Nyaraka za Petro #25: Mateso ya Muumini

Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

Imani >> Moto wa Mitihani/Mateso >> Wokovu

1Pet. 1:6-9:
Katika kutazamia kwa hamu wokovu wa siku ile ya mwisho, furaha yenu inazidi sana, japokuwa kwa sasa yaweza kuwa mnateseka kwa muda mkipitia mitihani ambayo malengo yake ni kwamba imani yenu idhihirike kuwa ni halisi. Uthibitisho huu wa imani yenu una thamani kuu zaidi ya dhahabu, kwani dhahabu, japo nayo hupimwa ubora wake kwa moto, mwisho wake huharibika. Bali imani yetu, inapohakikishwa kuwa ni halisi katika majaribio makali ya maisha, itawasababishia sifa, utukufu na heshima kwenu pale Bwana Yesu Kristo atakaporudi katika utukufu wake. Ijapokuwa hamjamwona, mnampenda tu. Ijapokuwa hamwezi kumwona kwa wakati huu, mna imani juu Yake. Kwa sababu hii mna furaha ambayo hamwezi hata kuielezea, ambayo inaonyesha ile milele ijayo yenye utukufu, pale mtakapokabidhiwa ule ushindi mkuu wa siku ya mwisho – wokovu wa maisha yenu – ambao ndiyo lengo na nia ya imani yenu hii.

Utangulizi: Kabla ya kumaliza masomo ya aya hizi za 1Petro 1:6-9 na kuendelea, tunahitaji kuzungumzia mambo mawili zaidi ambayo yameunganika pamoja kwa ukaribu sana: (1) mateso binafsi ya muumini (kuongezeka kwa “majaribu na mitihani mbali mbali” inayotajwa katika aya ya 6 hapo juu), na (2) wokovu wa nafsi wa muumini (ile tuzo kuu inayotajwa katika aya ya 9, ambayo ndiyo matokeo ya imani). Katika somo hili tutajihusisha zaidi na dondoo ya kwanza, yaani mitihani binafsi ya muumini, lakini kwa kuwa lengo hili la wokovu binafsi linafikiwa kwa safari ya imani yetu katikati ya mitihani yetu binafsi, itasaidia hapa tukizungumzia kwa kifupi ile tuzo kuu ya mwisho kabla ya kuzungumzia mitihani binafsi.

Tuzo Kuu ya Mwisho ya Wokovu: Wokovu, “ukombozi wa maisha yenu” (kama Petro anavyoazimia katika aya ya 9), ni, kama mtume Paulo anavyothibitisha pia, nia ya msingi ya kila muumini, na lengo lake kuu:

9.24  Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate [tuzo].
9.25  Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote [anayoyatamani]; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo [hatimaye]; bali sisi [twashindana ili] tupokee taji isiyoharibika.
9.26  Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa [katika mazoezi];
9.27  bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha [katika mapambano]; isiwe, nikiisha kuwahubiri[a] wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.
1Wakor. 9:24-27 SUV (cf. Wafi. 3:12-16).

Ni kwa jinsi gani, basi, unashinda tuzo? Unapataje ushindi? Kama inavyosema aya yetu, kwa imani:

Huu ndio ushindi unaouzidi nguvu ulimwengu: imani yetu. (1Yoh. 5:4)

Kufanikiwa kuipata ile tuzo kuu ya mwisho ya wokovu, lile “taji la mwisho la ushindi”, imani yetu inapaswa kuendelea kustahamili, ikipita kwa usalama majaribu ya maisha na kuvuka katika tanuu la moto la dunia hii bila kuharibika. Ili kuupata ule ushindi wa mwisho, imani yetu ni lazima isafishwe kwa moto wa majaribu na wakati huo huo isiteketezwe kwa mpito wa maisha. Kwa uhakika tutapewa njia za kufanikiwa kupata tuzo hii ya wokovu kama tutaendelea kuwa wafuasi wa Bwana kwa imani ya kweli, hata kama imani hii ni ndogo kama punje ya haradali pale tunaponyanyua msalaba wetu na kuanza kumfuata. Kwani Yeye, kwa uaminifu mkubwa, atatupatia mahitaji yetu yote mengine katika vita hii ya kufa na kupona:

Naye Mungu wangu atawapatia ninyi kila mnachohitaji kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Yesu Kristo. Wafi. 4:19 SUV

Msisumbuke basi … kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua kuwa mnahitaji hayo yote. Matt. 6:31-32 SUV

Katika somo #22, tumezungumzia mafundisho ya Biblia yanayohusiana na mitihani ya muumini katika maisha yake. Mitihani, kama tulivyoona (1Pet. 1:6-7 hapo juu), ni jambo au zoezi ambalo kila muumini wa kweli katika Bwana Yesu Kristo anapitia, ambayo ndiyo kipimo cha uhalisia wa imani yake, na ni jambo la kila wakati katika maisha ya imani:

Kwa uhakika, wote wenye nia ya kuishi maisha ya Kimungu katika Yesu Kristo watateswa. 2Tim. 3:12

Hata hivyo kuna nyakati katika maisha ya waumini ambapo mitihani hii inakuwa mikali kiasi kwamba inaonekana kuvuka mpaka wa mitihani tu. Aina hii ya “mitihani ya moto” ya majaribu na mateso ya Wakristo tunaweza kuyaita, kwa uhalali kabisa, dhiki kuu (tribulation), kwani nyakati hizi kikwelikweli ni nyakati za mgongano mkuu wa kiroho ambao utatoa changamoto kubwa kwa imani yetu na mizizi yake.

Katika nyakati hizi za taabu kuu kwetu sisi binafsi, sisi waumini tunapaswa kutumia akiba zetu zote za imani ambazo tulizijenga katika tembea yetu ya imani. Vinginevyo tutakuwa katika hatari ya kuingia katika kundi la wale ambao “mmea wao wa imani” hauna mizizi ya kutosha na inanyauka kutokana na “mateso na mitihani wanayoipata kwa sababu ya Neno”:

13.20 Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha;
13.21 lakini hana mizizi ndani yake (yaani imani yake; cf. Lk. 8:13), bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa (hukwazwa; cf. Lk. 8:13: anaasi).
Matt. 13:20-21 SUV

Imani ni lazima ipitie nyakati hizi ili mwenye imani hii aweze kufikia wokovu ulioahidiwa. Kutokana na Ukristo wa Ki-biblia (tofauti na upagani), msingi wa kujiamini juu ya wokovu wetu unapaswa kuwa siyo kazi zetu wenyewe, bali imani yetu katika Bwana Yesu Kristo na kazi Yake msalabani kwa ajili yetu. Anachokitaka Mungu kutoka kwetu ni kwamba tuendelee kumtegemea na kumfuata Yeye. Katika nyakati za shinikizo kali, katika nyakati za taabu kuu za binafsi, hata hivyo, uendelevu na ustahamilivu wa imani yetu unalazimu kiasi kisicho cha kawaida cha ushupavu.

Ushujaa/ujasiri Chini ya Mashambulizi: Tunapozaliwa upya na kuwa Wakristo, tunaianza safari mpya ya maajabu ambayo itabadilisha maisha yetu milele.

5.17  Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama! Yamekuwa mapya.
2Wakor. 5:17 SUV (cf. Waga. 6:15; Waefe. 4:23-24)

Kwa uweza wa Mungu, kufumba na kufumbua, tunahamishwa kutoka huu ufalme wa giza na kuingia katika ufalme wa utukufu wa Mwana wa Mungu (Wakol. 1:13), na kuwa warithi wa Mungu Baba Mwenyewe (War. 8:17; Waga. 3:29; Waefe. 3:6; Tito 3:7). Lakini mabadiliko haya katika hadhi yetu ni katika nafasi tuliyo nayo ya sasa inapohusishwa na nafasi yetu ya milele. Hii ni kusema, uhalisia wa uraia wetu mpya hautaonekana au kuhisiwa kwa wazi mpaka pale Ufalme halisi wa mbinguni utakaposimikwa atakaporudi Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Hivyo, ingawa hadhi yetu ya kwamba tumefanywa “wana wa Mungu” ni ya maajabu makuu, haimaanishi kwamba vita yetu ya hapa katika himaya ya Shetani imeisha. Kwa hakika, katika namna nyingi mapambano yetu halisi ndiyo kwanza yanaanza wakati ule tunapoanza kuwa waumini wa Bwana Yesu Kristo. Hapa duniani, Shetani bado ni mtawala, na kwa kuhamishia uaminifu wetu kwa Kristo, tutegemee ghadhabu kutoka kwake (1Pet. 5:3):

5.19  Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika [mamlaka ya ] yule mwovu.
1Yoh. 5:19 (cf. Yoh. 16:11; 2Wakor. 4:4; Ufu. 11:15)

Biblia iko wazi. Tunaweza kutazamia upinzani ikiwa tutajaribu kumfuata Kristo, na, wakati mwingine, tujue kwamba upinzani huu utakuwa mkali:

14.22 wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.
Matendo 14:22 SUV (cf. Yoh. 15:20; 16:33; 2Tim. 3:12)

