Aina za Mateso: Nyaraka za Mtume Petro #4

 

Na Dr. Robert Dean Luginbill

Wa https://ichthys.com

 

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

 

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahsusi na Dr. R. D. Luginbill

Permission for This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by

Dr. R. D. Luginbill

 

Mateso: Mtume Petro aliwaandikia barua mbili waumini waliokuwa wakiishi Asia Ndogo wakati ule wa karne ya kwanza – miaka kadhaa baada ya Bwana Yesu kupaa mbinguni. Wakati huo, Wakristo hawa wa mwanzo walikuwa wakipata shida sana, na mateso waliyokuwa wakiyapata yalianza kuathiri kasi yao ya kupevuka kiroho. Katika barua yake ya kwanza, Petro alijihusisha zaidi na tatizo la mateso. Kwa hakika anatumia neno la Kiyunani pascho (kitenzi ambacho maana yake ni “kuteseka”) mara nyingi zaidi katika barua yake hii fupi kuliko Mtume Paulo anavyolitumia katika barua zake zote. Shida, kurudishwa nyuma, masikitiko, magonjwa na aina nyingine za mateso/taabu, kusema kweli vyaweza kuwa kikwazo kwa imani ya mtu.

 

Sisi waumini husema kwamba tumekombolewa kutoka katika ghadhabu ya Mungu, tumesamehewa dhambi zetu zote kwa damu ya Bwana Yesu na kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Basi kama ni hivyo, kwa nini wakati mwingine maisha yetu yanakuwa na magumu kiasi hiki? Bila ya kupata majibu ya maswali haya kutoka katika Biblia, mateso makali yatatia shinikizo kwa imani ya Mkristo, na kumshawishi amtilie shaka Mungu. Lakini Mungu ametupatia kweli ili tupambane na mashaka ya namna hii, kweli ya Neno Lake. Kwa kutumia kweli iliyo ndani ya Biblia, Mungu ametupa uwezo wa kulinda imani yetu, kuelewa sababu ya mateso tunayopata, na kustahamili mateso hayo, na matokeo yake ni kwamba Mungu anapata utukufu na sisi tunapevuka kiroho. Katika kuandika barua yake ya kwanza, Petro alilenga kuwapa waumini wale walioshinikizwa na mateso habari muhimu na kuwatia moyo, kitu ambacho walikihitaji sana ili waweze kufaulu mtihani wa mateso, jambo ambalo ni muhimu kwetu sisi waumini wa leo pia, kama ilivyokuwa kwao, takriban miaka 2,000 iliyopita.

 

Aina za Mateso: Itatusaidia sana sisi kupambanua kati ya aina mbalimbali za mateso kwa mtazamo wa Biblia. Mateso ambayo huwapata wanadamu wote tunayaita ‘mateso ya kawaida ya wanadamu’ (mifano michache: Mwa. 3:16-19; 4:3-7; Mhubiri 1:2-3). Kwa jinsi alivyopanga Mungu, ulimwengu huu unaoonekana sasa unaendeshwa kwa kanuni zinazoweza kusomeka na kutabirika ambazo tunaweza kuziita “sheria za asili”. Vivyo hivyo, katika mazingira ya mahusiano ya wanadamu, Mungu ameunda mfumo wa mwenendo wa kawaida wa wanadamu, uliopandikizwa katika dhamiri ya kila mwanadamu – War. 2:14-15. Wanadamu wote, katika makundi yao tofauti, wana kanuni ambazo zinatokana na dhamiri zao wenyewe, na wametunga mifumo ya sheria ambayo tunaweza kuiita “sheria za wanadamu”.

 

