Changamoto [Tuliyopewa] ya Kukua Kiroho: Nyaraka za Mtume Petro #32

1st Peter 1:22-25

Na Dr. Robert Dean Luginbill
Wa https://ichthys.com

Tafsiri ya Kiswahili na Respicius Luciani Kilambo

Ruksa ya Tafsiri Hii Imetolewa Mahususi na Dr. R. D. Luginbill
Permission for this Kiswahili Translation has Been Kindly Granted by
Dr. R. D. Luginbill

1Peter 1:22-25 SUV:
1.22  Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa [ki]ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo [wa kindugu].
1.23  Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele.
1.24  Maana, Mwili wote ni kama majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka;
1.25  Bali Neno la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.

Utangulizi: Kabla ya kuenda kwenye fasili ya msitari hadi msitari, tunapaswa kuona kwamba wazo kuu la aya hizi zote ni uhitaji/ulazima kwa waumini kuendelea na mtazamo na utaratibu mwema uliopelekea katika wokovu wao ili waweze kukua, kuendelea na kuzaa matunda kwa ajili ya Bwana. Sasa tumefanywa watakatifu mbele ya macho ya Mungu, tumetakaswa na ile kweli – utakaso wa mwanzo (tumeokolewa kwa neema kutokana na kuiamini Injili), na inatupasa baada ya hapo kuendelea na mwendo wetu wa Kikristo katika namna hiyo hiyo: kufuatilia utakaso katika maisha yetu kwa kuliamini Neno la Mungu na kulitumia katika mazingira na matukio ya maisha yetu, ili kwamba mwenendo wetu katika mwendo wetu na Kristo, na kuzaa matunda katika kuutumikia Mwili Wake yaani Kanisa Lake, vitaendana na nafasi tuliyo nayo sasa kama wale walio “katika Kristo”.

Mbegu ile ile ya Neno lililotuokoa ndilo Neno la Mungu ambalo sasa tunapaswa kulisikiliza kwa makini kabisa ili kutimiza mapenzi ya Mungu kwa maisha yetu. Kwani kila kitu ambacho si cha kweli kitatupwa motoni na kuteketezwa, bali Neno la Mungu ladumu milele. Nasi pia tutadumu milele na Bwana wetu kwa sababu tumezaliwa upya kwa Neno hilo hilo la Mungu – na tutafaudu milele thawabu tunazopata [ambazo zinahifadhiwa mbinguni] kwa kujifunza na kulitumia Neno katika maisha yetu baada ya wokovu.

Lakini kuhusiana na maendeleo [katika kujifunza kanuni za Biblia] mliyoyafikia, endeleeni katika namna hiyo hiyo (yaani, kuipokea, kuiamini na kuitumia kweli)!
Wafi. 3:16

2.6  Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, [kama] Bwana [wenu], enendeni vivyo hivyo katika Yeye;
2.7  mkiwa na shina na mnaojengwa katika Yeye; mmefanywa imara katika imani, kama mlivyofundishwa; mioyo yenu ikiwa imejaa shukrani [hata ikamwagika].
Wakol. 2:6-7

