Kuungama Dhambi: Nyaraka za Mtume Petro #15

Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa: https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii ya Kiswahili Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission For This Kiswahili Translation Has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

Mapitio ya Kukua Kiroho: Kama tyulivyoona katika masomo yaliyopita ya mpangilio wa kukua kiroho kwa muumini, mchakato wa kukua kiroho unafanyika kwa awamu, ambapo ili tupate mafanikio makubwa kabisa tunapaswa:

• Kulitafuta Neno la Mungu (awamu ya kulisikiliza)

• Kuweka imani yetu katika kweli ya Neno hilo (awamu ya kuliamini)

• Kuishi maisha yetu kwa kulitumia Neno hilo (awamu ya kuli-ishi Neno)

• Kutumia vipaji vyetu kuwasaidia wengine wafanye hivyo hivyo (awamu ya utumishi au huduma)

Mpaka hapa katika masomo haya, tumejadili kusikiliza, ambayo ni awamu ya kwanza katika mchakato huu ambapo tunaanza kukua kiroho kwa kuitafuta kweli ya Biblia, na kuiamini, hatua ya pili ambayo inatilia mkazo kuingiza ndani ya mioyo yetu kwa imani ile misingi ya kweli tuliyoipokea.

Sasa umefika wakati wa kuchambua hatua za tatu na nne katika mchakato wa kukua kiroho, “kuli-ishi Neno” na “kusaidia wengine”. Kama tulivyojifunza ndivyo tunapaswa kutumia mafundisho hayo katika maisha yetu, na kama tulivyofaidika kutokana na neema za Mungu katika utafiti wetu wa kukua kiroho, vivyo hivyo tunapaswa kuwapa wenzetu mkono wa msaada katika njia wanamopita ya kufikia malengo hayo hayo. Kweli tuliyoipokea isikae bure ndani ya mioyo yetu. Kinyume chake, tutiwe nguvu, tutiwe motisha, na kweli hiyo. Tuichukue habari tuliyojifunza na kuiamini, na tuitumie kuunda upya maisha yetu, fikra zetu, sisi wenyewe, na kwa kuitumia kweli hiyo hiyo tuwasaidie wengine wafikie kiwango hicho hicho.

Kuzingatia Neno, Ambalo Ndilo Chanzo cha Uhai wetu wa Kiroho: Awali ya yote, kuishi maisha mema ya Kikristo na kumtumikia Mungu katika namna anayotaka Yeye kunahitaji tuendelee katika mpango aliouweka wa “kukua katika ufahamu wa Neno” (Wakolosai 1:10). Ama kwa hakika, Neno la Mungu ndilo chakula chetu cha kiroho, na kuacha “kula” chakula hiki kuna matokeo yale yale kama ya kuacha chakula cha kimwili yanavyokuwa nayo kwa miili yetu (1Pet. 2:2; cf. 1Wakor. 3:2; Waebr. 5:12-14).

Kuishi kwa Kulitumia Neno/Kuli-ishi Neno: Kulisikia Neno tu haitoshi. Tunapaswa kujua kwamba tumelisikia Neno ili liwe na faida kwetu. Na kama tumeliamini Neno hili la Mungu kikwelikweli, je, linaweza kuwa na matokeo ya nguvu katika tunalowaza, katika tunalofanya, katika jinsi tunavyoishi maisha yetu? Bwana Yesu alisema, “anayesikia mafundisho yangu na kuyatenda, atakuwa kama mtu yule mwenye busara ambaye amejenga nyumba yake juu ya mwamba – Mathayo 7:24, na pia ni katika maana hiyo hiyo Yakobo aliandika, “muwe watendaji wa Neno, wala msiwe wasikilizaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu” - Yak. 1:22. Aya zote hizi mbili zinaonyesha kwamba Mkristo anatoka kwenye kusikia na anaenda kwenye kulitenda Neno la Mungu (kuli-ishi), ikichukuliwa kwamba ikiwa mtu anaamini ukweli wa Neno la Mungu, na imani hiyo ni halisi, basi baada ya imani yatafuata matendo, yaani muumini kui-ishi imani yake. “Dini iliyo safi, isiyo na uchafu”, kama Yakobo anavyosema, inamlazimu Mkristo aishi maisha yake kutokana na imani yake – Yakobo 1:27.

