Ule Mpango wa Mungu: Nyaraka za Mtume Petro #3

 

Na Dr. Robert Dean Luginbill

Wa https://ichthys.com

 

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

 

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahsusi na Dr. R. D. Luginbill

Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by

Dr. R. D. Luginbill

 

Tafakuri na Muhtasari: Mtume Petro alikuwa anawaandikia Wakristo waliokuwako Asia Ndogo ambao walikuwa waumini kwa muda mrefu tu, lakini ambao walianza kutoka nje ya msitari wa Mpango wa Mungu na malengo ya Mungu katika maisha yao. Walianza kuruhusu mateso ya maisha na changamoto mbalimbali katika maisha yao kutikisa imani yao na kuwafanya waanze kutilia shaka fundisho la Biblia linalosema kwamba neema za mungu zinawatosha katika kupambana na mateso na changamoto hizo. Petro mwenyewe alikabiliana na kiasi kukubwa cha mateso katika maisha yake, lakini aliepuka kishawishi cha kusingizia shida za maisha kuwa ni sababu ya yeye (Petro) kutoendelea kukua kiroho na hivyo kushindwa kuhudumia Kanisa kwani alitambua kwamba nguvu zake mwenyewe hazitoshi kupambana na shida zake (jina lake mwenyewe Petros linamaanisha, kimsingi, “kajiwe kadogo [tu] katika mpango [mjengo] wa Mungu”, jina ambalo alipewa na Bwana Yesu Mwenyewe – Yohana 1:35-42). Katika nyaraka zake mbili kwa waumini wale wa Asia Ndogo waliokuwa wakiteseka kwa sababu ya imani yao, Petro aliwapa somo hili muhimu ili kulinda imani yao: wakati ulimwengu unapima mafanikio kwa kutazama mali, mamlaka, umaarufu na wanaona magonjwa yenu, umasikini wenu, upweke wenu, mateso yenu na shida zingine mnazopata kuwa ni dalili za kuachwa na Mungu, mtazamo huo si sahihi kwani Mungu anawapima watu Wake kwa kiwango tofauti. Mkristo anayemtegemea Yeye ndiye mwenye mafanikio halisi mbele za Mungu.

 

1Petro 1:1-2: (1) Petro, Mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule ambao japo wametengwa na kutawanywa katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia,

(2) wamechaguliwa na Mungu Baba kwani Aliwajua toka mwanzo kwa utakaso wa Roho Mtakatifu, hata mkapata kutii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani ziongezwe kwenu! (Revised Translation)

 

Ufafanuzi/fasili:… kwa wateule ambao japo wametengwa na kutawanywa”: Tumekwisha ona jinsi Wakristo wale wa mwanzo walivyovumilia kutengwa, kunyanyaswa na kuteswa kwa sababu ya imani yao. Petro aliyajua mateso waliyokuwa wakiyapata na hakusita kukiri jambo hilo. Aliwaita kwa Kiyunani “parepidemoi”, maana yake watu waliotengwa na jamii (“outcasts” kwa kimombo); Wayunani wenyewe walimwita hivi mtu anayeishi katika nchi kama mgeni au mkimbizi, (kwa mfano Waebrania 11:13-16); Petro anawalinganisha na taifa lililosambaratika, akitumia neno lingine la Kiyunani, “diaspora” - (mtawanyiko; mara nyingi neno hili hutumika kulielezea taifa la Israeli. Petro anasema, ndiyo, sisi Wakristo tunaishi kama wageni hapa duniani, tumesambaratika kutoka kwetu. Ulimwengu unatutizama kwa dharau, kama watu wa kusikitikia. Mbele za walimwengu, sisi ni watu tuliotengwa na jamii, dunia haitutaki; lakini mbele za Mungu sisi ni watu wa pekee kabisa, tumechaguliwa kama watakatifu kutoka katika dunia iliyosheheni uchafu. Neno la Kiyunani linalotumika hapa ni “eklektos” yaani “walioteuliwa, waliochaguliwa” linamaanisha kwamba sisi Wakristo tumechaguliwa kutoka katika ulimwengu ili tuwe hazina yake milele, na kwamba japokuwa bado tuko ndani ya ulimwengu, sisi si walimwengu tena. Kwa sababu hii tunapaswa kuelewa kwamba ulimwengu unatuchukulia sisi kama maadui, kama Bwana wetu anavyotuonya:

 

Yohana 15:18-19:

15.19 Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.