Mioyo Iliyotakaswa: Tumeona hapo nyuma kwamba utakaso na utakatifu (maneno ambayo ni visawe katika teolojia – yaani synonyms) ni maneno yanayomaanisha utengano na dhambi na uovu. Mungu ni mtimilifu na amejitenga kabisa na dhambi na uovu, na hivyo inatupasa sisi ambao tunaitwa kwa jina Lake kuwa hivyo hivyo pia. Tunatakaswa, tunafanywa kuwa watakatifu, tunapewa utakaso wa mwanzo mara tunapoamini katika Bwana Yesu Kristo – tunatakaswa kutokana na nafasi tunayopewa katika Kristo: positional sanctification. Tunapozaliwa upya, Mungu anatuchukulia kuwa tu watakatifu, tuliotakaswa na tuliowekwa wakfu kutoka ulimwenguni kama wale ambao sasa ni wake Yeye na Mwanaye milele. Ni wazi, [katika] wakati tunapookolewa tunabaki na hulka ya dhambi ambayo imeenea katika miili yetu ya muda ya sasa. Kwa sababu hiyo hatutakuwa huru kabisa na dhambi kiuhalisia mpaka "huu [mwili wenye] uharibifu utakapovaa kutokuharibika" katika ufufuo (1Wakor. 15:53). Kutimia kwa tumaini hili lenye neema atakaporudi Bwana wetu kutatupatia utakaso wetu wa mwisho (ultimate sanctification): utakaso-hitimisho, ambapo milele tutakuwa watakatifu, kama alivyo Bwana wetu. Kati ya wokovu (utakaso wa mwanzo, kuzaliwa upya kiroho) na milele, hapa katika ulimwengu wa Shetani, imempasa kila muumini "kuutafuta utakatifu" (Waebr. 12:14), "akitimiza utakatifu katika kumwogopa Mungu" (2Wakor. 7:1). Hii inaitwa "experiential sanctification" yaani utakaso katika maisha, kuutafuta na kuufuatilia utakaso siku hadi siku, jambo ambalo kila muumini wa Bwana Yesu Kristo anapaswa kulipa kipaumbele.

Kama tulivyoona hapo kabla, utakaso huu tunaopaswa kuuendeleza na kuudhihirisha kwa ulimwengu si jambo la kuonekana tu au kujifaragua kama kucheza katika tamthilia, au kama aya yetu inavyosema, "unafiki" au "ya kinafiki" kama ilivyokuwa kwa Mafarisayo hapo zamani na ilivyo sasa hivi katika makundi fulani ambayo yametunga sheria, desturi, mapokeo, tamaduni, n.k., ambazo wafuasi wao wanapaswa au wanashurutishwa kuzifuata ili kuonyesha "utakatifu" wao (hypocrisy ni neno la Kiyunani ambalo ki-etimolojia linamaanisha "play-acting", kuigiza mchezo). Lakini, utakaso wa kweli ni mwenendo wa maisha yanayomfurahisha Bwana kutokana na upendo halisi Kwake. Zaidi ya hapo, tumeona pia kwamba utakaso huu halisi (kinyume na kuigiza tabia za "kitakatifu") hauwezi kufanikishwa kwa kuubadilisha mwenendo wetu "wa nje" au tunapokuwa mbele za watu – katika namna ya Mafarisayo – ambao Bwana wetu aliwaita "makaburi yaliyopakwa rangi nyeupe" au kama yalivyofanya makundi ya ki-legalistic (yanayotunga na kufuata sheria, desturi, mapokeo, n.k.) ambayo yanakataza tabia fulani tu za wazi (ambazo wakati mwingine siyo hata dhambi!) wakati hazimbadilishi yule mtu wetu wa ndani. Utakaso halisi wa kimungu na utakatifu wa kweli unaweza tu kutoka ndani ya moyo kwenda kwenye mwenendo wetu wa nje (matendo yetu), na kamwe si kutoka nje kwenda ndani. Ili tuwe watakatifu wa kweli, tunapaswa kutembea karibu sana na Bwana Yesu Kristo, na hilo linawezekana tu kutokana na kukua kiroho kwa kujifunza kweli ya Neno la Mungu, kwa kuliamini kwa moyo wote, halafu kwa kulitumia katika nguvu ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu ya kila siku. Hii ndiyo maana Petro anasisitiza hapa katika aya ya 22 akitaja mahususi mahala pa utakaso wa kweli, "mioyoni mwenu", na pia namna ambayo walengwa wa waraka wake wamekwishafanya hivyo: "kwa kuitii ile kweli", yaani ni kwa kubadilika katika mioyo yetu, ndani, ndipo tunafuatilia na kutafuta utakaso halisi, na hili linaweza kufanikishwa tu kwa kujifunza, kuamini na kulitumia Neno la Mungu na kweli Yake katika maisha yetu.

