Neema Katika Mateso: Nyaraka za Petro #6

 

Na Dr. Robert Dean Luginbill

Wa https://ichthys.com

 

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

 

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahsusi na Dr. R. D. Luginbill

Permission for this Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by

Dr. R. D. Luginbill

 

1Petro 1:1-2: (1) Petro, Mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule ambao japo wametengwa na kutawanywa katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia;

(2) wamechaguliwa na Mungu Baba kwani Aliwajua toka mwanzo kwa utakaso wa Roho Mtakatifu, hata mkapata kutii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani ziongezwe kwenu! (Revised Translation)

 

Mapitio: Na tuchukue muda kidogo kujikumbusha uhusiano kati ya mada zetu mbili za mateso ya Wakristo na kupevuka kiroho katika nukuu ya hapo juu. Wasomaji walengwa wa barua ya Petro walikuwa katika wakati mgumu, na katika huzuni zao, walianza kumshakia Mungu, hali ambayo ilihatarisha kasi yao ya kukua kiroho. Katika kuwaita “wateule waliotengwa”, Petro alikuwa anawakumbusha kwamba Mungu hajawasahau.

 

Changamoto ya Maisha: Katika kufafanua/kufasili mwonekano wa mgongano katika kuwa wateule na watengwa kwa wakati mmoja, tuliona katika mjadala wa Mpango wa Mungu (tizama somo #3) kwamba Mungu hawatoi ulimwengini waumini Wake mara tu wanapoamini, na badala yake anawaacha hapa hapa duniani ili waweze kupevuka kiroho, na kuwasaidia waumini wengine ili nao waendelee hivyo hivyo. Mtihani huu wa hiari yetu ya moyoni unatupa fursa ya kudhihirisha kwamba tunampenda Mungu zaidi ya vyote licha ya magumu ya maisha, na pia inampa Mungu fursa ya kutuonyesha kwamba anaweza kutulinda, kutubariki na kutuzawadia furaha Yake timilifu bila kujali shida ambazo maisha yanatuletea.

 

Nyenzo Nyingi, Zisizokuwa na Kiasi, za Mungu: Mtu asiyeamini hupata mateso katika maisha yake duniani bila kupata msaada wala kuwa na tegemeo, na hatima yake ni adhabu mara baada ya kifo chake cha kimwili. Kwa upande mwingine, sisi tunaoamini tunafaidika na rasilimali za neema kuu ya Mungu katika kukabiliana na kupambana na mateso yanayokuja katika maisha yetu, na tunahakikishiwa kwamba katika maisha yajayo hatutateseka (tena) milele. Zaidi ya hayo, tunajua ya kwamba katika kuendelea kwetu kumtegemea Mungu licha ya shida zetu zote, tunapevuka kiroho, na tutapata thawabu kwa kupevuka huko na kwa matunda tunayozaa, katika milele ijayo. Maisha ya Mkristo ni vita ya kudumu ya maisha yake yote ya hapa duniani, haikomi mpaka tutakapokutana na Bwana uso kwa uso.

 

Uwanja wa Vita: Mahala pa kwanza kabisa ambapo vita hii inapiganwa ni mioyoni mwetu au ndani ya nafsi zetu. Hivyo tunapaswa kuchukua tahadhari katika udhibiti wa mtazamo wetu kuhusiana ya magumu yanayotukabili. Kishawishi cha dhambi ni mbinu ya waziwazi ya adui yetu (Shetani) katika vita hii, lakini pia anayo mbinu nyingine ya ujanja zaidi, ya kutuletea shambulizi la mateso katika maisha yetu. Hii mbinu ya pili ya mashambulizi ndiyo iliyokuwa inawakabili walengwa wa barua ya Petro. Dhiki inaweza kumfanya muumini kupoteza imani katika uwezo wa Mungu wa kumsaidia. Kukabiliana na magumu kunamfanya Mkristo atake kuuliza: “kwa nini mimi ee Mungu?” ambao ni mwenendo hatari sana, kwa sababu ukiachwa uendelee utapelekea Mkristo huyu kumlaumu Mungu kwa matatizo anayoyapata: (“Mungu hanijali”), au kujilaumu yeye mwenyewe: (“labda nimetenda dhambi kubwa sana!”). Ebu tuzichambue aina hizi za mashaka kwa undani zaidi:

 

Swali la uwongo #1:

 

“Bado ninaendelea kupata magumu! Je, Mungu hanijali?”

