Ustahamilivu wa Imani: Nyaraka za Petro #21
Na Dr. Robert Dean Lugibill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission For This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

1.3  Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;
1.4  ili tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.
1.5  Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani ili/[hata] mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.
1Petro 1:3-5 SUV

Utangulizi na Mapitio: Tasnifu au hoja kuu ya 1Petro 1:3-5 (nukuu hapo juu) ni kwamba, kama Wakristo, tumezaliwa upya, na kwamba kuzaliwa huku upya kunapelekea sisi kuingia katika mahusianao mapya ambayo yanabadilisha kabisa namna tunavyokabiliana na dunia hii. Petro anatuhesabia mabadiliko matatu muhimu, akitanguliza kila dhana ya badiliko kwa kutumia kihusishi (preposition) eis [katika lugha ya Kiyunani] maana yake “katika/ndani ya”, kikiwakilisha kuingia kwetu katika baraka mpya tatu mara tunapookolewa. Baraka hizi tatu ni, kama zilivyopangwa katika aya hizo hapo juu, tumaini lenye uzima, urithi usioharibika, na wokovu utakaofunuliwa siku ya mwisho. Baraka zote tatu zinazungumzia maisha ya utukufu yatakayokuwapo baada ya kurudi kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Uzima mpya tulio nao kama Wakristo, hadhi ya kuwa “wazaliwa wapya” mbele za macho ya Mungu ni [kama] kiunganishi katika mioyo yetu, kikituunganisha imara kabisa na uhalisia ulioko mbinguni ambao siku moja utafunuliwa. Tumaini lenye uhai, urithi usioharibika, na wokovu utakaofunuliwa, aina tatu za baraka ambazo ndani yake tumezaliwa upya kwa neema ya Mungu kupitia imani yetu kwa Bwana Yesu Kristo, zote ni zawadi tofauti za huu uzima mpya katika Kristo, na kila moja inaoana na moja kati ya maadili matatu ya maisha ya Kikristo ambayo tumeyazungumza.

Tumaini Lenye Uzima: Kwanza, tumezaliwa upya “katika tumaini lenye uzima kwa ufufuo wa Bwana Yesu Kristo kutoka katika wafu”. “Tumaini lenye uzima” linazungumzia ufufuo wa miili yetu, mabadiliko, kama tulivyoona, ya miili yetu ya hapa duniani, yenye dosari ya dhambi, na kuwa miili yenye utukufu wa milele kwa minajili ya ule uzima tulio nao sasa hivi kwa ahadi, ambao utakuwa wetu katika maajabu yake yote pale Kristo atakaporudi. Uadilifu wa tumaini una kiini chake katika imani kamili juu ya uhalisia wa matokeo haya ya wakati wa mwisho, na unatupa nguvu ya kuhimili uharibifu wa miili yetu na masikitiko mengi mengine ya maisha ya hapa duniani.

Urithi Usioharibika: Pili, tumezaliwa upya “ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, unaotunzwa mbinguni kwa ajili yetu”. Huu “urithi usioharibika” unamaanisha ile thawabu ambayo kila Mkristo atapokea mbele ya kiti cha hukumu (kutathminiwa) cha Kristo, ambapo matendo yetu yote ya hapa duniani (baada ya wokovu) yatafanyiwa tathmini na si mwingine bali Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe. Thawabu hizi zitadumu milele na hazifanani na kitu chochote tunachoweza kufaudu hapa duniani wakati huu wa utawala/himaya ya Shetani. Kama vile wana wa Israeli walivyongojea kwa shauku, kwa vizazi kadhaa, kuuona mwisho wa mizunguko yao isiyokuwa na makazi maalumu jangwani na kuingia kwa shangwe na utukufu katika nchi waliyoahidiwa na Mungu, vivyo hivyo nasi tunangojea kwa shauku siku ambayo tutaingia katika ufalme wa mbinguni tukimfuata Bwana Yesu Kristo, na kuvuna matunda ya kazi yetu tuliyoifanya hapa duniani [baada ya wokovu]. Uadilifu wa upendo unatangamana na taswira na ukweli huu wa kuzaliwa kwetu upya, kwani kama vile upendo wa Mungu kwa wanadamu ulioonyeshwa na nafsi ya Kristo unavyoakisiwa nasi katika mwenendo wetu na utumishi kwake, vivyo hivyo tutapata thawabu. Tofauti na thawabu za maisha ya sasa, thawabu za milele haziharibiki kamwe. Haziwezi “kuharibika, kunajisika wala kufifia”, na haziwezi kudhurika wala kupungua kwa namna yoyote, bali zitakuwa zetu kuzifaudu milele na hakuna mwizi anayeweza kuziiba na wala hakuna wadudu waharibifu wanaoweza kuziharibu. Thawabu hizi (ambazo zinaakisi upendo tulio nao kwa Bwana wetu Yesu Kristo na ambao tunauonyesha katika maisha yetu ya hapa duniani), msingi wake hauko katika kudonoa-donoa na makwaru-kwaru ya hapa duniani, bali uko katika ukaribu mkuu wa Mungu mwenye neema (tizama Petro #18 “Mataji”).

Wokovu Utakaofunuliwa Siku ya Mwisho: Tatu, tunao uhakika wa wokovu wetu, sisi, ambao kama waumini katika Kristo “tunalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata tupate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho”. Huu “wokovu wa siku za mwisho” unazungumzia kutimizwa katika historia ya wanadamu kwa ahadi zote za Mungu kwa kila mmoja wetu kama muumini, kwani “tunanyakuliwa kutoka katika moto wa hatia” hapo mwishoni mwa historia ya wanadamu. Petro anachukulia kwamba wasomaji wake wanajua zile hoja muhimu kuhusu zile “nyakati za mwisho” na hivyo wataungojea wokovu unaotegemea imani inayoendelea na isiyokoma kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika tukio la ufufuo ndipo ahadi hii ya maandiko itakapotimizwa, na hivyo wakati halisi na mazingira ya wokovu vitatofautiana, kwani ujio wa pili wa Bwana wetu unatenganisha matukio mawili ya ufufuo kama tulivyoona hapo nyuma. Lakini tutakaposimama mbele ya Bwana wetu tukiwa katika miili yetu mipya, tukitoa hesabu ya maisha yetu, lengo litakuwa ni kutathmini huduma yetu, utumishi wetu, na siyo wokovu wetu (1Wakor. 3:15). Kama vile “tumaini lenye uzima” linavyoelekezwa kwenye ufufuo na “urithi usioharibika” unavyoelekezwa kwenye fikra adilifu ya upendo, vivyo hivyo “wokovu wa siku za mwisho” unaelekezwa kwenye uadilifu mkuu wa imani. “Tunalindwa kwa nguvu ya Mungu katika imani yetu” kama aya ya tano inavyosema. Hulka ya nguvu ya Mungu isiyotetereka ni ya kutegemewa [wakati wote], lakini kutokana na udhaifu wa mwanadamu, tutalizungumza hili kwa kirefu hapa – suala la uhakika wa wokovu – kwa sababu “wokovu wa siku za mwisho” unategemea imani. Kama tulivyoona katika somo #18, taji la utukufu ni thawabu ya Wakristo wanaoongeza juu ya imani yao na juu ya tumaini lao, huduma na utumishi halali, unaochangia katika wokovu na kupevuka kwa Wakristo wenzao. Taji la uhai/uzima ni thawabu ya Wakristo wanaoendelea kiroho, wanaoongeza juu ya imani yao, maisha yanayodhihirisha imani hiyo katika kuukabili ukinzani, majaribu na mateso. Taji la uongofu/uadilifu ni thawabu wanayoipata wale wanaofanikiwa kupevuka kiroho katika maisha yao. Hivyo sasa tutaenda kwenye fundisho linalozungumzia kudumu katika imani, na kupoteza imani.

