Uongozi wa Roho Mtakatifu: Nyaraka za Mtume Petro #16
Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

Mapitio ya Kukua Kiroho: Hapa tumechepuka kidogo katika somo letu la kukua kiroho. Somo hili limesababishwa na matakwa ya Petro kwa kila Mkristo kupata ongezeko la neema na amani kutoka kwa Mungu – 1Peter 1:2. Kama tulivyoona mara ya kwanza tuliposoma aya hii, kukua kiroho ndiyo namna pekee, njia pekee, ya kufikia kutimiza kiu hii (ya ongezeko la neema na amani) katika maisha yetu. Kuuona uwezo wa neema na upendo wa Mungu katika maisha yetu, na ile furaha inaojaza mioyo yetu pale tunapoelekeza nia na akili yetu yote Kwake, kunataka kukua kwa yule mtu wa ndani yetu kunakoongezeka kila siku (Waefe. 3:16). Kukua kiroho ni sharti, na pia ni njia, ya kupata ongezeko la baraka za Mungu ambazo Petro anazizungumzia.

Lakini tusizifikirie baraka hizi kwa maana ya neema za kimwili [pekee]. Hii haina maana kwamba Mungu hawapi waumini wake neema za kimwili (wakumbuke kwa dakika moja tu Abrahamu, Yosefu/Yusufu, Ayubu – ambao walikuwa matajiri sana!). Hata hivyo, ni kweli kwamba Agano Jipya linatupa tahadhadhari juu ya magumu na mateso yanayoambatana na maendeleo ya kiroho (1Petro 4:12-19). Hivyo basi, ni vyema kuzifikiria baraka zinazotokana na kukua kiroho katika mtazamo wa kiroho. Hizi ni aina za baraka zinazotokana na kukua kiroho na ambazo zinavuka mipaka ya faida za kimwili (mali) hapa duniani (Mathayo 6:19-21):

• Kuijua furaha ya kweli ya kumweka Kristo katikati ya maisha yetu (Wafi. 3:8-11).
• Kutimiza uwezekano wa kuzaa matunda (utumishi katika Kanisa Lake) ambao kwa ajili yake tumeitwa (Math. 13:23; Luka 8:15).
• Kungojea kwa hamu pongezi kutoka kwa Mungu kwa kazi nzuri tunayofanya (Math. 25:21).

Misingi ya kukua kiroho: Tulipoanza kuzungumzia kukua kiroho, tulitumia muda mrefu tukizungumzia/tukijadili fundisho-fumbo la mpanzi wa mbegu (Mathayo 13; Marko 4; Luka 8). Mmea unaochipua kutokana na mbegu ya Neno la Mungu unamaanisha sisi, imani yetu na maisha ya kiroho. Wale wanaoota mizizi (ambao ndani ya mioyo yao kunachipua na kusitawi imani inayookoa ya Yesu Kristo) wanapitia awamu mbili za magumu kabla ya kuanza “kuzaa matunda” au kutumikia katika mpango wa Mungu:

1) wanapaswa kupenyeza mizizi yao kiasi cha kutosha ndani/chini ya udongo ili kuiwezesha kunyonya maji ya kutosha kuhimili joto kali la jua (wanapaswa kujilisha na kutunza moyoni, kwa imani, kweli ya Mungu au “chakula cha kiroho” ili kujenga imani yao kwa kiasi cha kutosha kuhimili nyakati za mitihani zinazokuja kwa waumini wote wa Bwana Yesu Kristo).

2) wanapaswa kukua na kupandisha matawi yao juu zaidi ya “magugu” ambayo vinginevyo yanaweza kusonga kukua kwao na kuwazuia kuzaa matunda (wanapaswa kutoitelekeza imani yao wakati wa mitihani, lakini pia wanapaswa kuyatumia mafundisho wanayojifunza katika maisha yao, wakiyashusha matamanio yao ya kidunia na kuyapandisha matumaini yao ya uzima wa milele mbinguni na kustahamili katika utumishi aliowapangia Mungu licha ya misongo ya maisha).

Kushinda mitihani ya maisha ya Kikristo kunahitaji “risasi na baruti” za kutosha za Ki-Biblia, zilizopangwa katika kanuni za kweli ya Mungu na kuhifadhiwa ndani ya mioyo kwa imani. Kuhimili dhoruba ya kila wakati ya maisha, hata hivyo, kunalazimu zaidi ya uwepo wa misingi unayoweza kuitumia wakati wa msongo; kunataka mtazamo mpya kabisa wa maisha, namna/njia/mfumo mpya kabisa wa kufikiri. Tutauita mtazamo huu mpya “fikra adilifu”.