17.14 Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
17.15 Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu.
17.16 Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
17.17 Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.
17.18 Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.
17.19 Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe kutokana na kweli.
Yoh. 17:14-19 SUV

Bila shaka wale wote waliosomewa waraka wa Petro hapo mwanzo walikuwa waumini, na hivyo tunaweza kusema kwamba walikuwa na utakaso wa mwanzo, pale walipoamini. Lakini huo si mwisho kwa waumini katika maisha haya. Tunaachwa hapa duniani baada ya kuzaliwa upya kwa malengo fulani, na ni kwa sababu hii Petro anawasihi wasomaji wake waende kwenye hatua ya pili katika maisha ya Kikristo, ambayo ni maendeleo ya kiroho katika kutembea na Bwana katika kutimiza ile amri kuu, ya upendo (1Wakor. 13:13).

Pendaneni kila mmoja na mwenzake kwa uthabiti ili upendo wenu wa kindugu usiwe na unafiki: Kama Bwana wetu anavyotufundisha katika Mathayo 22:36-40, Sheria yote na manabii vina msingi wake katika amri ile kuu, yaani kumpenda Mungu kwa mioyo yenu yote; pia anatuambia katika muktadha huo huo kwamba amri ya pili [kuu] – kama vile upande wake wa pili – ni kuwapenda majirani zetu (haswa waumini wenzetu) "kama [tunavyojipenda] sisi wenyewe". Anapotusihi hapa ili tuwe na upendo adilifu (virtuous love), Petro anatilia mkazo katika upendo kwa kaka na dada zetu katika Kristo (yaani philadelphia, "brotherly love" – upendo wa kindugu – maana ambayo iko wazi katika usemi/amri: "pendaneni") na sio upendo wetu kwa Bwana. Hii ni kwa sababu, kama mtume mwenzake, Yohana, anavyotufundisha, "yeyote asiyewapenda kaka na dada zake ambao anawaona, hawezi kumpenda Mungu, ambaye hajamwona" (1Yoh. 4:20). Kama tunataka kudhihirisha uadilifu wa msingi kabisa wa kumpenda Mungu kwa moyo wote, ni lazima tuonyeshe kwanza upendo kwa kaka na dada zetu.

Upendo huu kwa ndugu zetu, waumini wenzetu katika Kristo, haupaswi kuwa, na kwa kweli hauwezi, kuwa wa kuigiza tu, kwa ajili ya kujionyesha tu, ukitendwa tu katika unafiki. Katika kuweka wazi kwamba sehemu kubwa ya kile anachomaanisha kwa kusema hivi ni kwamba upendo halisi kwa kaka na dada zetu hauwezi kuwa wa kuonyesha kwa mdomo tu, Petro anaonyesha katika amri yake kwetu ya kupendana kwamba tupendane kwa uthabiti (katika Kiyunani Petro ametumia neno ektenos au kama vile "kuvuta mpira mpaka mwisho wake"). Unaweza kuonekana kuwa una upendo ukimwambia mwenzako mwenye uhitaji , "nenda kwa amani, ukaote moto na kushiba" (Yak. 2:16), lakini kama anavyotufundisha, "hakuna faida" katika maneno matupu kama hayo. Hivyo anachotuambia Petro hapa si haswa namna ya kudhihirisha upendo wetu kwa Wakristo wenzetu (ijapokuwa hii ni sehemu yake); msisitizo wake anapotusihi hivi upo katika kutuamrisha tuonyeshe upendo wetu kwa vitendo. Katika mfano wa Yakobo, hii inamaanisha tuwasaidie kaka na dada zetu ikiwa wana shida ya mahitaji fulani.

Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa msaada wenye matokeo chanya zaidi tunaoweza kuwapatia ndugu zetu katika Kristo ni ule unaotokana na matumizi ya karama za kiroho tulizopewa ... ili Mwili wa Kristo ufanye kazi katika namna iliyokusudiwa, kila sehemu ya Mwili ikitoa kwa sehemu nyingine kile kinachokosekana huko. Kwa uwazi kabisa, kuna aina nyingi za karama na kuna michanganyiko (combinations) mingi ya karama mbalimbali, bila kutaja hata aina mbalimbali za utumishi katika Kanisa halisi la Kristo (na tusifikirie tu kuhusu aina ya utumishi uliokuwa unakubalika zamani, na unaokubalika sasa katika *kanisa linaloonekana!). Hivyo basi, ijapokuwa waumini wanapaswa kutoa msaada (wanapoweza, na kwa yeyote mwenye uhitaji halisi), na kusali/kuomba, na kutia moyo (kwa mfano), kila mmoja wetu ana eneo la utumishi alilochaguliwa na Bwana wetu Yesu Kristo Mwenyewe ambalo linaoana kwa utimilifu kabisa na mchanganyiko wa karama tulizopokea kutoka kwa Roho Mtakatifu, na utekelezaji wake umeamriwa na Mungu Baba (1Wakor. 12:4-6). Na maana ya yote haya yanapotafakariwa katika muktadha