Kudumu Katika Imani: Imani ni moja kati ya maadili muhimu ya Kikristo. Ni katika imani yetu kwake Bwana Yesu Kristo sisi tunakuwa Wakristo na tunaendelea kuwa Wakristo. Tulipoamua kuwa Wakristo, imani yetu ilinyoosha mkono na kuipokea habari njema za Bwana Yesu Kristo. Si kwa uwezo wa kufikiri, wala kwa majaribio ya [ki]sayansi, bali kwa kuamini, kwa imani tumeipokea Injili, tulimwamini Bwana Yesu Kristo. Hatukumngojea Mungu atuthibitishie Injili, bali bila ushahidi/ithibati, bila kuona, tuliweka imani yetu katika Neno la Mungu, ahadi ya Mungu. Tuliamini kile Mungu alichotuambia katika maandiko Yake, kwamba kupitia imani katika Yesu Kristo hatutaangamia na ulimwengu huu, bali tutakuwa na uzima wa milele. Mungu alituahidi hivyo nasi tuliamini. Tulimtumainia, tulitegemea uadilifu Wake, hulka Yake, tulitegemea kwamba alichoahidi atakitimiza, bila upendeleo na kwa haki, kwani Yeye ni Mungu. Katika kumtoa sadaka Mwanaye wa pekee, Bwana Yesu Kristo, katika ushuhuda mkubwa sana wa maandiko, na katika maisha yetu ya kila siku, sasa tunaona kwa macho ya imani kile ambacho Roho Mtakatifu alituwekea wazi wakati ule: kwamba Mungu anastahili tumaini letu, kwamba Yeye anastahili kutumainiwa. Mungu hajawahi kutuangusha, na kamwe hatotuangusha. Wote wanaomwamini Mwanaye ni watoto wake; hawataangamia pamoja na dunia hii. Kwa hakika tunawekwa salama kwa sababu ya ulinzi wake wenye uwezo mkuu, hata kama macho yetu ya kimwili yanatuonyesha vinginevyo. Kwa hakika “tunawekwa salama kwa uweza wake” - na “kwa imani yetu”. Kwani kama Petro anavyotukumbusha katika aya ya 5, “wokovu wa siku ya mwisho” tunaouhitaji na tunaoutarajia unategemea imani yetu. Usifanye kosa juu ya hili! Imani ni yetu kuitumia wakati wowote tunapoamua; hatufanyi chochote “kuistahili” - ni zawadi ya Mungu, hatutumii mtaji wowote – wa pesa wala nguvu zetu; imani haihitaji maendeleo makubwa ya akili zetu, lakini imani ni muhimu sana. Bila imani, hatuwezi kuwa Wakristo. Kwa kweli katika Biblia Wakristo ni “wale wanaoamini” (kwa mfano Warumi 3:22).

Uhakika wa Wokovu: Pale yule askari mkuu wa gereza wa Filipi alipoona matendo makuu ya Mungu na kutambua uhitaji wake wa kuokolewa nafsi yake, aliwauliza Paulo na Sila moja kwa moja, “Mabwana, nifanye nini ili nipate kuokoka?”. Na wao wakampa jibu la moja kwa moja: “Mwamini Bwana Yesu Kristo nawe utaokoka, pamoja na wa nyumbani mwako” (Matendo 16:30-31). Ni muhimu sana, tangu hapa mwanzoni mwa mjadala huu (ambao utazungumzia kwa undani ukinzani na mashambulizi mbalimbali dhidi ya imani yako na umuhimu wa kudumu katika imani hiyo) kukumbuka kwamba imani katika Kristo na wokovu inaouleta ni mambo rahisi sana – rahisi kwa maana ya kwamba wokovu ni rahisi sana kuupata (kwani Kristo alilipia gharama yake), na kwamba nia ya Mungu kwa waumini wote ni kwamba wadumu katika imani hii maisha yao yote ili kuupata wokovu ulio wao kwa kitendo kile cha mwanzo cha kumwamini Kristo. Hivyo hatuna sababu ya kuwa na mashaka na wokovu wetu. Tunahitaji tu kujiuliza sisi wenyewe kama [je,] tunamwamini Bwana Yesu Kristo, kama kweli sisi ni wafuasi wake halisi? Hiki ndicho Paulo anachomaanisha pale anapofundisha Wakristo “tujipime wenyewe, tuone kama tunaishi katika imani” (2Wakor. 13:5). Na asitokee Mkristo yeyote akafikiri kwamba inawezekana kuishi maisha ya Kikristo bila ya imani yetu kupitia changamoto, kupimwa, kujaribiwa, na wakati mwingine kwa [moto] mkali sana! Tukumbuke kwamba tumesoma katika maandiko kwamba mwandishi wa Waraka huu wakati fulani [wa changamoto na mtihani mkali kwake] alimkana Bwana wetu mara 3 kabla hajajirudi na kutubu kwa uchungu mwingi! Ulikuwa mtihani mgumu [sana], hata hivyo, baada ya kuanguka vile, alisimama wima, na aliendelea [kupevuka] hata kuwa mmoja kati ya waumini wakuu kabisa katika historia ya Kanisa! Imani yaweza kukomaa tu ikiwa itapimwa, na jambo hili Petro alilifahamu vyema sana (1Pet. 1:6-9).

Imani: Kuamini ni kutumaini. Tunaposema kwamba “tunaamini katika Bwana Yesu Kristo, ina maana kwamba tumeweka tumaini letu Kwake, na ushuhuda wa Baba juu Yake. Tunamwamini Mungu na tunaliamini Neno lake kwamba Kristo ndiye Masihi, Yeye aliyekuja duniani kutuokoa kutoka katika dhambi na hatia, ambaye kazi yake ilimalizika kwa ufanisi na Mungu Baba aliridhika, na kwamba kupitia kazi hiyo ya kufa msalabani kwa ajili yetu, sisi ambao vinginevyo tungekuwa tumepotea, bila matumaini yoyote, tunaokolewa kwa imani tuliyo nayo Kwake. Tunapokabiliana na yule adui wa kale, KIFO, na maadui wengine katika ujumla wa historia ya wanadamu, kila kitu tunachokiona kinatuonyesha kwamba hakuna tumaini, kwamba kifo cha mwili ndiyo mwisho wa kila kitu; ndipo hapo tunamwamini Mungu badala ya macho yetu, kwamba tunatembea kwa imani itokayo kwa Mungu, na siyo kwa macho yetu ambayo yanauona tu ulimwengu huu wa kiini-macho wa Shetani. Ni kwa macho ya imani tu ndiyo tunaweza kupenya uzio wa maisha haya ya duniani. Lakini katika imani, tunaamini kwamba Mungu ameshinda kifo, kwamba kwa kweli amelipia dhambi zetu kwa kumtoa sadaka Mwanaye wa pekee kwa ajili yetu, na kwa kweli alimnyanyua Mwanaye Yesu Kristo kutoka katika wafu na atafanya vivyo hivyo kwetu sisi ikiwa tu tutamwamini Yeye, Bwana Yesu Kristo, ikiwa tutamtumainia Yeye.