Bwana Yesu alituambia “tuhesabu gharama”, yaani tutambue kabla hatujawa wanafunzi wake kwamba tutazamie wakati mgumu sana (Lk. 14:25-35). Katika hali ya kawaida kabisa kwao, Ibilisi na watumishi wake wanatupinga sisi na jitihada zetu zote za kunyanyua msalaba wetu kila siku na kumfuata Kristo (Lk. 9:23), taswira ambayo kwa wazi kabisa inaonyesha/inaashiria mateso ambayo wafuasi Wake halisi watapitia:

8.17  na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.
War. 8:17 (cf. Matendo 5:41; 2Wakor. 1:5; Wafi. 3:10; Wakol. 1:24; 1Pet. 4:12-13)

Hivyo tusishangae pale tunapoona kila hatua tunayopiga kwenda mbele katika kupevuka kiroho inakutana na upinzani kutoka kwa adui yetu. Tunapaswa kukubali ukweli kwamba katika maisha yetu yote ya Kikristo tutakuwa “chini ya mashambulizi kutoka kwa adui”, na mashambulizi hayo yatazidi pale tutakaponyanyua vichwa vyetu nje ya handaki na kuanza kwenda mbele katika namna ile Bwana wetu Yesu Kristo alivyotuonyesha kwa mfano Wake. Hivyo basi, ikiwa tunataka kukua kiroho na kuwasaidia wengine wafanikishe suala hilo hilo (kupitia utumishi ambao Mungu ametuwezesha nao), kwa uhakika tutakabiliwa na taabu za binafsi katika maisha yetu. Ili tuweze kupambana na upinzani huu ni lazima tuwe na “ujasiri chini ya mashambulizi”, yaani nguvu ya imani inayoweza kupambana na upinzani wa Shetani ambao ni lazima tutakutana nao katika maisha yetu kama wafuasi wa Kristo:

6.16  zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
Waefe. 6:16 SUV

Taabu na Mateso Binafsi: Kama tulivyoona mara nyingi katika masomo yaliyopita, majaribu ya imani yetu ni kiambato muhimu na cha lazima kwa kukua kiroho (tizama somo #22). Suala hili (kama tulivyoona) linazungumzwa kwa undani na Petro katika muktadha wa aya za 1Petro tunazozisoma hapa, na pia jinsi Petro anavyolizungumzia suala hili lote ndio chanzo cha somo hili zima la “Nyaraka za Petro”. Neno la Kiyunani linalotumika katika Agano Jipya katika kuelezea mateso binafsi ni thlibo, na maana yake halisi ni “kushinikiza kwa nguvu au kubana ndani ya sehemu nyembamba”, maelezo ambayo yanatupa taswira ya wazi ya kile kinachowangojea wale wanaokiri imani kwa Bwana Yesu Kristo.

Kama Wakristo, tutapitia mitihani.

Kama Wakristo, imani yetu itawekwa na kupitia shinikizo.

Kama Wakristo, tutakabiliwa na mashambulizi ya Shetani.

Na japo tutakabiliwa na kiasi fulani cha upinzani siku hadi siku, ni kweli pia kwamba mitihani fulani tutakayoikabili itakuwa mikali, mara nyingi ikitushambulia ghafla na kwa nguvu ya kimbunga/tufani. Mitihani ya namna hii kwa kweli iko katika kiwango cha taabu kuu, na tunatakiwa kuwa tayari, tumejitayarisha kukabiliana na [ma]shinikizo haya makali dhidi ya imani yetu.

Misingi ya Taabu na Mateso ya Mkristo:

1. Taabu na mateso ni jambo la kila wakati:

4.12  Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba (maana yake mateso) ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.
1Pet. 4:12 SUV

2. Taabu na mateso yatatukuta, lakini tunao uwezo wa kuyakabili:

10.13  Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida [katika maisha] ya wanadamu; ila [zaidi ya hapo] Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo [kustahamili]; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea [namna ya kutatua tatizo], ili mweze kustahimili [shinikizo].
1Wakor. 10:13

3. Taabu na mateso havina mbadala:
14.22 wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.
Matendo 14:22 SUV

4. Taabu na mateso ni muhimu ili kutuwezesha kusafisha/kutakasa na kuboresha imani yetu:

Katika kutazamia kwa hamu wokovu wa siku ile ya mwisho, furaha yenu inazidi sana, japokuwa kwa sasa yaweza kuwa mnateseka kwa muda mkipitia mitihani ambayo malengo yake ni kwamba imani yenu idhihirike kuwa ni halisi. Uthibitisho huu wa imani yenu una thamani kuu zaidi ya dhahabu, kwani dhahabu, japo nayo hupimwa ubora wake kwa moto, mwisho wake huharibika. Bali imani yetu, inapohakikishwa kuwa ni halisi katika majaribio makali ya maisha, itawasababishia sifa, utukufu na heshima kwenu pale [Bwana] Yesu Kristo atakaporudi katika utukufu wake.
1Petro 1:6-7