*NB: Kanisa linaloonekana: Tutofautishe hapa kati ya Kanisa la Kristo lenye waumini halisi waliozaliwa upya duniani kote, na kanisa linaloonekana machoni pa watu, linalojumuishwa na madhehebu mbalimbali duniani kote, ambamo Kristo anatajwa tu kwa Jina mara moja-moja, na mafundisho Yake halisi hayafundishwi na hayafuatwi (Matt. 7:21-23).
(context) wa sura hii ni kwamba kuna haja tangamano (corresponding need) ya kuendelea kukua kiroho na kuendelea kupevuka ili kufikia kiwango ambapo kikweli tutaweza kuwapenda kaka na dada zetu katika Kristo kwa namna yenye ufanisi kwa kuwatumikia. Katika kutilia mkazo kiwango cha juu ambacho ndilo lengo la mchakato wa maendeleo ya Kikristo – kiwango ambapo kwa hakika tunadhihirisha upendo thabiti na usio na unafiki kwa waumini wenzetu – Petro anatutia moyo kwa uthabiti kabisa ili tufanye yote tunayotakiwa kufanya kutuwezesha kufikia kiwango hicho: kukua kwa kutumia kweli ya Neno la Mungu, kuendelea katika kutembea na Kristo kwa kufaulu mitihani ya maisha itakayotukabili kwa kuitumia kweli hiyo, na hivyo kufikia kiwango cha kuwasaidia wengine tunapotekeleza utumishi ambao ndio lengo asilia na mahususi tulilopewa hapa duniani na sababu ya karama tulizopewa na Roho Mtakatifu. Hicho ndicho kiwango ambacho tukifikia tunaweza kikweli kuanza kutimiza ile amri kuu ya "kumpenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa *nafsi yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili (mind) zako zote" (Luka 10:27; Kumb. 6:5; Matt. 22:37).

Tumezaliwa upya, si kwa mbegu ya uharibifu bali kwa Neno la Mungu lenye uzima na lililo thabiti milele: Katika fundisho-fumbo la Mpanzi, Bwana wetu vivyo hivyo analinganisha Neno la Mungu na mbegu. Katika fundisho-fumbo lile, Neno ama linaota (kwa wale wanaoitikia), ama halioti (kwa wasioamini ambao hawaitikii); na kwa wale wanaoitika, mbegu yaweza kunyauka (wale wanaoanguka kutoka katika imani), au mbegu yaweza kusongwa na magugu na miiba (wale wanaoruhusu shughuli za kidunia kuzuia kukua kiroho, kuendelea, na kuzaa matunda), au mbegu inaweza kuanguka kwenye udongo mzuri na kuzaa matunda tele (wale wanaoliitikia Neno baada ya wokovu na kuendelea na ile kweli mpaka mwisho).

Akiongea na waumini, Petro anawakumbusha wasomaji hao wa waraka wake kwamba Neno la Mungu, haswa habari njema za wokovu katika Bwana Yesu Kristo kwa imani katika nafsi Yake na kazi Yake msalabani katika kuondoa dhambi zetu, ndiyo njia ya kuingia katika uhusiano na Mungu, na sasa anawatia moyo kuendelea kulikumbatia Neno la Mungu. Kama vile mbegu ya milele ya Neno la Mungu ilivyo bora na njema kwa kiasi kikubwa zaidi ya ile mbegu ya uharibifu ambayo haina faida katika [milele] ijapokuwa ina malengo na faida zake hapa duniani (kwa mfano kutoa majaribu na mitihani kwa waumini), vivyo hivyo majukumu na shughuli zetu zote za kimwili za hapa duniani, ijapokuwa zina uhalali na ulazima fulani kwa sasa, hazina umuhimu wowote katika uzima na maisha yetu ya milele. Tunaukubali ukweli huu pale tunapoipokea Injili kwa furaha na kuiamini; tunapaswa kuendelea na kusimama imara katika msingi huo na "kuendelea [kufuatilia upevu wa kiroho] kwa namna hiyo

