Matokeo ya Uteule Wetu: Nyaraka za Petro #8

 

Na Dr. Robert Dean Luginbill

Wa https://ichthys.com

 

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

 

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill

Permission for this Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by

Dr. R. D. Luginbill

 

1Petro 1:1-2: (1) Petro, Mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule ambao japo wametengwa na kutawanywa katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia;

(2) wamechaguliwa na Mungu Baba kwani Aliwajua toka mwanzo kwa utakaso wa Roho Mtakatifu, hata mkapata kutii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani ziongezwe kwenu! (Revised Translation)

 

Mapitio: Tumeona kwamba kama Wakristo, sisi ni wateule au tuemchaguliwa na Mungu maalum kuwa watu Wake. Kwa sababu Bwana Yesu Kristo alikuwa tayari kwenda msalabani kwa ajili ya wanadamu, Mungu Baba amewapa watu wote fursa ya kuwa wateule. Sote tuna uhai na tuna utashi, hivyo sote tuna nafasi ya kumwonyesha Mungu utayari wetu katika suala muhimu la kumfahamu Yeye. Msingi wa uteule wetu (au kuchaguliwa kwetu) ni uamuzi wetu wa kumwamini Bwana Yesu Kristo. Katika aya ya 2 ya 1Petro 1-2, Petro anaainisha dhima tofauti za kila Mwanajumuia wa Utatu Mtakatifu katika mchakato huu wa kutuchagua sisi kuwa sehemu ya familia ya Mungu na mpango wa Mungu.

 

1. Mungu Baba alipanga kuingia kwetu katika familia Yake kama Wakristo, hata kabla ya kuumbwa ulimwengu huu. Tumejifunza mada hii kama kanuni ya uwezo wa Mungu wa “kufahamu kabla ya tukio”, kwa Kiyunani prognosis, kwa Kiingereza foreknowledge, katika masomo yaliyopita (Petro #2 na Petro #5). Mungu anajua kila kitu. Hii ina maana kwamba anajua yote yaliyokuwako, yaliyoko sasa na yote yatakayokuwako. Anayajua yaliyotokea, yanayotokea sasa na yatakayotokea, kiuhalisia na yale ambayo siyo halisi, yaani yote ambayo yangetokea ikiwa maamuzi tofauti yangefanyika na/au matendo tofauti yangetendwa. Alitujua sisi kabla hajaumba ulimwengu – War. 8:29. Hii ina maana kwamba Mungu Baba alijua kwamba tutaamua kumwamini Mwana Wake Yesu Kristo kabla hata hatujazaliwa, na akaufanya Mpango Wake na maisha yetu katika namna ambayo itatupa fursa ya kufanya hivyo. Pale tunapotimiza hili na kuamini katika Bwana Yesu Kristo, ndipo tunaingia “rasmi” katika familia ya Mungu, lakini Baba alilijua hili kabla na alilipangia mazingira yake kabla ili lipate kutokea. Petro anaupa sauti ukweli huu anaposema kwamba “tumechaguliwa – katika kujulikana kabla na Mungu”.

 

2. Mungu Mwana ameulipia uchaguzi wetu, kwa kutimiza ile kazi kuu ya Mpango wa Baba. Amefanya hili kwa kutugomboa, yaani kwa kulipia gharama ya kututoa sisi katika utumwa wa dhambi kwa kifo chake msalabani. Kwa sababu ya kazi Yake msalabani kwa ajili yetu, tumekuwa huru kutoka katika vikwazo vinavyotuzuia kuingia katika familia ya Mungu (tutapata fursa ya kujifunza kanuni za ukombozi katika masomo yajayo).

 

3. Roho Mtakatifu ndiye Wakala anayeutia nguvu Mpango wa Mungu Baba katika hatua ya utekelezaji wake, yaani katika historia. Katika Mpango huu, Mungu aliwachagua wafuasi wote wa Mwanaye tangu kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu – War. 8:28-30; pia tizama Wagal. 1:15. Tunapoweka imani yetu kwa Bwana Yesu Kristo, Roho Mtakatifu anatuingiza katika familia ya Mungu, nasi tunaingia kikamilifu katika huu “uteule” ambao kwa ajili yake tuliwekwa pekee (tulitunzwa, tulilelewa) tangu kuzaliwa, tunakamilisha hatua ya mwanzo ya “utakaso” au kuwekwa wakfu ambapo, kama washirika wa Kristo, sasa tumo chini ya ulinzi wa Roho Mtakatifu na tupo na uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu.