5. Taabu na mateso ni dalili ya kupevuka kiroho (na kutokuwepo kwake ni dalili ya kutokomaa kiroho):

1.3  Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;
1.4  atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu.
1.5  Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu [katika huduma yetu kwenu], vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo.
1.6  Lakini ikiwa sisi tu katika dhiki, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu; au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu [mnayoipokea]; ambayo hutenda kazi yake kwa kustahimili mateso yale yale tuteswayo na sisi.
1.7  Na [hivyo] tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja.
2Wakor. 1:3-7 SUV

12.4  Hamjafanya vita hata kumwagika damu [yenu], mkishindana na dhambi;
Waebr. 12:4 SUV

6. Taabu na mateso yaweza kuwa chanzo cha furaha:

5.40 Wakakubali maneno yake; nao (baraza) walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao.
5.41 Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo.
Matendo 5:40-41

7. Taabu na mateso mara nyingi huja katika wakati mbaya kwetu (kwani Shetani anajua wakati mzuri kwake wa kushambulia):

5.8  Mwe na kiasi [watulivu - “sober”] na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.
1Pet. 5:8

8. Taabu na mateso vinatufanya tuwe na nguvu zaidi:

5.3  Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;
5.4  na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini [la thawabu ya milele]
War. 5:3-4

Mifano ya Taabu na Mateso Binafsi Katika Historia: Enzi za zamani, za sasa na za baadaye zinatupatia mifano ya kutosha ya mateso yanayowakuta na yatakayowakuta waumini wa Kristo. Tukitizama mtu mmoja mmoja, tunaweza kusema kwa uhakika kwamba, kutokana na ushuhuda wa zile Injili 4 za Kristo, hakuna aliyeteswa kwa sababu ya upendo wake kwa Mungu zaidi ya Bwana wetu katika wakati wa utumishi wake hapa duniani:

Kama ilivyotabiriwa katika Zaburi 22:12-18:

12 [Kama] Mafahali wengi wamenizunguka, [Kama mafahali] Walio hodari [wenye nguvu] wa Bashani wamenisonga;
13 Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma.
14 Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya mtima wangu.
15 Nguvu zangu zimekauka kama gae [la chungu], Ulimi wangu waambatana na taya zangu [kwa kiu]; kwani Unaniweka katika mavumbi ya mauti [cf aya 1-2]
16 Kwa maana [kama] mbwa, wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenizua [wamenitoboa] mikono na miguu.
17 Naweza kuihesabu mifupa yangu yote. Wao wananitazama na kunikodolea macho,
18 [Wakati] Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura.

Kama ilivyotabiriwa katika Isaya 53 SUV:

1 Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana (i.e. Masihi) amefunuliwa nani?
2 Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi [unaochipua] katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.
3 [Kinyume chake] Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu [wa maana].
4 Hakika ameyachukua masikitiko [magonjwa] yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
5 Bali [kwa kweli] alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa [sababu ya] maovu yetu; Adhabu ya [kufanikisha] amani yetu [na Mungu] ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
6 Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.
7 Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.
8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeyasimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
9 Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake [in His *deaths]; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
10 Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake;
11 Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi [walio na moyo shujaa - waumini] kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu (hatia zao) yao.
12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari**; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa, Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea [akajiweka mahala pa] wakosaji.

[*NOTE: In His Deaths (in the original Hebrew) to emphasite the intensity of His physical suffering and the spiritual separation of His humanity from the Father during the 3 hrs of suffering
** Waumini]

Tunapofuata nyayo zake na kuiga mfano wake [wa maisha yake], tutazamie upinzani kama ule alioukabili Yeye. Paulo anavyotuambia tumu-ige yeye (Paulo), kama yeye anavyomu-iga Kristo (1Wakor. 11:1), kwa uhakika hamaanishi kwamba hatutateswa kama Kristo, na, ukiacha Bwana wetu, hakuna mwingine aliyeteseka kwa ajili ya imani yake ya Kikristo kama mtume Paulo:

Kama anavyoeleza katika 1Wakor. 4:9-13 SUV:

4.9  Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume [tuonekane kuwa watu wa] mwisho [chini kabisa], kama watu waliohukumiwa wauawe; kwani tumekuwa tamasha kwa dunia [nzima]; kwa malaika na wanadamu.
4.10  Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya [utumishi wetu kwa] Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi [tunaonekana] tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima.
4.11  Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao;
4.12  kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili;
4.13  tukisingiziwa [uwongo] twasihi [na kufariji]; tumefanywa kama takataka za dunia, na [uchafu wa watu wote] tama ya vitu vyote hata sasa.

