wa kukua kiroho. Kwani kama vile kulivyo na mitizamo mingi kumhusu Yesu Kristo, lakini ni mtazamo mmoja tu, ule wa imani ndio unaopelekea kwenye wokovu, vivyo hivyo kuna mitazamo mingi kuhusu mafundisho Yake, lakini ni mtazamo mmoja tu, ule wa imani, ndio unaopelekea kwenye kukua kiroho. Katika fundisho-fumbo hili, mpanzi anaenda shambani kupanda mbegu katika aina nne tofauti za udongo: udongo mgumu (pembeni ya njia), udongo wenye mawe, udongo wenye magugu na miiba, na udongo mzuri wenye rutuba. Mbegu inayoanguka kwenye udongo mgumu kando ya njia ililiwa na ndege haraka; mbegu iliyoanguka kwenye udongo wenye mawe iliota haraka, lakini mmea ulikauka, ukafa kwa sababu mizizi ilikosa kina; mbegu iliyoanguka kwenye magugu na miiba iliota lakini ilisongwa; lakini mbegu iliyoanguka kwenye udongo mzuri iliota na kusitawi, na kutoa mazao mengi. Bwana Yesu anaelezea ule udongo mgumu kuwa ni yule mtu ambaye Shetani anamfanya (anamsababisha) kuikataa Injili; udongo wenye mawe kuwa ni yule mtu ambaye anatelekeza Injili akipatwa na magumu; udongo wenye magugu kuwa ni yule mtu anayesongwa na shida za maisha na kujiweka mbali na Injili; na udongo mzuri kuwa ni yule mtu anayeamini Injili na kuzaa matunda mengi kwa ajili ya Kristo katika maisha yake.
Hili jambo linaainisha aina nne za mwitikio wa watu kwa Injili, na ni mmoja tu anayeonyesha kuokolewa ikifuatiwa na kukua kiroho. Dondoo za fundisho-fumbo hili na tafsiri au maana zake ni kama ifuatavyo: “mbegu” inayopandwa ni Neno la Mungu, yaani Injili inayotamka kwamba Bwana Yesu ndiye Kristo/Masihi, na kwamba wokovu unapatikana kwa njia ya imani Kwake. “Mmea” ni imani ya yule mtu. “Udongo” unawakilisha moyo wa hao watu wanne tofauti. Ni muhimu kuona kuwa sisi ndio tunaoamua tutakuwa aina gani ya udongo; kama tutakuwa udongo mgumu, wenye miiba, wenye miamba/mawe au udongo mzuri, ni maamuzi yetu.
UDONGO MGUMU (imani kufa kabla ya kuzaliwa): Mtu wa “udongo mgumu” anaipata Injili, lakini anaamua kutomwamini Kristo. “Ndege” wanaokula mbegu kabla haijamea ni Shetani anayelitoa Neno kutoka moyoni mwa mtu huyu kwa sababu udongo ulio kando ya njia ni mgumu, na mbegu haiwezi kupenya, vilevile mioyo ya watu wengi ni migumu kwa ujumbe wa Injili wa imani kwa Kristo. Mioyo yao imekuwa/imeota sugu dhidi ya ile kweli ya Injili hivyo hawawezi kuipokea. Katika masimulizi ya Luka ya fundisho-fumbo hili kuna sababu ya ziada inayotolewa (Luka 8:5), kwamba mbegu hii “inakanyagwa” na wapita njia. Vivyo hivyo, kwa wale wanaokataa kuliingiza Neno mioyoni mwao mara moja, kweli ya Injili inadharauliwa na wanaomzunguka, na kupelekea yeye kumkataa Kristo. Bwana Yesu Kristo analielezea hili kuwa Shetani “anapora” kile kilichopandwa ndani ya mioyo yao. Shetani anafanya hivi ili wasiamini na kuokolewa – Luka 8:12. Masimulizi ya Mathayo ya fundisho-fumbo hili (13:19): watu wa aina hii “wamesikia Neno”, lakini “hawajalielewa”. “Kuielewa” kweli ya Mungu kunatokea tu kwa imani kama tulivyoona hapo nyuma. Kwa watu wenye mioyo ya “udongo mgumu”, kutotaka kwao kuelewa maana yake ni kwamba hawataelewa “ule wokovu mkuu” ambao wanauacha upotee – Wakor. 2:3, na habari hii ni “ujinga” kwao – 1Wakor. 1:8ff. Shetani anafanikisha vipi jambo hili? Tunapaswa kukumbuka kwamba japo Shetani ana mvuto na ushawishi juu ya watu hawa, jukumu na uamuzi wa kumkubali au kumkataa Bwana Yesu Kristo ni wa kwao wenyewe binafsi.
