Ufunuo wa Mungu katika Uumbaji na Kwa Njia ya Yesu Kristo:
Nyaraka za Petro #11

Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission For This Translation Has Been Kindly Granted By
Dr. R. D. Luginbill

Mapitio: Kama tulivyoona katika somo letu lililopita, kitabu cha 1Petro kwa kiasi kukubwa kinajihusisha na kupevuka kiroho (mahususi mchango wa mateso kama wakala wa mchakato wa kukua kiroho kwa Mkristo). Hivyo sisi pia tunapaswa kuchambua kanuni hii ya kukua kiroho kwa undani zaidi kabla ya kuendelea na fasili hii yetu. Zaidi ya hapo, ni faida kwetu kufanya hivyo kwani kusudi la maisha yetu hapa duniani kama Wakristo ni kupevuka kiroho na kuwasaidia wengine kufanya hivyo. Kuwasaidia wengine kukua kiroho inaitwa utumishi au huduma ya Mkristo, na kwa kiasi fulani kunategemea karama ya kiroho aliyopewa kila mmoja wetu. Lakini mchakato wa kukua au kupevuka kiroho unafanana kwa Wakristo wote. Japokuwa ni somo pana sana, kukua au kupevuka kiroho kunahusisha kuelekeza nia yetu yote kwa kitu kimoja tu: kweli. Kueleza hili kwa urahisi kabisa: kimsingi, kukua kiroho kunahusisha kujifunza Neno la Mungu na kulitumia katika maisha yetu. Hivyo kweli ndiyo ufunguo wa maisha ya Mkristo.

Kweli: Sasa, kweli ndiyo nini? Kwanza kabisa, tunaweza kusema kwamba hapa tulipo, katika himaya ya Shetani, kweli ya Mungu pekee ndiyo inayoweza kututoa katika ubinafsi wa kujishughulisha na shida zetu pekee, na kutuweka katika msitari wa Mpango wa Mungu, msitari wa mapenzi ya Mungu. Ni kweli pekee inayotufundisha, inayotupa faraja, inayotutia moyo na inayotuonyesha njia sahihi ya kuelekea. Zaidi ya kanuni yoyote ile, kujifunza na kuitumia kweli ya Mungu ndiko kunakotofautisha Wakristo na ulimwengu wote, na Bwana Yesu alitamka bayana kwamba sababu ya huduma yake ya hapa duniani ilikuwa ni kushuhudia hiyo kweli. Wakati akihojiwa na Ponsio Pilato (Yoh. 18:37-38), Bwana Yesu alisema, “Unasema kwamba mimi ni mfalme. Ndiyo, kwa lengo hili nilizaliwa, [na pia] nimekuja hapa duniani ili niishuhudie ile kweli.” Jibu la Pilato kwa Bwana Yesu lilikuwa: “Kweli ni nini?” Japokuwa Pilato hakuwa na nia ya kuijua wala kuifuatilia kweli ya Mungu, kwa Wakristo kweli ni chakula, ni mazima ya mama ambayo yanatuwezesha kuishi na kukua – 1Petro 2:2. Sasa, tunalijibu vipi swali la Pilato? Kweli ni nini haswa?

Kwanza, kweli yote inatoka kwa Mungu, kwani Mungu ndiye kweli. Bwana Yesu Kristo anasema katika Yoh. 14:6, “Mimi ndiye kweli na njia na uzima.” Hivyo kujifunza juu ya Bwana Yesu, ndiyo kujifunza kweli. Lakini kwa njia ipi, hapa duniani, tunaweza “kumjua” kwa ukamilifu yule Muumba wa vyote anayejua vyote, anayeweza vyote, aliye kila mahala – 1Wakor. 13:12? Katika neema zake, Mungu amewapatia wanadamu kweli mahususi kwa faida yao katika haya maisha , hazina ya ufahamu inayoweza kufahamika na kutumika. Kweli hii imegawanywa katika makundi makuu mawili:

(1) kweli inayoonekana na kila mwanadamu kupitia ufunuo katika uumbaji au ufunuo unaoonekana wazi kwa macho.