15.20 Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Nukuu kutoka SUV (Swahili Union Version).

 

Inawezekana tukauliza swali walilouliza wale Wakristo aliowaandikia Petro, wa Ponto, Galatia, n.k. kwamba kwa nini, kama Mungu ametuchagua sisi, bado tupo hapa katika ulimwengu, tukivumilia mateso ambayo kwa wengi wetu ni makali namna hii? Ili kujibu swali hili, tutatizama mpango wa Mungu, na pia tutaona Biblia inatufundisha nini kuhusu mateso.

 

Mpango wa Mungu:

 

1. Mpango Mzima wa Mungu: Kabla ya kuanza majira (“time” kwa kimombo), Mungu alikuwepo katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu – Mwanzo 1:1; Yohana 8:58. Tunajua kutokana na mistari mbalimbali katika Biblia kwamba kabla ya uumbaji Mungu aliunda Mpango Wake. Katika Mpango Wake huu ulichora kinaganaga historia yote ya malaika na wanadamu – soma Zab. 33; Isaya 25:1; 42:22-26; 43:9; 44:6-8 & 25-26; 48:3 & 13; Waefe. 1:11; 3:11.

 

Hapa nitanukuu Isaya 43:3 &13 pekee:

3Nilitabiri mambo ya kwanza [ya sasa] tangu zamani, kinywa changu kiliyatangaza na kuyafanya yajulikane, kisha ghafula nikayatenda nayo yakatokea.

…….

13 Naam, mkono wangu umeuweka msingi wa dunia, na mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu; niziitapo husimama pamoja. (SUV)

(nyongeza yangu katika mabano ya mraba [ ] kwa ajili ya kudhihirisha maana)

 

Ni mpango ulio timilifu na mkamilifu, na ambao unakumbatia kila tukio – hata likiwa dogo kiasi gani – kutoka mwanzo mpaka mwisho wa majira. Uwezo wa Mungu wa kujua yote, kudra ya Mungu, u-milele wa Mungu yaani uwepo Wake usio na mwanzo wala mwisho unaonyesha kwamba Yeye anazidi majira na anga kwa kiasi kisicho na ukomo. Kwa shughuli ya kubuni, kuumba na kumiliki kila tukio, kila kitendo kwa majira yote, kwetu sisi ikiwa ni vigumu kuelewa, kwake Yeye ni rahisi sana (tunapaswa kukumbuka uweza Wake kila mara tunapoingiwa na shaka: Anaweza chochote kile!)

 

a. Kusudi la Mungu: Mungu ni mtimilifu. Hapati faida yoyote kutoka kwetu wala hapati hasara yoyote. Hana uhitaji wa kitu chochote kutoka kwetu - Matendo 17:25.

 

Isa. 43:7:

7 Kila mmoja aliyeitwa kwa Jina langu, nilimwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya. (SUV)

 

Hapa Isaya anatuambia kwamba Mungu alituumba kwa ajili ya “utukufu Wake”, yaani kwa ajili ya kuudhihirisha utimilifu Wake, uongofu Wake na wema Wake.

Majira na anga, na Mpango wa Mungu unaoviendesha na kuvitawala vitu hivyo vyote viwili, vyote viliumbwa kwa ajili yetu sisi viumbe vyake (Isa. 45:18), ili tumjue, tumpende na tudhihirishe utukufu wa Nafsi Yake.

 