Afya ya Kiroho: Kama vile kula chakula bora kunapaswa kuenda sambamba na mazoezi ya mwili ili mtu awe na afya bora, vivyo hivyo kulisikia Neno la Mungu na kudai kwamba tunaliamini, haitoshi. Tunatakiwa tulitumie Neno tunalojifunza, katika maisha yetu ya kila siku ili tuwe katika “afya njema ya kiroho”. Kama Paulo anavyosema katika 1Timothy 4:7-8, “jizoeze kuwa mtauwa (mtakatifu)”. Bila ya kuendeleza tabia ya kuipa mazoezi imani yetu kulingana na misingi tunayoiamini, haiwezekani kukamilisha utakatifu tunaoutafuta, na kuna hatari ya kudhoofika kiroho na kuhatarisha afya yetu ya kiroho.

Mashindano ya Mbio: Katika 1Wakor. 9:24-27, Paulo analinganisha zoezi la kila siku la imani yetu katika maisha yetu na kufanya mashindano ya riadha (cf. Matendo 20:24; Wagalatia 2:2; Wafilipi 3:12-16; Wakolosai 2:18; Timoteo 2:5; 4:7-8; Waebrania 12:1; 12:12-13; 2Yoh. 1:9). “Kimbia kwa lengo la kushinda!”, anatuhimiza. Tutake, tusitake, sote tumo katika mashindano yanayohusu maisha yetu kama Wakristo hapa duniani, na ili “tushinde mashindano haya”, tunapaswa kujipa “mazoezi ya nidhamu ya nafsi katika kila kitu” kama wanariadha wa kale (na wa sasa) wanavyofanya ili kupata taji la ushindi – aya ya 25 ya 1Wakor. 9.

Maana rahisi ya jambo hili ni kwamba kuna mambo fulani ambayo tunapaswa kuyafanya na kuna mambo mengine ambayo tunapaswa kujizuia kuyafanya wakati wote ili kupata ushindi katika maisha ambayo Mungu ametupangia kuishi. Kama ilivyo katika mashindano ya aina nyingi ya riadha, vivyo hivyo katika maisha ya Kikristo tunapaswa kuwa na mfumo mzuri wa “kujilinda” na pia “kushambulia” (defence and offence) ili kushinda [katika mashindano hayo]. Hivyo kabla hatujaenda kwenye uchambuzi wa mambo yote mazuri yaliyo muhimu katika kukua kiroho, tunapaswa kwanza kutazama tatizo la dhambi tunazotenda na namna ya kupambana na tatizo hilo.
Tatizo la Dhambi: Mwanzo kabisa, tunapaswa kukubali kwamba hata mchakato halisi na nia halisi ya mabadiliko ya mioyo yetu haiwezi kuleta matokeo ya “utimilifu wa kutokuwa na dhambi”. Wakati Bwana wetu Yesu Kristo aliyakabili majaribu yote ya maisha yake bila kutenda kosa lolote (Waebr. 4:15), sisi wengine wote hatuwezi kufikia kiwango hicho (War. 3:23). Hii ni kwa sababu miili yetu ina uharibifu, au “inakaliwa” na dhambi (War. 7:20; Mwa. 6:5; 8:21). Hivyo tusifanye kosa la “kuifasili upya” dhambi kwa faida yetu, kwani dhambi siyo tu kile kitendo kinachotuchukiza sisi binafsi, bali ni kila kitu ambacho Mungu amekikataza. Hatuwezi sisi wenyewe tu tukaongeza tunavyotaka katika orodha ya yale tuliyokatazwa kuyafanya na Mungu, au kupunguza katika orodha hiyo. Kwa Mungu, dhambi zote ni kosa dhidi Yake, kwani dhambi ni kutokumtii Yeye. Adamu na Eva walifukuzwa kutoka katika paradiso [ya Edeni] kwa kula tunda lililokatazwa, tendo ambalo unaweza kuliona kwamba siyo baya ki-vile [ukilichukulia kama lilivyo], lakini lilifanyika wazi wazi kabisa katika namna ya KUPINGA amri na mamlaka ya Mungu (Mwanzo 2:16-17). Matendo yaliyokatazwa na Mungu, hata kama yanaonekana siyo mabaya sana kwetu sisi, ni dhambi kama vile matendo yanyotushtua, kututisha na kutuudhi sisi binafsi.

