Tatizo la Mateso/Shida za Maisha kwa Wakristo: Nyaraka za Mtume Petro #2

 

Na Dr. Robert Dean Luginbill

Wa https://ichthys.com

 

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahsusi na Dr. R. D. Luginbill

Permission for this Kiswahili translation has been kindly granted by

Dr. R. D. Luginbill

 

Mapitio: Waraka wa kwanza wa Mtume Petro ni wito kwa Mkristo akue kiroho. Katika waraka huu, Petro anaonyesha jinsi tatizo la shida za maisha linavyoweza kumwondoa Mkristo katika msitari wake/njia ya imani. Katika mfululizo huu wa somo la Nyaraka za Petro, suala la mateso kwa Mkristo litakuwa linagusiwa mara kwa mara.

 

1Petro 1:1-2:

  1. Petro, Mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule ambao japo wametengwa na kutawanywa katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia, (2) wamechaguliwa na Mungu Baba kwani Aliwajua toka mwanzo kwa utakaso wa Roho Mtakatifu, hata mkapata kutii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani ziongezwe kwenu!

(Revised translation)

 

Mateso ya Mkristo: Swali hili huulizwa mara nyingi: “kwa nini waumini wa Kristo wanateseka?” Swali hili ni zuri sana, na litachukua sehemu kubwa ya masomo yetu haya ya Petro: Waraka #1, na Petro: Waraka #2 kwa jinsi tunavyoizidi kuendelea nayo siku za usoni. Hata hivyo tunahitaji kutilia mkazo hoja kadhaa za msingi toka hapa mwanzoni mwa masomo yetu. Dakika ile tunapookolewa, tunapoanza kumwamini Bwana Yesu Kristo kama mwokozi wetu, tunapozaliwa upya, hatupelekwi mbinguni pale pale. Tunaendelea kuishi hapa duniani …

 

  • ili kujifunza juu ya, na kuutambua uaminifu wa Mungu.

  • ili imani yetu ipimwe uimara wake.

  • ili kusaidia katika kustawisha imani ya wengine.

 

Malengo haya yote matatu ni muhimu katika mchakato wa kukua kiroho kwa Mkristo: (1) kujifunza kuhusu Mungu na uaminifu Wake kwetu – kuamini tunayojifunza na kuyatumia katika maisha yetu – ni msingi wa mchakato wa kupevuka kiroho (2) kupimwa imani yetu ni namna Mungu anavyoonyesha uaminifu Wake kwetu na hivyo kuiimarisha, na (3) baada ya sisi kukua/kupevuka kiroho, tunapaswa kuwasaidia Wakristo wenzetu kuendelea kiroho, na hivyo kulijenga Kanisa la Bwana Yesu. Masuala/malengo yote haya matatu yanaonekana katika dibaji/utangulizi wa Waraka wa kwanza wa Mtume Petro (aya ya 1-2).

 

Mtume Petro: Neno la Kiyunani ‘petros’ (maana yake ‘jiwe’; nasi tunapata jina Petro) halikuwa jina lake la kwanza. Hapo mwanzo aliitwa Simoni, ambalo ni jina la Kiebrania (Shimon) ambalo maana yake ni “kusikia”. Yule mzee wa Ukoo Simeoni alikuwa mtu wa kwanza kupewa jina hilo. Mungu aliposikia maombi ya Leah (Mwanzo 29:33) na akamjalia kupata mtoto wa kiume, akampa mtoto jina hili kwa maana Mungu “alisikia” maombi yake. Bwana Yesu alipokutana na Simoni kwa mara ya kwanza akampa jina ‘Petro’ - Yohana 1:35-42. Injili ya Yohana inatuambia kwamba Andrea, ndugu yake Petro, baada ya kukaa na kumsikiliza Bwana Yesu kwa siku moja tu, aliamini kwamba (Bwana) Yesu ndiye masihi. Andrea akampeleka Petro kwa Bwana Yesu naye alipomwona akasema “wewe ndiye Simon mwana wa Yohana; wewe utaitwa “Cephas” (maana yake katika Kiarami ni “jiwe”).

