Imani na Damu ya Yesu Kristo: Nyaraka za Mtume Petro #9

 

Na Dr. Robert Dean Luginbill

Wa https://ichthys.com

 

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

 

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill

Permission For This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by

Dr. R. D. Luginbill

 

1Petro 1:1-2: (1) Petro, Mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule ambao japo wametengwa na kutawanywa katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia,

(2) wamechaguliwa na Mungu Baba kwani Aliwajua toka mwanzo kwa utakaso wa Roho Mtakatifu, hata mkapata kutii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani ziongezwe kwenu! (Revised Translation)

 

Mapitio: Katika somo lililopita tulizungumzia maelezo ya hatua tatu za hadhi yetu kama “wateule tuliotengwa”. Katika macho ya dunia tunaweza kuonekana si chochote na tunaweza kuonekana hatuna chochote, lakini licha ya hili, tumechaguliwa mahususi na Mungu tuwe watoto katika familia Yake kwa sababu ya imani tuliyo nayo kwa mwanawe Yesu Kristo. Zaidi ya hayo, kila Mmoja katika Utatu Mtakatifu alishiriki katika uchaguzi wetu:

 

  • Mungu Baba alipanga uchaguzi wetu (kutokana na ufahamu Wake kabla hata hajatuumba: yaani alijua kwamba tutamwamini Mwanawe, hivyo alipanga mazingira ya maisha yetu ili kuliwezesha tukio hilo)

  • Mungu Roho Mtakatifu alitimiza uchaguzi wetu (kwa kututakasa: kwa kututenganisha kimsingi na yote ambayo ni ya kidunia, na kututakasa ili tumtumikie Mungu)

  • Mungu Mwana akalipia uchaguzi wetu (kwa kutugomboa: yaani kwa kulipia gharama ya kututoa katika utumwa wa dhambi kwa kifo chake msalabani kwa ajili yetu)

 

Ufafanuzi: Hii inatuleta (tunapochambua andiko la 1Petro 1:1-2) katika usemi wa mwisho wa aya ya 2, unaoashiria tendo lililotokea zamani: “mlichaguliwa … kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo”. Hapa, neno “kwa” limetangulia na kusimamia maneno “utii” na “kunyunyiziwa”, na linatumika kuonyesha lengo la uchaguzi wetu kuhusiana na Yesu Kristo. Hapa Petro anatuambia kwamba kuingia kwetu katika familia ya Mungu, msingi wake ni kazi aliyoifanya Bwana Yesu Kristo msalabani, kwa sababu Yeye ndiye mlengwa wa imani yetu (yaani sisi tunaweka imani ya wokovu wetu katika Nafsi Yake; ndiyo sababu “tumechaguliwa … kwa utii katika damu ya Yesu Kristo”: ili tupate fursa ya kumwamini) na pia Yeye ndiye anayelipia gharama ya wokovu wetu (yaani Yeye ndiye ameweka uwezekano wa wokovu wetu; ndiyo maana “tumechaguliwa … katika kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo”: ili kwamba tunapomwamini Yeye tunagombolewa kutoka utumwa wa dhambi). Maneno “kwa utii” yanatuelekeza kwenye imani yetu katika Yesu Kristo na kazi yake msalabani kwa ajili yetu, na maneno “kwa kunyunyiziwa”, yanatuelekeza kwenye “kugombolewa”, “kukoshwa” kwa dhambi zetu pale tunapomkubali na kumpokea Yeye kama mwokozi wetu.

 

Kabla ya majira au historia kuanza, Mungu Baba alipanga uchaguzi wetu kutoka katika himaya ya giza ya Shetani na kuingia katika ufalme Wake wa uangavu (Wakol. 1:13), na Roho Mtakatifu anatekeleza mabadiliko hayo wakati wa uhai wetu hapa duniani tunapoamini. Lakini Bwana Yesu Kristo ndiye aliyelipia gharama ya wokovu wetu katika wakati ule mwafaka kihistoria alipoenda msalabani kwa ajili yetu – Waebr. 9:26b.