b. Mpango wa Mungu: Lakini tunajua ya kwamba si viumbe Wake wote wanaoamua kumtumikia – wawe malaika au wanadamu. Mungu angeweza kuumba ulimwengu ambamo watu wangemtii bila ubishi, kama vile mimea inavyofuata/inavyoligeukia jua. Badala yake Ameumba ulimwengu ambamo [nafsi zote] wote wanaomtumikia wanafanya hivyo kutokana na maamuzi ya utashi wao; alipanga hivyo Yeye mwenyewe. Katika busara zake timilifu, Mungu alibuni mpango ambao umezingatia maamuzi-huru ya kila kiumbe mwenye utashi (malaika na wanadamu) kabla hata hawajaonekana ulimwenguni - Yer. 1:5. Kabla Mungu hajasema “Iwepo nuru” Mwa. 1:3, alikwishaweka matukio, mtiririko wa historia kulingana na mpango Wake, na alifanya hivyo bila kutatanisha utashi wa viumbe Wake kwa namna yoyote ile: Yeye alijua kila kitu tutakachokifanya, kabla hatujakifanya (omniscience) na alikuwa na uwezo wa kuweka matendo yetu hayo yote katika Mpango Wake huo wa historia yetu sisi wanadamu na malaika (omnipotence). Kwa hivyo si sahihi kufikiria kwamba Mungu ana uwezo tu wa kuingilia katika matukio ya historia ya viumbe Wake, bali tufahamu kwamba Yeye aliidhinisha na kuthibitisha kila tukio na kila tendo litakalofanyika kabla halijafanyika na kabla halijatokea, enzi hizooo kabla hajaumba “majira”. Kwa mfano, kwa kuwa alijua (omniscience) kwamba Respicius ataamua kuzaliwa upya katika Kristo karne, mwaka, mwezi, siku, saa, dakika, sekunde, katika nchi, mkoa, wilaya, n.k. fulani (dhamiri-huru ya mwanadamu), basi aliweka/alipanga matukio yote yatakayompitia Respicius katika maisha yake katika namna ambayo ilihakikisha uamuzi huo HURU wa Respicius unafanyika na unatokea (omnipotence of God)! Hicho ni kielelezo kilichorahisishwa; katika uhalisia wake, mchakato huu ni changamano zaidi ya hapo kwa kiasi kukubwa sana. Hakuna mwanadamu wala super-computer inayoweza kuukamilisha.

c. Uasi wa Shetani: Historia imehusisha, na inaendelea kuwa, na matukio mengi yanayochukiza. Historia ina uovu. Uovu hautoki kwa Mungu, bali umeanza katika utashi wa viumbe wake, katika uasi wao dhidi Yake. Shetani na wafuasi wake waliasi dhidi ya Mungu – soma Isa. 14:12ff (na aya zinazofuata); Eze. 28:12-19; na yeye akamshawishi mwanadamu atende dhambi – Mwa. 3. Kwa utashi wao wenyewe, wazazi wetu wa kwanza walijitenga na Mungu. Lakini Mungu, kwa sababu alijua hayo yatatokea (omniscience), aliyaweka katika Mpango Wake tangu mwanzo, na akatupa sote nyenzo ya kumchagua tena Yeye, katika Mwana wa pekee wa Mungu, Yesu Kristo. Hivyo wakati Mungu Baba, akiwa na Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, na akaamrisha historia ianze, haukuwa uamuzi wa kiholela, kwani ulihusisha gharama kuu kupita uelewa wetu. Kwani Mpango ule wa Mungu, ulihusisha/ulilazimu kuja hapa duniani kwa Mungu Mwana kama mwanadamu, kutolewa dhabihu na Mungu Baba, na makubaliano ya tukio hilo kwa hiari Yake Mwana, kupitia maisha ya shida nyingi, na mwisho wake kufa msalabani – Lk 24:25-27;Matendo 2:23; 3:18; 7:52; 10:37; 17:3; 26:23; 1Pet. 1:11. Tunapoweka imani ya wokovu wetu katika Bwana Yesu, tunakubali kitendo hiki cha huruma kuu ya Mungu na hivyo kudhihirisha utukufu wa Mungu, ambalo ndilo kusudio la Mungu katika kutuumba sisi.