Imani ni suala endelevu, si suala la “mara-moja”. Ni kweli kwamba waumini wengi wanaikumbuka kwa furaha “ile saa walipoamini kwa mara ya kwanza”. Lakini kwa wengi kati yetu, imani imekuwa ikijengeka hatua kwa hatua, kidogo kidogo – kama mbegu ya mpanzi iotavyo – mpaka siku moja tukaanza kuuona ufahamu ndani yetu kwamba tunamwamini Mungu, tunamtegemea, kwamba pale ulimwengu unapoona hakuna tumaini, sisi tumeona uhalisia wa uzima wa milele – tukitumia macho ya imani. Kama tulipokea ahadi ya Mungu juu ya uzima wa milele katika Bwana Yesu Kristo siku fulani ambayo tunaikumbuka, au hatuna kumbukumbu ya lini au kivipi mwujiza huu [wa imani] umetokea, hata hivyo sisi sote TUNATUMAINIA Neno la Mungu, na TUMEWEKA imani yetu kwa Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya uzima wa milele baada ya kaburi na vivyo hivyo tumekuwa sehemu ya familia ya Mungu, tukistahamili maisha ya duniani kwa imani, tukitarajia maisha yajayo kwa imani.

Imani inataka kuamua na kuendelea na uamuzi huo. Kama vile Mkristo yeyote anavyoweza kushuhudia, kuweka imani yako katika Kristo si mwanzo wa maisha rahisi hapa duniani. Tunayo kauli yake Kristo mwenyewe, ikionyesha wazi kabisa juu ya maisha ya kujitoa yanayomkabili Mkristo tangu mwanzo kabisa ikituamrisha kubeba msalaba wetu na kumfuata Yeye (Matt. 16:24). Pia, kama vile mjenzi ni lazima afanye hesabu ya gharama kabla ya kuanza kujenga (Luka 14:28), vivyo hivyo kila mmoja wetu anapaswa kufahamu tangu mwanzo kwamba maisha ya kumfuata Bwana Yesu yatakuwa na magumu yake (1Pet. 4:12). Kama Wakristo, tunakabiliwa siyo tu na shida/mitihani na vishawishi vya dunia hii kama watu wengine, bali pia ukinzani kutoka kwa adui yetu Wakristo wote, Shetani, akisaidiwa na wafuasi wake (1Pet. 5:8). Fundisho-fumbo la mpanzi linaweka wazi kwamba si kila mmoja anayesikia habari njema ya Bwana Yesu Kristo ataingia katika ufalme wa mbinguni (Matt. 13:18-23). Fundisho-fumbo lile (ambalo tumejifunza kwa kiasi cha kutosha katika Pet. #12 - #13) linaorodhesha makundi 4 ya wale wanaosikia wito wa Kristo na kumfuata na namna ya mwitikio (response) wa kila mmoja wao: 1) baadhi hawaamini kabisa, japo wanalisikia Neno (mbegu inayoangukia kwenye udongo mgumu, kando ya njia); 2) baadhi wanalipokea Neno, lakini baadaye wanaliacha (mbegu inayoanguka kwenye mwamba, wenye udongo finyu); 3) baadhi wanavurugwa na matatizo na matamanio ya dunia hii (mbegu inayoanguka katika magugu na miiba); 4) ni kundi moja tu la watu ndilo linalosikia habari njema na kuipokea kwa namna inayostahili, ikidhihirishwa na kuzaa matunda kwa ajili ya Bwana (kumea, kukua na kuzaa matunda mara 100, mara 60 na mara 30). Pengine kundi #3 ndilo gumu kuliko yote katika kulielewa kutokana na muktadha tunaouzungumzia hapa. Mbegu inayoanguka katikati ya magugu na miiba inachipua “mmea wa imani”, lakini mmea huo unasongwa, na matokeo yake “matunda yake hayafikii kiwango cha kupevuka” kama Mathayo anavyoelezea. Kundi #4 ni la waumini ambao kwa uhakika wanaingia katika ufalme wa mbinguni, na tunaambiwa wazi kabisa kwamba kikundi #1 wanavurugwa na Shetani kabla hawajaamini, wakati kikundi #2 ni watu “wanaopigwa ngwala, wanababaishwa” katika mwendo wao wa imani, au kama Luka anavyosema (Lk. 8:13), “wanageuka” kutoka kwa Bwana (Neno linalotumika katika Kiyunani ni aphistemi ambalo lina mzizi ule ule kama neno “apostasy = uasi”). Kundi #3, hata hivyo, linatupa tatizo la [ku]tafsiri]. Tunachoambiwa katika masimulizi yote 3 ya fundisho-fumbo hili ni kwamba waumini wa kundi hili wanapotezwa njia na matatizo na starehe za dunia kiasi kwamba hawawezi kuzaa matunda. Kama tulivyoona katika somo #18, haiwezekani kwa muumini wa kweli kuishi maisha yake yote bila kuzaa tunda lolote (Yak. 2:26). Maelezo yanayotolewa katika fundisho-fumbo la mpanzi #3 linatufanya tusimame na kufikiri, kwani wazi kabisa, linaonyesha waumini wanaoshindwa kupevuka, na ambao wanazalisha kidogo sana au “zero” kwa ajili ya Bwana. Inawezekana kwamba waumini wa aina hii ni wale ambao hawafanikishi chochote kwa ajili ya Kristo katika maisha yao na ambao kazi zao zisizo na thamani zinaenda sambamba na zile kazi za waumini ambao matunda yao yatachomwa moto mbele ya kiti cha hukumu/tathmini cha Kristo (1Wakor. 3:12-15). Hata hivyo, kuna uwezekano kwamba watu wanaozungumziwa hapa ni waumini wa zamani ambao wameondoka katika msitari wa mpango wa Mungu kwa sababu ya tamaa zao wenyewe na shughuli za kidunia kiasi kwamba ule mmea wa imani uliochipua kwa sababu ya Neno unaishia kusinyaa. Katika hali zote 2, wale watu wa kikundi #3 ambao imani yao “inasongwa” wanaletwa kwetu kama kilelekezo cha tahadhari kwa waumini wote kuitunza, kwa bidii, imani yao. Uwezekano mkubwa hapa ni kwamba aina zote 2 – waumini hafifu na waumini walioasi – wanazungumziwa hapa. Kitu kimoja ni cha uhakika hapa bila kujali tunaitafsiri namna gani hii aya: si salama kabisa, na, ni hatari kwa afya yetu ya kiroho, kuwa katika kundi #3, “waumini walio katikati ya magugu na miiba”. Kama tulivyoona kabla na bila shaka kama tutakavyoona tena, njia pekee ya kuendelea kuelekea kwenye usalama wa kiroho ni kukua kiroho. Kukua katika Kristo ni lazima kujizatiti katika kumfuata Kristo.