Sasa, ikiwa tunaamua kudharau sehemu fulani ya/za aina zote hizi mbili za mifumo ya sheria (za asili na za wanadamu), tunapata mateso. Kwa mfano, unaweza kudharau “sheria ya asili” ya mvutano, ukaamua kuruka kutoka ghorofa ya pili ya nyumba; au unaweza kudharau “sheria ya wanadamu” kwa kuchukua redio dukani bila kulipa na kuipeleka nyumbani kwako! Kwa kweli unaweza “kuepa kuumia” katika mifano hii miwili mara moja au hata mara mbili, lakini ukiendelea na matendo hayo, kwa hakika utapatwa na mateso. Mara nyingi haiwezekani kabisa kuepuka kuumia mara unapodharau sheria hizi zilizo katika makundi haya mawili. Kwa mfano, kila mmoja wetu huambukizwa ugonjwa wa aina fulani katika maisha yake, ikiwa ni matokeo ya uvunjaji wa mojawapo kati ya sheria hizi za asili; na kwa upande wa sheria katika mahusiano ya wanadamu, hata kutimiza matakwa ya sheria yaweza kuwa na maumivu (kwa mfano kulipa kodi ya mapato). Katika upeo wake, mateso haya yanaweza kuwa makali sana (fikiria wahanga wa tufani, radi, mafuriko, matetemeko au unyanyasaji wa kisisasa unapofanyika kwa kisingizio cha ‘kulinda sheria na amani’). Kinachosemwa hapa ni kwamba, hata katika hali ya kawaida kabisa ya mwenendo wa ulimwengu huu, pamoja na mwenendo wa kawaida kabisa wa historia ya wanadamu, mateso huwakuta wanadamu waishio ndani yake. Sote tunaitambua hali hii na tunaweza kuzitambua sababu fulani zilzosababisha hali fulani, iwe ya kiasili au ya kisiasa, iliyoleta/iliyosababisha mateso.

 

Chanzo cha Mateso ya Kawaida ya Wanadamu: Tukiwa waumini wa Mungu, na katika utimilifu na wema Wake, inawezekana tukauliza ni kwa nini kuna maumivu na mateso katika dunia, ni kwa nini kuna unyanyasaji wa kiitikadi (au kisiasa) na majanga ya asili? Jibu rahisi na fupi la hili swali ni kwamba mateso asili yake ni uovu, na uovu asili yake ni viumbe wa Mungu, na siyo Mungu Mwenyewe. Tunapata fursa ya kujifunza mafundisho/masomo ya Biblia yanayohusiana na uovu katika: “The Satanic Rebellion” - https://ichthys.com; hata hivyo, mistari kadhaa kuhusiana na mateso inafaa hapa.

 

Uumbaji wa mwanzo wa ulimwengu ulihusisha aina ya viumbe wa kipekee kabisa (au bora sana) wanaoitwa malaika. Malaika wana utashi kama tulio nao sisi wanadamu, lakini katika uwezo wanatuzidi sana. Malaika mmoja aliyepewa karama kuu ambaye Mungu alimweka katika nafasi ya mamlaka makubwa alinuia rohoni mwake kumwasi Mungu na kisha kuchukua nafasi ya Mungu kama mtawala wa ulimwengu – Isa. 14:12-21; Eze. 28:12-19. Biblia inatupatia fununu chache kuhusu uasi huu ulivyotukia na ulivyoendelea, lakini tunajua kwamba ushindi wa Mungu dhidi ya Shetani na malaika wengine walioamua kumfuata katika uasi ule ni wa uhakika – Luka 10:18; War. 16:20; Ufu. 20:10.

 

Ni dhahiri, kwa kuwa Mungu ana nguvu na uwezo usio na kikomo, hakuwa na kipingamizi cha kumdhibiti kiumbe wake mwenyewe palepale, mara moja. Badala ya kuwadhibiti pale pale, mara moja, Mungu aliamua kudhihirisha kwa Shetani na malaika wengine wote kwamba Shetani na wafuasi wake walifanya uamuzi huru kabisa wa kuasi na hivyo kwamba kwa kuwa Mungu alimuumba Shetani, hii haikuwa na maana ya kwamba Mungu alibeba dhima au wajibu juu ya uovu ule alioufanya Shetani. Ili kudhihirisha hili, Mungu akamuumba mwanadamu, kiumbe aliye dhaifu sana (katika uwezo na nguvu) kulingana na malaika, lakini mwenye utashi sawasawa na malaika. Alipokabiliwa na changamoto hii mpya ambayo aligundua itamwangamiza, Shetani akafikiria matumaini ya kuepa hukumu yake yapo katika kuharibu mpango huu wa Mungu wa kuumba viumbe wapya wenye uwezo wa kumtii Mungu. Kwani kama wanadamu wale wakichagua kumwamini Mungu na kufuata amri Zake, itakuwa imedhihirika bila shaka yoyote kwamba Shetani alikuwa na maamuzi huru wakati anafanya uasi na kwamba alistahili hukumu. Hivyo Shetani akatafuta namna au mbinu ya kumtenga mwanadamu na Mungu wake kwa kuwapotosha wazazi wetu wale wawili wa mwanzo pale bustanini (Mwa. 3); lakini Mungu akampa ufumbuzi mwanadamu: japokuwa alitumia utashi wake kutomtii Mungu, Yeye akampa fursa ya pili. Mungu akampa mwanadamu fursa nyingine ya kuuutumia utashi wake kumtii na kumchagua Mungu kwa kumnyenyekea Mungu kupitia imani kwa Mwokozi anayekuja (kwa wakati huo Alikuwa bado kuja). Imani yao hii iliashiriwa kwa kuyakubali na kuyapokea yale “mavazi ya ngozi” ya Mwanzo 3:21, yaliyopatikana kutokana na dhabihu ya kuchinjwa wanyama, kitendo kilichokuwa ni ishara ya ujio na Dhabihu ya Kristo msalabani.