Utangulizi wa Kufikiri kwa Uadilifu: Tunapozaliwa upya na kuwa Wakristo, kunatokea mabadiliko makuu ndani yetu (2Wakor. 5:7). Japo tunaendelea kuishi katika himaya ya Ibilisi [hapa duniani] katika maisha yetu yote [yaliyobaki] ya kidunia, kiuhalisia tunakuwa tumeondolewa kutoka ufalme wa giza na kuingizwa katika ufalme wa Mungu (Wakol. 1:13). Hadhi yetu imebadilika kabisa, na sasa namna yetu ya kufikiri ina ulazima wa kubadilika pia. Makuzi yetu ya kiroho yanategemea sisi wenyewe kuichukua hadhi yetu ya kuwa “kiumbe kipya” na “kujifanya sisi wenyewe kuwa wapya kwa kufikiri kiroho – badala ya kimwili” (Waefe. 4:23; cf. Zab. 16:8 na Zaburi zote kwa ujumla).

Kuendeleza mawazo ya kiroho au kufikiri kwa uadilifu ni sehemu muhimu ya mchakato wa “utakaso katika maisha” (rejea Petro #13 kwa somo kamili la utakaso). Kama tulivyoona, “utakaso katika Kristo” na “utakaso milele” hufanyika mara moja na kufanikishwa na Mungu, na hauhitaji juhudi yoyote kwa upande wetu. Hata hivyo, kujaribu kutimiza agizo la kuwa watakatifu kama Mungu alivyo mtakatifu (1Petro 1:16), kunahusisha zaidi ya kujizuia na mwenendo mbaya. Kunahitaji pia maendeleo chanya katika mpango wa Mungu kwa sisi wenyewe kufuatilia kwa bidii lengo la kukua kiroho. “Nilipokuwa mtoto”, anasema Mtume Paulo, “nilisema kama mtoto, niliwaza kama mtoto, nilifikiri kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima, niliacha mambo ya kitoto (1Wakor. 13:11).” Kama vile tunavyopaswa kuwa na mtazamo uliopevuka pale tukiwa watu wazima katika shughuli zetu za kidunia, hivyo hivyo baada ya kuwa waumini tunapaswa kubadilisha mfumo wetu wa kufikiri ili tufikie kupevuka kiroho.

Hulka ya Mwanadamu: Wanadamu wote wana hulka iliyogawanyika katika sehemu mbili; maana yake, sisi sote tumeumbwa tukiwa na mwili na roho (Waebr. 12:9):

Bwana Mungu akamuumba mtu (mwili wa Adamu) kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi inayotia uhai (roho yake), naye mtu akawa kuimbe hai (Mwa. 2:7).

Yule mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa na sehemu inayoonekana, inayoshikika – mwili, ambayo Mungu aliiumba kutokana na udongo, na pia alikuwa na sehemu isiyoonekana (hapa inaitwa “pumzi ya uhai”), ambayo Bwana Mungu aliiweka katika mwili huo. Matokeo yake, mtu akawa kiumbe hai. [NOTE: Katika NIV Bible, neno lililotafsiriwa kama “being” linatokana na Kiebrania “nephesh” (ambalo mara nyingi hutafsiriwa kama neno “soul” ambalo nalo ni sawa na Kiyunani “psyche”)]. Matokeo ya uumbaji wa Mungu, yule mtu wa kwanza akawa kamili, nafsi hai. Ni pale Adamu alipopokea ile sehemu isiyoonekana, inayotia uhai, inayoendana na mwili wake unaoonekana, ndipo akawa kamili. Kama Adamu, sisi, kwa sasa na kupitia ufufuo, tutakuwa mwili na roho, milele. Lakini katika miili hii tuliyo nayo sasa ya uharibifu, mawazo yetu yanavutwa kuendana zaidi na ulimwengu unaotuzunguka kuliko upande wetu wa pili wa kiroho – War. 7:18.