Imani ni kuamini katika nafsi fulani au kitu fulani. Imani ina mlengwa, na sifa au stahiki zozote katika kitendo cha imani ni lazima ziwe katika mlengwa wa imani na siyo katika muumini. Tunamwamini Mungu, kwani anastahili tumaini letu Kwake. Amejidhihirisha kwetu katika Mwana wake na katika Neno lake na hivyo ametupatia Nafsi na kitu halisi cha kutuwezesha kuelekeza imani yetu. Ametupa amri ya kuamini, ametupa wakati, ametuwezesha, ametupa fursa na motisha ya kuamini, halafu ameleta mbele yetu Mlengwa mtukufu sana wa iamni yetu, Mwanaye, Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alikufa kwa ajili yetu, kwa ajili ya dhambi zetu, alikufa ili tuweze kuishi Naye milele. Imani haiwezi kuwapo kikwelikweli bila mlengwa wa imani hiyo. Bila Mungu, bila Neno, bila Bwana Yesu Kristo, [aliye] taswira halisi na kamili ya Mungu na mfano halisi wa Neno Lake (Waebr. 1:1-4), pasingekuwa na uwezekano wa imani. Kama imani hailekezwi kwa Mlengwa Huyu, basi hii si imani kabisa.

Imani ndiyo NJIA PEKEE tuliyo nayo. Ikiwa tunaendelea katika imani na tunaendelea kuweka tumaini letu kwa Mungu na mwanawe Bwana Yesu Kristo, basi tutaendelea kulindwa kwa nguvu za Mungu na imani tuliyo nayo Kwake hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa hapo mwisho wa majira kama aya ya 5 inavyosema. Hivyo, kwa gharama zozote, ni lazima “tuendelee kuamini”, kwa sababu matokeo ya kutoamini hayafai hata kuwazia kwani yanatisha mno.

Usalama [wa Wokovu Wetu] Milele: Ule ukweli wa maandiko kwamba sisi, kama waumini, tunalindwa na Mungu kupitia imani yetu ili tuweze “kuokolewa” kutoka katika hukumu na uharibifu ambao umepangiwa ulimwengu huu usioamini, mara nyingi katika duru za uinjilisti huitwa kanuni/fundisho la “dhamana ya uzima wa milele” wa Mkristo. Japokuwa hakuna dosari katika matumizi ya istilahi (terminology) yake, msemo huu, maneno haya, yanadokeza, na mara nyingi yanachukuliwa kumaanisha, kwamba baada ya mtu kutoa tamko la imani yake kwa Bwana Yesu Kristo, basi nafasi ya mtu huyu mbinguni ni salama kuanzia hapo, bila kujali chochote kitakachotokea. Kwa mujibu wa mtazamo huu, dhambi iliyo nzito, uhasama kwa Wakristo wengine na kwa imani, hata kumkataa Kristo moja kwa moja, kwa ufupi hakuna kitu chochote kinachoweza kututenganisha na upendo wa Mungu (War. 8:39). Kwa maneno mengine, “ukishaokolewa, wokovu wako hauna kikomo!”.

Tatizo la mtazamo huu usio na kadiri (extreme view) {ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba mtazamo huu unadharau/hautilii maanani aya kadhaa katika maandiko kama ambavyo tutaona hivi punde), ni kwamba hauhusishi hulka ya Mungu na haki ya Mungu. Mungu ni upendo (1Yoh. 4:8), na, ni kwa sababu aliupenda ulimwengu mzima hata akamtuma Mwanaye wa pekee, Bwana wetu Yesu Kristo, aje kufa kwa ajili ya kila mwanadamu (Yoh. 3:16). Hata hivyo si kila mmoja atakayeokolewa, kama ambavyo hata watetezi wa “usalama [wa wokovu wetu] wa milele” wanajua fika. Kama ambavyo amefanya kila kinachotakikana ili kuhakikisha kila mwanadamu anaokolewa, isipokuwa tu kuingilia uhuru wa kila mwanadamu wa kuachagua na kuamua (utashi), hali ni hiyo hiyo kwa waumini baada ya wokovu. Mungu anatupatia kila kitu tunachokihitaji ili tuendelee na imani, anatupatia mpaka uwepo wa Roho wake Mtakatifu ndani yetu, lakini kuendelea katika imani kunataka msimamo, ustahamilivu, na kila siku kumchagua Mungu dhidi ya dunia hii ya Shetani. Fundisho-fumbo la mpanzi (kwa mara nyingine tena) linaonyesha suala hili kwa uwazi kabisa. Wengi wanalisikia Neno; baadhi hawaliingizi kabisa ndani ya mioyo yao; baadhi wanaasi haraka sana mara tu wakisongwa; baadhi wanavurugwa pole pole na shida na tamaa za ulimwengu; ni waumini wale tu ambao imani yao inasitawi na kukua, na kuizidi kimo/nguvu miiba na magugu (misongo) ya maisha ya duniani na mwisho wake kuwa wanazaa matunda kwa ajili ya Mungu na, kwa kutumia maneno ya Petro, “wanathibitisha wito wao” (2Pet. 1:10). Hivyo basi, kwa kweli tuna uhakika na usalama katika wokovu wetu wa milele, lakini ikiwa tu tutaendelea kusimama kama waumini halisi, wa kweli, wa Bwana Yesu Kristo.

Ustahamilivu: Ustahamilivu maana yake ni kuendelea kuvumilia mpaka mwisho; katika muktadha wa Mkristo, ina maana kushikilia imani yako ukipita katika shida na raha, katika kila tatizo utakalokabiliana nalo, mpaka mwisho wa maisha yako ya hapa duniani. Ni kweli kwamba ustahamilivu si jambo rahisi. Kwa kweli, katika maandiko tunaona waumini wakipitia majaribu ya imani yao, mengine yakiwa magumu kwa kiasi kikubwa sana. Abrahamu aliambiwa amtoe sadaka mwanawe, Danieli katika tundu la simba, Yusufu alifungwa jela, na Yeremia katika shimo la tope, ni mifano ya hali ngumu zilizotaka imani kuu ili kuvumilia na kushinda, kwa upande wa waumini hawa. Katika magumu kama haya, Mkristo ni lazima ategemee kwa asilimia 100 kwenye haki ya Mungu na ili kupata nguvu iliyo muhimu kutuwezesha kuvumilia, kama ambavyo waumini hawa wakuu wa kale walivyofanya. Lakini ikiwa tutapangiwa kupitia kipindi kirefu cha mateso au kupitia mchakato mrefu wa kuokolewa (kama vile walivyopitia wana wa Israeli wakati wa kutoka Misri), au majaribu ya imani yetu yamepangwa kutoonekana na wale ambao hawako karibu nasi, tunaweza kuwa na uhakika na mambo mawili: 1) tukiwa hapa duniani, na katika maisha haya, imani yetu itajaribiwa; 2) Mungu ametupatia namna ya kukabiliana na chochote tutakachojaribiwa nacho (1Wakor. 10:13). Kizazi cha wana wa Israeli waliotoka Misri wakiongozwa na Musa kinatupatia somo muhimu kuhusu umuhimu wa uvumilivu. Kama Paulo anavyosema, “wote [wakabatizwa] wawe wa Musa … wote wakala chakula kile kile cha kiroho … hata hivyo Mungu hakufurahishwa na wengi wao, maana waliangamizwa jangwani” (1Wakor. 10:2-5). Watu wa kizazi kile walimwamini Mungu mwanzoni. Walichora ishara ya msalaba kwa damu katika milango yao na hivyo wakamuepuka malaika wa kifo (Kut. 12:13), na walivuka Bahari Nyekundu iliyotenganishwa na Mungu, “kwa imani” (Waebr. 11:29). Lakini licha ya imani yao ya mwanzoni, licha ya miujiza waliyoishuhudia na kushiriki katika utendaji wake, imani yao haikudumu. Walimweka Mungu (na Musa) katika majaribu wakati ule wakiwa safarini nyikani na matokeo yake Mungu akawaangamiza wengi kati yao (Yuda 5).