 

Yawezekana kuwa istilahi au maneno ya kiteolojia yaliyotumika hapo juu yakawa magumu, lakini dhana yake kwa uhakika ni rahisi tu. Mungu Baba alijua kwamba tutamwamini Kristo, hivyo alikamilisha mazingira ya maisha yetu kuwezesha tukio hilo lifanyike nasi. Wakati ule tunapomwamini Kristo, hadhi yetu inabadilika kabisa, kwani ni katika ile sekunde tunapoweka maisha yetu mikononi mwa Kristo ndipo tunachaguliwa ili tuwe kikweli wana wa Mungu.

 

Kwa sababu ya kuanguka kwa wazazi wetu wa mwanzo (Adamu na Eva), wanadamu wote wanazaliwa katika hali ya utengano na Mungu, kwani wote tunazaliwa tukiwa na dhambi War. 7:7-25. Hali hii mbaya ya wanadamu inadhihirishwa katika nyanja mbili:

 

  • hulka au mwelekeo tulio nao sisi sote, wa kutenda dhambi (War. 3:23; 1Wafalme 8:46).

  • ukweli usiopingika kuwa binadamu wote hufa kimwili, ambayo ndiyo adhabu ya kwanza ya dhambi (Mwa. 2:16-17).

 

Lakini, tunapoweka imani yetu na tegemeo letu kwa Bwana Yesu, Yeye ambaye alilipa adhabu ya dhambi zetu zote, hadhi yetu inabadilika kabisa, na “tunaokolewa kutoka katika ufalme wa giza na kuingizwa katika ufalme wa Mwana Wake mpendwa” – Wakol. 1:13. Mabadiliko haya katika hadhi yetu (pale tunapokuwa Wakristo) yana sura nyingi sana, na yanaelezwa katika namna tofauti katika maandiko:

 

  • Kuhalalishwa: Kwa mtazamo wa kisheria, kwa mfano, tunahalalishwa kwa imani yetu katika Kristo – War. 3. Hii ina maana kwamba japokuwa tulikuwa na hatia ya dhambi hapo mwanzo mbele ya Mungu, dhambi zetu na hatia yetu inaoshwa na imani yetu kwa Yesu Kristo.

  • Kutwaliwa: Namna nyingine ya kuieleza hadhi yetu kama Wakristo ni kwamba sasa sisi ni “watoto” wa Mungu. Paulo anaulezea mchakato huu kama “kutwaliwa” (adoption) na Baba kama watoto ambao hapo mwanzo walikuwa yatima, kwa wote wanaomwamini Kristo: sisi siyo watumwa tena wa sheria ya Mungu ambayo ilionyesha dhambi zetu kwa uwazi kabisa, bali ni watoto wanaopendwa katika Kristo Yesu Bwana wetu – Wagal. 3:21 – 4:7.

  • Utakaso: Petro anatilia mkazo sura nyingine ya “mabadiliko ya hadhi” yetu – ile ya “kuwekwa wakfu” au, kwa neno linalofahamika zaidi, utakaso.

 

Kanuni ya Utakaso: Mara tunapomwamini Bwana Yesu Kristo, moja kati ya yale yanayotutokea kupitia uwakala wa Roho Mtakatifu ni kwamba tunawekwa alama inayoonyesha kwamba sisi sasa ni tofauti na walimwengu wengine na pia tumekuwa watu mahususi kwake Yeye mwenyewe. Ebu tufanye uchunguzi kidogo wa dhana hii ya utakaso au kuwekwa wakfu na asili yake kisarufi. Neno la Kiingereza “sanctification” maana yake utakaso, msingi wake ni maneno mawili ya Kilatini: sanctus (maana yake kilichowekwa wakfu, kitakatifu, kilichotakaswa) na facio (maana yake kilichofanywa). Chanzo cha neno hilo la Kilatini ni kwamba limenyambuliwa kutoka kwenye mzizi wa Kiyunani hag. Kitenzi cha Kiyunani hagios kinamaanisha kitu “kilichotengwa kwa ajili ya miungu, kilichotakaswa, kitakatifu” (yawezekana umesikia habari za basilika lile maarufu la kale Hagia Sophia). Kwa upande wake, mzizi huu hag unahusiana na kitenzi cha Kiyunani hazomai, ambacho maana yake ni “kuogopa, kuhofia, kunyenyekea”. Kwa kifupi, mambo yote yaliyoitwa hag katika Uyunani ya kale yalikuwa chini ya utenganisho wa kidini, laana au ulinzi. Hivyo mambo yote yaliyohusishwa na neno HAG yalikuwa chini ya ulinzi wa kimungu. Zaidi ya hapo, mambo ya HAG yalikuwa tofauti na mambo ya kawaida ya kila siku ya kidunia. Yalikuwa mambo ya kipekee. Sasa, dhana zote hizi mbili zimo katika maelezo ya Kibiblia ya mambo yote ambayo tunayachukulia kwamba “yametakaswa”. Katika kutufanya hag, Baba Mungu ametutakasa, ametuweka wakfu, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu; ameweka alama Yake juu yetu kwa kutufanya tuwe tofauti na kututenganisha na watu wengine wa dunia hii. Hivyo utakatifu unaashiria kwamba muumini analindwa na Mungu na pia unaashiria uwepo wa mabadiliko chanya katika hadhi ya muumini. Sisi sio watu wa dunia hii tena. Sasa sisi ni watakatifu. Na mungu anatuamuru tutende matendo yanayodhihirisha hali hiyo yetu mpya:

 

Na muwe watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu.