Moyo: Mawazo ya wanadamu ni matokeo ya kile Biblia mara nyingi inakiita “moyo” (yaani yule mtu wa ndani, anayehusisha mawazo yetu yote, hisia zetu zote, n.k.). Kutokana na mfumo wa saikolojia wa Biblia, moyoni ndipo mahala ambapo mwili na roho vinakutana/vinaunganishwa, mahala ambapo ni tofauti kabisa na sehemu iliko hulka yetu ya kiroho (1Wakor. 2:12; 14:14). Mithali 23:7 inasema “jinsi mtu awazavyo moyoni mwake, ndivyo alivyo kiuhalisia”. Hivyo kwa mtazamo wa Biblia, mwanadamu alivyo moyoni mwake, ndivyo haswa yeye alivyo. Ni hapa, moyoni mwetu, Biblia inatufundisha, ndipo mahala ambapo hisia zetu zipo, ndipo uwanjani ambapo vita muhimu za kiroho zinapiganwa. Moyoni mwetu ndipo tunapomwonyesha heshima Mungu, na ndipo pia panapotokea “mawazo maovu”, mauaji, uzinzi, uasherati, wizi, udanganyifu, na kashfa – Mathayo 15:18-19.

Hivyo basi, mawazo/fikra “asilia” zilizotawala akili zetu kabla hatujaokolewa zilishawishiwa kwa asilimia kubwa na tamaa, hamu/kiu, hofu, na hisia nyingine zinazozalishwa na asili yetu ya dhambi – 1Wakor. 2:14. Baada ya kuwa waumini, sisi sio tena “wanadamu asilia” (yaani tunaoelekeza macho yetu katika sehemu yetu ya asili ya kimwili), bali tunakuwa “wa kiroho” (yaani tunaelekea kwenye sehemu yetu ya asili ya kiroho – 1Wakor. 2:15). Hata hivyo, katika hali yetu ya kuamini, bado tunashambuliwa na zile hisia zenye nguvu kutoka ule upande wetu “wa asilia” uliotupoteza njia wakati ule tulipokuwa hatujaokolewa. Ili tujiweke huru kutoka zile njia tulizopita kabla ya kuokolewa, na kubadilisha maisha yetu yaingie kwenye mwenendo chanya wa kukua kiroho na kutoa huduma kwa Mungu, inataka mabadiliko katika namna tunavyofikiri pia:

Wala msiifuatishe namna ya dunia hii, bali mbadilike kwa kutiwa nguvu katika mafikiri yenu, ili muweze kuyajua mapenzi ya Mungu, yaani yaliyo mema, yanyopendeza machoni Pake na yenye ukamilifu. Warumi 12:2

Mabadiliko ya maisha yanayotajwa hapa ni ya kiroho, yaani kuondoka katika hali ya zamani na kuingia katika hali mpya. Hii inaweza kufanikishwa kwa mwenendo mpya wa kufikiri kwa uadilifu ambao unatilia mkazo upande wetu wa kiroho na unasimama tofauti na mwenendo wa kufukiri kimwili tu wa dunia hii unaotuzunguka. Hivyo tunapaswa kufikiri katika namna tofauti na ilivyokuwa zamani; lakini hii ina maana gani?

Kubadilisha mtazamo wetu wa fikra: Kama waumini, tunayo namna ya uhakika ya kufanikisha jukumu tulilopewa na Mungu la kubadilisha mtazamo wa mawazo yetu. Tizama baadhi ya nyenzo tulizopewa na Mungu za kufanikisha jambo hili:

• Tunaye Roho Mtakatifu ambaye anatusaidia kuzielewa kanuni za kiroho ambazo zinalishia ukuaji wetu wa kiroho (1Wakor. 2:10-16), na kwa kweli ndiye anayetia nguvu matendo yetu yote ya Kikristo (1Wakor. 12:3).
• Tunayo haki ya kumsogelea Mungu katika sala na/au maombi, na pia kushirikiana Naye (Waefe. 3:18).
• Tunao waalimu na wachungaji wanaotusaidia kuelewa misingi ya kweli (Waefe. 4:11-16; 2Peter 1:13).
• Na tunayo Biblia, Neno la Mungu, ili iwe chanzo chetu cha kila siku cha mafundisho na tafakuri (Zab. 1:1-3).