(2) kweli inayopatikana kwa waumini wa Bwana Yesu Kristo pekee kwa njia ya ufunuo maalum au ufunuo wa kiroho – Neno la Mungu.

Ufunuo Katika Uumbaji (Natural Revelation): Mungu ndiye muumba wa ulimwengu – Mwa. 1:1. Kwa sababu hii, ulimwengu na vyote vilivyomo vinashuhudia uwepo Wake. Tunaweza kuuona ukweli huu kwa kuutazama ulimwengu na kuona mastaajabu ya ukubwa wake, na uwingi wa vilivyo hai na visivyo hai ndani yake. Kuna mengi tunayoweza kujifunza kumhusu Mungu kwa kutizama ulimwengu na kuufanyia utafiti wa aina mbalimbali, lakini maandiko yanatilia mkazo kanuni mbili ambazo Mungu ameziweka kwa ajili ya mtu asiyeamini uwepo Wake pindi akitizama na kuutafakari uumbaji Wake.

(1) Ukweli wa uwepo wa Mungu unaonekana wazi kwa kutafakari ulimwengu aliouumba. Katika Zaburi 19:1-6 tunasoma kwamba “mbingu zinasimulia utukufu wa Mungu” (pia Ayubu 36:24-25; Zaburi 8:1-3; 97:6). Yaani kwa kuutizama na kuutafakari ukuu na ukubwa ulimwengu, uzuri wa uumbaji, wanadamu wanafahamu mioyoni mwao kwamba Muumba lazima awepo. Mtume Paulo pia anathibitisha dhana hii kwa kauli yake madhubuti, bila kumumunya maneno:

Hulka [ya Mungu], japo haonekani, hata hivyo ni dhahiri, na iko wazi tangu Alipoweka misingi ya ulimwengu, kwani yaweza kufahamika kutokana na uumbaji Wake – [huu unadhihirisha] uweza Wake wa milele na Uungu Wake – hivyo kwamba [wasioamini] hawana kisingizio
Warumi 1:20 (Revised translation)

Zaidi ya hapo, Paulo anaenda hatua moja mbele ya mwandishi wa Zaburi. Katika Warumi 1:20, siyo tu kwamba tunaona ukweli wa uwepo Wake kutokana na uumbaji Wake wa kustaajabisha, bali pia tunafundishwa hulka ya Nafsi Yake. Yeye ni mwenye haki, na ni mwongofu na mwenye uweza mkuu. Dhana hii inaendelezwa katika kanuni ya pili ambayo wanadamu wanajifunza katika kuutafakari uumbaji wa Mungu.

(2) Uwepo wa Mungu unadhihirika ukitafakari dhana ya wema na ubaya. Pia katika Warumi 2:14-16, Paulo anasema kwamba baadhi ya wanadamu wasio Wayahudi ambao hawana maandiko ya kuwaongoza katika mwenendo wao, hutenda mema kwa silika yao tu (kwa Kiyunani physei, yaani kwa silika yao). Hii ni kwa sababu Mungu amepandikiza katika dhamiri ya kila mwanadamu kanuni muhimu za mema na mabaya – 1Wakor. 11:14-15. Paulo anaendelea kufundisha kwamba dhamiri za watu hawa wa mataifa wakati mwingine zinaunga mkono na wakati mwingine zinahukumu matendo yao (aya ya 15), hivyo kufahamu uwepo wa dhambi ni sehemu ya utu wetu kama watoto wa Adamu na Eva (tizama Mithali 20:27 ambapo tunaona hulka ya roho aliyopewa na Mungu ni kutathmini moyo wa mwanadamu).