 

2. Awamu Tatu za Mpango wa Mungu kwa Waumini: Katika Warumi sura ya nane, Mtume Paulo anatuonyesha, kwa vilelezo, jinsi Mpango mzima wa Mungu (katika ujumla wake, kwa watu wote) unavyounganika na mpango wa muumini mmoja mmoja. Paulo anatutoa katika milele iliyopita, anatupeleka katika milele ijayo pale anaposema kwamba sisi ni “wale Aliowajua tangu mwanzo” ([Mungu] Aliupangia uamuzi wetu wa kuamini uliowezeshwa na utashi wetu, toka mwanzo kwa sababu aliujua utafanyika – omniscience), “pia ndio aliowachagua tangu mwanzo” (akatuweka katika Mpango wake Mkuu), “akawaita” (akatuwekea mazingira ya kutuwezesha kumjua na kumwamini Kristo), “akawahesabia haki” (akatuokoa na kutuweka katika Familia ya Mungu), na “akawatukuza” (ufufuko wetu unaokuja). Kielelezo hiki cha Paulo kinaelezea jinsi maisha yetu yanavyoingia katika awamu tatu za Mpango wa Mungu kwa ajili ya kila mmoja wetu, sisi waumini wa Kristo:

 

a. Muumini Anapookolewa: Mungu anataka sote tuokolewe kwa kitendo rahisi cha kumwamini Bwana Yesu Kristo – Yoh. 1:12; 3:16; Waefe. 2:49; 2Tim. 1:9. Baada ya kupangiwa wokovu wetu tangu kale (kutokana na uamuzi wetu huru kujulikana tangu kale) na kuitwa katika wokovu huo wakati wa maisha yetu ya hapa duniani, tunahalalishwa pale tunapochukua hatua ya kuamini katika Kristo.

 

b. Muumini katika Maisha Yake, Baada ya Kuokolewa: Mungu anataka tujifunze na tuwe na ustahamilivu katika wokovu wetu (1Pet. 2:2; Wafi. 2:12). Sote tunapaswa kuendelea katika Mpango Wake wa wokovu wetu kama vile tulivyoanza wakati ule tulipookolewa. Tunasikia sehemu ndogo tu ya ukweli Wake Mungu (yaani Injili, inayosema kwamba tunaokolewa kwa imani yetu katika Kristo), na tunaiamini. Kwa namna hiyohiyo, tunapevuka kiroho kwa kusimilisha (assimilate) roho zetu na kweli yote iliyo katika maandiko ya Mungu. Tunaporuhusu kweli itawale nafsi zetu, kweli hiyo inatubadilisha na kutufanya tupevuke kiroho – War. 12:1-2- hatua kwa hatua. Ni muhimu sana kutambua ya kwamba tunapevuka kiroho kutoka ndani yetu kwenda nje. Kamwe hatukui kiroho kwa kubadilisha tabia au mwenendo wetu kwa kufuata na kuzingatia mfumo fulani wa sheria na kanuni zilizoundwa na watu (hata kama wakidai na kusisitiza kwamba mfumo huo una msingi wake katika maandiko!). Hata hivyo, kupevuka kiroho husabababisha mabadiliko katika tabia na mwenendo wetu; mwenendo wetu huwa mzuri zaidi kutokana na kupevuka kiroho baada ya kuamini mafundisho ya injili. Badiliko moja muhimu sana ambalo Mungu anapenda kuliona katika maisha yetu ni kwamba waumini wote watatimiza wajibu wao (kila mmoja sehemu yake) katika Mpango Wake (1Wakor. 12:12-31: Waefe. 2:10). Wakristo wote hupokea karama ya aina fulani wakati wanapookolewa (1Wakor. 12:11). Hata hivyo, kuzaa matunda halisi ni matokeo ya kukua kiroho na siyo nyenzo ya kukuwezesha kupevuka kiroho. Kwa kuwa tumehalalishwa, yaani tumehesabiwa na Mungu kuwa ni waongofu kutokana na kumwamini Kristo, tunapaswa sasa kuwa waongofu kikwelikweli katika matendo yetu katika maisha yetu yote hapa duniani.

 

c. Muumini Katika Milele: Baada ya maisha ya hapa duniani, hakutakuwa na machozi tena, kwani yale mambo ya kale hayatokuwako tena - Ufu. 21:4. Tutakuwa naye Bwana milele – War. 5:9-10; 1Wathess. 4:13-18, na basi tutarajie furaha ya milele – Ufu. 21:9 – 22:5, ambayo itatanguliwa na ufufuo wa miili yetu ya kidunia ambayo itabadilika na kuelekea hali ya utukufu tulioahidiwa na Mungu mwenyewe – 1Wakor. 15:50-58. Kwa kuwa tumekuwa waaminifu kwa Kristo hapa duniani, tutatukuka kupitia ufufuko pale atakaporudi Bwana Yesu.