Kila mwandisi (katika hao watatu wa Injili) anatumia jina tofauti kwa ajili ya Shetani, na hilo linatupa fununu juu ya mbinu anazozitumia kumdanganya asiyeamini na kumtia moyo katika kutoiamini Injili. Mathayo anamwita Shetani “yule mwovu”, na kwa kweli anayo kawaida ovu ya kuweka uwongo mahala pa ukweli. Marko anamwita “Shetani”, neno/jina la Kiebrania linalomaanisha adui, naye “hupinga” ile kweli popote pale ilipo. Luka anamwita “Ibilisi”, maana yake “mzushi, mwongo”, na kwa kweli Ibilisi hupotosha kweli kila inapojitokeza. Pale mtu asiyeamini anapokuwa na Injili ya Kristo moyoni mwake, akiipima na kuitafakari, adui yetu Ibilisi hufanya kila analoweza kumshawishi mtu huyu aitelekeze injili hiyo. Hufanya hivi, si kwa kujitokeza kimwili (na kuonekana), bali kwa kutumia uwongo, hofu na udanganyifu ulio ndani ya moyo wa mtu huyu ambao ameukusanya katika maisha yake hapa duniani. Ulimwengu huu ni wa Shetani – Yoh. 14:30, japo ni kwa muda tu, naye ameujaza kila aina ya uwongo, udanganyifu unaomtumikia. Kwa hakika, kila inapotokea mtu mmoja kufikiria kuwa Mkristo, “yule mwovu” atavuruga habari hii kwa uwongo (kwa kuupinga msingi wa kweli wa wokovu kwa imani, na kufundisha uwongo wa wokovu kwa matendo mema, kwa mfano); kama “adui”, atajaribu kumrudisha nyuma mtu huyu kwa kumtia woga na kumtisha (kumkumbusha gharama na hatari, za kimwili na/au za kijamii, za kutambulika kama “Mkristo”, kwa mfano); kama Ibilisi, atajaribu kumfanya mtu huyu asiyeamini kutilia shaka ukweli wa ujumbe huu rahisi wa Injili ya Kristo (kwa kumshawishi atilie shaka malengo ya wale wanaomfundisha – yaani waalimu wake, kwa mfano). Marko anasema Shetani “hufanya haraka” kupora ile mbegu ya kweli kabla haijamea na kuzaa imani halisi. Mbegu ilikuwa nzuri, lakini imani haikuwemo, katika moyo mgumu.
UDONGO WENYE MAWE (imani kufa): Yule mtu wa “udongo wenye mawe” anausikia ujumbe wa Injili na anamwamini Bwana Yesu, lakini “imani” yake ni ya mpito tu. Matokeo yake, japo “mmea” wake wa imani unaota haraka anapoupokea kwa “furaha” ujumbe wa wokovu kutoka katika dhambi na ahadi ya uzima wa milele kupitia imani katika Kristo, imani yake hii ya muda mfupi inaunguzwa na jua haraka tu. Bwana Yesu analieleza jua katika fundisho-fumbo hili kuwa ni unyanyasaji na magumu ambayo ni lazima kumsibu kila muumini katika Yeye. Huyu mtu wa “udongo wenye mawe/miamba” ni yule ambaye “hakuhesabu gharama” ya kuwa mfuasi wa Bwana Yesu – Luka 14:28ff, hivyo imani yake inapokutana na ukinzani mkali, inakufa.