Shida, kama tulivyoona, ni sehemu ya Mpango wa Mungu kwa kila Mkristo (1Petro 4:12). Bila ya magumu, hakuwezi kuwa na kupevuka kiroho – Yakobo 1:2-5. Mungu anatupima na dhiki ili kuimarisha imani yetu, kudhihirisha uaminifu Wake kwetu na kutuonyesha sisi (na kuwaonyesha watu wengine) kwamba tumepiga hatua kiroho, na kwamba tuko tayari kumtegemea Yeye katika nyakati za magumu na nyakati za mema.

 

Wazo la pili lisilo sahihi (wazo kwamba magumu ni aina fulani ya “malipo kutoka kwa Mungu” kwa dhambi tulizotenda zamani) nalo ni hatari pia. Ama kwa hakika, neno “mateso”, tunapolitumia kuhusiana na shida za waumini Wakristo kwa kiasi fulani linapotosha maana halisi, kwani kuna tofauti za msingi kati ya magumu ya muumini Mkristo na ya mtu asiyeamini. Sababu pekee ya dhiki wanazopata Wakristo inayofanana-fanana (kwa mbali) na dhiki wanazopata wasioamini ni ile inayosababishwa na adabisho la Mungu (Waebr. 12:1-13), na tumeona kwamba Mungu anapotuadhibu, hafanyi hivyo kama hakimu mwenye hasira, bali kama Baba mwenye upendo ambaye lengo lake ni kutusahihisha ili tufuate njia iliyo sahihi. Zaidi ya hayo, tunapokiri dhambi zetu, mabaki yoyote ya adhabu yanayokuwepo sasa yanakuwa ni dhiki kwa ajili ya baraka (kwa sababu baada ya kurejeshwa kwenye ushirika Wake, tunakuwa na faraja na msaada Wake katika kuikabili dhiki hiyo). Magumu mengine yote (tizama somo la Petro #5) tunayokabiliana nayo ni sehemu ya Mpango wa Mungu kwa faida yetu – War. 8:28. Tunapaswa kujifunza kumtegemea Yeye katika nyakati hizi za mitihani, kwani kwa uhakika anatujali.

 

Swali la Uwongo #2:

 

“Bado nina maumivu! Je, Mungu bado ana ghadhabu na mimi?” Tunapokiri dhambi kwa Mungu, Anatusamehe dhambi papo hapo, na bila masharti – 1Yoh. 1:9. Tunaporudi kwenye ushirika Wake kwa kukiri dhambi zetu Kwake, dhiki yote katika maisha yetu inakuwa si kwa malengo ya adhabu tena bali ni kwa malengo ya baraka – 1Wakor. 11:31. Japo wajihi wa toba ni sahihi tunapokiri dhambi zetu na inawezekana tukajutia kikwelikweli tendo lile baya tulilotenda (na kwa hakika adabisho litauma!), haifai kuwa na hisia zilizokithiri za hatia nafsini mwetu na kusononeka kupita kiasi mbele za Mungu. Hata katika magumu, Mungu anataka tuwe na furaha ili tuone uwezo Wake na baraka Zake vikitendeka katika maisha yetu. Tukikumbuka hili, hakuna sababu ya kuwa na msongo wa mawazo kutokana na kitu chochote tutakachokabiliana nacho katika maisha yetu. Mungu ametupatia uwezo, si tu wa kuwa wavumilivu katika Mpango Wake, lakini pia kuwa na furaha na amani. Kama inaendelea “kuuma” baada ya kukiri, basi tukumbuke kuwa Yeye hana ghadhabu dhidi yetu: mabaki ya maumivu kama hayo ni kwa faida yetu, ili tupate ufahamu, tusijisahau tena siku zijazo; hayo yanatoka kwa Mungu wetu ambaye hapendi kutuona tunaumia, kama vile wazazi au walezi wa hapa duniani wanavyomuadabisha mtoto aliyekosa.