1Petro 1:16 (cf. Walawi 11:44,45; 19:2; 20:7)

 

Utakaso (au kuwekwa wakfu) ni upande mmoja wa hadhi yetu mpya kama Wakristo. Kanuni hii inatufundisha kwamba sisi sasa ni watakatifu mbele ya Mungu. Sasa, neno utakatifu limepewa matumizi yanayosikitisha kidogo siku hizi. Petro anavyosema katika 1Petro 1:2 kwamba tumeteuliwa kwa njia ya utakaso wa Roho Mtakatifu, anamaanisha kwamba Mungu alitutenganisha kwanza na ulimwengu kabla hajatuchagua na kutuingiza katika familia Yake.

 

Ni kweli kwamba Roho Mtakatifu alifanikisha kutuingiza katika familia ya Mungu kwa kutufanya “watakatifu”, lakini utakatifu wa Kibiblia hauko kama watu wengi wanavyouchukulia maana yake. Kuna dondoo kadhaa kuhusu utakatifu halisi ambazo tunapaswa kuzingatia:

 

a. Utakaso Wetu ni Kazi ya Mungu: Ule utakatifu wa mwanzoni kabisa (utakaso au kuwekwa wakfu) anaopewa muumini na Mungu Baba kupitia uwakala wa Roho Mtakatifu (aya yetu ya 1Petro 1:2) ni kazi ya Mungu pekee. Tunamwamini Bwana Yesu Kristo, lakini hatufanyi “juhudi” yoyote na hatuna stahili yoyote katika tukio hilo. “Utakaso” tunaopata kama matokeo ya kuamini unasimamiwa na Roho Mtakatifu na hauhusishi “mwenendo wala matendo” ya aina yoyote kwa upande wetu, yawe mema au mabaya. Kama Wakristo, sisi ni “watakatifu” mbele za Mungu, yaani Yeye anatuchukulia sisi kuwa ni “hazina” Yake pekee, kwani tumetenganishwa na ulimwengu. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, na haitokani na stahili ya tendo lolote tulilotenda. Kwa upande mmoja, kama sisi tusingekuwa Wakristo, lakini tungeishi “maisha mema” ya kutii sheria za nchi na kupenda majirani zetu, tusingekuwa, kwa sababu hizo pekee, “watakatifu” mbele za Mungu; na kwa upande mwingine, hata kama, katika Ukristo wetu, tukiwa si watimilifu, bado sisi ni “watakatifu” mbele Yake (japo tunapaswa kukumbuka kwamba Yeye huchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wanawe wanaomkosea – Waebr. 12:1-13).

 

b. Utakaso Wetu ni Mchakato: Kama vile kulivyo na awamu tatu tofauti katika Mpango wa Mungu (awamu ya kwanza: wokovu; awamu ya pili: maisha ya muumini hapa duniani; awamu ya tatu: milele), vivyo hivyo kuna awamu tatu zinazolingana na hizo katika mchakato wa utakaso. Mpaka hapa, tumekuwa tukiijadili “awamu ya kwanza ya mchakato wa utakaso”. Tunapokuwa Wakristo, tunakuwa “watakatifu mbele ya Mungu” (awamu ya kwanza ya mchakato wa utakaso). Baada ya kifo, tutakuwa “watakatifu” milele katika ushirika na Mungu – Ufunuo 20:9, ambayo ni awamu ya tatu na ya mwisho ya mchakato wa utakaso. Lakini katika wakati wetu hapa duniani baada ya kuokolewa na kabla ya kifo, mambo ni magumu kidogo. Hapa duniani, mwenendo ni suala muhimu. Kwani, japokuwa ni kweli kwamba tunakuwa watakatifu kwa sababu tu ya hadhi yetu kama waumini wa Bwana Yesu kwa uwakala wa Mungu pekee, hatuachi mwenendo wetu mbaya wa kidunia hapo hapo, yaani mara baada ya kuokolewa. Kama waumini, tunaendelea kuishi ndani ya miili ile ile yenye dhambi - War. 7:20, na ulimwengu unaendelea kutushawishi tutende dhambi – 1Yoh. 2:15-17. Katika awamu ya pili ya mchakato wa utakaso mwenendo na tabia yetu vinapaswa kwenda sambamba na kukua kwetu kiroho, tukijipanga katika msitari wa hadhi yetu mpya kama Wakristo, kwa jinsi tunavyoendelea kukua katika Yeye. Kwa maneno mengine, tunapookolewa tunakuwa askari wa Bwana Yesu, lakini inachukua muda kidogo mpaka kuanza kuenenda kama nguli wa vita yetu hii ya kiroho. Alipowaandikia Wakorinto (1Wakor. 1:2), Paulo aliwaelezea wao kama “waliotakaswa katika Yesu Kristo” (awamu yao ya kwanza ya utakaso na hapo hapo anawaelezea kama “walioitwa kuwa watakatifu au walioitwa kuwa wateule wa utakaso” (ambalo ni lengo walilopewa na Mungu la kuenenda katika namna inayostahili katika hadhi yao hii mpaya). Ni katika kuendelea kukua kiroho pekee ndipo tuna matumaini ya kufanikisha agizo tulilopewa na Mungu la kuwa watakatifu katika marefu na mapana yake.