 

Ni muhimu kuona hapa kwamba Petro hajafanya kitu chochote (bado) kinachostahili kupewa jina hili jipya. Aliongozwa kwa Bwana Yesu na ndugu yake, na jina lake likabadilishwa hata kabla hajaongea neno lolote. Kwa kubadilisha jina lake, Bwana Yesu anamwonyesha Petro kwamba maisha yake yatabadilika kabisa kwa imani aliyoionyesha baada ya kusikia habari za Bwana Yesu kutoka kwa kaka yake, japokuwa hata imani hii amepewa na Mungu pia. Kama ilivyokuwa kwa Petro, Mungu anayajua maisha yetu yote kabla hatujazaliwa na pia anajua udhaifu au mapungufu yetu na uwezo wetu. Bwana anayaona maisha yetu yote, tangu kuzaliwa mpaka kufa, kwa kutazama (mara moja) tu. Maisha yetu hapa duniani ni mafupi mno. Sisi wanadamu tuna tabia ya kuelekeza fikra zetu kupita kiasi katika utondoti (details) wa maisha yetu hata tunasahau kwamba maisha haya yanadumu kwa kitambo kidogo sana; muda si mrefu tutakuwa na Bwana milele. Tunapaswa kukumbuka tamko la Bwana Yesu kwa Petro na maana yake: Yeye anaona taswira kubwa zaidi kuhusu maisha yetu kuliko tunavyoona sisi, hivyo tathmini Yake kuhusu maisha yetu ndiyo muhimu. Tunachotafuta na kukipata hapa duniani kitakuwa mavumbi tu muda si mrefu, lakini thawabu tutakayoipata kutoka kwa Bwana ni ya milele – Mathayo 6:19-20.

 

Jiwe na Mwamba: Hivi ni nini haswa Bwana wetu anamtabiria Petro kwa kumpa jina “Jiwe”? Watu wengi wanadai kwamba kwa kumpa jina “Jiwe”, Bwana Yesu alimaanisha kwamba Petro atakuwa ndiye jiwe la msingi la Kanisa Lake; na watu hao wananukuu Mathayo 16:13-20 kama msingi wa hoja yao hii, lakini hii si sahihi kabisa. Katika ibara ile Bwana Yesu anamwambia Petro: “Nami nakwambia kuwa wewe ndiwe Petro {katika Kiyunani petros maana yake ni jiwe la ukubwa wa kokoto} na juu ya Mwamba {katika Kiyunani mwamba ni petra, jiwe lenye ukubwa wa mlima} huu nitalijenga Kanisa Langu.” Sasa, katika muktadha (mazingira ya sentensi – kwa kimombo “context”) huu wa Mathayo 16, Petro amedhihirisha kwamba Bwana Yesu ndiye “Masihi, Mwana wa Mungu Aliye Hai.” Hivyo Bwana Yesu anaweka msitari chini ya kauli hii ya Petro, anaithibitishia ukweli wake. Kwa kusema “Mwamba Huu” Bwana Yesu anamaanisha Yeye Mwenyewe kuwa Ndiye jiwe la msingi la Kanisa. Fundisho au kanuni hii imefafanuliwa kwa ufasaha sana katika Biblia: soma Isa. 28:16; 1Petro 2:6; Waefe. 2:20; 1Wakor. 3:11. Bwana Yesu anatumia kauli “mwamba huu” kama vile anavyotumia kauli “Hekalu hili” katika Yohana 2:19 ambapo anatabiri ufufuo Wake mwenyewe: “bomoeni Hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu.”

 

Mawe Hai au Matofali Hai: Hata hivyo, Mathayo 16:13-20 inatupa mwanga unaotuwezesha kujua maana ya jina ‘Petro’. Bwana Yesu ndiye mhimili ulio katikati ya Kanisa (waumini halisi wa Bwana Yesu katika ujumla wao, siyo wanajumuiya wa dhehebu fulani!), bali Petro ni sehemu (jiwe) katika mfumo mzima. Petro anathibitisha tafsiri hii yeye mwenyewe katika 1Petro 2:4-6, ambapo anatuambia kwamba alichokitamka Bwana Yesu kuhusu yeye ni ukweli unaowahusu waumini wote. Kristo ndiye Mwamba, na ni Mwamba ulio hai, uliochaguliwa na Mungu, na sisi waumini Wake pia ni “mawe yaliyo hai”, ambayo yanajenga lile Hekalu la kiroho kwa ajili ya kutumika kwa kazi ya Mungu. Sisi sote ni “mawe” yanayolijenga Kanisa la Kristo. Petro alikuwa mtu wa pekee sana ambaye alikuwa na mwenendo uliomuweka katika mitihani na majaribu mbalimbali yaliyomletea mafanikio makuu ya kiroho, na kushindwa pia. Ni kweli pia kwamba yeye na mitume wengine walikuwa watu muhimu kabisa katika “ujenzi” wa msingi wa Kanisa la mwanzo, na ni kwa ajili hiyo walichaguliwa – Waefe. 2:20; Ufu. 21:14. Lakini lengo la hili jina jipya halikuwa na uhusiano na umuhimu huu wa Petro katika ujenzi wa msingi wa Kanisa la mwanzo. Kwa kweli ni kinyume kabisa. “Petro” maana yake ni “yeye ni tofali mojawapo katika matofali mengine yanayojenga Nyumba ya Mungu”. Kwa hiyo “Petro” ni jina la tunuku/staha/heshima kubwa ambalo linaonyesha unyeyekevu wa ki-Mungu aliokuwa nao Petro kama vile Mtume Paulo (jina ambalo maana yake ni “mdogo”) alivyokuwa, heshima ambayo Petro alidhihirisha kwamba alistahili mwishoni mwa maisha yake. Hakuna shaka kwamba Petro alifanikisha mengi katika maisha yake kwa ajili ya Bwana, lakini kitu muhimu hapa ni kwamba ikiwa tutakuwa na unyenyekevu wa kweli kama aliokuwa nao Petro – kutambua kwamba tunahitaji kuutegemea uwezo na busara za Bwana, na sio za kwetu wenyewe – ndipo Bwana anaweza kututumia katika kazi Yake kama Alivyomtumia Petro (Mithali 3:34; Yakobo 4:6).