Katika mfano wa mtu wa “udongo mgumu”, imani haikuweza hata kuota mizizi. Mtu wa “udongo wenye mawe” kwa upande mwingine, ana mizizi kwani mbegu ilimea, lakini “mizizi yake” (nguvu ya imani yake) haina kina cha kutosha. Hii ni kwa sababu udongo si mwingi wa kutosha kwenda chini. Imani inaota mizizi katika moyo wake, lakini kabla ya mizizi ile kurefuka kwenda chini, inakutana na mwamba usiopenyeka. Huwezi kumwambia Mungu “hapa ni mwisho wa kukua kwa imani yangu”. Huwezi kujito[le]a nusunusu kwa Bwana Yesu. Wakristo wanabakishwa hapa duniani baada ya kuokolewa kwa lengo la kupewa mitihani ili wadhihirishe imani yao kuwa ni halisi na yenye nguvu. Kujitoa nusunusu, kuweka umbali kati yako na Mungu maana yake “mizizi” ya imani yako haitaweza kupambana na “jua kali”na “joto” nao mmea utakufa.
Bwana Yesu Kristo (katika Mathayo na Marko) anafundisha kwamba katika nyakati za mitihani, watu wa namna hii “mara huchukizwa” - KJV. Neno linalotumiwa la Kiingereza ni “offended” na msingi wake ni neno la Kiyunani skandalon, ambalo ndilo chimbuko la neno la Kiingereza scandal, na linatumika katika Septuagint (tafsiri ya kale ya Biblia ya Kiebrania iitwayo “The LXX” - unaweza ku-google kwa maelezo zaidi) kutafsiri maneno mawili ya Kiebrania, moja linamaanisha “kikwazo”, na lingine linamaanisha “mtego”. Pande zote mbili za hili neno zinatufaa hapa kumwelezea mtu aliyempokea Bwana nusunusu tu, ambaye mwendo wake wa imani “unanaswa” na mtego wa manyanyaso, magumu na majaribu, na anajikuta “akitupiwa chambo na kunaswa” na juhudi za Shetani za kumshawishi arudie maisha yake ya zamani. Maneno ya Bwana Yesu katika Injili kama ilivyoandikwa na Luka yanaenda ndani zaidi: “Wanaamini kwa kitambo kidogo, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani.” Neno la Kiyunani linalotumika hapa ndilo linalotupatia neno la Kiingereza linalomaanisha “kuacha imani” au apostasy na maana yake iko wazi: watu wa namna hii waliamini, kwa kitambo, lakini katika wakati wa majaribu (ambayo hakuna Mkristo asiyepitia) wanaacha imani yao. Mbegu ilikuwa nzuri, lakini imani haikuweza kuota mizizi ya kudumu katika mioyo yao yenye mawe/miamba.
UDONGO WENYE MAGUGU/MIIBA (imani kudumaa): Mtu wa “udongo wenye miiba na magugu” anaweka imani yake kwa Bwana Yesu, lakini miiba inaota katika moyo wake. “Miiba” hii ni shughuli na mihangaiko ya duniani ambayo inashindana na “mmea wa imani” uliomea moyoni mwake, na mwisho “miiba” hii inashinda kwa kuisonga imani na kuidumaza. Mtu huyu “analisikia Neno jema”, lakini Neno hili lililopandwa moyoni mwake linanyongwa na kuzidiwa nguvu na mambo mengine ambayo mtu huyu anayaona muhimu zaidi kwake kuliko Bwana Yesu Kristo. Hii inatokeaje?
Hapa tutazungumzia aina mbili za mfadhaiko wa mawazo ambao unatutenganisha sisi waumini na Kristo; hii itatusadia kuelewa mchakato ambao Bwna Yesu anauzungumzia hapa. Aina hizi mbili za mfadhaiko wa mawazo ni (1) hofu, na (2) tamaa. Dunia hii ya Shetani imesheheni matatizo kwa kila mtu, kasa waumini wa Bwana Yesu, ambao wote wanajikuta wakikabiliwa na ukinzani wa Shetani. Kama watu wa kawaida, sote tuna wasiwasi na tuna matamanio kila siku ya maisha yetu, lakini ni muhimu sana tuwe na mtazamo sahihi kuhusu hivi vyanzo viwili vya msongo kwa imani yetu; huu ni mtazamo wa Ki-Mungu, mtazamo wa hali yetu kama inavyoonekana kutoka mbinguni. Kwa kuwa sisi ni wanadamu, ni shuruti tuwe na wasiwasi na ajira zetu, familia zetu, afya, maisha, lakini kwa mtazamo wa Mungu, hakuna sababu yoyote ya kuwa na wasiwasi.