Yaliyowakuta wale wa kizazi cha kutoka Misri pia ni muhimu kwa mtazamo mwingine tofauti. Kizazi cha Wakristo watakaolazimika kupitia Dhiki Kuu ya nyakati za mwisho watakuwa na matukio mengi yanayofanana na hayo na watahitaji kutahadhari dhidi ya “kuzimia kwa imani yao” kama ilivyokuwa kwa wale wa kutoka Misri. Maneno ya Kristo katika Matt. 24:13 yanazungumzia wakati huo ujao, lakini pia yanafaa kuzingatiwa tunavyopitia katika dhiki za kila siku ambazo kila Mkristo anapitia kwa kiasi kikubwa ama kidogo. Katika aya ile, Bwana Yesu anatuasa kwamba “atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa”. Maana ya msingi hapa ni ile kama tulivyoijadili hapo juu. Yeye atakayedumu katika imani mpaka mwisho wa uhai wake ndiye atakayetoka katika maisha haya kama muumini, yaani ule mmea unaositawi katika udongo mzuri na unaoendelea kuzaa matunda mpaka mwisho.

Imani ni kazi ngumu. Katika 1Wathess. 1:3, Paulo anazungumzia “kazi ya imani” ya Wathessalonike, akizungumzia juhudi zao za kuendelea katika imani huku wakikabiliwa na majaribu na mateso ya maisha ambayo yalionekana [kama vile] kuwasibu wao zaidi ya watu wengine. Kama ilivyo kwa hawa waumini wa Thessalonike “walioteseka kwa mkono wa ndugu zao wenyewe” kwa sababu ya imani (1Wathess. 2:14), uvumilivu mara nyingi una gharama zake. Hata hivyo, ni kwa uvumilivu wa aina hiyo, yaani subira na ustahamilivu wa imani, ndivyo waumini wa wakati ule ujao wa kipindi cha Dhiki Kuu wataokolewa kutoka katika wakati huo mgumu kabisa wa majaribu na mateso (Matt. 24:13; Lk. 21:19). Ustahamilivu una taswira nyingi, lakini kama mwandishi wa waraka kwa Waebrania anavyoweka wazi, sote tunayo fursa “ya kurudi” kwenye nchi ya “kutoamini”, kule tulikotoka kabla ya kuweka imani yetu katika Kristo (Waebr. 11:15). Kwa kuimarisha imani yetu, kwa “kustahamili”, tunaendelea kujiwajibisha na ile ahadi tuliyoiweka pale tulipomfanya Kristo kuwa Mwokozi wetu – tunakuwa waaminifu Kwake.

Kwa upande mwingine, “kurudi” katika “nchi ya kutoamini” mara nyingi ni mchakato wa udanganyifu [wa Shetani]. Ni mara chache sana waumini wataonyeshwa njia ya wazi inayoelekea upande mbaya [wa zamani] unaopelekea kupoteza imani yao. Adui yetu Shetani ni mjanja sana na anajua kuuficha mkono wake wa udanganyifu. Mara nyingi, barabara yenye mteremko inayoelekea kwenye kutoamini inakuwa imefichika na ni vigumu kujitambua kwamba umo katika barabara hiyo. Mara nyingi, barabara hiyo ina mteremko wenye utelezi wa dhambi anazotenda yule anayeelekea kwenye kutoamini [hivyo ni rahisi kuipita!]. Kama itakavyokumbukwa kutoka katika masomo yetu yaliyopita, hakuna muumini anayeweza kuishi bila kutenda dhambi, kwani tunaishi katika miili ambayo ina hulka ya dhambi. Hata hivyo, kujisahau mara moja moja (na hata dhambi hizi ndogo-ndogo Mungu huziadhibu) na ambako kunafuatiwa na kukiri kosa, kutubu/kujirudi ni tofauti sana na kutenda dhambi nzito, inayorudiwa-rudiwa, isiyofanyiwa kitubio, ambayo mtendaji wake haikiri, na pengine anaihalalisha moyoni mwake. Mwenendo kama huu mwisho wake humtenga muumini na Mungu – siyo tu kwamba unamuudhi Mungu, ukiambatana na hatua za kinidhamu kutoka Kwake, lakini pia uhusiano wa muumini huyu na Mungu wake unaingia ukakasi, hivyo kuharakisha mchakato wa kupoteza imani. Hii ndiyo picha tunayoiona katika kizazi kile cha kutoka Misri [katika Agano la Kale], ambacho kiliamini mwanzoni, lakini baadaye wakaanza desturi ya kumshakia Mungu, kumlaumu Mungu, na kumsaliti Mungu (cf. Zab. 78). Mwenendo wao uliharibu uhusiano wao na Mungu kwa kupunguza imani yao kwa Mungu, kisha kuimaliza kabisa. Hiki ndicho mtume Yohana anachomaanisha pale anaposema kwamba japokuwa tunapaswa kuomba kwa ajili ya waumini wengine ambao tunajua wanajihusisha na dhambi, tusiingilie kati pale tunapoona kuwa mtu huyo ameasi imani yake katika Kristo na sasa anateseka kwa matokeo ya uasi huo (1Yohana 5:16).