Utume wa Petro: Neno apostle, yaani mtume, linatokana na neno la Kiyunani apostolos ambalo maana yake ni “yeye aliyetumwa”. Japokuwa siku hizi neno mtume linatumika kuhusiana na “wale 12” tu (yaani ukimtoa Yuda Iskaryote na kumweka Paulo, Waefe. 2:20; Ufu. 21:14), katika Kanisa lile la mwanzo neno apostle lilitumika katika kuwatambulisha wamisionari wengine pia (Luka 11:49; Matendo 14:4; Waefe. 2:20; Ufu. 21:14). Petro alikuwa mmoja kati ya “wale Mitume 12 wa Kristo”, karama ya kipekee ya kiroho ambayo iliwapa mamlaka ya kipekee, majukumu ya kipekee, na iliwalazimu kujitoa kwa namna ya pekee. Petro anaanza nyaraka zake kwa kujitambulisha kama mtume, Paulo pia, kwa sababu ndiyo alama ya mamlaka yao. Ni mitume tu walioandika vitabu na barua za Agano Jipya (na mara chache walitoa mamlaka ya kuandika vitabu hivyo, kwa mfano Marko alivyoandika kwa kusimamiwa na Petro, na Luka alivyosimamiwa na Paulo). Japokuwa alikuwa mtu mnyenyekevu sana, Petro hakujishusha pale alipotakiwa kuonyesha mamlaka yake ya kiroho, ya Kitume, kwani alijua kwamba mamlaka hayo yalitoka kwa Mungu. Mitume wa kweli wa Bwana Yesu Kristo walikuwa na tabia/sifa zifuatazo za kipekee:

 

  • Hawakuzidi kamwe ile idadi ya wale 12 wa mwanzo (Mathayo 10:2 na mistari inayofuata; nafasi ya Yuda Iskaryote ilichukuliwa na Paulo, cf, Matendo 9:1-19; 22:1-21; 26:12-18). Soma hapa chini juu ya Mathiya.

  • Walijitambulisha wenyewe kama Mitume (1Petro 1:1; 2Petro 1:1; War. 1:1; 1Wakor. 1:1).

  • Wote walikuwa na vipaji kadhaa maalum vya kimiujiza, vya kiroho, kuonyesha uhalali wa mamlaka yao (Matendo 5:12-16; Waebr. 2:3-4).

  • Kila mmoja wao alipewa majukumu maalum (Matendo 9:15-16; War. 11:13; Wagal. 2:7).

  • Wote walishuhudia ufufuko wa Bwana Yesu (Matendo 1:8; 1:22; 1Wakor. 9:1).

 

Kwa kumfanya Mtume, Bwana Yesu alimpa Petro jukumu kubwa sana, lakini pia alimpa mamlaka na uwezo wa kufanya shughuli zake zote katika maisha yake. Mungu hatupatii majukumu makubwa kuzidi uwezo aliotupatia wa kufanikisha majukumu hayo.