 

3. Mpango wa Mungu na Wewe: Mungu ana mpango kwa ajili yako, mpango ambao kusudi lake ni wewe pekee. Alikufahamu katika milele iliyopita, muda mrefu kabla hujatokea hapa duniani. Alikupenda sana hata akamtuma Mwanaye ya pekee aje hapa duniani na kufa kifo cha kiroho kwa ajili yako. Alifanya hayo yote kabla hujamgeukia Yeye kwa ajili ya wokovu wako. Je, unafikiri hatakupatia mahitaji yako yote kwa sasa ambapo unaamini? - Warumi 5:6-11. Mungu anayajua matatizo yako yote, yale matatizo ya nje unayoyakabili, na yale maumivu na mateso ya ndani ya moyo wako. Yeye anatosheleza mahitaji yako haya yote. Huko milele ijayo hakutakuwa na shida tena. Kwa hivyo ni hapa dunianai tu, katika ulimwengu huu unaotawaliwa na Shetani, ndipo Bwana anayo fursa ya kukudhihirishia uaminifu Wake kwako katika mambo haya. Katika wakati huu ndipo na wewe unapoweza kuonyesha upendo wako kwake, na, katika imani, kuikabili changamoto ya maswaibu yanayokukabili, ukiwa na imani madhubuti kwamba anakupenda, na kwa vyovyote vile, atakupatia mahitaji yako yote. Tutakapokuwa na Mungu tutaona kila kitu kwa wazi, kikamilifu - 1Wakor. 13:12, lakini tukingali hapa duniani, taswira tunayoiona ina mapungufu. Hapa duniani tunapaswa kupiga hatua mbele kwa imani - 2Wakor. 5:7; Waebr. 11:1, na si kwa kutegemea macho yetu ya kimwili yanatuonyesha nini, bali kutegemea tunachokijua mioyoni mwetu na tunachokiamini kuwa ni kweli kutoka kwa ile chanzo ya kweli, Neno la Mungu.

 

Muhtasari: Kwa mujibu wa macho ya ulimwengu, wasomaji wa barua ya kwanza ya Mtume Petro walikuwa ni “watu walioshindwa maisha” na walioanza kuikubali hali hii yao ya “kushindwa” na [kuanza] kumlalamikia Mungu kwa kumwuliza “kwa nini sisi tunaishi maisha duni, ee Mungu?” Hivyo Mtume Petro anawajibu na kuwaambia kwamba japokua wao ni watu wasio na thamani mbele za ulimwengu huu, kwa kweli wana thamani kuu na umuhimu wa hali ya juu mbele za Yeye mwenye umuhimu: muumba wa ulimwengu na Mwokozi wao.Mungu, ambaye ana uwezo wa kupanga njia za mpito wa sayari, jua na galaksi lukuki; ambaye anaweza kupanga kila kipande cha mchanga katika kila pwani ya dunia hii (mahala pake), kwa kweli anaweza kuyatatua matatizo yako wewe kwa urahisi kabisa. Ana uwezo wa kukutunza wewe, ana shauku kubwa ya kukulea wewe; kwa kweli amekuwa akikuchunga kwa uaminifu na kwa uangalifu mkubwa maisha yako yote! Tunapaswa kutiwa moyo tunapokumbuka ukweli huu, na tuendelee katika msitari huu wa Mpango Wake kwa uvumilivu na kuendelea kukua kiroho. Sehemu ya kwanza ya swali walilouliza wale waumini waliokuwa wakiteseka wakati ule wa Petro inajibiwa hivi: tupo hapa duniani kwa ajili ya kuutimiza Mpango wa Mungu kwa maisha yetu. Uaminifu wetu kwake utatuletea baraka za milele na thawabu ambazo hazitafifia – 2Wakor. 4:17 – ukitofautisha na “mafanikio” yasiyodumu ya dunia hii – 1Wakor. 3:10-15. Tutajadili nafasi muhimu ya mateso tunayopitia katika kukua kiroho kwa muumini hapo sehemu inayofuata.

 

=0=

 

Translated from: The Plan of God: Peter’s Epistles #3

 

=0=

 

Basi, na tuonane katika sehemu #4 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!