 

Haya yote yanahusiana vipi na mateso ya kawaida ya wanadamu? Mungu alipomuumba mtu aliwaumba mume na mke (Mwa. 1:27); aliwaumba wakiwa hawana kasoro, watimilifu, na akawaweka katika sehemu iliyokuwa timilifu: Bustani ya Edeni (jina linalotokana na Kiebrania gan-'aden maana yake “bustani ya starehe” [au ya kufurahisha sana, ya kuteremesha], Mwa. 2:8). Katika sehemu hii na hali hii iliyokamilika, watu wale wawili hawakupata mateso ya aina yoyote, kama vile katika paradiso inayokuja hakutakuwa na mateso ya aina yoyote – Ufu. 21:4. Lakini matokeo ya kuanguka kwa mwanadamu kunakosimuliwa katika Mwanzo 3 ni mateso kwa watu wote katika maisha haya. Mungu aliwapa tahadhari Adamu na Eva kwamba kula tunda kutoka mti wa ujuzi wa mema na mabaya kutasababisha wao kufa (palepale kufa kiroho au kutengwa na Mungu, na, kufuatia kuzeeka kwa mwili, kufa kwa mwili, na hukumu ya milele – Mwa. 2:17). Baada ya kuanguka katika dhambi, Adamu na Eva wakaondolewa katika bustani timilifu ya Edeni (Mwa. 3:22-24), na kitu kipya kikaingia katika maisha yao: mateso. “Maumivu” yakatabiriwa kwa Eva (Mwa. 3:16) na “suluba” kwa Adamu, lakini maneno yote haya mawili, maumivu na suluba, katika Kiebrania yanatoka kwenye mzizi mmoja: neno 'atsab ambalo maana yake ni kuhisi au kusikia maumivu, uchungu na huzuni (unaweza kuona hapa asili ya neno letu la Kiswahili, adhabu, kutoka neno la Kiebrania 'atsab – na maana yake ni ile ile!). Adamu na Eva wakatuachia sisi, watoto wao, urithi wa mateso ya kawaida ya wanadamu. Lakini, wakati uhusiano wetu na wazazi wetu wa kwanza umetuletea mateso na kifo, uhusiano mpya ambao Mungu ametuahidi na kutupatia ili tuwe na Yeye kupitia imani kwa Mwana Wake Yetu Kristo, unatupatia furaha na uzima wa milele, kwani “… kama vile katika Adamu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Kristo wote wanafanywa hai” - 1Wakor. 15:22. Alipokuwa anatangaza hukumu dhidi ya Adamu na Eva, Mungu pia aliwapa ahadi Yake ya matumaini alipowaambia, katika Mwa. 3:15, kwamba Uzao wa yule mwanamke (Kristo) siku moja utaponda kichwa cha yule nyoka (Shetani). Ushindi huu ulitimia pale msalabani (Waebr. 2:14-15), hivyo kwamba sisi sote tulioweka matumaini yetu ya wokovu kwa Kristo sasa tunatazama mbele tukiwa na uhakika na siku ile inayokuja ambapo miili hii ya maumivu itafufuliwa na kuwa miili ya utimilifu (2Wakor. 5:1-10). Hapo tutaishi milele pamoja na Mungu Baba na Mwanaye Yesu Kristo katika paradiso mpya, Yerusalemu Mpya – Ufu. 21:22.