Dhambi na imani havikai pamoja, havichanganyiki. Tunapotenda dhambi, ni kama vile tunamwambia Mungu kwamba hatuamini kwamba Yeye atalishughulikia tatizo lolote lile ambalo dhambi ile tunayotenda inalenga kulishughulikia. Kwa muumini aliye katika njia sahihi ya kukua kiroho, kujisahau huko kunapaswa kushughulikiwa mara moja kwa kuchukua hatua ya kutubu (kulitambua kosa na kulikataa mara moja) na kukiri (kukubali kwamba tumekosa, katika sala). Mwenendo wa kutenda dhambi kwa makusudi (kwa kukaidi) bila kujali, bila majuto, kwa kumkaidi Mungu kutaipunguza imani yetu na mwisho itaisha kama mchwa wanavyokula mbao taratibu mpaka inapotea. Kwa kifupi hiki ndicho ambacho mtume Paulo anachosema pale anapotuambia “mshahara wa dhambi ni mauti” (War. 2:23): siyo kwamba dhambi moja tutakayotenda itatutia hatiani, bali kwamba kifo cha imani yetu ni matokeo ya kujiingiza katika maisha ya dhambi, na kwamba bila ya imani katika Kristo, hatuna tena mbadala au wakili (yaani imani hiyo) itakayosimama kwa ajili yetu siku ya hukumu. Hivyo tukiacha imani yetu, hatuwezi kutegemea Mungu kuwa na “furaha na sisi tena” (Waebr. 10:37-39). Kama Yakobo anavyosema, dhambi, ikipelekwa katika ukamilifu wake (yaani ikiwa/ikifanywa ndiyo mwenendo wa maisha), inazaa kifo – [aina ya] kifo cha kiroho, yaani kifo cha imani yetu. Kwa sababu hiyo hiyo Paulo anatutahadharisha tusiwe na majivuno katika imani yetu kulingana na wasioamini, akituambia kwamba kama vile “matawi” yasiyoamini ya Israeli “yalikatwa” kwa sababu ya kukosa imani, vivyo hivyo nasi “tutakatwa” ikiwa hatutaendelea na imani (War. 11:20-26). Swali muhimu zaidi ya yote ni kama tutaendelea katika kweli tunayoijua au la. Ikiwa tutakuwa waaminifu kwa ile kweli ya injili, “ikiwa ile kweli tuliyoisikia inakaa ndani yetu” kama mtume Yohana anavyosema, ndiyo tunakuwa na uhakika wa wokovu wetu (1Yoh. 2:24).

Moyo Kuwa Mgumu: Mungu ameuumba moyo wa mwanadamu ili uweze kuipokea kweli. Ni haki yetu ya kuzaliwa kama wanadamu kuweza kulitambua Neno la Mungu tunapolisikia mara ya kwanza. Hata hivyo, kulikubali kwamba ni la kweli yaweza kuwa jambo jingine kabisa. Kwa hakika, kuukataa uhalisia na kujitenga na yale Mungu aliyotushuhudia, ni desturi ya sehemu kubwa na ya muda mrefu ya wanadamu. Japokuwa Mungu ameuweka ukweli kuhusu Yeye mwenyewe, kuhusu Uungu wake na hulka yake, wazi kabisa kwa wanadamu, wengi kati yao, hata hivyo, wanachagua kuupuuza na kutoamini ukweli huu (War. 1:19-20). Kukataa kile tunachokijua kuwa ni kweli ni, kwa mtazamo wa Biblia, kosa kubwa sana. Sababu ya hali hii ni kwamba haiwezekani kutenganisha kati ya kuukataa ukweli na kukubali kilicho cha uwongo (au, kinyume chake [upande wa pili] kuukubali ukweli na kukataa kilicho cha uwongo) – dhana hizi mbili hazitangamani (yaani kwa kimombo they are mutually exclusive) kwetu sisi wanadamu tulio katikati ya vita iliyoenea ulimwengu mzima kati ya Mungu na nguvu za giza/uovu. Hakuna hata mmoja kati yetu asiyeguswa na shinikizo au uchaguzi kati ya ukweli na uwongo. Ndiyo sababu mtume Paulo anawazungumzia wasioamini kwamba wanaposhindwa kumtukuza Mungu kama Mungu (japo wanajua ndani ya mioyo yao kuhusu Uungu Wake) fikra zao mara moja zinakuwa “za kijinga” na mioyo yao “inaingia giza” (War. 1:21). Katika Waefeso 4:18, Paulo anatupatia fununu zaidi kuhusu moyo kuingia giza, hali inayotokana na [mtu] muhusika kuukataa ukweli. Katika muktadha huu, anawasihi Waefeso wasienende kama wasioamini wanavyoenenda “katika ujinga usio na faida wa mioyo yao, uelewa wao ulioingia giza na waliotengwa na Mungu”. Chanzo cha hii hali ya kusikitisha kinaelezwa kuwa ni “ugumu wa mioyo yao”, kwani baada ya “kuingia ganzi, wamejiingiza katika mambo ya ufisadi, kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi”.

Farao aliyetawala Misri wakati wa kizazi cha Waisraeli wa Kutoka [Misri], ni mfano mzuri sana unaodhihirisha mchakato wa kuufanya moyo kuwa mgumu, akili kuingia ganzi kuhusiana na Mungu kunakotokana na kuukataa ukweli wake na kuukubali uwongo wa Shetani mahala pake. Kama vile Mungu alivyomtabiria Musa, katika kukabiliana na miujiza iliyotendwa na Mungu kupitia Musa na Haruni, na kwa majanga mengi yaliyowasibu Wamisri kwa sababu ya ujeuri wake, Farao “aliendelea kuufanya moyo wake kuwa mgumu” na kukataa ukweli ulio wazi, kwamba mwishowe atalazimika kuwaachia wana wa Israeli (Kutoka 4:21; 7:13; 8:15). Kufanya hivyo ni sawasawa na kuikataa nguvu ya Mungu, japokuwa walikuwa wanakabiliwa na uhalisia mkuu na usiopingika wa nguvu hiyo. Kiuhalisia, Mungu alimwacha/alimruhusu Farao aufanye moyo wake uwe mgumu kwa kiasi ambacho kilikuwa hakijatokea kabla. Farao aliachwa na Mungu aendelee na mwenendo wake hasi hata akavuka msitari wa busara na kuonekana kichaa. Japo inatia kihoro kuuona uthubutu wa kijinga wa Farao, je, hatupaswi kuingiwa na kihoro zaidi tunapomwona mtu yeyote leo hii akiikataa nguvu ya Mungu na mpango wake wa wokovu katika maisha yetu kupitia Bwana Yesu Kristo? Si jambo la kushangaza kwamba fursa ya kuokolewa inapatikana tu katika maisha ya hapa duniani pekee, kwa wanadamu. Ikiwa wasiookolewa watapata fursa ya kumwona Mungu uso kwa uso katika utukufu Wake na wakapewa uchaguzi wa kutubu au la, basi halitakuwa jaribio halali la utashi wao. Ni katika maisha ya hapa duniani tu ndipo moyo wa mwanadamu unaweza kuwa mgumu hata mwanadamu huyu kumkataa Mungu.