Kama anavyoeleza katika 2Wakor. 11:23-28 SUV:

11.23  Wao ni wahudumu wa Kristo? [Nanena kiwazimu], hata kama hayo ni madai yao, mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo (kupigwa) kupita kiasi; katika [hatari ya] mauti mara nyingi.
11.24  Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja.
11.25  Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini [nikielea juu ya maji];
11.26  katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari [kutoka] kwa [watu wa] taifa langu [mwenyewe]; hatari [kutoka] kwa [watu wa] mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu [wakristo wa] za uongo;
11.27  katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu;
katika baridi na kuwa uchi [bila nguo stahiki].
11.28  [Na] Baghairi (zaidi) ya mambo ya nje (ya kimwili), yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote.

Ijapokuwa si wote tutakaoitwa “kuwa washiriki wa mateso ya Kristo” (2Wakor. 1:3-7) kwa kiasi ambacho Paulo alifikia, sisi pia ni lazima tuwe tayari kuzikabili changamoto zetu, ambazo nazo zinaweza kuwa ngumu kuvumilia. Taabu na mateso binafsi yatawapata waumini wote, sio tu waumini wa pekee sana wa kiwango cha Paulo. Ili kujitayarisha kwa ajili ya mtihani wa taabu na mateso binafsi na kustahamili mashambulizi yake, tunaweza kufaidika na yaliyowakuta waumini wengine waliokabiliwa na mitihani inayofanana [ili itusaidie]. Kwani, kama mwandishi wa waraka kwa Waebrania anavyoweka wazi, waumini wa kale mara nyingi walikabiliana na mateso makali kwa ajili ya imani yao:

11.32  Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii;
11.33  ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba,
11.34  walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.
11.35  Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya [waliteswa] wasikubali ukombozi [wakikataa nafuu ya mateso hayo kwa masharti], ili wa[u]pate [ule] ufufuo [wa mwisho] ulio bora;
11.36  wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;
11.37  walipigwa kwa mawe, walikatwa [kiwiliwili] kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;
11.38  (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.

Waebr. 11:32-38 SUV

Walengwa wa waraka wa kwanza wa Petro: Mara moja moja katika historia ya waumini hapa duniani, taabu na mateso yamezikumba jamii nzima za waumini katika vipindi/nyakati za mateso yaliyolenga kundi fulani. Hii ndiyo hali iliyowakuta jamii ya Wakristo wa Asia Ndogo ambao walikuwa sehemu ya walengwa wa barua/waraka wa kwanza wa Petro. Kama tulivyodokeza mwanzoni kabisa mwa mfululizo wa masomo haya, (somo #1), mateso ya Wakristo wa Roma yaliyofanywa na Nero katika takriban mwaka 64 A.D. yalisababisha pia mateso mengine katika majimbo ya Ufalme wa Rumi. Mwandishi wa historia ya Rumi Tacitus anasimulia mauaji ya kikatili ya jumuiya ya Wakristo kwa uwazi kabisa. Nero alijaribu kuwasingizia Wakristo kwamba walihusika na moto ulioteketeza sehemu kubwa ya mji wa Roma, moto ambao kwa kweli yeye ndiye aliyehusika nao, alianza kuwatesa Wakristo hao akitumia njia za kutisha na za kikatili. Kwa sababu tu ya imani yao, Wakristo walisulubiwa, walitupwa katika moto mkali, walivishwa ngozi mbichi za wanyama na kukimbizwa na kuliwa na mbwa mwitu.

Vurugu hizi zilizoanza Roma zilienea mpaka katika majimbo yote ya ufalme wa Rumi; historia haina fununu nyingi zinazosimulia matukio haya ya kale, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba mateso anayoyataja Petro katika 1Petro ni matokeo ya matukio haya ya mji mkuu – Roma – ambayo Petro bila ya shaka aliyashuhudia mwenyewe. Kwani kama tulivyoona, 1Petro na 2Petro ni nyaraka zilizoandikwa kutoka Roma katika kipindi hicho hicho (Petro mwenyewe yumkini aliuawa kwa ajili ya imani yake mara baada ya mateso haya ya Wakristo, miaka kadhaa kabla ya mwisho wa utawala wa Nero mwaka 68 A.D.).