 

Nyenzo za Neema ya Mungu Anazotupa Kutusaidia Kustahamili Magumu:

 

1. Mpangilio wa Neema wa Mungu katika Ujumla Wake: Maandiko yanatufundisha kwamba tunaokolewa “… kwa neema, kwa njia ya imani”, na kwamba hii ni “zawadi kutoka kwa Mungu” na siyo “kwa matendo yetu” - Waefeso 2:8-9.

Neema ni mpango timilifu wa Mungu katika kumsaidia mwanadamu aliye na dhambi. Yeye anafanya kazi, sisi tunapata faida za kazi Yake na tunaneemeka; na maandiko yako wazi kabisa katika kutuambia kwamba kazi yetu haichangii chochote katika wokovu wetu, bali wokovu unapatikana tu kwa sababu ya kazi aliyoifanya Bwana Yesu Kristo. Pale msalabani, Kristo aliteswa na kufa kwa ajili yetu sote. Jambo hili Mungu alitufanyia kwa “neema” zake, yaani alitufanyia bila ya malipo yoyote kutoka kwetu kwa neema zake, akitupatia zawadi na si tuzo kwa kitu chochote tulichofanya. Hivyo basi, tunaokolewa tunapomwamini Bwana Yesu Kristo. Matokeo ya wokovu huu ni kwamba tunatizama mbele katika maisha yetu kwa mategemeo yaliyojaa tumaini (Kiyunani elpis, tumaini) na tunaiona siku ile ambapo hakutakuwa na mateso teno. Alipohukumiwa kwa ajili yetu na kwa ajili ya dhambi zetu, Bwana Yesu alikamilisha kazi pekee yenye ustahili (merit) katika mpango wa Mungu, na tendo hili lilifungua “ile hazina kuu” ya neema za Mungu kwa waumini wote.

 

Mungu anahusiana nasi baada ya wokovu kwa namna ile ile aliyohusiana nasi kabla ya wokovu: kwa njia ya neema. Baada ya wokovu tunapewa baraka na karama nyingi kama watoto Wake. Baraka kuu ya kwanza ni wokovu na pia tumaini la kuishi milele (maisha yajayo yenye raha ambamo hakutakuwa na maumivu wala shida milele). Lakini, kwa sababu ya kazi ya Bwana Yesu (na makubaliano kwa upande wetu, kwa imani [ambayo si “kazi” bali ni ule “mfano wa Mungu” Aliotuumba nao – Mwanzo 1:26] ya kazi Yake hiyo), sisi Wakristo tunafaidika na neema za Mungu katika maisha ya hapa duniani pia – War. 6:14-15.

 

Neno la Kiyunani ambalo maana yake ni neema ni charis, na charis maana yake ni “fadhila” na “nia njema”. Wanadamu huzaliwa wenye dhambi (matokeo ya kuanguka kwa wanadamu wa kwanza – cf. War. 7:20) lakini tunapompokea Bwana Yesu Kristo kama Mwokozi wetu, mtazamo wa Mungu kwetu sisi unabadilika, kutoka kwenye uhasama na kwenda kwenye wema – Waefe. 2:3-7. Sasa sisi tumekuwa watoto Wake, na anatulea kwa upendo. Mwandishi/mwimbaji wa Zaburi anasema: “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki [mwongofu] ameachwa [ametelekezwa], Wala mzao wake akiomba chakula (Zab. 37:25). Ni vigumu sana kuiwekea mipaka ile nguvu na upeo wa neema au fadhila ya Mungu ambamo sisi Wakristo sasa tumo ndani yake, kwani inagusa kila sehemu ya maisha yetu. Sasa Mungu anatuchukulia kama watoto Wake wapendwa, wakati wote akitushughulikia na kutupatia mahitaji yetu yote – Mathayo 6:25-34. Hakujatokea wakati ambapo Mungu hakuwa mwaminifu katika kutupatia mahitaji yetu yote. Hashindwi kutimiza ahadi Zake, kwa upande Wake; kwa upande wetu sisi, wajibu wetu ni kukumbuka tu na kuamini kwamba Yeye hatotutelekeza.