Bila ya mawasiliano yoyote kutoka kwa Mungu, bila kutembelewa na malaika, bila mafundisho kutoka katika Biblia, wanadamu wote wanafahamu kanuni za kweli za kiroho, kutokana na kutafakari mambo ya ulimwengu ambayo yako wazi kwa kila mtu. Ikiwa wanataka kukiri kweli hii au la, watu wanajua kwamba Mungu yuko na aliumba ulimwengu na aliumba wanadamu. Wote wanajua kwamba Yeye ni Mungu mwenye haki na ni Mungu mwongofu. Wote wanaelewa kwamba kuna mema na mabaya, kuna mazuri na maovu. Na wote wanajua kwamba, hata wakijitahidi namna gani, kutenda mema ni jambo lisilowezekana, kwani uovu ni sehemu ya maisha yetu – mambo haya yamekuwa dhahiri zaidi tangu ujio wa Roho Mtakatifu – Yoh. 16:8-11. Mungu, katika neema zake zisizokuwa na mfano, ameumba ulimwengu kwa mpangilio hivi kwamba hata bila wamisionary na bila miujiza, wanadamu wote wanalifahamu tatizo la maisha ya hapa duniani: sote tutakufa, na ikiwa hatutapewa msaada, sote tutakabiliwa na maswali yatakayoulizwa na Mungu mwenye haki na mwongofu ambaye bila shaka yuko, na hatutakuwa na kisingizio kwa matendo maovu tuliyotenda hapa duniani. Katika mioyo yetu, katika nyakati mbalimbali za maisha yetu, hata kama ni kwa muda mfupi tu, kila mmoja wetu anauona ukweli huu. Akili ya kawaida tu inatoa rai kwamba dhana hii inapaswa kutupatia motisha ya kutosha, shauku ya kutafuta kujua zaidi kuhusu Mungu, kwani kama kuna ufumbuzi, basi ni wazi ufumbuzi huo unapatikana kwa Mungu huyohuyo.

Ufunuo Maalum (au “Ufunuo wa Kiroho”): Mungu, katika neema zake nyingi, humpa nafasi mwanadamu yeyote anayeonyesha kiu na shauku ya kumfahamu Yeye baada ya kujua kweli ya msingi ya uwepo Wake, ambayo inaonekana kwa kutafakari ilimwengu. Wakati wowote mtu fulani anapotambua uwepo wa Mungu kwa ufunuo unaotokana na kutafakari uumbaji na akiwa na shauku ya kufahamu zaidi, basi Mungu, kwa uaminifu mkuu humpa mtu huyu nafasi ya kuanza uhusiano Naye (humpa Injili), na nafasi ya kukua kiroho baada ya kuiamini Injili (katika dunia ya leo, hii ina maana mtu huyu hupewa Biblia, pamoja na mafundisho sahihi). Akizungumzia ujumbe wa Injili, Bwana Yesu alisema:

“… 4.14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.” Yoh. 4:14 (SUV); tizama pia Yoh. 3:5; Waefe. 5:26. Mungu hamwachi kamwe yeyote mwenye kiu ya kweli Yake aondoke bila ya kukidhi kiu hiyo. Kwa hakika Anawakaribisha wote tuje kwake na tunywe kiasi tunachohitaji pale katika Isaya 55:1:

“… 1 Haya, kila aonaye kiu, njoni palipo na maji …”

Hazina hii ya kweli aliyoiweka kwa ajili ya muumini na asiye muumini ambayo kwa kweli ni ya kiroho, huwezi kuiona kwa macho, inaitwa ufunuo maalum.