Fikra Adilifu Wakati Wote: Hata hivyo, ili kuwa na matokeo mazuri, na kufanikisha lengo la kila Mkristo la kukua kiroho, ni lazima tuwe na mtazamo wa kiroho wakati wote, siyo tu wakati ule tunapokuwa na Mungu katika sala/utumishi. Ni lazima kufikiri kiroho na kufanya maamuzi ya kiroho kila wakati wa maisha yetu. Tuna wito wa kuwa watakatifu katika maisha yetu ya kila siku kama vile tulivyo watakatifu katika hadhi yetu kama waumini wa Bwana Yesu Kristo. Kufanikisha hili si kazi rahisi, na kama vile lile somo refu juu ya dhambi tunazotenda na jinsi tunavyorudi kwa njia ya kuungama linavyofundisha (tazama Nyaraka za Petro #15), changamoto hii haiwezi kutatuliwa kwa kujizuia kutenda dhambi tu. Lengo hilo (la kutotenda dhambi 100%) haliwezekani kufikiwa, na hata kama ingewezekana, Mungu anataka tufanye mengi zaidi ya kuzuia dhambi tu.

Kwa Wayahudi wa Agano la Kale, Mungu aliwapa maelekezo marefu na ya kina yaliyoelezea kipengele kimoja baada ya kingine kuhusiana na lengo la “utakaso” ambayo kwa ujumla wake yanajulikana kama “Sheria ya Musa”. Pamoja na mambo mengine, maelekezo haya yalihusisha masharti kamili na kanuni mahususi na kali za vyakula ambazo, japo nyingi kati yazo hazikuhusiana na mambo ya kiroho haswa, lakini zilikuwa na lengo la kudhihirisha “upekee” wa taifa la Israeli kwa majirani waliowazunguka (Walawi 20:24-26). Hata hivyo, tunajua kutokana na fundisho mahiri la Mtume Paulo juu ya somo hili kwamba haiwezekani kutimiza masharti ya Sheria katika ukamili wake, na kwamba maana na lengo la ndani kabisa la Sheria ni kwamba ilikuwa ni nyenzo ya uinjilisti, kwani iliweka wazi kwa wote waliokuwa wanyofu na wakweli ndani ya nafsi zao kwamba utimilifu kwa juhudi za kibinadamu ni jambo lisilowezekana, hivyo “kupitia Sheria mtu anapata ufahamu wa dhambi” War. 3:19-20). Kama Wakristo na washirika waliopokea zawadi kuu ya Roho Mtakatifu, kitu kinachotarajiwa kutoka kwetu ni kikuu zaidi ya kiwango kisichowezekana cha “kutimiza Sheria ya Musa”. Kwani kwa kweli, wakati mengi kati ya yale yaliyokatazwa/yaliyozuiliwa na Sheria ya Musa bado yanaendelea kuwa si halali kwa Wakristo, kwa ujumla hatuhusiki na orodha ile ya amri hasi. Hatupo tena chini ya mamlaka ya Sheria, bali tuko chini ya mamlaka ya neema (War. 6:14-15), na chini ya Sheria kuu zaidi tuliyopewa na Bwana Yesu Kristo, yaani sheria ya UPENDO (Mathayo 22:37-40; 1Wakor. 9:21; Wagal. 5:22-23; 6:2; Yakobo 2:8). Uhuru wetu unapaswa kutumika si kwa lengo la kuifurahisha na kuridhisha matakwa ya miili yetu kwa matendo ya dhambi, bali ni kwa utiifu ambao lengo lake ni uongofu (War. 6:16-18). Tunapaswa kusimama imara katika uhuru huu tuliozawadiwa na Mungu wetu, na siyo tena kutumikishwa na Sheria ambayo ilitumika kutuonyesha hali yetu ya dhambi (Wagal. 5:1).

Kimatendo, hii ina maana kwamba ili sisi kama Wakristo tuweze kutimiza kudura au majaliwa ya imani yetu ya kukua kiroho na kumtumikia Mungu kwa vipaji vyovyote alivyotupatia, hatuwezi kuelekeza macho yetu kwenye amri hasi pekee za kanuni za Biblia, bali tuweke kipaumbele zaidi kwenye maagizo chanya. Kila wakati wa kila siku tuna wito wa kutumia kweli ya Mungu katika maisha yetu kwa usahihi, kuenenda kama Wakristo wanavyotakiwa, kuyafanya yale ambayo Bwana anataka tuyafanye. Katika kujaribu kutimiza wajibu wetu, kiuhalisia tunakabiliwa na idadi kubwa sana ya mazingira ambayo hakuna kitabu – hata kama kitakuwa ni kikubwa namna gani – kinachoweza kuorodhesha maelekezo ya fanya-hiki/usifanye-kile kwa kila hali inayotukabili. Hii ndiyo maana orodha ya amri hasi (yaani usi-), japo ni muhimu, lakini haitoshelezi. Hii ndiyo sababu pia kupevuka kiroho kunadai mabadiliko ya namna tunavyofikiri. Kwa hakika kuna misingi chanya inayofundishwa katika Biblia ambayo tunapaswa kuizingatia kwa ushupavu kama tunavyoizingatia ile misingi hasi. Kwa mfano:

• tunapaswa kufanya kazi kwa ajili ya kipato chetu (2Wathes. 3:10)
• tunapaswa kuhudumia familia zetu (1Tim. 5:8)
• tunapaswa kuwa raia wema (War. 13:1-8)

Hata hivyo, kanuni njema kabisa katika kuitumia kweli ya Biblia maishani mwetu ni kuweza kuitumia kweli hii ya Biblia katika mazingira yanayobadilika bila kuipotosha kweli hii, bila ya kuhatarisha uhai wako wa kiroho. Hii haina maana ya kwamba uitie matatani (uitumie vibaya) misingi ya kweli ya Biblia, bali inamaanisha kwamba ni muhimu kutambua kuwa Mungu ametupatia kitengo muhimu cha kweli chenye malengo ya kuyakabili maisha yetu ya kila siku katika njia ya Kikristo, yaani maadili ya Kikristo.

Kama tukipanga upya mwenendo wetu wa fikra kulingana na maadili Mungu anayotufundisha na kutuamuru kuyakumbatia, tutakuwa kweli kweli “tumebadilika kwa kutiwa nguvu mpya katika mafikiri yetu” - War. 12:2, na tutaona kwamba tunaelekea katika “kuzifanya upya nafsi zetu kwa njia ya kufikiri kiroho” - Waefe. 4:23. Kama Paulo anavyotufundisha katika Wagalatia sura ya 5, mchakato wa kuacha mwenendo wa kufikiri unaohusiana na maisha yetu ya zamani, na kuchukua mwenendo mpya, wa Kikristo, mwenendo wa fikra ambao unaoana na unatiwa nguvu na Roho Mtakatifu.

Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili muwe huru, hivyo msiitumie miili yenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi katika upendo – Wagalatia 5:13.

Hadhi yetu kama Wakristo ni ile ya watu wa Mungu walio huru, lakini uhuru huu sio leseni ya kufanya mambo kama watu wasiohusiana na nafsi yeyote, wanaofanya wanalotaka, liwe jema au baya. Uhuru wetu unakuja na [ma]jukumu, siyo tu [ma]jukumu [ya]/la kuacha dhambi, bali la kuwasaidia Wakristo wenzetu jinsi tunavyozidi kukua kiroho. Paulo anatumia mfano wa fikra kuu ya kwanza adilifu ya Kikristo, ile ya upendo, kama kielelezo muhimu cha kwamba Wakristo wanatakiwa kutilia mkazo mienendo chanya (fikra adilifu) zaidi ya amri hasi, kama vile usiue, usiibe, nk. Kama vile Mungu alivyotupenda na alivyomtuma Bwana Yesu aje kufa kwa ajili yetu, na kama Bwana wetu Yesu Kristo anavyotupenda, tunapaswa kuiga upendo wake, kuakisi upendo huu, na kutumia fursa ya maisha yetu hapa duniani kuwasaidia Wakristo wengine, siyo kujifurahisha sisi wenyewe:

Kwa maana Sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako” - Wagal. 5:13.

Paulo anaanza, kama sisi tutakavyofanya, na ule msingi mkuu wa uadilifu wa Mkristo: upendo. Uadilifu huu [chanya] wa upendo, kama utatimizwa kikamilifu na kwa usahihi, unakamilisha kusudi lote la Sheria ya Musa. Kama tunaweza kuuelewa upendo katika taswira zake nyingi, changamano na za ajabu sana*; na kama tukiweza kuzifanya fikra zetu ziukumbatie upendo katika taswira zake hizo wakati wote, basi maadili yote mengine tunayofundishwa katika maandiko yatajipanga katika msitari bila juhudi yoyote kwa upande wetu. Kama tunajali zaidi wokovu na maendeleo ya kiroho ya wengine kuliko tunavyojali hali yetu wenyewe na kama tukienenda kwa msimamo huu, tutakuwa tunatimiza Sheria ya Musa katika upendo tunaouonyesha.