 

Mateso ya Wakristo: Kama waumini, tunaishi katika awamu ya pili ya Mpango wa Mungu (awamu ya historia, majira, tizama somo la Petro #3). Awamu ya kwanza (wokovu) illiisha pale tulipomkubali Yesu Kristo kuwa Mwokozi wetu, na awamu ya tatu (milele) bado haijaanza kwa sisi ambao bado tuko hapa duniani. Japokuwa roho zetu zimebadilika katika utii kwa Bwana Yesu, miili yetu iko vile vile kama ilivyokuwa kabla ya wokovu, na bado tunaishi katika dunia hii isiyo timilifu kama tulivyoishi kabla ya kuamini. Kwa hiyo, tunaendelea kupata yale mateso ya kawaida ya wanadamu ambayo yamewasibu wanadamu wote tangu kuanguka kwa Adamu na Eva. Lakini kuna tofauti muhimu sana kati ya mateso haya ya kawaida ya wanadamu wote na mateso ya waumini wa Kristo.

 

Kwanza kabisa, mateso yetu sisi Wakristo yatakwisha. Tunajua kwa uhakika kwa kupitia imani yetu kwamba mwishowe tutakombolewa kutoka katika maumivu na machozi ya maisha haya, na, kama ulimwengu huu wa sasa, tunangojea kwa shauku kubwa ukombozi huu, tukijua kwamba magumu ya wakati huu wa sasa hayastahili kulinganishwa na utukufu (glories – plural/wingi) wa shani/ajabu wa mbinguni unaokuja (War. 8:18-23).

 

Pili, tunajua ya kuwa shida zote ambazo tunalazimika kuvumilia, yote ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa maisha yetu, na kwamba matokeo yake, hata yale ya mateso makali na ya uchungu mwingi, yatakuwa ni kwa ajili ya neema yetu, kwa mujibu wa busara na huruma za Baba yetu aliye mbinguni – War. 8:28.

 

Hata hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa kutofautisha kati ya mateso ya aina mbili wanayolazimika kupitia Wakristo ili kuzuia uharibifu wa imani yetu unaoweza kutokea kutokana na kutoelewa vyanzo vyake na makusudi yake. Wale Wakristo aliokuwa akiwaandikia Petro walikuwa wakipata changamoto ya kushindwa kutofautisha/kupambanua kati ya aina mbili za mateso ya waumini, ambazo ni:

 

(1) mateso tusiyostahili na

(2) adabisho (la kinidhamu) kutoka kwa mungu.

 

Mateso tusiyostahili: Haya ni mateso/magumu ambayo Mungu anayaruhusu yatupate ili kutupima (kutupa mitihani), kutupa utulivu wa kitabia, na kutupa mafunzo – tizama mfano wa Ayubu. Waumini wanaposhambuliwa na mateso ya namna hii, mara nyingi wanashawika kufikiri au kudhani - kimakosa – kwamba Mungu hawajali, au labda Mungu anawaadhibu. Lakini, shida katika maisha ya Mkristo siyo lazima zimaanishe kwamba Mungu hafurahishwi na Mkristo huyo. Kama tutakavyoona katika masomo yanayofuata, haiwezekani kupevuka kiroho katika maisha ya Mkristo bila kukutana na upinzani kiasi fulani, ambapo Mungu anayatumia magumu unayopitia kukuonyesha uaminifu Wake kwako (wakati wa magumu hayo, na pia anapokuokoa hatimaye), na pia wewe Mkristo unapata fursa ya kuonyesha lile wingu la mashahidi, la wanadamu na malaika – wabaya na wema – wanaotuzunguka (Waebr. 12:1-3), uaminifu wako kwa Mungu licha ya magumu unayopitia.

