WAKILI WANGU
Shalom. Mimi niliishi maisha mazuri tu, ya kawaida, ambapo nilimwamini Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya uzima wangu wa milele. Nilijaribu kwa kiasi nilichoweza kumfurahisha Mungu; muda wangu hapa duniani ulipofikia mwisho wake nikaondoka.
Kitu cha kwanza ninachokumbuka ni kukaa juu ya benchi refu katika chumba kimoja kilichofanana na chumba cha mahabusu wanaongojea kusikiliza kesi zao mahakamani. Ghafla mlango ukafunguliwa, nami nikaelekezwa kuingia katika chumba cha mahakama; nikaingia nikakaa katika kiti cha mshitakiwa. Nikazungusha macho yangu katika kile chumba cha mahakama nayo yakatua juu ya uso wa kiongozi wa mashitaka; huyu bwana alikuwa na uso wa kutisha ambaye alinitizama kwa kiburi na chuki. Nilikuwa sijapata kumwona mtu mwovu kama yeye katika maisha yangu. Nikatizama upande wangu wa kushoto nikaona ameketi Mwanasheria ambaye ni mtetezi wangu – alikuwa na sura ya upole na ukarimu; alinifanya nifikiri kwamba nimeshamwona mahala fulani.
Mlango uliokuwa pembeni ukafunguliwa na Hakimu akaingia; alikuwa amevaa joho kubwa la kifahari ambalo lilifika mpaka miguuni pake. Alikuwa na wajihi ulioonyesha mamlaka, na ukimwona tu mara moja utamheshimu sana. Nilimtizama na nikafikiri: “Hapa leo lazima haki itatendeka”. Hakimu akakaa nyuma ya meza yake ya kifahari, akatutizama sisi wote na kutamka: “Basi na tuanze hii kesi, kiongozi wa mashitaka, endelea!”.
Yule wakili kiongozi wa mashitaka akasimama na kuanza kutoa maelezo yake ya mashitaka juu yangu: “Jina langu ni Shetani, na leo niko hapa kudhihirisha kwamba huyu mshitakiwa (mimi!) anastahili kwenda motoni!” Akaanza kusimulia uwongo niliosema, vitu na mali nilizoiba, jinsi nilivyohadaa na kudhulumu watu wakati wa maisha yangu duniani. Shetani yule aliendelea kusimulia matendo yangu maovu na potofu niliyotenda zamani; alivyokuwa akizidi kuongea mimi nikanywea katika kiti changu; nikatamani kile kiti kiwe kisima au shimo nipotee kabisa. Niliona aibu sana kiasi kwamba sikuweza kumtizama Wakili wangu kwani Yule kiongozi wa mashitaka alisimulia hata makosa yangu ambayo mimi mwenyewe nilishayasahau!
Akili yangu ilivurugika sana, siyo tu kwa sababu kiongozi wa mashitaka alifunua makosa yangu yote ya maisha yangu, bali pia kwa sababu Wakili wangu alikaa tu pale mezani kimya, bila kutoa kauli yeyote ya kupinga jinsi shetani yule alivyokuwa akinishambulia! Nilijua kwamba nimetenda yale madhambi yote, lakini nilitenda na mema pia! Je, yale mema niliyotenda hayawezi kupunguza makali ya yale mabaya niliyotenda?! Shetani akamaliza hoja na mashambulizi yake kwa ghadhabu kali na kusema: “Mtu huyu anastahili kukaa na mimi kule motoni, kwani ana hatia ya kutenda maovu yote haya niliyoyataja; na hakuna yeyote anayeweza kupinga ukweli huu.”
Ndipo ikawa zamu ya Wakili wangu; naye akasimama na kumwomba Mheshimiwa Hakimu kama anaweza kuanza utetezi wake. Yule shetani kiongozi wa mashitaka akasema “pingamizi!” Mheshimiwa Hakimu akasema “pingamizi limekataliwa!” Na akamruhusu Wakili wangu kuanza utetezi. Wakili wangu akaanza kutembea kuelekea sehemu ambayo ataonekana vizuri na kila mmoja pale ndani ya chumba cha Mahakama. Ndipo nikashituka kwa mshangao baada ya kumtizama vizuri. Kumbe Wakili wangu ni Bwana Yesu Kristo! Yeye alikuwa na wajihi wa kifalme! Yeye ndiye Mwokozi wangu na Mkombozi wangu. Aliposimama akamgeukia Mheshimiwa Hakimu na kumsalimu: “Shalom Baba!” Mheshimiwa Hakimu akatabasamu kwa mbali, akaitika kwa kichwa. Halafu Wakili wangu akaanza utetezi wangu. “Shetani,” akaanza, “hajakosea aliposema kwamba huyu mtu ametenda dhambi. Upande wa utetezi hautapinga tuhuma zote zilizotolewa mbele ya Mahakama hii. Pia ni kweli kwamba mshahara wa dhambi ni mauti na mtu huyu anastahili kupata adhabu.” Bwana Yesu akavuta pumzi, akamgeukia Baba yake, Mheshimiwa Hakimu, akanyoosha mikono yake na kutamka: “Hata hivyo mimi nilikufa msalabani ili kwamba KILA MTU aweze kuwa na uzima wa milele. Mshitakiwa alinipokea na kuamini kwamba Mimi ni Mwokozi wake, hivyo mshitakiwa ni wangu.” Bwana akaendelea, “ jina lake limeandikwa katika kitabu cha Uhai na hayuko awaye yote anayeweza kumpokonya kutoka katika kiganja changu. Shetani bado haelewi kwamba mshitakiwa hastahili kupewa hukumu bali anastahili HURUMA.” Na hapo Bwana Yesu, Wakili wangu akakaa kitini, akamtizama Baba Yake na kusema: “Hakuna kitu kingine kinachotakiwa kufanywa, Mimi nimemaliza yote.”
Mheshimiwa Hakimu akanyanyua mkono wake ulioshika ile nyundo yake ya Mamlaka, akaishusha kwa kishindo na kutamka: ”Mshitakiwa yuko huru. Adhabu yake imekwishalipwa kikamilifu. Mashitaka yanafutwa.” Na pale Bwana wangu, Wakili wangu, Yesu Kristo aliponishika mkono na kuniongoza njia nikamsikia shetani kule nyuma yangu akifoka kwa ghadhabu: “Sitakata tamaa! Nitashinda kesi inayofuata!”
Mimi nikamwuliza Bwana Yesu wakati anampa maelekezo malaika mmoja juu ya mahala ilipo maskani yangu, “Bwana, umeshawahi kushindwa na Shetani hata mara moja?” Naye akanijibu: “Kila mtu aliyekuja kwangu na kuniomba niwe WAKILI wake amepokea maamuzi kama ya kwako:
AMELIPA KIKAMILIFU!
Respicius Kilambo
NB: Hii ni tafsiri kutoka lugha ya Kiingereza, makala hii imetoka: www.godandscience.org “My Attorney”