Mfano Mwingine Kutoka Kanisa la Yerusalemu: Ijapokuwa hatuna fununu za kutosha kuhusu uelekeo na ukubwa wa mateso ya Nero juu ya Wakristo katika majimbo ya ufalme wa Rumi, kuna ushuhuda wa kutosha katika kitabu cha Matendo ya Mitume (pamoja na dondoo zinzozungumzia mateso kwa Kanisa katika barua mbali mbali kama hizi za Petro) kuhusu njia ngumu ambayo Wakristo wa karne ya kwanza walilazimika kupita. Jamii ya Wakristo waliokuwa Yerusalemu inatupatia mfano wa kutosha wa athari na mwelekeo wa mateso yaliyofanyika pale ambapo ni chanzo/kiini cha Ukristo:

• Wakristo wa Yerusalemu walitengwa kijamii na kiuchumi na kuteswa (Matendo 2:42-47; 4:32-35; 11:28-30; 24:17; War. 15:25-28; 1Wakor. 16:1-4; Wagal. 2:10).
• Viongozi wao walipigwa (Matendo 5:41-42), walifungwa (Matendo 12), walipigwa kwa mawe (Matendo 7:57-60), na kuuawa kwa namna nyingine (Matendo 12:2-3).
• Baadaye waumini wenyewe waliteswa sana, walifukuzwa kutoka Yerusalemu, kutoka katika nyumba zao, walifungwa na kuuawa (Matendo 8:1-3; 9:1,13).
• Imani ya wengi wao ilipata changamoto nyingi kutokana na matukio haya (Yak. 1:2-7; cf. Wagal. 3:4; 1Wathess. 2:14). Miaka kadhaa baada ya migogoro hii kuisha, mwandishi kwa Waebrania alikumbuka majaribu na mitihani mikali waliyopitia:

10.32  Lakini zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano [majaribu] makubwa ya maumivu;
10.33  pindi mlipotwezwa kwa mashutumu, [dhihaki] na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo.
10.34  Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang'anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo.
10.35  Basi msiutupe ujasiri [wa imani] [y]wenu, kwa maana una thawabu kuu.
10.36  Maana mnahitaji [kuendelea kwa] saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate [kutimiziwa] ile ahadi.
10.37  Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.
10.38  Lakini mwenye haki [mwongofu] wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.
10.39  Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao [katika imani yao] na kupotea [kwa woga], bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu [milele]. Waebr. 10:32-39 SUV
Changamoto za Kuishi Katika Nchi ya Kipagani: Yaliyowatokea waumini wa Yerusalemu yanatupatia fununu ya magumu yanayohusiana na kuishi kama Mkristo katika nchi ambayo msingi wake umeunganishwa imara na ibada ya sanamu na mapepo. Matatizo haya yalifika hata nje ya maeneo ya kanisa la Yerusalemu. Kwa hakika, katika maelezo ya mtume Yohana katika Ufunuo sura za pili na tatu juu ya [ma]shinikizo waliyopitia makanisa yale saba ya Asia Ndogo, inaonekana wazi kwamba wengi kati ya Wakristo wa karne ya kwanza walikabiliwa na mateso kila siku.

Ukweli kwamba waumini hawa wa mwanzo walikuwa hatarini kuchukuliwa kama wahalifu unaonekana katika barua za Pliny the younger. Kuna barua yake moja ambayo imetunzwa tangu kale hizo inayotoka kwa Pliny (enzi hizo akiwa Gavana wa jimbo la Rumi la Bithynia la Asia Ndogo) ikienda kwa mfalme Trajan. Akiandika takriban mwaka 112A.D., Pliny alikuwa akiomba maelekezo ya namna ya kuwashughulikia Wakristo katika jimbo lake. Pliny alikuwa akimwomba mfalme Trajan amwelekeze bayana, ikiwa mtu akikubali kwamba yeye ni “Mkristo” basi (je) huo ni ushahidi tosha unaostahili kuchukuliwa hatua za kisheria(?), swali ambalo linaonyesha wazi hatari za kuwa Mkristo mahali pale na katika enzi hizo. Mfalme akamjibu Pliny kwamba hakuwa na sababu ya kuwasaka na kuwakamata [Wakristo], lakini mara mtu yeyote akitambulika kuwa ni Mkristo basi auawe kama atakataa kuikana imani yake hiyo na kutoa kafara stahiki kwa mfalme.