 

2. Neema za Msingi za Mungu za Kutusaidia Kustahamili Mateso: Kweli ndiyo neema ya msingi kabisa ambayo inatuwezesha kuyakabili na kupambana na matatizo ya maisha. Hili linahitaji maelezo kidogo. Aina ya kweli inayotusaidia katika magumu yetu ni ile “kweli” iliyomo moyoni, iliyoeleweka kikamilifu, iliyoaminiwa na inayotumiwa katika kuyakabili magumu yanayokuja katika maisha yetu. Maandiko yaliyo ndani ya Biblia, kama hayatafanywa kuwa ni “kweli” iliyo ndani ya mioyo yetu (kwa kuyasoma, kuyasikia na kufundishwa maana yake) basi hayatakuwa na msaada wowote mara magumu yanapokuja. Zaidi ya hapo, kama tunafahamu aya za Biblia na misingi ya Biblia, lakini tunaamua kutoiamini, basi haitakuwa na faida kwetu pindi magumu yanapobisha hodi. Kwa kweli, tuna nafasi gani ya kuyakabili mateso kwa ufanisi ikiwa Mungu hajatupatia mbinu za kufanya hivyo – War. 10:14-15?

 

Lakini Mungu ametuandalia neema zake ili tuweze kuyakabili magumu. Ametuandalia chakula, mahali pa kulala, mavazi, Biblia, mahala pa kusanyiko, waalimu wa Biblia na idadi kubwa ya Wakristo wenzetu walio tayari kusaidiana nasi (kila Mkristo ana karama au kipaji angalau kimoja kilichopangwa na Mungu ili kufanikisha kupevuka kiroho na kusitawi kwa Mwili - Kanisa - wote wa Kristo) ili kukabili mahitaji yetu yote. Mchango pekee unaohitajika kutoka kwetu ni imani tu! Mungu amepanga kwamba kweli yote ya Neno lake ichanganyike na imani iliyomo mioyoni mwetu (katika namna ile ile ilivyokuwa wakati ule tulipomwamini mwanaye, Yesu Kristo). Hivyo, ili tuweze kuyakabili magumu yaliyo katika maisha yetu katika namna ambayo Mungu anataka, tunahitaji kujua anachokifundisha kuhusu somo hili (kama ilivyo kwa masomo mengine yote), kuamini anayoyafundisha na kuyatumia katika kuyakabili magumu pindi yanapojitokeza katika maisha yetu. Kimsingi, ili kukua kiroho inatulazimu kujifunza mashauri yote ya Mungu, na siyo kujihusisha tu na masomo tunayojichagulia sisi wenyewe kwa sababu yanahusiana na mambo yanayoendelea katika maisha yetu wakati huo, au kwa sababu ‘tunapenda’ masomo fulani zaidi ya mengine. Mungu ana nia ya sisi kujitayarisha katika kuyakabili mazingira yote katika maisha yetu (ikiwa ni pamoja na mateso) kwa njia ya kulisikia, kuliamini na kulitumia Neno lake lililo ndani ya Biblia. Ametuandalia Biblia, waalimu wa Biblia, fursa na mbinu za kujifunza misingi yote ya kweli.

 

3. Misingi ya kweli inayohusiana na mateso:

 

1. Mungu analifanyia kazi kila jambo katika maisha yetu (pamoja na mateso) kuwa mema kwa ajili yetu War. 8:28; Mwa. 50:20.

 

2. Tunaweza kuwa na furaha katikati ya mateso tunayopitia, tukijua kwamba ustahamilivu wetu unazaa kukua kiroho (ukomavu wa kiroho) na tutapata thawabu kwa sababu hiyo – War. 5:3-4; 2Wakor. 4:17; 1Wathess. 5:18; Yak. 1:2-4; 1Pet. 1:5-8; 4:13.