 

Wokovu: Kwanza, neno “wokovu” maana yake ni ukombozi, uhuru. Wazo kuu hapa ni kwamba tumekombolewa na Mungu kutoka katika janga kuu na kupelekwa katika sehemu ya usalama. Sasa, tumeokolewa kutoka katika kitu gani haswa? Tumeokolewa kutoka hukumu ya Mungu baada ya kifo, na lile ziwa la kutisha la moto – Waebr. 9:27, Ufu. 20:11-15. Tumeokolewa kwa ajili ya nini? Kwa ajili ya ufufuo na furaha ya milele mbinguni - 2Wakor. 5:1-10.

 

Ni muhimu kukumbuka wakati wote kwamba wokovu huu haukupatikana bure. Umelipiwa. Kutoka kwa mzazi wetu wa kwanza Adamu, sote tumerithi mwili wa dhambi - War. 5:12-14, hali ambayo Paulo anaiita “dhambi ikaayo ndani yangu” - War. 7:20. Matokeo yake ni kwamba sisi sote hutenda dhambi - War. 3:23. Sasa, kwa sababu Mungu ana utukufu mtimilifu na kamwe habadiliki (yaani hachanganyiki na uovu wa aina yoyote) na habadiliki katika uongofu Wake (yaani hawezi kuruhusu uovu wa aina yoyote – Zab. 7:9-11), sisi wanadamu tuna tatizo kubwa. Tunawezaje kumridhisha Mungu aliye mtimilifu au tunawezaje kuishi Naye milele wakati tuna hii hali ya dhambi – Waebr. 10:30-31? “Jema” lolote tunalotumaini kulitenda ni lazima litaingia doa na kupata “harufu” ya hali yetu ya dhambi – War. 4:2; Waefe. 2:8-9; 2Tim. 1:9; Tito 3:5; cf. Kumb. 9:5-6; Isa. 64:6. Na kama vile hilo tatizo halitoshi, tunakabiliwa na kitanzi kingine pia: “kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa ...” - Waebr. 9:27. Hata kama tungeweza kujaribu kumfurahisha Mungu, bila Yeye kuingilia kati sisi ni watu wa kufa tu.

 

Kwa kifupi, hakuna kitu ambacho mwanadamu mwenye dhambi anaweza kufanya ili kujiokoa mwenyewe. Ni utambuzi wa ukweli huu muhimu na wa maana sana, ambao unatenganisha Ukristo halisi na “dini” zote nyingine. Watu wengi katika dunia hii (pamoja na baadhi ya Wakristo) wanajaribu kwenda mbinguni kwa kupitia matendo yao mema. Lakini Mungu ameridhika na kazi ya Kristo pekee. Katika busara na neema Zake nyingi, Mungu alipata njia ya kusamehe dhambi kwa haki. Hulka Yake timilifu haiwezi kuruhusu dhambi isiadhibiwe, hivyo Alipata Mbadala ambaye alikuwa tayari kubeba adhabu ya dhambi za wanadamu wote: Mwanawe Yesu Kristo. Hivyo ni kwa imani tu (kitendo rahisi cha moyoni na katika utashi wetu, kisichostahili ‘sifa’ wala thawabu yoyote) katika Yesu Kristo ambapo tunamkubali na kumpokea Yeye na kifo Chake kwa ajili yetu, na matokeo yake sisi tunakubalika na Mungu Baba. Hivyo ule usemi katika aya ya pili, “mumechaguliwa … kwa utii katika damu ya Yesu Kristo” unazungumzia huku kukubali kwetu ile kazi ya Kristo msalabani alipobeba dhambi zetu – Isa. 53:1-12; na usemi “mumechaguliwa … kwa kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo” unaelezea kuhusu msamaha wa dhambi zetu ambao tunaupata pale tunapoamini. Utiifu ambao Mungu anautaka kutoka kwa watu wote ni, kwanza kabisa, wamwamini Mwanaye Yesu Kristo, kuikubali na kuipokea dhabihu aliyoitoa kwao. Kunyunyiziwa (kusamehewa kutokana na wokovu) kunahusiana moja kwa moja na imani, katika aya hii. Bila imani kwa Kristo, hakuna msamaha wa dhambi, bali katika imani kwa Kristo, msamaha wa dhambi unafuata papo hapo.

 

Tutakuwa na fursa katika masomo yajayo kuichambua kanuni ya kugombolewa (yaani kazi ya Kristo msalabani kama iivyolengwa moja kwa moja katika kutatua tatizo la dhambi: Alitununua kutoka utumwani mwa dhambi), upatanisho (kazi ya Kristo msalabani ilivyoelekezwa kwa Mungu Baba: sadaka ya Kristo ilikubaliwa na Mungu Baba, na ikalipia dhambi za watu wote, kwa wakati wote). Ebu tuzungumzie kidogo kuhusu “taswira” inayohusishwa na neno “kunyunyiziwa” kama lilivyotumiwa na Petro katika aya ya pili.