“Fikra adilifu” inauchukua msingi huu na kuutumia katika maadili yote mengine yanayofundishwa katika Biblia, kwani, kwa mtazamo huu, hayo maadili yote mengine ni taswira tofauti tu za upendo ambazo zimewekwa kwa ajili ya mazingira maalumu – yaani kila kanuni moja adilifu lengo lake ni kumfanya Mkristo atende jambo fulani katika mazingira fulani. Yakieleweka na kutumika kwa usahihi, maadili yanakuwa viini/vitovu vya fikra zetu na yanatusaidia kukabiliana na mazingira mbali mbali ya maisha yetu kwa mtazamo chanya kwa jinsi yanavyozidi kushika nafasi kubwa katika fikra zetu. Kwa ujumla, kama wakati wote tunafanya yaliyo sahihi, hatutakuwa na sababu ya kuhofia kufanya yasiyo sahihi.

Ili tuweze kutenda yaliyo sahihi, tunahitaji kwanza kuwa na msimamo sahihi, mtazamo sahihi, namna sahihi, adilifu, ya kufikiri. Fikra adilifu ni njia ya kutimiza ile amri: “mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe”. Sasa, “upendo” ni dhana pana sana, kama tulivyoona hapo juu*, kwa kweli upendo unahusisha kila kitu. Lakini ili kuutumia Ukristo katika misingi yake, katika mazingira changamano ya dunia hii, tunapaswa kuchambua mambo kwa undani zaidi, na kutafakari maadili kadhaa yanayofundishwa katika maandiko, na pia mbinu zinazotumika katika kuyatekeleza maadili hayo.

Kama mkiumana na kutafunana kwa ulafi, chukueni tahadhari msije mkaangamizana. Kwa hiyo nasema enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili – Wagal. 5:15-16.

Inaonyesha Wagalatia wale walikuwa wameunda makundi ndani ya kanisa au kusanyiko lao, yaliyokuwa yanashindana kwa uhasama mkubwa kati yao. Badala ya kusaidiana, walikuwa wanafanya kila mbinu kupata kundi ambalo litakuwa ndilo “mshindi”. Paulo aliwadhihirishia kwa hoja kwamba mwisho wa mwenendo huu ni uharibifu wa kanisa/kusanyiko zima. Baada ya hapo akaendelea kwa kuwafundisha mwelekeo ulio sahihi katika kuishi Kikristo. Kama tukirekebisha namna yetu ya kufikiri na kuioanisha na namna ya kuenenda kwa uongozi wa Roho Mtakatifu na kuisikiliza sauti Yake ndani yetu inavyotuhimiza na kutuelekeza kupitia Neno tunalojifunza kila siku, tutagundua kuwa hatufuati tamaa za ile asili/hulka yetu ya dhambi na mwelekeo wake wa kidunia.

Roho Mtakatifu anatusaidia kufikiria na kutenda yaliyo sahihi ikiwa tutakuwa tayari “kushirikiana Naye”. Tukifuata yaliyo mema, basi kwa uhakika tutazuia yale mabaya. “Mipaka ya barabara” inayotusaidia tupite ndani ya njia sahihi ya Kikristo ni maadili kama vile imani, matumaini na upendo. Tunahitaji kuelewa zaidi kuhusu maadili haya na zaidi ya haya, na kujifunza kuelekeza mawazo yetu yapite katika njia hizi njema. Na tunavyofanya hivyo, Roho Mtakatifu anatusaidia katika mchakato huo, na pia anatusaidia katika kutenda yale mema yanayotokana na kufikiria fikra njema:

Kwani tamaa ya mwili inapinga Roho, na Roho inapinga [tamaa ya] mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yote mnayotaka. Wagal. 5:17.

Msukumo asilia wa miili tuliyo nayo kwa sasa ni dhambi katika uelekeo wake. Kama Wakristo, hata hivyo, tumepokea ahadi/dhamana ya Roho Mtakatifu. Kama Msaidizi wetu, anapinga ule msukumo wa dhambi ulio ndani yetu (Yoh. 14:16; 16:7). Hata hivyo, uamuzi wa njia gani tunaifuata ni wa kwetu sisi wenyewe. Tunaweza kujiona kama vile sisi ndio tunaendesha mambo, lakini, kama Paulo anavyotuambia hapo, sisi ni wafuasi wa hao viongozi wetu wawili – tamaa za mwili kwa upande mmoja, na Roho Mtakatifu kwa upande mwingine. Chocote kitakachotokea, tutachagua uongozi aidha wa Roho au wa mwili katika kila hali tunayokutana nayo. Tatizo la kiutendaji tunalokabiliana nalo kama Wakristo ni kwamba hii vita kati ya hawa wawili inafanyika/inaendelea ndani yetu, uwanja wa vita ni mioyo yetu, mahala ambapo roho zetu na miili yetu inapounganishwa, na vita hii haipiganwi kwa maneno na haionekani kwa macho.