*Tafsiri ya SUV inatumia neno "roho" hapa. Tafsiri za Kiingereza zinatumia neno "soul". Tafadhali rejea 3A: Biblical Anthropology: The Study of Man, Section II.4.(c) katika https://ichthys.com kwa mjadala wa kina zaidi. Ikiwa Kiingereza ni kikwazo kwako, tafadhali nitafute, nafundisha bure.
hiyo (Wafi. 3:16), yaani kwa kufuatilia kwa makini Neno la kweli baada ya wokovu pia. Kwani hiyo ndiyo mbegu "inayoishi na kudumu milele". Mwili wetu wa sasa na vyote tulivyo navyo duniani ni kama "majani" yaliyopo leo lakini kesho hayatakuwepo. Lakini tuna matumaini bora kuliko ubatili ambao ulimwengu unauona [una maana] kwa sasa. Tunajua kwamba kama vile mbegu ambayo kwayo tumezaliwa haina uharibifu na ni ya milele, hivyo hivyo tutafaudu uzima wa milele katika mwili usioharibika pindi Bwana wetu atakaporudi. Hilo ndilo "Neno lile jema lililohubiriwa kwenu" (1Pet. 1:25). Kufahamu hili, kwamba vitu tunavyoviona ni vya muda mfupi tu, vya kupita, lakini kila kitu kinachohusiana na Neno la Mungu na hadhi yetu kama watoto wa Mungu kwa sababu tumezaliwa upya Kwake na katika Yeye kwa Neno hilo hilo pale tulipoamini kwamba ni la milele (1Wakor. 4:18), hivyo kuna kila sababu ya sisi kujifunza, kuliamini na kulitumia Neno hilo hilo siku zote za maisha yetu, tuwe na jitihada katika "kupendana kwa uthabiti na bila unafiki" ili tumwonyeshe heshima Bwana wetu na ili tushinde thawabu kamili. Hilo ndilo "Neno la habari njema lililohubiriwa kwenu" (1Pet. 1:25).

Ukweli kwamba Petro anatumia hapa mtazamo (upendo) kuelezea mwenendo wa Kikristo katika ujumla wake ni kitu ambacho kinapaswa kuzungumzwa kwa undani zaidi. Namna pekee ya kufanikisha maagizo ambayo Mungu amewapa waumini baada ya wokovu ni kwa kujifunza ile kweli wakati wote, na kweli ni kitu cha kiroho, na si cha kimwili. Tunda/zao lake la kwanza, mara baada ya kupevuka kwa kuitumia ile kweli kwa kuisikia, kujifunza, kuiamini na kuitumia katika mazingira yetu yote, ni la kiroho pia, ingawa kuna taswira za kimwili na matumizi ya Neno ya kimwili katika maisha yetu ya Kikristo. Katika kutumia analojia ya mbegu ya kimwili dhidi ya (versus) mbegu ya Neno, Petro anaweka pointi wazi kabisa kwamba mtazamo wa kiroho ndio wenye umuhimu katika mchakato huu (kama ilivyokuwa wakati tulipoamini), na sio wa kimwili (Yoh. 6:63). Utumishi (ministry) wa kimwili ni muhimu, siyo tu wakati unapoelekezwa kwa waumini wenzetu, bali pia katika uinjilisti unaoelekezwa kwa wasioamini. Lakini, mambo yote ya kimwili yataharibiwa. Hivyo inapaswa kukumbukwa kwamba hata katika utumishi (ministry) ambao una sehemu kubwa ya mambo ya kimwili, bila ya taswira ya kiroho, bila ile kweli, basi utumishi huo hauna maana yoyote. Kwani kiini cha utumishi wa kweli ni ile kweli ya Neno la Mungu. Kwa upande wa waumini, utumishi halisi kwa kaka na dada zetu katika Kristo una lengo la kwanza kabisa la kuwapatia ile kweli (kwa mfano [utumishi] wa mafundisho ya Mchungaji-Mwalimu: Pastor-Teacher) au njia na fursa za kuipata ile kweli (kwa mfano kumsaidia, kwa namna mbalimbali, mwalimu na utumishi wake) na/au kuitumia ile kweli (kwa mfano kutia moyo, na pia katika mahala panapostahili, msaada wa kimwili ili wengine wajifunze na kukua kiroho na kutumikia wakati wao ukifika, baada ya mahitaji yao ya kimwili kupatikana). Kitu muhimu kabisa ni kwamba hili hutokea pia katika utumishi kwa wasioamini. Msaada wa madawa na utabibu, msaada wa pesa, au msaada wowote ule wa kimwili hauwezi kuwa na faida zozote zile za milele kwa mtu asiyeamini – kama hautaambatana na ile kweli ya Neno la Mungu katika ujumbe wa Injili ya wokovu kupitia (through) imani katika Yesu Kristo.