 

Kunyunyiziwa Damu: Ishara ya damu iliyonyunyizwa inatolewa kutoka katika Agano la Kale, mahususi kutoka katika ibada ambazo Mungu alianzisha kwa wana wa Israeli ili kuwafundisha kanuni zake mbalimbali. Baada ya Musa kumaliza kusoma “kitabu cha agano” (yaani Sheria ya Musa kama ilivyoelezwa kwa muhtasari katika Kutoka 20:1-23, akafanya “sadaka za amani”, na akakinga damu ya wanyama wote akisema, “tazama, damu ya agano”. Damu iliwakilisha kifo cha kuchinja (kama ilivyokuwa katika dhabihu zote za Agano la Kale), na msemo “damu ya agano” ulimaanisha kwamba kwa kifo cha mbadala, wana wa Israeli waliingia katika makubaliano na Mungu. Ukweli huu ulidhihirika na kuonyeshwa na Musa pale aliponyunyiza damu iliyotoka kwa wanyama waliochinjwa. Kitendo hiki kinaweza kuwa cha kutisha na kushitua kwetu sisi, lakini hilo ndilo lilikuwa lengo lake. Sadaka ya Kristo pale msalabani Imemgharimu kiasi ambacho hatuwezi kujua. Hatukufanya kitu chochote kumsaidia, sisi “tunanyunyiziwa” damu Yake tu. Tunapata faida ya sadaka ya kifo chake pale tunapomwamini, tunapoikubali kazi Yake kwa ajili yetu.

 

Damu ya Kristo: Damu ya Kristo, kwa upande mwingine, ni ishara tu, siyo damu halisi. Musa alitumia damu halisi kuwakilisha mateso na sadaka au kifo cha masihi anayekuja, lakini Bwana Yesu alitupatia wokovu, mimi na wewe, kwa kwenda msalabani na kufa kwa ajili yetu. Alipomaliza kazi hii, alitoa pumzi ya mwisho na kufa – Luka 23:46. Hakutoka damu hadi kufa – Yohana 19:33-35. Ni muhimu kwetu kuitizama ile sadaka na mateso ya Kristo wakati akihukumiwa kwa niaba yetu, kwa ajili ya dhambi zetu, na siyo kwa ishara ya Agano la Kale ambayo ilikuwa kivuli cha mateso na sadaka ile. Hivyo Biblia inavyosema kwamba “tunaokolewa kwa damu ya Kristo”, inamaanisha kujitoa kwake kwa upendo mkuu kuwa sadaka, kufa kwake msalabani, na siyo damu Yake halisi (kama Yohana anavyotufundisha, katika sura ya 19 ya Injili aliyoiandika).

 

Muhtasari: Sentensi ya kwanza ya Petro ni maelezo yenye vipengele 3 vya uteule wetu kuingia katika familia ya Mungu.

 

  • Mungu Baba anapangilia wokovu wetu (kujua Kwake historia yetu yote kabla hatujazaliwa)

  • Roho Mtakatifu anashughulikia mpango huo kiutekelezaji (utakaso)

  • Mungu Mwana ndiye analipia (anagomboa), nasi tunaweka imani yetu ya wokovu wetu kwake

 

Taswira hii yenye vipengele 3 ya awamu ya kwanza ya Mpango wa Mungu kwa maisha yetu (wokovu) inatumika pia katika awamu ya pili ya Mpango wa Mungu kwa waumini wote (muumini katika majira au historia: tizama somo #3 kwa maelezo ya awamu zote za Mpango wa Mungu):

 

  • Mpango wa Baba unatupatia namna ya kujikimu katika maisha yetu, katika historia

  • Kazi ya Bwana Yesu inaendelea kututakasa [kila] tunapotubu dhambi

  • Roho Mtakatifu anatusaidia katika kupevuka kiroho

 

Tutayazungumzia haya kwa kirefu katika somo linalofuata.

 

=0=

 

Translated From: Faith and the Blood of Christ: Peter’s Epistles #9

 

=0=

 

Basi, na tuonane katika somo #10 katika mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!