 

Kama Wakristo, ni muhimu sana kulitizama suala hili katika mapana na marefu yake pale madhila yanapotusibu (kwa kutojifikiria sana sisi wenyewe pekee) na tukumbuke kwamba kwa kuwa Baba yetu aliye mbinguni anatupenda sana hata akamtoa Mwanaye wa Pekee ili aje kufa kwa ajili yetu, kwa uhakika atatusaidia katika matatizo yetu mengine pia – War. 5:8-9. Kama tutachunguza maisha yetu ya kipindi kifupi cha nyuma/kilichopita na kuona kwamba hatujafanya makosa makubwa yoyote lakini kuna mateso katika maisha yetu kwa wakati wa sasa, ni muhimu kutambua hapo kwamba basi mateso tunayopitia hayajasababishwa na dhambi yoyote tuliyotenda. Mungu hushughulika na sisi katika msamaha na neema. Dhambi tulizotenda zamani (sana), tukaziungama wakati huo, tukasamehewa, na Mungu akashughulika nasi zama hizo, hazihusiki kabisa na mateso yetu ya sasa (tizama jinsi Ayubu na rafiki zake wale wawili wa mwanzo walivyohitimisha kwa makosa sababu za mateso ya Ayubu). Tunapaswa kujitenga na hisia zinazokithiri za kujiona tuna hatia (guilt), vinginevyo hisia hizi zinaweza kuvuruga maisha yetu ya kiroho kwa kiasi kikubwa sana. Hii ilikuwa ni sababu mojawapo ya Petro kuandika waraka wake huu wa kwanza, yaani kuondoa mkanganyiko katika suala hili kwani lilikuwa linatishia maendeleo ya kiroho ya wale Wakristo wa Asia Ndogo.

 

Adibisho Kutoka kwa Mungu: Kwa kweli sisi wanadamu si viumbe watimilifu. Hii ndiyo sababu tulihitaji Mwokozi aliye mtimilifu, Yesu Kristo, ili afe kwa ajili yetu. Kwa damu Yake sisi tumekombolewa (1Petro 1:18), tumenunuliwa kutoka katika nguvu ya dhambi. Lakini kwa kuwa tunaishi ndani ya miili isiyo timilifu (War. 7), na tunaishi katika ulimwengu usio timilifu (Yoh. 1:10), kwa masikitiko makubwa, hata baada ya kuzaliwa mara ya pili, kuishi bila ya kutenda dhambi bado kuko nje ya uwezo wetu (1Yoh. 1:10), japokuwa tumepewa jukumu la kushikilia utakatifu (Waebr. 12:14).

 

Kwa sababu ya hulka Yake ya uongofu ulio timilifu, Mungu analazimika kuadhibu dhambi ambazo sisi Wakristo/Waumini wake tunatenda; lakini Yeye hufanya hivyo kama Baba mwenye upendo mkuu kwetu. Watoto wetu wanapokosea, sisi kama wazazi wao tunawadhibu kama kweli tunawapenda – siyo kwa lengo la kuondoa hasira zetu, bali kwa kusudi la kusahihisha mwenendo wao kwa faida yao wenyewe. Vivyo hivyo, sisi tunapotenda dhambi, Mungu anatuadabisha. Katika Waebrania sura ya 12 tunaambiwa kwamba Mungu huwaadabisha “wale Anaowapenda” (msitari wa 6), na kwamba wale wote ambao ni watoto wa Mungu huadabishwa Naye (msitari wa 8). Lengo la Mungu katika kutuadabisha siyo kutukandamiza, siyo kutuangamiza, wala siyo kumwaga ghadhabu Zake juu ya vichwa vyetu, bali ni kutusahihisha, kutufundisha na kutufanya tuwe aina bora ya Wakristo (msitari wa 10 – 11).

 

Ni kwa jinsi gani basi tutalikabili tatizo la dhambi na adabisho la Mungu linaloambatana nalo? Kwanza kabisa, tunapoendelea kupevuka kiroho na kujifunza ukweli wa Neno la Mungu, tunapata umakini zaidi katika kupambanua tendo lipi ni dhambi na tendo lipi siyo dhambi. Kama tunafanya tendo ambalo ni dhambi, basi katika 1Yohana sura ya kwanza tunajifunza namna ya kupata suluhisho la tatizo hilo na kisha kurudi katika ushirika na Mungu. Katika msitari wa 8 Mtume Yohana anatufundisha kwamba sisi sote “tuna dhambi” (maana yake tuna hulka ya dhambi, na hivyo kwetu sisi kutenda dhambi ni kitu rahisi zaidi kuliko kutenda mema; pia Mithali 7:20), lakini katika msitari wa 9 tunaona ya kwamba “kama tukiungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na mwenye haki, Atatusamehe dhambi zetu na atatutoa kwenye udhalimu wote”. Sasa, neno la Kiyunani ambalo maana yake ni “kuungama” ni homologeo, na maana yake halisi ni “kukiri, kukubali kosa”. Hivyo basi, pale tunapotenda dhambi, basi na tukiri dhambi hiyo kwa Mungu (kwa sala fupi) na Biblia inatufundisha kwamba Mungu anatusamehe dhambi hiyo, na zaidi ya hapo, anatusafisha kabisa, siyo tu kutokana na hiyo dhambi, bali pia kutokana na udhalimu wote ambao tumeangukiamo.