Uasi: Hata hivyo, tofauti na sababu na matokeo ya kitendo cha mtu asiyeamini cha kumkataa Mungu, somo letu linajihusisha na utunzaji (na pia uwezekano wa upotevu) wa wokovu tulio nao kupitia imani yetu katika Bwana Yesu Kristo. Kama tulivyoeleza hapo juu, sehemu ya mwisho katika sentensi iliyopita ndiyo yenye umuhimu mkuu (underlined): ikiwa mtu anamwamini Kristo, basi mtu huyu ameokolewa, na anaweza kutarajia na kutegemea kwa uhakika kabisa “wokovu utakaopatikana siku ya mwisho” unaotolewa kwa uwezo wa Mungu na imani yetu. Kinachohujumu, kinachoharibu na mwisho wake kinachoua imani ya mtu ni dhambi (kiuhalisia, ni matendo kadhaa ya dhambi) iliyokithiri (cf. inayorudiwa-rudiwa), isiyoungamwa, na isiyofanyiwa kitubio. Mwenendo usio wa Kikristo, unaoendelea bila wasiwasi, bila kutiliwa shaka, bila hisia za hatia au bila kufanyiwa toba, mwisho wake utaiharibu imani ya mtu. Tunavyozidi, kwa juhudi zetu wenyewe, kujitenganisha na Mungu, tunajiwekea mazingira magumu zaidi ya kutuwezesha kumrudia tena. Mwisho wake tunaacha kabisa kuja Kwake. Mwisho wake tunamkataa, tunamkana na tunakanusha ukweli wake. Haijalishi kwamba kabla halijatokea tunasisitiza kwamba haiwezekani sisi kumwacha Mungu – tukio/tendo hili linashuhudiwa na kutabiriwa katika Biblia. Na je, sisi wenyewe hatujawahi kuwajua watu ambao wakati fulani walimshuhudia Kristo, lakini baadaye, kwa sababu moja ama ingine (labda janga lisilotazamiwa/lililotokea ghafla ambalo mhusika alimlaumu Mungu kwalo) wakamgeuka kabisa, kwa jinsi tunavyoweza kutathmini maisha yake? Ni kama vile muumini anayerudi nyuma, anajitenga na Mungu katika fikra zake kiasi kwamba anafikia hali ambayo hawezi “kumtazama Mungu usoni” tena. Mwisho wake, dhamira yake inaharibika kabisa na uasi wake unakuwa umekamilika.

Uasi ni neno lililotafsiriwa kutoka katika neno la Kiingereza APOSTASY, ambalo nalo limetokana na neno la lugha ya Kiyunani apostasis. Tafsiri sisisi ya neno hili (literal translation) ni “kusimama mahala pengine/mbali na” na katika fasihi za Kiyunani neno hili limetumika kumaanisha uasi na uhaini. Hivyo uchaguzi wa neno hili uliofanywa na waandishi wa Biblia ni wa kufaa sana. Kwani kama vile ambavyo mtu anapaswa kuonekana kuwa amekana na kukataa na ameacha uaminifu wake kwa mamlaka yanayotawala mahala fulani ili aeleweke kwamba ameasi na amehaini [ni mwasi na mhaini], vivyo hivyo katika milki/ufalme wa kiroho, uasi unaashiria kukataa kabisa mamlaka ya Mungu na Yeye mwenyewe pia. Haina maana kwamba mhusika haamini tena kwamba Mungu yuko (kumbuka, hata pepo “wanaamini” hivyo – na kutetemeka: Yak. 2:19), lakini mtu huyu ameacha imani yake, uaminifu wake, utiifu wake, kwa Mungu.

Dhana hizi mbili, kupoteza imani na kuasi, zinajadiliwa kwa pamoja na mwandishi wa waraka kwa Waebrania, ambaye anawatahadharisha wasomaji wake “asiwepo mmoja kati yenu ambaye moyo wake ni mwovu na wenye kutoamini katika uasi wake dhidi ya Mungu aliye hai”. Paulo anawaelezea baadhi ya waumini walioasi zamani kwa kutumia lugha kali na ya dharau anapowalinganisha na jinsi yeye anavyoishi maisha sahihi ya Kikristo; wakati yeye, Paulo, na wengine kama yeye ni “mfano” wa kuigwa na Wafilipi, kuna wengine waliopotea njia, hadi kufikia mahala pa “kuwa maadui wa msalaba wa Kristo: mwisho wao ni uharibifu” (Wafi. 18-19). Hili si jambo la kushangaza, kwani, kama ilivyotokea mara nyingi katika historia ya Kanisa, mwelekeo wa uasi mara nyingi umetoka “juu”, kutoka kwa wale walio katika nafasi za madaraka (yaani “waalimu wa uwongo”). Katika “siku za mwisho” waumini wengi watavutwa kuelekea kwa waalimu hawa wa uwongo, na matokeo ya mwenendo huu kwa wale watakaovutwa nao, yatakuwa ni kufanana na waalimu wao, “wakichomwa moto dhamiri zao” (1Tim. 4:1-5; tizama pia 2Pet. 2:1-3). Uhusiano kati ya kuharibika kwa dhamiri na uasi dhidi ya Mungu usisahaulike hapa; kwani kama Paulo anavyosema, “hakuna kilicho safi kwao walio najisi, wasioamini; bali akili zao zimekuwa najisi, na nia zao pia” (Tito 1:15). Ikiwa tunaendelea kujituma katika kufuatilia kile tunachokijua kuwa ni sahihi katika maisha yetu na kukielekeza katika maisha hayo, basi tutakuwa salama katika maisha yetu ya kiroho, lakini hatuwezi kukumbatia njia za uovu bila kumharibu yule mlinzi wa mioyo yetu, yaani dhamiri zetu. Kwani hiyo ndiyo njia ambayo mwisho wake itatufikisha mahala ambapo maisha yasiyo na imani na matendo yasiyoongozwa na imani yanakuwa hali ya kawaida kwetu (cf. Waefe. 4:17-19).

Kupoteza Wokovu: Si wote ambao mwanzoni humkumbatia Bwana wetu wana majaliwa au wana kudura (destiny) ya kuendelea kuwa waaminifu Kwake. Haswa katika siku zijazo za mwisho, wengi ambao mwanzoni walikuwa na imani, kama ile mbegu inayoanguka katika udongo wenye mwamba (mawe), wataiacha imani ambayo hapo mwanzo waliipokea kwa furaha (Lk. 8:13). Tunapofikiria mapana na marefu ya janga la kumwasi Mungu moja kwa moja na matokeo yake, tunalazimika, pamoja na mwandishi wa waraka kwa Waebrania, kusema kwamba “kwa sababu hii, imetupasa kusikiliza kwa makini sana yale tuliyoambiwa, tusije tukatetereka na kusogea mbali na Mungu” (Waebr. 2:1). Ulimwengu unaothamini mali ambamo tunaishi, unatoa fursa nyingi kwa matamanio yanayoleta “kuanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika hatia na uharibifu” (1Tim. 6:9). Lakini kama tulivyoona, mwenendo wa kurudia-rudia matendo ya dhambi unatia sugu katika dhamiri zetu (dhamiri inapoteza makali) na kumtenga muumini na Mungu. Kutambua na kukiri dhambi kunaleta kusafishwa na kufanywa wapya, lakini kukataa kwa majivuno kuacha dhambi kunafanya hatua za kujirudi zisiwezekane. Kama mwandishi wa barua kwa Waebrania anavyosema, “haiwezekani kuwafanya upya [kuwarejesha kwenye kitubio] tena wale walioasi, kwa kuwa wanaendelea kumsulibisha Mwana wa Mungu na kumfedhehi kwa dhahiri” (yaani wanaendelea na uasi wa kiburi dhidi ya Mungu: Waebr. 6:4-6). Hivyo tatizo siyo dhambi pekee, bali kiburi kinachoendelea, kinachorudiwa-rudiwa mbele za Mungu hata kufikia mahala ambapo mhusika anaasi imani yake wazi wazi, na tunaingia katika kupoteza wokovu, na hukumu inayowakuta waasi kama hao iko wazi (1Wakor. 6:9-10; Waga. 5:19-21; Waefe. 5:3-7): ingekuwa heri kwao kama wasingemkumbatia Kristo hapo mwanzo (2Pet. 2:21).