Nia njema pekee haitoshi katika kupambanua kati ya hawa waongozaji wawili. Roho Mtakatifu anafanya kazi kwa kuitumia ile kweli tuliyo nayo ndani ya mioyo yetu. Tunavyozidi kuelewa na kuamini mafundisho ya Biblia, ndivyo anavyoweza kuwa na mafanikio zaidi katika kutuongoza. Haswa, uelewa wetu wa maadili ya Kikristo unavyozidi kuwa kamili na maadili hayo yanavyozidi kuwa ndiyo kitovu cha maisha yetu, ndivyo msaada tunaoupata kutoka kwa Roho Mtakatifu unakuwa na mafanikio zaidi katika kupambana na uwezo wa mwili wa kutawala maisha yetu na tabia yetu, nasi tunaongeza uwezo wetu wa kuisikia na kuitii sauti tulivu ya Roho Mtakatifu:

Lakini kama mkiongozwa na Roho Mtakatifu, hamko chini ya Sheria – Wagal. 5:18

Na pale tutakapokuwa tumepata ufahamu, imani na mazoea ya kufuata mwenendo mwema wa fikra na matendo yanayoongozwa na Roho Mtakatifu, basi vizuizi vya Sheria havitumiki tena. Kwani Sheria ni takatifu na inatoka kwa Mungu, na hivyo tendo lolote ambalo ni la upendo, lisilo la kibinafsi na ambalo ni safi, lisilo na doa, haliwezi kwenda kinyume na Sheria. Kwa njia ya fikra adilifu tunatoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kutawala namna tunavyofikiri, na hivyo tunaacha kufuata mwenendo wa kimwili:

Basi matendo ya mwili ni dhahiri, nayo ni haya: uasherati, matendo ya aibu, ufisadi, kuabudu miungu wa uwongo, kujihusisha na pepo, uadui/visasi, ugomvi, wivu, hasira, fitina, kuchochea mifarakano, uzushi, husuda, ulevi, ubinafsi, ulafi na mengine [mengi] yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyowaonya mwanzo, kwamba watu watendao maovu kama hayo, na kuyafanya kuwa ni mwenendo wa maisha yao, hawata urithi ufalme wa Mungu – Wagal. 5:19-21.

Ukichunguza kidogo orodha hii ya Paulo, utaona kuwa nyingi kati ya dhambi hizi ni za mwenendo, tabia katika asili yake (tofautisha hili na mwenendo “mtakatifu” wa maadili mema). Zaidi ya hapo, ni muhimu kuona kuwa orodha hii haimaliziki – kwa makusudi kabisa. Paulo anasema “na mengine yanayofanana na hayo”, ili kutuonyesha kwa uwazi kabisa kwamba japokuwa hajataja udhaifu mahususi wa kila msomaji wake, watu wote hutenda dhambi, matendo yote ya kutomtii Mungu yanatokana na “kufuata tamaa za mwili” na kutochukua fursa ya kutumia msaada wa Roho Mtakatifu.

Aya ya mwisho ya nukuu ya hapo juu (Wagal. 5:19-21), inahitaji maoni kidogo. “Watu watendao mambo kama hayo, na kuyafanya kuwa ni mwenendo wa maisha yao” hawatakuwemo katika ufalme wa Mungu. Tumejifunza tatizo la dhambi kwa kina kidogo, na tumeona kwamba hayuko miongoni mwetu aliye mtimilifu, asiye na dhambi na kwamba hili haliwezekani kwa sisi wanadamu. Aya hii inatukumbusha kwamba “mshahara wa dhambi ni mauti” (Warumi 6:23): wale wanaofanya desturi ya kutenda dhambi wataanguka kutoka kwa Mungu na watausaliti utii wao kwa Bwana Yesu Kristo (War. 11:22). Lakini kwa kumfuata Roho Mtakatifu wakati wote anavyoifanyia kazi ile kweli iliyomo mioyoni mwetu, tunahakikishiwa kuepuka mtego huo:

Lakini matunda ya Roho ni upendo, furaha, amani, utulivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi. Katika mambo kama haya, hakuna Sheria. Wagal. 5:22-23.