 

Lakini je, tunapaswa kuwa na hisia kali za hatia kutokana na dhambi tunazotenda? Ni kitu kinachoeleweka kwamba tunaweza kuwa na hisia za masikitiko, huzuni juu ya dhambi tunazotenda, na kwa hakika tunahuzunishwa na maumivu yanayosababishwa na adabisho/adhabu ambayo Mungu anaitoa kwetu kwa sababu ya dhambi zetu, tusisahau kwamba Kristo ndiye aliyebeba hatia yetu halisi pale msalabani – 1Petro 2:24. Mungu Anatulazimu tuonyeshe moyo wa toba, wenye hisia halisi ya majuto (yaani toba halali ya unyofu ambayo inaonyesha kuwa inatambua fika kwamba tendo lililotendwa ni dhambi hasa na linajutiwa; cf. Zab. 51:17; Isa. 57:15-16; 66:2). Lakini ni shuruti tuelewe kwamba suala muhimu kwa Mungu siyo hisia zetu, bali ni kazi ya Kristo msalabani.

 

Kwa kweli, kama tukichukua jukumu la kujitesa sisi wenyewe katika hisia zetu (moyoni mwetu) kwa sababu ya dhambi zetu, au kwa namna yoyote ile kujiumiza sisi wenyewe kama namna fulani ya malipizi kwa dhambi hizo, hatutasamehewa kwa njia hizo (mifano ni Esau na Yuda Iskaryote). Bwana Yesu Kristo pekee ndiye aliyekuwa na sifa za kubeba mzigo wa dhambi zetu, na ni kazi Yake tu ndiyo inayokubalika na Mungu Baba. Kwa sisi kuwa na hisia za huzuni au hatia (guilt) kwa sababu ya dhambi zetu hakuondoi dhambi hizo mbele za Mungu bali pia kuna hatari ya kumfedhehesha Mungu Baba yetu. Kwa sababu tunapojiadhibu sisi wenyewe kwa hisia kali za hatia mioyoni mwetu, ni kama vile tunasema “alichokifanya Kristo hakitoshi, ninapaswa kumsaidia Mungu kwa kuongeza malipizi yangu pia”.

 

Mtazamo Sahihi Kuhusiana na Dhambi: Mtazamo wa Daudi katika Zaburi 51 ndio sahihi kwa Mkristo aliyetenda dhambi. Hapa Daudi ana maumivu makali kwani yuko chini ya adabisho la Mungu, hivyo anakubali au anakiri dhambi yake kwa Mungu (siyo kwa mtu) na anamwomba Mungu amrejeshe katika ushirika Wake. Daudi anajisikia vibaya kwa dhambi alizotenda, lakini anatambua kwamba cha muhimu hapo ni hulka ya Mungu (aya ya 4) na huruma ya Mungu (aya ya 9), na siyo hisia zake yeye mkosaji. Mtazamo wa Mungu kwa muumini anayekiri makosa yake katika namna hii iliyo sahihi unaonekana katika fumbo la mwana mpotevu – Luka 15. Kwanza, mwana yule anakiri kosa alilotenda dhidi ya baba yake (aya ya 15). Halafu, japokuwa mwana yule yuko tayari kupokea adhabu ya kufanya kazi ngumu ya mikono katika miradi ya baba yake (aya za 18 – 19), baba yake anamsamehe, kwa furaha na shukrani anamkaribisha (licha ya makosa aliyofanya) na kumrejeshea mafao na haki zake zote kama mwana mzaliwa katika familia ile (aya za 22 – 24). Vivyo hivyo, Mungu wetu, kwa msingi imara wa kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo kwa ajili ya dhambi zetu, kwa rehema nyingi Anatusamehe dhambi zetu na Anaturejesha katika ushirika Wake hata kama tumetenda dhambi gani, hata kama tunajisikia vibaya namna gani, ali mradi tunaonyesha nia ya kurejea Kwake na kukiri dhambi zetu Kwake.