Hali hii ya hatari iliwaweka Wakristo hawa bila ulinzi wowote [kutoka kwa serikali yao wenyewe], hivyo waliweza kushambuliwa na mtu yeyote mwenye nia mbaya nao, kama vile chuki binafsi (kwa mfano chuki ya wivu uliosababishwa na watu wa mataifa kuipenda Injili: Matendo 17: 1-5), au sababu za kiuchumi (kwa mfano mateso waliyopata Paulo na Sila kule Filipi, Matendo 16:19; na pia mfano wa fujo zilizotokea Efeso kwa sababu ya kuogopa kwamba imani hii mpya itahujumu biashara ya sanamu za mungu wa uwongo wa kipagani Artemis, Matendo 19:23-41). Pia ilikuwa vigumu sana kuwa nje [kujitenga na] ya ule ushawishi mkubwa sana wa kipagani wa jamii ya Kirumi ya wakati ule. Kwa mfano, kama mtu alikuwa anahusika na biashara au uzalishaji/viwanda, ilikuwa vigumu sana kwake kufanya kazi hizi bila kujihusisha na kujiunga na collegium ya maeneo yake – wilaya, mkoa, nk. Collegia (chanzo cha neno la Kiingereza “college”) ndivyo vilikuwa vyama vya wafanyibiashara na wenye viwanda/wazalishaji ambavyo vilikuwa na faida mbali mbali ikiwa ni pamoja na faida zinazotokana na kuwa mwanachama [leo hii] katika vyama kama Rotary Club, Kiwanis, Chamber of Comerce, au bodi ya Madaktari, Wahandisi, Wanasheria au wafanyakazi. Ni rahisi kuona hapa jinsi ilivyokuwa vigumu kwa Mkristo ambaye ni mfanyabiashara au mtaalamu wa aina fulani, kama mhandisi, nk, ambaye si mwanachama wa collegium ya nyanja yake hiyo kupata mafanikio au hata kuonekana tu kwamba yeye ni Mkristo. Tatizo lilikuwa kwamba hizi collegia zote zilikuwa kila moja ina mungu wake [wa sanamu] wa kipagani, na ili uwe mwanachama ni lazima utoe sadaka, ule vyakula vilivyotolewa kwa “mungu” huyo, na aina nyingine za kuabudu sanamu, mambo ambayo yote yamekatazwa kwa Mkristo (cf. Kutoka 23:13; Joshua 23:7; Zab. 16:4).

Hivyo waumini wa karne ya kwanza walikabiliwa na [ma]shinikizo na vishawishi vya jamii ambayo ilikuwa potovu kama hii tunamoishi katika karne hii, lakini pia walilazimika kujichunga dhidi ya hatari ya wakati wote ya mateso kwa upande mmoja, na hatari ya kuvuruga imani yao kwa upande mwingine (kupitia kuvunja sheria/amri ya Mungu). Katika mazingira ya namna hii, tanzia binafsi na vikwazo vinavyofanana vinafanya maisha kuwa ya taabu sana: ni imani chanya, yenye nguvu tu ndiyo inayoweza kustahamili vurugu kali kama hizi ambazo kwa kweli ni tishio katika kukua kiroho.

Kwa hawa Wakristo wa mwanzoni, msemo wa taabu na mateso binafsi ulikuwa na maana ya pekee. Hata hivyo, kinyume na unavyoweza kutarajia, miaka hii ya kukua kwa Kanisa ilikuwa kati ya vipindi vya kusisimua na kutia moyo ambavyo Kanisa la Bwana Yesu Kristo vilipata kupitia, hali hii ikitupatia ithibati ya ule msemo maarufu wenye hekima wa Tertullian kwamba “damu ya wale waliojitoa mhanga ilikuwa ndiyo mbegu ya Kanisa”. Hii ni sahihi kabisa kwa kanisa la Yerusalemu, kwani Luka anatuambia kwamba mateso waliyopitia yalikuwa na matokeo chanya na ya moja kwa moja katika kukua kwa Kanisa la Kristo:

Na hivyo walitawanywa, na wakaenda katika uelekeo mbali mbali duniani, wakitangaza habari njema kote walikopita.
Matendo 8:4

Mwelekeo wa Siku za Usoni Katika Ile Taabu, Mateso na Dhiki Kuu: Kwa uhakika si sahihi kudhani kwamba taabu na mateso binafsi ambayo sisi hukutana nayo kama waumini hayatatokea tena kama tatizo kwa imani yetu katika siku za usoni. Kitabu kilichoandikwa na Foxe kiitwacho Book of Martyrs, kwa mfano, kinatoa maelezo ya kutisha ya mateso makubwa waliyopitia Wakristo wengi wakati wa kipindi cha historia kinachoitwa “the Reformation”. Na kufa kwa ajili ya imani ya Kikristo bado kunaendelea hata leo. Katika nchi zenye utawala wa ki-imla (mfano China) na ule wa makasisi (mfano Sudan kabla ya kutengana) waumini, kwa wakati huu na uliopita, wanapitia na walipitia mateso makubwa na hata kufa kwa ajili ya imani yao katika Bwana Yesu Kristo. Tutakuwa tunakosea pia kudhani kwamba mambo kama haya hayawezi kutokea katika nchi zetu. Kwani pale Mungu atakapoondoa kizuizi cha Mungu kinachobana uvunjaji wa sheria Yake, ulimwengu mzima utaingizwa katika taabu, mateso na dhiki kuu (The Great Tribulation) – 2Wathess. 2:6-12.