 

c. Utakaso Huanza Moyoni: Kitu muhimu sana cha kukumbuka ni kwamba utakaso wa kweli kama unavyofundishwa katika Biblia unaanza moyoni au ndani ya Mkristo, na baadaye unaonekana katika matendo yake. Haiwezekani kufanikisha maendeleo yoyote ya maana ya kiroho kwa kubadilisha mwenendo au tabia yako pasipo msaada wa maandiko na kukua kiroho. Wakati anakaribia kuondoka duniani (baada ya ufufuko) na akijua kwamba atawaacha waumini wake hapa duniani, Bwana Yesu aliomba kwa Baba kwamba “Awatakase kwa ile kweli” - Yoh. 17:17. Njia pekee ya kufanikisha maendeleo halisi kuelekea utakatifu ni kukua kiroho, msingi wake ukiwa ni kuukubali/kuupokea, kuuamini na kuutumia ukweli wa maandiko. Tutakuwa na mengi ya kusema kuhusu kukua kiroho katika masomo yafuatayo, lakini ebu tugusie tu hapa misingi yake: unapokea kweli ya Biblia kwa kusoma na kufundishwa (kwa usahihi) Neno la Biblia; unaamini unayosoma na kufundishwa; unaanza kuitumia misingi unayofundishwa katika maisha yako. Unapoendelea na mchakato huu wakati wote, utakua kiroho na mwenendo wako utabadilika. Utakapozidi kukua kiroho na unaona mabadiliko katika mwenendo wako, unafikia mahala ambapo Roho Mtakatifu anakuongoza katika maamuzi yako, anakukumbusha pale unapofanya yale yasiyo sahihi au unapoacha kufanya maamuzi mema na sahihi; unapozidi kupevuka kiroho, ndivyo mabadiliko yako yanavyozidi kuwa halisi na chanya (na ya kudumu). Mabadiliko ya tabia kama haya yanafaa kufanyika kutokana na mafundisho ya kweli na halali ya maandiko, na yana faida zaidi yakitazamwa kiroho, kuliko yale mabadiliko yanayotokana na shinikizo la kijamii, au kutokana na tabia au mazoea ya ya kipekee ya kikundi au mtu fulani.

 

Kuzuia “Chokaa”: Bwana wetu aliwaita Mafarisayo “makaburi yaliyopakwa chokaa” kwa sababu “utakatifu” waliouonyesha ulikuwa wa nje tu. Walienda kubatizwa (na Yohane Mbatizaji). Walienda hekaluni na walishiriki kikamilifu katika shughuli za kidini. Walitoa zaka zao na walisali kwa usahihi mbele za watu. Lakini Bwana Yesu hakushawishika na tabia hizo. Siyo tu kwamba Mafarisayo wale walishindwa kuonyesha utakatifu halisi, bali hawakuwa na imani ya kweli kwa Mungu kabisa. Kwa nje, kwa mtu anayewatizama kwa juu juu tu, walikuwa kama chokaa safi. Lakini ndani yao walikuwa na uchafu wa kila aina. Mungu anajihusisha na mioyo yetu; anataka iwe safi, na kama tunaiweka safi kwa bidii na kukiri dhambi zetu Kwake na kuendelea kujifunza na kusoma Neno Lake takatifu, tutapevuka kiroho, na haya mabadiliko halisi ya ndani yataonekana mpaka nje kwa dhahiri kabisa.

 

=0=

 

Translated from: Peter’s Epistles #8: The Results of Our Election by God.

 

=0=

 

Basi, na tuonane katika somo la tisa la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!