Kuzaliwa upya: Kuna namna nyingi za kuielezea hadhi yetu [yenye baraka] ambayo sisi waumini tunayo, kama watu ambao wameokolewa kupitia imani yao katika Kristo. Kama Petro anavyosema pale mwanzo wa ibara, maisha yetu sasa "yametakaswa", akimaanisha kwamba Mungu ametuweka mbalimbali (apart) na ulimwengu na ametufanya tutengane mahususi na ulimwengu huu kama wale ambao ni mali Yake. Lakini wakati utakaso unafundisha kupatikana kwa wokovu wetu kwa msingi wa utengano (exclusion – kutoka ulimwengu, kifo na hatia), kuzaliwa upya kunafundisha kupatikana kwa wokovu huo huo kupitia msingi wa upamoja (inclusion): sasa sisi ni memba wa familia ya Mungu, watoto, wa kike na wa kiume, wa Mungu Baba kwa sababu sote ni wa Mwana, Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Tulikuwa tumekufa lakini sasa tumefanywa hai milele yote na tumepewa uzima wa milele, tukingojea kufunuliwa kikamilifu siku ile Bwana wetu atakaporudi.

Ule "utakaso wa maisha [yetu]" (yaani utakaso wa mwanzo na utakaso katika maisha yetu ya Kikristo, tunaotumaini kwamba sote tutaupitia ...), ambao Petro aliwaambia wasomaji wa waraka wake [kwamba] ni wao (na wetu) kutokana na kuitii ile kweli, na lengo la utakaso huu wa mwanzo na mwenendo wa utakatifu unaozidi kukua, tukumbuke, ni upendo thabiti kwa ndugu zetu [katika Kristo] bila unafiki, yaani tabia ya kuwasaidia na kuwatumikia kaka na dada zetu katika Kristo ambayo ni halisi, itokayo moyoni na yenye dhamira imara (determined), ili waweze kukua na kuendelea katika imani kutokana na kweli ya Neno la Mungu, halafu, kama itafanyika kwa ukamilifu, wafikie katika utumishi (ministries) wa kwao wenyewe. Hii ni kusema kwamba lengo la Mungu katika kututenga na ulimwengu linahusiana siyo tu na wokovu wetu, bali pia [linahusiana] na azma yetu katika maisha ya duniani baada ya wokovu, ikielezwa na Petro kwa kuihusisha na ile fikra-adilifu kuu ya Ukristo, yaani upendo (ambapo tunatambua kwamba kuwapenda Wakristo wenzetu ni jambo la lazima ikiwa pia tunampenda Yeye kwa mioyo yetu yote, kwa nafsi zetu zote, kwa akili zetu zote na kwa nguvu zetu zote). Pointi ya Petro hapa katika kuunganisha utakaso unaopatikana kwa njia ya kuijua kweli (aya ya 22), na hali [yetu] ya kuwa tumezaliwa upya kwa njia ya Neno la Mungu lisiloharibika, linalodumu milele katika Injili (aya za 23-25), ni kutukumbusha na kuelekeza fikra zetu katika mtazamo wa u-milele. Tumetakaswa – ni watakatifu mbele za macho ya Mungu; na tumezaliwa upya – tu hai sasa kwa Mungu kama watoto wanaopendwa na Mungu. Hii ni "habari njema kweli kweli" ambayo ni habari yetu kama wale waliopokea ile kweli ya Injili na wamekuwa memba wa Kanisa la kweli la Kristo kwa imani katika Yeye na katika kile alichokifanya kwa ajili yetu katika kulipia dhambi zetu zote.