 

Mapitio:

  • Mateso ya kawaida ya wanadamu: Mateso ya namna hii ni urithi wa wanadamu wote kwa sababu ya kutotii kwa Adamu na Eva, lakini kupitia dhabihu ya Bwana wetu Yesu Kristo, imepatikana njia ya watu wote kurudi katika mikono ya Mungu Baba yenye upendo kwa kumwamini Mwanaye kama Mwokozi. Baada ya kumwamini Bwana Yesu, Mkristo haondolewi duniani, bali anabaki hapa ili apevuke kiroho na hivyo kumtukuza Mungu.

  • Mateso tusiyostahili na adabisho kutoka kwa Mungu: Maskani yetu katika ulimwengu huu wa Ibilisi yanatuletea mateso ambayo hatustahili, na Mungu huyatumia mateso hayo kwa kuyaruhusu yatusibu ili kwa kuyapitia (chini ya uangalizi Wake madhubuti wenye upendo), tuweze kupevuka kiroho na ili tujiwekee baraka/hazina ya milele (na kumletea Mungu utukufu); lakini pia tunapitia mateso ambayo ni matokeo ya adhabu au adabisho kutoka kwa Mungu kutokana na dhambi tunazotenda. Ni muhimu kwa Mkristo kuelewa tofauti kati ya aina hizi mbili za mateso. Ungamo la dhambi (kukiri na kukubali au kuwajibika na tendo la dhambi tulilolifanya dhidi ya Mungu ndani ya roho yako kwa namna ya sala kwa mujibu wa 1Yoh. 1:9; cf. Mfalme Daudi katika 2Sam. 12:13) linakuletea msamaha, utakaso na rejesho la ushirika na Mungu. Mateso tusiyostahili kwa upande mwingine, ni changamoto kwa imani yetu, na pia ni fursa ya kumwonyesha Mungu imani yetu kwamba atatuokoa kutoka katika magumu, hata kama hali inaonekana kuwa ni mbaya kiasi gani.

  • Ufumbuzi wa tatizo la namna ya kupambana na mateso tusiyostahili, kama tutakavyoona katika masomo yanayofuata, ni kutulia kwa matumaini katika uwezo na neema ya Mungu.

  • Ufumbuzi wa tatizo la mateso yanayosababishwa na kuadabishwa na Mungu ni kukiri dhambi tuliyo[zo]tenda mara moja, papo hapo. Mara baada ya kuungama, dhambi husamehewa, na muumini kutakaswa. Kwa tendo la kuungama dhambi zetu kwa Mungu, tunakubali kwamba tumetenda tendo la kukosa utiifu kwa Mungu. Japokuwa ni sahihi kuazimia kutotenda dhambi za aina hiyo tena, hisia za hatia na hisia za huzuni hazina tija na hazituletei tija mbele za Mungu. Sera/msimamo Wake ni: neema. Hii maana yake ni kwamba anatusamehe bure kutoka katika hazina ya wema Wake na utukufu Wake kwa msingi wa kile alichokifanya Kristo msalabani, na siyo kwa msingi wa “kazi” yoyote tunayojaribu kuifanya sisi kama “malipizi” kwa dhambi zetu. Kukiri na kutubu dhambi ni jambo la lazima katika maisha ya Mkristo. Wakristo au waumini wote hutenda dhambi hivyo wote wanapaswa kukiri na kutubu dhambi hizo wanapozitenda, kwani hii ndiyo njia pekee ya kupata msamaha na kutakaswa ili tuendelee na ule wito wetu maalum katika awamu ya pili ya Mpango wa Mungu kwa ajili ya maisha yetu: kupevuka kiroho.

 

Haya basi, na tusiruhusu dhambi ambayo haijafanyiwa toba, na hisia za hatia zisizostahili kuwa kikwazo kwa imani yetu.

 

=0=

 

Imetafsiriwa kutoka: Categories of Suffering: Peter’s Epistles #4

 

=0=

 

Basi, na tuonane katika somo #5 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!