[Udanganyifu wa] Kuamini Kwamba Tunaweza Kufikia Utimilifu [wa Kutotenda Dhambi]: Japokuwa tumepewa dhima/jukumu la “kuweni watakatifu, kama Mimi nilivyo mtakatifu” (na hiki ndicho kiwango tunachotakiwa kufanya juhudi za kukielekea: 1Pet. 1:15-16), na japokuwa tunatarajiwa kuongeza kiwango chetu cha kukua kiroho (na hili ni lengo tunalotakiwa kujituma kulielekea: Waebr. 5:11-14), kufikia utimilifu wa kuwa na hali ya kutotenda dhambi ni jambo tusiloweza kufanikisha katika hii miili yetu ya uharibifu na tukingali katika hii dunia iliyoharibika. “Kutotenda dhambi kabisa” baada ya kumwamini Bwana Yesu, kama wanavyofundisha waalimu fulani, ni kanuni au fundisho la uwongo na la hatari sana, kwa sababu linampa mtu shinikizo la kisaikolojia ambalo mwanadamu hawezi kuhimili. Uhalisia wa dhambi, na ukweli kwamba tutatenda dhambi, mara nyingi hupelekea wafuasi wa mafundisho ya namna hii kukataa uwepo wa tabaka za aina fulani za dhambi au kusema kwamba wao hawatendi aina fulani za dhambi (ambazo kwa kweli wanazitenda). Lakini kwa kweli uwepo wa dhambi ni mpana sana na umeenea katika sehemu kubwa ya maisha yetu hadi kuingia katika motisha na/au nia za mioyo yetu na matendo ya viungo vyetu (Yer. 17:9; Wagal. 5:19-21; Waefe. 4:29-31;Wafi. 2:3-8). Hata tukijiwekea viwango vya juu namna gani vya utimilifu ili kuonyesha uongofu tulio nao, tutashindwa tu (cf. War. 9:31; 10:3). Amri kumi za Mungu ambazo zimenyumbulisha kwa wazi kabisa matakwa ya Mungu kuhusu mwenendo wetu, zinamalizia kwa kusema kwamba tamaa za kutaka kumiliki mali na wenza wasio wetu ni dhambi kama zilivyo dhambi za ibada ya/za sanamu au kuua (“usitamani”: Kutoka 20:17; cf. War. 7:7-12). Na kwa kweli, Paulo anatufundisha kwamba lengo la Mungu katika kutoa Sheria ya Musa ni kuwathibitishia watu wote na kuwadhihirishia kwamba bila shaka yoyote sisi sote ni wenye dhambi na hivyo tunahitaji ufumbuzi wa tatizo letu hilo la dhambi, Bwana Yesu Kristo (War. 3:9-20; Wagalatia 3:19-25). Wengi katika wafuasi wa “kidini” wa wakati ule walitaka “kudhihirisha uongofu” wao kwa kutumia Sheria ya Musa, lakini katika kufanya hivyo walifanikiwa kujihukumu wenyewe tu (Warumi 3:20). Uongofu halisi ni ule tunaopewa na Mungu pale tunapomwamini Mwana Wake (War. 4:5). Kama wafuasi wa Bwana Yesu Kristo katika ulimwengu unaotupinga unaotawaliwa na Ibilisi, hatupaswi kujidanganya kuhusu dhambi zetu, makosa yetu, hitilafu zetu. Tunapaswa kuyatambua mapungufu yetu na kuitumia rehema tuliyopewa na Mungu katika kupambana na chanzo chake.