Kwa kweli hii ni dhana ngumu kwa sisi viumbe dhaifu kuikubali, hasa magumu na maumivu yetu yanavyokuwa makali. Lakini pale Bwana Yesu anapotuambia “msiwe na wasiwasi” kuhusu nini mtakula, nini mtavaa na nini mtakunywa kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anafahamu kwamba mnahitaji hayo yote” - Mathayo 6:25, anatuonyesha maisha yetu yanavyoonekana kutoka mbinguni. Mungu anayajua matatizo yetu yote, na sasa hivi, hapa hapa, anahakikisha kwamba magumu yetu yote Yeye anayafanyia kazi ili yawe kuwa mema kwetu - Warumi 8:28. Wasiwasi na hofu vitaendelea kutukabili maisha yetu yote, lakini kamwe tusiruhusu kutawaliwa na mambo hayo mawili. Tunapaswa kukumbuka kwamba Mungu ni mkubwa kuliko kitu chochote tunachokiogopa, na kwamba Yuko hapahapa akitusaidia. Na zaidi ya hapo, magumu ya maisha hayatadumu milele. Injili ya Mathayo na ile ya Marko zinatilia mkazo kwamba magumu haya ni ya “muda tu”, katika maisha “haya” pekee. Kama Wakristo, tuweke tumaini letu kwa wakati ujao, ambapo hatutakuwa na hofu wala wasiwasi tena – Isa. 25:8; Ufu. 21:4.
Yule mtu mwenye moyo unaosongwa na miiba hamwamini Mungu kiasi cha kutosha. Majaribu yanapomsibu, haamini kwamba Mungu atamvusha salama, na hivyo imani yake inafifia/inapungua.
Yule mtu mwenye kusongwa na miiba anakuwa na tatizo lilelile anapokabiliana na tamaa zake. Pamoja na wasiwasi na hofu, tutegemee tamaa na shauku/hamu zetu kuwa sehemu ya maisha yetu. Tangu kuondolewa Adamu na Eva kutoka bustani ya Edeni, wanadamu wote wanalazimika kukabiliana na “dhambi iliyo mwilini” - Warumi 7:17, na tamaa haribifu zinazotokana na mwili. Tamaa inayowakilisha nyingine zote inayotajwa hapa ni ile ya mali. Tatizo siyo pesa (ambayo ni muhimu ili kuishi duniani), bali ni “tamaa ya pesa” - 1Tim. 6:10. Moyo wenye miiba na magugu unaruhusu tamaa ya mali kuchukua nafasi ya upendo kwa Mungu. Kama Bwana Yesu anavyosema katika fundisho-fumbo hili, mali “hudanganya”. Mali inaweza kutuingiza katika mtego ambamo tutaacha kumtegemea Mungu, na kumweka mahala pake BWANA mwingine: fedha (Mathayo 6:24).
Kufikiri kwamba mali itatatua matatizo yetu ni kuamini katika kiini-macho (illusion), na kuacha kumwamini Yeye Aliyeumba na Anayehimili ulimwengu huu wote na kutegemea mali ambazo ni vitu vya kupita na vya udanganyifu katika hii dunia ni kitu cha kushangaza kabisa. Bwana Yesu alitoa tahadhari dhidi ya ubatili wa kujaza mali hapa duniani ambapo “nondo na kutu huharibu, na mwivi huvunja na kuiba” - Mathayo 6:19ff. Akatuambia kwamba “tuweke hazina yetu mbinguni” kwani palipo na hazina yako, ndipo moyo wako ulipo pia”. Kuna faida gani kuwa na mali [za] dunia nzima, Bwana Yesu anauliza, kama unapoteza uzima wa milele badala yake – Mathayo 16:26? Yule mtu wa moyo wenye miiba anapuuza tahadhari hizi, na kuruhusu hofu na tamaa kuuteka moyo wake na kudumaza ukuaji wa imani yake. Matokeo yake “hazai matunda yoyote” kitu ambacho ni kinyume cha malengo ya Mungu kwa maisha yetu ya Kikristo – Yoh. 15:16.