Aya hizi zinaonyesha moja kati ya orodha nyingi za maadili tunayotakiwa kuyafuata zilizomo katika Biblia. Orodha hii haina maana kwamba imetaja maadili yote, bali ina lengo la kutimiza kusudi la muktadha (context) ambalo ni kutofautisha tabia/mwenendo adilifu na tabia/mwenendo mbaya uliotajwa mwanzoni/kabla. Katika makundi haya mawili, Paulo anatupatia taswira tofauti za mwenendo wa kimwili na ule wa kiroho ambazo ziko wazi kabisa. Tunapozisoma orodha hizi, zinaonekana kukusanywa katika kikundi cha sifa za uovu au ubaya kwa upande mmoja na kikundi cha sifa za kiroho/njema kwa upande mwingine. Mtazamo huu siyo kwamba haukukusudiwa, kwani uovu wote na maadili yote yaliyotajwa hapo juu yanatoka kwenye moja kati ya “vyanzo vya uwezo” viwili ambavyo vinatia nguvu na motisha katika maisha yetu: Roho Mtakatifu kwa mema, na asili yetu ya dhambi kwa mabaya.

Kufikiri kwa maadili kunaanza na kanuni za kiujumla (generalities) na kuelekea kwenye kanuni mahususi (specific). Kutenda dhambi hakuhitaji juhudi yoyote kwa upande wetu; dhambi hufanyika kwa urahisi sana kwani ndiyo asili ya miili tuliyomo. Kuishi kama Wakristo wanavyotakiwa kuishi, kwa upande mwingine, kunahitaji juhudi zaidi (sana). Kama waumini, tunayo, katika nafsi ya Roho Mtakatifu anayekaa ndani yetu, “akili ya Kristo” - 1Wakor. 2:15-16. Lakini ushawishi wa Roho Mtakatifu juu ya mioyo yetu unategemea, siyo tu utashi wa mioyo yetu, bali pia uelewa wetu wa kweli ya Mungu. Uelewa wetu (elimu + imani) wa misingi ya maadili ya Kikristo ndio mtaji wa kiroho ambao Roho Mtakatifu anautumia kutengeneza faida ya kiroho kwa ajili yetu; uelewa wa ile kweli, na, katika muktadha (context) huu, uelewa wa misingi ya maadili, ndio unaoongeza juhudi zetu changa tunapotembea katika ulimwengu huu wa Ibilisi.

Mwanga mng’aavu unaomulika kutoka Wagalatia 5:22-23 unapaswa pia kutizamwa kutokana na maelekezo yaliyomo katika aya hizo ili yaeleweke na kufanyiwa tafakari katika akili zetu:

Wote walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili [wao] pamoja na tamaa zake. Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi na tuenende kwa Roho - Wagalatia 5:24-25

Kwa kumwamini Bwana Yesu Kristo, tumeukataa uongozi wa dhambi katika maisha yetu na badala yake tumeukumbatia uongozi wa Bwana Yesu Kristo. Kwa njia ya Roho Mtakatifu tumebatizwa katika Yesu Kristo, tumekuwa mwili mmoja na Yeye, na pia ni Roho wake Mtakatifu ambaye ndiye Msaidizi wetu hapa duniani. Roho huyo huyo aliyetuongoza katika maisha mapya na Bwana Yesu Kristo sasa anatuongoza katika njia ya kukua na kuendelea kiroho. Kukua kiroho, “kupanda juu zaidi” ya magugu yanayotusonga katika maisha yetu, na kuzaa matunda mema tukingali katikati ya himaya ya Shetani kunataka mtazamo-tendaji (active approach) katika maisha ambao unaanza na kinachoendelea katika “uwanja wa maisha” wa mioyo yetu. Ukitiwa nguvu na Roho Mtakatifu, na wakati wote ukapashwa habari na kuelimishwa na kweli ya Neno la Mungu, mtazamo huu tendaji, ambao tumeuita “fikra adilifu”, tutauzungumzia kwa undani zaidi katika somo lijalo.

=0=

Translated from: The Leadership of the Holy Spirit: Peter’s Epistles #16

=0=

Basi, tuonane katika sehemu #17 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!