Kutakaswa na Kuachana na Dhambi: Kama Wakristo, dhambi zetu “zimeoshwa” na tumekuwa wasafi, maana yake tumesamehewa na kutangazwa kuwa watakatifu kwa kazi ya Bwana Yesu Kristo pale tulipoikubali na kuipokea kazi ile kwa imani (Waefe. 2:5-9). Hata hivyo, licha ya kuwa sisi ni wasafi na tuliotakaswa “katika Kristo” - 1Wakor. 6:11, bado inawezekana kwa miguu yetu kushika uchafu tunapotembea katika ulimwengu huu wa Shetani. Mungu ametupatia hadhi ya kuwa “watakatifu”, lakini tungali na mapungufu na bado tunaweza kutenda dhambi. Hivyo tunapaswa kujihadhari kwa sababu bado tunatembea juu ya uso wa dunia hii, na hivyo tutaendelea kutenda dhambi, na tunatakiwa kuwa tayari kukiri wakati wowote tunapojihusisha na “ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi” - Waebr. 12:1. Hili ndilo jambo Bwana Yesu alikuwa analiweka wazi pale alipokuwa anaosha miguu wa wafuasi wake kabla ya kula nao chakula cha jioni kwa mara ya mwisho – Yoh. 13:1-17. Petro hakupendezwa na tendo la Bwana wake kumwosha miguu yeye pamoja na wafuasi wengine. Lakini Bwana Yesu alipomwambia kwamba bila kuoshwa miguu yake “Petro hana sehemu Naye”, Petro akadai basi [kama ni hivyo] Bwana Yesu amwoshe mwili mzima pia, Bwana Yesu akamjibu, “mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake ni safi” (aya ya 10). Bwana wetu alikuwa anafundisha kwamba tendo la kuokolewa kutoka katika utumwa wa dhambi ambao umewasibu wanadamu wote tangu Adamu hutokea mara moja tu, na kwamba tukio hili la ukombozi linatokana na kifo chake mahala/badala yetu na sisi tunajitwalia wokovu huu kwa imani yetu kwake Yeye (Wakol. 2:13-14). Huku ndio “kuoga” au kusafishwa dhambi zetu ambako kumekwishafanikishwa na hakuna haja ya kurudiwa tena. Hata hivyo, sisi huendelea kutenda dhambi tukingali Wakristo, na pale inapotokea tumetenda dhambi, basi tutahitaji “kuoshwa miguu”, yaani kusamehewa na kurudishwa katika utakaso mara tunapokiri dhambi zetu kwa Mungu. Tunakoshwa dhambi zetu mara moja tu. Lakini tunasafishwa dhambi zetu kila mara tunapokiri baada ya [ma]tendo [ya]la dhambi.

Mafundisho ya Msingi ya Mtume Yohana Juu ya Dhambi: Kwa sababu zote zilizotajwa hapo juu, dhambi tunazotenda sisi ni suala zito, linalosumbua sana. Akiliandikia kusanyiko la waumini ambalo japo liliundwa na makabila aina tofauti na waliotoka maeneo tofauti, waliofaidika na mafundisho ya moja kwa moja kutoka kwa mitume wa Bwana Yesu mwenyewe kwa miaka mingi, hata hivyo Mtume Yohana aliona umuhimu wa kurudia kwa kirefu mafundisho kuhusu dhambi katika barua inayojulikana kama Waraka wa Kwanza wa Mtume Yohana. Katika sura ya kwanza, aya ya tano mpaka ya kumi, Yohana anazungumzia kanuni/mafundisho juu ya dhambi katika muhtasari muhimu sana:

Aya ya 5: Huu ndio ujumbe tuliousikia kutoka Kwake na tunawatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani Yake hamna giza lolote!