 

Mahitaji kwa Ajili ya Kukua Kiroho: Mpango wa Mungu juu ya Petro ulimletea mateso, kunyanyaswa na mwisho kumwaga damu yake, lakini Petro alimaliza mwendo wake na Kristo kwa kutumia neema zilizotolewa na Mungu kwa ajili yake. Naye Petro sasa amekuwa neema ya Mungu kwetu sisi. Kama vile tulivyohitaji Injili (ujumbe kuhusu Bwana Yesu) ili tuokolewe, vile vile tunahitaji ile kweli (misingi ya Neno la Mungu iliyo ndani ya Biblia) ili tuweze kupevuka kiroho. Petro aliitikia miito yote mitatu ambayo hutoka kwa Mungu: wito wa kuupokea wokovu, wito wa kupevuka kiroho na wito wa kuitumikia na kuieneza Injili. Na matokeo yake ni kwamba nasi pia tunapata fursa ya kukua kwa kujifunza na kuyaishi mafundisho yaliyomo katika barua zake zilizoandikwa takriban miaka 2,000 iliyopita.

 

“Mtume” Mathiya: Tukizungumzia suala la “Mitume 13” au “wanafunzi 13”, ni kweli kwamba mwanzoni kabisa mwa kitabu cha Matendo ya Mitume, Petro na wenzake “walimchagua” Mathiya kuchukua nafasi ya Yuda Iskaryote, lakini siyo kila kitu kilichoandikwa ndani ya Biblia ambacho watu mbalimbali wametenda kimeamriwa na Mungu (wazi kabisa)! Petro mwenyewe alifanya makosa mengi tu (mfano: “simfahamu mtu huyu!” - Mathayo 26:69-75; “Bwana, utaosha miguu yangu!?” “Basi na unioshe mwili wote!” - Yohana 13:6-11; na mengineyo). Kila sehemu katika maandiko ambapo Mungu mwenyewe anazungumzia Mitume Wake, anawataja 12 (kwa mfano kwenye misingi 12 ya ukuta wa Yerusalemu Mpya – Ufu. 21:14 na viti vya enzi – Mathayo 19:28). Ni majina ya nani yako kwenye ile misingi? Je, twaweza kudhani jina mojawapo litakuwa Mathiya? Sasa ni nani atakayeachwa? Kumbuka ule uchaguzi ulifanywa kabla ya Pentekoste, na baada ya hapo Petro na wenzake wakaanza kutenda mambo makuu (dhahiri, baada ya kujazwa na Roho Mtakatifu). Tazama pia kwamba ili “kumchagua” Mathiya walitumia ile dhana/mbinu ya Agano la Kale ya “bahati nasibu”, dhana/mbinu ambayo Bwana Yesu hakuitumia hata mara moja, na ambayo haikuhalalishwa katika Agano Jipya. Tizama pia kwamba Mungu hakuwasiliana na Petro na wenzake ya kwamba wakati umefika wa kumpata mwenzao mpya wa 12, japokuwa kumbuka Mungu alimwonyesha maona Petro wakati ulipofika wa kuipeleka Injili “kwa Wayunani” - yaani nje ya Israeli. Ona pia kwamba Mungu alipoamua kumdhihirisha “yule wa 12”, Kristo alifanya hivyo kwa kumtokea Paulo kimwujiza, katika namna ambayo ilimdhihirisha Paulo kuwa ndiye chaguo Lake la kuwa “yule wa 12”. Mathiya alikuwa muumini mahiri, bila shaka, lakini “hakuwa Mtume wa Kristo” isipokuwa kwa muda mfupi tu, mbele za macho ya wanadamu. Soma Matendo 2:14: “Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja ...” Hii ni baada ya ule “uchaguzi” wa Mathiya, uliofanyika katika Matendo 1:21-26. Alipochaguliwa Paulo, Mtume wa 12, ndipo idadi ya Mitume inakamilika tena. Kwani Bwana Yesu ndiye aliyechagua Mitume wake, sio mwanadamu yeyote, Naye alichagua kwa “kwa njia ya Roho Mtakatifu” si kwa “bahati nasibu”:

 

Matendo 1:1-3:

1.1 Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, [kwa ajili yako] Theofilo, katika habari ya mambo yote ambayo Yesu aliyafanya na kufundisha kutoka mwanzo,

1.2 hata siku ile Alipochukuliwa juu mbinguni baada ya kutoa maagizo, kwa mitume aliowachagua kwa njia ya Roho Mtakatifu. (SUV)

 

Matendo 9:15:

9.15 Lakini Bwana akamwambia [Anania], Nenda tu; kwa maana huyu (yaani Paulo) ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. (SUV)

 

=0=

 

Imetafsiriwa kutoka: Peter the Apostle and Suffering: Peter’s Epistle #2

 

=0=

 

Basi, na tuonane katika somo #3 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!