Kama ambavyo tumesema tena na tena katika somo hili, tuko hapa duniani ili kukua kiroho na kuwasaidia wenzetu wakue kiroho. Hili ndilo “zao” au “tunda” ambalo Mungu ametuwekea kama jukumu letu tuzae. Kulieleza hili katika namna rahisi kabisa, “zao” hili ni kuongezeka kwa imani yetu, na kuongezeka kwa imani ya wenzetu kutokana na msaada tunaowapatia. Ni rahisi sana kutamka kwamba “tunayo imani”, lakini, kama Yakobo anavyosema, “imani peke yake, kama haitoambatana na matendo, imekufa” - Yakobo 2:17. Hii maana yake ni kwamba ‘imani yetu inapaswa kudhihirishwa kwa matendo yatakayotokana na imani hiyo – yaani kufaulu mitihani ya imani’. Watu wengi wanaelewa kimakosa “matendo” anayomaanisha Yakobo katika sura ya pili. Yakobo hazungumzii “matendo fulani mema” (kama vile kutoa pesa kwa masikini, au kuwa mmisionari). Kwa hakika tunapaswa kusaidia wenzetu, lakini Yakobo anamaanisha utiifu kwa Mungu, haswa pale inapokuwa vigumu sana kutii, pale panapotakikana imani kuu iliyo dhahiri kwetu, ndani ya mioyo yetu. Yakobo anawazia nyakati zile katika maisha yetu ambapo tunatakiwa kuchukua hatua ngumu kutokana na imani yetu, lakini, mara tunapofanya hivyo, tunatizama nyuma na kusema, “nisingeweza kufanya hili kama nisingekuwa namtegemea Mungu!”
Yakobo anao mfano halisi wa kuainisha pointi yake: amri ya Mungu kwa Abrahamu ya kumtoa sadaka mwana wake wa ahadi Isaka. Tukilitazama tukio hilo sasa (kwani limekwishatokea), tunaona kwamba kila kitu kilienda sawa kutokana na mpango wa Mungu. Mungu aliweza kumzuia Abrahamu asimwue mwanawe Isaka, na akatoa mwanakondoo badala yake awe sadaka – mfano wa wazi kabisa wa Kristo akichukua mahala petu msalabani na kuhukumiwa badala yetu sisi. Lakini Abrahamu hakuwa na namna yoyote ya kujua hilo kabla halijatokea. Zaidi ya kujua kwamba amepewa amri ya kufanya kitendo cha kutisha kisichoweza kufikirika katika hali ya kawaida ambacho kilikuwa na lengo la kumwondoa mrithi wake aliyemngojea kwa subira kuu maisha yake yote, alikuwa na uhakika na kitu kimoja kingine: hulka na tabia ya Mungu aliyemjua na kumpenda kwa moyo wake wote.