Aya hii unauelezea msingi kwa msisitizo kabisa, kwamba Mungu hahusiki kabisa na dhambi. Yeye si mwanzilishi wa dhambi na hahusiki nayo kabisa. Hafanyi tendo la kupuuza dhambi hata kidogo. Dhambi ni kitu cha kigeni, kitu kinachoenda kinyume na Mungu, hivyo kama tunataka kuwa katika familia ya Mungu, dhambi haina nafasi katika maisha yetu.

Aya ya 6: Kama tukisema kwamba twashirikiana Naye huku tukienenda gizani, twasema uwongo, wala hatutendi lilo kweli.

Kwa kuwa Mungu anapingana kabisa kabisa na dhambi, tunapaswa kuchagua kama tunataka kumfuata Yeye ama tunataka kuishi katika dhambi. Hatuwezi, kwa wakati mmoja kufuata njia yenye giza ya dhambi, na wakati huo huo kuwa na ushirikiano na Mungu. Kama tukidai kuwa tuna ushirikiano na Mungu na wakati huo huo tunaishi chini ya wingu la giza, tunajidanganya wenyewe na tunamfanya Mungu kuwa ni mwongo, kwani anatuambia kwamba Yeye hakubaliani na kilicho dhambi. Bila ya nguvu na maajabu ya neema za Mungu, aya hizi mbili zinatisha kwa mtu yeyote anayejitazama na kujichunguza kwa moyo wa kweli/mkweli. Maneno ya wanafunzi wa Bwana Yesu yanakuja akilini: “Nani basi ataokoka?” - Mathayo 19:25.

Aya ya 7: Lakini tukienenda katika nuru, kama Yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Bwana Yesu Kristo, Mwana wake, yatusafisha sisi na dhambi zote.

Tazama vizuri pale Mtume Yohana anavyotuambia dhambi zote. Kwani kwa wale wanaochagua kwenda kinyume na Mungu katika maisha haya, hakutakuwa na kuikimbia dhambi na hivyo hakutakuwa na ushirikiano na watu watakatifu wa Mungu. Lakini kwa wale wanaochagua kutembea katika mwanga na kumfuata Kristo, Mungu amewapatia namna/njia ya kusafishwa kutokana na kila taswira ya dhambi: kazi ya Mwana wake Yesu Kristo msalabani (hapa inaelezwa kama Damu Yake, cf. Mathayo, na pia katika aya nyingi za maandiko). Kwa sababu ya kile alichokifanya Bwana Yesu kwa kufa badala yetu, Baba ana uhalali/haki ya kuikubali kazi yake kwa niaba yetu, akitusamehe dhambi zetu, na akituchukulia kuwa ni wasafi licha ya hulka ya dhambi tuliyo nayo katika hii miili ya hapa duniani tuliyo nayo, na licha ya dhambi tunazoendelea kutenda. Katika analojia/mfananisho unaotolewa, badala ya kuiona dhambi inayotuchafua, Mungu Baba anaiona “damu ya Kristo” ambayo “tumenyunyizwa nayo” (cf. Waebr. 10:22). Anaridhika kwamba adhabu ya kifo kwa ajili ya dhambi zetu imelipiwa kwa niaba yetu. Anatuchukulia kwamba hatuna hatia kwa sababu ya uhusiano wetu na Mwana wake Yesu Kristo badala ya kutuhukumu kulingana na kuchafuliwa kwetu na dhambi. Tazama kwa makini, lakini, katika aya ya 7, na uone kwamba Wakristo wanaoenenda katika maisha ya Kikristo kwa usahihi (wanaotembea katika mwanga) bado wanahitaji kusafishwa kutokana na dhambi kama sehemu ya kutembea mwendo wa Kikristo.