13.19 Kwa maana siku hizo zitakuwa na dhiki, jinsi isivyokuwa [ambayo haijakuwa] tangu mwanzo wa kuumba alipoumba Mungu hata sasa, wala haitakuwa [tena] kamwe. Marko 13:19 SUV

Hili neno “tribulation” ni tafsiri ya neno la Kiyunani “thlipsis” ambalo tumekuwa tukilitafsiri kwa Kiswahili kama “taabu na mateso binafsi” katika somo mpaka sasa:

Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo [mtapitia] dhiki (tribulation); lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu! Yoh. 16:33 SUV

Hulka ya Dhiki Kuu ijayo (Matt. 24:21; Mrk. 13:19) – kipindi ambacho sisi sote tulio hai wakati huu tunaweza kukutana nacho – inatupa tahadhari ya kiasi cha uimara wa imani inayotakiwa kupambana na tufani ile: Baadhi ya dalili zilizotabiriwa kwa wakati ule mgumu wa sura ya mwisho ya historia ya mwanadamu inaonyesha kwamba utakuwa wakati wa …

• “Uasi Mkuu pale waumini wa Kikristo watakapomwasi Mungu wao katika idadi kubwa (Matt. 24:9-14; 2Wathess. 2:3; 1Tim. 4:1).
• Vita kali za uvamizi (Dan. sura 7,9,11; Eze. Sura. 38-39; Ufu. 6:2; sura ya 13).
• Vurugu za kiraia (Ufu. 6:4).
• Taabu kuu za kiuchumi (Ufu. 6:6).
• Ukame, magonjwa ya mlipuko na majanga ‘ya asili’ yatakayosababisha kupotea kwingi kwa uhai (Ufu. 6:8; Isa. 13:12).
• Dini moja tu, kubwa ya kipagani kwa dunia nzima, itakayokuwa adui mkubwa kwa Ukristo wa kweli wa Kibiblia (Ufu. 13).
• Mauaji duniani kote ya waumini wa kweli wa Kristo (Ufu.6:9-11).
• Hukumu kali juu ya dunia (Ufu. 6:12ff; 9:1ff; 16:1ff).

Kipindi cha dhiki kuu kitakuwa cha kutisha, na changamoto itakayowakabili waumini wa kweli itakuwa ngumu, kiasi kwamba Bwana wetu alitamka: “… atakapokuja Mwana wa Adam, je! Ataiona imani duniani?” (Lk. 18:8 katika muktadha wa Lk. 17). Hata hivyo, kuna wale watakaoendelea katika imani yao licha ya tufani ya moto itakayokuwako, imani yao ikitakaswa na kuboreshwa na dhiki itakayokuwako (Dan. 11:35; 12:10; linganisha na 1Pet. 1:6-9 mwanzoni mwa somo hili).

Umuhimu Mkubwa wa Kustahamili: Hivyo, ikiwa tutalazimika kukabiliana na kipindi cha Dhiki Kuu (The Great Tribulation), au taabu na mateso binafsi “tu” (ambayo nayo ni makuu pia na yatatoa changamoto kubwa kwa imani yetu), umuhimu wa kustahamili katika imani yetu, tukiwa katikati ya magumu hayo nao pia unatiliwa mkazo hapa. Inabidi tuwe makini na uwezo wa shida hizi wa “kupima” imani yetu kwa kiasi (ukali) kikubwa sana. Biblia inatutabiria DHIKI KUU ya binafsi na DHIKI KUU kwa ujumla (kwa Wakristo wote), na kama tuna majaliwa (destiny) ya kuwepo katika ile dhiki kuu ya siku za usoni …

Je, tunaweza kudharau umuhimu wa kuimarisha imani yetu?

Je, tunaweza kudharau fursa [hata moja tu] ya kuimarisha imani yetu?

Je, tunaweza, kwa kifupi, kufanya lolote ambalo litahatarisha uimara wa mkono wetu ulioshika imani yetu ambayo ndiyo ushindi katika Bwana wetu Yesu Kristo dhidi ya kifo?

Tukiwa na maswali haya akilini, tutarudia tena misingi ya ustahamilivu katika somo lijalo, na tutazungumzia mchakato wa uasi ambapo baadhi ya waumini wanaanguka kutoka katika imani yao chini ya [ma]shinikizo ya taabu na dhiki binafsi au chini ya [ma]shikizo ya jumla/kanisa (cf. Kanisa la Yerusalemu, hapo juu), na tutaendelea kutoka hapo na kuingia katika somo la wokovu wa nafsi, lengo la ustahamilivu, katika somo linalofuata.

=0=

Imetafsiriwa kutoka: Personal Tribulation: Peter’s Epistles #25

=0=

Basi, na tuonane katika somo #26 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!