Ili imani yetu ikue, tunapaswa kufanya kama Abrahamu alivyofanya. Tunapaswa kuyakabili kwa imani, mazingira magumu, na wakati mwingine yanayoonekana kuwa hayawezekani, ambayo ndiyo muhimu katika makuzi yetu ya kiroho. Silaha zetu zikiwa ni ufahamu tulio nao kwamba Mungu ni mwema na imani yetu katika wema huo, na kwamba Anatujali, tunapaswa kuishinda hofu yetu na tamaa yetu kwa kumwamini Yeye. Baada ya kufanya hivyo tunaweza kutazama mafanikio hayo dhidi ya magumu na kuwa na uhakika kwamba imani yetu ni halisi na ya kweli. Yule mtu mwenye moyo wa miiba hana kumbukumbu za namna hiyo katika maisha yake ya Kikristo kwani hamtegemei Mungu katika nyakati za majaribu na mitihani migumu, na hivyo hana “matendo mema” au matokeo ya kuonyesha. Shughuli na majukumu ya dunia hii yanamfadhaisha na kumpeleka mbali na Mungu, hivyo basi yeye huutafuta msaada mahala pengine kwa ajili ya ufumbuzi pale anapojaribiwa na/au anapokabiliwa na magumu. Japokuwa anaipokea habari njema ya Bwana Yesu “kwa furaha”, kamwe, kama masimulizi ya Luka yanavyosema, “hawezi kuzaa matunda”. Kwa hakika tunaweza kujiuliza kama mtu wa namna hii ni Mkristo kweli (au la). Imani halisi kwa Kristo ndiyo ishara ya muumini, na tunajua kwamba yawezekana kwa imani kupotea na nafasi yake kuchukuliwa na kutoamini – War. 11:20-21. Hata kama mfano wa “udongo wenye miiba” unahusisha kiasi fulani cha Wakristo wa kweli (japo “wamedumaa”), inafaa kwetu kutahadhari na hali hii, kwani katika mateso ya kutisha yanayokaribia kuanza hapo mwisho wa enzi hii (yaani “the tribulation” - dhiki kuu), imetabiriwa kwamba Wakristo wengi wenye moyo nusunusu namna hii wataasi imani yao - Mathayo 24:10-12; 2Wathess. 2:3; 2Petro 2:1-22. Ni imani hai pekee itatuvusha katika vita za maisha haya na pia mihangaiko ya maisha yetu. Mwisho wa yote tunapaswa kuchagua kati ya kumtegemea Mungu na kusikiliza sauti za hofu zetu na tamaa zetu. Mahali ambapo miiba ya hofu na matamanio ikiachwa ikue bila kukatwa, uaminifu na utegemezi halisi kwa Mungu hauwezi kusitawi. Mbegu ilikuwa nzuri, lakini imani ambayo mwanzo ilipokewa kwa furaha, kitambo tu inasongwa katika moyo ulio katika mazingira ya miiba na magugu.
UDONGO MZURI (imani kukua): Udongo mzuri ndio ukamilifu ambao sote tunapaswa kuukusudia. Mtu wa “udongo mzuri” anamwamini Bwana Yesu Kristo, na anaendelea kukua kiroho kama muumini baada ya hapo. Katika moyo wake hakuna udongo mgumu usiotaka kupokea mafundisho ya Mungu, hakuna udongo wenye mwamba unaozuia Neno la Mungu lisiote mizizi, na hakuna magugu ya hofu na tamaa zinazosonga uhai wa imani mpya inayotaka kumea. Moyo wa mtu mwenye “udongo mzuri”, kama Bwana Yesu anavyotuambia katika Luka 8:15, ni ule “unaostahili na mzuri”. Maneno yote mawili ya Kiyunani yaliyotafsiriwa kama unaostahili na mzuri yanaweza kutafsiriwa kama “mzuri”, lakini tofauti kati yao ni muhimu sana. Neno la kwanza, kalos, linamaanisha kitu ambacho kinafaa kutumiwa (kama vile bandari “nzuri” inavyofaa kupokea meli). Moyo wa mtu wa “udongo mzuri” uko tayari kupokea mbegu ya ujumbe wa Neno a Mungu kuhusu Bwana Yesu kwa sababu una utayari wa kufanya hivyo na kwa hivyo “unastahili”. Neno la pili, agathos, linamaanisha kitu ambacho kinaweza kutoa matokeo mazuri/sahihi (kama vile askari mzuri anayepigana vita kwa ufanisi). Hivyo moyo mzuri pia unatoa mazingira stahiki kwa “mmea wa imani” (uliomea kutokana na mbegu ya Neno la Mungu) uendelee kukua na kuzaa matunda. Kiasi cha mazao kinaweza kutofautiana (Marko 4:8), lakini ni “udongo mzuri” pekee unaozaa matunda, na udongo wote ambao ni mzuri utazaa.