Katika historia ya wanadamu, Mungu ametumia njia mbalimbali za kuwasilisha kweli Yake kwa wanadamu, wake kwa waume, waliokuwa na moyo wa kuipokea kweli. Ametumia ishara (miujiza) na maono, malaika na ndoto, mitume na makuhani. Leo hii, chanzo pekee kilichopo cha kuipata kweli ya Mungu (ufunuo Wake maalum) ni Biblia. Lakini, japo inawezekana kwa mtu asiyemini kupata Injili iliyo katika Biblia yeye mwenyewe, na kwa muumini kupata kanuni fulani za kweli bila kusaidiwa, hii siyo njia pekee ya kupata kweli ya Mungu. Ebu tutumie analojia (hali ya kufanana) hapa, kama Biblia ni kijito ambamo maji ya kweli yanapatikana, namna nzuri ya kufanikisha kukidhi kiu yako ni kutumia kata ya kuchotea maji. Kama vile kijito hiki kilivyo na maji lakini hakijatengenezewa njia ya asili ya kukidhi kiu ya maji hayo, vivyo hivyo Biblia ina habari yote ambayo asiyeamini anahitaji ili aokolewe, na habari yote ambayo muumini anahitaji ili akue kiroho, lakini haiko katika namna ambayo inaweza kutumika kwa urahisi kwa sababu iko katika mfumo wa fasihi na siyo maelekezo ya ‘namna ya kutumia’ kama ‘user manual’ ya tv au simu janja.

Hii ndiyo maana Mungu ameteua katika Kanisa lake waalimu wa Biblia ili kuiweka habari iliyomo ndani ya Biblia katika mfumo unaoweza kueleweka kwa urahisi zaidi. Hivyo kila muumini anapaswa kusoma Biblia yeye mwenyewe, lakini pia anapaswa kupata mafundisho ya misingi iliyomo kutoka kwa walimu wa Biblia waliofuzu. Hivyo kama kweli uko makini na suala la kukua kiroho, unapaswa kutumia njia zote mbili za kupata kweli.

Mtu asiyeamini anaweza kuzunguka ndani ya Biblia kwa miezi kadhaa bila kuona Injili, haswa kama akianza katika Agano la Kale (japokuwa kwa hakika Injili imo katika Agano hilo – soma Yoh. 5:39). Mara nyingi, lakini, hakuna sababu ya mtu huyu kutumia njia ndefu na ngumu kama hii – ya kuhangaika yeye mwenyewe kupata Injili. Hii ni kwa sababu Mungu ametoa neema ya “kata” za kumwezesha mtu huyu achote na anywe ‘maji ya uzima’ kutoka katika kijito cha haya maji. “Kata” hizi ni nini basi?, utauliza. Jibu: kata hizi za kuchotea na kunywea maji ya uzima ni wewe na mimi! Sisi Wakristo ndio “kata” ambazo anatumia mtu ambaye hajapata ujumbe wa Injili ili anywe maji ya uzima ya habari hiyo njema – 2Wakor. 4:7. Hii ndiyo sababu sisi sote tunaoamini tunapaswa kuielewa Injili kwa uwazi, ili tuweze kumweleza kwa ufasaha mtu anayetaka kuujua wokovu wa Bwana wetu Yesu Kristo.

“Injili” ni neno la Kiswahili ambalo maana yake ni “habari njema”; linatokana na neno la Kiyunani euangelion. Kwa kweli hakuna “habari njema” zaidi ya kusikia kwamba Mungu ametupatia (sisi) njia ya kuepuka hukumu Yake na kuwa na uzima wa milele! Tunapompa habari hii njema mtu ambaye hajaokolewa, sisi tunakuwa ile “kata” ambayo imepewa heshima ya kubeba maji ya uzima, kweli ya Mungu kuhusu Bwana Yesu Kristo ambayo ndiyo habari njema ya Injili. Hakuna shaka kwamba ni mapenzi ya Mungu kuwa tunafanya hivyo kila wakati tunapopata fursa, kwani “… anataka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli” - 1Tim. 2:4; pia 2Pet. 3:9; Yoh. 3:16. Hivyo tunalitumia neno “Injili” kwa maana hii: habari njema ya Bwana Yesu Kristo; kwamba kwa kumwamini Yeye, tunaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu na kuwa na uzima wa milele.