Aya ya 8: Kama tunasema kwamba hatuna dhambi, tuajidanganya sisi wenyewe, wala kweli haimo ndani yetu.

Aya ya 8 ni tahadhari muhimu kwa waumini waliofundishwa na kujiona kuwa hawana dhambi (kwamba hawawezi kutenda dhambi). Kama tunapoyatazama maisha yetu hatuoni kuwa tumetenda dhambi yoyote hivi karibuni, uwezekano mkubwa ni kwamba hatuna uelewa wa wazi wa jinsi hulka ya dhambi ilivyo na uwanda mpana wa dhambi na uwezo wake wa kuenea katika taswira nyingi za maisha yetu. Biblia iko wazi katika hili. Japo sisi ni waumini, bado hutenda dhambi. Ni kweli, kwamba tumeamrishwa kutotenda dhambi. Ni kweli, kwamba kujizuia kutenda dhambi ni muhimu ili kukua kiroho na pia kwa usalama wa roho zetu. Lakini ni kweli pia kwamba kwa sababu tunaendelea kuishi katika miili hii isiyo timilifu na tunaishi katika himaya ya Shetani, tunapaswa kuendelea na vita dhidi ya matendo ya dhambi, hata kujizuia “hadi kiasi cha kumwaga damu” (Waebr. 12:4). Aya ya 8 ya 1Yoh. 1, imeandikwa si kwa lengo la kutukatisha tamaa katika kupambana na dhambi, wala kutuhamasisha kutenda dhambi, bali kutupa tahadhari dhidi ya ukweli usioepukika wa hali yetu, na kutuamsha ili tuone umuhimu wa kupambana na matendo ya dhambi katika njia iliyo sahihi, njia ya Kibiblia, yaani kuungama [kukiri na kutubu].

Aya ya 9: Kama tukiungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na mwenye haki, atatusamehe dhambi zetu kutoka kwenye udhalimu wote.

Aya ya 9 inamaanisha kwamba msamaha wa Mungu juu ya dhambi zetu unatokana na uaminifu Wake (Yeye havunji ahadi yake) na uongofu Wake (malipo yaliyofanywa na Kristo kwa niaba yetu); tunapoungama dhambi zetu katika sala kwa Mungu Baba, yeye anatusamehe na anaturejesha katika ushirikiano kamili pamoja Naye na Mwanaye.

Aya ya 10: Kama tukisema, “sijatenda dhambi!” tunamfanya Yeye kuwa ni mwongo na Neno lake halimo ndani yetu.

Kuungama dhambi ni sehemu muhimu ya maisha ya Mkristo ya kila siku. Ukichanganya kujichunguza na kuungama kila wakati, uelewa wa Kibiblia wa matendo ya dhambi utatufunulia matendo mengi tunayotenda yanayomchukiza Mungu, ambayo yanapaswa kuungamwa. Madai ya “kutotenda dhambi” ni ya makosa, na ni hatari sana kwa maendeleo ya kiroho – 1Wakor. 11:28-32.

Kuungama/Kukiri Dhambi: Kama waumini, tunakuwa “safi” kutokana na dhambi ikiwa tunatizamwa katika uhusiano wetu na Bwana Yesu Kristo. Kwa sababu ya “mahala tulipo” au kwa maneno mengine, kwa sababu ya “nafasi yetu katika Yesu Kristo”, Mungu Baba anatuhesabu kuwa “tumeoshwa” kabisa na dhambi zetu za zamani, za sasa, na za baadaye. Tunakuwa “wasafi ndani yetu”, unaweza kusema kwamba katika maisha yetu ya kila siku, mara nyingi “tunachafuka nje”. Hatuachi kuwa Wakristo kwa sababu tumefanya kosa – bado tunaendelea “kumshikilia Kristo” na hivyo Mungu Baba anaendelea kutuchukulia kuwa sisi ni wasafi katika jambo lile lililo muhimu – wokovu. Tunapokosea, hatuhitaji “kuoga ili tuokolewe”; ni “miguu” yetu tu inayohitaji “kuoshwa” kwa sababu ya dhambi tuliyo[zo]tenda.