Tuliposikia habari njema za Bwana Yesu Kristo, tulizipokea kwa furaha, na imani ilistawi ndani yetu. Hivyo tuwe waangalifu kuutunza “mmea wa imani” ndani ya mioyo yetu, na tusikate tamaa pale Mungu anapokata (anapopogoa - prune) matawi yasiyotakiwa kutoka katika mmea huo – Yoh. 15:2.Basi na tuwe makini katika kuitunza imani yetu, ili tuendelee kuwa sehemu ya mzabibu halisi, Bwana Yesu Kristo mwenyewe, ili tuzae matunda Aliyotupangia kuzaa pale msimu utakapofika – Yoh. 15:5.
“Imani inatokana na kusikia” (War. 10:17), lakini si wote waliosikia waliamini (udongo mgumu haukuamini), si wote walioamini waliendelea na imani yao (udongo wenye mawe na miamba haukuendelea na imani), si wote waliokuwa na imani walizaa matunda kwa ajili ya Bwana (udongo wenye miiba na magugu haukuzaa matunda). Hivyo, kitu muhimu hapa siyo kwamba mtu amelisikia Neno, la hasha, bali kitu muhimu ni mtu anafanya nalo nini baada ya kulisikia. Suala hili ni muhimu kwa maendeleo yetu ya kiroho, kwa sababu taswira inayoelezewa katika fundisho-fumbo hili ya kulipokea na kulikubali au kulikataa Neno la Injili inajirudia-rudia kila mara tunapolisikia Neno la Mungu. Haitoshi kusikia tu. Kama tukikataa mafundisho ya Neno la Mungu (udongo mgumu), tukilitelekeza baada ya muda (udongo wenye mawe), au tusipolipa kipaumbele katika maisha yetu (udongo wenye miiba), tunahatarisha maisha yetu ya kiroho na ukuaji wetu wa kiroho na imani yetu unakuwa mashakani.
Fundisho-fumbo hili, katika vitabu vyote vitatu, linazungumzia imani, yaani kuweka imani yetu katika Neno la Mungu. Katika vitabu vyote vitatu, moyo mzuri unalisikia Neno, lakini pia katika vitabu vyote vitatu, unafanya zaidi ya kusikia tu. Katika Injili ya Marko tunasoma kwamba mtu yule anasikia na “anapokea” (Kiyunani paradechomai): anapokea ukweli wa Biblia hata kama ni vigumu kwake. Injili ya Mathayo inasema kwamba anasikia na “kuelewa” (Kiyunani suniemi): anaelewa ukweli wa Neno la Mungu kwa kutumia sikio la imani na siyo macho yake (2Wakor. 5:7). Injili katika Luka inasema analisikia na “kuliweka moyoni” (Kiyunani katecho): anashika imara Neno la Mungu licha ya magumu aliyo nayo. Katika kupokea, kuelewa kwa imani, na kuliweka rohoni Neno la Mungu, moyo mwema au mzuri uko tayari kuendelea kukua na kuzaa kwa ajili ya Bwana. Uko tayari kukua kiroho na kuwasaidia wengine wakue pia.
NEEMA NA AMANI: Matakwa ya Petro kwetu sisi katika aya ya pili ni kwamba “neema na amani viongezeke kwenu”, kwa maneno mengine ni kwamba anatuombea tukabiliane na changamoto ya kukua kiroho kwa ushupavu, tuzitumie baraka na neema tele tulizo nazo kutoka kwa Mungu na tufaudu amani kuu ya kiroho ambayo ni matokeo ya baraka na neema hizo. Hii haitatokea ikiwa tutaifanya mioyo yetu kuwa migumu (udongo mgumu), au tukishindwa kuacha mizizi ya imani iote kwa ustawi ndani ya mioyo yetu na hivyo kukosa nguvu ya kupambana na magumu (udongo wa mawe), au kuacha imani yetu kufifia na kupotea katika matatizo yetu na magumu ya kila siku (udongo wenye miiba). Kama vile tulivyookolewa kwa kumwamini Bwana Yesu Kristo, tutapevuka kiroho ikiwa tutakuwa tayari kuyatafuta mafundisho Yake, na kukua kwa kuyapokea, kuyaelewa na kuyaweka rohoni katika imani.
=0=
Translated from: The Parable of the Sower: Peter’s Epistles #12
=0=
Basi, na tuonane katika sehemu ya 13 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!