Lakini hapo sio mwisho wa simulizi. Tumetakaswa kwa malengo mahususi: kukua kiroho, kuendelea na kuzaa matunda (ambamo tunadhihirisha upendo wetu kwa ndugu zetu katika Kristo). Vivyo hivyo, tunazaliwa upya, Mungu anatufanya hai kwake Yeye na tunafanywa wamoja katika Kristo, kwa malengo hayo hayo. Kwani haikuwa mbegu ya uharibifu iliyotuzaa, mbegu ya ulimwengu huu ambayo leo iko na kesho imeondolewa. Hapana. Tumezaliwa upya "kwa Neno la Mungu lenye uzima na linalodumu milele" (aya ya 23), na hivyo, kama Petro anavyotaka tutambue, matendo yetu katika ulimwengu huu wa mpito yana matokeo ya milele. Kwa sababu hiyo maisha yetu hayahusiani na kutazama nyuma katika siku ile tulipozaliwa upya (ingawa ile ni siku kuu kwelikweli, na kwa kweli ni siku pekee inayostahili kukumbukwa), bali maisha yetu ni kutazama mbele kwenye siku ile tutakaposimama mbele ya Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Na wakati tafakari ya hiyo milele ijayo, ambapo tutakuwa hatuna uharibifu na tutakuwa wa milele kama vile alivyo Yeye Neno wa kweli ambaye kwa Yeye tumezaliwa upya inapaswa kutujaza furaha na matarajio ya hamu na shauku (War. 8:23), inapaswa pia kutupatia hofu ya kimungu kuhusiana na tathmini tutakayofanyiwa na Bwana wetu mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo (2Wakor. 5:10-11). Hivyo kutakaswa kunakuja na jukumu – kupata faida kubwa zaidi tunayoweza kuipata kutokana na maisha ya Kikristo tunayopewa. Vivyo hivyo kuzaliwa upya siyo mwisho bali ni mwanzo, kwani si kwamba tumepewa uzima [mpya] wa kimwili, kama vile mbegu iliyotupatia uzima mpya ni ya muda tu, ya kupita tu; tumepewa uzima wa milele kwa njia ya mbegu isiyoharibika, Neno la milele la Mungu kutoka kwake Yeye ambaye ndiye Neno la Mungu, mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo. Na, kama vile ile mbegu ya kweli tuliyoipokea kwa furaha ili tuzaliwe upya ni ya kiroho, isiyoharibika, ni ya milele, vivyo hivyo vipaumbele vyetu baada ya wokovu vinapaswa kuwa vinaelekezwa kwenye mambo ya kiroho, yasiyoharibika, ya milele.

3.1  Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
3.2  Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.
3.3  Kwa maana mlikufa [kwayo yaliyo chini], na uhai wenu [halisi] umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.
3.4  Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu [wa ufufuo].
Wakolosai 3:1-4 SUV

Hivyo basi, na tujizatii kuishi maisha yetu ya sasa katika mwanga wa milele ambamo maisha yetu halisi yamefichwa katika Kristo, ili Afurahishwe nasi katika siku ile kuu inayokuja, ili tuweze kusikia, "umefanya vyema, mtumishi mwema na mwaminifu!" kutoka kwake Yeye ambaye tunampenda zaidi ya haya maisha ya mpito.