 

3. Tunaweza kupata faraja katika ufahamu kwamba Mungu kamwe hatotupa mzigo ambao hatuwezi kuubeba, na siku zote atatupatia njia/mlango wa kutokea kutoka katika magumu yetu, njia ambayo yaweza kupita katikati ya hayo mateso (Mungu mwenyewe akikulinda kwa upendo na uangalifu mkuu, kama ilivyokuwa kwa Wana wa Israeli jangwani na baharini), au kukuepusha kabisa na mateso hayo – 1Wakor. 10:13.

 

4. Bwana, siku zote huwa ana makusudi Yake pale anaporuhusu tupitie magumu, kitu ambacho sisi wenyewe tunaweza tusikione wakati ule. Kifo na ufufuo (hapa, tofautisha na Ufufuo wa Mwisho wa Watakatifu wote, ambapo tutafufuliwa katika miili mipya) wa yule mtoto wa mjane ulipelekea katika kumletea imani yule mama yake mjane – 1Wafalme 17:24. Kifo na ufufuo wa Lazaro ulimletea maumivu ya moyoni Bwana Yesu, lakini alifarijika na tukio hilo kwani liliamsha imani kwa walioshuhudia – Yoh. 11:15. Mlemavu wa Yoh. 9 hakuzaliwa vile kwa sababu ya dhambi ya mtu yeyote, bali kusudi la kudhihirisha utukufu wa Mungu – Yoh. 9:3. Ayubu alipitia mateso makali kwamba subira yake katika mateso aliyopata imekuwa chanzo cha sifa tele, lakini hakujua kwamba Mungu Alikuwa Akimtumia kudhihirisha uwezo na utukufu Wake – Ayubu 1:8; 2:3; soma pia Ayubu 42:10.

 

5. Mateso yanapotusibu yanatupa faida kiasi kikubwa tu: tunapata uzoefu ambao unatuwezesha kuwasaidia Wakristo wengine katika saa yao ya kupata magumu au mitihani, kwani kila mmoja wetu atapata aina fulani ya magumu katika maisha yake, 2Wakor. 1:3-7; 1Peter 4:12; 5:9.

 

6. Tunaweza kupata matumaini katika magumu yetu kutoka katika mifano ya Biblia. Maandiko yana matukio mengi ya waumini wenzetu ambao walipitia mateso makubwa. Tukisoma tu magumu ya Ayubu na Yeremia, Danieli na Ezekieli, au unaweza kusema muumini yeyote aliyejitoa kiasi cha kumfurahisha Mungu. Waumini hawa walipitia mateso yao binafsi, na pia walistawi katika imani yao na waliendelea kumpenda na kumwamini Mungu, na kuendelea katika kukua kwao kiroho, katikati ya magumu hayo makuu. Mwandishi wa barua kwa Waebrania anaorodhesha mateso haya katika sura ya 11, akituambia kwamba “kwa imani yao kuu”, waumini wote maarufu wa kale walifanikiwa kushinda katika magumu na mitihani iliyowakabili, wakijua kwamba Mungu Amewawekea hazina njema kuliko utajiri wa dunia hii. Hata hivyo, Bwana wetu aliteswa kwa ajili yetu ili tuweze kuishi milele kwa amani na furaha – 1Petro 2:21; 4:1.

Hitimisho: Mwisho, tusisahau kwamba Mungu ametupatia Mfariji, Roho Mtakatifu – Yoh. 14:16. Kama tu tutakuwa watulivu na kumtegemea Mungu, Roho Wake Atatusaidia, Atatufariji, atajaza mioyo yetu na furaha ambayo inazidi maumivu yetu ya sasa, hata kama maumivu hayo ni makali kiasi gani, hata kama mateso hayo yanauma kiasi gani – 1Petro 4:14; War. 5:3-5.

 

=0=

 

Imetafsiriwa kutoka: Grace in Suffering: Peter’s Epistles #6

 

=0=

 

Basi na tuonane katika somo #7 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!