Hivyo basi, msitari muhimu unaotenganisha kati ya mbinguni na jehanamu, kati ya wokovu na hatia, ni msimamo wa imani (au kutokuwa na imani) ndani ya moyo wa mhusika. Wayahudi wasioamini katika miaka ya uhai wa Paulo walikuwa, kama anavyotuambia mwenyewe, wametenganishwa na Mungu kwa kutoamini kwao; kwa hakika walikuwa wamekatika kutoka katika mti wa uzima kwa sababu ya kukosa kwao imani; lakini Paulo anawaasa watu wa mataifa kutahadhari, kwani watasimama kwa imani yao na wataendelea kusimama ikiwa tu imani yao itaendelea kuwa imara (War. 11:20-21). Kwa sababu hii, sisi tunaoamini tuna ulazima wa kutahadhari; tunapaswa kuogopa kujiamini kupita kiasi juu ya hali yetu – si kwa sababu inawezekana tumepoteza wokovu wetu (kwani kama tunaamini, basi tumeokolewa), bali kwa sababu kutokuwa na bidii katika imani yetu (yaani kuwa na ‘lackadaisical attitude’) kutapelekea tuingie katika hatari kama ilivyokuwa kwa wale wa kizazi cha kutoka Misri (1Wakor. 10:1-12). Mwisho wake hawakuingia katika nchi ya ahadi kwa sababu kutoamini kulichukua nafasi ya kuamini ndani ya mioyo yao licha ya maajabu na miujiza waliyoishuhudia (Waebr. 3:18-19). Kwa hiyo hatuwezi kutegemea hali nzuri ya ki-imani tuliyokuwa nayo hapo zamani; tunapaswa kuendelea kufuatilia uongofu na utakaso “kwani bila ya hivyo hakuna awezaye kumwona Mungu” (Waebr. 12:14). Kwani ikiwa tunaendelea kuamini, ikiwa Neno la Mungu linaendelea kuishi ndani ya mioyo yetu, basi nasi tutaendelea kuwa ndani Yake (1Yoh. 2:24).

Masharti Aliyotuwekea Mungu: Ni muhimu sana kukumbuka kwamba wokovu wetu hautegemeani na Mungu Mwenyewe binafsi. Mungu, ambaye aliupenda sana ulimwengu hata akamtuma Mwanaye wa pekee ili afe kwa ajili yetu (Yoh. 3:16), na ambaye anataka wanadamu wote waokolewe (1Tim. 2:4), si tatizo katika wokovu wetu huo: katika kumtoa sadaka mwanaye na kuunda mpango unaofaa ili kila mmoja wetu aweze kuokolewa, tayari amekwishafanya kila kitu kinachohitajika kwa wote kuweza kuokolewa. Hata hivyo, kuna masharti fulani yanayohusiana na uzima wetu wa milele, masharti yanayotawala mwenendo wetu hapa duniani katika kipindi kabla hatujaingia katika uzima wetu wa milele. Mtume Paulo anatufundisha kwamba tumejaliwa kupelekwa na kuonyeshwa kuwa hatuna lawama mbele Yake “kama mmefanywa imara na thabiti katika imani, pasipo kuliacha tumaini [lile] lililoahidiwa na Injili ile mliyoisikia” (Wakol. 1:23); na kwamba ni kwa kupitia imani katika hii habari njema ndiyo tunaokolewa “kama mkishikilia kwa uthabiti neno nililowafundisha ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili” (1Wakor. 15:2). Ili tubaki na tuendelee kubaki kuwa wa Kristo, tunapaswa kushika imara, kama ilivyokuwa mwanzo, imani yetu mpaka mwisho (Waebr. 3:6, 14). Lakini “kama tukimkana Yeye, Naye atatukana sisi” (2Tim. 2:11-13; cf. Matt. 10:33; Lk. 12:9).

Adhabu/Hatua ya Nidhamu ya Kutusahihisha: Mara tu waumini wanapoanza kuingia katika lindi la dhambi, Mungu huwapatia adhabu/nidhamu ya kuwasahihisha kwa malengo ya kuwaepusha na upotevu wa wokovu. Mwandishi wa barua kwa Waebrania anaelezea msingi wa adhabu/hatua hii ya kinidhamu (Waebr. 12:9). Kuhusiana na mwitikio wetu kwa adhabu/nidhamu kutoka kwa Mungu, anatukumbusha kwamba hatukubisha pale tulipopewa adhabu ya kuturekebisha mwenendo wetu kutoka kwa baba zetu wa hapa duniani, halafu anauliza: “Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi?” Hivyo, lengo la kupokea maadibisho ya haki kutoka kwa Mungu ni uzima wa milele. Bali mwisho wa kukataa na kubisha kwa kiburi, ni kifo.

Hii ndiyo sababu, kwa mfano, ya tamko la Paulo (ambalo kwa haraka haraka linaweza kuonekana kama ni kali kupita kiasi) juu ya muumini mmoja wa kanisa la Korintho ambaye alijihusisha katika dhambi kuu. Paulo anasema kwamba, kwa kutumia uwezo wake mahususi wa kitume, ameamua “kumkabidhi mtu huyu kwa Shetani, ili asili ya dhambi yake (yaani mwili wake) iangamizwe lakini roho yake iokolewe siku ya Bwana (1Wakor. 5:5). Kwa maneno mengine, Paulo alimwondoa mtu huyo kutoka katika ulinzi wa Mungu, ili kwamba adhabu atakayoipata [labda] itasababisha mabadiliko ya moyo wake ulioingiwa na uovu na hatimaye imani yake iweze kulindwa. Kwa maana hiyo hiyo, Paulo anasema katika waraka huo huo, kuhusiana na matumizi mabaya ya ibada ya komunyo, kwamba sisi waumini “tunatathminiwa na kuadibishwa na Bwana, ili kwamba tusije kutiwa hatiani pamoja na ulimwengu” (1Wakor. 11:32). Kwani “iko dhambi ya [inayopelekea kwenye] mauti” (1Yoh. 5:16-17).

Wito kwa Wenye Ufahamu: Somo letu limethibitisha maneno ya Paulo kwamba “mshahara wa dhambi ni mauti” (War. 6:23; cf. 6:16; 6:21), lakini pamoja na mwandishi wa Barua kwa Waebrania tunaweza kusema kwamba “ingawa tunasema hivi, ndugu zangu wapendwa, kwa upande wenu tuna uhakika wa mambo mema zaidi, mambo yale yahusuyo wokovu” (Waebr. 6:9). Ikiwa tunaendelea kujenga imani yetu, tumaini letu, upendo wetu kwa Mungu, tutakuwa kama Petro anavyotuelekeza kufanya, “kuweni na bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu, kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe” (1Pet. 1:10). Kwa namna hii, “ule wokovu siku ya mwisho” utakuwa wetu kwa uhakika, pamoja na taji la uongofu katika siku ya Bwana tukiwa pamoja na wote wanaokua kiroho katika Kristo Yesu.

=0=

Imetafsiriwa kutoka: Perseverance of Faith: Peter’s Epistles #21

=0=

Basi, na tuonane katika somo #22 la mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amen!