2.15  Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba [kwa uhalisia] hakumo ndani yake.
2.16  Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima [yaani majigambo ya alicho nacho na anayoyafanya], havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.
2.17  Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu [akiwa hai] hata milele.
1Yoh. 2:15-17

Hitimisho: Kabla ya kujadili dhana mahususi za kukua kiroho katika sura zinazofuata, pamoja na mafundisho yanayohusiana nayo ya kukabiliana na mitihani, na utumishi, hapa katika sura ya kwanza Petro anachukua muda kidogo kutukumbusha kama Wakristo jinsi tulivyookolewa na mtazamo wetu wa msingi unatakiwa uweje: tunatakiwa tuishi katika mwanga wa milele katika mtazamo wa kimungu na wa ki-mbingu, na siyo mtazamo wa ki-dunia na wa ki-ulimwengu. Hii ni muhimu sana, haswa kwa sababu ni rahisi sana katika kelele na vurugu za ulimwengu hata kwa waumini waliopiga hatua katika maendeleo yao ya kiroho, kuondoka kwenye msitari mwema waliomo wakati wowote katika mwendo wao wa kila siku na Bwana na kufikiria kupita kiasi matatizo yao binafsi na "ubora na taswira" ya maisha yao ya kimwili hapa duniani, wakapepesa macho na kupoteza mtazamo juu ya yaliyo muhimu , yaani mpango wa Mungu na nafasi yao ndani ya mpango huo. Pia ni muhimu kukumbuka, kama ilivyowekwa wazi na Petro kwa kutofautisha kati ya mbegu ya uharibifu ya duniani na mbegu ya milele ya Neno la Mungu, kwamba hii ni vita ya kiroho, si ya kimwili.

10.3  Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;
4) Kwani silaha za vita tunayopigana si za kimwili, bali zina uwezo katika Mungu, wa kuangusha ngome,
2Wakor. 10:3-4

Kama vile milele na thawabu tunazotazamia katika ufufuo kwa sasa havionekani kwa macho, vivyo hivyo utekelezaji wa malengo halisi ambayo Kristo ameyapanga kwa ajili ya maisha yetu ni, [kwanza kabisa], wa kiroho, na utekelezaji huu unatumia rasilimali za kimwili kutimiza malengo ya kiroho. Kwa wakati tukiwa hapa duniani, "tunatembea katika mwili" – lakini si kwa jinsi ya mwili (Wagal. 5:16-25). Vita yetu ni ya kiroho, ikipiganwa kwa silaha ambazo haziwezi kuonekana kwa macho ya kimwili, karama za Roho Mtakatifu zilizotiwa nguvu na Mungu Baba na kupewa mwelekeo na Bwana Yesu Kristo kwa ajili ya kuwaboresha wote wanaoomba msaada katika Jina Lake takatifu. "Hili ndilo Neno la habari njema lililohuburiwa kwenu" (aya ya 25).

2.17  Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu [akiwa hai] hata milele.
1Yoh. 2:17 SUV

Ulimwengu kamwe hautatushukuru wala kutuelewa. Kwa hakika, hauwezi. Kwani sisi tunatumikia wito wa juu zaidi, ambao hauwezi kuonekana kwa macho ya kimwili, wito ambao tumepewa na Mwana wa Mungu Mwenyewe. Katika ulimwengu huu tunaweza kukabiliwa na kila namna ya mateso (Yoh. 1:33), na tunaweza kuwa na uhakika kwamba wale waliochagua ulimwengu na mtawala wake mwovu badala ya Yeye aliyekufa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote siku zote watatuchukulia sisi kuwa ni wapumbavu (1Wakor. 1:18; 2Wakor. 6:14). Lakini kwetu sisi, waumini katika Bwana Yesu Kristo, kitu pekee chenye umuhimu – kitu pekee kinachopaswa kuwa na umuhimu – ni kumfurahisha Yeye aliyekufa kwa ajili yetu.

4.16  Kwa hiyo hatulegei [yaani hatufi moyo]; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.
4.17  Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana [zaidi ya dhiki hiyo];
4.18  tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.
2Wakor. 4:16-18 SUV

=0=

Imetafsiriwa kutoka: A Challenge to Grow Spiritually: Peter's Epistles #32

=0=

Basi, na tuonane katika sehemu #33 ya mfululizo huu, kwa neema ya Mungu, Amina!