Kuungama ndio ufumbuzi alioutoa Mungu wetu kwa tatizo la dhambi. Kama ilivyo kwamba Kristo anatosha kutuweka huru kutokana na dhambi katika dakika ile tunapomwamini Yeye (jambo linalowakilishwa na ibada ya kusafishwa na ubatizo), vivyo hivyo kazi hiyo ya Kristo inatosha kutusafisha na kuwa wasafi kila mara tunapotenda dhambi baada ya dakika ile ya wokovu.

Ile Zaburi kuu ya Daudi ya kuungama, Zaburi ya 32, ni mfano mzuri wa hatua za kuungama kwani inadhihirisha wazi kabisa kanuni mbili tunazopaswa kuziweka akilini tunapolikabili tatizo linalokera la dhambi. Kwa upande mmoja, tunapaswa kukiri kwamba tumekosea tukijua kwamba dhambi ni tatizo zito ambalo lina matokeo mazito, na tunapaswa kwenda kwa Mungu na kuomba msamaha tukiwa na moyo wenye majuto halisi. Kwa upande mwingine, tunapaswa kwenda mbele Yake tukiwa na uhakika kwamba Atatusamehe mara moja bila masharti, kwani msingi wa msamaha wake sio kwamba tunastahili msamaha huo, bali ni kazi aliyoifanya Mwanawe, Bwana wetu, Yesu Kristo. Mara nyingi tunapoitumia kweli ya maandiko katika maisha yetu ya Kikristo, tunapaswa kujizuia kuegemea (kuelekea) sana (zaidi) upande wa kushoto au wa kulia wa kanuni inayohusika (extremism); katika suala la dhambi, hatuwezi kudharau uzito wa ubaya wa dhambi/kosa tulilotenda, lakini pia haifai kuwa na hisia zilizokithiri za hatia nafsini mwetu au kuwa na mashaka kuhusu msamaha wenye utimilifu na upendo wa Mungu wetu.

Mfalme Daudi anatupatia kielelezo mwafaka cha kanuni hii. Alipojaribu kuficha dhambi yake kutoka kwa Mungu, aliadibishwa vikali – Zab. 51:3-4. Lakini alipokiri au alipoikubali, “alipoacha kuificha na akaungama dhambi yake”, Mungu alimsamehe, (aya ya 6). Sasa, kukiri, kukubali, kuacha kuficha na kuungama si “hatua” tofauti katika kuungama dhambi, bali ni taswira tofauti za mchakato ule ule za kukubali kwamba umetenda dhambi. Kanuni inayofundishwa hapa ni kwamba tunahitaji kukiri kwa Mungu katika sala (aya ya 6), tukubali hatia yetu, na tukubali uhalisia wa dhambi yetu. Tunapofanya hivyo, basi tutegemee kwa kujiamini kabisa, kwamba Mungu anatusamehe, kama alivyomsamehe mfalme Daudi (cf. 1Yoh. 1:9). Kama tunavyosoma katika Mithali 28:13:

13 Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.

*Soma pia Zaburi yote ya 51.

Katika somo lijalo tutaendelea kujifunza kuhusu maisha ya kiroho; tutaendelea kuanzia kwenye suala tunaloweza kuliita la “kulinda goli”, la kupona baada ya maisha/matendo ya dhambi, na kuelekea katika msingi wa “mashambulizi” dhidi ya dhambi unaoitwa “fikra adilifu za Kikristo”.
=0=

Imetafsiriwa kutoka: Confession of Sin: Peter’s Epistles #15

=0=

Basi, na tuonane katika Somo #16 la mfululizo huu, kwa neema za Mungu, Amina!