Sasa, japo Injili ina taswira nyingi, na inagusa kanuni nyingi za maandiko, mwanzoni kabisa mtu asiyeamini anapaswa tu kuelewa na kuamini amri ya Mtume Paulo katika Matendo ya Mitume 16:31: “mwamini Bwana Yesu, nawe utaokolewa”, kwani wowkovu unapatikana kwa neema ya Mungu, kwa imani katika Yesu Kristo – Waefe. 2:8-9. Hivyo mtu asiyeamini anaweza kuokolewa bila hata kusoma Biblia. Kiu yake inamalizwa kwa urahisi na kwa haraka, lakini maji ya kweli yanayoimaliza kiu hii yanatoka kwenye chanzo ambacho ni Biblia. Maji yale yametoka kwenye Biblia yakaingia kwenye moyo wako, yakaingia moyoni mwake, na hapo yakafanikisha kazi ambayo Bwana ameikusudia – Isa. 55:10-11.

Tuseme nini juu ya huyu muumini basi? Kanuni ya ile kata ya maji inatumika kwa huyu muumini pia. Wakati wowote tunapowasaidia waumini wengine kujifunza Neno la Mungu, tunatumika kama ile kata ya maji ya uzima. Prisila na Akwila walifundishwa misingi ya kweli na Paulo, na hivyo walikuwa na uwezo wa kumwelekeza Apolo “kwa usahihi” kuhusu namna ya kuwa Mkristo – Matendo 18:24ff (ff inamaanisha “na mistari inayofuata”). Hivyo sote tuna jujumu la kuitamka ile kweli, kila mmoja kwa mtu mwingine – Waefe. 4:15,25. Yaweza kuwa ni mafundisho ya kanuni fulani tuliyojifunza, au neno la kutia moyo, sisi sote tunawajibika “kufundisha” wakati fulani. Kwa njia hii, Kanisa linajengeka kama vile waumini walio katika Kanisa hilo wanavyojijenga kwa njia ya kusaidiana – Waefe. 4:16; Wakolosai 2:19. Wakati wowote tunapozungumza na waumini wengine, tunapaswa kukumbuka “kuweka chumvi ya neema katika maneno yetu siku zote” - Wakol. 4:6, mkiwatia watu moyo kwa kutumia nguvu iliyo ndani ya kweli ya Mungu. Kukua kiroho kuliko endelevu kunahitaji “kujilisha” chakula kilichotayarishwa vizuri, na ndiyo maana Mungu ameweka “kipaji” cha “mwalimu” katika orodha ya vipaji vinavyotolewa kwa Kanisa lake – Waefe. 4:11ff. Baadhi ya vitu muhimu sana katika mchakato wa kukua kiroho, yaani mchakato wa kuingiza rohoni kweli ya Mungu ni:

(1) nia thabiti,
(2) unyenyekevu,
(3) mafundisho ya Biblia yaliyopangwa, na
(4) Huduma ya Roho Mtakatifu.

Mapitio: Shabaha ya maisha yetu kama Wakristo ni kupevuka kiroho na kuwasaidia Wakristo wengine katika jitihada zao za kukua kiroho. Kupevuka kiroho kunatokana na kuielewa na kuitumia kweli ya Mungu katika mazingira yako ya hapa duniani. Japo tunaweza kujua mambo kadhaa yanayohusu kweli ya Mungu kwa kuchunguza ulimwengu (natural revelation), na tunaweza kuokolewa kwa kuelewa na kuamini jambo moja tu la kweli (Injili: wokovu unapatikana kwa imani yako kwa Kristo), kupevuka kiroho kunahitaji kujifunza na kuelewa mfumo wote wa kweli iliyo ndani ya maandiko. Katika somo lijalo tutachunguza dondoo zinazohitajika ili kuielewa kweli, na kutazama mchakato unaotumika katika kufanikisha kupevuka kiroho.

=0=

Translated from: Natural and Special Revelation: Peter’s Epistles #11

=0=

Basi, na tuonane katika somo la 12 la mfululizo huu, kwa neema za Mungu, Amina!